Hakimu alitaja kesi ya kifo cha mke wa Inspecta, ambaye kwa maelezo ya muendesha mashitaka, ni mke huyo kauwawa, na mshitakiwa amahusika, kwahiyi mshitakiwa
akatakiwa kukubali au kukataa kosa, na kama ilivyotarajiwa mshitakiwa akakataa kosa,
na kwa vile ulikuwa ni utangulizi tu, kesi ikapangwa tarehe rasmi ya siku ya
kuanza kusikilizwa.
endelea na kisa chetu....
Watu
hawakupendezewa na hali hiyo kabisa, wengi wakaanza kulalamika;
‘Mnaona
hawa watu walivyo wajanja, wanachofanya ni kupoteza muda, ili haki ya marehemu
isipatikane, kama mtu alisikika akitoa kauli hizo kuwa ataua, mbele za watu, na
baadaye mauaji yametokea, na mtuhumiwa akakamatwa akiwa na kisu, kuna haja gani
ya kutafuta ushahidi zaidi……’akalalamika ndugu mmoja upande wa marehemu.
‘Ni
utaratibu wa kimahakama ni lazima ufuatwe,hawawezi kutaja kesi siku hiyo hiyo
na kuanza kusikilizwa, kwani kila mtu ana haki haki…mshitakiwa ana haki yake
kujitetea, na ndio maana mshitakiwa anaulizwa kama anakubali kosa au analikana
kosa, akishatoa kauli yake, ndio hapo sasa kesi inaanza au hakimu kutoa hakimu
kama mshitakiwa kakiri kosa….’akaeleweshwa huyo mtu.
‘Siku
zote hizo hao watu walikuwa wapi,…mimi najua kinachotafutwa ni ili ionekane
kuwa marehemu alijiua mwenyewe, wewe utaona tu…’akasema huyo mlalamikaji.
‘Yote
yatabainika tu,…mahakama ndio sehemu haki inapopatikana, hata ikigeuzwa kinyume
nyume, ipo siku itabainika tu….’akasema mwingine
‘Hiyo
ilikuwa zamani, siku hizi haki inanunuliwa bwana, wewe unatuambia nini, kwani
hao wasimamizi ni malaika , na wao wana shida zao vile vile…tusidanganyane hapa…’akasema
mtu mwingine.
‘Lakini
vyovyote iwavyo, watu watasikia, na ukweli utawekwa wazi, na kumbukumbu
zitakuwepo kisheria, kama kuna tatizo, kesi inaweza kutajwa tena na tena..au
kukata rufaa….muhimu ni kumbukumbu ziwepo kisheria…..’akasema mtu mwingine.
‘Dunia
hii ionege hivi hivi,..wengine wanajifanya hawapo kabisa katika dunia yetu hii,
wapo mbali ajabu kwa vile wana pesa, matajiri, wanauwezo, ni viongozi,
..hawajui kuwa yote hiyo ni mitihani, …ipo siku na yeye yatamkuta hayo, maana
kifo hakina masikini au tajiri….’akalalamika mama mmoja, na watu wakatawanyika.
Wakati
hayo yakiendelea, mshitakiwa alirudishwa mahabusu, hakutakiwa kupewa dhamana,
kwa sababu nyingi zilizotajwa na hata kuongezea kwa kusema kuwa mshitakiwa ni
mjanja anaweza kuharibu ushahidi, na pia wafiwa wana hasira lolote linaweza
kutokea….
Hakimu
akasema japokuwa mshitakiwa ana haki ya kupewa dhamana, lakini kwa kuangalia
hali ya usalama wake, na mambo yanayoendelea hivi sasa, ameona ni bora
mshitakiwa aendelee kuwa mahabusu, hadi hapo kesi yake itaposomwa tena.
Inspecta
akaingia kwenye gari la wafungwa na kurudishwa mahabusu, na hakutaka kabisa
kuongea na mtu, na alipofika mahabusu,kabla hajatulia mara akaitwa kuwa kuna
mtu kaja kumtembelea,…
‘Ni
nani tena, sihitajii kuongea na mtu….’akasema
‘Ni
wakili wako…’akasema askari
‘Wakili
wangu….sina ahadi ya kuonana na wakili wangu leo….’akasema
‘Kasema
ni muhimu sana, kuna mambo muhimu yanahusu kesi yako…’akaambiwa, na Inspecta,
akawa hana ujanja, akasimama na kutoka kuelekea sehemu ya wageni. Na alipofika
hakmuona wakili wake, aliyemuona ni yule yule anayemrusha roho yake-mdada.
