Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, October 29, 2014

DUNIA YANGU-54



Msaidizi wa mkuu, akiwa ndiye kiongozi wa kikao kingine maalumu kilichoitishwa kwa haraka, alionekana kuchoka, na kuwa na wasiwasi, ndani ya kikao hicho alikuwepo muendesha mashitaka, Moto na msaidizi mwingine, ...na mwanzoni ilijulikana kuwa ni kikao cha kupeana majukumu kuhusu kesi iliyopo mbele yao, lakini ikaja hoja nyingine kinyume na matarajio.

'Nimetumwa tena na mkuu, kuwa kesi iahirishwe kwanza, kwani mkuu anaona maandilizi ya kesi hii ambayo ni kubwa sana, haijakamilika ‘itakiwavyo’, na pia yeye mkuu ana mambo mengi ambayo keshayagundua kuwa yanahitajika kufuatiliwa kwanza...

‘Kesi iendelee, ..nyie mliniteua mimi kama msimamizi wa hiyo kesi, ...kama hamtaki basi mniondoe mumuweke mtu mwingine, mimi nina uhakika na kazi niliyoifanya, na kila kitu nimeshakiweka wazi kwa muendesha mashitaka, sasa kwanini tuahirishe hii kesi....’akasema Moto

‘Mkuu ana maana yake kuwa, kesi  hii inaingilia mambo mengi, na inawagusa watu mashuhuri  na wawekezaji muhimu, huoni kwa namna moja tunaweza kuleta sintofahamu katika nchi, kisiasa na kiuchumi na hata tunaweza kukosa misaada kama wenye nchi wanapotoka hao wawekezaji watapelekewa taarifa mbaya dhidi yetu...’akasema msaidizi.

‘Kila nchi ina sheria zake, na sheria hizo zinatambulikana kimataifa, hatuwezi kuwapendelea wawekezaji hata kama wamekiuka sheria, walipokuja kuomba uwekezaji, waliambiwa wafuate sheria, sasa iweje wazivunje, cha muhimu ni sheria ifuatwe, na  mahakama ndiyo yenye nafasi nzuri ya kuamua hilo...’akasema Moto.

‘Hujanielewa, hilo linaeleweka vyema, lakini tunatakiwa tuwe na tahadhari, na tahadhari hiyo ndio anayotaka kuichukua mkuu, kuongea na wakubwa kwanza, ili tuone jinsi gani ya kufanya, ili kukwepa lawama baadaye,  hata kama ...itabidi tunaweza kutumia njia nyingine,kesi hii isiwepo kabisa, wahusika wakarudishwa kwao...’akasema msaidizi

‘Mimi sioni kama kuna tatizo hapo, mahakama ndicho chombo kizuri cha kuliangalia hilo, kama ni muwekezaji, kama ni mtu mashuhuri mhakama italiangalia hilo na haki itatendeka....’akasema muendesha mashitaka

‘Mkuu kasema hataidhinisha hiyo taarifa ya kuwa kesi iendelee, kwahiyo tusubiri kibali chake , na mimi kama msaidizi wake, siwezi kukiuka amri yake, siwezi kuidhinisha hili kuwa kesi ifanyike...’akasema msaidizi.

‘Kwa hatua iliyofikia, hatuna haja ya kusubiria kibali chako mkuu,….tumeshafanikisha kila kitu, kwa vile kuna kibali tayari cha kunipa mimi mamlaka ya kusimamia hii kesi, mimi sioni kama kuna haja ya nyie kusaini chochote, sisi tunakwenda mahakamani....’akasema Moto na kumuangalia muendesha mashitaka

‘Ni kweli hilo halihitaji kibali chenu tena, maana mlishaidhinisha mapema kuwa Moto aendelee na kesi hiyo ipo mikononi mwake, na kibali hicho ninacho, kesho tunaanza kesi....’akasema muendesha mashitaka

‘Kwahiyo kesi hiyo mumejiamulia wenyewe,haihitaji baraza za sisi wakubwa zenu ...’akasema msaidizi

‘Mlishanipa Baraka hizo mapema, unakumbuka siku ile, tena kimaandishi,  mkuu, kwani kuna nini cha kutilia mshaka hapo, msiwe na wasiwasi kila kitu kitakwenda vyema mkuu, ...kama kuna tatizo jingine tuambieni...’akasema na kumuangalia muendesha mashitaka

‘Tatizo jingine ni kwa hao mashahidi je wataweza kutoa ushahidi wao kwa hiyo hali waliyo nayo?’ akauliza huyo msaidizi

‘Tutapata taarifa kutoka kwa muuguzi, sizani kama watashindwa kutoa  ushahidi ..hali zao sio mbaya kihivyo….’akasema Moto

‘Una uhakika na hilo,...?’ akauliza mkuu huyo

‘Kwanini unatia uwalakini, wapo hospitali, kama ingelikuwa haiwezekani tungelishapata taarifa, tukitoka hapa tutapitia na muendesha mashitaka, kukamlisha baadhi ya taratibu...’akasema Moto

‘Bora upige simu huko hospitali, uthibitishe hilo, ni moja ya vitu alivyokuwa akiniuliza mkuu, hasa kuhusu mashahidi, ….mambo ya kisiasa, uchumi,….mambo mengi tu, ana wasiwasi kuwa hao mashahidi wataitwa mahakamani washindwe kujielekeza na hapo itakuwa aibu kwetu...’akasema

‘Mkuu anaumwa, hawezi kujua afya za hao watu, hil ni jukumu letu, na wewe ndiye mwenye mamlaka kwa sasa, je wewe unahisi halitawezekana hili, wakati sisi watendaji wako tumeshakuthibitishia....’akasema Moto

‘Piga simu huko hospitalini, uhakikishe, ni muhimu sana, kama wapo tayari nitamuondoa wasi asi mkuu, ....’akasema na moto akapiga simu hospitalini

‘Je wale wagonjwa, tuliowaleta hapo wanaendeleaje?’ akauliza na kusikiliza kwa muda, halafu akasema

‘Mbona hamkuniambia mumekaa kimia na mnajua hao ni watu muhimu mahakamani kesho..’akasema moto na kusikiliza kwa makini, baadaye akasema kwa mshangao

‘Ina maana, Msaidizi wa mkuu anajua, mlishamuambia, haiwezekani kwanini...’akasema na kumgeukia msaidizi wa mkuu, halafu akakata simu

‘Mkuu kumbe uliambiwa kuhusu hali ya hao watu kuwa bado hawajagundua tatizo ni nini, na bado wana hali mbaya, lakini hukunipa hiyo taarifa..’akalalamika

‘Ndio maana nikataka uthibitishe wewe mwenyewe,…, hii ilikuwa ni kazi yako kuhakikisha hayo, unaona jinsi gani unavyopeleka mambo yako,…. Na ndio maana nilipoongea na mkuu wetu, akasema kwa hali hiyo inaidi tuahirishe kesi....’akasema

‘Kesi haitaahirishwa mkuu, kwasababu ya watu hao,...kuna mashahidi wengine watasimama kabla yao na wao ni muhimu vile vile...’akasema Moto

‘Akina nani hao wengine, wakati mahakama inawasubiria mshahidi hawa ambao tulishaona ni muhimu kwenye hi kesi...?’ akauliza huyo mkuu na kumuangalia moto inspecta Moto akachukua simu yake na kupiga namba, akasikiliza kwa makini halafu akauliza

‘Kila kitu kipo sahihi, umehakikisha,..sawa, tutakutana mahakamani kesho...’akasema na kugeuka kumuangalia muendesha mashitaka, halafu akageuka kumuangalia mkuu.

‘Tuna mashahidi watatu wengine muhimu, mmojawapo ndio huyo niliyekuwa nikiongea naye yupo tayari, na wawili wengine, tukitoka hapa tutawapitia na muendesha mashitaka, ila ,..kuna mambo nayafuatilia kwanza, nahitajia kupata kibali kwa mshahidi wengine maana ni watu wakubwa...’akasema

‘Kibali kutoka kwa nani, na ni watu gani hao wakubwa..?’ akauliza

‘Tutakutana jioni,...ngoja nifuatilie hicho kibali,...’akasema Moto, na kutoka akiwaacha msaidizi wa mkuu na muendesha mashitaka

‘Unamuelewa huyu mtu kibali anatakiwa akipate kutoka kwangu, ananikiuka mimi , kama mkuu wake wa kazi anakwenda kutafuta kibali wapi, huyu mtu hatufai, anakiuka sheria za kijeshi...’akasema na kusimama kwa hasira

Muendesha mashitaka akawa kautulia kimiya, halafu akasema;

‘Vita imeanza mkuu, na ukiona kiongozi wa vita anarudi nyuma,b asi huyo hafai kuwa kiongozi, na hatuwezi kusimamisha vita wakati tumeshafika uwanja wa mapambano, ina maana tumeshindwa, ...’akasema muendesha mashitaka

‘Vita haiwezi kuendeshwa, kiholela, kuna wakuu wa vita , na wakuu ndio sisi, kama tumeona muda wa vita bado ni lazima mtuskilize,mimi kama mkuu wenu, ni lazima mtii amri yangu kwahiyo  kesi hiyo haitafanyika kesho, mimi mwenyewe nitaongea na hakimu aiahirishe....’akasema muendesha mashitaka

‘Haiwezekani mkuu,maana kila kitu tumeshakiwakilisha kwa hakimu na  tumemthibitishia kuwa kesi ipo, na kibali cha kuiendesha, mlichomkabidhi moto kipo,kimeshawakilishwa kwa hakimu,  sioni kwanini tumsumbue hakimu kwa swala hilo tena, wakati keshawasiliana na sisi na keshawaeka ratiba ya hiyo kesi kesho na imeshatanganzwa, mimi nakushauri, acha kesi iendelee kama kuna wasiwasi mwingine, niambieni, mimi nitajua jinsi ya kuusawazisha kinamna ndani ya mahakama, maana hiyo ndio kazi yangu...’akasema

‘Mkuu kasema nisije kufanya makosa kuipeleka hii kesi mahamani, kwani kuna mambo mengi yanahitajika kufuatiliwa kwa  undani,, unafikiri mimi nitakwenda kumuambia nini, sikiliza fanya ufanyalo hii kesi isifanyike kesho,  ...’akaambiwa

‘Haiwezekani mkuu, nashangaa hata jana nimepokea ujumbe wa vitisho, sijui ni wahuni gani, hata hivyo hawanibabaishi..!’ akauliza muendesha mashitaka

‘Ujumbe gani huo…hata mkuu katumiwa ujumbe kama huo, wa vitisho, ndio maana anasema kuna mambo ya kuangalia kwa makini…hivi kwanini mnataka kukimbilia  mahakamani wakti mnaona kuna mambo muhimu hatujakamlisha?’ akauliza

‘Mhh,tutaonana mahakamani, mimi sibabaishwi na vitu kama hivyo...kesi ipo pale pale, na kibali kikipatikana, tutaweza kuwasimaisha mashahidi wengine wakubwa.....’akasema

‘Kwani kibali kitolewe juu , kwanini manakiuka sheria za utendaji, hata wewe mtu unayejua sheria unalikubali hili, huyu Moto, inabidi awajibike kijesh na hili nitahakikisha linafanyika....’akasema mkuu huyu akismama kwa hasira.

‘Wakati mwingine inabidi ifanyike hivyo, …tutaonana  mahakamani….’akasema muendesha mashitaka akiweka makabrasha yake kwenye mkobwa wake.

*************

Siku hiyo usiku kukawa na heka heaka za hapa na pale, mashahidi wapya waliotafutwa wakawa wanahojiwa na muendesha mashitaka ili kuona utaratibu mzima unakamilika, akawa sasa anahojiwa mtu ambaye anaishi karibu na eneo la makaburini, ambapo kunahisiwa kuwa huenda ilikuwa ni makao maalumu ya magaidi

 ‘Wewe umeishi maeneo  hayo kwa muda gani…?’ wakaulizwa

‘Zaidi ya miaka kumu, nipo hapo, nilikuwa na kibanda changu hapo, badaye nikapauza, lakini bado nikawa naendelea kuishi hapo nikiwa na biashara yangu ya genge…’akasema

‘Kwahiyo nyumba iliyolipuliwa unaifahamu sana, na mwenye nyumba hiyo?’ akauliza

‘Nawafahamu sana, mwenye nyumba hiyo ni mume wa marehemu, huyu mama anayeitwa Kikagula, hapo ndipo walipoanzia maisha yao awali kabla hajawahamia huko mjini….’akasema

