Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, October 15, 2014

DUNIA YANGU-48


‘Sasa wao ikawaje, hawakupata urithi wa utajiri wa mume wako, wakati ni watoto halali wa huyo mzee?’ akaulizwa.

‘Mhh, sasa wewe unanichimba, …kwanini wewe mwenyewe usiwaulize wao wenyewe, kuwa kwanini walikimbia, sijawakataza kuja kuchukua kile wanachoona ni chao, kama kweli ni chao, walikimbilia wenyewe kuelekea huko kijijini wakawahi mashamba, mbona huniulizei kwanini mimi sikuwafuta kuwanyang’anya hayo mashamba, kama wao walichukua huko, basi huku na wao hawana chao, unasikia vyema…

'Lakini hakuwahi kukaa na kukubaliana hilo, wewe uliamua mwenyewe kuchukua kule unapooana ni kunono au sio, ....

'Hahaha, waulize, nahisi wao wenyewe walisogopa kuja kushindana na mimi, hivi ni nani angeliweza kushindana na  Kigagula hahaha, hamnijui eeeh, ngojeni leo mtaniona, hahaha…’

‘Labda wewe uliwatisha, ukawaambia waondoke?’ akaulizwa.

‘Waliondoka wenyewe kwa uwaoga wao,sikuwahi kuwaambia waondoke usinipakazie uwongo, kama unabisha nenda kawaulize mwenyewe……’akasema

‘Sasa ni  kwanini walifanya hivyo,ni kwanini walikimbia, tunataka kujua kutoka kwako, tunataka ukweli kutoka kwako, waliogopa nini, je walikuogopa wewe.....

Tuendelee na kisa chetu

**********

 Wakati mahakama ikiendelea kikosi maalumu kilichotumwa kuchunguza kupotea kwa  hao watu ambao ni mshahidi muhimu wa kesi ya kundi haramu, kilikuwa kazini, na mara kwa mara kilikuwa kikiwasiliana na Inspecta Moto. Na kwa vile Inspecta Moto alikuwa mahakamani, ilibidi mara kwa mara awe anatoka nje, kila anapopigiwa simu, na safari hii akatoka nje tena kusikiliza simu,

‘Mnasema magari yamekuja kuchukuliwa na nani?’ akauliza.

‘Ni madereva wa hao watu, madereva hao wanasema walipokea ujumbe jana kuwa ikifika muda huo, wafike kuchukua hayo magari…’akaambiwa.

‘Ujumbe huo ulitumwa na nani?’ akauliza.

‘Na kwa hao wenye magari, lakini tumegundua jambo…’akasema.

‘Jambo gani sema haraka maana nataka nimsikilize huyu  mama akitoa ushahidi wake ni muhimu sana…’akasema.

‘Ujumbe huo unafanana, ina maana ni ujumbe ulioandikwa na mtu mmoja ukatumwa kwa hao madereva wote…’akasema.

‘Ya-ya-ya, …nilijua tu,..’akasema Inspecta., halafu akiwa na haraka akasema;

‘Kwahiyo mnasubiri kibali cha kuyaruhusu hayo magari?’akauliza

‘Ndio mkuu….’akasema

‘Hapana, hatuwezi kuyaruhusu mpaka tujue hatima ya hao watu, hao watu ni muhimu sana katika hii kesi, na pia tuna wasiwasi kuwa hao mashahidi wapo hatarini….’akasema

‘Lakini mkuu tumegundua jambo jingina, kuhusu huo ujumbe wa kuwa wapo hatarini, inaonekana ni ujanja wao, kwani ujumbe kama huo upo kwenye simu zilizoachwa kwenye magari ya kila muhusika…’akasema.

‘Kuna simu mumeziona kwenye magari  ya hao watu wengine?’ akauliza Moto kwa mshangao.

‘Ndio, kuna simu zimeachwa na tukaona tuangalia kama kuna kitu tutagundua kwenye hizo simu, na hapo tukaona huo ujumbe wa kualikwa kwenye kikao, na ujumbe wa kuonywa kuwa wasiende huko walipoalikwa maana ni mtego….’akasema.

‘Ok, …..naona wanajileta wenyewe, nimegundua jambo hapo…wanajiona ni wajanja sana…’akasema Moto, halafu akauliza swali;

‘Je mumechunguza sehemu zote, hakuna sehemu amabayo hao watu wameingia chini….shomo handaki, na kitu kama hicho?’ akaulizwa

‘Hakuna, mimi mwenyewe nimeingia kwenye kile kibanda, baada ya wao kuchukua ule mwili, wakati wametoka kwenda  kuuzika,..sikuona kitu kaam hicho, na cha ajabu waliokuwepo hapo, sio wale walioingia, sio wale mashahidi wa hiyo kesi, ni watu wengine kabisa,  na tulipowahoji, wanasema huo mwili ni wa mmoja wa ndugu aliyekuwepo hapo, na taarifa alishapeleka polisi…’akasema.

‘Kituo gani?’ akaulizwa.

‘Kituo kidogo cha kati, na nimefuatalia kuhakiki hilo nimeona ni kweli, taarifa zilifika hapo kituoni, na wakapewa kibali cha kumchukua ndugu yao huyo, na kumchunguza, kuna askari aliyekuwa nao kwa ajili ya uchunguzi huo, kuhakikisha kama hakuna tatizo…’akasema.

‘Uliongea na huyo askari?’ akaulizwa.

‘Ndio nimeongea naye na akanipa jinsi walivyopata taarifa ya kuokokotwa huyo mtu akiwa amekufa, na wao wakafanya uchunguzi hawakugundua jambo, na ndugu hao wakaomba wao wenyewe ili kujirizisha waufanyie uchunguzi huo mwili, na wamegundua ni kweli kuwa marehemu huyo  alikufa kifo cha kawaida…’akasema.

‘Ni docta gani alifanya huo huo uchunguzi?’ akaulizwa.

‘Ni docta, eeh, Che-, yes Cheza,….’akasema.

‘Huyo docta ulionana naye?’ akauliza.

‘Haonekani mkuu, hata familia yake wanamtafuta, hawajui kaenda wapi, wanasema kwa mara ya mwisho alisema anakwenda kufanya uchunguzi wa mwili, na atachelewa kwani ana kikao muhimu, na pia anatakiwa kesho yake kuwepo mahakamani…’akasema.

‘Je na ile boti bado lipo?’ akauliza Moto akiwa na haraka ya kuingia ndani kusikiliza ushahidi wa huyo mama.

‘Bado ipo mkuu,…walitaka kuondoka tukawazuia….’akasema.

‘Hakikisheni hilo boti haliondoki, na wale wazamizi wa majini wazunguke sehemu zote kuona kama kuna lolote chini ya maji eneo hilo…’akaambiwa.

‘Mkuu eneo hilo sio refu sana, sizani kama kuna kitu kinaweza kupitia chini kwa chini, hata hivyo tumechukua tahadhari zote mkuu…’akasema.

‘Ngoja kidogo….., je huo mwili wa huyo mtu waliyekuwa wakimchunguza mliuona, na sehemu alipozikiwa mliweza kufika?’ akaulizwa.

‘Sehemu alipozikiwa tumepaona, ila huo mwili hatukuwahi kuuona…’akasema

‘Haya kuweni makini, …hakikisha mnachunguza kila mahali kama mkiona dalili za kuwepo mahali hao watu nifahamisheni mara moja, kna watu wengine watakuja kuwapa nguvu mpya,….’akasema.

‘Sawa mkuu, ….’akaambiwa na yeye akaingia ndani kuendelea kusikiliza kesi.

*************

‘Ndio labda, walikuwa wakiniogopa mimi, lakini mimi sikuwatisha , sikuwaambia wasije, wangelikuja mimi ningeongea nao…’akasema kwa sauti ya kutamba.

‘Kwanini wakuogope wewe?’ akaulizwa.

‘Wao wanadai eti mimi ni mchawi, hahaha,….’akasema na kucheka kwa dharau

‘Wanadai au ni kweli...?’ akaulizwa.

'Ni kweli kuhusu nini?' akauliza kwa sauti ya kukasirika

'Kuwa wewe ni mchawi labda, huoni hata jina lenyewe linajieleza...'akasema huyo muendesha mashitaka kwa mzaha

‘Wewe unaamini hayo, hebu nipe kifungu kinachokubaliana na hayo, kisheria, wewe si mwanasheria, wapi mumesema kuna uchawi,...hakuna....'akasema akionyesha kutamba.

'Lakini je wewe unasemaje, wewe ni mchawi?' akaulizwa

'Nikuulize wewe je wewe unasemaje je mimi ni mchawi,..uchawi wanao wao wanaogopa, na kama unahisi mwenzako ni mchawi basi hata wewe ni mchawi,utajuaje uchawi kama hujawahi kuuonja..’akasema na watu wakacheka.

‘Hebu tuambie kuhusu mume wako, alifariki vipi?’ akaulizwa,na hapo akatulia kidogo bila kujibu neno, na alipoinua kichwa akawa anabubujikwa na machozi,hakusema neno kwa muda huo alitulia sana hadi hakimu akataka kuingilia, lakini ghafla yule mama akainua uso akawa kama anaangalia kitu hewani kwa mbele yake, na macho yakawa yanapanuka kama kuogopa jambo,

Yule muendesha mashitaka akamsogelea, na kumuangalia vyema usoni, alipoona huyo mama katulia vile vile akiwa anaangalia sehemu moja na huyo muendesha mashitaka akamshika yule mama begani na kuuliza;

‘Mama upo sawa kweli?’ akaulizwa.

‘Mume wangu, kaja, …..anataka na mimi nife, anataka na mimi nife na mtoto wangu, hapana….nimekosamume wangu nisamehe..nitasema yote mume wangu,nisamehe…..’akawa anajitahidi kuinuka kwenye kile kitu.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu,unaona kinachotokea, tulisema huyo mama kachanganyikiwa,waendesha  mashitaka, wakadai ni mzima hivi kweli huyo mama ni mzima…hamuona anaongea mambo ambayo hayapo?’ wakauliza upande wa utetezi.

Hakimu hakusema kitu akawa anamuangalia yule mama, na yule mama akawa anajaribu kama kurudi nyuma, akawa kama anaogopa jambo,na  akaanza kuongea kwa sauti ya aina yeka akisema;

‘Nitasema ukweli wote, nisamehe mume wangu, nitawaambia kila kitu,kuwa mimi na mtoto wangu tulishirikiana kukuua wewe, tukakuua kwa kisu cha urithi, ili kupata mali yote ya familia yako,na mtoto wangu sio damu yako, hatukuzaa na wewe, na hakusstahili kurith mali yenu…’akatulia akizidi kupanua macho ya uwoga.

‘Ni kweli kabisa, mali hiyo tuliipora sisi, na mwanangu ndio akawa kinara wa kuifisidi hiyo mali, akaanza kuiendeleza ndoto zake za kuanzisha dunia yake….ndio mumewangu, alianzisha dunia yake kwa kisu chenye damu yako…’akatulia.

‘Kisu hicho kimekuwa kikiua kila aliyemkaidi, hata hivyo,kwa akili zake za ziada, aligundua njia nyingine ya kujiwezesha kuwa na nguvu zaidi, aliwakusanya wataalamu wote wenye vipaji, akawawezesha na kwa kutumia utaalamu wake ndio akaweza kuitengeneza ndoto yake, ndoto yake ya kuwa na dunia yake…’akasema na sasa akawa analia kwa kwikwi

‘Nisamehe mume wangu usiniue…nitawapeleka huko alipo mwanangu..’akasema

‘Yupo huko,yupo nakupia yupo huko,….tukienda utamuona, hajafa kabisa,…hajafa….hajafa….’akasema mara nyingi neon hilo ‘hajafa…’ kwa sauti kubwa, na baadaye akatulia.