‘Ni
wewe tena, kwanini unadanganya kuwa wewe ni wakili wangu?’ akauliza
‘Ni
ili nipewe kibali cha kuongea nawe…na kuanzia sasa mimi ni wakili wako, au
hujui kuwa mimi ni wakili..’akasema na kutoa kitambulisho, kinachoonyesha kuwa
kweli yeye ni wakili.
‘Sasa
kama wewe ni wakili, umesomea sheria, kwanini unafanya hayo huku ukijua kuwa
hayo unayofanya ni makosa…?’ akaulizwa
‘Kila
jambo lina sababu, na sio kila sababu inatakiwa kuwa wazi,…mambo mengine
ynafanyika kwa sabau inabidi yafanyike,..’akasema na usoni hakuonekana na
furaha.
‘Haya
nambie umekuja kwa lipi?’ akauliza
‘Unakumbuka
tuliongea nini kwenye kikao kilichopita….?’ Akaulizwa, Inspecta alipoulizwa
hivyo akakumbuka maneno ya huyo mdada ambayo yalihitajia yeye kutoa jibu kuwa kweli
kakubali wazo la hao watu, ili kesi hiyo ionekane kuwa mkewe alijiua mwenyewe,
‘Sikiliza kati ya watu wanaoweza kukuokoa
katika hii kesi,…. mmojawapo ni mimi, mimi naweza kukiri mambo mengi sana, na
yakaja kukusaidia, mwenyewe unafahamu hilo, na pia mimi ninaweza kukuangamiza
nikitaka, na hakuna ushahidi wowote utakaoweza kukutetea kama nikiamua kufanya
hivyo…kweli si kweli…
**********
Inspecta
akasogea kwenye kiti na kukaa wakawa wanaangaliana na huyo mrembo, mrembo
alikuwa na mawani usoni, akayavua, akatabasamu, halafu akasema;
‘Sasa
twende kazini,…huu hapa ni mkataba kuwa mimi ni wakili wako….’akasema na
kusogeza mbele ya Inspecta
‘Lakini…..’akaanza
kujitetea, hata hivyo, akakatisha pale alipoona maandishi yaliyopo hayaendani
na kauli ya huyo mdada, ilikuwa ni mkataba tofauti,..akausoma kwa haraka, na
yaliyomo ni makubaliano kuwa kakubali watu binafsi wafanye uchunguzi, ili
kubainika kifo cha mkewe, na uchunguzi uliofanyika, umegundua kuwa mkewe
kajiua,…
‘Maana
yake nini sasa?’ akauliza Inspecta
‘Kila
kitu kipo wazi, wewe ulinipa hiyo kazi kama wakili wa kujitegemea, mimi nina
ofisi yangu ya uchunguzi, tumefanya uchunguzi wetu na tumebaini kuwa kweli mkeo
kafa kwa kujiua,….’akasema
‘Haaah,
halafu ni nani atakubaliana na uchunguzi wenu, polisi wao wapo wapi, …?’akauliza
‘Umesahau
kuwa wazo hilo limetoka kwa rafiki yako, au…usitake niongee kila kitu, cha
muhimu ni kweka sahihi kuwa wewe ulikubaliana na sisi, na ofisi yangu,
uchunguzi ukafanyika, na haya ndio maelezo ya uchunguzi wetu, na ushahidi upo
hapa, kila kitu kipo wazi, hakuna mahakama inayoweza kupinga hili…’akasema
‘Sijakuelewa….’akasema
Inspecta akifungua yale makabrasa yaliyokuwepo mbele yake, na miongoni mkwake
akaona CD’ ndogo, iliyowekwa kwenye kimfuko cha palstiki, juu
kumeandikwa,..yalitokea siku marehemu alipojiua….
‘Hii
mumepatia wapi?’ akauliza
‘Ni
kazi uliyotutuma,…humo kila kitu kipo wazi, mkeo, alitoka hotelini akiwa kalewa
chakari, na alipofika nyumbani akaona picha, inayoonyesha kuwa wewe upo na
mwanamke mwingine, bila kujua kuwa wewe upo kazini, yeye akachukulia hasira,
akachukua kisu na kujiua….’akasema
‘Kirahisi
hivyo…?’ akauliza Inspecta.
