Akatoka
na kwenda barazani, akachukua kiti, maana lile kabati ni refu, akaweka kiti na
kusimama juu yake na hapo akaweza kufikia mwisho wa lile kabati na kuanza
kuangalia pale juu, looh,....kile kitu hakikuwepo..
‘Nina
uhakika niliona kitu hapa juu…ilikuwa kitu kama bahasha ni nani kaichukua...’akasema
‘
Ni
hiki unakitafuta mkuu….’akasikia sauti, iliyomshitua hadi kutaka kudondoka
kwenye kile kiti. Sauti anayoifahamu, na sauti hiyo ni ya watu wawili,
wanaofanana wakiongea, mmojawapo ni yule muuaji wa kundi ambaye akitumwa kwako
ujue wewe ni maiti, na wapili… akagwaya….
Na
pale alipokuwa kasimama kwenye kiti aliogopa hata kugeuka, akilini akijaribu
kuhakiki, kuwa kweli sauti hiyo ni ya mtu anayemfahamu, na kili hapo ilifanya kazi kwa haraka sana, akasema;
‘Wewe
ni nani, umetumwa kuniua sio…..’akasema na kwa haraka akaruka hewani na kujiviringisha
kisarakasi hewani kutoka kwenye kile kiti na kutua chini tayari kwa mapambano….
Tuendelee na kisa chetu....
*****
Inspecta
Maneno alipofika sakafuni akajiviringirika kiaskari, na kwa haraka sana akasimama
akiwa kwenye kisimamo cha kurusha teke, lakini alipopepesa macho yake kwa
haraka, kuangalia wapi pigo litue, akajikuta yupo peke yake, hakuona mtu,
akatuliza kichwa na kutega masikio, hakusikia chochote,..
Alitembea
mwendo wa kuvizia akiwa tayari kwa lolote huku bastola ikiwa tayari mkononi,
akiwa na bastola, ni kama wapo kumi, ….hadi muda huo alijua kuwa labda adui
yupo sehemu kajificha, lakini pale chumbani hakuna sehemu mtu anaweza kujificha.
Humo ni chumba cha kulala, kuna kitanda, kabati kubwa, na meza ya kusomea, na meza nyingine ipo kwa
pembeni ikiwa na luninga hakuna sehemu mtu anaweza kujificha kabisa, lakini
hata hivyo hakuamini, huyo mtu kama ni yeye, anaweza kutumia kila mbinu,
akajificha sehemu isiyofichika,….mmmh.
Haraka akagundua kitu, Mlango ulikuwa
wazi, kwahiyo huyo mtu alishatoka kwa haraka…..basi huyo mtu ni mwepesi sana,
akawaza hivyo.
Akatoka
kuelekea barazani , kwenye chumba cha maongezi akijua huenda huyo mtu yupo hapo
anamsubiria sehemu yenye nafasi kwa mapambano,lakini alipofika hapo, akasikia
kwa nje ni sauti ya pikipiki ikiondoka kwa kasi..akasonya, na kusema;
‘Huyu
mtu atakuwa ni nani…’akatoka nje kwa haraka, lakini pikipiki ilishatoka nje ya
geti, na hakumuona huyo mtu , na hata mlinzi alikuwa hayupo,…akaangalia huku na
kule, na kusema;
‘Huyu
mlinzi kaenda wapi…?’ akajiuliza, lakini hakupata jibu, akajaribu kukumbuka
sauti ya huyo mlinzi kama ni yeye aliyeingia humo ndani, lakini sauti ya yule
mlinzi haifanani kabisa na hao watu anaowafikiria yeye…kwahiyo atakuwa ni huyu
huyo jamaa anayemfikiria yeye…
‘Atakuwa
ni ‘Kifo…’akasema kimoyo moyo
‘Kifo’
ni mmoja wa watu kwenye kundi ambaye kazi yake kwenye kundi ni moja tu,
kumaliza maisha ya maadui. Akipewa kibali hakosei, na kawaida yake
haonekani ovyo, akionekana kwako ujue
ndio kifo chako.
