‘Ndugu
muheshimiwa hakimu, kutokana na haya yaliyojItokeza tunaomba tuiwakilishe upya
kesi hii ya kifo cha mke wa Inspecta, kwani ushahidi uliowakilishwa sasa hivi
una uzito mkubwa, na tunaomba tupate muda wa kuupitia vizuri…’akasema mundesha
mashitaka.
‘Kwahiyo
sasa hivi mnamshitakia nani?’ akaulizwa.
‘Ndugu
muheshimiwa hakimu, tunashindwa kuliweka hilo wazi mpaka tuweze kupitia ushahidi wote, na kupitia kila
kitu kwa makini, ili kuchelea kurudia rudia tena hii kesi, tuna uhakika sasa
hivi tutaweza kuimaliza hii kesi bila kuwepo na manung’uniko…’akasema
muendesha mashitaka.
Upande
wa utetezi ukaanza kupinga hoja hiyo mpya, na kusema kwa vile kesi ya kwanza
imeshaisha, basi kama kuna kesi nyingine iwakilishwe kama kesi nyingine, lakini
swala la kuwa mke wa Inspecta alijiua limeshahkumiwa halina kesi tena ya kujibiwa.
‘Kesi
inaweza kurudiwa mara nyingi tu, ndio maana kuna kukata rufaa…’wakasema
waendesha mashitaka.
Hakimu
alisikiliza mabishano ya pande zote mbili bila kuingilia kwa muda, na baadaye
akasema;
‘Kwa
vile kesi hii ilishafungwa, waendesha mashitaka, wanatakiwa kuwakilisha kesi
hiyo nyingine mpya, na natumai sasa hivi hakutakuwa na utata, nataka muelewe kuwa
wananchi wanaifuatili akesi hii kwa makini sana, na kwa jinsi mnavyofanya hivi
mtasababisha wananchi wasiamini mahakaza zao….’akaongea hakimu kwa muda, na
baadaye akafunga kesi hiyo rasmi.
Wakati
Inspecta Moto anatoka, waandishi wa habari wananchi mbali mbali wakawa
wanamzonga kutaka kujua zaidi kutoka kwake, lakini hakuweza kuongea lolote, na
kuingia ndani ya gari alilokuja nalo likiwa na ulinzi wa hali ya juu.
Inspecta
Maneno alipotoka hapo alifululiza moja kwa moja hadi Paradise hoteli, kwani
alitakiwa kwenda huko kuendelea na uchunguzi kuhusiana na kundi hilo haramu,
alipofika alikwenda na kuingia kwenye ofisi moja maalumu.
******
Siku
ya kesi ikaanza kwa kishindo, kulikuwa zaidi ya washitakiwa watano pale mbele,
wote wakiwa wawekezaji katika hoteli ya Paradise, wakishitakiwa kujihusisha na
kundi haramu, na kuendeleza mauji ya raia wasiokuwa na hatia.
‘Kwa
pamoja wote wanashitakiwa kwa kesi za kuanzisha kundi haramu, kuendeleza
mauaji, na shughuli nyingine, kama za utapeli, unyang’anyi na kunyanyapa watu
kwa kutoa mapicha mabaya kwenye mitandao….’kesi ikasomwa.
Kama
ilivyotegemewa wote walikana mashitaka, na kwa vile ni watu mashuhuri wenye
nyadhifa zao, walikubaliwa dhamana,na ikapangwa siku ya kusikilizwa kesi.
Maneno
ambaye alikuwa akihaha huku na kule kutafuta ushahidi alikutana na Moto kwenye
ofisi maalumu makao makuu, na aliyeanza kuongea alikuwa Moto.
‘Kwanza
hebu sogea huku…..’akamshika mkono na kumvuta kwenye mashine maalumu ya
kumchunguza mtu kama ana chombo cha hatari cha kunasia sauti, lakini hakuweza
kugundulikana kuwa na chochote.
‘Kwanini
unafanya hivyo, …?’ akauliza kwa hasira.
‘Najua
….lakini anyway, hata wakisikia nataka kukupa ukweli wote ili ukae ukijua kuwa
wewe unajulikana kuwa ni miongoni mwa kundi hilo haramu…’akaambiwa na Moto.
‘Mimi
sikuelewi, hilo la kushutumiwa hivyo lipo na nimeongea na wakuu, nimewaambia
yote wanayotaka, ….’akasema.
‘Kama
ni hivyo kwanini na wewe hukuwepo kwenye kundi la washitakiwa…?’ akasema kwa
hasira.