‘Mimi
nimeeleza kirahisi hivyo, lakini ukiangalia huo ushahidi, una kila kitu,
kuanzia moja hadi mwisho, kunaonyesha tabia ya mkeo, alivyojikuta yupo na ….wanaume,
wakamuhadaa…..inabidi kila kitu hapo kiwe wazi kuhusu mkeo,….tunajua mengi
kuhusu yeye, na alipokuja kugundua kuwa watu wanafahamu, ndio akaanza
kunywa,..unaona eeh….’akasema
‘Sikiliza
wewe mdada, nikuambie ukweli, wewe ndiye uliyenifikisha hapa, kama usingelikuwa
ni wewe haya yote yasingelitokea, kwahiyo moja kwa moja nakuona kama muhusika
wa mauaji ya mke wangu , japokuwa sio wewe uliyemchoma kisu…na hayo mnayotaka
kufanya mimi sikubaliani nayo kabisa..’akasema Inspecta
‘Siwezi
kukulaumu kwa hilo, hata kama ingelikuwa ni mimi, ningelifanya hivyo hivyo, ila
twende mbele na turudi nyuma, mimi sikuwahi kukufuata kwako na kudai mapenzi,
mimi sijawahi kukulazimisha kitu, na ukiona mara nyingi ukija, nakuwa kama
najipendekeza kwako….ni ukweli usiopingika kuwa nafanya haya yote kwa vile
nakupenda, lakini je mimi niliwahi kuja kwako….’akasema
‘Hiyo
kauli yako ni ya kinafiki, unajua jamii itanielewa vipi, kuwa wewe ni hawara wangu,
wewe ni nyumba ndogo yangu ambayo nilikuwa nayo hadi mke wangu akajua na kuanza
kuelewa…unalifahamu hilo…au ndivyomlivyopanga iwe hivyo na lengo lenu lilikuwa
hilo hilo ajie mwenyewe, na mlipoona hafanyi hivyo, mkaamua kumuua wenyewe…kweli
si kweli?’ akauliza Inspecta.
‘Mkeo
alikuwa na yake kichwani, hata kama isingelikuwa mimi, au wewe kukutana na mimi
bado alikuwa na mawimbi yake kichwani, ungelichunguza hilo ungeligundua, kuna
watu walishaanza kupandikiza fitina kwenye kichwa chake, na yeye bila
kutafakari akaingia kichwa kichwa, alishakuwa na mahusiano na wanaume nje, wewe
hilo hulijui lakini sisi tunajua na tuna ushahidi….’akasema
‘Ni
nani kama sio kundi lenu waliofanya hilo , na mlimfanyia hivyo, ili muweze
kupata mnayotaka, na mlifanyia hivyo kama mlivyonifanyia mimi…’akasema
Inspecta.
‘Maswala
ya kundi kiukweli mimi siyajui kwa saana, nayasikia kama unavyoyasikia wewe..ei
kuna kundi, kwahiyo hilo mimi halinihusu, mimi kinachonihusu ni huu uchunguzi,
na kama unataka kuthibitisha kuwa mkeo alikuwa anakusaliti, ushahidi huu hapa….’akasema
‘Usinidanganya
kwa hilo…hata siku moja, usije kujidanganya kwangu kuwa wewe huhusiki moja kwa
moja na hilo kundi, wewe ni mmojawapo na mshirika mkuu wa hilo kundi, na
mipango mingi unaifahamu…sasa sijui nia yako ni nini, na sijui madhumuni yenu
ni nini kutaka mimi nikubaliane na nyie…na hayo kwa mke wangu siwezi kuona
ajabu, kwani mimi mumenifanyia nini, si hayo hayo…..’akasema.