‘Kwahiyo hii nyumba ni ya muwekezaji wa hoteli ya  Paradise?’ akaulizwa

‘Nasikia alipofariki mjengaji wa hiyo nyumba,…yaani mume wa Kigagula, waliamua kupauza,..na mnunuzi  aliyekuja kupanunua, akapotea kiajabu, ikaja kanunuliwa na mtu mwingine ikawa hali hiyo hiyo , kukaanza tetesii kuwa nyumba hiyo ina majini…’akasema

‘Kwanini?’ akaulizwa

‘Kwanza kila anayenunua eneo hilo hufa , au hupotea kimiujiza, na waliowahi kupanga humo wanasema kuna vitu vinatembea usiku, kuna kama karakana, watu wanagonga gonga vyuma, kama wanajenga, sauti hiyo inasikika hewani, au ..chini hakueleweki na watu wanaongea, na kuna muda watu wanapiga ukelele kama wanateswa….lakini kukipambazuka, kunakuwa kimiya…’akasema

‘Kwahiyo unahisi kulikuwa na nyumba ya chini kwa chini?’ akaulizwa

‘Hapana,..wengi wanadai sio chini, ni kwenye paa la nyumba, …sizani kama kulikuwa na kitu kama hicho, eti kuna nyumba ardhini, hapana..tungelijua, sisi tulioishi hapo miaka mingi, nyumba hiyo naifahamu sana….’akasema

‘Lakini bomu lilitokea ardhini, …’akasema na shahidi akawa hana zaidi hata alipohojiwa kuhusu mabomu na akaitwa shahidi mwingine.

Mwingine nay eye  alikuwa jirani na yeye maelezo yake yalikuw a hayo hayo…ila huyu alipoulizwa mtu ambaye anaonekana kuishi hapa anamfahamu akasema;

‘Huyu mtu ni mvuvi, ambaye aliamua kuishi hapa tu kwa vila anajiamini, nahisi hata yeye ni mchawi, kwahiyo akikutana na wachawi wenzake kunakuwa hakuna tatizo…’akasema

‘Kwanini unasema ni mchawi?’ akaulizwa

‘Hajulikani, haongei na watu,..jirani gani huyo, na kuonekana kwake ni mara chache sana, akija anaingia ndani , lakini humuoni muda wa kutoka..na mara nyingi hapendi kuonekana usoni, huwa kavalia mawani, au kavaa sweta lenye kofia, ya kuficha sehemu kubwa ya kichwa..ni mtu wa ajabu sana….’akasema

‘Je wakati mabomu yanalipuka huko makaburini mlikuwepo maeneo hayo, ...?’ wakaulizwa

‘Mimi nilikuwa ndio nimerudi kutoka sokoni, nilikwenda kuchukua bidhaa zangu Buguruni, nikawa nimerudi na gunia la viazi, wakati naweka hilo gunia la viazi chini , ili nianze kuvichambua viazi, kitu kikalia, tuuuh….ooh, ardhi yote ikatetemeka, mimi haraka nikalala chini, niliposimama, sikuangalia kushoto au kulia, nikalala mbele..sijui kilichotokea huku nyuma…’akasema

‘Usiku wake, kabla, au jana yake,  hakuna chochote mlichosikia, mlichoona …?’ akaulizwa

‘Tulisikia..hata mimi niliona, kuna mtu aliuwawa, na kulikuwa na taratibu za kumzika, lakini wahusika hawakukubali mazishi yafanyike, wakadai mtu wao afanyiwe uchunguzi…kwahiyo kulikuwa na watu wageni, askari, na taratibu kama hizo,….ila nilisikia mlango wa hiyo nyumba, ukifunguliwa mara kwa mara kuashiria kuwa huyo jamaa alikuwepo….’akasema

‘Jamaa yupi?’ akaulizwa

‘Si huyo mwanga….’akasema

‘Lakini hukumuona?’ akaulizwa

‘Tunaogopa hata kumuona siku hizi, maana nasikia ukimwangalia sana, unapotea kimiujiza….’akasema

‘Kuna watu yamewatokea hayo?’ akauliza

‘Wapo, ndio kwani siri..na inasadakiwa na kwasababu ya huyo mwanga…anaogopeka kweli kweli…’akasema

‘Hamna mtu anayeweza kumjua vyema sura yake..hebu angalieni hizi picha hapa…’wakaonyeshwa picha mbali mbali, lakini hakuna aliyeweza kuzitambua kuwa zinafanana na huyo mtu.

