Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, October 3, 2014

DUNIA YANGU-42


 Watu wanne, wakiwa watu wa usalama, walifika hoteli ya Paradise, ambapo waliambiwa kuna sehemu anaishi mama  wa mtoto ambaye anamiliki hoteli hiyo. Kuna tetesi kuwa huenda mmiliki wa hoteli ya Paradise, ana mafungamano na kundi haramu, linalosadikiwa kuwepo nchini, na huenda huyu mtoto alikuwa ndiye kinara wa kundi hilo haramu. Lakini kwa taarifa rasmi mtu huyu ni marehemu.

Walipofika eneo hilo ambalo ni eneo la hoteli ya Paradise, wakajieleza na kueleeka eneo la sehemu ambayo wameambiwa mama huyo anaishi, na walipofika hapo wakazuiwa na mlinzi aliyekuwa mlangoni akiwa na silaha. Alipoelezwa kusudio la watu hao kufika hapo, huyo mlinzi akasema;

‘Docta kasema huyu mama hastahili kusumbuliwa kutokana na hali yake….’akasema

‘Tuliomba kibali mapema, tukaambiwa tuje leo,  na hatuna nia ya kumsumbua, sisi ni watu wa usalama, …’akasema msemaje, na yule mlinzi akazidi kusisitiza kuwa amri iliyowekwa hapo na dakitari wa huyo mama ni kuwa asisumbuliwe mpaka mwenyewe awepo, au atoe kibali.

Maneno ambaye alikuwa kimiya, akasema;

‘Usiwe na wasiwasi hatapata usmbufu wowote, mwambie huyo aliyekuzuia kuwa mimi Maneno nipo….’akasema Maneno, na yule mlinzi akachukua simu yake na kupiga namba, na mara akamgeukia huyo Maneno na kumpa hiyo simu.

‘Ni Maneno, nimekuja kuongea na mama kuna mambo ya kiusalama tunahitajika kuyaweka sawa….’akasema na kusikiliza kwa muda, baadaye akasema.

‘Usitie shaka tupo pamoja, …’akamrejeshea yule mlinzi, na yule mlinzi akaipokea na kusikiliza, halafu akageuka na kwenda mlangoni, akabonyesha kitufe, na ukapita muda, mlango ukafunguliwa.

Walipoingia ndani, wakaelekezwa wapi waende na kukaa, na hapo wakaulizwa wanahitaji vinywaji gani, na kila mmoja akataja kinywaji chake wakaletewa na kuanza kunywa. Baadaye akaja mtu mmoja na kusema;

‘Mama anakuja, lakini tunaomba muwe wastahimili, msimuulize sana maswali ya kumchosha, na kawaida yake akitoa amri sisi tunahitajika kuitimiza…’akasema mtu mmoja aliyekuwa na jambia, au panga kiuononi na upande mwingine bastola.

‘Hamna shaka….’akasema Maneno, na kweli kukaonekana kigari cha kukokotwa na mikono…kilikuwa kikijiendesha chenyewe, japokuwa kulikuwa na mtu nyuma yake, akiwa kavalia kama yule mtu mwingine aliyewakaribisha, naye akiwa na jambia, kiuoni, na bastola upande mwingine.

Kwenye kile kigari, alikuwepo mama akiwa kakaa kwenye hicho kigari cha bei mbaya, na kikawa kinasogea karibu na pale walipokaa hao watu wa usalama wa polisi, na kwa heshima wakasimama.

‘Heshima yako mama…’wakasema.

‘Heshima zenu nyie watumwa wa watu wengine, niambieni mumefuata nini hapa, mnataka nini hapa, kama mnamtaka mwanangu yupo kaburini, nendeni mkafukue mtamuona, mzima kabisa…’akasema na wale maofisa wakawa wametulia na huyo mama akasema;

‘Mnasubiri nini, mumeshawapa hawa wau damu ya shetani?’ akauliza

‘Ndio mama…’akasema huyo aliyewapokea.

‘Sawa kabisa, haya anzeni kuongea…’akasema.

‘Mama tulikuja hapa kukuuliza kuhusu vitega uchumi vilivyokuwa vikimilikiwa na mtoto wako, nasikia ulisema hutaki mwanao aondolewe kwenye orodha ya wamiliki, na wakati hayupo hai, ni kwanini mama..?’ akaulizwa na mmoja wa maofisa.

‘Nani kawaambia kuwa mwanangu hayupo hai, mumemuua nyie….niambie ni nani kamuua mtoto wangu…?’ akauliza akiwaangalia maofisa hao akipepesa pepesa macho.

