Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, November 3, 2014

DUNIA YANGU-57


‘Ndugu muheshimiwa hakimu, najua wengi wameshajenga chuki dhidi yangu tayari, ndio maana wengine wamefikia kuniita muumiani , jamani mimi sio mbaya kihivyo, kama mnavyofikiria  nyie...mimi ni docta kweli wa kuwasaidia watu....’akasema na watu wakaguna

‘Nafahamu kwanini mnaguna, siawalaumu kwa hilo....., lakini hamjui ni maisha gani niliyopitia hadi kuingia  huko na kuwafanyia kazi hao watu watakavyo wao, sikupenda na sio fani yangu kutenda hivyo kwani kazi yangu ina miiko yake, lakini sikuwa na jinsi,...’watu wakacheka na wengine kusema `tamaa hizo...’

‘Kiukweli sikupenda kabisa lakini nilijikuta nipo ndani ya hili kundi na sikuwa na uwezo wa kutoka tena kwani walishanitega, swa myasema ni tamaa, lakini hiyo ni siri ya mtungi aijuaye ni kata, niwaambie ukweli ukijiunga na hilo kundi iwe kwa hiari au lazima, hutakiwi kutoka tena...na kuondoka hapo labda wakuue, au ujiue mwenyewe, kama alivyojiua mke wa...wa....inspecta Moto...’akasema.

‘Kiukweli maisha yangu yalikuwa magumu, kwani nilianza kazi ya udocta nikiwa nalipwa mshahara mdogo tu, sikuwahi kupewa mashahara sitahiki yangu, maisha yangu yalianza kuwa ya shida kuanzia hapo, maana mshahara ulikuwa mdogo sana,ukiuliza unaambiwa subiri, subiri, wakati wengine wanalipwa vizuri tu,...

‘Nilisubiri wee, hakikueleweka,…ndio tatizo la nchi hii hakuna sehemu ya usawa,…madawa vyakula sijui nini kuna TBS, je kazini kuna namna gani ya kuwapima watu kuwa kweli wanatendewa haki, eti niambieni, hata hivi vyama vya wafanyakazi, kweli wanaingilia hayo, hakuna kitu kama hicho, ni kuumizana tu, ndio maana kunatokea wajanja wajanja wanaharibu hizi fani, na watalaamu kama sisi tunajikuta kutaka kukimbia nchi…wao wanathamani waongeaji....’akatulia na watu wakacheka.

‘Kiujumla, mshahara haukuweza kukidhi mahitaji yangu, ndipo nikaanza kubuni njia mbadala ili niweze kumudu gharama za maisha, kama wakubwa wanakula ten percents, mimi nitakula nini,niumie tu, nife na tai shingoni,…na kwa haraka nikagundua kuwa kumbe ninaweza kuanzisha biashara ya madawa, …’akatulia kwani watu walikuwa wakicheka.

‘Sio hilo tu, pia nikagundua kuwa kumbe utaalamu wangu  unalipa, hata kama sio kwa njia ya mshahara, ...mimi ni docta wa upasuaji kwa akina mama, kipindi hicho nilikuwa nimeajiriwa kwa fani hiyo ya matatizo ya uzazi na mambo kama hayo kwa akina mama hata kwa akina baba, nikajiuliza na kupata jibu kuwa kumbe naweza  kuutumia ujuzi huo kwa namna nyingine...

‘Nikabuni kazi kutokana na ujuzi wangu huo, kazi ambayo niliona zinafaa, japokuwa hazikubaliki, lakini zinalipa....’akasema na kutulia watu wakacheka, ilikuwa kazi kwa hakimu kupiga kirungu mara kwa mara kwani hata yeye ilifikia muda akawa anacheka.

‘Kazi gani hizo ambazo uliona zinafaa na zinalipa?’ akaulizwa

‘Kama zakutoa mimba,...’akasema na watu wakacheka, na wakati wanacheka akawa anaongea kwa haraka

‘Unajua kuna watu hawataki ujauzito kwasababu zao binafsi, na wanatafuta watu kama mimi, lakini hayo hayaruhisiwi, nikaona niifanye hiyo kazi kwa siri, na..kiukweli kama ningelikuwa na tamaa  ya kuwalipisha hao akina dada, ...au akina mama walionijia kwa siri, ningekuwa na pesa nyingi sana, lakini nilikuwa na udhaifu mwingine, nikawa nawalipisha pesa kutokana na walivyo, mrembo, sio lazima pesa....’akasema na watu wengine wakacheka

‘Haikupita muda nikagundulikana nikafukuzwa kazi..balaa ….shida matatizo mikosi…ikaniandama..’akasema na kutulia.

