Usiku
inspecta hakuweza kulala kabisa, mawazo, huzuni upweke vikawa vinamuandama,akili
ilikuwa ikimuwaza mkewe, na yote yanayoendelea, hakupendezewa kabisa kwa hayo
waliyofanya wenzake, ambao wanadai kuwa kweli kuna ushahidi wa kutosha kuwa mke
wake alijiua.
Kuna
muda alitamani atoke kwenda kwenye ukumbu wa starehe, akapoteze mawazo, lakini
aliogopa kuwa akienda huko ni lazima atashawishika kunywa, na alijua udhaifu
wake kuwa akinywa na hasira alizo nazo anaweza akafanya kitu kibaya, na hasa
kama atabahatika kuwa na silaha, akaona avumilie hovyo hivyo.
Akaelekea
kitandani na kujilaza, ilikuwa kama humo kitandani kuna mashetani yamelala humo
kwani kila alipojaribu kupitiwa na usingizi, alijikuta akikutana na ndoto
zakutisha, mara anaota anatokewa na mkewe, akiwa na sura ya kutisha, mara
anaona watu wanataka kumuua, ikawa anapata taabu, mpaka ikafika saa sita usiku
sasa kichwa kikawa kinamuuma.
Akawa
anajaribu kukumbuka matukio ya mchana ili kupoteza mawazo, na ndipo akakumbuka
ujio wa mama mkwe, ambaye alipofika, walipata muda wa kuongea, mama mkwe
alikuwa tofauti kabisa na alivyokuwa siku za nyuma.
********
‘Mwanangu
nimekuja kwanza kabisa nataka hata kupiga magoti kukuomba msamaha, nisamehe
sana mwanangu, maana unajua tena, ….’akasema huku machozi yakimlenga lenga.
‘Mama
usijali, …nilijua tu ipo siku utagundua ukweli, kuwa mimi siwezi kumuua mke
wangu,…mke wangu nilimpenda sana, licha ya mitihani ya hapa na pale, lakini
nisingeliweza kufanya huo unyama…’akasema
‘Yaani
hata siamini, lakini kwanini ilifikia hapo, mpaka aamue mwenyewe kujiua, kuna
nini kilitokea kati yenu,…na kama ni hayo ya wivu kuwa aliambiwa kuwa una
mwanamke mwingine, ndio ifikie hatu ya kujiua…’akasema.
‘Mama
mengi yatasemwa, na kwa vile mke wangu hayupo duniani, hataweza hata kujitetea
na kujieleza, lakini mimi nina imani kuwa ukweli wa kifo chake bado
haujajulikana vyema, sina uhakika wa hilo la kujiua, huenda ndio hivyo,….’akasema.
‘Ndio
hivyo mwanangu, nimeonyeshwa ushahidi wote, …jamani inatisha, lakini kwanini
akafanya hivyo, mungu amsamehe madhambi yake, …’akatulia, akionekana
akisononeka moyoni.
‘Mama,
hili jambo, niachieni mimi, nataka nilichunguze mwenyewe kiundani, maana mimi
ndiye ninayemfahamu sana mke wangu, japokuwa wewe ni mzazi wake, lakini mimi
niliishi naye ukubwani, na nimemsoma na kumjua vyema mke wangu, hilo la kujiua,
halijaniingia akilini…’akasema Inspecta.
‘Mwanangu
ndio hivyo,… huo ndio ukweli, nimethibitisha, na sina shaka na hilo,…muhimu ni
kumuombea mungu tu, kwani hiyo imekuwa ndio sababu ya mwisho wa maisha yake, na
kila mmoja ataondoka kwa sababu yake …’akasema na kushika shavu.
‘Na
mwanangu nakuomba na wewe utulie umuombee mwenzako mema, aishi pema peponi, na wewe
pia utubu dhambi zako, kwasababu yote yalitokea akiwa na dhana kuwa wewe una
mwanamke wa nje…’akasema.
‘Lakini
mama…’akataka kujitetea.
‘Mimi
nafahamu kuwa kutokana na kazi zenu unaweza kujikuta ukiwa na mwanamke, hapa na
pale, na cha muhimu kwa kazi zenu ni kujua mipaka ya ndoa yenu..mimi na mume
wangu tuliishi hivyo hivyo…’akatulia kidogo na baadaye akasema;
‘Mwanangu
siwezi kukuficha kuwa sisi tulivumiliana kihivyo…hapana, kuna kama hayo yalishawahi
kutokea kwa mume wangu, unamkuta kabisa akiwa na mwanamke mwingine…unaumia,
mnagombana kweli, mnafikishana mpaka kwa wazee, lakini baadaye tunasuluhishwa,
na ukikaa na kuja kuchunguza, unagundua kuwa ni kweli kumbe alifanya hivyo
katika kutekeleza majukumu yake….’akasema
‘Mama
kwa hili la kifo cha mke wangu, kuna mengi yamejificha, nakuomba tu, unielewe
hivyo….’akasema lakini mama yake akawa kama hamuelewi, akaendelea kuongea kwa
kusema;
‘Kazi
zenu hizo zina mtihani mingi, na kiukweli ingelikuwa ni uwezo wangu nisingelipenda
mtoto wangu aifanye hiyo kazi yenu, siipendo, siipendi …maana ni sawa na
waigizaji, unaona kabisa kuna tendo chafu linafanyika, lakini ni katika kuleta
ujumbe, halikadhalika kwenye kazi zenu kuna muda unalazimika kuingia kwenye matendo
machafu ili kupata ukweli fulani…..’akasema.
‘Ni
kweli wakati mwingine tunakumbana na mitihani kama hiyo, na wakati mwingine
mitihani hiyo inaletwa kama mitego tu,..yote hayo ndio yananifanya nishindwe
kuamini kifo cha mke wangu kama kweli kilikuwa ni cha kujiua… bado kabisa
sijakubaliana na hilo, kama ilivyo kuwa kifo cha muheshimiwa….nahisi, kuna kitu
kipo nyuma yake….’akasema Inspecta.
‘Niliwashauri
wasikuonyeshe huo ushahidi walionionyesha mimi,….maana utakuumiza sana,
japokuwa hata mimi kuna sehemu wamenificha kama mzazi, wakisema ushahidi huo utaniumiza
zaidi, lakini huo mchache nilioonyeshwa, na uchunguzi wangu mwenyewe, nimethibistisha
kuwa kweli binti yangu alijiua mwenyewe, sitaki kusikia zaidi…’akasema, na
kabla inspecta hajasema neno, mama huyo akasema;
‘Na
hiz shutuma kuwa kajiua kwa wivu kuwa wewe ulikuwa na mwanamke wa nje,
nimeufanyia kazi, nimegundua mengi, na hili nisiwafiche nyie wanaume
mnajiendekeza, pamoja na kuwajibika kwenye kazi zenu, wakati mwingine mnatumia
visingizo vya kazi, kujinufaisha na tamaa zenu za kimwili, hilo mnalo….’akatulia
‘Mama
ni kweli lakini…’akasema,lakini mama akamkatiza na kusema;
‘Ilibidi
nifanye hiyo kazi ya kupeleleza mwenyewe, maana hata mimi nilipitia pitia huko,
japokuwa nilikuwa mwalimu, na nlipofanya uchunguzi, nimegundua kuwa kweli
ulikuwa na mwanamke wa nje…usikane, huo ndio ukweli….’akasema
‘Ama
kama ulikuwa naye kwa ajili ya kuwajibika, hilo ni jingine...nilipogundua hilo,
sikutaka kujua zaidi, ila mwanangu nakukanya, hata kama nikufuatilia jambo,
jitahidi sana kuchunga mipaka ya ndoa yako, usitumie visingizio, utaua wengi
bila kupenda, maana hata mimi nilitamani kujiua…’akasema mama.
‘Ni
kweli mama,…mnisamehe sana,..ni kweli mama hilo nimeliona, hata hivyo,kama
nlivyokuambia hili tukio lina mambo mengi yamejificha,…nahitaji muda wa
kutuliza kichwa kuyaangalia haya matukio kwa mapana yake…’akasema.
