Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 8, 2014

DUNIA YANGU-29


Inspecta Moto alitolewa nje ya eneo lile la choo, wakapita eneo la chumbani kwake, akatupa jicho kwa haraka kuona kama kuna chochote anaweza kukipata kama ushahidi, lakini kwa hali ile ilivyokuwa asingeliweza kufanya lolote, akasema;

‘Hapa ni nyumbani kwangu nahitaji kupaacha kukiwa salama, nipeni nafasi niweke mazingira ya nyumba yangu vyema…’akasema.

‘Usiwe na wasiwasi na hilo,  walinzi watakuwepo muda wote hadi hapo tutakapomaliza kazi yetu ya uchunguzi, tukishamaliza, utaruhusiwa kufanya upendavyo, hatutaki uvurugike ushahidi wowote, nasikia wewe ni mjanja sana….’akasema kiongozi wa kile kikosi cha kumkamata.

‘Mimi ni askari mwenzenu, nafahamu fika kuna mtu kahusika na hili, …..’akasema na yule inspecta mgeni akasema.

‘Mimi hilo sijui nimeletwa hapa kuhakikisha utaratibu wa kikazi unarejea mahali pake, kwan kuna malalamiko mengi ya utendaji wenu usirizisha, na hili limethibitisha hayo, anayway, usiwe na shaka, hakuna kitakachoharibika, …nitahakikisha kila kitu kipo salama na ukweli wote utabainika, huwezi kutudanganya kwa lolote lile, wewe kuanzia sasa upo chini ya ulinzi, ni vyema ukafuata taratibu ili tusije kulaumiana,…’akasema

‘Ipo siku utagundua ukweli wa haya,..na nitahakikisha ukweli wote unabainika, hata kama nitakuwa kifungoni, ….lakini waliyofanya haya yote watajuta…..’akasema

‘Mtoeni huyu mtu humu ndani, tunataka kumaliza hii kazi haraka iwezekanavyo….’akasema mkuu huyo.

Inspecta akatolewa nje ya kile chumba cha choo na bafu, na sasa akapitishwa kwenye chumba chake cha mapmziko, hapo akamkuta Inspecta Maneno, akiwa kakaa kwenye sofa kakunja nne  huku kainamisha kichwa chini. Na alipowaona wakitokeza, akasimama…..

‘Mumeshamaliza ….?’ Akauliza

‘Tumemkamata , lakini inaonekana tumechelewa,…’akasema huyo kiongozi wa huo msafara.

‘Oh, hili sasa ni tatizo kubwa,…..’akasema, na kumsogelea Moto, akamuangalia kama anataka kumuambia jambo, lakini hakutoa kauli, akampita na kuingia ndani huko walipo wenzake kuendelea na shughuli za kiaskari baadaye akatoka na kwenda pale alipokuwa kashikiliwa Inspecta Moto, akiwa chini ya ulinzi, akamsogelea na kwa sauti ya chini akasema;

‘Pole sana rafiki yangu, sijui ni kitu gani kilikufika hadi ukashikwa na hasira kiasi hicho, imekuwaje, hebu nielezee ili nijue jinsi gani ya kukusaidia, maana hili sasa ni tatizo zito sana, kuna kila ushahidi kuwa wewe umemuua mke wako…sielewi kwanini umafikia hatua hiyo, kwanini umefanya hivyo?’ akauliza.

Inspecta Moto, akainua kichwa na kumuangalia, kilichofuata hapo ni machozi mengi yaliyokuwa yakimtoka Inspecta Moto…., hakuweza kusema akatulia kimiya.

‘Wewe ni askari na mwanaume unatakiwa ujikaze, kwasababu huo ndio ubaya wa hasira, kama askari ulitakiwa ujue madhara ya hayo yote, sasa unaona ulichofanya,hasira yako itagharimu vibaya sana, hata sijui nitakusaidieje, …..’akasema

 Inspecta Moto akawa kimiya tu, na Inspecta Maneno akauliza;

‘Ok, sasa je una lolote la kusema ili niweze kukusaidia, maana nataka kuongea na wenzangu kabla hatujapeleka taarifa kwa wakubwa?’ akauliza.

Inspecta Moto, aliendelea kuwa kimiya, huku moyo akijitahidi kuvumilia, alijua akianza kuongea hapo ataongea kauli mbaya, akatulia, lakini baadaye akainua kichwa na kumuangalia Inspecta Maneno, na safari hii ulikuwa uso ulijaa makunjazi ya hasira na chuki,…akamuangalia Inspecta Maneno moja kwa moja usoni, wakaangalia kwa muda.

Inspecta Maneno, akiwa anasubiri kauli ya Inspecta mwenzake, lakini hakuna kauli iliyotoka zaidi ya kuangaliwa kwa hasira, hadi Maneno akahisi vibaya, akageuka kutaka kuondoka, na ndipo akasikia mwenzake akisema;

 ‘Tutaona, labda mniue kabla, lakini wewe na dunia yako tutapambana, hilo naahidi…’ ilikuwa kauli ya Inspecta Moto, iliyomfanya Maneno kugeuka na kumuangalia mwenzake, halafu akajitahidi kutabasamu na kusema;

‘Mimi sikuelewi unachokiongea, naona mshituko umekupoteza akili yako, usijali, tutaona itakavyokuwa…..’akaondoka kwa haraka kukutana na wenzake.


********

Taratibu za mazishi zikafanyika, baada ya kukamilika taratibu zote za uchunguzi, na Inspecta Moto, akatolewa jela, kushiriki kwenye hayo mazishi ya mkewe, japokuwa familia ya mkewe, haikutaka kabisa Inpsceta huyo ashiriki, lakini baada ya kuombwa sana, wakakubali, na hata kwenye mazishi hayo, hakuna aliyekuja kumpa pole huyo inspecta, alangaliwa kama muuaji, na baada ya mazishi akasindikizwa kurudi jela..

Na siku moja baadaye baba wa mke wake akafika kuongea naye kitu ambacho Inspecta hakukitarajia,wakaa kwenye chumba kidogo cha maongezi, kama mzazi alionyesha zile chuki za wazi, akasema;

‘Ina maana nilikuozesha mtoto wangu uje umfanyie hivyo, haya sasa umemuua, umepata faida gani, ndio sasa unataka kumuoa huyo malaya wako…’akasema
‘Mzee, ….’akasema.

‘Nisikilize kwanza, nikuambie niliyoja hapa, aitaki ukaidi wako, ujue hapa naongea kwa hasra sana, mimi nakuambia hivi, hili halitaishia hapa, kwanza nataka nihakikishe kitanzi kinapita shingoni mwako, na kama hawatafanya hivyo, mimi mwenyewe nitalipiza kisasi cha binti yangu….’akasema kwa hasira.

‘Mzee amini ninayokuambia, mimi sijamu-ua binti yako, sijamuua mke wangu, hilo nakuambia, kama mzazi ulielewe, yote hayo ni viini macho tu, ni mambo yaliyotengenezwa, ipo siku utayaamini maneno yangu,..lakini kama huamini, siwezi kukulaumu, maana yamepangwa yawe hivyo, li muamini hvyo, kwa hivi sasa ninachoweza kusema mungu yupo pamoja nami…’akasema Inspecta huyo, na maneno hayo yakamgusa mzee, na huyo mzee akasema;

‘Mara nyingi hakuna mhalifu anayekubali kosa lake, hasa kosa la mauaji, lakini wewe ni askari, na ni mtu ambaye nakuamini sana, hadi sasa sijaelewa, ni kitu gani kilikupata hadi ufikie hatua ya kufanya hivyo, …..sijaamini kama kweli ni wewe umefanya hivyo, nitachunguza mwenyewe, na kama ni kweli umefanya hivyo, tutapambana mimi na wewe…’akasema mzee huyo.

‘Baba niamini mimi, nilifika pale na kukuta mke wangu yupo kwenye beseni la kuogea keshajiua….sina uhakika kama alijiua mwenyewe au kuna mtu kafanya hivyo. Lakini ninahisi kuna mtu kafanya hivyo, kama ningelipewa nafasi kwa muda ule ningeligundua hilo ….ila ninahisi kuna mtu kamuua, na imepangwa makusudi ionekane , kuwa kajiua au mimi nimemuua…’akasema

‘Inavyoonekana ni wewe umemuua, ushahidi wote unaonyesha hivyo,…labda itokee vinginevyo, maana kuna kauli za utata kwa wetu wenu, …sijui wewe kwa kujitetea utasema nini, sijui ni nani ataukubali utetezi wako,…hebu nambie ilikuwaje,  nataka nijue wapi pa kuanzia?’ akauliza mzee huyo ambaye awali alikuwa askari mpelelezi, aliyefikia hadi hatua za juu za uongozi na kabla ya kuastaafu kwake.

‘Siku hiyo kweli nilikuwa hotelini, nikiwa katika mbinu za kupambana na hilo kundi, na walichofanya ni kunitega ili wapate cha kufanya, wakatafuta kila mbinu, na mojawapo ni kuhakikisha nalewa, walijua nikilewa, huwa nakuwa na hasira sana, kwahiyo walipoona nimeshalewa, wakaanza kunikasirisha, kuhusu mke wangu, na nahisi nilitoa kauli za vitisho, na ndicho walichokitaka kutoka kwangu, na nahisi waliweka kitu kwenye kinywaji changu , na hii sio mara ya kwanza…..’akasema

‘Ina maana walishawahi kukufanyia hivyo kabla, na safari bado ukakubali, usiniambie ulifanya hivyo tena kwa minajili ya kufanya uchunguzi wako, …?’ akaulizwa,

‘Ni mlolongo mrefu mzee wangu, lakini yote hayo yamefanywa ili niweze kutii matakwa yao, na hapo hotelini ilikuwa mbinu zaidi ya kunulazimisha nitii matakwa yao mzee, sikumuua mke wangu, hata kama ningelikuwa na hasira kiasi gani, nisingeliweza kufanya hivyo….’akasema.

‘Hebu niambie ni watu gani hao?’ akaulizwa.

‘Inaonekana ni kundi kubwa, lililojijenga kitaalamu zaidi, sizani kama wewe peke yako unaweza kupambana nalo, nakuomba usijiingize huko, sitaweza kubeba lawama nyingine…mzee hilo kundi ni hatari la lina kila utaalamu wa kisasa na wakubwa wengi wamo humo,…..hata hujui ni nani yupo na nani hayupo…’akasema.

‘Hilo sitaacha, hadi hapo nione haki imetendeka, na kama wewe wameshakunasa na umeshajiingiza huko, ujue tutapambana, sasa niambie ukwel, wewe ilikuwaje mpaka ukawa unatembea na huyo Malaya?’ akauliza

‘Zote hizo ni mbinu zao za kuninasa, na huyo mwanamke, ametumika kama chambo, ni mtu wao, katika mbinu zao wapenda sana kuwatumia mabinti warembo, ulevi, madawa ya kulevya, na kuharibu itikadi njema, na pia wanatumia sana mitandao kujenga itikadi chafu, ni mbinu za hali ya juuu za kimataifa, ikiwemo pia blackmail…...na ikishindikana wanakumaliza kinamna ambayo haitaonekana kama umeuwawa, itaonekana umekufa kwa kifo cha kawaida tu..’akasema

‘Nimeliona hili kwenye uchunguzi wangu, nimegundua kuwa kuna jambo kubwa sana, nimeshaanza kukupata, sasa, mimi sitajishirikisha moja moja, sitaki kabisa ijulikane kama nafanya uchunguzi, najua jinsi gani nitafanya, ila narudia tena, kama umehusika kwa namna yoyote ile kwa kifo cha mtoto wangu, mimi mwenyewe nitahakikisha natumbukiza kisu tumboni mwako kama ulivyofanya kwa binti yangu…’akasema.

‘Nakuhakikishia mzee, sijafanya hivyo, na kama ukipata ushahidi huo, …kama ni kweli, nitakukabidhi kisu ufanye hivyo utakavyo,..ila kwa sasa ninachoweza kusema mungu wangu ndiye shahidi kwa kauli yangu hiyo, …’akasema na yule mzee akasimama akitaka kundoka, Inspecta akasema.

‘Mzee wangu, hata mimi statulia hadi nimpate aliyefanya hivyo, najua hawatanipa hiyo nafasi, ila nikitoka hapa sitatulia mpaka niwapate wote waliofanya hivyo,…’akasema

‘Kama usemayo ni kweli, tupo pamoja…nashangaa mbona kauli yako na ya mwenzako zinafanana, utafikiri mlipanga kuniambia hivyo, ila mwenzako sijamuambia kuwa nitafanya uchunguzi wangu, nimemuambia ajitahidi kufanya uchunguzi ili agundue muuaji wa kweli ni nani kwahiyo akikujia ujue yupo katika kutekeleza ahadi yake….’akasema.

‘Mwenzangu yupi una maana Inspecta Maneno…sitaki hata kumuuona, na akija sijui kama kutakuwa na usalama humu ndani, labda wanifunge pingu nikiongea naye, na nitaongea naye nini, msaliti mkubwa yule…..amesema atakuja kuonana na mimi?’ akauliza.

‘Sina uhakika hilo la kuja kuonana na wewe, lakini kama ndiye anafanaya uchunguzi ni lazima akuhoji, au alishafanya hivyo, kiukweli mimi simuamini huyo mtu tena, …kabadilika kabisa, siku hizi ni tajiri , nashindwa kujua pesa hizo kapatia wapi, na mtu ukishajikita kwenye utajiri, hasa usio wa halali, ubinadamu unapotea kabisa,….’akasema.

‘Kwakweli hata mimi simuelewi, na sijui, kwani sijakaa kumchunguza maana nimekuwa nikimuamini kama rafiki yangu, sasa kama unavyosema, basi kuna haja ya kuwa makini naye, maana adui sasa anaweza kuwa hata rafiki wako wa karibu, hata ndugu, kwa jina la utajiri, sijui sasa katika dunia hii utamuamini nani,…..’akasema Inspecta.

‘Ndio maana nimekuambia mimi sitajihusisha moja moja, na kama nitakuja kwako, ujue nakuja kwa mambo mengine, na nitachomeka mambo yangu kinamna…’akasema na kuanza kuondoka Inspecta akasema;

‘Na naomba umwambia mama kuwa hili ni pigo letu sote sijui utamshawishi vipi akubaliane na hiyo hali, kwani nahisi keshanichukia kiasi kikubwa, najua fitina zimeshapandikizwa vichwani mwa watu, na kila mtu ananiona kuwa kweli mimi ndio nimeua,…’akasema

‘Hata magazeti ya udaku yameandika hivyo, na yametoa picha mbali mbali za ushahidi , nyingine zinaonekana ukiwa na akina dada warembo ukistarehe nao, lakini cha ajabu huyu Malaya wako, hawajamuonyesha sijui ni nani hasa….’akasema mzee

‘Hizo ni mbinu zao, kuhakikisha kuwa naonekana mbaya, wanatumia hiyo mbinu kuwa ukitaka kumuua mbwa kwanza umuite huyo mbwa majina mabaya, ili chuki zizidi moyoni….’akasema

‘Mzee unajua kabisa moyo ukijazwa chuki, na ubaya ambao kila siku unarudiwa rudiwa dhidi yako…ni lazima watu watakuchukia, na hata hukumu ikitoka, kila mmoja ataona n halali yako, ….lakini mimi nina imani haki na ukweli una nguvu,…kwa vile sijafanya huo ubaya, mungu yupo pamoja nami, …..’akasema Inspecta na yule mzee akageuka kumuangala, halafu akageuka na kuanza kuondoka kwa hatua ndogo ndogo, kama vile hatak kuondoka, huku akisema;.

‘Twende kazini, ila uwe makini huku jela ulipo, na pa uwe makini na watu wako maana hata sijui ni nani wa kumuamini kwa sasa, ..’akasema

‘Na wewe uwe makini mzee wangu, usimwambie yoyote hata mama usimwambie lolote kuhusu utakayoyagundua hadi hapo ushahidi utakapokamilika,….’akasema Inspecta,na mzee akaondoka sasa kwa hatua za  haraka.

 Inspecta akabakia pale, akiwa kajiinama, na akijaribu kutuliza mawazo yake, alitaman apate mahali alale kidogo, ili akili itulie, akasogea hadi kwenye ukuta akakaa,  lakini kabla hajajtuliza, akaja askari mlinzi na kusema kuwa kuna mgeni wake mwingine kaja

‘Nani ….’akauliza akiwa hana hamu ya kuongea na mtu mwingine tena

‘Inspecta Maneno….’akaambiwa

NB: Haya haya, twende pamoja

WAZO LA LEO: Watu wakiwa katika harakati za kutafuta, hutumia mbinu za kila namna kuhakikisha wanafanikiwa, na hata inafikia watu kukengeuka, na hata wale waumini au vongozi wa dini wanadiriki hata kuyageuza maandiko kwa masilahi yao, yote hii ni kutaka kuchuma, kupambana na hali ngumu, lakini sio hali ngumu tu, bali pia ni kutaka kujitajirisha,lakini tukumbuke dunia ni mapito tu, na muda wa kuishi ni mchache tu, siku itafika kila mmoja atarejea kwa mola wake, na hapo hakimu wa kweli atafanya kazi yake.

Kuchuma tuchume, lakini liwe chumo la halali, na kila mmoja akifanya hivyo, mbona Baraka itapatikana tu.

Ni mimi: emu-three

No comments :