‘Usitumie kisingizio
cha kazi yako kufanya mambo yenu, nawafahamu sana nyie wanaume mnapenda sana kujiendekeza
kwa visingizio mbali mbali, unadai una kazi za ziada kama hivyo kumbe una mambo
yako mimi nitakuja huko huko unapokwenda kukutana na huyo aliyekuita....’.
‘Kuja...kufanya
nini....?’
Tuendelee
na kisa chetu...
***********
Inspecta
hakuwa na amani, lakini aliona ni vyema kwenda huko alikoambiwa aende, kuonana
na mdada wa urembo, alijua kuwa kwa kufanya hivyo inaweza kuwa ni sehemu ya
kupata hicho anachokitaka kukijua, japokuwa kwa namna nyingine, anazidi
kujiingiza kwenye mtihani mkubwa;
‘Moja
ya kazi yangu ni mitihani, kwahiyo ngoja niende tu,....’akasema na kwanza
akabadili nguo zake, ili aonekane toauti kidogo, akaliacha koti lake na
kubakiwa na shati,...mtanashati kidogo, akatoka nje ya ofisi na alipofika
kwenye gari kichwa akawa anasikia sauti ya mkewe ikimwambia;
‘Kila laheri, sina
zaidi, utanijulisha mkielewana na mwenzako,kuwa niende au nisiende..kama
sitakwenda basi mimi nitakuja huko huko unapokwenda kukutana na huyo aliyekuita...’
‘Mhh,
sasa huu ni mtihani, inaweza kweli mke wangu anaweza kuja huko, ...?’ akajiuliza
huku akiingia kwenye gari, na moyoni akawa kama anakanywa asiende huko
anapotaka kwenda, akawa anahisi hali isiyo ya kawaida,...
‘Hali
kama hii inaniashiria hatari...lakini kwanini, kwani huko kuna hatari gani, huu
sasa ni uoga...’akasema
Akaanza
kuendesha gari, na alipofika kati kati ya bara bara , mara akahisi kuna mtu
nyuma yake , akaangalia kiyoo cha juu
kinachoonyesha nyuma, kile kiyoo kilikuwa kimegeuzwa na tofauti na
kinavyotakiwa kiwe, akajua kuna mtu kafanya hivyo kwa makusudi, akapiga mahesabu,
jinsi ya kufanya.
Alihisi
kwa vyovyote kuna mtu nyuma yake, je huyo mtu ana malengo gani, akatupa jicho
kwenye kiyoo cha runinga ndogo iliyopo hapo mbele ambapo kuna kiyoo kinachoweza
kuakisi kitu cha nyuma,kinaonyesha mandhari ya nyuma, lakini hakuona mtu, kuna
kitu kama kitambaa kinapepea, hakumbuki kuweka kitambaa nyuma, lakini muoshaji
jana alisahau kitambaa chake.
‘Nahisi
kabisa kuna mtu nyuma sijui kakaa vipi kiasi kwamba siwezi kumuona...’akawa
anaongea komoyo moyo
‘Hili
ni kosa kubwa nimefanya, kwanini sikuwa muangalifu wakati naingia ndani ya
gari....’akawa anajilaumu
‘Kama
ni mtu kaingiaje kwenye gari langu, wakati eneo la ofisi lote kuna usalama wa
magari, ..?’ akawa anajiuliza bila jibu.
‘Huyu
atakuwa mtu wa ndani, sasa ni nani...’akaendelea kujiuliza huku akitauta njia
ya kugeuza kicha aangalia nyuma, lakini inakuwa vigumu, kwani kama ni mtu
atakuwa nyuma yake kabisa, na kumuangalia ni mpaka usimamishe gari.
Akawa
anaendesha gari hivyo hivyo, akijifanya hana wasiwasi, lakini kwa mashaka hadi
akafika sehemu ambayo anajua hakuna hatari inayoweza kutokea, hata kama
atakabliana na huyo mtu, ni sehemu ya watu, akapunguza mwendo kutaka kusimamisha
gari, mara akahisi hatari...