‘Lakini
haya tunayoyafanya ni kwa manufaa ya nani, je huoni kama tusipofanya hivyo,
wewe moja kwa moja unakuwa ni muuaji, je utafanikiwa vipi kutafuta ukweli wa
hilo jambo kama utaendelea kusota huku mahabusu, na utaupataje huo ushahidi
wakati sisi tuna kila kitu, usijidanganye mpenzi wangu …’akasema
‘Kwani
nia yenu ni nini , hata tusema
nimekubali wazo lenu, halafu iweje, kwa malipo gani nitakayowalipa, maana
nijuavyo nyie hamna cha bure, ni lazima mna mipango yenu , kuwa nikikubali hivyo, niwe ndani ya
masharti yenu, …kama mlivyowafanyia wengine….’akasema
‘Hivi
kwa hali ilivyo, una hali ya kupinga hili,…huna ujanja ni bora ukubali hilo, na
uje ukubaliane na hayo masharti,kama nilivyokuambia, mimi nina karata zote za
ushindi, nikitaka nakuangamiza,..lakini nakupenda siwezi kufanya hilo mpaka
unilazimishe, ndio maana nimekuja kwako kuweka kila kitu wazi…’akasema
‘Kwahiyo
kwa kifupi mnataka mimi nifanye nini?’ akauliza Inspecta
‘Mimi
nataka kukusaidia, mimi najua sheria, naifahamu sana, …hutaamini, ndio maana
nikatafutwa kwa kila njia, najua utauliza na nani,….watu tunafuta pesa, ukipata
sehemu mtu anakulipa vizuri , basi unamfanyia kazi yake vyema, japokuwa awali
sikupendezewa, lakini baadaye nikajiuliza hivi mimi nataka nini…
‘Sasa
kutokana na hilo wazo, mimi kama mwansheria wako,..sio lazima niwe wakili wako,
unaweza kutafuta wakili mwingine…mimi hapa nasimama kama mshauri wako kisheria,…
kwa wao langu la rafiki yako yanafanana, basi tukaona tushirikiane na yeye,
sasa hivi mwenzako yupo anakuhangaikia, kuhakikisha hakuna kizuizi, sio kazi
ndogo, …’akasema
‘Lakini
mimi sijakubaliana naye, kama anafanya anafanya kwa masilahi yake binafsi, na
anajua yote haya mnayafanya kwa masilahi yenu, mna lengo lenu jingine…’akasema
‘Lengo
ni kukusaidia wewe, maana tumeona huna hatia kihivyo, hata kama uliamua kumuua
mke wako, lakini ni kwa hasira tu na kibanadamu inatokea,….’akasema
‘Nimefanya
hayo mimi….msitake kunipandikizia madhambi, mimi sijaua, sijamuua mke wangu,
hilo ni lenu mumelitunga ili iwe hivyo…na wewe ni chambo cha hayo yote…’akasema
‘Ndio
, mimi ninekuwa chambo, sasa inaniuma sana, ndio maana nikaona nijitoe kimasomaso,
liwalo liwe, huo ni ukweli kutoka moyoni kuwa nayafanya haya kwa ajili ya mapenzi yangu kwako, lakini pili mapenzi gani yasiyo na pesa, ….tutaishije huko
mbele, watoto na familia yetu itaishije, ni lazima hilo nilifikirie, nikaona
nisaidia yote, kwasababu hatujui mtizamo wa waajiri wako, wanaweza kukutema, au
ukashushwa cheo…ili usiumie, ni lazima uwe na namna nyingine ya kujiendeleza…’akasema
‘Kwa
vipi, unataka kusema nini?’ akauliza
‘Hayo
utakuja kuyajua..angalia rafiki yako sasa hivi yupo wapi, hana shida tena,
kajijua, na kajiaminisha, huku anawajibika, huku anajijenga, ni hali
inayokubalika tu, hakuna sheria ya kukuzuia wewe kujiendeleza kwa miradi
mingine…na hilo nataka nikusaidie pia…je kweli utapata wapi mwanamke anajitolea
kihivyo,…una Bahati sana wewe…’akasema
‘Kama
unataka kunisaidia kweli, mimi nataka wewe usimame mahakamani kuwa wewe kweli
ndiye uliyeniingiza kwenye matatizo haya, ukaniwekea madawa ya kulevya, ili
nifanya hayo yaliyotokea, na uwataja wahusika wote mahakamani, ukifanya hivyo
nitajua kuwa kweli kauli yako ni ya ukweli….’akasema Inspecta.
‘Mimi
naweza kufanya hayo yote, nipo tayari kusema hivyo, unavyotaka wewe, lakini kwanza
ukubaliane na msharti yangu,…’akasema
‘Masharti
gani?’ akauliza
‘Kwanza
ukubali wazi, maana kimoyoni umeshakubali, ila unaogopa kuliweka wazi , kuwa
kuanzia sasa mimi ni mchumba wako…maana nikisimama na kusema hivyo, unafikiri
muajiri wangu atanikubalia tena,…hatanitaka tena, nitapoteza kazi, sasa
nitakwenda kwa nani…unaliona hilo lilivyo…..’akatulia kidogo kama kutaka
Inspecta aliweke hilo akilini
‘Jingine
unalotaka kutoka kwangu ni nini?’ akauliza Inspecta
‘Ukubaliane
na msharti yale niliyokuambia awali, ikibidi kwa vile polisi wamefikia hatua
hiyo ya kukufunga, na hata hawana msaada na wewe tena, achana na kazi ya
uaskari ufanya kazi nyingine..yenye masilahi kwako….unalionaje hilo, hata kama
utaendela kuwepo, lakini punguza punguza,…uwajibikaji…’akasema
‘Sijaelewa
sharti hilo, umesema kuwa ni yale uliyoniambia awali, ambayo nakumbuka ulisema
kuwa nisijihusishe na uchunguzi wa kesi zinazoendelea huko kazini kwetu,
niliwahi kukuuliza kesi gani, lakini hukutaka kuzitaja, sasa kama mimi ni
muajiriwa wa polisi, nitakiwa nifanye nini, nikatae kazi za watu, sasa nitakuwa
nimefanya nini.?’ Akauliza
‘Utandelea
kufanya kazi yako kama kawaida, kama unataka kuendelea kuwa mtumwa wao, lakini
huku ukisikiliza maagizo utakayopewa, …’akasema
‘Na
akina nani?’ akauliza
‘Hilo
ni sharti jingine, usijiingize au kutaka kujua zaidi, muhimu kwako ni kufanya
yale unayotakiwa kufanya, na kuacha yale utakayaambiwa uache, sasa nani , na
kwa vipi utaelekezwa …hilo lisikupe shida…’akasema
‘Je
nikikataa mtafanya nini?’ akauliza
‘Unafahamu
ni nini kitakachotokea, hebu angalia nje,…watu wanasemaje kuhusu wewe, hapo
bado tu ushahidi wa uchafu wako haujawekwa magazetini, je ukiwekwa, unafikiri
kutatokea, nini, na je ni nani atakuamini tena…fikiria kwa makini, kuanzia sasa
itakuwa inabigwa dana dana, hadi kesi inafutwa, kama utakubaliana na hilo
wazo…’akasema
‘Nimekuuliza
kama nikikataa mtafanya nini, hayo kuhusu watu mimi siogopi, maana ukweli
naujua mimi,….’akasema
‘Kama
unatikisa kibiriti, sawa, ngoja tuone kesho itakavyokuwa, …’akasema akionekana
hana raha.
‘Sikiliza
nikuambie mimi hata kama nitakubaliana na matakwa yenu, ujue kuwa nimekubaliana
kwa mdomo tu, sio kweli kuwa nitafanya hayo mnayotaka mimi nifanye, hilo
sikufichi,…’akasema Inspecta
‘Muhimu
ni wewe kukubali, hayo mengine tuachie sisi…wewe sio wa kwanza kusema hivyo,
hata mimi mwenyewe niliwahi kusema hivyo, wapo waliosema hivo hivyo ,sasa
wanakula bata kilaini, wananenepeana, wana kila kitu, wewe bwana, toka lini
asali ikaonjwa mara moja, wewe toa jibu kuwa umekubali na huu ndio mkataba wa
kuwa ulitupa sisi kazi….’akasema
‘Mkataba
huu, mimi siwezi kukubaliana nao, kama nikikubali nakubali kwa maneno tu,
siwezi kuwekeana maandiko na nyie, maana sitaweza kukaa kimiya, ni lazima
nitafute ukweli wa hayo yote…’akasema
‘Ni
lazima usaini mkataba huu kukubali kuwa sisi tumefanya uchunguzi wa kesi yako, nikuambie
ukweli, wenzako sio wajinga,..natumai tuemelewana, weka sahihi yako hapa
tumalizane, wewe unaogopa nini bwana, hakuna kipiya hapa..vinginevyo, sina
jinsi mimi , itabidi nifuate wanayotaka wao, japokuwa nitaumia sana…’akasema
‘Haya
nimekubali…’akasema Inspecta na kuchukua kalamu, kwanza akamuangalia mdada
usoni, halafu, akafunua zile karatasi, akasoma soma weee…halafu akaanza
kusaini, na alipomaliza akaweka kalamu juu ya ile karatasi, akasema
‘Haya
nimefanya mnavyotaka, nini zaidi…’akasema Inspecta.
