Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, November 13, 2014

DUNIA YANGU-62  Inspecta Moto, alipotoka mahakamani moja kwa moja alielekea huko hospitalini alipokuwa kalazwa mkuu wake wa kazi,..akilini akitaka kujua jinsi gani huyo mtu aliweza kutoroka hapo hospitalini, na wapi mtu huyo amekimbilia, na alijua sehemu ambayo itampa fununu, ni hapo hapo hospitalini, na atakayeweza kumsadia ni huyo nesi aliyekuwepo siku hiyo, na huyo docta msaidizi lakini kwanza lengo lake ni kuonana na huyo nesi

Na inspecta Moto alipofika hapo akaanza kuongea na nesi, kutokana na uzoefu wake, akahisi kuna jambo, nesi huyo atakuwa na jambo zaidi ya hayo anayoongea, akaona atumie mbinu zake za kiupelelezi, na kama hatafanikiwa kwa huyo atakwenda kuonana na docta msaidizi, alijua muda ni mali, lakini huenda muda atakaotumia hapo ukaweza kumsaidia, kichwani akiwa na hoja;

‘Kwanini mkuu wake akatoroka hospitalini, kwanini alipenda kutibiwa hapo, na kama alipenda kutibiwa hapo, basi watu wa humo wanamfahamu, je kuna nini kati ya mkuu huyo na kundi haramu,…’

Akazidi kumchimba yule nesi, kwa kumuuliza maswali

‘Uliwahi kumhudumia kwa kumuosha majeraha yake majereha yake mwilini, ukayaona vyema?’ akaulizwa

Tuendelee na kisa chetu.

*************

‘Hapana, hakutaka kabisa nesi  kumuhudumia  majeraha yake zaidi ya huyo docta mkuu na sana sana msaidizi wake, mwanzoni mimi aliniamini nikataka kumvua shati ili nimsafishe majeraha yake, akasema hapana yeye anahitaji docta mwenyewe amuhudumie  sijui ni msimamo wake, kuwa mwanamke hatakiwi kumuangalia mwilini au ana sababu nyingine….’akasema nesi

‘Ukisema labda ana sababu nyingine una maana gani?’ akamuuliza

‘Maana mgonjwa akifika hapa, docta humchunguza kwa mara ya kwanza, na wanahudumia majeraha mara nyingi ni manesi, baada ya kupata maelekezo kutoka kwa docta, sasa kwanini yeye akatae, ....ina maana yeye hana mke, sikumuelewa, lakini kwetu ni shangwe, maana unapunguziwa kazi...’akatulia

‘Kwahiyo hujui kabisa ana majerahani gani makubwa mwilini mwake?’ akauliza

‘Hayo yaliyopo mwilini yaliyofunikwa na shati, siyajui, ila hayo yanayoonekana mkononi nayafahamu, na uso wake hauonyeshi kabisa, kwa vile kafungwa karibu nusu ya uso, na hata kabla ya hapo mara nyingi yeye anapendelea kuvaa mawani ambayo yanaficha sehemu kubwa ya uso wake…’akatulia

‘Usoni na mkono ana majeraha ya kuungua...wanasema gari lake liliwaka moto…kwahiyo aliuungua vibaya, na nahisi kuna majereha mengine  makubwa mwilini, mimi hayo ndiyo siyajui….’akasema

‘Wanasema gari lake liliungua..akina nani hao, na alipofika hapa, wewe ulikuwepo  wakati analetwa.....?’ akaulizwa

‘Ndio nilikuwepo, ni kweli gari lake limeungua, wamesema hao maaskari wanaomlinda, wanasema kaponea chupu chupu,…na ni kwa vile kuna mtu aliwahi kumvuta mapema nje ya hilo gari, kwani alishapoteza fahamu..., vinginevyo, angeliungua kabisa….’akasema huyo nesi

‘Hebu nikuulize wakati anajipiga piga akiwa kama unavyosema, kama ana mashetani huwa anaongea lolote akiwa katika hali hiyo?’ akaulizwa