Hata
Inspecta alimuona mara moja siku alipotambulishwa kwake, na akaambiwa wazi huyu
akija kwako tena ujue ni umauti wako,…
‘Huyu
anakuja kwangu tu…..akija kwako ujue anakuja kukumaliza…’akaambiwa.
Lakini
walikuwa wakiwasiliana naye kwa simu, na kuweza kuizoea suati yake hasa pale
alipokuwa akitakiwa kumuelekeza wapi mtu fulani anayetakiwa kwake au anayetakiwa
kumalizwa yupo…
‘Mbona
sauti yako inafanana na ya mtu ninayemfahamu…?’ siku alipotambulishwa kwake
alimwambia wakat wanaongea.
‘Huenda
mtu huyo tuna tabia zinazofanana, lakini sizani kama sauti yangu inafanana na
mtu mwingine, mimi najijua kuwa nina sauti ya kivyangu…’akasema
‘Inafanana
kabisa na sauti ya rafiki yangu mmoja, ukiongea wewe utafikiri ni yeye anayeongea….’akasema
‘Basi
uwe makini na hilo…’akaambiwa, na hakukaa naye sana akaondoka, na ikawa ndio
mwisho wa kuonana naye uso kwa uso.
Alipokumbuka
hayo mazungumzo, akasema;
‘Huyu
mtu hakunifuata mimi, kama angenifuata mimi angelishaniua, inawezekana alikuja
kuhakikisha kuwa Inpecta Moto hayupo, na kama yupo ammalizie, atakuwa ni yeye
tu…’akasema
Na
mara akamuona mlinzi akitokea chooni, huku anafunga funga suruwali yake
vifungio, na akawa anakuja muelekeo wa getini kwake, na alipokaribia pale
aliposimama Inspecta akageuka kuangalia pale lilipokuwapikipiki ambalo kwa muda
huo halipo tena.
‘Mbona
sielewi, nimesikia pikipiki ikiondoka, nikajua ni wewe umeondoka nalo…?!’akauliza
kwa mshangao.
‘Una
uhakika hakuna mtu aliyeingia humu, wakati nipo ndani…?’ akauliza Inspecta
akimuangalia yule mlinzi akiwa kamkazia macho.
‘Nina
uhakika mkuu, na sijakaa sana humo ndani, nimeingia sasa hivi tu, na masikio
yangu yalikuwa yanasikia kila kitu…hakuna mtu aliyeingia, nilichosikia sasa
hivi ni sauti ya hilo pikipiki likiondoka. …’akasema.
Mlinzi
huyu ni mzee wa makamo, aliwekwa hapo kusaidia ulinzi, katika kusaidiana,
mwanzoni aliwahi kulitumia jeshi, akastaafu, na wakaona kwa vile bado ana nguvu
basi katika kusaidiana awe anakuja kufanya hiyo kazi hapa na pale.
‘Sasa
ni nani kachukua pikipiki langu na kuondoka nalo..na huyo mtu anatumia funguo
za bandia, au aliwahi kuiba ufunguo wangu na kuchongesha, basi ni mtu anayenifahamu,…
siwezi kuelewa, kwa jinsi alivyoweza kuingia, na kuchukua na uharaka wake wa
kufanya haya….ooh, atakuwa ni yeye tu…’akasema
‘Ni
nani,…ina maana unamfahamu, lakini mbona unanichanganya, mbona sikuona mtu
akiingia hapo getini mkuu, nikiwa chooni, kuna tundu pale nachungulia muelekeo
wa getini, hakuwahi kuingia mtu na niliposikia pikipiki likiondoka, nikawa sina
wasiwasi tena, nikajua ni wewe umeondoka na pikipiki lako…’akasema
‘Umefanya
makosa sana kuondoka kwenye lindo lako ukijua hakuna mtu aliyeshika nafasi
yako..na uzoefu wako wote leo umeharibu…’akasema Inspecta.
‘Mkuu,
hakuna mtu aliyeingia, mimi nina uhakika labda awe kapitia sehemu nyingine, lakini
sio kupitia getini…’akasema
‘Angepitia
wapi sasa, kuwa aliruka ukuta, haiwezekani, ukuta huu mrafu halafu una nyaya za
umeme, …..’akauliza akikagua kwa macho ukuta unaozunguka hiyo nyumba, lakini
hakuweza kupata sehemu ambayo mtu angeliweza kuruka na kuingia ndani…
‘Yawezekana
aliruka kupitia nyuma,…kule nyuma kuna sehemu ina uwazi kuna nyaya
hazikuunganishwa, kwa wenye uzoefu wa kazi za namna hiyo wanaweza kupitia hapo,
hata hvyo kwanini afanye hivyo, na kama alifanya hivyo …angelipitaje na kuingia
mlangoni mimi nisimuone…’akasema
‘Kwanini
wewe uliingia chooni muda gani ….?’akauliza
‘Nimeingia
sasa hivi nikijisaidia haja ndogo, hebu fikiria haja ndogo inachukua muda mrefu….’akasema
akiangalia saa yake
Inspecta
akachukua simu yake na kupiga namba yake ya siri, akasubiri na mara sauti ikawa
hewani na akajitambulisha kwa maneno yao, halafu sauti ikauliza
‘Kwanini
umenipigia, tulipanga nini na unafanya nini?’ akaulizwa
‘Nauliza
ulimtuma `kifo’ kuja kwa Moto…..?’
akauliza
‘Nimetume
kuje kwa Moto? Mbona sikuelewi, mbona kazi hiyo nilikupa wewe, kwanini nimtume
mtu mwingine au umeshindwa, nimpe kazi huyo jamaa, na ujue sisi tunasubiri
utupe taarifa kuhusu huyu mtu wako, siwezi kutuma mtu, hususani Kifo, kama
umeshindwa hiyo kazi nitamtuma yeye, lakini kwanza atapitia kwako kwasababu
umenisaliti….’akaambiwa
‘Bosi…’akataka
kujitetea
‘Uliitwa
kwenye kikao maalumu cha watu wenu, hukutoa taarifa ya muito huo, na pili
ulizima kinasa matukio unachotakiwa kuwa nacho kila mahali, kwanini ulifanya
hivyo, kama sio nia ya kusaliti kundi, unafikiri nitamwambiaje bosi mkuu..?’ akaulizwa
‘Sehemu
kama ile huwezi kuingia ni kifaa chochote, utagundulikana tu, ndio maana
nilifanya hivyo,….’akasema
‘Hicho
kifaa hakiwezi kugundulikana kwa mashine yoyote, nina uhakika na hilo, na
sisemi bila ushahidi, nilishawahi kutuma watu wangu wakaingia nacho, na
hawakugundulikana kuwa na kifaa kama hicho, kwa hilo usinidanganye…’akasema
‘Bosi
ina maana sasa huniamini….?’ Akauliza
‘Kukuamini
kwangu ni hapo utakaponiletea kichwa cha Inspecta Moto, na pili nataka huyo
inspecta Mpya asalimu amri ….kwa kila njia kama umeshindwa useme, na ukishindwa
wewe najua una njama za kutusaliti, na umekiuka masharti tuliokubaliana. Na
mimi sioni kwanini
'Kifo' asikutembelee, ila kwa sasa nimetuma kazi moja, muda
wowote atakurudi, akirudi ujue ni mgeni wako..’akaambiwa.
‘Kaenda
wapi bosi mimi nina uhakika alikuwa hapa kwa Moto…’akasema
‘Sio
yeye..na kwasababu wewe umevua kile kifaa cha ulinzi, hatuwezi kujua ni nani
aliyefika huko,na unakumbuka hapo tulishaondoa vifaa vyote vya kuonyesha
matukio,kwahiyo imekuwa shida kujua lolote ..’akasema huyo anayeitwa bosi.
‘Ninachotaka
kujua ni je Kifo alifika eneo hili?’ akauliza.