‘Kesho,
kazi inaanza, kila kitu sasa kinageukia upande
mwingine…’akasema
‘Kugeukia
upande mwingine , una maana gani?’ akauliza
‘Dunia
inazunguka sio….jana ilikuwa wewe ni muuaji, kesho, itakwua mkeo alijiua yeye
mwenyewe…au sio….’akasema na kusimama kuondoka.
‘Sawa
fanyeni muonavyo nyie, ila …tutaona huko mbele…’akasema Inspecta.
‘Usijali
ya huko mbele huwezi kuyajua, kwanza hili la leo…natumai tumeshaafikiana, na
kuanzia sasa naweka silaha zangu tayari, ukikiuka hata sharti moja, mwenyewe utasikia
mlio tu, kesho hili keshokutwa hili, mwenyewe utatamani kujiua…’akasema
‘Kama
mlivyomuua mke wangu…’akasema
‘Hahahaha,
nani kamuua mke wako, umemuua mkeo mwenyewe kwa mihasira yako, au unataka
tulithibitishe hilo, ….kuanzia sasa sisi tumeshatengeneza mazingira kuhusu huo
ukweli, iliyobakia ni wewe mwenyewe kuwajibika tu ..’akasema
‘Una
maana gani kusema hivyo?’ akauliza Inspecta
‘Vuta
subira, usiharibu utamu, kwaheri mpenzi, uwe na amani, ujue kuwa kuna mtu
anakujali wakati wote wa shida na raha…..’,akasema na kubusu kidole chake, na
kukiweka mdomoni mwa Inspecta, Inspecta akageuka kukataa hicho kitendo, lakini
kidole kilishagusa mdomo wa Inspecta.
‘By
baby….’akasema na kuondoka kwa mwendo wa haraka haraka…
NB
: Hayo ndiyo yalitokea kihivyo, sasa tuone kivingine itakuwaje
WAZO LA LEO: Siku hizi kuna mikataba
mingi ya kiujanja ujanja, hasa makazini, kwa vile mtu kaja mikono nyuma ana
shida ya kazi, basi atapewa mkataba uliojengwa kumkandamiza mfanyakazi bila
hata yeye kujijua, kama una shida ya kazi utafanyeje, unakubaliana nao unaweka
sahihi, kesho na kesho kutwa unaligundua hilo, ukilalamika, kazi huna.
Je
ina maana ubwana na utwana umerejea,…Hili linatakiwa liwekwe wazi kuhusu haki
za wafanyakazi, haki za waajiriwa, kikatiba, najua vipo vyama vya wafanyakazi,lakini
sio makapuni yote yanawajibika kwao, nionavyo mimi kama kuna NSSF, PPF, PAYE,
zinawajibishwa kwa muajiri, kwanini mazingira hayo hayo yasiwepo kwa kila
muajiri, kuwa mikataba yote ya wafanyakazi ni lazima kwanza ipitie kwa vyama
vya wafanyakazi…ni wazo langu la leo, kwa waheshimiwa wetu bungeni.
Ni mimi:
emu-three
4 comments :
Yaani kila ukipita hapa na kusoma hivi visa hamu haiishi ni raha sana na nampongeza sana mwandishi anafanya kazi nzuri sana ambayo jamii nzima ilibidi wasome
Ndugu wangu Yasinta nashukuru sana kwa kunipa moyo wa kuendelea kuifanya kazi hii, japokuwa imejaa changamoto nyingi, lakini yote ni heri tupo pamoja
Emu three, unafanya kazi nzuri sana. Nafuatilia kisa hiki na kujifunza mengi. Hongera sana!
Nashukuru sana @Christian Bwaya, tupo pamoja
Post a Comment