‘Mama kama ulivyosema mtoto wako yupo kaburini, kuna mtu anaweza kupelekwa kaburini kama hajafa?’ akaulizwa.

‘Sio wote waliopo makaburini wamekufa,..hivi hamuoni, kwani mimi hapo nipo wapi, si nipo kaburini , hamlioni hili kuwa ni kaburi, hebu angalieni tofauti ya hapa na huko nje,…au na nyumba nyingine,…. Lakini mnanionaje mimi sijafa, ..na yeye kapalekwa huko hajafa, tatizo ni lazima uwe vile uondokene na roho yako, wanaita kufa, hebu niambieni kama engalikufa na kila kitu kingelikufa au sio.

Mumeliona hilo jumba kuwa hapo nje, ni la nani, ni lake, mnaifahami miradi yake mingi, inaongozwa na nani, mbona inaendelea kama kawaida…kuweni na akili nyie….wajinga wakubwa nyie….’akasema na kukohoa mfulululizo.

‘Mama tunaweza kupata picha ya mtoto wako?’ akasema mmoja wa maofisa.

‘Sihitaji picha yake, mimi namfahamu mwanangu, kwanini niwe na picha yake,mwanangu yupo hapa moyoni,…kama mnataka pasueni hapa moyoni mwangu kama hamtamuona…’akasema akifunua kifuani kuonyesha.

‘Mama samahani sana kwa usumbufu, lakini nikuulize swali mtoto wako alizikwa sehemu gani, maana tumeuliza sana , hatujaweza kuonyesha kaburi la mtoto wako?’ akaulizwa

‘Mnataka niwapeleke ehe, huko anatakiwa maiti, kwanza mfe ndio niwapeleke, askari wangu upo….’akaita na yule mtu aliyekuwa akimuendesha kwenye kigari akaja na kusema;

‘Nimekuja mama..unasemaje?’ akauliza yule askari akija kusimama mbele yake.

‘Una jambia lako hapo tayari….?’ Akauliza na yule askari kwanza akatulia na kuwaangalia wale, akawaonyesha ishara ya kuondoka,, halafu akasema;

‘Ninalo mama…’akasema akishika mpini wa lile jambia lililopo kiuoni mwake.

‘Wewe ni mtu wangu na unanitii au sio?’ akauliza

‘Ndio mama, …’akasema huyo askari

‘Kila ninalokuambia fanya unafanya…au sio?’ akauliza

‘Ndio mama,…’akasema

‘Sasa nataka hawa watu wakazuru kaburi la mwanangu, na msharti ya huko siunayajua?’ akaulizwa

‘Ndio mama ninayajua…’akasema yule askari

‘Masharti yake ni nini?’ akaulizwa

‘Ni lazima mtu huyu awe ni marehemu, atengane na roho yake, awe na roho nyingine ya ya kuzimu…’akasema huyo askari.

‘Anaipataje hiyo roho ya kuzimu?’ akaulizwa

‘Ni kwa kufa kwanza…..’akasema yula askari akiwa kama anataka kulitoa lile jambia kiuoni

‘Sasa hawa watu wanataka kwenda huko kuzimu, wanataka kumtembelea mtoto wangu, eti mtoto wangu yupo wapi?’ akauliza.

‘Makaburini….’akasema.

‘Sasa, waulizeni hawa watu je wapo tayari kwenda huko, na wapo tayari kwa msharti yake…’akasema huyo mama.

Na yule mlinzi akawaangalia wale maofisa akipepesa macho yaliyojaa ujasiri, kuonyesha kuwa yupo tayari kwa lolote, na wale watu wa usalama japokuwa walijitahidi kuwa wakakamavu, lakini kwa ile hali, walishaanza kuonyesha wasiwasi.

‘Mumesikia jamani, ..mpo tayari…’akasema huyo askari, na wakati huo mkono wake umeshikilia mpini wajambia lililokuwa kiunoni.

‘Sikiliza mama …sisi ni watu wa usalama, hatukuja hapa kwa shari, na nia yetu ni njema kabisa, kama hutaweza kutusaidia  kwa hilo tunaondoka mama…’akasema

‘Aaah subirini, hatujamalizana na nyie bado, msije kusema mama ni mkorofi, …mlichotaka mtakipata, lakini masharti yake ndio hayo, toka alipofariki mwanangu nimekuwa nikiwauliza watu kama kuna mtu anataka kuliona kaburi la mwanangu, na wakisema sawa, nawapa hayo masharti, lakini wanaogopa..hivi kwanini mnaogopa kufa, wakati ni lazima kila mtu atakufa…’akasema

‘Mama tumemaliza tunaondoka…’akasema Maneno.

