Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, October 2, 2014

DUNIA YANGU-41



Kesi ikaanza na cha ajabu kabisa kilichotokea ni kuwa mashitakiwa ambaye alitakiwa kusimama pale mbele, kama mshukuwa wa mauji, hakuwepo, na hata wakili alipoulizwa mshitakiwa yupo alichosema ni kuwa;

‘Mshitakiwa hayupo hapa kwa sababu za kiusalama lakini muda utafika atakuwepo…’akasema

‘Kama hayupo ni kwanini kesi hii inaendelea?’ akaulizwa

‘Kwasababu mume wa marehemu anataka iendelee, ..’akasema

‘Lakini mume wa marehemu si ndiye huyo anayeshukuwa kuwa ndiye aliyemuua?’ akauliza

‘Ndio ilivyo , yeye anataka haki itendeke….’akasema

‘Anataka haki itendeke ya kuwa yeye hakumuua, au mkewe kauwawa, lakini sio yeye?’ akaulizwa.

‘Yeye hakumuua mkewe, hilo ni moja, lakini jingine la muhimu, ni kuhakikisha huyo aliyemuua mkewe ambaye hajajulikana akamatwe,..’akasema.

‘Ina maana sio kweli kuwa mkewe alijiua?’ akaulizwa.

‘Inawezekana kweli alijiua, lakini kwanini alijiua, ….’akasema

‘Kwanini alijiua?’ akaulizwa

‘Ndio maana tunahitaji mahakama hii tukufu itafute ukweli, kama kweli alijiua, au aliuliwa, na kama alijiua mwenyewe ni lazima kuna sababu,…’akasema

‘Je upande wa mashitaka unasemaje?’ akauliza hakimu

‘Sisi kwa upande wetu leo tulikuja kumaliza hii kesi , kwasababu ushahidi uliopatikana unaonyesha kuwa marehemu alijiua mwenyewe…’akasema

‘Mnao ushahidi wa kutosheleza hiyo hoja?’ wakaulizwa

‘Ndio tunao ushahidi….’wakasema

‘Kwahiyo mshitakiwa mliyemlta hapa mahakamani hana kosa, hakuua, kama mlivyowakilisha sitaja lenu….?’ Wakaulizwa

‘Ndio mshitakiwa hana kosa, kesi dhidi yake tunaomba iondolewe…’wakasema

‘Basi tunataka muonyeshe huo ushahidi ili mahakama iweze kuamua….’ wakaambiwa

************

Wakati kesi ikiendelea, mkuu wa idara ya usalama alikuwa kiteta na watu wake kuhusu harakati za kulisambaratisha hilo kundi haramu, na mmoja wa watu wake akasema;

‘Mkuu, tumejitahidi sana kumpata mumiliki halali wa jengo la hiyo hoteli ya Paradise lakini imekuwa kama kitendawili, wanavyodai mtu huyo hayupo tena…’wakasema

‘Una maana gani, kusema hayupo tena….?’ Akaulizwa

‘Huyu mtu amefariki, alikufa kwa shinikiza la damu, na inadadakiwa alikufa kutokana na kuchanganyikiwa, ….’akasema

‘Kuchanganyikiwa….!?’

‘Ndio inavyoonekana kuna mambo ylitokea ndani ya familia yao, ambayo yalimchanganya huyo mwenye hiyo hoteli, wanasema mtu huyo alikuwa akiweweseka na kupiga kelele, akisema, wananiua, wanataka kuniua…, basi ikafika siku moja akadondoka, na wlipompima wakaona shinikizo la damu lipo juu, na hiyo ikawa ni chanzo cha kifo chake…’akasema

‘Sasa ni nani wanaomiliki hiyo hoteli kwa sasa?’ wakauliza

‘Kulikuwa na wanahisa…ambao waliungana naye kabla, akiwa yupo hai, na ukiangalia waraka wa umiliki wa huo mradi, au kitega uchumi hicho utaona kuwa yeye alikuwa akimiliki hisa hamsini na moja, na zilizobakia zilikuwa zikimilikiwa na wanahisa wengine..’akasema

‘Kisheria mtu baada ya kufa, kunakuwa na mrithi wake, je ni nani anayerithi hizo mali?’ wakauliza

‘Ni mama yake, lakini mama yake alisema hataki jina la mtoto wake liondolewe, na akasema nyaraka hiyo ya umiliki ibakie kama ilivyo…’akasema

‘Huyo mama yake yupo wapi?’ akaulizwa

‘Tatizo kubwa alilo nalo huyo mama ni kuwa kachanganyikiwa,…hayupo sawa kiakili, halafu kapooza upande mmoja…’akasema

‘Mhh, sasa hayo ya kusema mama huyo alisema utaratibu wote wa umiliki ubakie kuwa hivyo, aliutoa vipi kama unasema yupo kama kachanganyikiwa….?’ Akaulizwa

‘Hayo aliyatoa kipindi mtoto wake alipofariki, na muda huo alikuwa na akili zake timamu, wanasema kifo cha mtoto wake ndicho kilichomchanganya….’akasema

‘Huyo mama yupo wapi, anaishi wapi?’ akaulizwa

‘Kwenye ile hoteli, kwa chini kuna sehemu kuna nyumba iliyotengenezwa vizuri sana, ukifika utaona sehemu imejitokeza, huyo mama anaishi hapo, na wafanyakazi wanaomuhudumia, ukiingia humo kulivyotengenezwa huwezi kusikia lolote linalotokea nje, imentengenezwa kiasi kwamba, hakuna sauti inayoweza kupenya ndani au kutoka nje….’wakasema.

‘Ni nani dakitari wake anayemuhudumia?’ akaulizwa

‘Kuna docta mmoja mtaalamu sana, alisomea nje, akaja hapa nchini na kuanzisha hospitali yake, wengi wanamfahamu, ni bingwa kweli,…..anaitwa Docta Chiza…’akasema

‘Docta Chiza…?’ akauliza mkuu

‘Ndio mkuu….’akasema

***********

Ilikuwa ndani ya hospitali moja kubwa inayosifika sana kwa matibabu mbali mbali. Ni hospitali ya gharama kubwa sana, hata ukifika utaona kila kitu chake ni cha hali ya juu, viti vya kusubiria wagonjwa ni masofa ya bei mbaya, kuna kiyoyozi, na kila aina ya vitu vya kumfana mgonjwa asijisikie yupo kwenye ofisi, na sio hopsitali.

Kwenye mlango mmoja ulioandikwa, `dakitari mkuu..’ kulikuwa na jamaa mmoja kakaa kwenye sofa la kusubiria zamu yake ya kuingia, alikuwa kashika gazeti akisoma, na mara akaja msimamizi wa eneo hilo na kumuomba kadi yake.

‘Kadi yako tafadhali…’ akaulizwa

‘Hii hapa….’akasema ule mtu na yule msimamizi akaichukua na kuikagua, akamtupia jicho yule mtu, na walipoaangaliana akainama kwa haraka na kuangalia chini, halafu akasema

‘Kwa vile tatizo lako sio kubwa sana, unaonaje ukienda kumuona msaidizi wake..’akasema yule mhudumu, akiendelea kuiangalia ile kadi

‘Hii  ni mara ta tatu nafika hapa na kuambiwa hivyo hivyo, nataka kumuona docta mwenyewe,….ndio maana nimelipia hivyo….’akasema yule mgonjwa

‘Hamna shida utamuona tu….ni ushauri wangu , maana huyo docta sasa hivi anaongea na simu, kuna mgonjwa mwingine anahitajika kutoka, kwenda kumuona..lakini ngoja tuone kama anaweza kukuhudumia,….’akasema huyo msamamizi.

‘Leo sitoki hapa mpaka nimuone….’akasema huyo mgonjwa.

Yule msimamizi akaingia ndani, na baadaye akatoka,na kusema ingia, na yule mtu akaingia kumuona docta. Na yule mtu alipoingia akamkuta yule docta akiendelea kuongea na simu, yeye akakaa kwenye kiti kama sofa kilichopo hapo, akatulia kumsubiria docta amalizie kuongea na simu yake.

‘Ni nani anataka kumuona huyo mama?’ akauliza docta akiongea na simu

‘Watu wa usalama!?Kwani hao watu hawajui kuwa huyo mama kachanganyikiwa, waambie mimi kama docta wake, nimesema huyo mama harushusiwi kuongea na mtu, kutokana na hali yake ilivyo…’akasema

‘Wanataka kuniona na mimi pia, kuhusu nini?’ akauliza

‘Sawa wapange muda wao nikiwa na nafasi nitakutana nao wafike ofisini watakutana na katibu muhutasi wangu atawapangia siku na saa lakini sio leo…., sitaki waniingilie kwenye kazi zangu, …mimi ni mtaalamu na bingwa,najua nini ninachokifanya….’akatulia

‘Eti nini, wanauliza kuhusu mtoto wa huyo mama?’ akauliza kwa mshangao, na akainua uso kumuangalia huyo mgonjwa aliyeingia na kukaa kwenye kiti.