‘Mwanangu
nikushauri jambo, achana na hilo..hata kama utakesha, utalia, utachunguza
kupitiliza, binti angu hayupo tena duniani, na hataweza kurejea tena..muhimu ni
wewekujipanga upya, jiangalie maisha yako…unasikia, wewe umebakia duniani, li
uwajibike, mungu kampenda yeye akapumzike huko mbele ya haki, sasa wajibika ….’akasema.
‘Unajua
mwanangu, kuna siku niliongea na marehemu , binti yangu,…maana kuna siku
tunakaa kama mtu na rafiki yake, akaniambia jinsi wenzako wanavyojiendeleza,
akasema wewe muda mwingi upo katika kazi yako tu,..hutaki hata make na mwenzko
mshauriane maisha yenu ya baadaye, ….sikatai kazi ni muhimu, lakini ujue kazi
pekee haiwezi kukufanya ukawa na maendeleo….’akasema mama.
‘Mama
ni kweli, lakini….’akataka kujitetea lakini mama akaendelea kusema
‘Mimi
na baba yako, tuliishi maisha ya dhiki sana, yeye alikuwa kama wewe, kazi na
yeye, hasi anafikia kustaafu, bado tu anang’ang’ania kuendelea kufanya kazi, akawa
hana mbele wala nyuma, kiinua mgongo alichopewa, hakikuweza kumsaidia lolote,
ashukuru mungu kuwa mimi na ualimu wangu, ndio uliotufanya hadi tuweze kusonga
mbele, vinginevyo, tungeumbuka….’akasema.
‘Mhh,
hongereni sana…’akasema.
‘Sasa
nyie wakati wenu huu mna uhuru wa kufanya shughuli nyingine, kipindi chetu
hukuruhusiwa kama muajiriwa kujibidisha na ajira nyingine, na kama mna uhuru
huo,utumieni vyema kwa kujiendeleza, ongea na mwenzako, inspecta mwenzako ana
akili kweli, ya kuona mbali, unajua kanisaidia sana hata mimi, hadi sasa naweza
kusema, sina shida, kanipa mawazo, kanionyesha njia….’akasema.
‘Pamoja
na uzee wangu huu kumbe ninaweza kufanya jambo, ninaweza kuzalisha, nikawa
siwategemei tena watoto,…siku nyingi amekuwa akituelimisha jinsi ya
uwezekazaji, kuna walimu wao, wanajua sana kuelimisha watu, tumeanza miradi na
sasa tupo mbali,…’akasema.
‘Ina
maana mumeanza muda kufanya hayo aliyowaelekeza rafiki yangu?’ akauliza
‘Tatizo
lako, wewe ni sawa na mume wangu, muda wote unafikiria kazi, jipange mwanagu
wakati ndio huu , huku kazi huku unaangalia maisha yako ya baadaye, usije
ukafanya makosa kama ya mume wangu. Mume wangu hadi sasa anaota kazi, japokuwa
kastaafu, maongezi yake ni kazi yake ilivyokuwa, angepata nafasi angelifanya
nini…yaani yeye na kazi…, kazi, kila jambo,kazi, yaani atakufa akikumbuka kazi,
kazi ambayo imeshamtema, keshastaafu, atafanya nini tena na uzee ule..’akasema.
‘Lakini
huo ndio uzalendo, kupenda taifa lako na watu wake, uzee sio tija ya kuacha
kueleza, na kuelekeza, tukiwatumia wazee kama wao, tunaweza kufanikiwa zaidi,…tatizo
ni kuwa watu kama hao hawathaminiki, kwa vile hawajui kuongopa…ukweli, haki na kujitolea
kwao, unaonekana kama hadithi za Alinacha…’akasema Inspecta.
‘Hahaha,
mwanangu ni kweli, hayo hakuna duniani tena…’akasema mama.
