Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, October 17, 2014

DUNIA YANGU-50

 
 
 
 
 
 
 
Ni wakati magari sasa yanaanza kuondoka, na king’ora cha polisi kikaanza kulia ili masafara huo uweze kupita, mara simu ya Inspecta ikaita, alipoangalia mpigaji wa hiyo simu ni nani akaona hakukuwa na namba yoyote, hii iliashiria kuwa mpigaji hakutaka atambulikane, na mtu anayependa kupiga hivi kukiwa na hatari ni mmoja, Inspecta Maneno,..
 
 
 
Kwa mashaka akweka simu sikioni, huku akiwa kaweka kiwambo cha kunasia sauti, na kuiweka hewani

‘Ni nani mwenzangu?’ akauliza

‘Kwenye hilo gari la huyo mama kuna bomu…msimruhusu huyo mama aingie humo,..fanyeni juhudi..huyo mama akifa nitapambana na nyie, aaaah’ kukawa kimiya
 
'Hii sio sauti ya Inspecta Maneno, ni nani huyu...'akajiuliza
 
Inspecta Moto akaamrisha gari lao lisimame,akawa anataka kuwasiliana na mkuu wa msafara huo wa kuelekea huko makabaurini,  lakini hata kabla hajaipiga namba ya mkuu wa msafara huo, kukasikika mlio mkubwa mbele yao …..
 
Endelea na kisa chetu....

Mlipuko huo uliwashitua watu wengi, watu wakawa wanakimbia ovyo, kelele za vilio vya tunakufa tunakufa vilisikia kwa wingi, na hata magari yakaanza kugongana kwani madereva walishachanganyikiwa kila mmoja akiendesha kivyake na wengine hata walikuwa hawajui  wanaelekea wapi.....kwa hali ile ya ghasia na watu kukimbia huku na kule,kusababisha ajali nyingine za hapa na pale, ilichukua zaidi ya dakika kumi nzima hadi pale watu wa usalama walipoweza kuituliza ile hali na wao kuweza kufanya kazi yao vyema.

Baada ya hali ile kutulia watu majeruhi  na wengine walikuwa wamepoteza fahamu, ikawa kazi ya watu wahuduma ya kwanza kufanya kazi yao, na kundi moja la watu waliokuwa wakihudumiwa karibu na aliposimama Inspecta Moto likawa linaongea;

‘Mimi nilijua yale mabomu ya Gongolamboto yamehamia hapa....’mmoja akasikika akisema alipoambiwa hana tatizo na anaweza kuondoka.

‘Kwani wewe huoni, ndio hay ohayo mabomu, angalia lile gari lipo wapi, kumebakia vipande vipande utafikiri lile gari lilikuwa  limetengenezwa kwa vipande vya miti…jamani vita vibaya, kumbe wenzetu wa gongolamboto ilikuwa hivi...’akasema mwingine

‘Mbona hata sielewi ina maana  ooh....hapana sio lenyewe, kama ndio lenyewe, sizani kama kuna, kuna mtu kapona ….hivi imekuwaje, ndio yale mambo ya magaidi nini…hawa watu wamehamia huku kwetu..?’ akauliza mwingine.

‘Akipona mtu pale huyo sio mtu.....sijui walikuwa watu wangapi mle ndani, wote watakuwa maiti, na hata miili yao sizani kama inaweza kupatikana...’akasema mwingine na mara kukasikika sauti za vilio, kuashiria kuwa kuna msiba.

‘Huu sasa ni ugaidi, Osama kahamia huku tena, unakumbuka ile ya Ubalozi wa Marekani, naona ndio hao tena...’akasema mwingine.

‘Mhh, kila kitu Osama, magaidi si lazima Osama,….wanaweza wakawa wananchi wetu wenyewe weney tamaa zao za utajiri…’akasema mwingine

‘Sasa ni nani hao…..?’ akauliza mama mmoja akijaribu kusimama.

*******

Inspecta Moto ambaye alishuhudia yote hayo kwa macho yake mwenyewe, alikuwa akihangaika na mawasiliana na watu wake, na kwa muda huo huo, ndio akaweza kupokea simu yake, maana mawasiliano yalikatika ghafla, akawa anawasiliana na mtu wake aliyekuwa huko makaburini.

‘Mkuu, mawasiliano yalikatika ghafla, huku kumtokea tatizo, kuna mlipuko mkubwa umetokea eneo hili la makaburini…..’akaambiwa

‘What…?’ akauliza kwa mshangao kama haamini.

‘Ni pale pale alipozikwa yule mtu aliyeletwa kipindi kile kwa ajili ya uchunguzi…’huyo msemaji akaendelea kuongea akionyesha kuwa wasi wasi, na alikuwa kihema,kama vile alikuwa akikimbia

‘Huo mlipuko umetokeaje?’ akauliza Inspecta kwa mshangao, maana hapo alipokuwepo kulimuhitajia na huko sasa kuna jambo limetokea anahitajika pia awepo, hapo akamkumbuka rafiki yake Maneno, kwani angelikuwepo kazi hiyo angelifanyika kama atakavyo.

‘Wakati tumeamua kwenda kupachunguza pale mahali, kama ulivyotuagiza, kabla hatujakaribia hilo eneo ,  mara ghafla  mlipuko mkubwa ukatokea eneo hilo, na lile kaburi likazama kabisa, na moto mkali ukawa unatokea hapo kwa ndani, tuliwaita watu wa zima moto, na tunashukuru walifika haraka, na kikosi cha askari wa kazi hizo, sasa hivi wapo wanafanya kazi yao, wakichunguza chanzo cha hilo bomu, ndio hivyo  mkuu,...

‘Imetoka saa ngapi, na kwanini mawasiliano yakate ghafla, hawa watu wana uwezo gani wa kufanya hivyo...?’ akauliza naalipotajiwa saa, akagundua kuwa ni muda ule ule ambapo bomu la kwenye gari  ulipotokea, inaonekana ilipangwa itokee muda huo huo.

‘Mkuu ulipotokea mlipuko, kila mmoja alitafuta usawa wake wa usalama, hata mimi  kwa vile nilikuwa msitari wa mbele kuelekea pale makaburini, ilibiai nilale chini na nilipoona naweza kusimama, nikatafuta uelekeo salama, maana sikujua ni nini kitafuata baadaye, nilirudi sehemu hiyo nikaona moto usio wa kawaida kutoka ardhini kwenye eneo hilo ambalo lilikuwa na kaburi.

‘Cha ajabu ndio hicho,  nilipojaribu kukupigia  nikaona mawasiliano hakuna, hadi ikapita dakika kumi hivi, ndio mawasiliano yakaanza kupatikana...’akasema

‘Nilikuwa kwenye mihangaiko mingine, hata mimi nililiona hili, kwani nilikuwa najaribu kuwasiliana na makao makuu, lakini kukawa hakuna mawasiliano....’akasema Moto.

‘Mkuu ukifika hapa sasa hivi utakuta ni handaki la kwenda chini, na kwa vile moto haujatulia vyema, hatujaweza kugundua kuna nini ndani yake, bado wanahangaika kuweka mambo sawa, kwahiyo sikuweza kukuelezea vyema humo ndani kupoje, ila ni handaki,..bomu hilo limechimba hasa....’akasema huyo mtu wake

‘Oh, endeleeni kuangalia eneo lote hakikisheni hakuna mtu anayekimbia , angalieni eneo lote kuzunguka ukuta wa makaburini, nahisi kuna sehemu ambapo hao watu wapo, wapange vijana vyema, japokuwa kikosi cha mambo kama hayo wapo huko, lakini sis tunahitajika kwa ajili ya kuwasaka hao watu, wasiwazui kufanya akzi yenu, ngoja niwasiliane na makao makuu, tuone tutafanya nini,....’akasema

‘Sawa mkuu, na sasa hivi ndio nimesikia huko nako kumetokea mlipuko, mpo salama kweli mkuu, je kuna watu wamefariki?’ akauliza huyo askari

‘Ndio mlipuko huo umetokea sambamba na huo wa huko, kwa muda ulionitajia ndio muda ambao mlipuko kwenye gari ulitokea huku,...na hali ilivyo, hakuna uhai kwenye hilo gari, hata sisi huku tunasubiri  hali itulie, gari hilo limeungua kabisa, ni gari ambalo kumetokea huo mlipuko, .....’akasema na muda huo alikuwa akisogelea pale kwenye hilo gari akikagua kwa macho, lakini askari wa kazi hizo akawa anamzuia.