‘Mhh, kuna muda anasema, sijui...dunia, kitu kama dunia…halafu anacheka kwa mbwembwe, huku ekiendelea kusema, dunia yangu, dunia yangu..kitu kama hicho....ehe..anakuwa kama anaona kitu, halafu anatabasamu, halafu huyo analala muda  huo ikeshapigwa sindano....’akasema

‘Unafikiri ni kwanini anasema `dunia yake, nakumbuka hata wewe wakati unanisalimia ulitamka kitu kama hicho, hio dunia yangu ina maana gani?’ akauliza Moto

‘Hata sijui, …unajua tumeshamsikia akisema hivyo, na sisi tunamuiga tu kama vichekesho, siunajua tena mkishakutana mahali jambo dogo linawezwa kukuzwa ikawa ndio wimbo,….’akasema akiwa kaangalia kmuelekeo wa mapaja yake.

Inspecta Moto, akatulia kidogo kuwaza, halafu akamuangalia yule nesi kwa makini, kabla hajamuuliza swali, na yule nesi akainua uso na uso wake ukakutana na wa Inspecta, Inspecta akatabasamu, na huyo nesi aonyesha uso wa kushangaa, kumuona Inspecta anamuangalia hivyo, anatabasamu, akataka kusema neno lakini Inspecta akamuwahi kwa kumuuliza swali;

‘Hapa kazini kwenu mnalipwa vizuri eeh?’ akauliza

‘Kawaida tu…..’akasema

‘Mhh, na wateja kama hao wenye pesa wakija, wanawakatia kitu kidogo,au sio?’ akauliza

‘Naona kama umeishiwa maswali,  naweza kuondoka?’ akasema nesi.

‘Bado, usiondoke mpaka hapo nitakapomalizana na wewe, ni muhimu sana….’akasema Moto

‘Kwani unataka nini zaidi, nimeshakuelezea kila kitu…na sasa unataka kuingilia maisha binafsi….’akasema Nesi.

‘Una uhakika hukumuona huyo mgonjwa akitoka hapo mlangoni…?’ akauuliza Moto akimuangalia moja kwa moja usoni

‘Nimeshakambia sikumuona,  tatizo lenu nyie watu mking’ang’ania kitu, hamtaki kukubali ukweli, au unataka nikuapie, naapa sikumuona akiondoka, mimi nilikuwa kwenye chumba cha docta nikisubiria, nilipoona anachelewa ndio nikatoka kumfuata docta mkuu msaidizi...’akasema kwa hasira

‘Tulia mpendwa, tunasaidiana tu, unajua hata mimi sipendi kukuotezea muda wako, lakini sisi watu wa usalama kuna mambo tunaangalia, jambo dogo kwako, kwetu linaweza kutusaidia sana….usijali tafadhali shirikiana na mimi, siku yako ipo pale pale, ikibidi tutatoka wote…’akasema

‘Sitaki kutoka na yoyote, siku yangu umeshaiharibu, nikitoka hapa ni kwenda kulala….unajua nimekimind ile mbaya, yaani moyoni, ungelijua,…..nilijua siku imefanikiwa kumbe mkosi….’akawa analalamika…

Inspecta akamuangalia, halafu akatabasamu na kuuliza swali

‘Kuna milango mingapi kwenye hicho chumba alichokuwa huyo mgonjwa?’ akauliza Moto bila kujali hayo malalamiko ya huyo binti, kwake yeye ni nafasi ya ushindi.

‘Kuna mlango wa dharura, unatokea nje, na mlango huu wa huku ndani....’akasema

‘Kwahiyo yawezekana alitokea mlango huo wa dharura?’ akaulizwa

‘Inawezekana….mimi sijui, lakini huko kulikuwa na maaskari wakilinda, angelitokaje huko askari wangelimuona, ....’akasema akionyesha kutokuwa na furaha.

‘Basi atakuwa alitokea mlango huu wa ndani au sio..lakini na wewe muda huo ulikuwa wapi…?’ akauliza Moto.

