Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, November 17, 2014

DUNIA YANGU-64



Inspecta Moto aliwasiliana na watu wake tayari, na kutaka kuhakiki kama kweli huyo binti anachosema ni kweli, aliwaambia watu wake wafuatilie kama huyo mtu aliwahi kufika hapo,  lakini isijulikane, na ulinzi mkali ufanyike kuzunguka hilo jengo, kuhakikisha kuwa huyo mtu hatoki hapo. Kwa taarifa za haraka zilisema hajafika hapo, akamgeukia nesi na kumuuliza.

‘Una uhakika huyo mgonjwa alikuambia atakuwepo huko?’

‘Ndivyo alivyoniambia, kama huniamini basi….’akasema kwa hasira

‘Tunachotaka ni kuwa na uhakika, maana muda kwetu ni muhimu sana, mimi nakuamini, na tutakwenda huko,cha muhimu ujua kuwa huyo mtu sio mtu mwema, kama kuna alichokuwa amekuahidi ujue ni mbinu za kujinufaisha, …’akasema Moto

Nesi ambaye sasa alikuwa hana raha, akionekana kukata tamaa, akamwambia;

‘Mimi hata sijui, hata sijielewi, …’akasema

‘Kila jambo lina mwisho wake, na mwisho wa hawa watu ni huu, ninachokuomba ni kutoa ushirikiano ili tumnase huyu mtu, na haki itendeke, hatujasema kuwa ni mhalifu, uhalifu wa mtu ni mpaka afikishwe mahakamani na ndicho tunachokitafuta ...’akasema

‘Mimi sikujua kabisa kama huyo mtu ni mhalifu, na niliamua kumsaiida kwa nia njema, hata mnavyoniambia nashindwa kuelewa, mtu tajiri, ana mapesa yake, kwanini tena awe mhalifu, ndio maana nasema mimi sielewi, nitafanya mtakvyo tu,...’akasema

‘Nimekuelewa, ila kukuamini kwetu kuwa kweli upo na sisi ni wewe kufanya hayo tutakayokuambia…sawa, haya hebu geuka kidogo…’akasema  inspecta akawa anamvalisha kitu kwenye nguo ya huyo nesi kwenye ukosi, ni kitu kidogo tu ambacho hata nesi hakuhisi kuna kitu kimewekewa na kingine akakiweka kwenye nywele kinamna tu, kinafanana na ywele huwezi kuhisi kuna itu kimewekwa

‘Unaniweka nini?’ akauliza

‘Ni lazima ufike pale ukiwa mtanasahati, kola ya koti lako ilijikunja….’akasema Inspecta

‘Hata sijali tena, siku yangu yote umeiharibu, hata sitamini kwenda huko tena…’akasema

‘Kwenda ni lazima uende huko utakutana na watu wangu watakulinda, usiwe na sahaka….’akasema Moto

‘Kuna watu wako nitakutana nao…!, kwani wewe utafanya nini, utaniacha niende peke yangu, ....mimi nimeshaanza kuogopa, najua akifahamu kuwa nimemsaliti anaweza kunifanya kitu kibaya...’akasema

‘Ndio maana nataka uwe makini kwa kila hatua, hatutaki kabisa afahamu hilo,....wewe ukifika hakikisha unakuwa kama unavyofanya siku zote, na usijishuku, uchunge kauli zako,  na akikuuliza lolote kuhusu mimi au kama kuna kitu chochote, utasema uliongea na mimi, ukaniambia hujui lolote basi....’akasema

‘Wewe humfahamu huyo mtu anashuku kama mchawi....’akasema nesi

‘Kwahiyo unamfahamu vyema, inaonekana mnafahamiana  sana, ...ok tusipoteze muda, wasiliana naye kuwa unakwenda kwake, usikie atasemaje….’akasema, na nesi akachukua simu yake na kutuma ujumbe wa maneno, na ikachukua muda, ujumbe ukajibiwa, na Inspecta akachunguza ile namba, ni namba ngeni, haikuwepo kwenye zile orodha za namba alizokuwa nazo mwanzoni

