Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, October 28, 2014

DUNIA YANGU-53‘Kuna maombi kuwa kesi iahirishwe kwa vile mashahidi wote hawajulikani wapi walipo, lakini pia wengi wa watu wetu ukiwemo wewe ni majerehi, je wewe unasemaje?’ akaulizwa Inspecta Moto na msaidizi wa mkuu wake, walipokutana ofisini kwa kikao maalumu.

‘Mkitaka ushauri wangu,na ndivyo nionanvyo mimi, kesi iendelee kama kawaida, mashahidi wapo na watapatikana zaidi, kwa hivi sasa siwezi kuwataja wengine, ila ni muhimu mashahidi wetu wa awali wapatikane, hilo nalifanyia kazi siku ya leo nina uhakika watapatikana tu, ilimradi wapo hai....’akasema Moto.

‘Mkuu mwenyewe katoa hiyo taarifa kuwa kwa vile anaumwa ni vyema kesi hii iahisrishwe, hataki kuwaingiza watu kwenye hatari zaidi, anahisi tunajionyesha zaidi kwa maadui badala ya kufanya kazi kama askari kanzu, ...’akasema msaidizi wake.

‘Kesi hii ina mitihani mingi, tukiamua kuiahirisha kama watakavyo wapinzani wetu, tutakuwa tumefanya kosa kubwa, na mimi sitakubaliana na hilo,…hawa wenzetu kila mwanya kwako ni hazina, na  kwa jinsi walivyojipanga nia yao hii kesi hii ichukue muda mrefu, ili wahusika halisi wapotee, na jinsi tunavyocehelewa kundi hili haramu linakuwa kubwa na baya zaidi, kwa uoni wangu, mimi nataka kesi kesi hii iendelee, na ni vyema kila hatua ijulikane kisheria, mahakamani...’akasema Moto

‘Hii kesi ipo mikononi mwako, ulishapewa wewe jukumu la kuisimamia na ukahidi mbele ya mkuu kuwa utaimaliza kwa haki na kwa sheria, na kwa hiyo  ujue kama itakwenda kombo utawajibika wewe...’akasema msaididzi wa mkuu

‘Kama ipo mikononi mwangu , basi mimi nasema hivi kesi iendelee kama kawaida, mimi nitaongoea na muendesha mshitaka, msiwe na wasiwasi na kuwajibika kwangu, nina imani hii ndio njia muafaka ya kuwashinda hawa watu, vita iwe mahakamani, mbele ya sheria....’akasema Moto.

Kikao hicho kikaisha, na Inspecta Moto akandoka kuonana na muendesha mashitaka, na wakati anaondoka, simu yake ikaingia ujumbe; akaona ujumbe huo hauna namba, na maneno yaliyoandikwa kwa herufi kubwa yakasomeka;

‘UNAKUMBUKA UCHAFU WAKO....? huu hapa...’ kulikuwa na kibahasha cha kuashiria kuna picha au video fupi...
Inspecta hakuifungua ile bahasha, akaufuta ule ujumbe, mara ujumbe mwingine ukaingia ukisema;

‘ KAMA UTAENDELEA NA HII KESI, TUTAKUCHAFUA, UTAADHIRIKA KUTOKANA NA UCHAFU WAKO, SASA HIVI TUTAANZA KUTUMA  KWA WATU WAKO MUHIMU, FUNGUA  HAPA  UONE BAADHI YA UCHAFU WAKO..’kukawa na kialama cha kifurushi, kuonyesha kuna video ya kucheza

Inspecta hakutaka  kuendelea kuusoma huo ujumbe akaufuta, na kutoka kuendelea na shughuli zake, na ujumbe mwingine ukaingia, ukisema;

‘Hata kama hutaucheza huo ujumbe na kuona klichopo kesho angalia gazeti la udaku utaona uchafu wako,kama onyo, na mengine mabaya yatafuata, tutahakikisha maisha yako yanakuwa hayana amani...’hakujali, akatoka hadi kwa muendesha mashitaka,

Alipofika alimkuta muheshimiwa huyo akiongea na simu, na alisubiri mpaka akamaliza, ndipo akaingia na kukaa kwenye sofa, hakukaa kwenye meza ya mongezi, na muheshimiwa huyo akaonyesha uso wa mshangao, na bila kusema jingine, akauliza;

‘Unasema kesho tuendelee na kesi yatu kama kawaida, hao mashahidi wapo wapi?’ akauliza muheshimiwa huyo

‘Nina shahidi mmoja ambaye nahisi tukimsimamisha, yeye atakuwa kawakilisha mashahidi wote....’akasema

‘Ni nani,.... docta Cheza....?’akauliza muendesha mashitaka

‘Kwani huyo docta yupo?’ akauliza Moto akifunua macho ya mshangao.

‘Kamtibia mkuu wako wa kazi , nimepewa taarifa na watu wangu, nikaona ajabu, ina maana watu wako wanafanya kazi gani,?’ akauliza muendesha mashitaka kwa sauti ya ukali kidogo.

‘Hilo hata mimi nimelisikia hapa karibuni, hii ni kuonyesha kuwa kumbe hao watu wapo, na wamefichwa mahali...inanipa shida sana kuliweka hilo akilini, kwani nakumbuka kwa macho yangu mwenyewe aniliona watu wamelala hawajitambui pale kwenye lile jengo kabla ya mlipuko na nilijua ndio wao...’akasema Moto.

‘Uliwaona sura zao...?’ akaulizwa

‘Hapana, ila mavazi yao, ...’akasema

‘Kwa vipi, mavazi yao yanawezaje kukutambulisha hao watu?’ akaulizwa

‘Siku ile ya tukio, nilifika maeneo ya makaburini, na niliwaona hao watu wakifika na magari yao, na mavazi yao, ambayo ndiyo yaliyonitambulisha kuwa wale waliokuwa wamelala pale sakafuni walikuwa ndio hao mashahidi....’akasema

‘Kwahiyo kuna mchez ulichezwa hapo, viini macho....’akasema muendesha mashikata

‘Naona..na karibu wanipate, ...nilishaamini kuwa hao watu wamekufa kwenye hilo jengo, na nia yao ni kutaka nitambue hivyo...’akasema Moto, na muendesha mashitaka akatoa simu yake na kupiga namba

‘Ngoja niongee na mtu kwenye hospitalia anapotibiwa mkuu wako, nihakikishe kitu....’akasema

Muendesha mashitaka akapiga simu kwenye  huko hospitali , na kuuliza maendeleao ya mkuu wa  Inspecta Moto,  akaambiwa hajambo kiasi, akauliza ni nani aliyemshughulikia akaambiwa ni Docta wa hiyo hospitali.

‘Docta gani, hana jina?’ akauliza na simu ikakatika.
Muendesha mashitaka akamgeukia Inspecta Moto na kusema;

‘Kwanini huyu mtu kakata simu, ..?’ akauliza

‘Anataka kuuliza ajue ni kitu gani cha kusema, na ukimpigia tena atakuja na jibu jingine,....muhimu kuwatafuta hawa watu, kuna sehemu wamefichwa....’akasema Moto

‘Ina maana hawa watu wapo wanatuchezea akili yetu...?’ akauliza muendesha mashitaka kwa  hasira

‘Ndio maaana nataka kesi hiyo iendelee ili hakimu ajue kuwa hao watu wapo, ila kwa mbinu mbali mbali wamefichwa kinamna, mwanzoni tuliambiwa wametekwa nyara,sasa watasema nini..amri itolewe wakatafutwe wakamatwe....’akasema Moto

‘Sioni haja ya kusubiri amri ya mahakama, hili lifanyike haraka iwezekanavyo...’akasema muendesha mashitaka kwa hasira.

***********

Muendesha mashitaka akapiga simu polisi, na kutoa amri kuwa mashahdii wote watafutwe, kwani wapo na wakamatwe haraka iwezekanavyo, na haikupita ,muda, simu kutoka kwa mkuu ikapigwa kwa  muendesha mashitaka, ikisema, kuwa kesi iahirishwe.

‘Kwanini mkuu,...kutokana na mtu wenu anayesimamia uchunguzi anasema kila kitu kipo tayari, sasa kwanini tuendelee kusubiri....?’ akauliza muendesha mashitaka.

‘Lakini hajanifahamisha hivyo,...mimi nijuavyo, nikuwa mashahidi wote wanaohusika, hawapo, wamepotea, sasa iweje tena, kesi iendelee kuna mashahidi wengine?’ akauliza

‘Hao hao watapatikana, ..na hata wasipopatikana wao, bado ana mashahidi wengine wanaoweza kuendeleza kesi kuliko kuahirisha...’akasema muendesha mashitaka

‘Nimesikia pia kuna amri ya kukamata watu, hilo agizo limetoka kwa nani?’ akauliza mkuu huyo

‘Limetoka mahakamani...’akasema muendesha mashitaka

‘Hakimu gani aliyetoa agizo hilo, bila ya mimi kuhusushwa.....?’ akauliza

‘Hakimu anayeendesha hii kesi mkuu, na hata hivyo, tuliona tusikusumbue kutokana na hali yako ilivyo, mkuu...’akasema muendesha mashitaka.