‘Atafikaje
huko bila kibali changu, atarudi karibuni, na akirudi kazi ya kwanza
nitakayompa ni kuhusu nyie wawili, hilo nakuthibitishia, vinginevyo umalizie kazi
uliyopewa hasa kuhusu huyo rafiki yako…nakupa nusu saa niskie matokea zikipita
utakutana na Kifo…’akaambiwa
‘Bosi
nina uhakika ni yeye, sasa kama sio yeye ni nani…’akawa anajiuliza
‘Mimi
sijui hilo na sina haja ya kulijua hilo kwasasa, maana halina umuhimu kwakngu,
la muhimu kwako , nataka huyo mwenzako apotee , nashindwa kuelewa kwanini ile
sumu haikufanya kazi kama ilivyofanya kwa wengine ni nani kagundua jinsi ya
kuitoa hiyo sumu mwilini, hakuna dawa inayoweza kuiondoa hiyo sumu, nahisi kuna
tatizo,…’akasema
‘Hata
mimi bosi nashangaa sana..sielwei maana nilitarajia kusikia mwili wake
umeokotwa huko alipoenda kutupwa…..’akasema
‘Naona
haikufanyika hivyo, huenda huyo mtu mliyempa hiyo kazi, hakutumia sindano
inayostahiki,…sasa basi kama sumu haikufanya kazi, mimi nataka uniletee kichwa
cha huyo mtu, au kama huwezi basi nataka kichwa chako…’akasema
‘Bosi,
kwasasa haitawezekana…’akasema
‘Ok,
kama haitawezekana kwako wewe, nitampa kazi huyo uliyemtaja, …naona nyote
wawili kwasasa ni tatizo kwa kundi, hata hivyo kazi mliyohitajiwa kwenye kundi
mumeshamaliza, kubakia na nyie ni mzigo tu,…na kwa vile umemuota Kifo kuwa
kakujia basi kwanini hiyo ndoto yako sasa isiwe kweli,…kifo atakuja kukutembelea
hilo nimelithibitisha rasmi, kazi kwako ….’akasema na simu ikakatika.
‘Oh,….’akaguna,
akijua huyo bosi akisema neno ni lazima linatimizwa, ndio sera yake, kwahiyo
anatakiwa kujiandaa na umauti wake.
‘Sikubali
siwezi kufa hivi hivi…nitafanya atakavyo….’akasema na kuelekea barabarani kutafuta
usafiri, akakuta pikipiki ipo barabarani…akamwambia mwenye pikipiki,
‘Nipeleke
hapo kituo cha polisi..’akasema
‘Sawa
bosi….’akashituka, sauti ni ile ile aliyoisikia kule ndani, akataka kumuangalia
yule mtu, lakini yule mtu akawa ameshavaa kofia la waendesha pikipiki, hakumuona
sura yake, na kabla hajasema neno, akahisi kitu kikipenya mkono wa kushoto, ….akajua
hiyo ndio ile, sindano ya umauti. Kifo keshafanya kazi yake…..
WAZO LA LEO: Dhamira mbaya kwa
wenzako, chuki, na husuda ni udhaifu usio na tija. Ukiona mwenzako kaendelea
kafanya maendeleo, basi mpe hongera na kwa nia njema unaweza kuomba ushauri
kwake ili uwe kama yeye au zaidi.
Lakini
wengi wetu tunaishia kujenga chuki, kuona wivu, na hata kuhisi vibaya kwa huyo
mtu. Ni kweli , huenda kaupata utajiri huo, au maendeleo hayo kwa njia mbaya,
kama una uhakika na hilo, basi chukia matendo hayo, usiyafuate, lakini kama
kaupata kihalali, basi ungana naye, pata ushauri kwake, na huenda ukifuata
alivyofanya yeye kwa nia njema unaweza kufanikiwa, lakini kamwe usifuate
matendo mabaya yenye dhuluma kwa nia ya kupata utajiri, utajiri huo hauna
mwisho mwema.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Hapa duniana baadhiyetu tunapenda kupata kirahisi . Hatufikirii aliyepata amepataje...wazo la leo ni ujumbe mzuri sana kwa jamii
Post a Comment