Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, September 3, 2014

DUNIA YANGU-26‘Unataka kwenda wapi?’

‘Naondoka zangu nyumbani, kama hutaki kuniambia ulichoniitia hapa mimi inabidi niondoke tu….…’

‘Uende wapi, nyumbani kwako, kufanya nini, na wakai mkeo yupo anastereje na mpenzi wake wa siku ya leo..’

‘Unasema nini, usinidanganye na propaganda zenu,…Mke wangu yupo nyumbani hawezi kufika hapa, na hapa hajawahi kufika, angefika ningelishafahamu…’akasema kwa hasira akitaka kuondoka, na Yule binti akacheka na kusema;

‘Hahahaha, unasema nini, eti mke wako yupo nyumbani una uhakika na hiyo kauli yako, hebu njoo huku nikuonyesha wapi alipo mke wako…’yule binti akamshika Inspecta mkono na kunza kumvuta waende huko anakopelekwa…

‘Wapi….’akalalamika

Tuendelee na kisa chetu

                    **************

Inspecta kwa kutaka kuhakiki, akachukua simu yake ya mkonoi, na kumpigia mke wake, hakuweza kumpata mke wake, akapiga tena na tena, lakini simu haikupatikana, akageuka kumuangalia binti, Jembe kwa macho ya hasira.

Muda huo, binti Jembe alikuwa anasoma ujumbe kwenye simu yake, na alipohisi kuwa Inspecta anamuangalia,akainua uso kumuangalia Inspecta na kwa macho ya kurembua akasema;

‘Baby, upo tayari twende, nakusubiria wewe, au bado una matumaini ya kumuona mke wako nyumbani?’ akauliza

‘Twende wapi sasa?’ akauliza Inspecta akimuangalia huyo binti, na macho yake yalipokutana na kuna hali ikamnasa Inspecta,…siri ya maanani. Inspecta akajaribu kukwepesha macho, lakini ibilisi alishateka nafsi yake.

‘Na wewe bwana, kwani tuliondoka pale mezani kwa madhumuni gani,…wewe si umesema unataka kwenda kuhakiki kauli yangu,….’akasema kwa sauti laini ya kumpagawisha Inspecta, na inspecta japokuwa alikwepesha macho, lakini ibilisi akamcheza shere, akamuambia hebu muangalie tena….Inspecta akafnya hivyo.

‘Sikiliza wewe….nikaumbie kitu, usinione hivi, ukafikiri mimi ni hivyo mnavyofikiria nyie, utajukuja kujuta kwa hiki mnachokifanya, nakuambia ukweli…’akasema

‘Usijali..yote haya nayafanya kwa vile nakupenda,…yaani usipungue uzito kabisa, kwa maneno mengi, wewe fanya kile unachoona ni sahihi,…ila ujue kuwa mimi nafanya haya kwa vile nakupenda, sio utani, sio kwa ajili ya kazi, hili nakuambi kutoka moyoni, kwahiyoukitaka kuniua,..niue, lakini …’akamsogelea inspecta na akawa kama anamkumbatia, na kutaka kumbusu mdomoni, na Inspecta akamsukuma.

‘Jamani baby, mbona hivi tena, kwani tumekubaliana nini tena…usitake na mimi nibadilike, mimi sitatumia nguvu, natumia akili, mtandao chaaah, unaumia ..na utaumia kweli, na hata ukitaka kunitafuta, hunipati ng’ooooh, hilo nakuhakikishia, muda huo unafikiri takuwa wapi….’akasema

‘Usinitishe kabisa, mimi sasa naondoka, …’akasema akitaka kuondoka, na Yule binti akasema;

‘Nenda halafu utakutana na uchafu wako,…utakutana na yale tuliyoyafanya kulee, unakumbuka sana,…mimi nimekuita leo niwe na wewe, nina mazungumzo nyeti na wewe, pamoja na yote, nitakusaidia mambo mengi tu, …niamimini mimi,…ila muhimu usivuruge utaratibu, usivunja mkataba au sio?’ akauliza

‘Mkataba wetu ulikuwa usiihusishe familia yangu, naona nyie ndio mumetangulia kuvunja huo mkataba…’akasema Inspecta

‘Nani kaihusisha familia yako baby, nimekuambia mke wako kaja mwenyewe kwa hiari yake mwenyewe, na kuja kwenye hii hoteli sio mara ya kwanza, hilo nakuambia , kama unataka kuhakiki, twende nikakuonyeshe…’akasema na Inspecta akasita, na taratibu akarudi kukaa kwenye kiti.

‘Mbona unarudi kukaa kwenye kiti tena bosi,…mimi nataka twende chumbani.haya mambo na mengine hayatakiwi hapa hadharani, au unataka tumeage radhi hapa hapa, unaona wenzetu kule hapa ni kila mtu na wake, ni ruhusa tu…ni kwa wanachama tu…unawaona wale kule..wapo huru kabisa….’akasema

‘Wewe mwanamke wewe, unajua nilikuwa nakuheshimu, na sijui kwanini umenileta hapa, hapa sio mahali pangu,..na huko chumbani unataka tukafanye nini, unataka kunitia majaribuni tena…’akasema na mara simu yake ikatoa ujumbe, akautizama ule ujumbe, haukuwa na namba, akaufungua ule ujumbe, haukuwa na maneno, ila kuna alama ya kuashiria kuna kitu kama picha au kifurushi cha video, kwanza akasita kukifungua, lakini baadaye akaona kwanini asifungue…

Kilipofungua akamuona mkewe akiwa kakaa kwenye meza, na pembeni yake kuna mtu, mwanaume, lakini huyo mtu mwanaume alionyweshwa sehemuu ya mgongoni tu, sura ilikuwa haionekani, wakawa wanakunywa na kuongea, na mkewe alionekana mwenye furaha tu, na ilionekana walikuwa wakiongea jambo lililokuwa likimfurahisha sana mkewe,na sauti ya kiume ikauliza;

‘Je upo tayari kuwa na mimi, …ujue mimi nakupenda sana….’sauti ya kiume ikasema

‘Unanipenda, kwa vipi?’ akauliza mke wake

‘Acha mzaha wako, ….ina maana hujui nakupenda kwa vipi, kama mume wako anavyompenda huyo aliye naye huko alipo…’akasema

‘Unasema nini?’ akauliza mkewe akionyesha hamaki, na hata ule uma aliokuwa nao ukiwa umeshikilia kipande cha tunda ukamdondoka, kuonyesha jindi alivyo shituka.

‘Mumeo sasa hivi ana msichana mrembo, anastarehe naye, ukitaka kuona 
nitakuonyeshe…’akasikia sauti ya kiume ikisema.

‘Hapana najua siku hizi kuna mitandao ya uwongo, siwezi kukubaliana na hilo na sina haja ya kuona hilo jambo, mimi naona nirudi nyumbani, maana umeshaniumiza kichwa changu…’akasema mkewe

‘Hahaha. Hivi unataka nikueleweshe vipi, hayo siku hizi ni mambo ya kawaida tu, na wewe unatakiwa uyazoee, leo ukiwa na mwingine usiogope,kwa vile na yeye yupo na mtu, na yeye atakuja kuyazoea, lakini ukikaa nyumbani ukasononeka, utakuja kufa, na mwenzako atabakia na huyo anayestarehe naye…’sauti ikasema

‘Yaani hata wewe unaniambia hivyo..ina maana hata wewe…..’sauti ikawa kama inakatika katika, maneno mengine yalikuwa hayasikiki…’

‘Lakini mipango yetu umekubaliana nayo, au sio?’ akauliza huyo mwanaume

‘Nitafikiria, nahitaji kujua mengi kwanza, pia…’maneno yakakatishwa, na ideo hiyo haikuendelea tena.

‘Ni nani huyu alikuwa na mke wangu?’ akauliza Inspecta

‘Utamuuliza mke wako wako, na mke wako anachofanya ni kama hicho unachokifanya wewe, sio jambo geni au sio, usimulaumu sana, maana ukitenda ujue na wewe utatendewa,au sio…?’ akawa kama anaulizwa

‘Kwani mimi nimemtenda nani mke wangu, hebu niambie?’ akauliza

‘Hahaha, hivi wewe hukuja kwangu kwa hiyari yako mwenyewe, na kuna ushahidi unaonyesha jinsi ulivyokuwa ukiongea na mlinzi kuwa umenipenda, na unahitaji kunifuatilia, ukafika sehemu ukabadili nguo, ili uonekane mtanashati, au sio, …je huo ni uwongo, sema mwenyewe, hukunifuatilia,…?’ akaulizwa

‘Hizo ni mbinu zenu, mimi nilipanga kuja kwako kutaka kupata taarifa, na hizo zilikuwa mbinu zangu, hayo mengine mumeyapanga wenyewe kwa kuunganisha unganisha habari ili ziendane na mnavyotaka nyie…’akasema

‘Yoyote atakayeiona hio kanda ya video hatakuwa na mashaka, na hata ukipeleka kwa wataalamu wa video wanaoweza kutambua kuwa video hiyo ni kuunga unga au ni ya asili, watathibitisha hilo,….kauli, vitendo, na kila kitu ni asilia, hakuna kuunganisha hapo,..kwanini nikusingizie baby, je kweli hukunifuata, je kweli hatukustarehe na mimi siku ile, je hayo ni ya kuunga unga….?’ akauliza

‘Mliniliwesha nikawa sijatambui…’akasema kwa sauti ya kukata tama.

‘Hahaha, ukitaka nikuonyeshe hiyo video utaona mwenyewe, kama kweli ulikuwa umeleweshwa, kila kitu kipo wazi, inaonekana kabisa ulilewa mahaba….ukanizimia, na ukawa unatamka mwenyewe, kwa kauli yako pana, kuwa hujawahi kuona msichana mrembo kama mimi, na hutaweza kuniacha kamwe..’akasema

‘Mimi!!?, Mimi nilisema hivyo, haiwezekani?’ akauliza

‘Twende chumbani ukaone mwenyewe…’akaambiwa akishikwa mkono.

‘Ina maana hiyo kanda chafu unayo, unatembea nayo?’ akauliza Inspecta

‘Kuna utaalamu baba, mimi nikitaka kuipata naipata, na sio wote wanaoweza kuipata, na  hata mimi naipata kwa kibali maalumu…tunahakikisha siri zako zote zinachungwa hadi hapo utakapokiuka mkataba….’akasema

Mara ujumbe ukaingia kwenye simu ya Inspecta, ilikuwa ujumbe wa mtandao kuwa namba ya mkewe,aliyokuwa akipiga, kwa sasa anapatikana. Inspecta alipoona ule ujumbe, kwa haraka akampigia mkewe, na mkewe akapokea, na kila mmoja akauliza

‘Wewe upo wapi…?’ kauli zikakutana

‘Mke wangu upo wapi?’ akauliza Inspecta

‘Na wewe mume wangu upo wapi?’ akauliza mkewe

‘Ina maana tunashindana, hukunielewa kuwa nafanya haya kikazi…’akasema Inspecta

‘Kwani mimi haya nafanya kimaigizo, hata mimi nafanya kikazi, ..’sauti ya mkewe, ikasema na ilikuwa sauti ya kama mtu kalewa.

‘Kwani upo wapi?’ akaulizwa

‘Niambie kwanza na wewe upo wapi, na huyo mwanamke ni nani?’ akauliza mkewe.

