Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, November 14, 2014

DUNIA YANGU-63Inspecta Moto, alipotoka mahakamani moja kwa moja alielekea huko hospitalini alipokuwa kalazwa mkuu wake wa kazi,..akilini akitaka kujua jinsi gani huyo mtu aliweza kutoroka hapo hospitalini,

Iliitwa kutoroka kwasababu taarifa iliwafikia walinzi wa hapo, na wao hawakuona akitoka, na mkuu huyo hakutoa taarifa kuwa anatoka, kwahiyo moja kwa moja ikachukuliwa kuwa ametoroka…ni kwanini alitoroka, ikabakia swali kwa watu.

Inspecta Moto, akaanza kuunganisha matukio, akaanza kumshuku mkuu huyo, lakini bado alikuwa hana uhakika na hicho anachokiwaza, kwahiyo alipofika hospitalini pamoja na kutaka kujua jinsi gani huyo mkuu alitoroka, lakini pia alitaka kumfahamu vyema mkuu wake kutokana na kupenda kuja kutibiwa hapo ambapo kuna shahidi muhimu ambaye anahusika na kundi haramu

Swali, ni wapi mtu huyo amekimbilia,….

Inspecta Moto alipozidi kumbana huyo nesi, akajikuta anaanza kupata fununu, kuwa huyo nesi anaweza kujua mengi zaidi ya hayo aliyokuwa akiyawazia yeye, kwahiyo akaona amtumie huyo huyo nesi, na huenda akawa ni njia ya kumpata mkuu huyo;

‘Kwanini mkuu wake akatoroka hospitalini, kwanini alipenda kutibiwa hapo, na kama alipenda kutibiwa hapo, basi watu wa humo wanamfahamu vyema, je kuna nini kati ya mkuu huyo na kundi haramu,…’

Akazidi kumchimba yule nesi, kwa kumuuliza maswali

Endelea na kisa chetu.

************

‘Kwani  wewe unanishuku nini mimi, mpaka unifanyie hayo yote, yaonekana kama unanishuku mimi kitu fulani, nimekosa nini, naomba uniweke wazi , ili kama ni kumtafuta wakili wangu nifanye hivyo, unanitia mashaka, nina kosa gani….?’

‘Nesi, kwenye kumbukumbu za matukio, inaonekana wewe uliingia kwenye chumba cha vifaa vya kunasia matukio, hebu niambie ulifuta nini huko?’ Inspecta hakujali hayo malalamika akamuuliza huyo nesi hilo swali, na nesi akashtuka, na kusema;

‘Mimi, nani kasema....?’ akauliza akimuangalia Inspecta kwa macho makubwa

‘Sio nani kasema, mitambo inaonyesha hivyo, ulionekana ukiingia kwenye chumba cha  mawasiliano, na kutoka kwa haraka, je ulifuata nini?’ akauliza inspecta Moto kwa mtego, moyoni akisema uwongo mwingine unaweza kusaidia,

Aliwaza hivyo, akijua kule kwenye kumbukumbu, hakuona tukio hilo la huyo nesi kuingia huko, lakini moyoni alishahisi kuwa huenda ni yeye aliyeingia huko au docta msaidizi kwani wao ndio wenye nafasi ya kuingia huko.

Alipomuona huyo nesi akishituka, akajua keshampata. Huyo nesi akamuangalia Moto, kwa macho makubwa, akionyesha kushitushwa na swali hilo, halafu kwa haraka akajibadili kuonyesha hakuna kitu, akasema;

‘Nilikwenda mara moja kumuangalia mlinzi, nikitaka kumuambia awe makini maana mgonjwa anaweza kuleta matatizo...’akasema

‘Kwahiyo uliingia chumba hicho, ….?’ Akaulizwa inspecta akijua sasa keshampata huyo nesi

‘Wewe si umesema uliniona…wewe…..kwanini unanitega?’ akauliza kwa kubabaika.

