Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, September 12, 2014

DUNIA YANGU-31


 Hakimu alitaja kesi ya kifo cha mke wa Inspecta, ambaye kwa maelezo ya muendesha mashitaka, ni mke huyo kauwawa, na mshitakiwa amahusika, kwahiyi mshitakiwa akatakiwa kukubali au kukataa kosa, na kama ilivyotarajiwa mshitakiwa akakataa kosa, na kwa vile ulikuwa ni utangulizi tu, kesi ikapangwa tarehe rasmi ya siku ya kuanza kusikilizwa.

endelea na kisa chetu....

Watu hawakupendezewa na hali hiyo kabisa, wengi wakaanza kulalamika;

‘Mnaona hawa watu walivyo wajanja, wanachofanya ni kupoteza muda, ili haki ya marehemu isipatikane, kama mtu alisikika akitoa kauli hizo kuwa ataua, mbele za watu, na baadaye mauaji yametokea, na mtuhumiwa akakamatwa akiwa na kisu, kuna haja gani ya kutafuta ushahidi zaidi……’akalalamika ndugu mmoja upande wa marehemu.

‘Ni utaratibu wa kimahakama ni lazima ufuatwe,hawawezi kutaja kesi siku hiyo hiyo na kuanza kusikilizwa, kwani kila mtu ana haki haki…mshitakiwa ana haki yake kujitetea, na ndio maana mshitakiwa anaulizwa kama anakubali kosa au analikana kosa, akishatoa kauli yake, ndio hapo sasa kesi inaanza au hakimu kutoa hakimu kama mshitakiwa kakiri kosa….’akaeleweshwa huyo mtu.

‘Siku zote hizo hao watu walikuwa wapi,…mimi najua kinachotafutwa ni ili ionekane kuwa marehemu alijiua mwenyewe, wewe utaona tu…’akasema huyo mlalamikaji.

‘Yote yatabainika tu,…mahakama ndio sehemu haki inapopatikana, hata ikigeuzwa kinyume nyume, ipo siku itabainika tu….’akasema mwingine

‘Hiyo ilikuwa zamani, siku hizi haki inanunuliwa bwana, wewe unatuambia nini, kwani hao wasimamizi ni malaika , na wao wana shida zao vile vile…tusidanganyane hapa…’akasema mtu mwingine.

‘Lakini vyovyote iwavyo, watu watasikia, na ukweli utawekwa wazi, na kumbukumbu zitakuwepo kisheria, kama kuna tatizo, kesi inaweza kutajwa tena na tena..au kukata rufaa….muhimu ni kumbukumbu ziwepo kisheria…..’akasema mtu mwingine.

‘Dunia hii ionege hivi hivi,..wengine wanajifanya hawapo kabisa katika dunia yetu hii, wapo mbali ajabu kwa vile wana pesa, matajiri, wanauwezo, ni viongozi, ..hawajui kuwa yote hiyo ni mitihani, …ipo siku na yeye yatamkuta hayo, maana kifo hakina masikini au tajiri….’akalalamika mama mmoja, na watu wakatawanyika.

Wakati hayo yakiendelea, mshitakiwa alirudishwa mahabusu, hakutakiwa kupewa dhamana, kwa sababu nyingi zilizotajwa na hata kuongezea kwa kusema kuwa mshitakiwa ni mjanja anaweza kuharibu ushahidi, na pia wafiwa wana hasira lolote linaweza kutokea….

Hakimu akasema japokuwa mshitakiwa ana haki ya kupewa dhamana, lakini kwa kuangalia hali ya usalama wake, na mambo yanayoendelea hivi sasa, ameona ni bora mshitakiwa aendelee kuwa mahabusu, hadi hapo kesi yake itaposomwa tena.

Inspecta akaingia kwenye gari la wafungwa na kurudishwa mahabusu, na hakutaka kabisa kuongea na mtu, na alipofika mahabusu,kabla hajatulia mara akaitwa kuwa kuna mtu kaja kumtembelea,…

‘Ni nani tena, sihitajii kuongea na mtu….’akasema

‘Ni wakili wako…’akasema askari

‘Wakili wangu….sina ahadi ya kuonana na wakili wangu leo….’akasema

‘Kasema ni muhimu sana, kuna mambo muhimu yanahusu kesi yako…’akaambiwa, na Inspecta, akawa hana ujanja, akasimama na kutoka kuelekea sehemu ya wageni. Na alipofika hakmuona wakili wake, aliyemuona ni yule yule anayemrusha roho yake-mdada.

‘Ni wewe tena, kwanini unadanganya kuwa wewe ni wakili wangu?’ akauliza

‘Ni ili nipewe kibali cha kuongea nawe…na kuanzia sasa mimi ni wakili wako, au hujui kuwa mimi ni wakili..’akasema na kutoa kitambulisho, kinachoonyesha kuwa kweli yeye ni wakili.

‘Sasa kama wewe ni wakili, umesomea sheria, kwanini unafanya hayo huku ukijua kuwa hayo unayofanya ni makosa…?’ akaulizwa

‘Kila jambo lina sababu, na sio kila sababu inatakiwa kuwa wazi,…mambo mengine ynafanyika kwa sabau inabidi yafanyike,..’akasema na usoni hakuonekana na furaha.

‘Haya nambie umekuja kwa lipi?’ akauliza

‘Unakumbuka tuliongea nini kwenye kikao kilichopita….?’ Akaulizwa, Inspecta alipoulizwa hivyo akakumbuka maneno ya huyo mdada ambayo yalihitajia yeye kutoa jibu kuwa kweli kakubali wazo la hao watu, ili kesi hiyo ionekane kuwa mkewe alijiua mwenyewe,

Sikiliza kati ya watu wanaoweza kukuokoa katika hii kesi,…. mmojawapo ni mimi, mimi naweza kukiri mambo mengi sana, na yakaja kukusaidia, mwenyewe unafahamu hilo, na pia mimi ninaweza kukuangamiza nikitaka, na hakuna ushahidi wowote utakaoweza kukutetea kama nikiamua kufanya hivyo…kweli si kweli…

**********

Inspecta akasogea kwenye kiti na kukaa wakawa wanaangaliana na huyo mrembo, mrembo alikuwa na mawani usoni, akayavua, akatabasamu, halafu akasema;

‘Sasa twende kazini,…huu hapa ni mkataba kuwa mimi ni wakili wako….’akasema na kusogeza mbele ya Inspecta

‘Lakini…..’akaanza kujitetea, hata hivyo, akakatisha pale alipoona maandishi yaliyopo hayaendani na kauli ya huyo mdada, ilikuwa ni mkataba tofauti,..akausoma kwa haraka, na yaliyomo ni makubaliano kuwa kakubali watu binafsi wafanye uchunguzi, ili kubainika kifo cha mkewe, na uchunguzi uliofanyika, umegundua kuwa mkewe kajiua,…

‘Maana yake nini sasa?’ akauliza Inspecta

‘Kila kitu kipo wazi, wewe ulinipa hiyo kazi kama wakili wa kujitegemea, mimi nina ofisi yangu ya uchunguzi, tumefanya uchunguzi wetu na tumebaini kuwa kweli mkeo kafa kwa kujiua,….’akasema

‘Haaah, halafu ni nani atakubaliana na uchunguzi wenu, polisi wao wapo wapi, …?’akauliza

‘Umesahau kuwa wazo hilo limetoka kwa rafiki yako, au…usitake niongee kila kitu, cha muhimu ni kweka sahihi kuwa wewe ulikubaliana na sisi, na ofisi yangu, uchunguzi ukafanyika, na haya ndio maelezo ya uchunguzi wetu, na ushahidi upo hapa, kila kitu kipo wazi, hakuna mahakama inayoweza kupinga hili…’akasema

‘Sijakuelewa….’akasema Inspecta akifungua yale makabrasa yaliyokuwepo mbele yake, na miongoni mkwake akaona CD’ ndogo, iliyowekwa kwenye kimfuko cha palstiki, juu kumeandikwa,..yalitokea siku marehemu alipojiua….

‘Hii mumepatia wapi?’ akauliza

‘Ni kazi uliyotutuma,…humo kila kitu kipo wazi, mkeo, alitoka hotelini akiwa kalewa chakari, na alipofika nyumbani akaona picha, inayoonyesha kuwa wewe upo na mwanamke mwingine, bila kujua kuwa wewe upo kazini, yeye akachukulia hasira, akachukua kisu na kujiua….’akasema

‘Kirahisi hivyo…?’ akauliza Inspecta.

‘Mimi nimeeleza kirahisi hivyo, lakini ukiangalia huo ushahidi, una kila kitu, kuanzia moja hadi mwisho, kunaonyesha tabia ya mkeo, alivyojikuta yupo na ….wanaume, wakamuhadaa…..inabidi kila kitu hapo kiwe wazi kuhusu mkeo,….tunajua mengi kuhusu yeye, na alipokuja kugundua kuwa watu wanafahamu, ndio akaanza kunywa,..unaona eeh….’akasema

‘Sikiliza wewe mdada, nikuambie ukweli, wewe ndiye uliyenifikisha hapa, kama usingelikuwa ni wewe haya yote yasingelitokea, kwahiyo moja kwa moja nakuona kama muhusika wa mauaji ya mke wangu , japokuwa sio wewe uliyemchoma kisu…na hayo mnayotaka kufanya mimi sikubaliani nayo kabisa..’akasema Inspecta

‘Siwezi kukulaumu kwa hilo, hata kama ingelikuwa ni mimi, ningelifanya hivyo hivyo, ila twende mbele na turudi nyuma, mimi sikuwahi kukufuata kwako na kudai mapenzi, mimi sijawahi kukulazimisha kitu, na ukiona mara nyingi ukija, nakuwa kama najipendekeza kwako….ni ukweli usiopingika kuwa nafanya haya yote kwa vile nakupenda, lakini je mimi niliwahi kuja kwako….’akasema

‘Hiyo kauli yako ni ya kinafiki, unajua jamii itanielewa vipi, kuwa wewe ni hawara wangu, wewe ni nyumba ndogo yangu ambayo nilikuwa nayo hadi mke wangu akajua na kuanza kuelewa…unalifahamu hilo…au ndivyomlivyopanga iwe hivyo na lengo lenu lilikuwa hilo hilo ajie mwenyewe, na mlipoona hafanyi hivyo, mkaamua kumuua wenyewe…kweli si kweli?’ akauliza Inspecta.

‘Mkeo alikuwa na yake kichwani, hata kama isingelikuwa mimi, au wewe kukutana na mimi bado alikuwa na mawimbi yake kichwani, ungelichunguza hilo ungeligundua, kuna watu walishaanza kupandikiza fitina kwenye kichwa chake, na yeye bila kutafakari akaingia kichwa kichwa, alishakuwa na mahusiano na wanaume nje, wewe hilo hulijui lakini sisi tunajua na tuna ushahidi….’akasema

‘Ni nani kama sio kundi lenu waliofanya hilo , na mlimfanyia hivyo, ili muweze kupata mnayotaka, na mlifanyia hivyo kama mlivyonifanyia mimi…’akasema Inspecta.

‘Maswala ya kundi kiukweli mimi siyajui kwa saana, nayasikia kama unavyoyasikia wewe..ei kuna kundi, kwahiyo hilo mimi halinihusu, mimi kinachonihusu ni huu uchunguzi, na kama unataka kuthibitisha kuwa mkeo alikuwa anakusaliti, ushahidi huu hapa….’akasema

‘Usinidanganya kwa hilo…hata siku moja, usije kujidanganya kwangu kuwa wewe huhusiki moja kwa moja na hilo kundi, wewe ni mmojawapo na mshirika mkuu wa hilo kundi, na mipango mingi unaifahamu…sasa sijui nia yako ni nini, na sijui madhumuni yenu ni nini kutaka mimi nikubaliane na nyie…na hayo kwa mke wangu siwezi kuona ajabu, kwani mimi mumenifanyia nini, si hayo hayo…..’akasema.

‘Lakini haya tunayoyafanya ni kwa manufaa ya nani, je huoni kama tusipofanya hivyo, wewe moja kwa moja unakuwa ni muuaji, je utafanikiwa vipi kutafuta ukweli wa hilo jambo kama utaendelea kusota huku mahabusu, na utaupataje huo ushahidi wakati sisi tuna kila kitu, usijidanganye mpenzi wangu …’akasema

‘Kwani nia yenu ni nini  , hata tusema nimekubali wazo lenu, halafu iweje, kwa malipo gani nitakayowalipa, maana nijuavyo nyie hamna cha bure, ni lazima mna mipango yenu  , kuwa nikikubali hivyo, niwe ndani ya masharti yenu, …kama mlivyowafanyia wengine….’akasema
‘Hivi kwa hali ilivyo, una hali ya kupinga hili,…huna ujanja ni bora ukubali hilo, na uje ukubaliane na hayo masharti,kama nilivyokuambia, mimi nina karata zote za ushindi, nikitaka nakuangamiza,..lakini nakupenda siwezi kufanya hilo mpaka unilazimishe, ndio maana nimekuja kwako kuweka kila kitu wazi…’akasema
‘Kwahiyo kwa kifupi mnataka mimi nifanye nini?’ akauliza Inspecta
‘Mimi nataka kukusaidia, mimi najua sheria, naifahamu sana, …hutaamini, ndio maana nikatafutwa kwa kila njia, najua utauliza na nani,….watu tunafuta pesa, ukipata sehemu mtu anakulipa vizuri , basi unamfanyia kazi yake vyema, japokuwa awali sikupendezewa, lakini baadaye nikajiuliza hivi mimi nataka nini…
‘Sasa kutokana na hilo wazo, mimi kama mwansheria wako,..sio lazima niwe wakili wako, unaweza kutafuta wakili mwingine…mimi hapa nasimama kama mshauri wako kisheria,… kwa wao langu la rafiki yako yanafanana, basi tukaona tushirikiane na yeye, sasa hivi mwenzako yupo anakuhangaikia, kuhakikisha hakuna kizuizi, sio kazi ndogo, …’akasema
‘Lakini mimi sijakubaliana naye, kama anafanya anafanya kwa masilahi yake binafsi, na anajua yote haya mnayafanya kwa masilahi yenu, mna lengo lenu jingine…’akasema
‘Lengo ni kukusaidia wewe, maana tumeona huna hatia kihivyo, hata kama uliamua kumuua mke wako, lakini ni kwa hasira tu na kibanadamu inatokea,….’akasema
‘Nimefanya hayo mimi….msitake kunipandikizia madhambi, mimi sijaua, sijamuua mke wangu, hilo ni lenu mumelitunga ili iwe hivyo…na wewe ni chambo cha hayo yote…’akasema
‘Ndio , mimi ninekuwa chambo, sasa inaniuma sana, ndio maana nikaona nijitoe kimasomaso, liwalo liwe, huo ni ukweli kutoka moyoni kuwa nayafanya haya kwa ajili ya  mapenzi yangu kwako, lakini pili  mapenzi gani yasiyo na pesa, ….tutaishije huko mbele, watoto na familia yetu itaishije, ni lazima hilo nilifikirie, nikaona nisaidia yote, kwasababu hatujui mtizamo wa waajiri wako, wanaweza kukutema, au ukashushwa cheo…ili usiumie, ni lazima uwe na namna nyingine ya kujiendeleza…’akasema
‘Kwa vipi, unataka kusema nini?’ akauliza
‘Hayo utakuja kuyajua..angalia rafiki yako sasa hivi yupo wapi, hana shida tena, kajijua, na kajiaminisha, huku anawajibika, huku anajijenga, ni hali inayokubalika tu, hakuna sheria ya kukuzuia wewe kujiendeleza kwa miradi mingine…na hilo nataka nikusaidie pia…je kweli utapata wapi mwanamke anajitolea kihivyo,…una Bahati sana wewe…’akasema
‘Kama unataka kunisaidia kweli, mimi nataka wewe usimame mahakamani kuwa wewe kweli ndiye uliyeniingiza kwenye matatizo haya, ukaniwekea madawa ya kulevya, ili nifanya hayo yaliyotokea, na uwataja wahusika wote mahakamani, ukifanya hivyo nitajua kuwa kweli kauli yako ni ya ukweli….’akasema Inspecta.
‘Mimi naweza kufanya hayo yote, nipo tayari kusema hivyo, unavyotaka wewe, lakini kwanza ukubaliane na msharti yangu,…’akasema
‘Masharti gani?’ akauliza
‘Kwanza ukubali wazi, maana kimoyoni umeshakubali, ila unaogopa kuliweka wazi , kuwa kuanzia sasa mimi ni mchumba wako…maana nikisimama na kusema hivyo, unafikiri muajiri wangu atanikubalia tena,…hatanitaka tena, nitapoteza kazi, sasa nitakwenda kwa nani…unaliona hilo lilivyo…..’akatulia kidogo kama kutaka Inspecta aliweke hilo akilini
‘Jingine unalotaka kutoka kwangu ni nini?’ akauliza Inspecta
‘Ukubaliane na msharti yale niliyokuambia awali, ikibidi kwa vile polisi wamefikia hatua hiyo ya kukufunga, na hata hawana msaada na wewe tena, achana na kazi ya uaskari ufanya kazi nyingine..yenye masilahi kwako….unalionaje hilo, hata kama utaendela kuwepo, lakini punguza punguza,…uwajibikaji…’akasema
‘Sijaelewa sharti hilo, umesema kuwa ni yale uliyoniambia awali, ambayo nakumbuka ulisema kuwa nisijihusishe na uchunguzi wa kesi zinazoendelea huko kazini kwetu, niliwahi kukuuliza kesi gani, lakini hukutaka kuzitaja, sasa kama mimi ni muajiriwa wa polisi, nitakiwa nifanye nini, nikatae kazi za watu, sasa nitakuwa nimefanya nini.?’ Akauliza
‘Utandelea kufanya kazi yako kama kawaida, kama unataka kuendelea kuwa mtumwa wao, lakini huku ukisikiliza maagizo utakayopewa, …’akasema
‘Na akina nani?’ akauliza
‘Hilo ni sharti jingine, usijiingize au kutaka kujua zaidi, muhimu kwako ni kufanya yale unayotakiwa kufanya, na kuacha yale utakayaambiwa uache, sasa nani , na kwa vipi utaelekezwa …hilo lisikupe shida…’akasema
‘Je nikikataa mtafanya nini?’ akauliza
‘Unafahamu ni nini kitakachotokea, hebu angalia nje,…watu wanasemaje kuhusu wewe, hapo bado tu ushahidi wa uchafu wako haujawekwa magazetini, je ukiwekwa, unafikiri kutatokea, nini, na je ni nani atakuamini tena…fikiria kwa makini, kuanzia sasa itakuwa inabigwa dana dana, hadi kesi inafutwa, kama utakubaliana na hilo wazo…’akasema
‘Nimekuuliza kama nikikataa mtafanya nini, hayo kuhusu watu mimi siogopi, maana ukweli naujua mimi,….’akasema
‘Kama unatikisa kibiriti, sawa, ngoja tuone kesho itakavyokuwa, …’akasema akionekana hana raha.
‘Sikiliza nikuambie mimi hata kama nitakubaliana na matakwa yenu, ujue kuwa nimekubaliana kwa mdomo tu, sio kweli kuwa nitafanya hayo mnayotaka mimi nifanye, hilo sikufichi,…’akasema Inspecta
‘Muhimu ni wewe kukubali, hayo mengine tuachie sisi…wewe sio wa kwanza kusema hivyo, hata mimi mwenyewe niliwahi kusema hivyo, wapo waliosema hivo hivyo ,sasa wanakula bata kilaini, wananenepeana, wana kila kitu, wewe bwana, toka lini asali ikaonjwa mara moja, wewe toa jibu kuwa umekubali na huu ndio mkataba wa kuwa ulitupa sisi kazi….’akasema
‘Mkataba huu, mimi siwezi kukubaliana nao, kama nikikubali nakubali kwa maneno tu, siwezi kuwekeana maandiko na nyie, maana sitaweza kukaa kimiya, ni lazima nitafute ukweli wa hayo yote…’akasema
‘Ni lazima usaini mkataba huu kukubali kuwa sisi tumefanya uchunguzi wa kesi yako, nikuambie ukweli, wenzako sio wajinga,..natumai tuemelewana, weka sahihi yako hapa tumalizane, wewe unaogopa nini bwana, hakuna kipiya hapa..vinginevyo, sina jinsi mimi , itabidi nifuate wanayotaka wao, japokuwa nitaumia sana…’akasema
‘Haya nimekubali…’akasema Inspecta na kuchukua kalamu, kwanza akamuangalia mdada usoni, halafu, akafunua zile karatasi, akasoma soma weee…halafu akaanza kusaini, na alipomaliza akaweka kalamu juu ya ile karatasi, akasema
‘Haya nimefanya mnavyotaka, nini zaidi…’akasema Inspecta.
‘Kesho, kazi inaanza, kila kitu sasa kinageukia upande  mwingine…’akasema
‘Kugeukia upande mwingine , una maana gani?’ akauliza
‘Dunia inazunguka sio….jana ilikuwa wewe ni muuaji, kesho, itakwua mkeo alijiua yeye mwenyewe…au sio….’akasema na kusimama kuondoka.
‘Sawa fanyeni muonavyo nyie, ila …tutaona huko mbele…’akasema Inspecta.
‘Usijali ya huko mbele huwezi kuyajua, kwanza hili la leo…natumai tumeshaafikiana, na kuanzia sasa naweka silaha zangu tayari, ukikiuka hata sharti moja, mwenyewe utasikia mlio tu, kesho hili keshokutwa hili, mwenyewe utatamani kujiua…’akasema
‘Kama mlivyomuua mke wangu…’akasema
‘Hahahaha, nani kamuua mke wako, umemuua mkeo mwenyewe kwa mihasira yako, au unataka tulithibitishe hilo, ….kuanzia sasa sisi tumeshatengeneza mazingira kuhusu huo ukweli, iliyobakia ni wewe mwenyewe kuwajibika tu ..’akasema
‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza Inspecta
‘Vuta subira, usiharibu utamu, kwaheri mpenzi, uwe na amani, ujue kuwa kuna mtu anakujali wakati wote wa shida na raha…..’,akasema na kubusu kidole chake, na kukiweka mdomoni mwa Inspecta, Inspecta akageuka kukataa hicho kitendo, lakini kidole kilishagusa mdomo wa Inspecta.
‘By baby….’akasema na kuondoka kwa mwendo wa haraka haraka…
NB : Hayo ndiyo yalitokea kihivyo, sasa tuone kivingine itakuwaje
WAZO LA LEO: Siku hizi kuna mikataba mingi ya kiujanja ujanja, hasa makazini, kwa vile mtu kaja mikono nyuma ana shida ya kazi, basi atapewa mkataba uliojengwa kumkandamiza mfanyakazi bila hata yeye kujijua, kama una shida ya kazi utafanyeje, unakubaliana nao unaweka sahihi, kesho na kesho kutwa unaligundua hilo, ukilalamika, kazi huna.

Je ina maana ubwana na utwana umerejea,…Hili linatakiwa liwekwe wazi kuhusu haki za wafanyakazi, haki za waajiriwa, kikatiba, najua vipo vyama vya wafanyakazi,lakini sio makapuni yote yanawajibika kwao, nionavyo mimi kama kuna NSSF, PPF, PAYE, zinawajibishwa kwa muajiri, kwanini mazingira hayo hayo yasiwepo kwa kila muajiri, kuwa mikataba yote ya wafanyakazi ni lazima kwanza ipitie kwa vyama vya wafanyakazi…ni wazo langu la leo, kwa waheshimiwa wetu bungeni.
Ni mimi: emu-three

4 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Yaani kila ukipita hapa na kusoma hivi visa hamu haiishi ni raha sana na nampongeza sana mwandishi anafanya kazi nzuri sana ambayo jamii nzima ilibidi wasome

emuthree said...

Ndugu wangu Yasinta nashukuru sana kwa kunipa moyo wa kuendelea kuifanya kazi hii, japokuwa imejaa changamoto nyingi, lakini yote ni heri tupo pamoja

Christian Bwaya said...

Emu three, unafanya kazi nzuri sana. Nafuatilia kisa hiki na kujifunza mengi. Hongera sana!

emuthree said...

Nashukuru sana @Christian Bwaya, tupo pamoja