‘Naomba urudi nyumbani, tutaongea nikifika huko nyumbani, na ni nani kakuleta hapa, umepajuaje hapa, …?’ akaulizwa

‘Kwani wewe ulipajuaje hapa, ulivyopajua wewe ndivyo na mimi nilivyopajua, unachofanya wewe na mimi ndicho ninachofanya tatizo lipo wapi..’ilikuwa sauti ya mkewe na sasa haikujificha, kulikuwa na hali ya kulewa, kutokana na sauti ilivyokuwa ikitoka.

‘Ina maana umelewa mke wangu, au umeleweshwa…?’ akauliza akionyesha sauti ya kusikitika.

‘Nimekunywa mwenyewe kwa hiari yangu, na wala sijalewa,kwani wewe hunywi, hapo ulipo hujakunywa, japokuwa nimekunywa lakini hapa nilipo nina akili zangu timamu kabisa..kabisa…nastarehe kwa raha zangu, kama unavyofanya wewe..halafu unasema au nimeleweshwa, kwanini nileweshwe wakati mimi ni mtu mzima na nina akili zangu hahaha utajijuuuh…’akasema mkewe na kucheka, na sauti nyingine ikaguna, ilikuwa ni sauti ya kiume.

‘Upo wapi huko wewe mwanamke, ninakuja huko na kitakachokupata usije kunilaumu ..utanitambua…?’ akauliza Inspecta mwili mzima ukimzizima kwa hasira

‘Hahaha heeya,..njoo, nipi kwenye vyumba maalumu  vya starehe, najua na wewe upo kwenye chumba cha starehe na mwenzako, kwani kuna tatizo gani, siku moja moja sio mbaya, hahaha, kama wewe umeshatosheka, nitakukuta nyumbani….’akasema na mara sauti ya kiume ikiguna tena, Inspecta akazidi kuchemka kwa hasira na wivu, akageuka kumuangalia binti Jembe na kusema;

‘Hii maana yake nini?’ akauliza Inspecta akiwa katoa jicho la hasira

‘Kuhusu nini?’ akauliza Binti mrembo

‘Haya mumeyafanya nyie kwa makusudi , nauliza maana yake nini, mnataka nini kwangu…?’ akauliza akimsogelea binti Jembe na binti Jembe hakusogea nyuma akawa kasimama, hadi pale mkono wa Inspecta uliposhika bega la Binti Jembe , na Binti Jembe akahisi maumivu, akainua mkono wake na kuushika mkono wa Inspecta, akasema.

‘Sikiliza baby,unaniumiza, hatuendi hivyo, mimi nikitaka kukuumiza nitakuumiza kweli, na mimi nakuumiza moyoni, ondoa mkono, au ulegeze mwanamke hafanywi hivyo, nguvu hazilipi kamwe…’akasema halafu akashika mdomo na kunyosha kidole kuelekea kwenye simu ya Inspecta

Kumbe simu ya Inspecta bado ilikuwa hewani, Inspecta hakuwa ameizima hiyo simu, na kwenye simu akasikia mkewe naye akisema;

‘Nimesikia huko ukiitwa baby eeh, kumbe bado una na huyo baby wako, usijali na mimi nina baby wangu hapa,.... sogea huku baby tumalize kazi yetu……’ilikuwa sauti ya kilevilevi …
Inspecta akatoka pale kwa haraka akaelekea sehemu ya mapokezi, akaongea na Yule muhudumu lakini walionekana hawaelewani, akatoa kitambulishi chake..

‘Inspecta humu vitu kama hivyo haviruhusiwi, unataka kufanya nini, unakumbuka mashartii ya kuingia humu, nilikuonyesha na ukayasoma, ….

Kuna sehemu imeandikwa wazi, ..`hata kama utaona mke wako au mume wako yumo humo na mtu mwingine, huruhusiwi kumuingilia, maana kila mtu kaja kwa hiari yake mwenyewe… unakumbuka hayo maandishi, uliyasoma na ukaweka sahihi yako,..’Ilikuwa sauti ya mdada ikasema kutoka nyuma yake, na Inspecta akageuka kwa hasira kwa dhamira ya kutoa kipigo, lakini alipogeuka akamuona mdada yupo na walinzi wawili huku na huku yeye yupo kati kati.

‘Kama unataka nikupeleke alipo mke wako, kwanza twende chumbani, huko nitakuambia wapi alipo mke wako, na ukitaka nitakupeleka, mguu kwa mguu umuone akiwa na mpenzi wakeeeh, hehehhe…,Inspecta , Inspecta….’akasema huyo mdada kwa dharau, na wale wapambe wake wakawa wanatunisha vifua vyao, …walionekana ni watu wa kazi kweli.

‘Upo tayari twende,… lakini kwanza utii masharti yangu,…’akasema Yule binti akimuangalia Inspecta machoni, hakuonyesha wasiwasi, abasamu lilijaa tele mdomoni.

‘Masharti gani?’ akauliza Inspecta.

‘Unayafahamu sana, sihitaji kuyarudia, ukumbuke usipoyatii, kwanza hutamuona mke wako, na pili uchafu wako utazidi utasambazwa kila kona …, na safari hii utamfikia hata baba na mama mkwe wako, unaihisije hiyoo, inauma lakini ndio ukweli ulivyo, mimi natimiza wajibu wangu, pole Inspecta, I love you baby….’akasema Binti Jembe, na Inspecta akawa katulia, akitetemeka mwili mzima kwa hasira.

Yule binti bila kuogopa akamsogelea Inspecta na kupitisha mikono yake laini kifuani kwa huyu simba aliyejerushiwa, akapeleka kidole kwenye mdomo wa Inspecta, akasema;

‘Twende zetu baby, hizo hasira zina dawa yake wala usijiumize, ukistarehe na mimi utasahau kila kitu….mimi ndiye dawa ya yote hayo…’akasema na kumshika mkono Inspecta.

Inspecta, hakuweza kusema neno akawaangalia wale mabaunsa wawili, akilini alitaka kuwaonyesha kuwa yeye hawaogopi, na anaweza kupambana nao, lakini akachelea , akijua yupo sehemu ambayo vitu kaam hivyo havitakiwi…akanywea,

‘Baby twende..hebu fikiria, kama mwenzako kaamua kukufanyia hivyo…yupo anastarehe na mwenzake, wewe utapungukiwa na nini ukiwa na mrembo unayempenda, kwani hunipendi, … mimi nakupenda sana baby, twende basiiiih….’akasema akimvuta mkono Inspecta kuelekea huko chumbanii….

NB Haya wapendwa mimi sisemi zaidi ndiyo mambo ya dunia yangu, mwenye akili atatambua

WAZO LA LEO: Hadaa katika maisha yetu imekuwa ni jambo la kawaida tu, mtu kumuhadaa mwenzake ili apate jambo, atatutumia kila lugha za mapambio ili kitu chake au jambo lake lipokelewe, na yeye kupata pesa au malipo ya hicho kitu au hili jambo, huku mtu huyo akijua alichokisema sio kweli, hii ni dhuluma na huu ni wizi.


 Wewe ukiona mwizi anapigwa kaiba, unachhekelea tu, au wewe ukiibiwa unaumia sana, na unakuwa msitari wa mbele kumpiga huyo mwizi na kumlani, lakini kila siku unaibia wenzako, kwenye biashara zako, kwenye shughuli zako za kila siku unazozifanya kwa njia ya hadaa. 

Tuweni makini, kwenye kuzitafuta riziki zetu, tujishughulishe kwenye kupata kipato halal , kwa kuwa wakweli kwa kufanya hivyo riziki na maisha yetu yatanyooka, maana ukweli ni Baraka, na Baraka itakuza vipato vyetu.

Ni mimi: emu-three

No comments :