‘Kwanini
unasimamisha gari...’sauti ikasema na mara akahisi chuma kikigusa kwenye
kisogo, akajua hiyo ni bastola
‘Wewe
ni nani na kwanini umeingia ndani ya gari langu bila rushusa na kuharibu
utaratibu wa viyoo vya usalama, huoni unaniweka kwenye hatari ya kuleta
ajali...?’ akauliza
‘Hilo
lisikusumbue, cha muhimu ni kuelekea huko huko ulipotakiwa kwenda...’sauti
ikasema
‘Wapi?’
akauliza
‘Kwani
uliambiwa uende wapi, hukumbuki uliambiwa nini ,kuwa ukakutane na nani...?’
akaulizwa
‘Sijui
unachokisema, wala sikuelewi, niambie wewe unataka nini kwenye gari langu,....’akasema
‘Kwahiyo
unataka nikukumbushe...au sio, mimi sio kazi yangu, lakini ukinilazimisha
nitaweza kufanya hivyo...’sauti ikasema
‘Sijakuelewa...’akasema
‘Hapa
nyuma nina sindano ya virusi vya magonjwa, nikuchome nayo, au...?’ akaulizwa
‘Usinitishe
bwana, kama ni kwenda huko nitakwenda kwa hiari yangu, kwani nilipanga kwenda
huko ninapokwenda, sasa sijui huko unapotaka wewe ni wapi, au kuna sehemu gani
nyingine unayotaka mimi niende, nielewe wewe...’akasema Inspecta
‘Huko
huko unakoelekea ni sahihi, twende kazini...ile sauti ikasema na kile chuma
kisogoni kikaondolewa, ambacho Inspecta
alijua ni mdomo wa bastola, na hapo Inspecta akapumua akijua angalau sasa
anaweza kuendesha bila mashaka. Katika vitu ambavyo anajitahidi katika kazi
yake kuwa na tahadhari navyo, kimojawapo ni silaha, kwani alishahudia mtu
akiuwawa kwa bahati mbaya tu, kwa mzaha kama huo...
‘Umeingiaje
kwenye gari langu....?’ akauliza Inspecta, lakini kukawa kimiya, hakusikia jibu lolote
kutoka kwa huyo mtu ambaye alijua kabisa bado yupo nyuma yake, kulikuwa kimiya
kama hakuna mtu.
‘Nataka
kuweka gari langu mafuta , huwa nina kawaida ya kuongeza mafuta kila ninapotoka
ofisini, kwahiyo nataka kuingia kituo cha mafuta...’akasema Inspecta
‘Hilo
limeshafanyiwa kazi, ukifika hapo unapokwenda utajaziwa mafuta yako, hayo
yaliyopo yatakufikisha sehemu unayotakiwa bila kuisha, ...’akaambiwa
‘Ina
maana umechunguza kila kitu, kwanini umefanya hivyo, au ni nani kakutuma?’
akauliza, akitaka aendelee kusikia sauti ya huyo mtu huenda akaweza kumtambua,
maana ni lazima awe mtu wa ndani ambaye anaweza kuingia ndani ya gari lake bila
kuhisiwa vibaya.
‘Yah,
...kila kitu...’akasema na kutulia
‘Unajua
mimi ni askari, na sipendi hicho unachonifanyia, hapa naweza kufanya lolote,
lakini sitaki shari, kwanini tusielewane, tuongee na tujuane, ....’akasema
Inspecta
‘Usijali,
..’sauti ikasema na kunyamaza
‘Binti
wa urembo, au jembe, unajuana naye kivipi?’ akauliza na sauti kama ya kuhema
nyuma ikasema
‘Endesha
gari, ...’Mara akahisi kitu, na haruu ya dawa za hospitalini ikasambaa ndani ya
gari, na mara sindano yenye dawa au kitu ndani ikapitishwa mbele kidogo kupitia
sikioni, ...
‘Unaona
hii humu ndani kuna virusi, sijui vya ugonjwa gani mimi nimepewa maagizo kuwa
ulileta ubishe nikudunge nayo...kwahiyo endesha gari na kaa kimiya....’sauti
ikasema
Ilikuwa
onyo kwa Inspecta, na akilini akawa anawaza, inawezekana kweli ni kuna virusi,
au ni vitisho tu,lakini hakutaka kubahatisha, akaona ni bora kufuata anavyotaka
huyo mtu, akaendesha gari taratibu hadi hoteli ya Paradise, ...
Alipofika
maeneo haya mara akasikia mlango wa nyuma wa gari ukifunguliwa, na baadaye
kukawa kimiya, alipoona kimia kingi, na hakuna lolote linaloendelea akageuka
kuangalia nyuma, kwenye kiti cha nyuma yake, ambapo huyo jamaa alikuwepo,
hakuona dalili ya mtu.