‘Ukiwa
mkeli, ukatenda yaliyo haki…, unaonekana kama kuvaa kanzu tu…vitu kama hivyo,
havithaminiki tena,…ujanja-ujanja, udhalimu, ufisadi ndio sifa ya siku hizi,
ukiwa navyo umesoma sana, utapata kazi, utapata mshahara mkubwa, wewe unaona
mbali, ukiwa navyo, wewe unafaa katika mikutano, katika uongozi, …sijui kama
kweli dunia itakuwa na amani kwa hali hiyo…’akasema Inspecta.
‘Ndio
hivyo mwanangu, bora uwe mjanja, ujiandae kwa maisha yako ya baadaye, maana
hakuna atakayeangalia maisha yako na familia yako zaidi ya wewe mwenyewe,
hakuna atayekutetea kuwa ulikuwa mfanyakazi bora, hakuna…hilo nakuambia, sifa
zaitakwenda kwa yule aliyekuwa mjanja, akajijenga, hata kama ni kwa dhuluma,
hata kama ni kwa ufisadi, lakini sasa ana miradi,ana maisha mazuri,…huyo
atasifiwa, wewe uliyejifanya mchapakazi, una maisha magumu, unaaibika kwa
kutembea na ndala huku na kule ukiomba omba, utazaraulika tu….’akasema.
‘Sawa
lakini mimi nina imani kuwa haki , ukweli, ndio msingi wa maisha, na hivyo
vingelipewa nafasi, dunia ingelikuwa na amani, kusingelikuwa na vita, watu
wangelipendana, dunia inagubikwa na vita kwasababu hakuna haki, wale
wanao-onewa, hawana wa kuwatetea,…’akasema Inspecta.
‘Ndio
wakati wake huo mwanangu, ….’akasema mama na Inspecta kwa sauti ya taratibu
akasema;
‘Mama
huo ndio ukweli, ndio maana kunatokea makundi yenye siasa kali, imani kali, makundi
haya yanajaribu kutoa hisia zao kwa kupitia maeneo yao yanayowazunguka, wao sio
wajinga, wana yao yamewatinga, lakini hawapewi nafasi ya kusikilizwa, …’akasema
‘Ndio
hivyo mwanangu na wenzao wajanja, mafisadi, wenye nafasi zao, ambao ndio
waligeuza haki kuwa batili, wanatumia mwanya huo huo, wa hayo makundi, kuwekeza
fitina, …wanazidi kumwagia mafuta kwa manufaa yao…biashara ya silaha
inashamiri, ubeberu unarudi kwa mtindo mwingine umasikini unazidi duniani..hayo
yapo, ni wakati wake…’akasema mama.
‘Unaona
eeh mama, sasa kwa mtaji huo hebu niambie tutafika wapi…’akasema Inspecta.
‘Mwanagu
sasa kwa hali hiyo utafanyaje, inabidi na wewe uangalia muelekeo, maana
ukijifanya mcha mungu saana, utaachwa kwenye mataa, ni vyema uwe bega kwa bega
na wenzako ili na wewe uende na wakati….ni hilo tu mwanangu, mimi nakushauri,
kaa na mwenzako, akuonyeshe njia, yeye ni mjanja, yeye anajua maisha, ….mtumie,
utafanikiwa, vinginevyo, naogopa kusema unaweza kuishia kubaya….kwaheri
mwanangu, na natumai tumesameheana…’akasema.
‘Mimi
mama sina kinyongo na wewe, na nashukuru sana, kuwa umelewa, na umenisamehe na
mimi, kwani kama binadamu huwezi kuwa mkamilifu,….nina mapungufu yangu, na
ndivyo tunahitajika kuishi hivyo, kukubali ukweli kuwa kila mmoja ana mapungufu
yake, na tukikosea, tusameheane, …’akasema.
‘Ni
kweli, lakini pia tukosoane tukikosea au sio, tuonyesheane njia tukipotea au
sio, na mimi nakushauri umshike mwenzako bega akuonyeshe njia, kabla hujapotea…..’akaambiwa
‘Mama,
mimi hayo nayafanyia kazi, kama kuna ukweli, nitafuata njia, lakini kwanza
mpaka nijua ukweli, maana njia nyingine ni mtihani, zimejengwa kiujanja-ujanja
kwa masilahi ya wajanja, badala ya kwenda pema, unaelekezwa kutumbukia kwenye
moto…’akasema Inspecta na mama akindoka, akasema;
‘Acha
mawazo hayo, …kumbuka raha na maisha mema unajipa wewe mwenyewe, hakuna wa
kukutafutia….kwaheri mwanangu kaa fikiria, jipange….’akaondoka.