‘Mimi nilikuwa ofisi ya docta, ile pale,  kama angelitokea mlango huu wa ndani, ningelimuona akipita, labda kama alipita haraka nikiwa sijaangalia mlangoni, maana mlango wa docta ulikuwa wazi, na muda huo sikuwa na mashaka ya kuchunguza, si unajua...’akasema

‘Kwahiyo unataka kusema nini, kuwa huyo mgonjwa alipaa hewani?’ akauliza Moto

‘Nataka kusema hivi…..aah, mimi nimeshachoka…’akasita kidogo

‘Aaah, wewe niambie ulivyotaka kusema, ulivyoelewani, uwoni wako, kama nilivyokuambia nia ni kusaidiana, tumpate huyo mtu…..’akasema Moto.

‘Nilitaka kusema hivi, huyo mtu ni mtu wa ajabu,  fikiria matendo yake, halafu fikiria kuwa ni mgonjwa, ...sasa kama alipita hapo mlango kwa haraka hivyo, nahisi sio mtu wa kawaida, ...na ndio hivyo kutoweka  hata hatujui kakimbilia wapi, lakini sizani kama atakuwa na matatizo,yupo salama mahali kapumzika tu,,...ila namuona kama sio mtu wa kawaida...’akasema nesi

Inspecta, akatulia kwanza kama anawaza jambo, halafu akasimama na kusema;

‘Hebu nisubiri hapa, kuna kitu nataka kuhakikisha…usiondoke…’akasema Moto na kutoka pale kwenye sofa, na kutembea kuelekea chumba alichokuwa amelazwa huyo mgonjwa, huku nyuma nesi akawa analalamika kwa kusema;

‘Ukichelewa mimi naondoka…kama mna matatizo mengine, tutaongea siku nyingine, nasubiri kidogo tu….’ Inspecta hakujali, alijua hawezi kuondoka, akaingia chumba alichokuwa amelazwa huyo mgonjwa aliyetoroka.

Inspecta Moto, alijaribu kuangalia kile chumba alichokuwa anahudumiwa  huyo mgonjwa , kilikuwa na kitanda, na vifaa vyote vya kimataibabu, na mawaya waya, mashne za kupumulia, na kulikuwa baridi, kutokana na kiyoyozi kufanya kazi, akakagua dirisha, akaona mtu hawezi kupitia dirishani, na hakuna sehemu nyingine ya kutokea zaidi ya milango hiyo miwili,

‘Kwahiyo ni lazima alipitia kati ya hii milango miwili, ....sasa ni mlango upi....?’ akawa anajiuliza, na wakati anajiuliza akawa sasa anatoka nje kwa kupitia mlango huo wa dharura, akatoka nje kabisa, na kuanza kutembea, akijaribu kuhisi kama huyo mtu alitoka, atakuwa kapitia hivi au vile, akatembea hadi kwenye chumba kilichojitokeza na kiko kama ofisi ya nje inayojitegemea, akaona kumeandikiwa;

‘Chumba cha usalama, na mawasiliano, usiingie hapa….’

Yale maandisi yakamvutia, akasogea pale mlangoni, akagonga, ilichukua muda na alipotaka kugonga tena, mara mlango ukafungulia, alitoka jamaa akiwa na sare za askari za hapo hospitali maana wao wana sare zao kama hospitali.

‘Samahani mimi, ni askari usalama, naweza kuongea na wewe kidogo…..’akasema akitoa kitambulisho chake kumuonyesha huyo askari, na huyo askari hakukiangalia, akasema;

‘Karibu, nimeshakufahamu….’akasema

 Inspecta hakutaka kumuuliza kamfahamu kivipi wakati hawajakutana…aliingia ndani, na mlango ukawa umejifunga nyuma yao. Alipofika ndani akaanza kuchunguza kile chumba kwa macho, kulikuwa na mitambo ya mawasiliano, komputa kubwa, inayoonyesha matukio na mizunguko ya watu humo kwenye hilo jengo.