‘Oh, mkuu poleni sana, je muheshimiwa hakimu na watu wake wapo salama?’ akauliza huyo askari wake

‘Wapo salama, ...nyie endeleeni huko mniarifu kinachoendelea, maana siwezi kujigawa, na makao makuu naona hawapatikani, sijui kuna nini huko, simpati mkuu wala msaidizi wake…, toka jana imekuwa ni tatizo kumpata, sijui kapatwa na nini, sio kawaida yake....’akasema akijaribu kumpigia kwa simu nyingine.

‘Hata huku wanamtafuta hapatikani mkuu, huenda kapatwa na dharura, lakini nakumbuka aliondoka akiuguliwa na mzazi wake, kwani alirudi....?.’akauliza

‘Nyie endeleeni tu, nitaona jinsi ya kumpata, ila muwe  makini maana hatujui lengo lao ni nini, na ionavyoonekana wanataka kuhakikisha kuwa hakuna ushahdi wala mashahidi,...’akasema Moto,  huku akiendelea kukagua kwa macho kwenye lile gari, akatikisa kichwa  na kusema;

‘Sawa mkuu..’akasema huyo askari

Eneo sasa likazungukwa na maaskari kuhakikisha hakuna janga jingine, na magari yote yaliyokuwepo hapo yakachunguza kusije kukawa na bomu jingine, na kikosi cha uchunguzi wa mabomu kikawa kinaendelea kufanya uchunguzi wake, na kwa taarifa za haraka. walisema bomu hilo lilitegewa kwenye simu kinamna amabyo mtu huwezi kugundua, na wote waliokuwemo kwenye gari hilo ni marehemu hata miili yao haiwezi kutambulikana tena.

Taarifa hiyo ilimfanya Inspecta Moto ambaye kwa muda huo alikuwa njiani kuelekea huko makaburini, kuwaarifuu watu wa uchunguzi, ambao walikuwa wakichunguza simu walizopelekewa, wawe makini na hizo simu.

‘Mkuu tumehakikisha hakuna kitu kama hicho, hazina bomu kabisa ...’wakasema

‘Hao watu ni wataalamu wa hali ya juu, wanaweza kuweka bomu kwa njia ya mitandao, kinachotokea ni hali ya hewa na viundo-mbinu  vya miozi, vilivyopandikizwa humo, ambavyo husababisha mlipuko…huwezi kuviona, ni utaalamu wa aina yake…’akasema Moto

‘Mkuu tunaendelea kuchunguza, kama kuna kitu kama hicho, naona ha watu wanatumia ugaidi wa hali ya juu wa kupiga kwa kutumia setelaiti na mionzi ni hatari,lakini tunao wataalamu hapa wanaendelea kuhakikisha kuwa kitu kama hicho hakipo, na ishara ya mawasilioana  haionyeshi wapi mpiga au mtumaji wa yale mawasiliona yametokea wapi, kwa jinsi ilivyoweza kupatikana lakini sio kwa uhakika, ni kutokea baharini, muelekeo wa makaburi ya Msasani….

‘Baharini?’ akauliza kwa mshangao

‘Ndio mkuu, ndio tumeweza kugundua hivyo, lakini hakuna uhakika zaidi….’akasema

Inspecta akawa sasa amefika eneo la makaburini na kuanza uchunguzi wa kina, akawa yupo na kundi la maaskari wengine wakikagua lile handaki ambalo mwanzoni lilikuwa ni kaburi.

‘Mkuu hapa palikuwa sio kaburi, mnaona huku, hili ni handaki, kuna njia ya kuelekea nje ya huu ukuta, ila kwa vile kumebomoka, njia yote imezibwa, unaona huku ...’akasema mtu ambaye alikuwa chini pamoja na kikosi maalumu.

Ikabidi Inspecta na baadhi ya watu watoke nje ya ule ukuta kukagua huko kulikuwa na nyumba, na watu wamezunguka wakishangaa, kulikuwa na moshi unatokea kwenye hiyo nyumba, kuashiria kuwa kuna moto unawake ndani, na wakati huo akili yake ilikuwa ikifikiria kauli ya mtu wa uchunguzi kuwa mawasiliano yametokea baharini, akatupa jicho kuangalia lile boti, akaliona bado lipo na kuna askari wapo tayari kwa lolote.

‘Hii nyumba ni ya nani?’ akauliza Inspecta, na wakati huoa moshi ulikuwa ukizidi kuongezeaka kutoka kwenye hiyo nyumba

‘Ni  ya jamaa mmoja mvuvi, huwa muda mwingi hayupo, haonekani mara kwa mara humo, nyumba hii imekuwa kama imehamwa, ni mara chache sana unasikia kuwepo na mtu humo ndani, sasa tunashangaa kuona huo Moshi, na umeanza pale kuliposikika mlipuko wa huko makaburini, watu walikuwa wamekimbia, sasa hivi ndio wamerudi na ndio tukaona hivyo...’akasema jirani wa hiyo nyumba.

‘Huyu mvuvi mnafahamu...?’ akaulizwa

‘Tunamfahamu kwa kumuona , huwa haongei na watu, hufika na kuingia ndani, akiingia humo hatoki, na anavyotoka huwezi kujua katka muda gani, kwani unaweza kumuona akiingia lakini akitoka humuoni, huwezi kujua kaenda wapi, ...’akasema huyo jirani.

‘Anafananaje?’ akaulizwa

‘Mhh, ndugu yangu, mtu huyo muda wote kavaa mawani, na kofia pana, hata sura yake siwezi kumfahamu ipoje, na wakati mwingine akiwa katokea baharini huwa na na koti linalimfunika unaweza kuona kidogo usoni, ..labda ukawaulize wavuvi huenda wanaweza kumtambua...’akasema huyo jirani akionyesha kuwa na wasiwasi

‘Sasa umejuaje kuwa ni mvuvi?’ akaulizwa

‘Kwa vile akiingia humo huwa kabeba matenga ya samaki, au vifaa vya uvuvi ndio hivyo, lakini kuna kitu mimi kinanitia wasiwasi siku nyingi nimekuwa nikiwaambia wenzangu,..’akasema huyo jirani

‘Kitu gani hicho?’ akauliza

‘Huyu mtu hafanani kuwa mvuvi….kwa jinsi anavyoonekana japokuwa kavalia hayo mavazi, lakini wavuvi tunawafahamu hali zao,..huyu bwana hata….labda ndio hao wavuvi matajiri, jana nilimuona akiwa katika hiyo hali, kavalia koti,akionekana na wasiwasi, akaingia humo ndani hajawahi kutoka…’akasema huyo mtu

Inspecta aliposikia hivyo, akawa na hamasa ya kuonana na huyo mtu, hata hivyo, hali ya hiyo nyumba ilionekana kuwa hatarini, kulikuwa na kila dalili kuwa kuna moto ndani tena mkubwa,
'Tuvunje tuingie....'amari ikatolewa, na Moto akiwa na kikosi chake ikabidi wavunje hiyo nyumba, waingie ndani, kwani hali ilivyo ni tofauti na jinsi watu walivyodai kuwa ni vipande vya bomu vilivyodondokea humo ndio vinaleta moshi....

Mlango ulipovunjwa, tu, watu wakakaribishwa na mbaya, ilikuwa ni harufu ya gesi, na  ghfla mlipuko mkubwa ukasikika…….

WAZO LA LEO: Moyo wa mwanadamu ukishatawaliwa na dhuluma utu huondoka kabisa na kinachobakia ni chuki,  huruma inakuwa haipo tena, na hapo ni bora kukutana na mnyama hatari kuliko huyo mwanadamu.  Ndio maana ni vyema mara kwa mara tunahitajika kusaidiana kwa kukatazana mabaya, na kuelekezana mema. Kwani ubaya ukizidi, amani haipo tena. Tujaribu hasa viongozi kuwa waadilifu, tuhakikishe haki na ukweli vinakuwa ndio dira yetu.


Ni mimi: emu-three

No comments :