Alijua
ameshateremka,..basi akafungua mlango na kutoka nje ya gari, akafungua mlang nyuma na kukagua akaona kitambaa kinachofanana
na viti vya gari lake kikiwa kimetandikwa kama shuka ina maana huyo jamaa
wakati yeye anaingia kwenye gari, alijilaza sambamba na viti akajiunika hicho
kitambaa kama shuka..
Akakitoa
na kukikunja akakiweka kwenye sehemu nyuma ya gari,na alipohakikisha kuwa gari
lake lipo vyema, akalifunga, na kuweka kufuli ya mtandao, ina maana hakuna mtu
yoyote anayeweza kulifungua mpaka awe na neno la siri.
Akatoka
na kuanza kutembea kuelekea sehemu ya mapokezi ya hiyo hoteli, na mara simu
yake ikaita, akaangalia, alikuwa mkewe...
*****
‘Unasema
kweli, uliwaona lini...?’ akaulizwa
‘Siku
hiyo nilikuwa zamu kwa mdada mmoja....’akasema
‘Hapana
huyo sio mume wangu ninayemfahamu mimi, ...hajawahi kunifanyia hivyo hata siku
moja...’alikuwa mke wa Inspecta Moto akilalamika kwa uchungu, na mwenzake
akamuangalia kwa jicho la pembeni huku akichekelea kwapani
‘Nilikuambia
wanaume hawaamaniki, wewe ooh, mume wangu ni muadilifu, oooh, mume wangu ni
mcha mungu, sasa kipo wapi, ipo siku nitakuletea picha zao utawaona `live’ wakifanya vitu vyao...’akasema
‘Lakini
wewe uliyajuaje hayo, na ulimuona wapi akifanya hivyo?’ akaulizwa
‘Mimi
ni mfanyakazi katika nyumba ya huyo binti Urembo,wanayemuita jembe, ni mfanyakazi
wake wa ndani, na siku hiyo, nilikuwepo huko kwenye nyumba yake ya Msasani,
japokuwa sifanyi pale nyumbani kwake mara kwa mara, huwa nafanyia kwenye nyumba
yake nyingine, ana nyumba yake mwenyewe kuacha hiyo ya kupanga...’akasema
‘Huyo
binti Urembo au Jembe sijui hana mume au mchumba?’ akauliza
‘Ana
mchumba, lakini wanawake kama hao watakuwa na mume bwana...hao wanawake
hawahitaji mume wa kudumu, leo ana huyu kesho ana yuke, ndio maisha yao yalivyo,
nilisikia tu akisema ana mchumba wake anasoma nje, mimi sijawahi kumuona...’akasema
‘Ningelimjua
huyo mume wake au mchumba wake...ohoooh..’akakatiza huyo mke wa Inspecta
‘Ina
maana na wewe ungalimfanyizia au sio,...hahaheeeh?’ akauliza huyo shoga yake na
kucheka kwa dharau
‘Sasa
na hiyo ya kukutana na huyo mwanamke huko hotelini, mnasema inaitwa hoteli gani
sijui umesema...?’ akauliza
‘Paradiso,
au paradise humo kuna starehe za kila namna, ukumbi za mikutano, vyumba vya
kupanga, na kila aina ya jambo unaloweza kulihisi linapatikana humo, hiyo
hoteli ni kubwa na ina eneo kubwa, huwezi amini, kuna mpaka nyumba za ibada
humo, ...’akasema
‘Humo
humo ndani kuna nyumba za ibada!? Za nini na wakati inavyoonekana ni hoteli ya
ufusuka?’ akaulizwa
‘Wenzetu
hawa ni wajanja, wao wana kila mbinu ya kuingiza pesa, huyo mtu anataka kila
aina ya shughuli inayoingiza senti aifanye yeye kwenye miradi yake, kila aina
ya kipaji, ikiwemo hiyo ya karama, maombi sijui....anataka zote awe nazo...’akasema
na kutulia kidogo.
‘Ni
kuambie ukweli, hizo nyumba za Ibada ni vitega uchumi vyake, kuna watu
wanajiita wana karama, za kutibu kuponya, kuombea, basi wao ndio wanaendesha
hizo shughuli, wanapata chao na mwenye jengo au kitega uchumi anapata chake....’akasema
‘Hiyo
sasa ni kumkufuru mungu...’akasema
‘Wao
wanasema wameambiwa watafute riziki, na wasiofanya kazi hawatakiwi kula au sio,
sasa wanye kazi za kumtumikia mungu watapata wao kula yao kumbuka hao wapo
kwenye nyumba za ibada kuwasubiri waumini au sio...hebu jiulize watapata wapi
kula yao, kama wasiokusanya kinachoitwa sadaka, ....ina maana wao hawahitaji
maisha mazuri, kuoa, kuzaa, kutembelea magari mazuri, wao kama binadamu
wanahitaji hivyo vitu vyote au sio...’akawa kama anauliza
‘Hiyo
sio kweli, huko ni kujidanganya kwa mungu, na mungu hadanganyiki...’akasema mke
wa Inspecta.