‘Kwahiyo hapa mnaona kila kitu kinachoendelea hapa hospitalini?’ akauliza

‘Kabisa mkuu..’akasema huyo jamaa

‘Kama ni hivyo, basi mtakuwa manafahamu huyu mtu aliyetoroka alikwenda wapi, au sio?’ akauliza

‘Mhh, hapana kwa huyo hatujui kwasababu..’akasema na kutulia

‘Niambie sababu zenyewe….’akasema Moto.

‘Sikuwa hiyo ya tukio mitambo yote ilikuwa haifanyi kazi…’akasema na Moto alitarajia kitu kama

‘Kwanini  siku hiyo mitambo ya kunasia matukio ilikuwa imezimwa ?’ akaulizwa huyo mlinzi

‘Kulikuwa na hitilafu tu za kawaida huwa inatokea mara kwa mara, ila safari hii ilibidi tumuite fundi, maana tulishindwa kugundua tatizo, tulijitahidi tulivyozoea, lakini ikagoma kabisa, ikabidi tumuite fundi, na fundi alipofika akagundua kuwa kuna waya mmoja ulikuwa umeachia...’akasema

‘Waya huo uliachia au ulichomolewa…au mlimuita fundi ili awe shahidi kuwa mitambo ilikuwa haifanyi kazi.?’ Akaulizwa

‘Hapana mkuu, sio hivyo….kwanini tumuite tu, tulimuita kwa vile kweli kulikuwa na tatizo, sema tatizo limetokea siku kuna taizo kama hilo….’akasema

‘Lilikuwa tatizo gani?’ akauliza

‘Ni kama mtu alikuja akauchomoa waya, kwa jinsi alivyodai fundi, lakini hakuna mtu ambaye angeliweza kufanya hivyo, mimi siku hiyo sikuwepo, alikuwepo mwenzangu, yeye anasema alitoka kidogo tu,na hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia huku bila sisi wenyewe kuwepo, labda viongozi wa hospitali tu, na akitoka mlango unajifunga mpaka uwe na namba ya siri kama unavyoona hapo mlangoni....’akasema

‘Viongozi ukiwa na maana wamiliki wa hii hospitali au kuna viongozi wengine.....ni nani mwingine zaidi ya hao viongozi, ni wewe na mwenzako na nani mwingine?’ akaulizwa

‘Ni mimi na mwenzangu, mwenzangu ndiye aliyekuwa zamu siku hiyo,...’akasema

‘Hebu niambie alisema ilitokeaje?’ akauliza

‘Alisema yeye alitoka kidogo,...kuna kitu alifuatilia masijala, na alijua hatachukua muda, na kweli hakuchukua muda sana akarudi  aliporudi, akakuta mtambo haufanyi kazi, komputa imezima,  haraka akajaribu kurekebisha , lakini mitambo haikukubali kabisa....basi yeye kwa haraka akanipigia simu nijaribu kutoa mawazo yangu, nilimuelekeza nilivyoweza, lakini hakufanikiwa, ndipo nikamshauri amuite fundi, na ndio fundi akagundua kuwa waya huo ulikuwa umechomoka....’akasema

‘Naweza kuuona huo waya..’akasema Inspecta, na huyo jamaa akamuonyesha, ni waya mnene kidogo, unaonekana ukichomoka unazima kila kitu

‘Hakuna chombo cha kuhifadhia moto, kama umeme ukikatika?’ akauliza Moto

‘Huo waya sio swala la umeme,…ni waya wa mtandao wenyewe..hapo ulikuwa umeliwa na panya siku za nyuma, ukaunganishwa, kwahiyo, uliachia, …au mtu aliuvuta ..tunataka fundi aweke waya wenyewe kabisa sio wa kuunga kama hivi, hilo linafanyiwa kazi….’akasema

‘Yeye alikuambia wakati anatoka, kulikuwa na kiongozi anayeruhusiwa kuingia hapo siku kati ya hao wanaoruhusiwa kuingia…..?’ akauliza

‘Kama nilivyosema, wanaoruhusiwa kuingia humu ndani , ni docta mkuu, hakuwepo na msaidizi wake, alikuwa huko kazini kwake, ....na..ndio na mwingine ni nesi mkuu., ukiacha sisi walinzi..’akasema

‘Nesi mkuu ndio yupi?’ akaulizwa

‘Ni huyo aliyepo zamu leo, nilikuona ukiongea naye...’akasema na inspecta akatikisa kichwa kukubali jambo.