‘Unasema wewe ulikwenda kumona huyo mlinzi, au sio, ili kumuambia mlinzi awe makini, ni kawaida yenu kufanya hivyo ikitokea jambo kama hilo….?’ Akauliza huku moyoni akisema ` 

'Nilitaka kuwa na uhakika kuwa kweli uliingia humo, na sasa nimekupata’.

‘Ndio...ni kawaida, ....mmh unafahamu mimi ni nesi mkuu, mmoja wa viongozi, na moja ya wajibu wangu ni kushirikiana na viongozi wote, na siku hiyo, kiongozi aliyekuwepo, kuachia msaidizi wa docta, ambaye kwa muda huo alikwenda kumuona mgonjwa, nikabakia mimi kuhakikisha hali ipo shwari,  kwahiyo ilibidi niwajibike kwa jinsi nilivyoweza….’akajitetea

‘Kwahiyo ikitokea tatizo cha kwanza kufanya ni kuwsiliana na walinzi wa mawasiliano, ..?’ akauliza tena Moto na nesi akaonekana kukerwa na swali hilo, kwanza alikaa kimia na alipoona Moto anasubiri jibu akasema;

‘Sijui hunielewi, au huniamini….unaweza kufanya hivyo kutegemeana a tukio, siwezi kusema kuna sheria kama hiyo, inatokea mtu kuaona ni kitu gani ufanye kwa wakati gani, ni hivyo tu.....’akasema

‘Ok, ..au nikuulize hivi, siku hiyo kulikuwa na walinzi wengine nje….ambao wanalinda usalama , na kulikuwa na mlinzi pale karibu na mkuu alipokuwa akihudumiwa, kwanini hukuwaambia wao kwanza, wewe ukakimbilia kuongea na huyu mtu wa mitambo?’ akauliza moto

‘Nilitaka kuongea na huyo wa mawasiliano maana yeye angeliweza kuona kila mahali… labda nisema hivyo, hata hivyo, sikuwa nimetarajia kutokea kitu kama hicho, ndio maana sikuona umuhimu wa kuwaambia polisi’akasema nesi kwa kujiamini.

‘Lakini maelezo yako awali umesema ulikwenda kumuona huyu mtu wa mawasiliano, kuwa mgonjwa, anasumbua, huenda akaleta matatizo, hapo umehisi tatizo, na watu wazuri wa kusaidia kwa muda huo, mimi niliona ni polisi, ambao walikuwa hapo kwa ajili ya mkuu wao, au sio…nimelewa hivyo,….’akasema moto.

‘Sawa elewa unavyopenda na mimi nilifanya kilichoinjia akilini kwa muda, kama ilitakiwa iwe hivyo, basi imeshafanyika nifanyeje tena..’akasema

‘Ulipofika ulimkuta huyo mlinzi?’ akaulizwa

‘Hakuwepo...alikuwa katoka....’akasema

‘Ulijuaje kuwa katoka, yaani uligonga mlango kwanza, au uliingia ndani kwanza?’ akaulizwa

‘Yote mawili yalifanyika..niligonga , nilipoona kimia nikafungua, mimi naweza kufungua na kuingia, nilitaka kuhakikisha kuwa kweli hayupo, maana mtu unaweza kupitiwa na usingizi,…’akasema
‘Ulipoingia, hukukuta mtu, ulifanya nini?’ akauliza

‘Nilitizama mitambo, kuona usalama, ….na, nilishangaa kuona mitambo haifanyi kazi,….’akasema

‘Ulikuta mitambo haifanyi kazi, au ilizimika hu mtambo?’ akauliza

‘Nilikuta haufanyi kazi, umezimika kabisa….’akasema akionyesha wasiwasi

‘Ukachukua hata gani?’ akaulizwa

‘Mhh, unajua nilihitajika kujua kinachoendelea huko kwa mgonjwa, kwahiyo nikakimbilia huko, nikijua wenyewe wakifika, watajua cha kufanya, mara nyingi inatokea hivyo, unajizima,na wao wenyewe wanajua jinsi ya kufanya, nilijua katoka kwasababu hiyo ya kuhangaikia, uwake, inatokea ni  kawaida tu ….’akasema

‘Hukuulizwa kama uliingia humo, na walinzi baadaye?’ akaulizwa

‘Mhh, kama nilivyokuambia kulikuwa na mambo mengi yametokea muda huo kwa wakati mfupi, nakumbuka kama niliulizwa kitu kama hicho, na sijui niliwajibu vipi, nilikuwa nimezongwa na mambo mengi, maana kwa kipindi hicho ndio nimegundua mgonjwa hayupo, na msaidizi wa docta ana hali mbaya ….unaonaeeeh, kwahiyo huenda niliwajibu sivyo ndivyo, hata siwezi kukumbuka,….’akasema.

‘Hebu kumbuka vizuri, Wakati unaingia hukugusa waya, …inaonekana kuna waya ulikuwa umechomolewa, na wewe ndiye uliyeingia, na mlinzi anasema alitoka na kuacha kila kitu kipo sawa, je hukuchomoa, au kugusa waya?’ akaulizwa.

‘Waya gani , mbona sikuelewi....?’ akasema nesi kwa sauti ya kushangaa huku akiwa katoa jicho, kama kukasirikika au kutishia.

‘Unaniuliza mimi waya gani, unafahamu vyema huo waya ni waya gani, nesi,….unajua tusizunguke, kwenye huo mitambo kunaonyesha kila kitu,..hata kama waya ulitolewa, lakini kuna jinsi nyingine ya kuonyesha matukio,…kuna waya wa akiba unaofanyakazi kukitokea hitilafu, unalifahamu hilo…?’ akauliza.

‘Waya wa akiba! Waya gani huo wa akiba mbona mimi sijawahi kuuona, lakini mimi sijui zaidi mambo ya huko, waulize wenyewe….’akasema akiwa na mashaka.

‘Kuna waya wa akiba, unaoweza kufanya kazi hata kama waya mkuu umechomolewa, na tukaufanyia kazi, tukaona wewe, ukifuta kumbukumbu za siku, halafu ukichomoa huo waya na komputa ikazima,ungekuwa mjanja wewe ungefuta tu, na kuzuia, kumbukumbu zisipokelewe, sasa ujanja mwingi umekuumbua, unajua hilo ulilofanya ni kosa kubwa sana…..’akasema Moto akitaka kumaliza malumbano.
 ‘Mimi sijui lolote,na sikuelewi unachoongea, ina maana umekuja hapa kunishutumu, kunisingizia mambo ambayo siyajui, mbona sijasikia walinzi wakisema  kuna waya ulichomoka,...na kwanini nichomoe huo waya, kwanza waya gani unaozungumzia,ujue mimi ni kiongozi, siwezi kufanya kitu kama hicho….’akasema lakini sauti ilionyesha kushindwa.

‘Utaona kila kitu mahakamani,...tutaonyesha kama ushahidi,  na wewe utashitakiwa kwa kumsaidia mhalifu, kwa kufanya mgonjwa atoroke, na hujui ni kitu gani kimempata huko alipokwenda…’akasema Moto, na nesi macho yakaanza kulenga lenga machozi.

‘Nesi wewe ni mrembo, hebu fikiria uingie jela, wakuone hivyo, hebu mateso ya jela, na ukumbuke kama utaficha ukweli, kuna mteso makubwa utakumbana nayo ili useme ukweli wote, unaweza kuteswa kwa waya wa umeme, au ufungiwe kwenye chumba chenye nyoka, upo tayari kuzalilika, ni bora uongee na mimi nijua jinsi gani ya kukusaidia….’akasema Moto.

‘Chumba cha nyoka, mungu wangu, hapana, hamuwezi kufanya hivyo, nyoka, hapana, ninavyogopa nyoka…..’akasema sasa akionyesha woga

‘Ndio hivyo, mimi sitaki hayo yakukute, lakini nikishindwa, na kwa vile ukweli mimi ninao, nitawaachia wahusika wakushughulikie,…wakichka utarudishwa kwangu, najua hapo utasema kila kitu…’akasema Moto

‘Kwanini unanisingizia kitu ambacho sijafanya, mimi nimechoka, nahitaji kwenda kupumzika, kwanza umeshaniharibia kabisa siku yangu, kwani kuna nini kikubwa kimetokea, na kama unanishutumu kwa hilo, nitatafuta wakili wangu, naona sasa siongei tena….!’ Akasema akikunja uso kwa hasira.

‘Mpendwa, mitambo inaonyesha  kila kitu au unataka nikuonyesha,…’akasema Moto, kama vile anatafuta kwenye simu yake ili amuonyeshe jinsi ilivyokuwa na nesi akawa anamuangalia kwa mashaka.

‘Kwani hiyo simu yako inaonyesha matukio yaliyotokea kwenye Mitambo yetu...?’ akauliza

‘Hii mitambo  yenu pia ina mawasiliano na vituo vyetu vya usalama, kila tukio likitokea huku, inanakiliwa kwenye kituo chetu cha usalama kikubwa,  kwahiyo moja kwa moja, kila kinachotokea humu kinaonekana huko kwetu, tumekuona jinsi ulivyotoka wodini, ukaingia ndani ya hicho chumba.....ukafanya jambo kwenye komputa,  ukachomoa waya , halafu ukarudi chumba chako cha mapumziko…kila kitu kipo wazi,….’akasema Moto, akijua hapo anaweza kumpata.

‘Mimi nakubali kuwa  kweli nilikwenda hicho chumba, ….lakini ….sikuchomoa waya....hilo unanisingizia....kwanza waya gani, ni ule uliokuwa na matatizo, kama ni ule huwa uanachomoka wenyewe, huenda wakati naingia ulichomoka kwa bahati mbaya....’akatulia.

‘Swali ni  kwanini ulichomoa huo waya…nijibu vyema mpendwa, maana umeonekana kwenye hiyo mitambo…haikuwa Bahati mbaya, ulifanya makusudi,sasa swali ni kwanini ulichomoa huo waya?’ akaulizwa.

‘Nani kasema nilichomoa huo waya, kwanza waya gani?’ akasema akionyesha kama kuchanganyikiwa.

‘Tatizo lako unasahau kuwa japokuwa ulichomoa huo waya, lakini tukio la mwisho hapa kwenye mitambo yenu, achilia huko kwetu ambapo tuliona kila kitu, hapa kwenu  inaonyesha wewe uliingia kwenye hicho chumba, ukakuta mlinzi hayupo, na mlinzi aliporudi akakuta waya umechomolewa, na mtu aliyeingia humo ndani wakati yeye hayupo ni wewe, hakuna mwingine zaidi yako, sasa utakataa vipi kitu ambacho kipo wazi....’akaambiwa na hapo nesi  akatulia na Moto akajua sasa keshamfikisha kwenyewe, na nesi  sasa machozi yakaanza kumlenga lenga, akasema;

‘Sijasema mimi sijaingia, ....niliingia, lakini....’akasita.

‘Sasa nakupa nafasi ya mwisho,....usiposema ukweli, mimi na wewe mguu kwa mguu hadi kituo cha polisi,  unashitakiwa kwa kuvuruga mitambao ya usalama, utashikiliwa kama mtuhumiwa, uliyesaidia mhalifu kutoroka,na ukumbuke mateso, kuingizwa chumba cha nyoka uchi, ...’akaambiwa, nesi hapo akaonekana kuogopa, akasema;

‘Kwani huyo mgonjwa ni mhalafu,....mimi huyo mgonjwa aliniomba nimsaidie, sikujua kuwa ni mhalifu,,… alisema yeye anataka kutoka hapo hospitalini kuna kitu chake anafuatilia, lakini anaogopa akitoka ataonekana,...akaniomba nimsaidie  akimaliza atarudi, na atanilipa pesa nyingi, na mimi nikakubali, sikujua kuwa ni mhalifu...’akasema na Inspecta moyoni, akasema `bado hujafunguka vyema, umetunga tunga habari, mimi sikuachilii…’

‘Na inavyoonyesha kule hiyo sio mara yako ya kwanza kumfanyia hivyo, tulikuwa tukijiuliza kwanini unamfanya hivyo huyo mgonjwa,…ni kweli au si kweli?’ akaulizwa na nesi akatikisa kichwa kukubali.

‘Kwahiyo hilo la kuhangaika na kujipiga piga, mlitunga uwongo, wewe na yeye?’ akaulizwa.

‘Hapana hiyo inamtokea ana matatizo kama hayo kweli anaumwa,hata ungelikuwepo wewe ungejua kabisa anaumwa,ndio maana mimi nikamuonea huruma ....’akasema

‘Hebu niambie , huyo mgonjwa aliwezaje kutoka na alitokea mlango gani?’ akaulizwa
‘Alivaa nguo zangu za unesi..kwahiyo walinzi walijua ni mimi natoka,,..ndio maana hakuna aliyemshitukia....huwa mimi nikitoka, navaa mawani meusi,..na naendesha pikipiki, na yeye alifanya hivyo hivyo....alichukua pikipiki yangu...’akasema na Inspecta moyoni akajipongeza, akisema ;`sasa kazi imekwisha, kumbe ni mshirika wa kweli…’

‘Alielekea wapi?’ akaulizwa

‘Hapo sijui, ila alisema atarudi...’akasema

‘Wewe na yeye ni marafiki wa muda mrefu au sio?’ akaulizwa

‘Hapana nimejuana naye humu humu hospitalini...’akasema na inspecta akatoka simu yake, na kumuonyesha picha, picha hiyo ilionyesha nesi huyo akiwa kwenye hoteli wakila chakula na huyo mkuu

‘Hapa inaonyesha wazi kuwa wewe na mkuu mna mafungamano , au urafiki wa karibu, sio kweli kuwa mlijuana humu humu hospitalini, sisi tunafahamu, tuanwafahamu, hapa nakupima tu ili useme ukweli, ikibidi nijue jinsi gani ya kukusaidia, lakini naona hubebeki, ..’akasema Moto.

‘Sasa nimekuamia ukweli, naomba unisaidie, tafadhali….naogopa nyoka, naogopa kufungwa, nisaidie, nitakuambia kila kitu…..’akasema sasa akipiga magoti.

‘Nesi niambie ukweli,…. unapoteza muda wangu, na huyu mtu akipotea, wewe ndiye tutakushika, na kumbuka nyoka, ukiwa uchi, sema kila kitu huyo mtu apatikane na wewe uwe salama ....’akasema moto kwa ukali..

‘Atakuwa kaenda hoteli ya Paradise...’akasema

‘Kwanini unasema kaenda huko?’ akauliza Moto kwa ukali zaidi huku akianza kutafuta namba kwenye simu yake, na kutuma ujumbe

‘Aliniambia tutakutana huko...’akasema Nesi sasa akitaka kulia

‘Chumba gani…. ?’ akaulizwa Moto, akiwa keshaweka imu sikioni, akili sasa ikianza kuwazia jambo jingine, akijua hapo kazi imekwisha sasa anaingia kwenye mapambano ya mwisho.

NB: Tuendelee…..hapana tusubirie sehemu muhimu, ambao inaweza ikawa hitimisho
WAZO LA LEO: Kuficha muhalifu uliye na uhakika naye, ni sawa na kuficha nyoka mwenye sumu ambaye ipo siku atakugeukia. Mtu mwenye tabia ya uhalifu, ni mgonjwa, anahitajia kutibiwa, na kuna watu wanajua jinsi gani ya kuwasaidia hao watu, tusiwafiche, tukawatetea wakitenda uhalifu kama kweli tunahitajia wapone.

Na mara nyingi uhalifu tunautengeneza sisi wenyewe, kwa jinsi gani tunavyowalea watoto wetu, hatuwi karibu na watoto wetu, tukajua shida zao, elimu inakuwa ni gharama, na tunaona ujinga ni bora, watoto hawa wanaanza kuiga,kuingia kwenye makundi , wanaharibiwa, na mwisho wake wanakuwa wahalifu kweli. Tuwajibike kwa watoto wetu, tukiweka kipaumbele cha elimu, gharama nzuri kwa mtoto ni elimu.

No comments :