‘Hahaha,
wao wana malengo yao, bwana...sikio, kumbe, kuna watu hao wenye karama, ambao huonyesha
miujiza yao, na watu wanaikubali, iwe hata mazingaumbwe, yeye akaona ohoo,
kumbe nako huku kunalipa..., akakibuni hicho kitengo, akajua kumbe watu
wakitoka makazini wakapitia hapo hotelini kwake, wakala, wakastarehe, lakini
bado wanamuhitajia mungu wao, wanahitaji kuombewa, kutubu dhambi zao, basi
wanaingia kwa hao wataalamu wake wa maombezi, wanaombewa...hahaha...jamaa
mjanja huyo...’akasema huyo shoga na kucheka
‘Sasa
yeye anapata nini hapo?’ akauliza
‘Hutaamini,
sehemu hizo zinaingiza pesa kama nini, kuna wataalamu wa kutoa maneno ya mvuto,
wana mbinu za kumpagawisha mtu, mpaka anatoa senti zote alizokuwa nazo mfukoni,
...watu hao wamefundishwa nchi za nje, walikwenda huko huko kunakosifika kwa
hizo dini, wengine wametoka huko Nigeria, unakufahamu kwa sifa zake, wengine wapi
huko sijui, wanakopigana vita kila siku, wengine mashariki ya kati, wanajua
lugha za huko za ushawishi kama wamezaliwa na hizo lugha ..’akatizama saa yake
‘Kwahiyo
kwa vile wabongo wengi hawakusoma, na hawataki kusoma wakisikia hizo lugha
wanajua ni kweli,eeh ...ndivyo wanavyofanya hivyo eeh...?’ akauliza
‘Kama
ulikuwepo, hao jamaa wanajua kila lugha za kimataifa, na hapo ukimkoga mbongo
kwa lugha za nje, ooh, wewe waonekana msomi kweli, wewe unajua dini kweli, wewe
unajua..yaani we acha tu, wakichanganya na
mazingaombwe yao, watu wakapagawa,...sijui wanafanyeje bwana, watu wenye
mapepo, wanapandisha, eeh, na utaona wenye mapepo wanapona kabisa....’akasema
‘Hahaha,
hao basi wana mapepo makubwa ambayo yanagopa hivyo vipepo vidogo, ni yale yale
ya mtu kwenda kwa mganga wa kienyeji, waganga wa kienyeji wengi ni wachawi,
wanachofanya ni kutoa na kupandikiza, unapona leo kwa uchawi wa mwanzo , na kesho
unaumwa kwa uchawi wake aliokuwekea ili urudi tena...mimi siamini hayo, lakini
yote ni ushirikina tu...’akasema
‘Sasa
wenzako wakajua kuwa huko nako kuna namna ya kupata vijisenti, watu wanafika na
magari ya kifahari kuombewa, kufanyiwa makafara ya kupata utajiri, na sijui
inakuwaje, kesho na kesho kutwa, unawakuta watu hao ni matajiri kweli,...pia
wana namna ya kujitangaza, kwahiyo hutaamini wanaohudhuria hapo kwenye nyumba
hizo za ibada zao ni watu wakubwa, matajiri, na nasikia wana chama chao, wana
nembo yao, ipo kama dunia hivi....’akasema
‘Kama
dunia kwa vipi?’ akauliza mke wa Inspecta
‘Niliiona
wakati nafagia kwa huyo mdada mrembo, ipo dunia inazunguka, ina ramani za nchi,
kama ile wanayotumia watoto mashuleni, si unaifahamu dunia ya kusomeshea watoto
shuleni ilivyo,....’akasema
‘Lile
tufe la dunia linalozunguka?’ akauliza
‘Eheeeh,
hilo hilo, basi hiyo ndio nembo yao, halafu mara kunatokea mikono mbali mbali,
ile mikono ni fani za watu, vipaji vyao, maana inaonyesha mkono ule una
komputa, ule una vifaa vya hospitali, ule una watu wa dini, waheshimiwa, akina
mama warembeshaji na kila aina ya kazi...inakuwa mikono mingi, ambayo baaaye
inakuja kukutana kwenye lile tufe inashikilia lile tufe...na sauti ya ya