Muheshimiwa hakimu, akawa katulia akimuangalia huyo mama  kwa mshangao na mahakama ilikuwa kimiya, na baadaye akauliza;

‘Je kuna ushahidi gani kuwa hayo anayosema ni kweli, je ni kweli yeye na mtoto wake ndio waliomuua mume wa mama huyo, na je motto wake kweli yupo hai,..?’ akauliza

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, kauli yake ina ukweli, na ilikuthibitisha ukweli huo, ndio tukawahitaji mashahidi ambao walitumiwa na mtoto wa mama huyo,..mashahidi hao wangelithibitisha hilo, lakini kundi hilo likaligundua hilo, ndio maana wakawateka nyara wote na inawezekana wameshikiliwa hapo alipo mtoto wa huyu mama……’akasema.

‘Kwani mtoto wake yupo hai?’ akauliza muheshimiwa hakimu.

‘Kwa kauli ya huyu mama mtoto huyo mtoto yupo hai, na anasema tukienda huko makaburuni tutampata huyo mtoto wake…’akasema.

‘Makaburi ya wapi,ina maana huyo mtoto anaishi huko makaburini?’ akauliza hakimu

‘Kwa kauli ya mama huyo ndio,…tuliwatuma askari, wetu,lakini hakuna dalili ya kuonyesha kuwa kuna mtu anayeishi huko,lakini huyo mama kazidi kusisitiza kuwa mtoto wake yupo huko,na kinachotupa wasiwasi ni kuwa mama huyu anadai kuwa mume wako anamjia akitaka mtoto huyo akamatwe, na haki itendeke…

‘Ndio twendeni nikawaonyeshe wapi alipo,….ili na mimi nife kwa amani, …’akasema huyo mama.

‘Twende wapi mama,watu wamefika huko hakuna aliyeona wapi mtoto wako yupo, anawezaje kuishi huko makaburini….?’ akauliza.

‘Mnaogopa eeh, nilishawaambia sharti la mtu kufika hapo alipozikwa mmtoto wangu ni moja tu….lakini kwa sasa tuliache hilo, muhimu ni nyie mfike hukomkutane na huyo mnayemtafuta , na…na ..na tukichelewa, hatutamuona tena, na wote waliopo naye huenda ikawa ndio mwisho wao wa kuonekana hapa duniani…..twendeni haraka…..’akasema.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, tunahitaji kibali chako, mahakama hii ihamie huko makaburini ili tuone ukweli wa hili tukio…..’akasema muendesha mashitaka, lakini watetezi wa hiyo kesi, wakakataa hilo ombi, na kusema hayo ni mambo ya kishirikina, hakuna mtu anayeweza kuishi makaburini na huyo mama kacjhanganyikiwa hajui anachokiongea…

Hakimu akatulia kwa muda na baadaye akauliza;

‘Je askari waliokwenda huko wanasema nini?’ akauliza
Akafika Moto na kuteta na muendesha mashitaka, na waakti wanateta yula mama akasema kwa hasira;

‘Twendeni mbona mnachelewa,msije mkanifanya nife kifo kibaya,twendeni ili nife kwa amani, twendeni haraka….’akasema na kugeuka huku na kule akasema;

‘Askari wangu yupo wapi,nataka nitangulie mbele….’akasema na kuanza kusukuma gari lake mwenyewe.

Hakimu akaangalia saa yake, akageuka kuwaangalia wasaidizi wake.


WAZO LA LEO: Ushindi wenye ghiliba, hadaa na uzushi ni  batili, na hata kama wengi wataukubali kwa kuburuzwa, lakini kama kuna nia mbaya ndani yake, yenye masilahi binafsi, tujue kabisa muelekeo wa ushindi huo ni wa muda tu, na mwisho wake unaweza kuleta madhara, na madhara hayo yatawakuta wote hata hao waliopitisha ushandi huo, kwani kila mchumia janga hula na wakwao.

Ni mimi: emu-three

No comments :