Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, August 22, 2014

DUNIA YANGU-21


Inspecta aliondoka mapema sana kuelekea ofisini, ni kawaida yake kuwahi ofisini, hasa akiwa na kazi inayomtinga sana. Lakini kwa vile ilitambulikana kuwa alikuwa mapumziko ya kuumwa, asingelitakiwa kuwahi hivyo.

Akilini alikuwa na mengi ya kufanya, na yote yalihitaji tahadhari, kwahiyo akaona ni vyema afike ofisini kabla watu hawajafika, apitie mambo fulani fulani na kuyaweka sawa, akajenga nadharia ya kufanya kazi ukiwa na nyuso mbili katika utendaji wake kuanzia sasa hadi hapo atakapoona mwisho wake, alijua atashinda tu, hata kama itachukua muda zaidi ya alivyotaka iwe, cha muhimu ni kujifanya yupo kote kote.

‘Inabidi nifanye hivyo,..sina jinsi, na nitaona jisni gani nitakabiliana na hili tatizo, najua nipo peke yangu, na sioni wa kumuamini kwa sasa, lakini huko mbele nitapata mshirika...’akasema kimoyo moyo.

Akafika maeneo ya ofisini, na kusalimiana na walinzi wa zamu, hakuongea nao sana, na hakuhitaji kuangalia nani kafika, alijua muda kama huo ni nadra sana kwa wafanyakazi kuwepo ofisini, inatokea tu kama kuna kazi ya dharura.

Akaingia kwenye ofisi yake, ambayo mwanzoni alikuwa akichangia na huyo inspecta mwenzake lakini baadaye kutoka na majukumu ya kikazi wakapewa kila mtu na ofisi yake. Alipofungua mlango, akasimama na kuegemea huku ngumi kaweka ukutani, na kuigemea kwa kichwa huku akiwaza afanya nini..

Akaona kuwaza haisaidii, akaiendea meza yake na kukaa, kwanza akapitia kwa haraka kazi zake hakujali kama kuna mtu kazipitia, ni kawaida kama mtu anahitaji kitu anaweza kuingia kwenye ofisi ya mwenzake akachukua anachohitaji au hata kufanyia kazi, ilimradi hagusi kazi za mwenzake.

 Hakujali sana kuangalia kama kuna mtu alipitia kazi zake, na kama yupo atakuwa Inspecta mwenzake, yeye alichojali ni jambo ambalo lilimfanya afike hapo ofisini mapema, na akalitafuta makabrasha yanayohusiana na kesi iliyokuwa mbele yake, akayapitia hadi pale alipokuwa ameiahia,...

Akatoa karatasi za alizokuwa ameweka kuhusu utafiti wake na watu aliowahoji na kuweka nyingine ambazo zilikuwa za awali kabisa kuwa kesi hiyo haina mshiko, kwani marahemu alikuafa kifo cha kawaida...

Alipomaliza, akachukua jalada jingine, akalifungua na kuandika ` kazi maalumu, akaziweka zile karatasi na kuandika mambo fulan fulani aliyotaka kuyaandika na alipohakikisha ameandika kila kitu, akatoa ile CD, ni nakala moja aliyoweza kuichukua kwa siri, kwa yule jamaa wa komputa aliyemkuta kwa yule mdada.

Akaiweka na ikaanza kufanya kazi,..kitu cha kwanza kuonekana ni nembo ya dunia na maandidhi makubwa ya ‘Dunia yangu...’ halafu kukaanza maelezo ya mbali mbali ya miradi, ..ilikuwa kama mradi uliobuniwa, ambao lengo ni kuzalisha na kuwekeza, na kuwavuta vijana kujiunga,..ulindikwa vizuri sana, na mikakati mizuri..

‘Hii mikakati ni mizuri sana, lakini hii nembo ina maana gani, je hii ni taasisi au kampuni ya mtu binafsi...?’ akajiuliza na wakati anajiuliza mara simu yake ya mkononi ikaita, akaangalia na kuona mpigaji hajulikani, hakuna namba, akahisi inaweza ni simu kutoka kwa wahasimu wake,...akasita kuipokea, lakini akasema;

‘Kwanini niogope bwana,..’akaipokea na alipoiweka sikioni akasikia sauti, sauti ambayo ilimfanya mwili uzizime, na kuanza kukumbuka mambo mengine, ..

‘Baby naomba tukutane Paradise hoteli, jioni, ukitoka kazini...’akasikia sauti, na kabla hajasema lolote simu ikakatwa...

‘Baby,....nani baby wako..na ananitaia nini huyu mwanamke...ooh, hili sasa ni tatizo..anyway tutaona huko mbele.....’akasema huku akiiangalia ile simu, lakini mwili ulishanyong’onyea kutokana na ile sauti, na hisia asizozitaka zikamtawala,..akajaribu kuondoa hayo mawazo kwa kuendelea kuangalia ile CD’s..

Hakupata maelezo zaidi, zaidi alielekezwa kufungua mtandao wao, na hata alipofungua mtandao wao aliona maelezo hayo hayo, na walisema ukitaka zaidi ujiunge na mtandao huo, akajaribu kujiunga lakini haukukubali.

Akaitoa ile CD, na kuiweka ndani ya lile jarida alilolifungua na akaliweka lile jarida mahali mahususi , ambapo hakuna mtu anayeweza kuliona, akafunga na ufungua, halafu akasimama kujinyosha, mara akahisi sauti, akatega sikio na kuangalia saa yake, kwa muda huo haiwezekani kuwepo mtu.

Akagundua kuwa sauti hiyo inatokea upande wa ofisi ya pili yake ambapo ndipo alipo Inspecta mwenzake, na anavyomjua Inspecta mwenzake muda kama huo hawezi kuwepo kazini, akajiuliza ni nani huyu kaingia ofisini kwa mwenzake.

Kwanza alitaka kupiga simu, kwani zipo simu za mawasiliano ya ndani kwa ndani, lakini baadaye akaona kwanini asiende kuangalia yeye mwenyewe, akainuka na baada ya kuhakikisha kuwa kilie alichokuwa anakifanya kipo salama, akaanza kuelekea kwenye ofisi ya mwenzake, na alipofika akagonga mlango, lakini kulikuwa kimya, akashika kitasa na kufungua mlango, hakukuta mtu, akawa kasimama kati kati ya mlango, hakuingia ndani, akasema;

‘Kuna hali inayoashiria kuwa kulikuwa na mtu humu ndani...’akasema na kwa vile taa zilikuwa zimezimwa, akaona huenda ilikuwa ni hisia zake, au kuna panya wamewaingilia, lakini bado akawa na mashaka, akasema kwa sauti ndogo;

‘Nina uhakika kulikuwa na mtu humu ndani, ...lakini  ni nani huyo kwa muda kama huo, na alifika saa ngapi....’akajiuliza  na baadaye, akageuka na kuurudishia mlango hakutaka kuingia ndani kuangalia zaidi; akawa anatembea kuelekea nje na kuwakuta walinzi wa zamu akawauliza

‘Ni nani aliwahi asubihi ya leo kabla yangu?’ akauliza

‘Ni Inspecta Maneno...mkuu’akasema mlinzi

‘Oh alifika saa ngapi, na kaondoka saa ngapi?’ akauliza

‘Alifika mapema sana, siku hizi anawahi sana, na huondoka kabla watu hawajafika, kaondoka sasa hivi, na pikipiki, ...’akasema mlinzi.

‘Anafanya kazi gani ya dharura ?’ akauliza

‘Hatujui mkuu...’akasema yule mlinzi wa zamu, na Inspecta akaamua kurudi ndani kumalizia kazi yake.

 Ni wakati anapita karibu na ofisi ya Inspcta mwenzake ndipo akaona karatasi mlangoni, ilikuwa inaonekana kipande kidogo, sehemu kubwa ilikuwa kwa ndani, akaona ni vyema kuangalia ni karatasi gani, na kama ina muhimu aihifadhi malai pake...

‘Au Inspecta aliondosha wakati anatoka...’akasema, akaaona ni vyema aiangalia na kama ni ya mwenzake akaiweke huko ofisini kwake, na alipojaribu kuivuta ikawa haitoki, ndipo akaona ni vyema kufungua mlango ili aweze kuitoa vyema, akaufungua mlango.

Ilikuwa ni zile karatasi nyeupo zisizo na misitari na mara nyingi zinatumiwa kwenye komputa, akaigeuza, kwani aliona maandishi makubwa upande wa pili yake, akaikunjua ile karatasi na maandishi makubwa yaliyoandikwa na kalamu za matangazo yakaonekana, akayasoma...ooh

Ulikuwa ujumbe uliolekezwa kwa mke wake, uliandikwa jina la mke wake, halafu maelezo kuwa yeye hatafika nyumba kwa leo...hapo hapoa, akaukumbuka yale aliyoambiwa na mke wake kuwa kulikuwa na ujumbe uliosema kuwa yeye hatafika nyumbani, ina maana gani sasa, umefikaje huo ujumbe hapo, ofisini kwa Inspecta mwenzake, na akakumbuka mkewe alivyolalamika kuwa ujumbe huo haupo pale alipokuwa ameuweka...

‘Ile karatasi yenye ujumbe wako kuwa haupo na chini yake kulikuwa na maelezo ukasema kuna picha zako...mbona siioni, na mimi niliweka hapa, ilikuwa juu juu, na sizani huyu mfanyakazi wa ndani kaingia na kupekua huku kabatoni, hawezi kufanya hivyo ni wewe meichukua,?’

Akachukua simu na kumpigia mkewe, haikupokelewa hapo hapo, iliita kwa muda mrefu halafu mkewe akawa hewani na kuongea kwa sauti ya mtu anayetoka usingizini

‘Vipi tena unanisumbua asubuhi hii na mapema kuna nini kimetoka, au ndio unataka kusema hutarudi leo nyumbani, nimeshakuzoe, haya sema mimi nataka kumalizia usingizi wangu....’mkewe akalalamika.

‘Uliniambia uliporudi kutoka nyumbani uliona ujumbe wangu mezani, hebu niambie huo ujumbe ulikuwaje, ....?’ akauliza Inspecta

‘Ulikuwaje kwa vipi...!’ Akauliza mkewe akipga miayo kuashiria kuwa bado ana usingizi na anataka kulala, na kabla mume hajafafanua akasema;

‘Ulikuwa, ni ujumbe umeandikwa kwa maandishi makubwa, sijui ulifanya hivyo kwa vile unafahamu macho yangu yana shida ya kuona...kwanini unaniuliza hivyo...?’akauliza mkewe na kupiga tena miayo.

‘Hamna shida nilitaka kuwa na uhakika tu, maana sikumbuki kuandika ujumbe wowote...’akasema

‘Kama umeandika shauri lako, huenda aliandika shetani...., kuna jingine au ulitaka kunisumbua tu, ..’akasema mkewe sasa kwa sauti ya kuonyesha kukerwa.

‘Tutaongea baadaye nikirudi nyumbani...’akasema na kukata simu, akaichukua ile karatasi na kuikunja vyema akaiweka mfukoni kwa nia ya kwenda kumuonyesha mkewe akirudi nyumbani, lakini kabla hajafunga mlango akatupa jicho kwenye komputa kubwa ya mezani ya Inspecta mwenzake  akaona kama haijazimwa taa za nyekundi zilionekana kuwaka kwenye komputa hiyo.

‘Huyu jamaa bwana, kwanini kaondoka bila kuzima komputa yake , au kuna kitu alikuwa akikinakili nini, na kaacha kiendelee kujinakili, lakini hii ni hatari,..ngoja nihakikishe...’akasema

 Akasogea hadi pale kwenye hiyo komputa kuhakiki, na kama ikiwezekana aizime, akagusa kile kitufe cha kuzimia, baada ya kuona hakuna kitu chochote kilichopachikwa kwa nia ya kunakili faili, au jambo lolote.

Alipogusa kile kitufa mara ile komputa ikiwaka, na mara, nembo kubwa ya dunia ikaonekana imetanda kwenye kiyoo cha hiyo komputa na maandishi makubwa ya kumeta meta yakawa yanazunguka, huku kukiwa na jama akiiangalia ile duni aikizunguka na mikono mbali mbali ikaonekana kama inaishika ile dunia, jamaa anayeiangalia akawa anatabasamu na akawa anaongea maandishi yakitoka mdomono mwake na kwenda kuizunguka ile komputa, maneno na maandishi yalisema;

‘DUNIA YANGU’

‘What,..dunia yangu..ana maana gani huyu mtu!?’ Inspecta akashituka na kukumbuka maneno hayo ameyaona wapi, akakumbuka kuwa nembo kama hiyo hiyo aliiona kwa yule mtu wa komputa aliyekuwa kwa mdada, akakumbuka pia aliyaona kwenye laptop ya mdada halafu kwenye hiyo CD, aliyokuwa akiiangalia muda mfupi uliopita ile nembo hii ya sasa ina mtu kakaa kwenye kiti kakunja nne na mikono hiyo ikiwa imeshikilia hiyo dunia...

‘Hii ina maana gani?’ akajiuliza kwa sauti, na mara akasikia mlango ukisukumwa akageuka kuangalia ni nani kaingia  na akajikuta akiangalia na Inspecta mwenzake, akiwa kaweka mikono miwili katikati ya kifua na tumbo,akimuangalia ....

NB: Nimeona siku isipite bure, angalau tupate sehemu hii ndogo, mitihani ni mingi, lakini ndio maisha

WAZO LA LEO: Ubaya ni sawa na wizi, kama wasemavyo za mwizi ni arubaini, basi na ubaya una kikomo chake, usione unawafanyia wenzako ubaya ukawa unashiba, unatajirika, au unafurahia, ukajiona mjanja, ipo siku utaambuka tu, na kuzalilika, kama ulivyodhamiria kumzalilisha mwenzako, kwani mwisho wa ubaya ndio huo, kamwe hauna mwisho mwema, mwisho wake ni kuumbuka tu. Tuache ubaya, tutubu na kuyasafisha mabaya hayo kwa tuliyotenda kwa kufanya mambo mema.

Ni mimi: emu-three

No comments :