‘Kwa
kosa gani nililolifanya hadi nishitakiwe kama unavyotaka wewe?’ akauliza
‘Wewe
hujui kuwa ulikuwa kibaraka wao, hebu niambie huo utajiri ulio nao umeupata
wapi kama sio mapesa yao machafu waliyokupa ili uwafanie kazi zao?’ akaulizwa
‘Kumbe
ni wivu wa utajiri wangu ndio unakusumbua, kama unataka sema nikuonyeshe njia
mimi sina hiana, sasa hivi utabadilika, sasa hivi utakuwa ni tajiri mkubwa,
tatizo lako huoni mbali, na hao kama hao, wana yao,na mimi nina yangu, utajiri
nilionao hautokani na wao kabisa…’akasema
‘Wewe
wataka unifundishe nini mimi, hiyo tabia chafu, au ni zile njia zako za
kujiunga na kundi, ili na mimi waniwezeshe au…?’ akaulizwa.
‘Hayo
ni ya kwako, na ukiendelea kunisakama kwa shutuma zisio na ushahidi
nitakuchukulia hatua …’akasema.
‘Ndio
nataka ufanye hivyo…’akasema Moto.
‘Wewe
umehangaika kutafuta kila mbinu za kuniharibia jina langu umeshindwa iliyobaki
ni kuongea ovyo, hilo halitakusaidia kitu, kumbuka tulipotoka, kumbuka
nilivyokusaidia hadi kesi dhidi yako ikafutwa ndio fadhila zako hizo?’ akauliza.
‘Hujanisaidia
lolote, ulichokitaka wewe ni kuharibu ushahidi tu, uonekana upo na kazi yako,
ili uweze kutoa taarifa kwa watu wako, nakufahamu sana, ila bado nataka nijue
ukweli, kuhusu mauaji ya mke wangu, wewe utakuwa ulihusika, hilo bado
nalifanyia kazi….’akasema.
‘Endelea
mimi sijakukataza, hiyo ni haki yako kutafuta ukweli na ukitaka msaada wangu
mimi nipo tayari…’akasema.
‘Unisaidie
au unichote mawazo yangu, ili ujue ni jambo gani ninalolifanya….’akaambiwa
‘Kama
hutaniamini mimi, ujue hutafanikiwa, hujui jinsi gani ninavyothamini urafiki
wetu…nilihangaika sana kukuteta, lakini najua hutaweza kuniamini mpaka hapo
utakapofikia mwisho wa upelelezi wako…’akasema
‘Hebu
niambie jana ulipotoka mahakamani ulikwenda wapi?’ akamuuliza
‘Nilikwenda
kufanya uchunguzi wangu kuhusu kundi hilo haramu linalodaiwa kuwepo…’akasema.
‘Wewe
ulipofika Paradise uliongea na nani?’ akaulizwa.
‘Na
watu mbali mbali….’akasema.
‘Habe
sikiliza maongezi yako na hao watu wako….’akaambiwa na Inspecta Moto akatoa
simu yake na kuweka hewani, na maongezi yake aliyoyafanya siku hiyo yakasikika;
***
‘Naona kesi ya kifo cha mke wa Inspecta
imefufuliwa upya na sasa hivi yaonekana wana ushahidi wa kutosha…’akasema
Maneno.
‘Tunafahamu
yote hayo, kwahiyo wewe unataka nini kwetu?’ akaulizwa.
‘Kama
mlivyoniahidi, nimekuja kwenu kwa kutaka msaada..’akasema.
‘Msaada
gani unaohitajia kutoka kwetu?’ akaulizwa.
‘Msaada
wa kipesa, maana inabidi kuongea na watu mbali mbali,ili kuweza kupata ushahidi
wa kutosha…’akasema.
‘Hilo
halina shida,…na wala haikuwa ni kazi yako, ukumbuke kuwa wewe umeshavunja
mkataba na sisi, ulitakiwa sasa hivi uwe kaburini, tumekustahi tu tuone jinsi
gani utakavyoosha mikono yako, na tumerizika na utendaji wako, tunaangalia
jinsi gani ya kukusaidia,na ikibidi kumalizana na wewe kabisa….’akaambiwa.
‘Kwahiyo
sasa hivi nifanye nini?’ akauliza kwa hamasa, lakini kichwani akawa anajiuliza
hawa watu wana maana gani kusema; `ikibidi kumalizana nay eye kabisa’.
‘Endelea
na shughuli zako kama kawaida, usibabaike, inapofikia sehemu ya hatari wewe
tuambie tutajua nini la kufanya, japokuwa tunakuona kwa kila unachokifanya...’akaambiwa.