`Muheshimiwa hakimu, naeleza haya sio kwa kufurahisha watu, ni ili muelewe kwanini  nilishinikiwa hadi kuingia huko…,

‘ Nilipokuwa mitaani kwa vile kuna watu wananifahamu, wakawa wananifuata, wanataka huduma za bei chee,wengine  wataka madawa, ..nilikuwa nayo kidogo, na pia wengine wanataka nifanye hiyo kazi ya kutoa mimba..nikaona kwanini nilale njaa, nikaanzisha zahanati bubu....

‘Kiukweli maisha kama huna ajira, ikizingatia kuwa mimi nilisomea masomo hayo ya udakitari, sina utaalamu sana wa biashara,..kuongea sana...nilipata taabu sana,  kuna muda niliona huenda ndio mwisho wa maisha yangu, nilianza kuishi maisha ya dhiki, ndio nikaamua kutumia ujuzi wangu huo niliusomea huko mitaani, unaona sikufanya kwa kupenda, ila hali ikanilazimsiha nifanye hivyo...’akatulia

‘Ukumbuke wazazi wangu walinsomesha kwa shida, wanauza ng’ombe, wanauza hiki na kile ili mtoto wao nisome, sasa sina kazi, wataishije, mimi mwenyewe nahitajika nipate pesa ya kula, kodi ya nyumba, na pesa za kunifanya nionekane docta….unajua, kuna hadi yake..sasa naumbuka…’akasema akibadili sauti.

‘Nikaanzisha Zahanati bubu, isiyosajiliwa,…wewe kuna watu wa njaa kali, wakanigundua, kiukweli  haikudumu,..polisi wakapata taaarifa wakawa wananisakama...hasa kwa kosa hilo la kuta mimba...kuna wazazi walinishitaki, na pia hao hao niliowatoa mimba, wengine wakawa wanalalamika, maana sikuwa na vifaa hasa, ni vile vya kubabaisha tu, nikawa nimewatoa hizo mimba kimakosa, unajue tena pesa ndogo, halafu....basi I ikafikia muda nikafanya makosa ya kibindamu...’akasema watu wakaguna

‘Taarifa zikafika polisi, nikaanza kusakwa, na hospitali bubu, haikuwa na makao maalumu, mara leo hapa kesho kule, nikawa naishi maisha ya kibongo, bora liende,mjini hapa...lakini hata hivyo, sikuweza kumudu maisha , kodi inahitajika, nahitajika kula, kunnua madawa, vifaa..nikajikuta sina pesa kabisa...sasa hebu fikiria, docta, aliyekuwa kahitimu, sasa hana kazi, na anatafutwa na polisi angelifanya nini,  ndipo nilikutana na huyu mtu anayeitwa Diamu...’akasema

‘Huyu Diamu ndio nani’ akaulizwa

‘Ndiye huyo aliyekuwa mumiliki wa hoteli ya Paradise...’akasema

‘Una maana gani kusema aliyekuwa…?’ akaulizwa

‘Kipindi yupo hai, ndiye aliyekuwa mumiliki mkuu…’akasema

‘Kwahiyo sasa hayupo , ameshakufa, si ndio maana yake?’ akaulizwa

‘Mtu akifa hafufuki bwana, alishakufa….ila mambo yake yamekuwa yapo, nitakuja kuyaelezea huko mbele…’akasema.

‘Lakini mama yake alidai kuwa bado yupo hai…’akaambiwa

‘Hahaha, mama yake, huyo alishachanganywa na madawa….nitakuja kuwalezea kwanini alikuwa hivyo, yote hayo ni kazi a madawa yangu,…mnipe nafasi, nitawasimulia yote, maana sina cha kupoteza kwa sasa nimeamua kutubu dhambi zangu zote, na haki itendeke…’akasema.

'Katika fani ya udakitari, kwenye kundi ulikuwa wewe peke yako ...?' akaulizwa

'Yupo mtaalamu mwingine kichwa kama mimi, yeye alichukua fani nyingine tofauti, tukiwa wawili mwili wa mwanadamu, ni kitu kidogo kwetu,...lakini masikini ameshakufa....'akasema

'Alikufa kufaje....?' akaulizwa.

'Mhh, inasikitisha ndio maana hata mimi nikaona nikimbie...wanadai kazi yake imeshakwisha, na kuendelea kuwepo kwake ni hatari kwa kundi,...nitakuja kuelezea baadaye,kama hamtojali...'akasema

‘Kipindi mnakutana na huyo Diami, alikuwa keshajenga hiyo hoteli?’ akaulizwa

‘Ndio ilishajengwa lakini vitega uchumi vingine vilikuja kuongezwa baadaye, na wawekezaji mbali mbali waliokuja kuijiunga  baadaye...kila muda kumekuwa kukiongezeka, hiyo hoteli imekuja kuongezeka baadaye kwa wawekezaji wapya walioiunga.....’akasema

‘Unaweza kututajia baadhi ya wawekezaji wa hiyo hoteli?’ akaulizwa na mawakili wa utetezi, wakalipinga hilo kuwa halina msingi na kinachoongelewa hapo, lakini hakimu akasema hilo swali lijibiwe.

‘Baadhi yao ndio hao mliowakamata, lakini pia wapo waheshimiwa  mbali mbali, kama mkiangalia kwenye orodha ya wawekezaji  wa hiyo hoteli mtawaona, sina haja y akuwataja hapa,...’akasema.

‘Docta hebu tuambie, mlipokutana na Diamu, kwa mara ya kwanza alikuambia vipi?’

‘Kama nilivyosema, kipindi hicho nilikuwa sina kazi, na nilikuwa na kashifa nyingi tu , kama za kuuza madawa ya hospitalini, nilishaanzisha mtindo wa kutoa  mimba kwa akina mama waliotaka kufanyiwa hivyo, na nimesahau kitu, kwani hicho ni muhimu sana mkielewe, siku moja nilikutana na ....’akageuka kuangalia, kwenye wale watu waliokuwa wameingizwa na vigari vya kukokotwa na mkono, kulikuwa na mwanamama, ambaye kwa muda huo alikuwa akimuangalia kwa macho yaliyojaa hasira.

‘Yah , yule peale, siku moja, alikuja huyu mdada, kipindi hicho alikuwa mdada kweli, akataka nimtoe mimba, kama kawaida yangu wadada warembo kama hao, sikuhitajia  malipo, ..nikamuuliza una pesa, akasema anayo kidogo, nikamwambia hiyo haitoshi…akasema hana nimsaidie tu, atakuja kunilipa baadaye, mimi nikamwangalia …mm, tamaa…’watu wakacheka.

‘Nikamwambia sina haja ya pesa yake, yeye mwenyewe analipa, ….alikataa ombi langu, nikamwambia wewe unakuja dukani bila pesa, unahitajia vifaa kweli hiyo ipo, nilipoona hanielewi nikatumia ujanja wangu wa kumpotezea fahamu, nikafaya kilichofanika, lakini kwa pupa, na…kiukweli nikamharibu…’akasema, na watu wakaguna

‘Ndio maisha yangu ya awali yalivyokuwa hivyo…’akasema

‘Unasema ulimharibu huyo mdada kwa vipi?’ akaulizwa

‘Nilimkosea kumtoa hiyo mimba, ..nikamtoa kihasara, ….alikuja baadaye kwenda sehemu nyingine wakagundua kuwa kizazi kimeharibika, wakamsafisha, …nasikitika sana….’akasema kwa saui ya uchungu.

 ‘Dada huyo akaenda kunishitakia, na kwa vile alikuwa na watu anaowafahamu huko polisi, basi nikaanza kutafutwa kama jambazi,..nikakimbia mji, nikaenda kijijini, na huko nikaoana maisha hayanifai nikarudi tena, nikakuta hali ni ile ile..nikawa nalala majalalani,..hebu chukua picha, kutoka udocta hadi uchokoraa,..na siku moja ikanitokea ngekewa....’akasema na watu wakacheka.

‘Ndio nikakutana na huyo bwana Di-amu...’akasema

‘Nilipokutana naye akanitambua,…tulisoma naye , lakini sio darasa moja, kwahiyo sikuwa nimemtambua sana kabla, ila yeye alinitambua kwa vile shuleni nilikuwa kichwa, ..aliponiona kwa ile hali, muda huo nakwenda kuomba omba, nimefua shati langu, haya maisha jamani, …’akatulia kidogo kama anazuia kulia, uchunu na simanzi.

‘Basi  akanichukua na kuniambia atanisaidia na hata kunilinda, kumbe maisha yangu yote ya nyuma anayafahamu, akasema atanisaidia, nisiwe na wasiwasi, na cha kwanza kunisaidia ni kunisomesha, ...’akatulia

‘Anisomeshe nini tena, wakati mimi nilishahitimu, iliyobakia ilikuwa kufanya kazi,…yeye akasena atanipeleka nje ya nchi, ..hebu fikiria wewe kichwani,  kunisomesha huko sio hapa nchini, atanipeleka nje...hiyo jamani sio ngekewa, …akawa kama anauliza

‘Na akazidi kuniambia kama nitakubaliana naye umasikini  kwangu bye bye,  na zaidi atanlinda kutokana na matatizo yanayonikabili..kwa hali niliyokuwa nayo, ambayo nilikuwa natafutwa na polisi, kwa kashifa hozi mbalimbali, sina kazi, njaa, kuadhirika nk, yote hayo atayasawazisha, mungu akupe nini,.....nikaona hapo ndipo pa kutokea, nikakubali…na kweli nikaenda kusoma nje

‘Kwahiyo mpaka wakati unandoka, bado  ulikuwa ukitafutwa na polisi kwa kosa gani ?’ akaulizwa

‘Ndio bado nilikuwa natafutwa na polisi kwa kosa lile lile la kuwaharibu watu vizazi,...mdada, alinikalia puani, aliahidi kuwa ni lazima nikafungwe, na muda hupo alishafikisha shitaka hilo kwa mkuu wa kituo,  aliyekuwa mkuu wa kituo hicho kidogo , alikuwa sio mchezo,  .....’akasema

‘Diamu, mlikutana naye, akakuambia yupo tayari kukusomesha, na kukulinda  na matatizo yako hayo,  ukakubali, ulikuwa na uhakika gani kuwa ataweza kukulinda na polisi...?’ akaulizwa.

‘Alinithibitishia hilo, ..alikwenda kituoni nilipofunguliwa hayo mashitaka, na akapata barua ya kuniidhinisha niende nikasome, na kesi yangu itafutwa kama nitafuata masharti nitakayoambiwa, ikiwemo hilo la kusoma, kutulia kubadilika, na kuwa chini ya huyo mdhamini hadi…kieleweke.....’akasema

‘Masharti hayo aliyayatoa nani?’ akaulizwa

‘Ni  huyo mdhamini wangu, na pamoja na hayo masharti aliambatisha, hicho kibali cha polisi kuwa ninaweza kwenda kusoma chini ya udhamini wa huyo Diamu, ...’akasema

‘Barua hiyo aliitoa nani?’ akaulizwa

‘Barua hiyo aliitoa mkuu wa hicho kituo…’akasema

‘Alikuwa nani..?’ akaulizwa

‘Oooh, jamani msinitake mabaya….’akasema

‘Hapa upo mahakamani, .usiwe na wasiwasi….’akaambiwa

‘Ndio maana niliwaambia, nataka uhakika....huyu mtu ananiandama kweli, utafikiri...sijui nilimuelezea yote, lakini hataki kunisaidia, na matokeo yake ananitishia maisha,...ni huuyo mkuu wako wa kazi,  kwa kipindi hicho alikuwa bado hajafikia kiwango cha cheo aliacho nacho sasa, alikuwa mkuu wa kituo kidogo, cha maeneo ya pale kwetu, pale niliposhitakiwa na huyo mdada, niliyemtoa mimba nikamharibu kizazi....’akasema

‘Unasema ulipewa masharti, ni huyo mkuu aliyekuapa hayo masharti au ni huyo mdhamini wako..?’ akaulizwa

'Mkuu, alitoa kibali ...na maelezo machache kuwa huyo nimtii kwa vile ndoye mdhamini wangu, masharti aliyetoa ni huyo mdhamini, inaonekana walikuwa wakiivana..sijui...maana naona kama ananisakama badala ya kunisaidia,..'akasema.