‘Hao watu hawajui walifanyalo, huyo mtoto wa huyo mama amefariki siku nyingi, kama wanahitajia vithibitsho vya kidakitari vipo, tutawaonyesha, au kama wanataka kuliona kaburi la huyo marehemu wapelekwe walione, shida ipo wapi hapo, wanataka nini zaidi, maelezo gani wanahitajia kutoka kwangu, kuhusu huyo mama…unasema kuhusu vitega uchumi vyake…aaah, kila kitu kipo sahihi bwana….wasiwababaishe hao watu, kwani ni ofisa gani huyo….?’akasema kwa dharau na kuuliza

‘Haya ngoja nimalizane na huyu mgonjwa mmoja , ninakuja huko tuliongee hili, maana naona kuna tatizo, lakini sio tatizo kubwa sana, tutalimaza tu,..na waambie wengine, wajipange vyema…..’akasema na kukata simu

Akainua uso na kumuangalia mgonjwa aliyekaa kwenye kiti mbele yake, kwanza akakunja uso kuonyesha kutokufurahishwa na kitu , halafu akatabsamu na kuuliza

‘Kwanini umefuga ndevu nyingi hivyo, huoni zitakusumbua, na kiusafi ningekushauri angalau uzipunguze, ni ushauri tu kama docta, sio kwamba nakuingilia mambo yako…’akasema

‘Hilo sio kusudio langu la kufika hapa…’akasema huyo mtu, na Docta akatulia kusoma maelezo kwenye ile kadi ya huyo mgonjwa.

‘Na mbona umeandika jina moja tu, hujaweka ubini wako, kwa kumbukumbu za kiofisi ulitakiwa uandike kile kitu, na….kila kitu kipo sahihi, huna tatizo, moyo, damu….ok, samahani kwa kukushauri kuhusu hizo ndvu, najua kuna watu wana imani hizo za kufuga ndevu, lakini zako zimezidi hazikusumbui…?’ akauliza akitabasamu, alionyesha kweli ni mtaalamu na anafhamu vipi kumweka mgonjwa sawa, ajisikie yupo nyumbani.

‘Hazinisumbui, na kama zingenisumbua ningezinyoa….’akasema huyo mgonjwa na huyo docta akawa kama kahisi jambo, akamuangalia yule mgonjwa kwa makini, akauliza

‘Ni nini shida yako…?’ akauliza

‘Shida yangu ni kubwa ni kutaka kuongea na wewe..’akasema huyo mgonjwa

‘Eti nini…..?’ akauliza huyo docta kwa mshangao, halafu akaangalia kwenye komputa yake iliyopo mbele yake, halafu akashika kidevu, kumuangalia huyo mgonjwa, akaangalia saa yake na kusema;

‘Umakuja kutibiwa au kuongea na mimi…?’ akauliza

‘Nataka kuongea na wewe kuhusu huyo mtoto wa huyo mama, na mahusiano yake na wewe……’akasema huyo mtu, akito kitu mfukoni, kilikuwa ni kitambulisho caha kuonyesha yeye ni nani , na huyo docta hakutaka kabisa kukiangalia,akasema;

‘Hapa nipo kazini siwezi kufanya hayo, nahitajia kuwahudumia wagonjwa kwanza…’akasema akionyesha kutokujali, na tabasamu la kuigiza likajaaa mdomoni.

‘Najua hilo…, lakini kwa akuli yako mwenyewe hapo kwenye simu, umesema kuwa mimi ni mgonjwa wa mwisho kuhudumia na wewe, mimi nikitoka, wewe unakwenda kuonana na watu wako kuongelea swala la mtoto wa huyo mama aliyechanganyikiwa, mtoto wake ambaye anamiliki miradi mingi ikiwemo mradi wa hoteli hiyo kubwa ya Paradise au sio….?’akasema huyo mtu na kumfanya docta akaonyeshe uso wa kutahayari kidogo, lakini akatabasamu na kusema;

‘Lakini hayo yanakuhusu nini wewe, kuna kosa nimefanya, na je huu ndio utaratibu unaotakiwa kufuatwa, twende mbele turudi nyuma, au…?’ akauliza

‘Yananihusu sana, ndio maana nataka kuongea na wewe, na nafanya hili kwa nia njema tu, …’akasema huyo mgonjwa.

‘Haya niambie unataka tuongee nini….?’ Akauliza huyo docta akitulia kumsikiliza huyo mgonjwa, na simu ya mkononi ya huyo docta ikalia kuashiria ujumbe, na alipousoma huo ujumbe, akakunja uso…

WAZO LA LEO: Hakuna usafi mnzuri kama usafi wa moyo, ukiwa msafi wa moyo, huwi na wasiwasi, na mara nyingi, tabia zetu na matendo yetu yatakuwa ni mazuri. Wengi wetu tunajali usafi wa mwili, nguo, na unadhifu n.k, lakini mioyo yetu ni michafu, zaidi ya mtu aliyejipaka kinyesi. 

Tunakuwa na roho mbaya, ubinafsi, wizi, na kila aina ya matendo mabaya. Huo ni uchafu mkubwa sana, lakini hatuuoni, na mwilini tunajifanya kuvaa kinadhifu. Tunaoga kupindukia, na harufu nzuri za manukato, lakini tunanuka rohoni.


Ni muhimu sana, tukajisafisha mioyo yetu kwanza, ili kweli tuonekane wanadhifu.

Ni mimi: emu-three

No comments :