Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, September 1, 2014

DUNIA YANGU-25‘Hahaha...... unamuwazia mkeo sio, hahaha, ungelijua, kuwa mkeo naye yupo anastarehe na wa kwake,usingelisumbuka hivyo, hahaha….wanaume bwana, mnaiona wajaaaanja, hujui kuwa unayestarehe naye ni mwanamke, na kama sio wa kwako wa ndoa ujue ni mke wa mtu au mchumba wa mtu…hahaha, sasa nataka nikuambia ukweli

Tuendee na kisa chetu 

                                    ***********

Wakati hayo yanaendelea huko hotelini, mke wa Inspecta alifika hapo hotelini na shoga yake, na shoga yake kuonyesha kuwa ni mwenyeji, akatangulia kuingia ndani ya hiyo hoteli na kusalimiana na walinzi,

Mke wa Inspecta, alimuangalia mwenzake kwa mshangao, kwa jinsi alivyokuwa akisalimiana na walinzi, hana wasiwasi, alionekana kama mwenyeji tu, basi yeye akawa anamfuatlia nyuma nyuma, akionekana mwingi wa mawazo, kuna muda alikuwa akijawa na hasira, kuna muda alikuwa akiona amefanya hasira kuchukua hatua hiyo.

'Ngoja tukae hapa kidogo tunywe angalau kinywaji, ....'akasema
'Lakini....'akasema mke wa Inspecta kulalamika.

'Hii ni moja ya mbinu zetu, we niachie mimi,najua ni nini tukakifanya tunatakiwa tuonekane tumefika kihoteli, sio kumfuatilia mtu , unaonaeeh, mjini shule shoga...'akasema na wakakaa kidogo wakiagizwa vinywaji vyepesi.

‘Haya tumefika, hii ndio Paradise Hoteli, unaiona ilivyo,…ulishawahi kufika hapa kabla?’ akaulizwa na yeye kwanza akatabasamu, halafu akasema kwa mashaka.

‘Nilishawahi, ….’akasema na akasita kuendelea kuongea.

‘Ulishawahi kufika hapa?’  mwenzake akamuuliza kwa mshangao, lakini mke wa Inspecta hakusema kitu akatulia kama vile kaongea kitu ambacho hakutaka kukiongea, na mwenzake akasema;

‘Kama uliwahi kufika, utakuwa unafahamu jinsi huko ndani kulivyo, au?’ akaulizwa

‘Shoga, sikuwahi kuingia ndani,…na  ilikuwa jioni jioni hivi inaelekea usiku,…yaani, siku hiyo, ilitokea tu, …’akasema akiona aibu.

‘Mhh, basi kumbe na wewe wamo, eeh, au …?’ akataka kusema lakini mwenzake akamkatiza na kusema;

‘Hebu acha hayo, sivyo kama unavyofikiria wewe, alinileta rafiki yake mume wangu, akinionyesha miradi yake,wakai tunapita hapa ndio, akasema tuje kula na kunywa kidogo, …lakini sikupenda, hata hivyo, kwa vile ni rafiki wa mume wangu, nikaona sio vibaya, nikamkubalia …’akasema

‘Hamna shida, huna haja ya kujitetea kihivyo,…’akasema na kumfanya mke wa Inspecta kujuta moyoni, kwanini kamuambia aliwahi kufika hapo, lakini hakuona tatizo sana, na siku hiyo hakuwa makini sana kuichunguza hoteli, kwani alifikishwa hapo kama kushitukizwa tu.

‘Sasa kama uliwahi kufika ,basi hutakuwa mshamba sana wa hapa, ila kwa huko ndani kuna sehemu nyingi, kuna sehemu za starehe, kuna sahemu za mikutano, kuna sehemu maalumu kwa wanachama tu, sasa sijui mume wako atakuwa upande gani, ngoja nifanye utafiti…’akasema na wote wakawa ndani sehemu ya mapokezi.

‘Wewe nisubiri hapa, niongee na hawa watu wa mapokezi, ….’akasema na kusimama kuelekea sehemu ile ya mapokezi, akawa anaongea na yule jamaa wa mapokezi kwa muda, halafu akaja pale aliposimama mke wa mtu, akasema;

‘Ukiwa mjanja bwana, hakuna kitu kinakushinda, nimetumia ujanja wa mjini, mpaka nikajua mume wako anaweza kupatikana sehemu gani, japokuwa hapa huwa hawataji mtu yupo wapi hasa wanachama wa hiyo sehemu maalumu, ..ukiona wanasita kukuambia mtu wako yupo wapi ujue ni lazima atakuwa mwanachama na yupo sehemu ya wanachama tu…’akasema

‘Sasa wewe umejuaje yote hayo, inaonekana wewe ni mwenyeji kwenye hili jengo,…ni kiukweli, mimi hapa hata sijui niende wapi, maana jengo hili ni, kwa mapana na kwenda juu, na huku juu tutapandaje…?’akauliza mke wa Inspecta.

‘Unaona pale kwenye ukuta,pale kuna maelekezo, ofisi zote zilizomo kwenye hili jengo zimeorodhweshwa pale, kama ni kwenda juu, tunatumia lifti ile pale, unaona pale watu wanatoka na kuingia, eheee, sasa twende pale, nina uhakika mume wako yupo sehemu ya hoteli ya watu maalumu, humo wanaingia wanachama tu, kwahiyo kumuona itakuwa ngumu…tutaona huko mbele…’akasema

‘Kwahiyo?’ akauliza mke wa Inspecta kwa sauti ya kukata tamaa

‘Wewe twende huko huko juu, mimi nitajua la kufanya…’akasema akitembea kuelekea kwenye ile lifti, na mke wa Inspecta akamfuata huku akionyesha wasiwasi, kichwani akijiuliza atajuaje jinsi ya kurudi mwenyewe, kama mwenzake ataamua kuondoka.

‘Lakini si umeniambia unatakiwa kuwahi kazini kwako, vipi tena, mimi naona tuishie hapa tu, sina haja ya kuendelea zaidi, ngoja nirudi nyumbani…?’ akasema, na mwenzake akamuangalia kwa macho ya kushangaa,na kusema;

‘Unafikiri kazini kwangu ni mbali basi, sio mbali sana kutoka hapa,… ni hapo jirani tu, muda ukifika mimi nitaondoka, kama tutakuwa hutujamuona mumeo wako basi wewe utarudi nyumbani, au…?’akasita akiangalia huku na kule kama kutafuta jambo.

‘Au nini tena, umeona nini…?’ akauliza mke wa Inspecta.

‘Hao wanaonekena kutoka huko juu, nilijaribu kuwaagalia , mume wako anaweza kutoka tusimuona..’akasema akizidi kuwaangalia wale watu, na ujumbe ukaingia kwenye simu yake akawa anausoma, halafu akasema

‘Naona muda unakwenda, twende haraka huko juu, kama tutamuona sawa,kama hayupo humo, basi watakuwa wamechukua chumba…siunajua tena humu kuna kila kitu….’akasema.

‘Wamechukua chumba, una maana gani?’ akauliza mke wa Inspecta.

‘Wewe sio mtoto mdogo bwana, hayo ndio maisha ya waume zetu, wewe kaa nyumbani, pika, subiri, mwenzako akirudi anakuambia nimechoka kweli, hata sijisiki kula, unarizika tu…kumbe keshamaliza kila kitu huku wanaposema wanakwenda vikaoni…’akasema

‘Mhh, hayo makubwa, nahisi kama unataka kunichinganisha tu, mume wangu hawezi kufanya hivyo….unachoongea kinanitia mashaka hata naanza kuogopa…’akasema

‘Wala usiogope, mwenyewe utajionea, mimi muda wangu ukifika nitaondoka, mengine utajua wewe mwenyewe, au vinginevyo, tutarudi pale chini, wewe unaweza kuendelea kumsubiria nitakuonyesha sehemu ambapo wanapitia watu wote, akipita tu unamnasa…’akasema akiangalia upande wa pili kuna watu walikuwa wakija muelekeo wao.