‘Je
ushahidi huo mpya ulioletwa mahakamani mna taarifa nao, ?’ akauliza
‘Sisi
hatuoni kama una lolote jipya, kwa vyovyote iwavyo tumeshajiandaa, tunajua ni
nini cha kufanya, ujue kabisa kama itabidi, ….hasa tukiona unaweza kuingiza
kundi kwenye matatizo, hatuna budi kuagana na wewe,…’akaambiwa
‘Una
maana gani kusema hivyo?’ akauliza
‘Hilo
lipo wazi, ndio maana tulishakuambia uwe makini, na kosa dogo ullolifanya,
japokuwa tumeshalisahihisha, limeweza kuingiza kundi kwenye matatizo makubwa,
sisi kama wanachama tunahitajia kuliangalia hilo kwa macho mawili, na sheria
zetu zipo wazi, najua ulishazielewa vyema..au unataka tukusomee tena upya…’akaambiwa
‘Lakini
mkisema hivyo, mimi nina kosa gani, maana yote nilifanya kama kundi
lilivyotaka, au sio, sasa nitawajibikaje wakati hayo yaliyotokea ni maagizo ya
kundi, mimi nilikuwa ni msimamizi tu…’akajitetea.
‘Swali
ni je wewe ulifanya kama ilivyotakiwa ufanye, au ulifanya hivyo huku ukimlinda rafiki yako, ukilianda masilahi
yako, sisi sio watoto wadogo, sisi tuna akili yako mara mbili, tunakufahamu
vyema kabisa...’akaambiwa
‘Nilifanya
hivyo ili ionekane kuwa namlinda huyo anayeitwa rafiki yangu kumbe natafuta
njia ya kumnasa hivi nyie hamlioni hilo…’akasema
*********
Inspecta
Moto akazima simu yake na kumuangalia mwenzake usoni, akamuuliza
‘Hebu
niambie ni kwanini usikamatwe kwa kushirikiana na hilo kundi haramu, hebu niambie
ni kwanini nikuamini, kwanini usikamatwe kama muuaji wa mke wangu….?’
Akamuuliza kwa hasira.
‘Huo
sio ushahidi wa kunifunga mimi, na hata hivyo, huoni kuwa hizo ni mbinu zangu
za kupata ukweli, bila kufanya hivyo nitawapataje hao watu, hauoni kuwa sasa wote
waliokuwa wakishukiwa wamekamtwa, …..’akasema
‘Hao
waliokamatwa ni viini macho tu, wahusika wenyewe hawajakamatwa hata mmoja…’akaambiwa
‘Ni
akina nani hao wahusika, kama unawafahamu kwanini usiwataje wakakamatwa…?’
akauliza Maneno
‘Mmojawapo
ni wewe, na wengine wengi, ambao wamechukuliwa kutokana na taaluma zako….najua
jamaa zako wanakusikiliza, ila nataka wajue kuwa mimi nawafahamu wote,….waambie
hao mabwana zako…’akasema na Maneno akamuangalia rafiki yake kwa muda bila
kusema neno, halafu akasimama na kusema
‘Nimekumbuka
nina ahadi ya kuonana na mtu muhimu hoteli ya Paradise unaonaje tukaongozana,
nataka uhakikishe mwenyewe kuwa mimi sihusiki, nawajibika tu, ukaonane na huyo
mtu niliyekuwa nikiongea naye …’akasema
‘Janja
yako…’akasema Moto
‘Ndio
nafasi peke yake ya kuhakiki shutuma zako, twende au uje kinamna, ili
tuyamalize haya..’akasema
‘Wewe
endelea na shughuli zako, mimi sishirikiani na wewe, …’akasema Moto
‘Uwe
makini na hayo unayoyafanya…wewe ni rafiki yangu , kuna mbinu za kukumaliza
kabisa,..usije ukasema sikukuonya,…’akasema
‘Umejuaje
hayo kama huhusiki…?’ akamuuliza
‘Dunia
hii haina siri, kama ulivyojua ya kwangu ujue nafahamu mengi ya kwako….lakini
mwisho wa siku ni ujanja kupata…’akasema na kuinuka kuondoka.
Inspecta
Moto akachukua simu yake na kuandika ujumbe wa maneno.
WAZO LA LEO: Katika shughuli za
kikazi ni muhimu kuwa na malengo,na mipangilio mizuri ya pamoja yenye maafikiano kwa wahusika wote.Kusiwe
na malengo yenye ajenda binafsi kila mtu akiangalia masilahi yake, kwa kufanya
hivyo, itakuwa kama mpo katika ya bahari, mpo kwenye mtumbwi mmoja mnatakiwa mfike ng’ambo,
ikiwa mtapiga makasia kwa pamoja kwa mpingalio mmoja, safari yenu itakuwa
salama, lakini kama kila mtu atapiga makasia kivyake mjue mtumwbi utayumba, na
usalama wetu utakuwa hatarini.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment