Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 15, 2014

DUNIA YANGU-32Inspecta Moto alifika nyumbani kwake, na kushika kitasa, kuzungusha ili afungue mlango, mara mlinzi akaja nyuma yake na kusema;

‘Mkuu ngoja nkfungulie ufungua ninao mimi…’akasema na Inspecta akasogea pembeni na huyo mlinzi akafungua mlango wake, na yeye akaingia nyumbani kwake.
Upweke huzuni, vikaanza kumtawala,, japokuwa mwanzoni, alijitahidi kutokuliwazia hilo, lakini akili ya kibinadamu ikamjia, akaanza kuhisi upungufu fulani akilini na mwili ukaanza kuisha nguvu…

Akajitutumua, na kuingia ndani akaangaza huku na huku kwa haraka, halafu akaingia chumbani, hali ikaanza kubadilika zaidi, akaanza kuhisi upweke, huzuni, na kwa hali hiyo hakuweza kukaa hapo chumbani kwake, akatoka nje, na kukaa sebuleni, lakini baadaye akasimama alikumbuka jambo,akarudi chumbani;

Akaangaza macho huku na kule, lakini aliona chumba kipo kisafi, hakuna kitu cha kuweza kumsaidia, hakukata tamaa, akarudi tena sebuleni, akili ilikuwa haijawa safi, kuna kitu kinamsumbua,…

‘Ngoja….’akasema.

Japokuwa alijua kuwa polisi wameshafanya uchunguzi wao, na hataweza kupata chochote cha kumsaidia, lakini aliona ajaribu tena, safari hii akatoka nje kabisa, akazunguka zunguka nje, alifanya hivyo mara nyingi, baadaye akarudi ndani na safari hii, akawa anatembea kwa taratibu, akikagua kila sehemu hatua kwa hatua, na kwa muda huo haukujua anatafuta nini.

Alipofika chumbani,akakukumbuka jambo,… leso…

Akakumbuka siku ile, aliona leso ngeni karibu na kitanda, alipokumbuka hivyo, akaona kuna kitu anatakiwa kukifanya kwanza,

Akasogea kwenye kabati lake na kuchukua mfuko wa plastiki , ni mifuko maalumu ya kuweka vidhibiti vya polisi kwa ajili ya uchunguzi, alijua ataweza kuona kitu, na ni vyema kuvihifadhi kwenye chombo maalumu, akachukua na soksi za mikono, kwa tahadhari…

Akachuchumaa na kuangalia eneo la kitanda, kwa chini, akasema;

‘Nakumbuka hapa kulikuwa na leso hapa chini….’akasema na kuinama kuangalia, na kweli ile leso ilikuwa imesogezwa na kuzama chini ya mguu wa kitanda, kwa uangalifu akaitoa na kuweka kwenye huo mfuko maalumu wa plastiki.

Akaendelea hivyo hivyo, na kila alichokiona kipya kwenye chumba chake akakiweka kwenye huo mfuko, halafu akaelekea chooni na bafuni, huko kulikuwa kumesafishwa, na harufu ya madawa ilitapaa kila mahali, ilionekana walihakikisha hakuna kitu kinachobakia,…akafika kwenye beseni la kuogea,…

Alipofika hapo akashindwa kuvumilia, maana akili yake ilikumbuka lile tukio lililopita, hapo akachuchumaa na kuanza kulia, alilia kwa muda mrefu, na alishitushwa na mtu akimgusa begani.

‘N-nani wewe…?’ akauliza na kusimama kwa hasira

‘Rafiki yangu, usisononeke sana, najua hii hali inachukua muda kuondoka kichwani, lakini yote yakubali kama ni mapenzii ya mungu….’sauti ikasema, na hapo akasimama na alitaka kumvamia huyo jamaa na kumfanya kitu kibaya, lakini akakumbuka masharti, akageuka na kuangalia lile beseni la kuogea

‘Unajua rafiki yangu, hata mimi kuna muda hali hiyo inanijia na huwa nalia sana,…nalia sana maana shemeji nilimzoea sana, alikuwa kama dada yangu , mshauri wangu mkubwa, kuna muda nakorofishana na mke wangu, lakini nikikutana na mkeo, natapata maneno ya hekima, ..na kuyasahau yote….namrudia mke wangu kama hakuna lililotokea….’akasema

‘Naomba uondoke…’akasema Moto.

‘Nitaondoka tu, nimekuja mara moja, kwanza kuhakikisha usalama wako, hali yako, na kama kuna lolote naweza kukusaidia…’akasema Maneno.

‘Hakuna cha kunisaidia, nahitahi muda wa kukaa peke yangu…..’akasema

‘Najua, nafahamu sana,…lakini mimi ni rafiki yako, ujue haya yote ya kuhakikisha unatoka jela, na hatima ya kesi hii, ni mimi nimejitolea, kwa ajili ya urafiki wetu….’akasema

‘Nashukuru, kama sio kwa masilahi fulani…hata hivyo, sizani kama hili litapia hivi hivi…’akasema.

‘Kwahiyo unataka kufanya nini, kumbuke niliyokuambia, usije ukajifanya kichwa ngumu, nakuhakikishia utakuja kujuta, na …sijui, labda kama hujui hatari ya hao watu…’akasema

‘Ndio maana nataka uondoke, …sitaki kuwa na mtu hapa kwa hivi sasa…’akasema

‘Sawa,…upendavyo……‘akasema Maneno

‘Leo sitaki kukutana na mtu, nimemwambia hata mlinzi hapo nje, sijui kwanini umeingia?’ akauliza.

‘Samahani nimeingia kwa nguvu, nimemwambia nataka kuhakikisha kuwa upo salama, na kuhakikisha pia mambo mengine yanakwenda kama tulivyokubaliana…’akasema.

‘Leo sitaki kuongea na mtu naombeni mnielewe…samahani sana, sio nakufukuza lakini inabidi … nakuomba uondoke, leo ni siku ambayo nakumbuka mengi, na sitaki kuongea lolote, moyoni nina hasira…ninaweza kufanya jambo bay asana, nakuomba uondoke…..’akasema huku akikunja ngumi kwa hasira.

‘Ni sawa lakini lililonifanya nije hapa ni kukupa habari njema….’akasema Maneno.

‘Habari gani?’ akauliza Moto , sasa akikunjua ngumi aliyokuwa ameanza kuikunja.

‘Uchunguzi umekamilika, na mambo yamekwenda vizuri, ushahidi uliopatikana umethibitisha kuwa kweli mke wako alijiua, na hata hakimu kakubaliana na huo ushahidi, hata ndugu wa mkeo,…mama mzazi wa mkeo wako, amekubaliana na huo uchunguzi…’akasema.

‘Hata mama mzazi kakubaliana na huo ushahidi wenu, haiwezekani mumeonana naye lini ?’ akauliza.

‘Sasa hivi nimetoka kwake, na mara nyingi nakutana naye, nikimpa maendeleo ya uchunguzi wetu, na sasa kaamini, na ndio maana anataka kuja hapa kukuomba msamaha, kwa dhana yake dhidi yako…..’akasema.

‘Ipo siku ukweli utagundulikana tu….’akasema.

‘Ni mpaka, kama kuna ukweli mwingine ambao mimi siujui, ila ukweli halisi ndio huo….’akasema na Moto akawa akimiya kwa muda na mwenzake alipoona kuna huo ukimiya akasema;

‘Ni hilo tu nililokuja kukuambia na mimi nakushauri, ni vyema kuanzaia sasa ukaanza kujipanga upya, uwe kama mimi sahau yote yaliyopita,ujue katika haya maisha, hakuna anayepoteza muda kuangalia jinsi ya maendeleo ya mwenzake, kila mmoja yupo katika maisha yake, maendeleo yake binafsi, hata ndugu…sembuse mtu baki, jaribu kujiangalia wewe mwenyewe kwanza….utafanikia..’akasema.

‘Wewe unasema tu, hujafiwa, hasa na mtu ambaye ndiye ubavu wako…we sikia tu kwa wengine, hilo kwangu halitaisha hivi hivi, mpaka nijirizishe, bado nahisi kuna jambo, sizani, kama mke wangu alijiua mwenyewe….’akasema.

‘Sasa utafanyeje, ni hali halisi ndio hiyo, na kiukweli imeshatokea hivyo, huna la kufanya, au sasa unataka kufanya nini, ujiue na wewe, kama unaona hiyo ndio njia rahisi basi jiue, unafikiri ukifanya hivyo utaipunguzia nini dunia, kila siku watu wanazaliwa, wanakufa, wanazaliwa…au una mipango gani?’ akauliza.