‘Ni kweli, hali yangu ilikuwa mbaya, na hata sijaamini kuwa nipo hai, lakini bado wangeliweza kuja kuniambia muendelezo huo wa kesi, mimi sioni haja ya kukamata watu, na je mna uhakika kuwa hao watu wapo,..msiwasumbue familia zao, maana hizo familia hazina makosa...’akasema

‘Ina bidi tufanye hivyo, kwani  familia hizo zinaweza kufahamu wapi walipo hao ndugu zao, au hao watu kama wamejificha wakisikia familia zao zimeshikiliwa watajitokeza...’akasema muendesha mashitaka.

‘Hizo ni mbinu za kitoto...hilo mimi siliafiki, na huyu Inspecta Moto yupo wapi, nampigia simu hapokei?’ akauliza

‘Anashughulikia msako wa hao mashahidi mkuu...’akasema

‘Ok, nitawasiliana naye, ila agizo la kukamata familia za wahusika, lisitishwe, hatuwezi kutumia nguvu kwa kitu kama hicho, kuna mbinu nyingine za kuwapata hao watu bila kuisumbua jamiii, na kwaa jili hiyo tarehe ya kesi hiyo ibadilishe hadi hapo tutakapokamilisha ushahidi na mashahidi, sitaki kazi za aibu....’akasema na kukaat simu.

Muendesha mashitaka, akatulia kidogo, akataka kumpigia Inspecta Moto simu, na kabla hajafanya hivyo, simu yake ikaanza kuita, na aliyekuwa akipigia alikuwa Inspecta Moto,

‘Wakuu wako wanakutafuta...’akaanza kusema

‘Nitakwenda kuonana nao, nimeshapata huo ujumbe,...ila napenda kukufahamisha kuwa tumewakamata baadhi ya mshahidi wetu...’akasema

‘Mumewakamatia wapi wapo salama.... ?’ akauliza muendesha mashitaka kwa hamasa.

‘Hutaamini wapo hapa kwa docta Chize kama wagonjwa waliolazwa....’akasema Moto

‘Wagonjwa na docta Chize mwenyewe?’ akauliza

‘Docta Chize hayupo, ....na tunahisi anataka kukimbilia nchi za nje, lakini tuna watu wetu waaminifu uwanja wa ndege hawezi kupita, ......’akasema

‘Kazi nzuri, nina imani sasa kesi inaweza kuendelea......,’ akauliza

‘Ila kwa hali waliyo nayo, siwezi hata kuongea nao, ni kama mateja, wamepigwa masindan ya usingizi, nimewaamrisha madakitari wa hapo wahakikishe, hali hiyo inaondoka, la sivyo, hospitali hiyp inafungwa, na sasa hivi hospitali hiyo isimamishwe, lakini....wanaonekana kutokujali, sijui wana kiburi gani hawa watu....’akasema Moto.

‘Mkuu wako umemuona?’ akauliza

‘Bado yupo chumba cha wagonjwa wasiotakiwa kusumbuliwa, nahisi  hao watu wanajiamini kwa vile mkuu wangu anatibiwa hapo, lakini hilo sio tatizo sana , sheria ni sheria.....’akasema

‘Ngoja hilo nilifanyie kazi, nahisi kuna tatizo, kuna jambo limejificha hapo, natumai hata wewe ueliona, lakini kwanini tuandikie mate wakati wino upo,…..ngoja niongee na mkuu wako moja kwa moja, nisikie atasemaje’akasema

‘Mimi naona sio muda wa kuongea na mkuu wangu wa kazi, kwa vile anaumwa, watu wapo wa kufanya kazi yake, isitoshe,  walishanikabidhi mimi hii kazi…’akasema Moto

‘Kwahiyo…..?’ akauliza Muendesha mashitaka, akitaka kuongea zaidi, lakini moto akamkatisha kwa kusema

‘Kwanza ni muhimu sana, hawa watu kuwaondoa kwenye hii hospitali, na tuwapeleke kwenye hospitali nyingine,  tukiifungulishia mashitaka hii hospitali, kwa kosa hili…..’akasema

‘Kwa kosa gani?’ akauliza muendesha mashitaka

‘Waliwapokeaje hawa watu, najua watasema hao watu wameletwa kwao,. Kwa matibabu, na nani, nimejaribu kumuuliza msaidizi wa hii hospitali, yeye kasema hakuwepo, na mkuu wake wa kazi hayupo, hajui ni nini kilitokea..kuna kutupiana mpira, kwahiyo tukuchukue sheria, hospitali ishaitakiwe, na wawekezaji wake….’akasema Moto.

‘Hapo uwe makini..ngoja tuone tutawachukulia hatua gani, lakini kwanza tushughulikie hili la kesi yetu, tusichanganye mambo…’akasema muendesha mashitaka.

‘Hawa watu ni mashahidi muhimu wanahitajika kuwa tayari kuongea, kwa hivi sasa hawajiwezi, ni muhimu wachunguzwe vyema, tuone kama hawajapigwa madawa ya kulevya, kama imefanyika hivyo, tutazidi kuwa na ushahidi wa kuweza kuifunga  kabisa hii hospitali...’akasema Moto

‘Ok, hilo ni sawa, na…naona hapa kwenye makabrasha, hiyo hospitali inamilikiwa na Chize kwa hisa kubwa, lakini ina wawekezaji  wengine, ...mmojawapo ni huyu eeh, ina maaana hata huyu marehemu kawekeza hapa, huyu aliyekuwa mumiliki mkuu wa hoteli ya Paradise...mmh, naanza kuitamani hii kesi, nahisi kuna madudu humu ndani...’akasema muendesha mashitaka.

‘Unaonaeeeh,...kumbe ulikuwa hujapitia taarifa yangu yote, kuna mambo mengi sana yamejificha nyuma ya pazia, utakuja kuyaona mwenyewe kwenye hii kesi, na utakuja kugundua kuwa kuna waheshimiwa wengi wamewekeza kila kwenye hayo makampuni ya hawa watu tuliowashika,ndio maana hao watendaji wanajiamini, wanajua wana godfather  juu...’akasema Moto.

‘Unajua nilichukulia hii kesi juu juu, nikijua ni zile kesi zenu za hapa na pale, lakini sasa naanza kuiona jinsi gani kesi hii ilivyo, ni kesi ngumu,na itazidi kuwa ngumu kama kuna waheshimiwa ndani yake….sijui lakini nahisi siasa zitatusumbua sana kwenye hii kesi..ila nikuambie kitu, hapa hapendwi mtu, sheri ndio itaongea tu, mimi nipo pamoja na wewe, ...sasa kwanza nataka nimjue vyema huyu marehemu...asili yake, katokea wapi huyu mtu...’akatulia

‘Kwenye ripoti niliyokupa utamuona vyema, japokuwa hutaamini hakuna picha yake….kitu cha ajabu kabisa….’akasema Moto.

‘Na huyu mama yake, inaonekana alikuwa na nguvu fulani za utajiri, utawala eeh,..unajua bado najiuliza, kwanini huyu mama, masikini sasa na yeye ni marehemu, kwanini alidai kuwa, mtoto wake yupo hai,...nahisi kuna jambo ndani yake,.....nataka kila kitu kuhusu huyu mama, na je mtoto huyu alikuwa vipi na wazazi wake, hasa baba yake, nahisi kuna kitu kurithi hapa, huenda chimbuko zima la hii familia likatupa jibu , ....’akatulia halafu akasema

‘Pia nataka taarifa za hawa wawekezaji wote wa hiyo hoteli, na miradi yote ambayo, marehemu alikuwa na hisa nazao, pia nataka taarifa zote za hawa mashahidi nataka kujua hisa zao , makampuni yao....na..na...kila kitu chao, unaweza kunipatia hiyo taarifa, kabla ya kesi yenyewe.....?’ akauliza

‘Yote hayo utayapata.....’akasema Moto akionyesha hamasa

‘Utayapata kabla ya hiyo kesi..usijali muheshimiwa…’akamalizia kuongea maneno hayo wakati alishakata simu.

NB: Sasa naona tuingie kwenye hitimisho ndani ya mahakama, sijui wenzangu mnasemaje

WAZO LA LEO: Asili ya mtu, tabia ya mtu, inaweza ikawa sababu ya uadilifu  au ufisadi wa huyo mtu katika utendaji wake wa kazi, hasa akiwa madarakani na hili tuliangalie pale tunapochagua viongozi wetu, kiongozi ni lazima achunguzi , alipotokea, utoto wake, maendeleo yake shuleni, na maisha yake na wenzake shuleni, au katika jamii, hadi hapo anapokuja kwako kukuomba kura, Manen0 mazuri sio tija ...tija ni ukweli wa hayo maneno yanayotoka mdomoni mwa huyo mtu

No comments :