'Anayekusakama ni nani hasa?' akaulizwa.

'Huyo mkuu wenu, kesi , na matatizo yote nilishamwambia, nilitegemea yeye achukue hatua, lakini....'akatulia.

'Hebu tuambie kuhusu hayo masharti, yalisemaje?' akaulizwa

‘Kwanza nikubali kuwa huyo atakuwa mdhamini wangu, na kwa vile ni mdhamini wangu, atawajibika kwangu, na kwahiyo nimtii kwa lolote lile, ......hiyo ilikuwa barua ya polisi, kulikuwa na mkataba mwingine ambao ulianinisha masharti yote anayotaka huyo bwana Diamu...’akasema.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, tutauwakilisha huo mkataba kama ushahidi...’akasema muendesha mashitaka.

‘Haya tuendelee, ulikubali hayo masharti ukaenda kusoma Ulaya, ulikwenda kusomea nini huko...? akaulizwa.

‘Mimi nina kipaji cha udakitari, udakitari ni fani iliyopo kwenye damu, nilipofika huko Ulaya nilisomea fani hiyo ya uzazi, nikahitimu, nikaomba nisomee mambo ya ubongo na mishipa ya fahamu, nikahitimu vizuri tu, yaani nikwa na hamsa na kusoma fani tofauti tofauti, hadi wazungu wenyewe waliniona kuwa mimi sio mtu wa kawaida, ukumbuke kwenye huo mkataba kuna msharti, kuwa nikifika huko kuna mambo muhimu mengine  natakiwa kuyasomea, zaidi ya hayo niliyokwenda kuyasomea ..’

‘Kwanza sikujua kwa jinsi gani nitaweza kuyasomea hayo masomo mengine, kwani kwenye ule mkataba yalikuwa hayakutajwa kuwa ni masomo gani, au utaalamu gani..., lakini nilipofika huko nikakuta kila kitu kipo tayari, kwahiyo pamoja na masomo hayo ya udakitari bingwa wa magonjwa, lakini pia nikawa nasomea masomo hayo mengine ambayo hayakutajwa moja kwa moja ni magonjwa gani......’akakatiza.

‘Ni masomo gani hayo ya ziada uliyoambiwa uyasomee..?’ akaulizwa na hakimu

NB: Huyu docta ana mambo mengi sana, na kwenye kundi alikuwa ni mtu muhimu sana, ndio maana tunachukua nafasi kubwa kusikia maelezo yake, yupo pia shahidi mwingine,…mtaalamu wa mitandao, yupo mama uzuri na urembo,….

'Kwenye hitimisho hili tutajaribu kuwasikia hawa watu walioweza kuunda hii dunia yangu, japo kwa kualazimishwa,, kesi ipo mahakamani na Diami, anapima ubavu wake na sheria, tuone haki itavyoweza kutendeka …swali je huyu kiongozi wao alikwenda wapi, alikufa, na kama alikufa alikufakufaje, …na kama alikufa ilikuwaje `dunia yangu’ iendelee kuwepo.

WAZO LA LEO: Tuweni makini sana na hizi hospitali za mitaani, japokuwa hali za kiuchumi ni ngumu, na kila mtu anatafuta unafuu, kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa, na hapo hapo unaumwa, huna pesa, utajiuliza sasa ufanye nini, unaweza kukimbilia hizi hospitali za mitaani zisizosajiliwa kama zipo, kumbe wenzako nao wanatafuta njia za kubana matumizi, wakakuuzia madawa yasiyostahiki, au kuuziwa dawa zitakazo kuumiza baadaye, unaweza ukapona kwa muda, lakini utakuja kuumia zaidi, rahisi ni gharama.

Ni mimi: emu-three

No comments :