‘Inawezekana yeye aliingia?’ akaulizwa

‘Sizani, hapana, kwasababu aliulizwa, akasema  hakuwahi kuingia kabisa,...’akasema

‘Hawezi kudanganya?’ akaulizwa

‘Hapana hawezi kudanganya maana ni kiongozi,...na kwanini adanganye, kwanini achomoe waya, sioni sababu ya msingi.....’akasema huyo askari

‘Hebu nionyesha matukio ya kabla ya mtambo haujazimika….’akasema Inspecta, na mtambo ukarudishwa nyuma na kuonyesha matukio kabla ya mtambo kuzimika siku hiyo.

‘Mhh, sasa, ina maana mtambo ukizimika, matukio ya siku nzima hufutika, maana naona yameanzia mbali kidogo, kwa tarehe hiyo, naona hapa, kuanzia, asubuhi saa..mmmh, ikafika hapo saa nne, kukakatika, hakuna kitu mpaka, saaa mmmh, huoni hpa kuna pengo,….ni kama kumefutwa au?’ akauliza Inspecta

‘Hata sisi uliliona hilo,…inawezekana katika `ku-save data’, mtambo uliporekebishwa, fundi alianzisha bila kuangalia kama matukio yote ya siku hiyo yamehifadhiwa, akakubali tu kuwa ipo safi, na komputa ikachukulia zile kumbukumbu za nyuma zilizohifadhiwa, alitakiwa abonyeze kitufe cha marekebisho, ambacho kingemuonyesha matukio yaliyokuwa hayajahifadhiwa, ili yawepo, kwahiyo yakapotea yaweza ikawa hivyo…..’akasema

‘Ok sawa,  nashukuru, ila ninaweza kurudi baadaye kama nitakuhitajia au kumuhitajia mwenzako, mwenzako anaingia saa ngapi…?’akaulizwa

‘Leo hatakuwepo mpaka kesho…..’akasema, na  Inspecta na akarudi kule alipomuacha nesi, na akamkuta  akiongea na simu yake, akiwa kasimama, na Inspecta hakuchkua haraka kumsogelea , yule nesi alikuwa hajamuona, akamaliza kuongea na simu, sasa akarudi kukaa kwenye sofa na kuanza kuchati, inspecta akatuma ujumbe kwa watu wake kwa kuandika:

'Chunguza nesi kapmpigia nani muda huu'

Halafu taratibu akamsogelea nesi,nesi hakuratajia kabisa kuwa Inspecta atatokea mlango huo, alipomuona Inspecta, akitokea mlango wa kuingilia, sio kule alipokuwa ametarajia kuwa atatokea kwenye chumba cha wagonjwa mahututi, akasimama, utafikiri bosi wake kaingia.

‘Mbona umechelewa, hivyo, …na mbona umetokea huku, mimi nilijua upo ndani ya chumba hicho cha wagonjwa wa dharura…?’ akauliza akionyesha wasi wasi

‘Mhh, yah,…usijali, ndio kazi zetu hizo,….’akasema akimuangalia yule nesi akiwa kasimama sasa kwa adabu, akiwa kama anaficha simu yake macho ya Inspecta yakahisi, na akasema;

‘Mhh, Kumbe una adabu namna hiyo, hebu tafadhali naomba hiyo simu  yako mara moja…’akasema Inspecta na yule nesi akasita, halafu akainua mkono na kumkabidhi inspecta , Inspecta akachukua, na kuangalia simu za karibuni, na nani alikuwa akimpigia, namba haina jina, akaangalia simu zilizopigwa siku mgonjwa huyo alipotoweka,  majina yalikuwa yameandikwa kwa kifupi kifupi,….akachukua kalamu yake, na kuandika baadhi ya namba.

‘Samahani nafanya haya kuhakiki jambo, sio kwamba naingilia mambo yako binafsi, muhimu ni kupima ukweli wako…nimeona tarehe hiyo ya tukio, siku mgonjwa alipotoroka,  uliongea na watu watatu, wane, naona hii namba imejirudia rudia lakini haina jina, unaweza kuniambia ni nani huyu….?’akaulizwa Inspecta…

‘Mhh sikumbuki kwakweli, nikiwa kazini naweza kuongea na watu wengi tu, ni mpaka nimpigie ndio nitajua ni nani, ina maana hata watu nilioongea nao ni kosa, mbona wanatia mashaka…..’akasema

‘Aaah, usijali, mpendwa,…ni kawaida,…..’akasema

‘Sasa utauliza, siku hiyo nilalala na nani, si unataka kujua kila kitu cha siku hiyo, siku hiyo,nilichoka sana, tena nilikuwa sipo safi,...si unataka kujua,  nilifika nyumbani nikalala kama gogo, huo ndio ukweli….’akasema

‘Ok, kuna mambo muhimu, nahitaji kukumbushana, yanaweza kusaidia sio kila jambo , huenda ikabidi kukumbushana, ila kama itahitajia kujua ni nani mliongea naye, kama ni muhimu kumjua usijali nikija kukuuliza tena, na wala usije kumpigia huyo mtu simu kumshitua kuwa asema hiki au kile, hayo tunaweza kuyapata ofisi za simu, tukitaka,…..’akasema Moto na yule nesi akaonekana kuwa na wasiwasi sana.

‘Kwani  wewe unanishuku nini mimi, mpaka unifanyie hayo yote, yaonekana kama unanishuku mimi kitu fulani, nimekosa nini, naomba uniweke wazi , ili kama ni kumtafuta wakili wangu nifanye hivyo, unanitia mashaka, nina kosa gani….?’ Akauliza

‘Kwani unahisi una kosa?’ akauliza Moto

‘Unavyonifanyia, kama vile mimi ni mhalifu….’akasema

‘Nesi, kwenye kumbukumbu za matukio, inaonekana wewe uliingia kwenye chumba cha vifaa vya kunasia matukio, ulifuta nini?’ Inspecta hakujali hayo malalamika akamuuliza huyo nesi hilo swali, na nesi akashtuka, na kusema;

‘Mimi, nani kasema....?’ akauliza akimuangalia Inspecta kwa macho makubwa

‘Sio nani kasema, mitambo inaonyesha hivyo, ulionekana ukiingia kwenye chumba cha  mawasiliano, na kutoka kwa haraka, je ulifuata nini?’ akauliza inspecta Moto kwa mtego, japokuwa hakuona tukio hilo kwenye hiyo mitambo, maana  kumbukumbu za karibu siku nzima hazikuonekana zote. Huyo nesi akamuangalia Moto, kwa macho makubwa, akionyesha kushitushwa na swali hilo.

NB: Huyu Nesi ni muhimu sana kwahiyo bado tupo naye, na huenda akatupeleka kwenye hitimisho la kisa ngoja tuone?


WAZO LA LEO: Ushindi wa ulaghai, usio na nia njema, sio ushindi, ushindi huo hauna thamani, hata kama kwa kufanya hivyo, umefanikiwa, kimasilahi, kimadaraka, lakini moyoni unafahamu dhahiri kuwa hujashinda kihalali,  ujue huo ni wizi, unakula dhuluma, hapo aliyeshinda ni huyo uliyemlaghai, japokuwa hana kitu, au hajapata wadhifa, au vyovyotevile,  lakini kwa mungu huyo ndiye mshindi, na ana thamani kubwa kuliko wewe hasidi, fisadi, mlaghai. Tuache tabia ya ulaghai, kupata jambo kwa dhuluma, ni wizi .

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Kisa kinazidi kunoga,nasubiri cha kesho