kutisha, inasema
‘Dunia
yangu...’ na maandishi hayo ya dunia
yangu, yanakuja na kuizungua ile dunia, halafu anatokea jamaa mmoja kakaa
kwenye kiti, akiiangalia hiyo dunia yake, nasiki huyo ndiye tajiri mwenyewe....’akasema
‘Yupo
wapi huyo tajiri mwenyewe?’ akaulizwa
‘Mimi
sijui, ...maana sijawahi kumuona,wengine wanasema yuko nchi za nje, wengine
wanasema ni marehemu lakini mizimu yake ndiyo inafanya kazi, wengine wanasema
yupo humu humu nchini, lakini hajulikani ni nani...hata mimi simjui...’akasema
‘Nikuulize
umefanya kazi kwa huyo mdada kwa muda gani?’ akaulizwa
‘Nina
miaka mitano kwa huyo mdada, kabla ya hapo, nilikuwa nafanya kazi kwa mama
mmoja ambaye tulikuja kukosana naye maana mtoto wake ni muhuni, alikuwa akitaka
kutembea na wafanyakazi wa humo ndani, mimi nikaona siwezi kuzalilika,
nikaondoka zangu..’
‘Mama
gani huyo?’ akaulizwa
‘Aaah,
hata sina haja naye tena, japokuwa sasa ni tajiri kweli, ..nasikia ana hisa
kwenye hiyo hoteli ya Paradise, sasa sijui kwa vipi, ..’akasema na kuangalia
saa kwenye simu yake
‘Shoga
yangu unajua natakiwa kuingia kazini, nina zamu ya usiku, mimi naondoka, ila
ninachokushauri, kama unataka kuthibitisha hayo niliyokuambia kumuhusu mume
wako, nenda jioni hii, jifanye unapita, au unashida kwenye hiyo hoteli,
utamuona mume wako akiwa na huyo kimwana...’akaambiwa
‘Mimi
sitaki wala kumfuatilia, ataniumiza kichwa changu bure, kama ni umalaya wake,
aendelee nao tu, na mimi nitajua ni kitu gani cha kufanya, nataka nianzishe
miradi yangu, ..ile uliyonishauri, kuna rafiki yake huyo mume wangu, kasema
anaanzisha miradi ya kuwasaidia akina mama , sasa nataka nijiunge na mimi..’akasema
‘Hapo
umelenga kwenyewe, hata mimi nimesikia na mimi nitajiunga huko huko, tutakutana
huko huko.....’akasema
‘Lakini
mume wangu hataki...’akasema
‘Ndio
hayo hayo niliyokuambia, ....mimi naondoka, kama upo tayari tuongazane maana
mimi hiyo hoteli naifahamika sana, nitakuelekeza wapi pa kumpata huyo mume wako
ushuhudie mwenyewe kwa macho yako, akila raha na huyo mrembo...’akasema
‘Ooh,
kweli eeh, utanisindikiza eeh, hilo neno,...kama ni hivyo ngoja nijiandae
twende...nikajionee mwenyewe na nikimuona ama zake ama zangu,...utaona vumbi
langu...’akasema na kuingia ndani kujiandaa na huyo shoga yake akachukua simu
yake na kuandika ujumbe wa maneno
‘Keshaingia
kwenye mtego, anakuja kazi kwenu...’
WAZO LA LEO:Unaposaidia mtu, kwa
jambo lolote lile, hutakiwi kumtangaza kuwa umemsaidia huyo mtu, au kuja
kumyanyapaa tena kuwa wewe ndiye umemsaidia kama sio wewe asingelifanikiwa kwa
jambo fulani au angelikua njaa, au asingelipona na vitu kama hivyo.
Pia
unapofanya jambo lenye manufaa kwa jamii kama msaada, haina haja ya wewe kujitangaza
na kujinadi kuwa wewe ni mfadhili wao, kama usingelikuwa wewe hilo jambo
lisingelifanyika, huo sio uungwana, huo sio msaada tena hiyo ni biashara yenye
masharti. Msaada wa kweli hauna masharti, msaada wa kweli ni kama sadaka, ambayo
inatakiwa ukiitoa kwa mkono huu, mwingine usifahamu.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment