Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, November 6, 2014

DUNIA YANGU-59


‘Huyu mtu ameshakufa sio?’ akaulizwa
‘Ndio ameshakufa..’akasema docta
‘Haya hebu tuambie kuhusu kifo chake, kilitokeaje

Tuendee na kisa chetu

*************

‘Kifo cha huyu muheshimiwa kilikuwa cha kusikitisha kidogo, japokuwa kwa wengi ilionekana ni furaha,  watu wengi, hawa wanachama wa hilo kundi, walishanza kumchukia , kutokana na tabia zake za ubabe, alikuwa ni kiongozi mwenye msimamo mkali, akitaka jambo lifanyike ni lazima lifanyike, na lisipofanyika, adhabu yake ni kubwa, mateso makali, ambayo humfanya hata mtu mwenyewe atamani kujiua, au kifo cha hapo hapo, wengi walipotea kiajabu na  inasadikiwa yeye ndiye aliyewaua.

‘Lakini hakuna hata aliyemshuku….’akasema

‘Mimi mwenyewe nilishudia mtu akiteswa kwa hizo dawa,  hadi anaamua kujiua mwenyewe, na kesho yake mtu huyo anaokotwa majalalani au kwenye mtaro, inaandikwa kuwa alijiua mwenyewe, aua lipigwa kama kibaka, au aliuwawa na majambazi, na hakuna zaidi…lakini asilimia kubwa waliteswa na madawa niliyotengeneza…’akasema

‘Madawa gani hayo..?’ akaulizwa

‘Kuna madawa ukipigwa na sindano unapata maumivu makali sana mwilini, maumivu yake ni makali sana,..mwenyewe utatamani ujiue..inategemea umepewa dozi kiasi gani, kama ni mateso ya muda, kuna kiwango chake, na kama unatakiwa ujiue, kuna kiwango chake…’akasema

‘Kwahiyo kumbe wewe ndiye uliyekuwa ukitumika kwa dawa zako kufanya watu wengine wajiue, wafe…?’ akaulizwa

‘Kwakweli hali hiyo sikuipenda, ..na ili kuonyesha hilo, mimi mwenyewe nilikwenda polisi, nikiwa na ushahidi  , nikamuendea mkuu wa kituo, ….huyo jamaa siku hayupo, kahamishwa kwenye hicho kituo angelithibitisha hili,…nikamuelezea kinachoendelea akasema atafuatilia, lakini sikuona matokea, nikaona kwanini nisende kumuona mkuu wa kitengo cha usalama kabisa ambaye  kutokana na kusakamwa kipindi kile nilishajenge mazoea kidogo na yeye, , kama nilivyoelezea awali, mkuu huyo ndiye aliyetoa kibali cha mimi kwenda kusoma,nilijua nikiongea naye mambo yatakwenda haraka..

‘Siku moja nikaonana naye kwa siri, nikamsimulia yote yanatokea hapo, ni kipindi  jamaa alipofariki, nilijua hakuna atakeweza kunisakama tena,  nilimsimulia kila kitu, hakuamini, akasema namsingizia huyo jamaa, kwani yeye anamfahamu vyema, ni mtu wa kusaidia jamii, haweza kufanya hayo mambo …akasema

‘Mimi nina ushahidi huu hapa..’anikamwambia

‘Upo wapi, ni huu wa CD, hivi vitu watu waantengeza tu, hebu nione…’niamuonyeshea, akaangalia na kusema;

‘Ok, niachie nitachunguza, na kama nikiona ni fitina, utwajibika, unanifahamu nilivyo…’akasema na mimi nikaondoka, nikijua kuwa atachunguza

 ‘Siku hiyo niliporudi kazini kwangu, nikijua sasa hilo kundi litagundulika, na litafikia mwisho wake nikakutana na ujumbe kuwa nahitajiwa makaoni,makaoni ina maana ofisi maalumu ambayo unaongea na huyo  jamaa, lakini yeye humuoni, ni nembo yake, ile ya ‘dunia yangu..’ na sikutarajia tena kuwa hali hiyo ya kuitwa kama hivyo itakuwepo, kwani jamaa alishakufa, sasa ni nani anaweza kuniita kihivyo

‘Nilipofika, nikaonyeshwa jinsi gani nilivyokutana na huyo mkuu, na yote nliyoangea naye, nilichoka,..nikajua sasa nimekwisha, sasa niuwawa..akilini nikawa nawaza ni nani anayefanya hiyo kazi yake, sikuweza kupata jibu….’akasema

‘Kwani ukifika hapo mnawasiliana vipi na huyo jamaa?’ akaulizwa

‘Kuna sauti inatokea kwenye spika, ndani ya hicho chumba….mnawasiliana kabisa kama vile yupo hapo karibu mnaongea naye, mnajibishana kama kawaida tu, ila yeye ndio haonekani…’akasema

‘Baada ya kuonyeshwa hivyo uliambiwaje?’ akaulizwa

‘Sitakuua, ..ila nitakupa adhabu ya kukupa fundisho,…kwa dawa zako mwenyewe….’nikaambiwa, na mra akatokea docta mwenzangu, huyu ambaye nasema ni docta mwenzangu kwenye kundi, akaambiwa anipige ile sindano ya mateso…kitu nilichokitengeneza mwenyewe, kikanitesa,..niliomba waniue….ilikuwa nusu saa, lakini mateso yake….toka siku hiyo nikasalimu amri..hapana, inatesa, sikujua nimetengeneza kitu chenye kuumiza kiasi hicho..’akatulia.

‘Baada ya hapo ikawaje?’ akulizwa

‘Kwahiyo nikawa nafuata kila ninaloambiwa…’akasema

‘Ehe, hebu tuambie kifo chake kilitokeaje?’ akaulizwa

‘Masiku kabla ya kifo chake  ilikuja taarifa kuwa huyo jamaa anaumwa, lakini anachoumwa hakijulikani, mimi natakiwa kumchunguza, maana wanahisi ni matatizo ya akili, siku hiyo nikasema sasa na mimi nitapata nafasi ya kumuonyesha kuwa na mimi ni docta..nilidhamiria kumfanya lolote baya, hasa nikikumbuka hayo mateso,…

‘Kabla sijaonana naye, Ikaja taarifa kuwa huyu jamaa kachanganyikiwa, anaongea ovyo, na hapatani na mama yake,  na hataki kuonana  na mtu yoyote zaidi ya mama yake, akawa ni mtu wa kushikwa, nikasema basi niende huko alipo nionane naye, lakini siku hiyo kabla sijafika akatoroka na hakupatikana, mpaka tuliposikia mwili wake umeokotwa, ufukweni mwa bahari, akiwa amekufa…’akasema

‘Ni nani aliyekwenda kukagua mwili wake?’ akaulizwa

‘Ni docta mwenzangu yule mtaalamu mwenzangu wa kundi, mimi siku hiyo nilikuwa na kazi nyingi, akaenda yeye, na yaliyofanyika huko aliyajua yeye, ila aliporudi aliniambia kuwa kuna siri kubwa imejificha kwenye kifo chake..’akasema

‘Siri gani hakukuambia?’ akaulizwa

‘Hakuwahi kuniambia, maana yeye kama nilivyo mimi tulikuwa na mihangaiko yetu ya kimaisha, kukutana labda ndio kama kuna kikao cha dharaura, na kila mmoja aliogopa kuongea na mwingine kuhusu ubaya wa hilo kundi, kwani ukiongea chochote kinakuwa kimeshafika kwa huyo jamaa au watu wake..’akasema

‘Watu wake akina nani zaidi na nyie.?’ Akaulizwa

‘Kulikuwa na watu wake wa karibu, hao ni kama walinzi wake, ambao walikuwa wakimtii haswa….na wenyewe hata hatujui wamepotelea wapi, ….’akasema

‘Je Mazishi yake yalikuwaje…?’ akaulizwa

‘Ajabu iliyoje…ilitangazwa kidogo kuwa huyo jamaa mumiliki wa hiyo hoteli amekutwa akiwa amekufa, na haikutangazwa zaidi, hata kwenye ile habari kwenye gazeti ilikuwa ni maneno machache tofauti na kujilikana kwake..hata mazishi yake yalikuwa ni ya ajabu ajabu, kwani walikuja wazee kutoka kijijini, na wakamzika kimila, wanadai huyo ni mmoja wa viongozi wa kimila, na taratibu zao, ni hivyo, anazikwa na watu wake maalumu.

‘Kwahiyo waliokuwepo kwenye mazishi, yaani kwenye makaburi ni hao wazee na mama yake, hakuna mtu mwingine aliyeruhusiwa kufika karibu, sisi tulihudhuria, lakini tulikaa mbali kabisa, wao wakiendelea na mambo yao, wakamzika, tukaja kuambiwa tayari tunaweza kutawanyika, na kuanzia hapo mama ndiye atashika hatamu…’akasema

‘Kwahiyo mama akawa ndiye kiongozi wa kundi au familia?’ akaulizwa

‘Kundi kama kundi lilikuwa likiendeshwa kinamna, sijui ni nani alikuwa akitoa maagizo, ila kila mara kukitakiwa jambo, inakuja ile ile nembo yake kama ailivyokuwa, awali….na mambo yaliendelea vile vile, mtu akikosa adhabu ni vilevile…hakukuwa na mabadiliko, sasa ni nani alikuwa akifanya mambo yake, mimi kwakweli skuwa nafahamu, ndio maana kipindi kile nikaamua kwenda polisi lakini ndio kama ilivyotokea…’akasema

‘Huyo bosi wenu alizikiwa wapi?’ akaulizwa

‘Pale pale makaburini ya msasani, …kaburi lake lilikuwa karibu na nyumba yao ya awali, ndio hiyo iliyoungua,…kwahiyo hata kaburi lilipangwa liwe karibu na hiyo nyumba, …’akasema

‘Kaburi lake halikujengewa,..?’ akaulizwa

‘Hapana, walisema mila zao haziruhusu kaburi kujengewa,…lilikuwa la kawaida tu, na alama kuonyesha kuwa kuna kaburi..’akasema

‘Je wewe uliwahi kufika eneo la hilo kaburi?’ akaulizwa

‘Hapana…..kuna kitu tuliambiwa kuwa hakuna mtu anayeruhusiwa kufika eneo hilo,..hata watu wakienda kuzika, hawasogeleo eneo hilo, kuna wengine wanasema, kila aliyesogelea hapo, anapatwa na matatizo, anakufa….kwahiyo ikajengeka nadharia kuwa ukitaka kwenda kuliona hilo kaburi, ujue unakwenda kutafuta umauti wako…watu wakaogopa kabisa kukaribia eneo hilo…..’akasema

************
‘Ndugu muheshimiwa hakimu, tulihitajika kumuita shahidi mwingine, mtaalamu wa mitandao kwenye hili kundi, lakini bado akili yake haijawa sawa, kutokana na hayo madawa waliyodungwa nayo, pia wenzake ambao ni mashahidi muhimu, hali zao hazijakaa sawa, tunaona tuendelee na huyu shahidi  ili tupate ushahidi anaoujua yeye, 

‘Huyu ni docta anayetambulikana kwahiyo ushahidi wake unakuwa na nguvu zaidi,…..’akasema muendesha mashitaka na hakimi akasema aendee na huyo shahidi

‘Hebu tambie kuhusu kifo cha muheshimiwa mbunge, je aliuwawa na kundi au alikufa kwa shinikizo kama ilivyodaiwa ?’ akaulizwa.

‘Kifo cha muheshimiwa mbunge kiukweli sikuwa na uhakika nacho, ila inawezekana aliuwawa na mbinu za kundi…sina uhakika, maana kipindi hicho, nilikuwa bado mgeni, nilikuwa siambiwi kinachoendelea, ila siku kabla hajafariki huyo muheshimiwa, niliambiwa nitengeneze hizo dawa,…’akasema

‘Dawa za namna gani?’ akaulizwa

‘Dawa ambazo akipewa mtu anaanza kujenga hali ya kujisikia vibaya, na hali hiyo hiyo inakwenda kupandisha au kushusha mapigo ya moyo, na hapo hujenga mashinikizo ya damu, na kinachofuata hapo ni kiharusi..’akasema

‘Hebu tufafanulie kiharusi ni nini?’ akaambiwa

‘Kiharusi ni hali inayotokea pale mishipa inayosambaza damu kwenye ubongo inapopatwa na misukosuko kiasi cha kushindwa kupeleka damu kwenye ubongo na hivyo kuathiri ufanyaji kazi wa ubongo kwa zaidi ya masaa 24,…

‘Dawa ninazotengeneza mimi ukishapewa, kwa kupitia kwenye kinywaji,au sindano, au inaweza ikapakwa kwenye kipaza sauti cha kuongelea ukavuta,….basi dawa hiyo hufanya kazi haraka, na kwahiyo hata kabla ya masaa manne, utakuwa umeshaathirika, na kiharusi huja haraka, na kinachofuata ni kifo tu, na huwezi kujua kabisa kama kuna dawa umepewa, dawa hazo hazina kipimo cha kuzigundua…’akasema

‘Kwahiyo kutokana na hizo dalili, muheshmiwa mbunge atakuwa amuwawa na hizo dawa?’ akaulizwa

‘Yawezekana,….kwa jinsi nilivyopewa taarifa zake na dalili za kifo chake, yawazekana kabisa aliathirika kutokana na hizo dawa..’akasema.

‘Kuna kifo kingine kilitokea, cha mke wa Inspecta, je  alijiua mwenyewe, au ni kutokana na hayo madawa yako?’ akaulizwa

Wakati swali hilo linajibiwa, Inspecta Moto akiwa ametokea nje, ambapo alitoka kusikiliza simu, aliingia na kumuendea muendesha mashitaka, Inspecta Moto alionekana mwenye wasiwasi, akawa anamnong'oneza kitu mundesha mshitaka, na muendesha mashitaka akasema;

'Haiwezekani, una uhakika, imekuwaje, basi akamatwe haraka...kwanini, hayupo ametoweka, ooh, shittt..'akakatiza na kugeuka kuendelea na kesi akimuomba hakimu samahani...

'Muheshimiwa hakimu, samahani kwa hali hii niliyoionyesha sasa hivi , ni kwasababu kuna tatizo limetokea.....'


WAZO LA LEO: Elimu yako uliyo nayo haitakuwa na maana kama haitakuwa na msaada kwako, na kwa jamii inayokuzunguka, elimu sio shahada tu au stashahada au ganda kuonyesha kuwa umehitimu. Elimu inatambulikana kama elimu, kutokana na matunda yake kwa jamii na mabadiliko yako katika shughuli zako, elimu bora ni ile yenye matunda mema kwa jamii, kutokana na elimu yako wenzako wakaiona kama dira, na kutamani kuwa wawe kama wewe. Elimu ni mtaji unahitaji kuwekezwa ili kueleta faida chanya.

Matokeo ya mitihani darasa la saba yameshatoka, tunawapa hongera watoto wetu na tunachopenda kuwaambia ni kuwa huo ni msingi tu, bado kupandisha ukuta ili nyumba iweze kusimama, bofya hapa uone matokeao yao kutoka NECTA:

http://necta.go.tz/psle2014/

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Kiss kinazidi kunoga,nasubiri cha kesho