Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, August 25, 2014

DUNIA YANGU-22


'DUNIA YANGU’

‘What,..dunia yangu..ana maana gani ?’ .....akakumbuka hiyo nembo aliiona wapi, kule kwa mdada, na kwenye CD, aliyoichukue kule kwa mtaalamu wa komputa kwa uficho...akajikuta akijiuliza mara nyingi,...


‘Hii ina maana gani?’ 

mara akasikia mlango ukisukumwa akageuka kuangalia ni nani alyeingia asubuhi hiyio, na kujikuta akiangaliana na Inspecta mwenzake ....

 Tuendelee na kisa chetu...

                           ************
‘Umeshapona mkuu...?’ ilikuwa sauti ya Insecta Maneno, akiwa kashikilia mikono kifuani kuonyesha kuwa hana wasiwasi, lakini macho yake yalikuwa uakiangalia komputa yake ya mezani, Inapecta alimuangalia rafiki yangu, akaona jinsi mwenzakew alivyobadilika, afya yake na usoni alionekana mtu mwenye kurizika, tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, sijui karizika na nini.

‘Oh, unajua leo nimeona ajabu sana, nimefika hapa asubuhi na kushangaa kusikia na wewe siku hizi unafika asubuhi na mapema, vipi kuna dharura gani?’ akauliza Inspecta

‘Wewe ulikuwa haupo, na unavyojua wewe na mimi ndio tuna kazi nyingi kwenye kikosi chetu, ..kwahiyo inabidi niwajibike, sikutaka ufike ukute mlundikano wa kazi, hata hivyo, ..nimerudi kidogo kuna kitu nilisahau...’akasema

‘Ulisahau kuzima komputa yako au sio?’ akauliza na Inspecta kwa haraka akaelekea kwenye komputa yake na kusema;

‘Oh, Mbona imezimika!?’ akasema kwa mshangao

‘Nilifika na kuikuta kama ipo haijazimwa, maana kitaa cha kuashiria kuwa haijazimwa kilikuwa kinawaka, na wakati nataka kuhakiki, ndio ukatokea,...’akasema

‘Ok, hamna shida, naona imeshajizima, ilichelewa kuzimika yenyewe, niliacha ikiwa inaendelea kuzima, nikaharakisha kwenye dharura zangu, mambo ya kifamilia, si unaelewa tena....’akasema

‘Kwani shemeji karudi?’ akauliza

‘Bado ana vikao vyao huko kwao, mke wangu ni mtu wa shughuli, na hapendi kuwa mbali na shughuli, kila shughuli yumo, sasa imenijia akili, kama anapenda shughuli, inabidi nibuni miradi ya kumshughulisha....’akasema na huku anawasha komputa yake tena.

‘Kama ipi..?’ akauliza mwenzake.

‘Yeye si mama shughuli, na mimi naanzisha mrdai wa shughuli, namuanzishia mradi ambao yeye atausimamia, nikitafuta na akina mama wengine majembe wa kumsaidia,...unajua mkuu, tusikalie kuwazia ajira tu, hiiz ajira zetu zina mwisho wake, na mwisho wa sisi tuliobobea kwenye ajira mara nyingi inakuwa ni mbaya, unaacha kazi huna cha kukuendeleza, unakuwa kama unaanza maisha mengine upya...’akasema

‘Ok,..sasa tufanyeje...?’ akauliza na hilo swali likamfanya mwenzake amuangalie Inspecta kwa macho ya udadisi, maana siku zote akianza kuongea mazungumzo kama hayo mwenzake anakuwa kwenye kupinga tu.

‘La kufanya ndio hilo, tuwaanzishie wake zetu miradi, tunachotakiwa kuangalia ni je mke wako ana kipaji gani, kama ni msusi, muanzishie mradi unafanana na hivyo, kama ni mama shughuli kama mke wangu, unamuanzishia mradi wa shughuli, unamjengea mazingara ya shughuli, kama ni ukumbi au ofisi, unaangalia ni kitu kinahitajika kwenye shughuli, unatafuta mtaji, unamuanzishia, cha muhimu kwanza ni kumuelismisha hata ikibidi kumpeleka shule...’akasema

‘Ni wazo zuri, siwezi kukukatalia, lakini je ataelewa, maana unaweza ukatumbukiza sukari baharini, unatategemea nini hapo...mimi hilo la shule kwanza nakuunga mkono, ili ajua ni kitu gani anakifanya, sio kujaribu, .....eeh, au...?’ akasema na kuuliza na Inspecta Maneno akaona mwenzake anakuja kwenye anga zake, akasema,

‘Ndio hapo nikasema ikibidi unampeleka shule, kuna semina za kuwekeza, kuna shule za kuwekeza pia, zipo nyingi tu siku hizi, ni pesa yako tu,....kwa mfano nikuambie  kuna huyu tajiri mmoja eeh,...sijui kama unamfahamu, yeye keshabuni hilo wazo, kaanzisha shule za namna nyingi, na anatoa semina na wakati mwingine bure, akilenga vipaji vya watu....’akasema

‘Tajiri yupi huyo?’ akauliza Inspecta kwa mashaka, lakini akijifanya anataka kujua

‘Huyu..eeeh, bwana Diamu, huyu jamaa kichwa, kabuni miradi mingi kutegemeana na vipaji vya watu, ukimuona navyofanya utazani anapoteza pesa zake bure kumbe ana malengo mapana, anaanzisha mradi huu, anawafundisha watu, ....kwa malengo maalumu, ambayo mwisho wa siku ana[ata nay eye chochote humo...’akasema

‘Umesema tajiri gani?’ akaulizwa

‘Diamu....ushamsikia?’ akaulia

‘Namsikia tu, sijawahi kumuona, kweli yupo hapa nchini?’ akauliza

‘Ana watu wake, yeye ni muelekezaji tu, ana vichwa vingi vyenye vipaji, watu hao kwa vipaji vyao, wanatumia mikono yao wanazalisha...kwa kupitia wao, ananeemeka, na wao wananeemeka, ndio kujiajiri huko, ukikalia hizi kazi za mshahara usiokidhi mahitaji , utakufa masikini....’akasema

‘Sawa sasa hebu niambie wewe utawezaje kuelekeza nguvu zako kwenye miradi huku unatakiwa kuwajibika ofisini, utagawaje muda wako...?’ akaulizwa

‘Hilo mbona linawezekana,...mfano ndio hivi nawahi ofisini mapema, najipanga , najua mwenyewe jinsi ya kufanya, kiasi kwamba siharibu kazi za watu...’akasema

‘Kwa ufupi haiwezekani, unachofanya ni kuiba muda wa watu wa kazi, kwa manufaa yako, au sio?’ akaulizwa

‘Sasa hebu niambie utafanyaje, kama ni hivyo, ili usifanye haya yote, watoe mshahara wa kukidhi mtakwa ya wafanyakazi wao,...kama wangekuwa na haki, wasingelitoa marupurupu mengi kwa watu wachache, wangatoa kiasi na kiasi kingine wakaelekeza kwenye kipato cha wafanyakazi wa chini..hili halipo, kwa vile wao wanajifikiria wao wenyewe....’akasema.

‘Haya bwana, sasa niambie kwa jinsi gani utamuwekea hiyo miradi mkeo, au unamtegemea huyo huyo tajiri ?’ akaulizwa, na hapo Inspecta akakukunja uso kidogo, inaonekana kauli ya mwenzake hakuipenda, ila hakuvunjika moyo akasema;

‘Sio kumtegemea huyo tajiri, yeye ametoa fursa, watu wajifunze, sasa utajifunza bure, ni lazima umlipe kwa vile kawekeza, ni ujanja wake...mengine yanayofuata ni wewe mwenyewe, sijui unanielewa...’akasema.

‘Sawa nauliza hivi utamuwekezeaje mkeo, utampeleka shule, au ulishamuandaa , na lini maana nijuavyo, yupo kwao, au,...hapo nataka kujua ili na mimi nifahamu...au na wewe unataka ulipwe ndio unielekeze na mimi...’akauliza na kucheka kama mdhaha, lakini inspecta sasa hivi hakuonyesha lile tabasamu lake la awali akasema;

‘Mimi namfahamu sana mke wangu, na nimeshampima, nikisema kwa hivi sasa nimpeleke shule hatutaelewana, yeye na shule ni kama maji na mafuta, mke wangu hapendi kusoma,...niliwahi kumshauri awalia akakataa...’akasema

‘Kwahiyo...?’ akauliza na kabla hajamalizia swali lake Maneno akasema

‘Japokuwa mke wangu hapendi shule, lakini ana akili ya kuzaliwa, ana kipaji cha kuongea, kwahiyo nitaelekeza nguvu zangu huko huko, ninachotaka kufanya kwa sasa ...nikumtafutia majembe, yaani akina mama wengine vichwa, ambao watashirikiana naye, kwa vile mimi natoa mtaji, na wazo na kila ...ofisi nk, basi yeye atakuwa msimamizi, kiongozi wao,...wewe mwenyewe utaona...’akasema

‘Na hao akina mama wengine utawapataje, maana nionavyo, unachotaka kufanya hapo ni ujanja ujanja utumie nguvu za wengine a,bazo unaziita vipaji kwa manufaa yako, na ukumbuke kiongozi ni lazima ajue elimu ya kuongoza, awe na hekima ya maamuzi, ili kuhakikisha haki inakuwepo, huoni kuwa ukimfanya mke wako kiongozi, wakati hana ufahamu wa huo uongozi, utasababisha kutokuelewana na wenzake, atakuwa anatumia nguvu kuliko hekima na akili?’ akaulizwa

‘Wewe utaona tu,..hiyo kazi ndogo, nimeshapata shule ya maana ya jinsi ya kuwekeza,na kuwaelekeza watu wa namna hiyo, mimi nitakuwa mwalimu wake,na mwalimu wao pia, ni kazi ndogo tu..’akatulia kidogo kama anawaza jambo.

‘Kidogo kidogo mwenyewe atakubali, ni njia ya kusaidiana, nitaona kama inawezekana, kigharama, wengine nitawapeleka semina au shule,...hilo nitalifanyia kazi,na njia mojawapo ya kuwavuta wadhamini,..unapata misaada kwa njia hiyo, ilimradi uwe na ushawishi, na ushawishi mkubwa kwa sasa ni kuona unawasaidia akina mama, wewe mwenywe utakuja kunivulia kofia...’akasema

‘Mimi bado nina mashaka, japokuwa nakuunga mkono na akili hiyo, lakini najiuliza jinsi gani ya kuwapata hao watu, ikizingatiwa kuwa ni wake za watu au sio, umesema wake, ina maana ni wake za watu, hujasema lolote kuhusu waume zao, usije kuleta mifarakano, uwe makini na hilo...’akaambiwa

‘Hahaha, unajua mkuu, unajifanya kama huelewi, hao akina mama wenyewe watajileta...tatizo unashindwa kunisifia tu, si unakumbuka tabia yangu, nikitaka jambo ni lazima nilpate, na wazo hili ni lazima nilifanyie kazi na nitafanikiwa tu, anyway,, ...samahani kuna jambo jingine nimefuatilia hapa naona muda umekwenda, inabidi niharakishe kabla kazi hazijaanza, unaonaje tukija kuliongelea hili swala kwa nafasi yake, ....’akasema akisogelea komputa yake, na inspecta akaelewa kwanini mwenzake anasema hivyo

‘Hamna shida mimi nipo ofisini kwangu, ukimaliza tutaongea, hata mimi nina mambo muhimu nataka kuongea na wewe,...’akasema Inspecta Moto

‘Mmabo gani tena hayo, ya kikazi au ni haya haya tuliyokuwa tukiyaongelea...?’ akauliza Maneno kwa wasiwasi, akimuangalia Inspecta mwenzake.

‘Mimi nilikuwa sipo,...siku mbili hizo, sasa nitajuaje umefikia wapi...’akasema Moto

‘Ok, ok, nimekuelewa, nilifikiri kuna jambo jingine maana na wewe bwana huachi kujilimbikizia kazi hata sizizo na maana, ...kama ni hivyo, nitakupa muhutasari wa niliyofanya na nimeishia wapi....’akasema akiendelea kufanya analolifanya.

‘Sio kweli kuwa najilimbikizia kazi zisizo na muhimu, hizo kazi ni wajibu wetu, ila tunapenda kuziacha mpaka zipate msukumo fulani, sio vyema, mimi sipendi hivyo...’akasema

‘Nikuambie kitu, achana na tabia hiyo, utajizeesha muda si wako, angalia mbele, maisha yalivyo, ...maisha ni mafupi, muda wa kufanya mambo hautoshi,sasa hivi utafikia muda una majukumu mengi, huna miradi, huna akiba, watoto wanahitaji ada, majukumu ya kifamilia, ya kijamii, yanaongezeka, mshahara ni ule ule mwisho wake ni nini kama sio kufa kwa shinikizo la damu, fanya kazi kwa wasaa, jipe muda wa kutafakari mambo yako...’akasema

‘Unasema kufa kwa shinikizo la damu, mmmh, kama alivyokufa muheshimiwa au sio...?’ akauliza Inspecta

‘Hilo umesema wewe, ..’akasema akionyesha kutaka muda wa kufanya mambo yake.Na Inspecta Moto akawa anataka kuondoka, lakini kabla hajasogea mwenzake akamuuliza swali;

‘Kwa vile umegusia swala la muheshimiwa, hebu niambie vipi mipangilio yako maana kwenye kikao na wakubwa mimi niliwaelezea hali halisi...’akasema Maneno

‘Hali halisi ipi, maana nikumbukavyo, bado tulikuwa kwenye kukusanya ushahidi...na sijapitia hayo maelezo uliyopeleka kwa wakubwa...’akasema Moto.

‘Ushahidi upi zaidi ya huo wa madakitari, kuwa kweli muheshimiwa alikufa kwa shinikizo la damu, na ndivyo nilivyopeleka taarifa yetu, na nimesema tumekubaliana hivyo, mimi na wewe, utaona taarifa yangu, fupi, na yenye umakini wa kitaalamu...hakukuwa na zaidi, na wao wakasema sawa,...’akasema Maneno

‘Wakasema sawa, kirahisi hivyo, hawakutilia mashaka, maana kwa hali ilivyo, hata mimi ningelitilia mashaka, kama kweli unamfahamu huyo muheshimiwa...walikubali kirahisi hivyo?’ akauliza Inspecta kwa mshangao

‘Kwani wangelisema nini, wakati vitu vipi wazi, je wewe unapingana na taarifa ya madakitari, je wewe unapingana na familia husika, mashahidi tuliowahoji,....hebu niambie kama familia husika wanahisi mtu wao kafa kifo cha utata wangelileta malalamiko kwetu, je walifanya hivyo, ina maana wao wamerizika na kifo cha jamaa yao kuwa kafa kifo cha kawaida, sasa wewe unataka kufanya nini, tusiendelee na malumbano yale yale,...oka, nona uniache, nina kazi nataka kufanya...’akasema

‘Wewe ndio umeanzisha hiyo hoja...nilikuwa sijajipanga kuliongelea hilo, na kwa vile umeligusia ni vyema tukawekana sawa, ninachosigishana na wewe ni ile kusema tumekubaliana, hatukuwahi kukubaliana kwa hilo,....’akasema Inspecta Moto.

‘Nimefanya hivyo , kwa nia njema kabisa...kuweza wewe kutuliza kichwa na kuangalia mambo mengine kwa nia njema kabisa kwako wewe na kwa majukumu yetu pia, kuna mambo mengi ya kufanya, kwanini tupoteze muda kwa kitu ambacho kipo wazi, ina maana mimi nimefanya vibaya, ?’ akauliza akionyesha mshangao

‘Siwezi kusema umefanya vibaya au vizuri, tatizo hapo ni kuwa hukunishirikisha kwenye hiyo taarifa, mimi ningekushauri nionavyo mimi, wewe ulichofanya ni kukimbilia kutoa hitimisho lako binafsi na kunishikirisha na mimi, ...hilo ndilo tatizo...’akasema

‘Ok, sasa unataka kusema nini?’ akashika vidole viwili karibu na shavu, huku akimuangalia Inspecta mwenzake.

‘Umeshapeleka hiyo taarifa kwa wakubwa na mumekubaliana iwe hivyo,mimi nitasema nini hapo,....na hali ilivyo, yaonekana inatakiwa iwe hivyo, mimi inaniuma sana kuona haki na ukweli unapindishwa...’akasema

‘Haki ipi na ukweli upi uliopindishwa mkuu,...hebu nipe ufafanuzi wa kitaalamu, maana wewe ni mkufunzi, na unajue vyema ni kitu gani kiwepo, ili kushinikiza hoja, haya nipe hoja yako ya kitaalamu...’akasema

‘Unajua mimi mpaka kesho sikubaliani na hiyo kuwa muheshimiwa amekufa kifo cha kawaida, kuna hujuma zipo, na zimetengenezwa kitaalamu, ili iwe hivyo,na watengenezaji walijua hizo hoja zitalindwa vipi.....sasa mimi nilitaka hili tulifanyia kazi ili hali hiyo isije kujirudia tena...’akasema

‘Una uhakika na hiyo kauli yako, maana usiseme tu, nipe uhakika wako na ushahidi wako wa kitaalamu,....ili nikuelewe’akasema Maneno

‘Ndio nilitaka kulifanyia kazi hilo, siku mbili hizi nimejikuta nashindwa kulifanya hilo 
kwasababu zilizokuwa nje ya uwezi wangu....’akatulia

‘Sababu za kuumwa sio, au kuna jingine lililokuzuia,...?’ akauliza Maneno

‘Unajua mimi sikupendezewa kwa wewe kupeleka hitimisho hilo kwa wakubwa, mimi na wewe tulitakiwa tuwe kitu kimoja, unakumbuka tumetoka mbali, sasa iweje ifike mahali tuanza kuachana njia panda...hebu niambia tatizo hapo ni nini, unakumbuka kiapo chetu, kuwa tupo tayari kufa kwa ajili ya kusaidia watu...kiapo hicho kimepotelea wapi...’akasema Moto

‘Sijakuelewa unataka kusema nini hapo...’akasema Maneno akiwa hamuangalii Moto, akawa anafanya jambo kwenye komputa.

‘Huwezi kunielewa kwasababu wewe umeshaamua, na hatua uliyofikia, umesharizika nayo, huwezi kuona tena uchungu,...lakini kumbuka mwenye kovu usidhani kapoa, kumbuka dhuluma haidumu, kumbuka,kiapo ni ahadi...’kabla hajamaliza, Inspecta akasimama na kusema;

‘Unajua sikuelewi, kwani unanishuku nini mimi...?’ akauliza kwa hasira

‘Sijakushuku chochote usijihami, ila nakutahadharisha, ...unakumbuka siku zetu za mwanzo, hilo la kuambiana ukweli ndio ilikuwa msimamo wetu, mwenzako akitetereka unamuonya hapo hapo, ili tuwe na msimamo mmoja, je upo kwenye kile kiapo au kuna namna nyingin inakusukuma ufanye vinginevyo...’akasema

‘Kama vipi nimefanya vinginevyo, nionyeshe kosa langu lipo , ni huko kupeleka taarifa ambayo wewe unaona haijakamlika, au kuna jingine unanishuku?’ akauliza kwa sauti ya juu kidogo.

‘Bwana wewe endelea na kazi yako tutakuja kuongea ukiwa umetulia, ...’akasema Inspecta na kuondoka, na Inspecta mwenzake akabakia amesimama akimuangalia mwenzake akiondoka, akawa kama anawaza jambo, akashika simu yake na kupiga namba..

******

‘Mume wangu, leo ujitahidi kufika nyumbani mapema...’ilikuwa sauti ya mke wa Inspecta Moto.

‘Oh, mke wangu, unajua ndio nimefika kazini na siku mbili nilikuwa na hiyo mitihani ya kufuatilia jambo, sasa nimejikuta nina kazi nyingi za kufuatilia hapa ofisini, sizani kama nitaweza kuwahi kwani kuna nini cha zaidi?’ akauliza

‘Unasema una siku mbili hujafika kazini,...ulikuwa wapi, mimi najua ni hiyo siku moja?’ akauliza mkewe kwa wasiwasi.

‘Siku hiyo nyingine nilikuwa kwenya kufuatilia jambo, sikuwaeleza wenzangu, hayo ni maswala yetu ya kazini wewe niachie mwenyewe, niambie kuna kitu gani muhimu unachohitajia mimi kuwahi?’ akauliza

‘Kuna kitu gani muhimu?!, yaani mimi mkeo nakuomba uwahi unauliza kuna kitu gani muhimu!, na nakuomba muda ambao sio wa kazi, ..mume wangu mbona unabadilika hivyo kuna nini kinachoendelea, ....?’akauliza mkewe

‘Ni maswala ya kazini tu, nitakuja kukuambia kwa wakati muafaka...ila nahisi sitaweza kuwahi kufika nyumbani labda kama kuna swala muhimu sana...’akasema

‘Sasa ni hivi, mwenzako kanialika kutembelea miradi yake, nia ni kunivutia na mimi niweze kuwekeza, sasa hivi akina mama wana miradi yao, wanasaidiana na waume zao, nimeona ni jambo jema tukiongozana na wewe ukajionee mwenyewe ....’akasema

‘Mwenzangu yupi?’ akauliza kuonyesha mshangao, na akilini akajua ni yale yale ya Inspecta mwenzake.

‘Mwenzako yupi tena, si Inspecta rafiki yako....’akasema mkewe

‘Lakini mkewe si hayupo, atakualikaje wewe bila mimi kunihusisha, mbona nipo na yeye hapa ofisini hajaniambia kuwa atakualika wewe,....?’ akauliza

‘Mangapi,mumekuwa mkifanyiana kama ndugu na tulikuwa tunaitana uwepo au usiwepo, wewe unatoka na mkewe na mimi natoka naye tukiaminiana kabisa leo mbona unauliza hivyo, ile hali ya kuaminiana imeishia wapi, mbona mimi sielewi, kuna nini kimetokea....’akasema mkewe

‘Lakini tulikuwa tunambizana mimi na mwenzangu, sizani kama ilikuwa inatokea tu, bila kujulishana kinachoendelea, je uliwahi kuitwa au kwenda naye mahali bila mimi na yeye kuliongelea kabla,  hili naliona kama lina ajenda ya siri..’akasema

‘Kama ni ajenda ya siri umeianzisha wewe mwenyewe, maana leo unasema utachelewa kikazi, lakini sio kweli, kuna sehemu unakwenda kukutana na mtu, na nahisi mtu mwenyewe ni mwanamke ni kweli si kweli, na huyo simuamini kabisa, je tuliwahi kukubaliana hilo ....’akasema mkewe kwa sauti ya kulalamika

‘Nani kakuambia hayo, nani kakumbia huo uwongo, toka lini ukanitilia mashaka katika maswala yangu ya kazini, umeanza lini hiyo tabia mbaya, sasa nasema hivi huko unapotaka kwenda usiende, mpaka nitakapo-ongea na huyo, mwenzangu, kama kweli ana nia njema na wewe....’akasema

‘Hahaha mume wangu, naona huo sasa ni wivu, halafu unamuonea wivu rafiki yako kipenzi, au urafiki wenu umekwisha lini,..mimi hapo mahisi kuna jambo, na mara nyingi mtenda anaogopa sana kutendewa, nahisi kuna kitu kinaendelea,..sasa ufanyavyo wewe unahisi hata wewe utafanyiwa....’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza Inspecta kwa sauti ya hasira.

‘Unaelewa sana, ...ukikutana na huyo mnayeenda kukutana naye utalijua hili ya kuwa nina maana gani,...ukumbuke hilo tu, na ujue vyema mara nyingi mtenda akitenda, huishi kwa mashaka, na kila mara anahisi na yeye anatendewa hivyo hivyo....;akatulia

‘Mke wangu ina maana huniamini, mimi ninayofanya ni sehemu ya kazi yangu, naweza kukutana na watu wa aina tofauti, lakini mara zote nachunga mipaka ya ndoa yangu, hebu niambie ni nani kakutumbukizia hzio fitina...?’ akaulizwa

‘Fitina!, hakuna cha fitina hapo bali ni ukweli ninaousema, si zaidi....’akasema na kutulia

‘Mke wangu, haya yameanza lini , mbona sio mara ya kwanza kuchelewa  au kukutana na watu tofauti, na haya yote nayafanya kutokana na kazi yangu ilivyo, siwezi nikakuambia kila kitu, maana kazi yetu ina mitihani mingi....’akasema

‘Usitumie kisingizio cha kazi yako, nyie wanaume mnapenda kujiendekeza, unadai kazi kumbe una mambo yako, ila nakuambia ukweli ipo siku utaumbuka,....’aasema wa hasira mkewe, na kabla mumewe hajasema kitu, akasema

‘Kila laheri, sina zaidi, utanijulisha mkielewana na mwenzako,kuwa niende au nisiende..kama sitakwenda basi mimi nitakuja huko huko unapokwenda kukutana na huyo aliyekuita....’akasema na simu ikawa haipo hewani.

‘Kuja...kufanya nini....?’ akauliza lakini kumbe mkewe hakuwepo kwenye mawasiliano, simu ilishakatwa na Inspecta akainua kichwa na kuanalia mlangoni, akamuona Inspecta mwenzake kasimama, kwa msimamo wake ule ule akimuangalia,na tabasamu la dharau mdomoni ...


WAZO LA LEO: Dharau na kiburi sio tabia njema, ikitokea wewe unacho, au unaweza, zaidi ya wenzako, basi mshukuru mola wako, na waone wenzako kwa jicho la huruma, wasaidie kadri ya uwezo wako, lakini usijenge tabia ya kuwadharau na kuwakebehi wenzako, na hata kuwaona wao eti ni wazembe, hicho ni kiburi, na kiburi sio uungwa mwema, maana aliyekupa wewe ndiye aliyewanyima wao, yeye huyo huyo aliyekujalia, ukapata, ndiye huyo huyo anayeweza kukunyanganya ulicho nacho na kuwapa hao unaowadharau. Mifano ipo hai chunguza utaona, na mwenye akili ataelewa.

Ni mimi: emu-three

No comments :