**********
Mawazo
yake na mama mkwe, yalimfanya atulize kidogo kichwa, lakini mawazo hayo
yalipoisha kichwani, akawa bado hajapata usingizi, na alipoona hivyo, kuwa
hataweza kulala, akatoka kitandani na kuanza kuzunguka zunguka mle ndani, sijui
ni kitu gani kilimuambia achungulia mvungoni,
Akainama
na kuangalia mvunguni, aliona boksi ndogo ni kama vile viboksii wanaotumia watu
kuwekea pesa za mchezo,akainua godoro, na kukichukua kile kiboksi, mwanzoni
alijua ni mkewe aliweka kwa ajili ya kudunduliza pesa zake, maana kalikuwa
kazito.na kimefungwa na ufunguo.
‘Sijui
ufunguo wake upo wapi…?’ akajiuliza, akatafuta sana bila mafaniko, akasema;
‘Huenda
aliuweka mahali ili asihangaike kufungu mara kwa mara, lakni mpaka nijue humu
ndani kuna kitu gani…’akasema.
Akajaribu
kukafungua ikawa vigumu, akapanga akivunje, lakini akaona kuvunja ni kosa
huenda kuna vito vya thamani ambavyo mkewe aliweka, akakichukua na kwenda nacho
varandani, akakaa kwenye sofa, akiwazia afanye nini.
‘Hata
ni lazima nikifungue….’akasema, sasa akaenda jikoni na kuchukua pisipisi na
nyundo, akarudii na kuanza kazi ya kukivunja, ilichukua muda kidogo hadi
kikavunjika, na kufunguka.
Mle
ndani kulikuwa kweli na baadhi ya vito vya thamani, lakini pia kulikuwa na
bahasha mbili, na moja ilikuwa na vitufe vidogo sana kama vile vya kumbukumbu
kwenye simu(memory card), lakini ni vile vya hali ya juu, vinaweza kuweka
kumbkukmbu nyingi sana, zikiwemo picha za video.
Kabla
hajaamua kufanya lolote na vile vidude vya kumbukumbu, akafungua bahasha ya
pili, humo kulikuwa na picha, na hizo picha ndizo zilimfanya ashikwe na
mshituko, mshtuko, uliomfanya adondoshe hata lile boksi, akawa kama anaangalia
kitu cha kutisha.
Ilichukua
muda kutuliza kichwa chake, na baadaye akajipa moyo na kusema;
‘Labda
ni mapicha ya kubuni, haiwezekani, na kwaninialihifadhi hiyo picha, akainama na
kuzichukua zile picha na kuanza kuangalia, kwa makini, picha ya kwanza, ni ...
‘Oh,
haiwezekani…ina maana ..hapana…’akasema na kuanza kuangalia nyingine kama mtu
anayeangalia kitu kichafu, na mara akakutana na picha nyingine, akaona sura
yake, akasita,
‘Ina
maana mke wangu alijua….’akasema na kuiangalia ile picha, ni kweli ilikuwa
picha yake akiwa na mrembo jembe….
‘Kwanini,
naimefikaje hapa, tulikubaliana vipi na hawa watu…’akasema, akachukua simu yake
na kuanza kupiga, na ilichukua muda na kupokelewa, ..ilikuwa sauti ya mdada
Jembe
‘Wewe
vipi mbona unanipigia simu saa mbaya kama hizi…umeniharbia ndoto yangu nzuri,
unasemaje…..?’ akauliza
‘Tulikubaliana
nini, mbona kuna picha za ule uchafu wako, zimefika kwa mke wangu?’ akauliza.
‘Mbona
sikuelewi unaongea nini, subir tutaongea kesho, nitakuja kuziona, maana mimi
sizani kama hawa watu wanaweza kukusaliti, ni lazima kulikuwa na jambo,..una
uhakika na hilo?’ akauliza.