‘Na wewe sio Maneno wewe?’ akauliza aliposikia sauti ya mmoja wa maofisa, akageuza kichwa kumuangalia.

‘Ndio mimi mama…’akasema.

‘Umeamua kunisaliti au sio?’ akauliza

‘Hapana mama…’akasema Maneno

‘Ole wako,…..siku zako zinahesabika, karibuni utakwenda kulizuru kaburi la mwanangu, hakuna anayeweza kumsaliti bibi Kikagula abakie hai, mimi ndilo jina aliloniachia bibi yangu, Kikagula,nimerithi jina lake hahahaha…’akasema na kujipiga kifuani.

‘Haya kama hamna maswali mengine ondokeni na msirudi hapa tena…’akasema kwa sauti ya hasira, na wale maofisa wakaanza kuondoka, na yule mama akasema.

‘Wewe Maneno, umenisikia?’ akauliza

‘Ndio mama…’akasema Maneno.

‘Mjinga mkubwa wewe, unafikiri mali zinapatikana kirahisi hivi, hivi mimi nimekuzaa wewe, mpaka nikulee kama mwanangu,ufaidi mali za bure bure…mjinga kweli kweli wewe, mtoto huna shukurani wewe, kila kitu nimekupa, leo hii unanisaliti, utakufa kama walivyokufa wengine mjinga mkubwa wewe…’akasema huyo mama akionyesha sauti ya kukasirika.

‘Mama nimekosa….’akasema Maneno

‘Waambie na wenzako , mimi Ndiye Kikaguala, sifi…watakufa wao, mimi ninadunda tu,na mwanagu ananiangalia huko alipo, ananiona..nyie hamumuoni, hahahahaha…wajinga wakubwa nyie, mwanagu anaijua dunia, akaitengeneza ,kaiweka vizuri, na kila anayetka kuwa naye, anafurahi tu, maisha mazuri, utajiri, lakini ole wake atakayemsaliti…..ni lazima atafanya nini?’ akauliza na wale maofisa wakakaa kimia

‘Nimesema nini nyie watu?’ akasema kwa ukali na Maneno akasema

‘Atakufa…’

‘Hahahaha, hao wengine hawataki kujibu eehe, askari, unasubiri nini fanya kazi yako…wapanue midomoo yao, ….’akasema akijaribu kujiinua kwenye kile kiti, na yule askari akatoa panga, ambalo ni kama jambia.

Wale watu wa usalama walipoona hivyo, wakaanza kutimua mbio kuondoka, na yule mama akaanza kucheka na kutetemeshwa mwili mzima

‘Hahahahaha….mimi kikaguala, hakuna anayeniweza mimi, na dunia yangu itazunguka itazunguka, hahaha, na kila mmoja atatii amri moja, kama hutaki, wewe ni adui, ukikubali, wewe ni rafiki, lakini hakuna rafiki wa kudumu, ukikiuka mashari wewe ni adui….’ Akatikisa kichwa kama kukubali, na ghafla akawa kama kshitulia na kuanza kupiga ukulele

‘Oooh,ooh, naumia, ooh, nihurumie, oooh, ..naumia….hapana, nisamehe mimi, mwanangu, …ooh, alimuua, ndio,…alikosea mshemehe, nisamehe na mimi, ndio nili…ooh, nili….ooh, naumia,….’alianza kulalamika, na haraka yule mlinzi akamsogelea na kutoa sindani akamdunga begani, na haikuchukua muda yule mama akatulia na kuonyesha kuwa amelalala.

Na wakati huo huo mlango ukafunguliwa, akaingia docta akiwa kaandamana na jamaa moja mwenye midevu…

WAZO LA LEO:Jitahidi sana katika maisha yako kutokumdhulumu mtu jasho lake, uwe ni mwekezaji una wafanyakazi wako walipe stahiki zao kwa haki, awe ni mfanyakazi wa ndani mlipe ajira yake halali, na wafanyeni wafanyakazi wenu ni sehemu ya familia, ni sehemu ya ile kazi…acheni kasumba ya ubosi na utwana. Hao waliopo chini yako sio watuma wako.


Tukumbuke tukifanya hivyo, kwa uadilifu na utawala bora, wanaoongozwa watajiona ni sehemu ya hiyo kazi, watawajibika bila kusimamiwa. Na wewe uliyechini ya mamlaka, tii sheria, wajibika kwenye sehemu yako ya kazi bila kutegea, kwani kwa kufanya hivyo, riziki yako ya halali itakuwa na Baraka.

Ni mimi: emu-three

No comments :