‘Hii namba aliwahi kuitumia kabla?’ akaulizwa

‘Hapana yeye huwa anabadili namba za simu kila mara, hii namba sijawahi kuiona kabla...’akasema nesi

‘Soma huo ujumbe unasema nini...’akasema Inspecta

Kama tulivyopanga, uwe na makini....’akasema Nesi

‘Mlipanga nini?’ akaulizwa

‘Nifike huko, tuongee, tustarehe kwa kunywa na kula, kupoteza muda, ikifika usiku mimi narudi zangu ni yeye anarudi hospitalini kuendelea kuwa mgonjwa ni hivyo tulivyopanga, sasa sijui kama itakuwa hivyo.., .....’akasema

‘Sasa nikuelekeza jinsi gani utakavyofanya, ukifika huko, fika kama kawaida, usiwe na wasiwasi, mengine wewe utuachie, utatumia usafiri wako kama kawaida, hutakwenda na mtu,..ila hakikisha humwambia chochote zaidi ya kuwa umeongea na mimi....natumai umenielewa....’akasema

‘Eti nisiwe na wasiwasi, hivi kwa hali hiyo utakuwa huna wasiwasi, hilo siwezi kukuficha,…hata sijui kuigiza..’akasema

‘Jitahidi….’akasema Moto

Yule nesi alitangulia kuondoka, na Inspecta akakutana na mmoja wa watu aliyemuagiza vifaa mbali mbali ikiwemo bastola yake. Akachukua kifaa maalumu, akakiweka kwenye simu yake,, sasa akawa anamuona nesi hatua kwa hatua kwa kutumia simu yake ya  mkononi. 

Alipohakikisha kuwa kila kitu kipo shwari na ameshabadili nguo zake na kuvaa nguo za kikazi na fulana maalumu ya kuzuia risasi zisipenye, akaanza kuondoka.

Alipofika mlangoni akakumbuka kitu, akarudi hadi ofisini kwa msaidizi wa doctai ambaye kwa muda huo alikuwa akihudumia wagonjwa, japouwa alionekana hayupo kwenye hali nzuri, akamsalimia tu,

‘Naona mlikuwa manaongea na nesi wangu ....’akasema huyo docta msaidizi kwa sauti ya kilevi levi

‘Ni kawaida tu, je umewasiliana na docta wenu mkuu......’ akauliza

‘Ndio kaniambia kila kitu, na nakuhakikishia tutashirikia nanyi hadi mwisho, hata mimi natamani hali hiyo iishe, ili tufanye kazi kwa uhuru, nilikuwa naishi maisha yasiyo na amani. 

Nilipokuja kugundua kuna kitu kisicho cha kawaida kinachoendelea hapa kwenye hii hospitali..’akasema

‘Kuna lolote ambalo unaweza kuniambia kwa hivi linaloweza kusaidia, maana sina muda wa kupoteza kwa hivi sasa?’ akaulizwa

‘Kwa ujumla mimi sijui mengi, aliyekuwa karibu na huyo mgonjwa ni docta mkuu...kwakweli sikuamini jinsi huyo mgonjwa livyonifanyia, mimi nilijua anaumwa kweli nilivyoitwa kumuona na nesi, ....nilipofika kitandani kwake nikijua kuna mtu, kumbe kaweka mito mithili ya mtu kalala, nilipoinama kufunua, mara nikahisi mtu anakuja kwa nyuma kabla sijageuka, akanipiga sindano hiyo ya usingizi...’akasema

‘Ok, tutajua zaidi baadaye, na  ujue utasimama mahakamani kutoa ushahidi...’akaambiwa

‘Hamna shida, nipo tayari kwa hilo, nitaeleza kila ninachokifahamu..’akasema

 Inspecta akaondoka, huku akiendelea kuwasiliana na watu wake kujua wamefikia wapi, na nesi keshafika wapi, katika simu yake ambayo ina mitandao alikuwa akimuona nesi hatua kwa hatua, huku pia akiwasiliana na watu wake , akachukua pikipiki yake na kuendesha kuelekea huko Hoteli ya Paradise.

Alipofika maeneo hayo, akakutana na watu wake, akapewa taarifa nini kinachoendeelea, yeye akawaambia mengine anayafahmu, yeye anaingia ndani ya jengo, na wakati huo, alishamuona nesi akiwa keshafika orofa ya juu, akawa sasa anatembea kuelekea chumba alichoelekezwa, kabla hajakifika moja ya chumba kingine kikafunguliwa, na mtu aliyevaa sweta lenye kuficha uso,akatokeza na kumshika nesi mkono, akamvutia ndani ya hicho chumba

Inspecta akawasilianna na mtu wake aliyekuwa karibu na eneo hilo, na huyo mtu akasema keshaliona hilo tendo, je achukua hatua gani

‘Subiri kwanza....’akasema Inspecta na muda huo alishafika eneo la rosheni hiyo, na akawa anaangalia simu yake, akamuona nesi akiongea na huyo mtu.

‘Una uhakika hakuna mtu aliyekufuatilia...?’ huyo jamaa akauliza

‘Hakuna..nina uhakika, akasema nesi, na huyo mtu akachukua kifaa fulani akawa anamkagua nesi, kuhakikisha kuwa hana kinasa matukio, na Inspecta alikuwa na mashaka kuwa kile kifaa alichomwekea nesi kitaonekana, na ndicho kinachomsaidia kujua ni nini kinachoendelea, lakini yule mtu kabla hajamaliza, akapigiwa simu, akamuacha nesi na akawa anaongea na simu.

‘Ameshafika…’akasema

‘Sawa nitamuambia…’akasema halafu akamgeukia nesi na kusema;

‘Sasa mkuu yupo chumba kingine sio kile alichokuagiza, kafanya hivyo kwa tahadhari, toka hapa nenda chumba namba 285, gonga mara tatu...tulia gonga tena mara tatu, atakufungulia...’akasema huyo mtu.

‘Kwanini anafanya hivyo, ana wasiwasi gani,mbona siku zote tunakutana bila tahadhari za namna hiyo...’akasema nesi

‘Wewe huoni katoroka huko hospitalini, ni lazima atakuwa anafuatiliwa, na nahisi kama kuna kitu umevalishwa, sikioni, lakini sio hoja, wewe nenda tu..’akasema huyo mtu akimkagua nesi kwa macho

‘Kitu gani, na nani anivalishe, nyie watu bwana, kwanini mnaniweka roho juu, na mbona siku nyingine alikuwa anatoka na kurud kwanini sasa atoroke, hamuoni kuwa mimi mnaniwekwa kubaya,...’akasema

‘Usijali yeye anajua ni ni cha kufanya...mtaongea naye, mimi nimemaliza kazi yangu, …..’akasema huyo mtu na akawa anaongea na simu, na baadaye nesi akatoka, na kuelekea chumba alichoelekezwa, akagonga kama alivyoambiwa, na chumba kikafunguliwa, na nesi akawa yupo ndani ya chumba

Hakukuonekana kuwepo na mtu yoyote ndani ya hicho chumba, lakini mlango ulijifungua, na nesi alipoingia ndani ukajifunga wenyewe, na kulipita muda, mara sauti ikitokea kwa juu kwenye kitufe, ikasema;

‘Nitakuwa na wewe dakika chache nahakikisha usalama kwanza, mitambo yangu yote imezima ghafla, nahisi kuna tatizo,na kama ni tatizo n bora wewe uondoke bila ya kuonana na mimi…’sauti ikasema

‘Hata mimi sina muda wa kukaa zaidi, nitakuwa natafutwa huko nilipotoka, ujue kuondoka kwako kumeleta matatizo, unatafutwa haujulikani wapi ulipo..’akasema nesi.

‘Nafahamu hayo, nimefanya hivyo makusudi, waache wanitafute tu,....ni nani mwingine zaidi ya Moto mliyeongea naye….maana mitambo yangu haifanyi kazi siwezi kujua kinachoendelea…’akasema

‘Hakuna mwingine, ….na mtu mmoja niliekutana naye akanielekeza nije hapa, basi, hakuna mwingine…’akasema

‘Huyo ni mtu wangu ndiye aliyebakia wa kumuamini…..’akasema

‘Lakini sasa, mimi unaniweka katika mahali gani, huoni kuwa umeniingiza kwenye matatizo….?’ akauliza nesi

‘Usiwe na wasiwasi, ...nitakulinda ikishindikana utakuwa kama hao wengine, hawatakuona tena, na watakusahau basi tutafanyaje....’akasema

‘Watanisahau una maana gani?’ akauliza nesi

‘Utakuja kujua nina maana gani baadaye ikibidi
, sasa hivi nipo vitani, na kwenye vita hatuangalii mtu machoni yoyote atakeyekuja mbele yako, ukamuhisi ni adui, unatakiwa kummaliza mara moja...’akasema

‘Sijakuelewa,..upo vitani na nani?’ akauliza nesi

‘Sio muda wa kuulizana maswali, unakumbuka nilikuambia ukija nitakuagiza kitu...’sauti ikasema

‘Kitu gani, mimi nikitoka hapa narudi nyumbani kwangu siwezi kuja hapa tena, naogopa kbisa na sasa hata sikuelewi, naoana kama ulikuwa ukinitaka ili tu nikusaidie mambo yako, kumbe wewe ni mhalifu...’akasema

‘Achana na upotofu huo,….sikiliza kuna kifaa, kuna mtu kapewa kifaa na Inspecta Moto, kifaa hicho ni muhimu sana kwangu, nakihitaji, kuna mambo yangu mengi humo, ...sasa wewe unatakiwa uende na pesa nyingi tu umshawishi huyo mtu akupe hicho kifaa, yule kijana akipewa pesa nyingi hatakuwa na maneno, namfahamu sana..’akasema

‘Kifaa gani hicho....?’ akauliza nesi, akajikuna kichwa akahisi kitu kigumu, akataka kukivuta lakini akasita akatulia akimsikiliza

‘Ni kifaa cha komputa, kina kumbukumbu zangu za nyuma, ....nakihitajia sana, hicho kikifika mikononi mwa hao watu, ...basi...nimeumbuka,..unasikia, ni muhimu sana kwetu, alikuwa nacho mama, nikajua kimeshaharibika,..lakini kumbe..bado kipo, unajua mimi nakupenda sana, na ndoto zangu kiukweli ni mimi na wewe, wewe uwe malikia wangu wewe huoni sina mke mke mke wangu mtarajiwa ni wewe, lakini sasa...oh , hicho kitaharibu kila kitu...’akasema

‘Umejuaje kuwa hicho kifaa bado kipo...ulisema kila kitu kipo shwari, hakuna kikwazo, sasa kwanini unasema hivyo?’ akauliza nesi

‘Kuna mitambo niliyokuwa nikiitumia, nilikuwa naona kila kitu, lakini sasa haifanyi kazi na mtu wangu wa mitambo  na mitandao ameshakamatwa, ndio maana hawa watu sikutaka waendelee kuwepo,...nilijua kila kitu naweza kukifanya mwenyewe baadaye, lakini naona bado nawahitaji, sasa....lakini….,  sijui ilitokeaje, wakapona, wangetoweka kabisa ningejua jinsi gani ya kutoka tena, kutoka tena kama mtu mwingine, lakini haiwezekani bila hicho kitu,....’ akasema.

‘Mimi hata sikuelewi,...mambo yako unayongea ni kama muota ndoto isiyowezekana, sasa niambie moja, ndoto yetu ya kuwa pamoja, ya kunisomesha niwe docta mkubwa, yote ilikuwa ni mashairi ya kuniteka akili, au….?’ akauliza nesi

‘Sijui....natamani ingelikuwa hivyo, lakini sijui...muhimu, ni hicho kifaa, unaona hapa nipo gizani, wala sijui kinachoendelea, Moto, huyu mtu anayeitwa Moto, kaharibu kila kitu, nataka huyu mtu afe, lakini kila mbinu zakumaliza zimeshindikana,......angekubalia akawa kama Maneno, isingelikuwa ni taabu...mmh, hawa watu bwana, wanataka niniI katika hii dunia, ….wanataka kishi maisha ya taabu, mimi utajiri ninao, nilitaka na wao wawe matajiri, lakini hawanielewi, ....aah, unaona hapa, hata siwezi kabisa kuwasiliana na yoyote...’akasema