‘Hapana huwezi kuniacha huku juu mwenyewe, mimi hata sipaamini, ..’akasema

‘Hahaha kweli wewe mtoto wa geti kali, unaonekana wa kijijini..jichanganye mwenzangu, dunia itakuacha njia panda…lakini si umesema rafiki wa mume wako huwa anakutoa out siku moja moja….au’akasema

‘Mhh, na wewe bwana, sijasema hivyo, usikuze maneno, na hata hivyo mimi nitajichanganyaje wakati mume hanipi hiyo nafasi, mimi na kazi za nyumbani, san asana ukitoka ni kwenda sokoni, siku hiyo huyo shemeji alinipitiza hapa tu kunionyesha miradi yake na tukitoka naye ni kama katumwa na rafiki yake kunipeleka mahali, na sio kama unavyofikiria wewe…’akasema

‘Sio kama ninavyofikiria mimi, usijidanganye bwana, dunia hii haina siri, ipo siku utaona mambo yenu yote yakiwa hadharani, ndipo utasema, wamejuaje..mmh, usijali mimi ni shiga yao tu, haya tunaongea tu…ila jua hayo hayo sababu kubwa ni wanaume,umeonaeeh, kama akikufuga ndani ujue ana mtu wake nje…’akasema.

‘Sio kweli, na sio wote wana tabia hiyo…’akasema.

‘Hahaha,heeya…mmh, nimecheka utafikiri nipo mitaani kwetu…’akasema akiangalia huku na kule kama kuna watu wamemsikia.

‘Mara nyingi mume wangu ni mtu wa kazi, na kazi zake, zinamruhusu kuja sehemu kama hiii au sehemu yoyote, siwezi sana kumlaumu, ila hicho ulischosema kwa huyo mwanamke, kinanitia wasiwasi sana…’akasema.

‘Unaonaeeh, ndio maana wanaume zenu wanawadanganya, anakudanganya kuwa ana kazi nyingi, ana kikao sijui, vikao vyenyewe siku hizi vinafanyika mahotelini, unajua kwanini…’akamuuliza akiangalia simu yake.

‘Kwanini?’ akauliza mwenzake

‘Wakimaliza kikao mambo mengine yanaendelea humo humo, hakuna kutoka kwenda wapi tena, kama ni kulala, kama ni nini ni humo humo..hahaha, wewe lala nyumbani tu, endelea kusubiria ukiota ndoto za mume mwema, mume mwema karna hii hakuna…’akasema.

‘Huo sasa ni ushetani….’akasema.

‘Kwako wewe ni ushetani, kwa wenzako ni maendeleo, mwenye kitega uchumi anafaidikia kwa yote hayo…ndio dunia ilivyo, wenzako wanakuwa na dunia zao akilini, wewe unabakia gizani tu, umelalaaaa, huamuki, ukiamuka umeshazeeka, nani atakutaka tena..hahahaheyaah…’akasema na kucheka, mwenzake akazidi kujawa na hasira moyoni.

‘Mimi sipendi maneno yako, naona unazidi kunichefua….’akasema.

‘Sasa sikiliza, twende huko huko juu, hapa sio penyewe, kama tukimkosa kabisa wewe unaweza kurudi nyumbani mwenyewe au sio…’ akawa kama anauliza na mke wa Inspecta akawa anaangalia huku na kule kuwaangalia wale watu waliokuwa wakitoka na kuingia kama atamuona mume wake.

‘Mmm, hapana huwezi kuniacha hapa mwenyewe, kama ukitaka kuondoka, inabidi wewe unitoe hadi barabarani,….yaani hapa tu nimeshachoka, hata hamu ya kumuona huyo mume sina tena….’akasema.

‘Unajua wewe ni rafiki yangu, sipendi haya wanayotufanyia wanaume yaendelee, lakini nikikuambia kwa mdomo hutaamini ndio maana nikaona uje hapa ujionee mwenyewe kwa macho yako mwenyewe..unaonaeeh…’akasema akimshika mkono mke wa Inspecta

‘Lakini mimi naona haya ya kumfuatilia mtu, nikujisumbua maana mtu hujichunga mwenyewe hasa mnapokuwa kwenye ndoa, na ukiamua kumchunga mwenzako ni kujiumiza mwenyewe tu, mmi tabia hii siipendi kabisa,…’akasema mke wa Inspecta.

‘Ni sawa hakuna anayependa hilo, hata mimi sipendi kuvunja ndoa za watu…ila wakati mwingine ni muhimu kuhakikisha maana unaweza kusema rafiki yangu ana lengo baya la kuvunja ndoa yangu, hilo ndio silitaki, sipendi umbea kabisa,…unaonaeeh,…’akasema na yeye akijifanya anaangalia huku na kule kutafuta.

‘Mimi naona tunajisumbua bure tu, naona huyu mume wangu hayupo hapa, labda bado yupo ofisini kwake…’akasema mke wa mtu.

‘Usijali, ..mimi nina uhakika yupo hapa, ngoja kwa sasa nikupeleke huko wanapokaa watu wanachama tu, ni sehemu maalum sio hapa, mimi nina uhakika ni lazima atakuwa huko, ..mara nyingi watu kama hao hawawezi kukaa sehemu hii ya kuonekana na kila mtu, tukifika huko niachie mimi…’akasema.

‘Kwahiyo sio hapa tena?’ akauliza mke wa Inspecta.

‘Hapa pia ni sehemu ya hoteli, ni sehemu ya watu kujibuudisha, hata hapa ukiingia kwenye mlango ule, unaona pale pameandikwa nini, wanachama tu, lakini hapa ni kwa watu wengine wakunywa na kula na kuondoka, lakini huko ninaposema mimi, ni zaidi ya hapa..’akasema.

‘Kwa vipi, huko kuna nini zaidi?’ akauliza

‘Kila kitu..’akasema.

‘Kila kitu kwa vipi?’ akauliza.

‘Wewe usijali utajionea mwenyewe, tutafika sehemu ya mapokezi kama hapa, utaulizwa utoe kadi, hapo utaniachia mimi, nitajua la kufanya, ..ila tukishindwa kabisa, kuna namna nitaongea na jamaa analinda usalama, nafahamiana naye, atajua la kufanya na hapo utaona maajabu ya hii hoteli…’akasema.

‘Aaah, mimi naona nirudi nyumbani tu…nakusumbua sana rafiki yangu,…’akasema mke wa Inspecta

‘Yaani umefika hadi hapa, unataka urudi nyumbani hivi hivi, hapana, usiniangushe mwanamke wee, mimi nilijua wewe ni mtoto wa mjini kumbe bado mshamba, hivi utajuaje jinsi dunia inavyokwenda, wewe twende huko juu ukaona mambo, hatutakaa sana…’akasema na kumshika mkono na mke wa Inspecta ikabidi wakubali na wakaingia kwenye chombo cha kupandisha juu…

NB Haya hayapo….mke katoka kijijini kafika mitaani kwetu, anakutana na wanawake wa mitaani, anachukuliwa kihivyo, mwishowe unakuwa nini…haya tutaona kutatokea nini huko mbele...

WAZO LA LEO: Uaminifu wa mtu ni mtu mwenyewe, kila mtu anapofikia umri wa utu uzima, akafikia hadi kuoa, ina maana ameshafahamu masharti ya ndoa, kwahiyo mienendo yake, na umanifu wake, hauwezi kupimwa kwa kuchunguzana, kwani kiapo cha ndoa kinatosha kuwa mchunga, na kiapo cha ndoa huwa kimeshafika kwa mungu, atakayekivunja, anapingana na mwenyezimungu, na kwahiyo keshatangaza vita na muumba wake. Tuwe waaminifu hasa wale waliopo kwenye ndoa, kwa masilahi ya vizazi vyetu.
Ni mimi: emu-three

No comments :