‘Moyo wangu unglitulia, kama ningeligundua ukweli wa hili jambo, na kama kuna wau wapo nyuma ya hili, waweze kufikishwa mbele ya sheria…’akasema.

‘Basi nikaushauri hivi, nenda kwa hakimu ukasema wewe ndiye uliyemuua, ili mambo yaishe, au ?’ akawa kama anauliza.

‘Mimi sijamuua mke wangu, hilo lilipangwa, na kama lilipangwa, nataka kujua kwanini, na kama kuna mtu kamuua mke wangu nataka ajulikane ni nani, na sababu, mimi nina imani kuwa kweli mke wangu hakujiua, na kwa vile nimesingiziwa mimi kwa mipango maalumu, ni muhimu kumpata muuaji wa kweli ni nani, na kwanni wanisingizie mimi, huoni hapo kuna jambo limejificha, huoni ni sababu ya mimi kukubaliana na hayo matakwa yao…’akasema Moto.

‘Hilo unasema wewe kujikosha, lakini hakuna haja ya kuhangaika tena, hayo mambo yamekwisha, wewe sio muuaji tena kama ilivyozaniwa, muhimu ni kujipanga kwa jinsi inavyotakiwa, ila hapo nakukunya, na mhimu uwe makini , maana kila hatua , kila unachofanya kinachunguzwa, ukionekana unakwenda kinyume cha makubaliano huwezi kuamini yatakayofuata baadaye…’akasema.

‘Kutoka kwa nani?’ akauliza.

‘Kwa hao waliokusaidia…’akasema

‘Akina nani?’ akauliza

‘Hivi hapo kuna umuhimu kweli wa kutaka kuwajua hao waliokusaidia….?’ Akawa kama anauliza, na kabla hajapata jibu akasema

‘Cha muhimu kwa sasa ni kushukuru kuwa wewe sasa upo huru, huna kosa, unahitajia nini tena?’ akauliza, na aliposema hivyo, Inspecta akakumbuka jinsi alivyoletewa hiyo taarifa akiwa mahabusu, kuwa dhamana yake imekubaliwa.

***********

Inspecta akiwa kaduwaa, kajichokea, akakaa chini na kujiegemeza ukutani, na ghafla akahisi usingizi ukimjia;

Sauti anayoitambua vyema ikamuambia;

‘Mume wangu usisononeke sana, haya yote yana mwisho..’sauti ikamuambia, na akajaribu kuinua uso, kuona ni nani anayemuelezea hayo maneno, na taswira akiwa mahali, wapo mahali, na mkewe mara yupo mbele yake, wakati mwingine wamekaa, lakni haonyeshi ni wapi.

‘Mke wangu, wewe hujui ni nini kinachoendelea, dunia hii ni ngumu na ina mambo magumu, yasiyoelezeka…’akasema

‘Najua,…na sasa najua hata usiyoyajua, lakini vyovyote ufanyavyo, ujue kuwa kuna leo na kesho, hata uhangaike vipi, ujue kuna siku mimi na wewe hatutakuwa pamoja…’akasema mkewe.

‘Kwanini unasema hivyo…?’ akaumuuliza na kujaribu kumuangalia mkewe, lakini uso wa mkewe ukawa hauonekani, alikuwa kainama na baadaye akainua uso na kuangalia mbele, hakuangalia muelekeo wa mumewe, kama vile hataki mume wake amuangalie usoni.

‘Ni kuthibitisha kuwa vyovyote tufanyavyo, hatujui hatima ya kesho, kwahiyo kila linapotokea jambo mshukuru mungu wako,…yeye ndiye mwenye neema, yeye ndiye anajua hatima ya kesho…je wewe unajua kesho kutatokea nini…hujui,lakini mola wako anajua…..’akasema

‘Ni kweli..lakini ina maana tusihangaike kutafuta ukweli jambo likitokea?’ akauliza na mkewe akaonekana kama anatabasamu; na kusema

‘Kama ukweli upo utajulikana tu…cha muhimu ni kutokuushinikiza , kwani ukitumia nguvu sana utaumia mwenyewe, na kwa namna hiyo unaweza hata kushindwa kuupata  huo ukweli wenyewe, wapo watu wanatafuta mwanya wa kila hali, wanaangala kasoro zako, makosa yako kwao ni sababu ya kukuharibu, muhimu sana, wewe tuliza kichwa, tumia hekima, na mwisho wa kila jambo utafika, kwaheri…’akasema mkewe