‘Huyu arehemu anayemiliki hoteli ya Paradise, alikufakufaje?’ akaulizwa mtu anayeifahamu hiyo familia

‘Kwanza alipotea , akawa anatafutwa sana, baadaye ukaonekana mwili wake, akiwa amekufa, wakaja kumzika hapo makaburini , mimi mwenyewe nilishuhudia mazishi yake…’akasema

‘Sasa kwanini mama yake alidai kuwa hajafa?’ akaulizwa

‘Ni kuchanganyikiwa tu, kwani mtoto wake alikuwa huyo huyo, na alikuwa anampenda sana, kwahiyo kufa kwake, akawa kachanganyikiwa, na watu wanahisi ni kutokana na mambo yao ya kishirikina yaliwageuka…’akasema

‘Walikuwa na mambo hayo?’ akaulizwa

‘Aaah, sana, unafikiri, hebu angalia utajiri walioupata, wameupata pata vipi, kwanza ni wanga, halafu mtoto huyo alikuwa jambazi,….simsemi vibaya maiti, lakini mtu gani haonekani, mchana kalala , usiku tu ndio anatoka, anakwenda wapi……mimi ni mtu wao wa karibu, lakini nikuambie ukweli, tangu alipofariki baba yao, na huyo mtoto akapewa umiliki, ikawa ndio mwisho wa kumuona huyo jamaa, ..unamsikia usiku tu akiongea na watu wake….’akasema

‘Kwahiyo hata sura  yake huijui , sura ya ukubwani….?’akaulizwa

‘Mhh, Sura nikimuona naweza kuikumbuka, sina uhakika sana..lakini mmh, unajua ni siku nyingi, ni kipindi hicho alikuwa bado kijana kijana….unafahamu, vijana siku hizi wanabadilika haraka sana, na hata hivyo kiukweli, ukikua na sura zinabadilika, ..ili huyu jamaa toka ujanani, alipendelea sana kuvaa mawani nasikia hadi usiku..sijui alikuwa akificha nini sura yake au ni matatizo ya macho,….’akasema

Walihojiwa watu wengi, lakini hakuna aliyweza kuikumbuka sura ya marehemu au picha yake, na wote walidai kuwa huyo mumiliki akufa kweli, ila mwili wake hakuna aliewahi kuuona..

‘Sasa tufanyeje…?’ akauliza muendesha mashitaka akimgeukia Inspecta Moto

‘Nasubiri kibali …mimi nina uhakika, hao waheshimiwa  wanahusika, na wao watakuwa wanajua mengi, na hata kuhusika, wakisimama kizimbani , niachie mimi….’kasema Moto.

‘Moto….unanichekesha kweli, unataka urudie kazi yako ya uwakili, wewe sasa ni askari kazi hiyo niachie mimi, lakini ujue ni hatari kubwa, kama wataoenekana hawana hatia ujue na wewe kazi huna…..’akasema mwendesha mashitaka.

‘Najua,….lakini ni lazima iwe hivyo, ngoja tupate hicho kibali…’akasema na simu ya Moto ikalia, na alipoangalia, akaona ni ujumbe, unamuhitaji kwenda makao yao makuu…..

NB: HIYO NI KATIKA HARAKATI ZA KUWEKANA SAWA, SASA TUNAINGIA  MAHAKAMANI, NA ITAKUWA MWANZO WA HITIMISHO TUWE PAMOJA

WAZO ZA LEO:  Kila kazi ina utaratibu wake, na  ndio maana kuna nyanja mbali mbali za kusomea hizo kazi, ni ajabu kuona mtu anajifanya yeye  anafahamu kila kazi, iwe ni ofisi au mitaani, na matokea yake kazi nyingine, zinaendeshwa kiholela, na  kiutaratibu usio sahihi, na matokeo yake ni kushuka thamani ya ile kazi,…kwanini tusiwape nafasi wanastahiki, kwanini tuhodhi madaraka tu kwa ubinafsi wa masilahi na huku tunalalamika kuna upungu wa ajira wakati mtu mmoja kashikilia ajira ya watu watatu,…utendaji mbovu….tuliangalie hili kwa masilahi ya wote..



Ni mimi: emu-three

No comments :