‘Kwa hiyo unataka mim nifanye nini....? akauliza nesi

‘Unajua, nilimuona Inspecta Moto akiwa nacho, sikujua kipo wapi kabla, maana hakikutakiwa kuwepo kabisa, kiltakiwa kiharibiwe mapema mama,…akakificha,….ajabu nakiona anacho huyu mtu anayeitwa Moto, akampelekea huyokijana, unakumbuka kuna siku nilikuambai unisaidia nitoke, lakini ikashindika..?’ sauti ikasema

‘Yah, ...unajua isingeliwezekana siku ile...ilikuwa ni hatari, bosi alikuwepo, alikuja bila kutarajia,.....unajua kila kitu, chako ni cha kuficha ficha ningelijua ni nini kinachoendelea ningelijua cha kufanya...’akasema nesi

‘Basi siku hiyo nilipanga kwenda kumvamia huyo kijana kwani alikuwa akifanya juhudi ya kukifungua, kila kina namna ya kukifungua, nahisi atakuwa keshagundua, yule kijana ni mtundu sana, ningelijua nikamchukua huyo kijana  kwenye anga zangu, sasa hata sijui nifanyeje,...na kwa utundu wake, najua sasa hivi atakuwa ameweza kukifungua....kwahiyo nataka uende kuonana naye. Mapema iwezekanavyo, vinginevyo ndoto yetu itakuwa kweli ya kufikirika...’sauti ikasema

‘Kwani wewe sasa hivi  upo wapi., nimeambiwa tutaona hapa..?’ akauliza

‘Nipo wapi hilo sio muhimu, nipo duniani tu,....huwezi kuniona, hakuna anayeweza kuniona kwa hivi sasa….nilishakufa na ….na sijui kama nitarudi tena….’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza nesi

‘Hapa nilipo huwezi kuniona, na …oh, unaona mitambo yote haifanyi kazi,hapa naweza kuwasiliana na wewe tu, kweli hawa watu wameniweza, nimejaribu kila njia, lakini ....mmh, naona sasa muda umefika, nahisi, namuona ooh mama yule, baba yule…..kuzimu kuleee…hahahaha, nenda, kamalize hiyo kazi...’sauti ikasema na kukawa na kucheka kwa mda mrefu

‘Unajua mimi nashindwa kukuelewa, kila siku unakuja na mambo mapya, hebu niambie ukweli, kwani wewe ni nani hasa na hapa kwenye hili jengo umekuja kufanya nini, kwanini uweze kufika hapa na kufanya kila ukitakacho kama vile hapa ni kwako,..au kweli wewe ni mhalifu...?’ akauliza

‘Mhalifu,...hahaha, watasema hivyo, lakini kwenye dunia hii kila mtu ni mhalifu, maana hakuna wema, kama kungelikuwa na wema, aah, basi sote tungelikwua watakatifu, lakini, wema,..nani mwema hapa duniani hakuna,….. ubaya ubaya tu,....kila mtu anashindania tumbo lake,au sio, nipate , ni change .....’akasema

‘Hata sikuelewi...’akasema nesi

‘Kama huamini, kwanini kila mtu anataka kupata zaidi ya mwingine, kungekuwa na wema, mtu akipata kitu, angelipenda kugawana na mwenzake,..nani anaweza kufanya hivyo, hakuna, kila mtu hatosheki na anataka kupata zaidi ya mwingine...wema ni ndoto, hakuna kitu kama wema, asikudanganye mtu,.....unanielewa...’sauti ikasema

‘Kwahiyo unataka kusema nini?’ akauliza

‘Ndio maana na mimi niliona njia ya kupata zaidi...ni, ni....kujiunga na dunia yangu, kama walivyowenzangu, kila mmoja ana ndoto yake, ana dunia yake, na mimi dunia yangu ndio hiyo, imeshaundwa na mimi nikajiunga nayo, na sasa natakiwa niwe nayo, na kama ni kufa basi nife na dunia yangu, kila mtu akafa na dunia yangu, nimekabidhiwa na mimi ikifika mwisho wangu nitakufa nayo..’sauti ikasema

‘Umesema mama alikuwa nacho, mama yako ni nani, mbona sijawahi kumuona, na mbona ulisema aliyeunda hilo wazo la dunia yangu alishakufa, kwani wewe ndiye mrithi wake, au..?’ akauliza nesi.

‘Mama,mama,...oh usinikumbushe mbali,...mama yangu umeshawahi kumuona mara nyingi tu...ila ..inasikitisha sana, sijui kwanini ilitokea hivyo, sijui, ..sasa sikiliza angalia ujumbe kwenye simu yako, pitia hapo kwa muhasibu atakupa kiasi cha pesa nilichomuagiza, utaondoka nazo hadi sehemu niliyokuandikia kwenye huo ujumbe, hapo utakutana na huyo kijana....najua ukimuonyesha pesa tu, atabadilika, pesa, inambadili kila mtu, ana njaa kali, na tamaa, wewe mwenyewe utamuona,....fanya hilo kwa ajili yetu.’sauti ikasema

‘Lakini mimi sirudi tena huku,....’nesi akasema

‘Hutaki tuonane tena sio..hutaki pesa zako sio,  hutaki noto yetu ikamilika sio, unajua nataka tuwe pamoja hata kama ni huko kwenye dunia isiyojulikana, twende pamoja, kama kweli unanipenda urudi hapa,tutaondoka pamoja, na dunia itabakia kutukumbuka tu,....kama hutaki pesa zak o, utajiri, au ndoto yetu itimie, basi, ..mimi nitajua la kufanya, ,...’sauti ikasema

‘Sasa hata nikija hapa nitakuona wapi , kwani i wewe sasa hivi upo wapi, hayo makao yako yapo wapi ....?’ akauliza nesi

‘Nenda huko nilipokuagiza, sikuhitaji hapa kwa hivi sasa nahisi kuna hatari inakuja,..nahisi dunia yangu imevamiwa, ....umesema ulimuacha wapi Moto,...huyo ni adui yangu,...kwaheri, ila lolote litakalotokea ujua mimi nakupenda na wewe ulikuwa mtu pekee yake aliyebakia ...sasa nahisi hata wewe huenda, umeniacha, wewe ondoka,....ondoka haraka, nataka kumaliza kazi,,....’sauti ikasema na kukawa kimiya

‘Yule nesi akatoka, mle kwenye kile chumba, na akawa anatembea kwenye corido, kueleekea kwenye ngazi, na alipokaribia kwenye ngazi, akakutana na Inspecta Moto.

‘Oh, umeshafika,...mimi narudi nyumbani, sitaki tena kuwepo hapa, naogopa...nakwenda zangu, wala sitaki mambo yenu, naona naingia hataraini bure, sitaki hata kumsikia huyo mtu tena, basi imetosha.....’akawa anaongea huku akitembea kwa haraka, na Moto akasema;

‘Wewe fanya kama alivyokuagiza , mengine tuachie sisi, usijali tupo pamoja....’akasema Inspecta na nesi hakujibu kitu akaingia kwenye lifti kushuka chini.

Inspecta moto akawasiliana na watu wake, ambao walikuwa wanafuatilia  tukio hilo kwa karibu, na kila mtu alikuwa tayari kwa lolote lile, alipomaliza kuongea nao, akawapigia watu wa idara ya mawasiliano, ambao walikuwa wakitafiti simu zote zinatoka na kuingia kwa huyo nesi , na Inspecta Moto alipouliza;

‘Mumempata huyo mtu yupo eneo gani kwenye hili jengo, ...?’ akauliza

‘Hayupo kwenye vyumba vya hapo chini....’akaambiwa

‘Atakuwa wapi sasai?’ akauliza

‘Yupo juu kabisa summit, alama inaonyesha hivyo....kuna  sehemu imejengwa kama chumba kwa kwenda juu, mawasiliano ya hapo ni magumu, ila kifaa chetu kimenasa sehemu hiyo,  inaonekana kumewekewa vifaa vya kuzuia mtu asigundue, miale ya mawasiliano haipenyi hapo ....’akaambiwa

Inspecta moto, akapiga simu sehem nyingine na kuongea na watu wake wengine

‘Hao mashahidi hali zao zipoje?’ akauliza, na akaambiwa kidogo wana nafuu

‘Mwambie huyo mtu wa mawasiliano, huyo shahidi aliyekuwa mtaalamu wa mawasiliano wa hao watu, ajitahidi aingie kwenye mtandao, tunamuhitajia sana, hatujui huyo mwendawazimu anafanya nini kwa hivi sasa, ajitahidi mpaka aweza kuingie kwenye mitandao yake, kwa vile yeye ndio kaibuni , ni lazima atajua jinsi gani ya kuweza kuiingia huko ...’akasema

‘Ina maana aje huko?’ akauliza huyo mtu

‘Hapana sio lazima yeye kuja huku, akiwa hapo, akipata vifaa vyake ataweza  kuwa sambamba  na huyo mwendawazimu, atadhibiti mawasiliano yake yote na kujua kitu gani anachokifanya, hatujui kwa hivi sasa huyu mtu ana lengo gani....’akasema Moto.

‘Sawa, ngoja niongee naye , vifaa vyake tumeshavileta, sasa hatujui kama akili yake itaweza kufikiria vyema maana bado wapo kama walevi-walevi, docta kasema hali hiyo itachukua muda, sijui kama na y eye anafanya hivyo kuchelewesha au ni kweli...’akasema

‘Muiteni yule mzee wa tiba mbadala,..yule aliyenitibia mimi, ataweza kulimaliza hilo tatizo, ....’akasema Moto.

‘Sawa ngoja tumtafute, nasikia alikuwa hapa mjini, ngoja tuone yupo wapi....’akasema huyo mtu wake.

Inspecta moto alipomaliza kuwasilana na watu wake, akawageukia makomandoo wake aliokuwa nao, akawaambia;

‘Sasa mimi na askari wawili, tutatangulia kwenda juu, wengine msubiri, maagizo,...’akasema

‘Mkuu hiyo kazi ungetuachia sisi...’akasema mojawapo

‘Hapana, ni lazima nionane na huyo mtu ana kwa ana, nataka kuwa na uhakika kama ni 
yeye, ni mjanja sana huyu mtu,....’akasema Moto

‘Ina maana tunaweza tukamkuta mtu ambaye sio yeye....?’ akauliza mwingine.

‘Yote yawezekana kwa hawa watu yote yawezkena, maana hata mimi hapa sijamelewa vyema, kauli yake alipokuwa akiongea na nesi inanichanganya, ngoja tutaona, huona hisia zangu za awli ni kweli,..twendeni....’akasema na wakaanza kazi ya kwenda juu na askari wawili

‘Tupo pamoja mkuu...’akasema mmoja wa askari wake, waliokuwa wakisubiria amri.

‘Hata hivyo muwe makini, japokuwa hakuna mawasiliano yake na watu wengine, lakini hatuwezi kujua, huenda bado kuna watu wake wapo kwenye jengo wanamsaidia...kuna huyo aliyemchukua nesi na kumuelekeza wapi pa kwenda, mkamateni,, na hakikisheni hana mawasiliano na huyo mtu tena, vyumba vyote vikagueni, kuona kama kuna watu wake, na hakikisheni hakuna mawasiliano tena kutoka juu....’akasema Moto


Moto akatoka na kuelekea huko juu summit, akiwa na hao askari wawili anaowaamini- makomandoo.

WAZO LA LEO: Amani, upendo, hujengwa kuanzia utotoni, malezi bora ya  watoto wetu, elimu safi, na huduma bora kwa watoto wetu, ndio chanzo kizuri cha jamii yenye muelekeo mwema, jamii yenye mendeleo na amani. Tusipoangalia chanzo hiki muhimu, tukaangalia ubinafsi wa kuendeleza wangu tu, tukapuuzia watoto wengine, tukiwa tumepewa majukumu hayo, tujue kuwa tunajenga jamii itakayokuja kuishi kwa shida,...hata kama tumejizungushia uzio wa umeme, .... ghasi na amani itakuwa ni kitendawili. Tukumbuke hili, Jamii njema inategemea malezi mema ya watoto wetu, elimu na huduma safi kwa watoto wote.




Ni mimi: emu-three

No comments :