‘Kwaheri kwani unakwenda wapi?’ akauliza akitaka kumshika mkewe asiondoke karibu yake lakini hakuweza kuinua mkono wake, ilikuwa kama viungo hivyo havipo

‘Nakwenda kuupumzika…’akasema, na alipojaribu kujikakamua ainuke amshke mkewe asiondoke, sauti ikasikika kigonga mahali,…oooh

Inspecta akashtuka, kumbe alikuwa akiota, akapangusa uso, na kuangalia huku na huko kama anamtafuta mkewe, na wakati huo moyo wake ulikuwa ukimuenda mbio, akasimama, na mara akasikia sauti ikisema;

‘Moto, unaitwa kwa mkuu….’akaambiwa

Akageuka sauti ilipotokea, akamuona askari akiwa kashika kirungu, kumbe yeye ndiye aliyegonga ule mlango wa geti, akamuangalia yule askari, bado akiwaza kuhusu ile ndoto.

‘Twende….’akasema yule askari, huku akifungua geti la chumba chake, na Inspecta hakuwa na kipingamizi,  akatoka na kumfuata huyo askari mlinzi kwa nyuma, na alipofika kwa huyo mkuu, hakuambiwa mengi aliyoambiwa, zadi ya kuambiwa kuwa dhamana yake imekubaliwa, na akapewa mashart ya dhamana kwa mujibu wa sheria…’akaambiwa

‘Kwahiyo, unataka kusema nini?’ akauliza kwa sauti ya kutoamini hayo anayoambiwa

‘Upo huru kuondoka…kama unahitaji kujiandaa, rudi sehemu yako kajiandae, ama kama upo tayari, unaweza kuondoka sasa hivi….’akaambiwa.

Inspecta hakutaka hata kurudi mahabusu, akatoka na kuelekea nje na alipotoka tu nje mara akaja mtu mmoja na kumwambia kuna gari linamsubiri kumpeleka nyumbani kwake, hakutaka hata kuuliza gari hilo kaleta nani, akaingia kwenye hilo gari na kufikishwa nyumbani kwake…

************

‘Kwangu mimi cha muhimu ni kujua ukweli…nahitaji kuujua ukweli, ni nani alimuua mke wangu,…’akasema akiendelea kuongea na Inspecta mwenzake.

‘Kwahiyo wewe huamini kuwa mkeo kajiua mwenyewe?’ akaulizwa

‘Siamini, hata wewe huamini hilo, …yoyote hawezi kuamini hilo, ndio maana nikakamatwa mimi, kwa hisia za kuwa nimemuua mke wangu, haya ya kujiua mwenyewe yamekuja baadaye, je nitaamini kivipi….’akasema

‘Sasa mimi nakuambia kama rafiki yako, kiukweli mke wako alijiua mwenyewe, kukamatwa kwako ilikuwa ni moja ya kukuweka sawa,…japokuwa dhamira ya ililenga utumiwe mwanya huo, kama hutakubaliana, basi uwajibike kama muuaji,…na kama tusingelikusaidia, ungehukukumiwa kama muuaji, lakini sasa ukweli wenyewe wa jinsi ilivyokuwa umefichuluwa, na kuwekwa wazi, kiukweli mke wako alijiua mwenyewe….’akasema

‘Umayajuaje hayo, kama sio mipango yenu mipya?’ akauliza

‘Sikiliza Moto, kila kitu kilichokuwa kikifanyika hapa kwako kilikuwa kinajulikana, hilo nakupa kama siri, lakini pale ulipokubaliana kuwa upo tayari kukubali na kushirikiana, basi hali hiyo ya kumulikwa kila mahali ikaondolewa,…sasa tukio zima la mke wako kufika hapa hadi kujiua lipo,…ila wewe hutaonyeshwa, kwa usalama wako….maana inatisha…’akasema

‘Kwa vipi?’ akaulizwa

‘Sababu za kuchukia, kuogopa kudhalilika hadi kufikia kujiua,….mmh ni vyema usione kabisa, itakuumiza sana, mimi mwenyewe nimeumia sana moyoni, lakini nitafanyaje,…wewe ni rafiki yangu, niamini haya ninayokuambia, na ukubali hivyo, kwanii ndivyo ilivyo….’akatulia kidogo kama anawaza jambo halafu akasema;

‘Kwahiyo hata wenzangu tulioshirikiana kuupata huo ushahidi wameonelea hivyo kuwa wewe ufahamu hivyo tu, kuwa mke wako alijiua mwenyewe,inatosha, ukitaka kupekenyua kuwa ilikuwaje, hutafanikiwa na hata kama ungefanikiwa, utasononeka maisha yako yote, nakushauri ni bora iwe hivyo, na amini hivyo….’akasema

‘Inaonekana kuna mengi ambayo siyajui, na huenda hata wewe unahusika kwa namna moja au nyingine, na hutaki nifahamu au sio….’akasema

‘Ngoja nikuache, maana umechoka, unahitaji kupumzika, na kupumisha kichwa chako, kwaheri, tutaonana ukiwa tayari…’akasema Inspecta Moto, na usoni alionekana kujawa na huzuni, akawa anatembea huku kaangalia chini, na alipofika mlangoni akasema

‘Jiandae mama mkwe wako anaweza kufika hapa kwako leo, na kama hutaki muonane naye leo useme, mimi nitawasiliana naye aje kesho….’akasema

‘Nitaonana naye hata leo…ila mimi sijarizika na hayo uliyoniambia, ukumbuke wewe ni rafiki yangu tumetoka mbali, lakini kama nitakuja kugundua kuwa unahusika na haya yote, hasa kwa kifo cha mke wangu, sitajali kabisa kuwa tulikuwa marafiki…’akamuangalia mwenzake na wakawa wanaangalia, na akiwa kakunja uso wa hasira akaendelea kuongea

‘Kama unahusika, nitahakikisha ni jino kwa jino…unanielewa, nitalipa kisasi ambacho hutaweza kuamini…hujui ni kiasi ninavyoumia moyoni, nasema tena, ole wako, kama unahusika, ole wa hilo kundi…’akasema Moto, na Inspecta akabenua mdomo wa zarau na kusema;

‘Kumbuka ahadi na masharti kuzingatiwa, usije kujijutia baadaye, mimi nimetimiza wajibu wangu, nimekusaidia kama rafiki yangu, ili usije kuhukumiwa kwa kesi ya mauaji, sasa upo huru, lakini bado unachunguzwa, nikushauri kama rafiki yangu, unachotakiwa kwa sasa ni kujipanga, angalia maisha yako mbele, hayo mengine hayana umuhimu kwa sasa, utajipotezea muda wako bure….’akasema Maneno

‘Natumai kauli yangu umesikia, na unafahamu vyema nilivyo…’akasema Moto

‘Na mimi nakutahadharisha kuwa ukihini huo mkataba, yatakayotokea  mimi sitakuwepo….’akasema Inspecta Maneno, na Moto akawa kimiya, na baadaye Inspecta Maneno akasema;

‘Hata hivyo, karibu ndani ya ulimwengu wa kisasa, uione dunia ilivyo, hiyo ndio dunia ya kisasa, ya sayansi na tekinolojia, …’akatabasamu, na kuangalia chini, halafu akaendelea kusema;

‘Unajua kila mtu ana ndoto zake za kufanikisha maisha yake, na ingeliwezekana kwa jnsi akli za watu zilivyo, ni kama vile kila mtu ana dunia yake mwenyewe,..ni nadharia ya kufikirika, ila kwa hili nakuomba tushirkiane,kwani mmi nmekudhamni,… au sio, kwahiyo ninachoweza kukisema kwa sasa ni kukaribisha ndani ya  dunia yangu…’ akasema na kuondoka.

Inspecta akiwa katingwa na mawazo,hakujali alichokuwa akiongea mwenzake, lakini neno la mwisho llilotamkwa na Inspecta Maneno lilidumu kichwani mwake, na kujirudia rudia kichwani mwake,….dunia yangu, dunia yangu…mwishowe akasema;

‘Eti nini, Dunia yangu…!’


WAZO LA LEO: Ugumu wa jambo, raha na shida za jambo lolote alijuaye ni muhusika mwenyewe, ndio maana watu wengine hukimbilia kusema yule analalamika sana, yule hawezi kuvumilia. Lakini mpaka mtu anafikia kulalamika, kulia au kusema...., ujue keshafikwa, siri ya mtungu aijue kata.
Ni mimi: emu-three

No comments :