‘Ahadi
mumeanza kuivunja wenyewe, na kitakachofuata msije kunilaumu, nahisi kuna mengi
zaidi ya haya, nitahakikisha naisambaratisha hilo kundi, hilo nakuahidi
nilishapanga kufuata masharti, lakini kwa hili, …sitavumilia…’akasema.
‘Sikiliza
baby, hilo haliwezekani, huenda hiyo ni picha ya kupanga ilitengenezwa kwa
ajili ya kumuweka mke wako sawa, kuna watu walikuwa wakimtafuta mke wako labda
kwa ajili ya kupata siri zako, labda, kwa ajili ya kufanikiwa jambo, ndio
wakaamua kutumia picha yako, lakini haikutakiwa ibakie huko, nahisi kuna jambo…’akasema.
‘Mimi
sijui, waambie mabwana zako labda waniue,…labda nife mapema, lakini ni lazima
nitafanya kitu ambacho hawataweza kunisahau…’akasema.
‘Sikiliza
baby, kuwa na subira, tatizo lako una jaziba za kitoto, nikuambie ukweli,
unachotaka kupambana nacho sio kitu kidogo, ni dude, ….kwahiyo uwe makini,
nakuonya tena na tena, uwe makini, tuliza kichwa chako, jipange kama unataka
kufanya unachotaka kufanya, ila sizani kama utafika kokote…’akasema.
‘Tutaona, ….’akasema na kukata simu.
Akachukua zile picha zote na kuziweka kwenye
mtandao kwa kutumia komputa yake yenye uwezo huo, na kila alichokiona chenye
umuhimu akakidurufu na kukiweka kwenye mtandao, sasa akajipanga kuangalia vile
vidude viwili, ambavyo alitakiwa kuviweka ndani ya komputa yake ili aweze kuvisoma,
na kujua ni kitu gani.
Wakati anavichukua ndani ya ile bahasha, akahisi
mwili ukimsisimuka, akajua sasa hayupo peke yake. Akajuta kwanini alimruhusu
mlinzi kuondoka, mlinzi, aliomba ruhusa akisema ana matatizo ya kifamilia, yeye
hakuona kizuizi, maana mwenyewe yupo, na yeye mwenyewe ni askari.
Alipohisi hivyo, kitu kwanza kukifanya ni
kuvirudisha vile vidude (memory card) kwenye bahasha, na ile bahasha akairusha
juu ya kabati lake la nguo, na halafu akajifanya anaendelea kupekua, akilini,
na hisia zake za ziada zilimtuma kuwa kuna mtu, yupo karibu, mlangoni, au
dirishani.
Kwa haraka akatupo jicho dirishani, na
akashangaa, kuona lipo nusu wazi, hakumbuki kulifungua kabisa, akajiandaa kwa
lolote, akajuta kwanini hawajamrudishia bastola yake, humo ndani hakuwa na
silaha yoyote ya moto, zaidi ya visu vya kurusha, lakini vipo mbali, pale alipo
hakuwa na cha kujitetea, kama ikibidi.
Akaanza kuhesabu , moja mbili , tatu,
akasimama, lakini kabla hajafanya jambo, akahisi kitu kikichoma upande wake wa
kushoto,…sindani, iliyorushwa kama risasi, ilikuwa imetokea dirishani, hakuweza
hata kuigusa, ilifanya kazi mara moja, akahisi giza likitanda usoni….
WAZO LA LEO: Tukubali kuwa sote
wanadamu sio wakamilifu, kuwa kila mtu ana mapungufu yake, akikosea, tukikosea
tusameheane, hata hivyo, pia tukubali kukosoana, kurekebishana kwa amani na hekima ili tufikie malengo yetu,
kwa ajili ya maendeleo yetu.
Ni mimi:
emu-three
1 comment :
Akahisi giza limetanda usoni....sijui hapo kiliendelea nini...nashubiri. Pia wazo la la ni bonge la wazo ambalo wengi katika jamaii wanasahai..Tena ni bora zaidi palepale unapokosea kuomba msamaha...Ahsante
Post a Comment