Inspecta akawa na hamasa
ya kulichunguza tukio la kifo cha muheshimiwa, na kila hatua akajikuta
anakutana na mambo mengi makubwa, na leo akawa amepangilia kwenda hospitali kukutana
na docta aliyempima na kumpa dawa marehemu kabla ya kifo chake, na akiwa njiani
akawa anamuwaza msaidizi wake ambaye alionekana kupingana.
‘Kwanini Inspecta
mwenzangu haniungi mkono kuwa muheshimiwa anaweza kuwa hakufa kifo cha
kawaida... ngoja nikikutana naye nitajaribu kuona maoni yake kuhusu haya
niliyoyagundua, lhata hivyo kama hatakubaliana na mimi, mimi mwenyewe nitalifuatilia
hili jambo hadi nione mwisho wake, akubali asikubali....’ akawa anawaza, na
mara akafika kwenye hoteli moja anayopenda kuingia kupata chochote.
Alipofika akakutana na
muhudumu mmoja anayependa kuongea naye mara kwa mara, na alimwambia kuna tatizo
liliwapaat kuhusu jamaa yao aliyepotea kimiujiza, na mara kwa mara analalamika
kuwalaumu polisi kwa hawalifuatilii, na wakati anapata chakula, akamuomba
amsimulie ilivyokuwa;
Tuendelee
na kisa chetu..
************
‘
Siku hiyo nilikua kwenye zamu ya kuwapokea wateja, na nikiwa nimeshachoka, mara
akaingia Msichana mmoja mrembo , alikuwa mrembo kweli, nikavutika naye, lakini
kwa hali niliyokuwa nayo msichana kama yule kwangu ni ndoto...ni matawi ya juu,
hata hivyo nikajibaragua na kumfuata kwani ilikuwa moja ya majukumu yangu
kuwakaribisha kwa siku hiyo.
‘Samahani
dada, nikusaidia nini dada yangu mpendwa.....’nikamuuliza na yule dada
akanitupia jicho la haraka na kusema;
‘Nataka
kukaa kwenye meza ile, kuna mtu namsubiria, akija nitakuambia nina shida gani,
unanielewa...’akasema huku akielekea kwenye hiyo meza, na ile meza
aliyoionyesha ilishachukuliwa na watu maalumu, walikuwa na kashughuli kao
kadogo tu , lakini kwa mrembo kama huyo kumkatalia ikawa ni shida kwangu, nikasema;
‘Nitakutafutia
meza nyingine, kuna sehemu nyingine nzuri zaidi ya hapo, unaonaje, maana kama
unavyoona ile meza imeshawahiwa ndio maana imepambwa vile...’nikasema
‘Yaani
kupamba meza mpaka kuwe na mtu na shughuli maalumu, au..manichekesha kweli..?’
akasema kwa dharau na huku akiendelea kuelekea kwenye ile meza bila kujalia
maelezo yangu, sikuwa na jinsi ya kumzuia, lakini nikamfuata na kusema;
‘Ok,
tuelewane mpendwa wangu, utakaa kwa muda, natumai huyo mtu wako akifika
mtakwenda kukaa kwenye meza nyingine, au sio mpendwa..tutakuandalia kama vile
vile ukitaka...unaonaje mpendwa?’ nikamuuliza na yeye akaniangalia kwa macho ya
dharau, pamoja na kuniangalia kwa dharau, lakini uzuri wake ulikuwa sio wa
kawaida, .....’akasema
‘Je
huyo binti huwa anafika mara kwa mara, au ulishawahi kumuona kabla?’ akauliza
Inspecta
‘Hapana
ilikuwa mara ya kwanza kumuona,sura hiyo ni ngeni kabisa kwangu...na kama
ningeliwahi kumuona kabla ningelishamtafuta na kuongea naye, mimi nawajulia
wasichana kama hao, pale alinidharau kwa vile nilikuwa kwenye vazi la kikazi
zaidi...’akasema akijikagua
‘Lakini
nikitoka hapa huwezi amini kuwa nafanya kazi kwenye hoteli hii, na kama
nimetokea kumpenda mrembo kama huyo, ni swala la kumgharamikia tu...nikiamua
sishindwi, ila sasa pesa ni shida, nikiwa nazo, nikiamua nampata...unajua
ninachofanya ni nini, nitakodi gari la
kifahari kwa siku moja tu inatisha,, nakodi hata nyumba ya maana...nahakikisha
siku hiyo anaingia kwenye hilo gari, na akilogwa akiingia kwenye hiyo nyumba ya
kukodi, amekwisha, mimi ni mtoto wa mjini bwana...’akasema
‘Endelea
na kisa cha jamaa yako ikawaje?’
‘Basi
yule msichana alikwenda na kukaa kwenye kiti, kabla ya kufanya hivyo, alipiga
simu yake ya mkononi na nilimuona akiongea kwa madaha, nikajua anaongea na huyo
mtu wake anayetarajia kuja kuonana naye,
na nilivyoona hivyo nikahisi moyo wa wivu moyoni, unajau ukipenda kitu hata
kama sio chako moyo unajawa na wivu ukijua kina mtu mwingine...’akasema jamaa
huyo ambaye anapenda sana kusimulia vituko.
Mara
nyingi inspecta amekuwa akipata mambo kwa kupitia kwa jamaa huyu, ni muongeaji
mchunguzaji na mfuatiliaji wa mambo ya mjini, ukimpatia pesa kidogo, au
kinywaji ukamsifia, anaweza kuongea jambo utafikiri yeye alihusika, ..na
ukifuatilia utaona ni kweli tupu,...inspecta akiwa na mawazi anakuja kwa huyu
jamaa.
‘Baadaye
huyo binti akaniita na kuagiza kinywaji na kuanza kunywa huku akicheza na simu
yake nahisi alikuwa akiandikiana ujumbe na huyo jamaa yake na mara kwa mara nilimuona
akitabasamu nikajua huenda anawasiliana na huyo jamaa yake na mara kwa mara
nilimuona akiangalia saa yake ya mkononi, nikajua kweli kuna mtu anamsubiria.
Mara
akafika ndugu yangu...ni jamaa yangu wa akribu tu, japokuwa hatukuzaliwa tumbo
moja,...ila ni ndugu wa ukoo...na jamaa yangu alipofika kwa vile nilishawasiliana
naye na alikuwepo hapo kabla, alijua wapi anastahili kwenda, meza anaifahamu
ipo wapi.
‘Kwahiyo
akaingia, na kuikaribia ile meza, kwa muda huo nilikuwa upande wa ndani nikimuelekeza
mteja mmoja wapi pa kukaa, hata hivyo, kila mara nilitupa jicho kule kuona
kinachoendelea, na yule ndugu yangu alipomuona yule binti kakaa kwenye ile meza
nilimuona akionyesha kushangaa, na kugeuka kutizama kule nilipo, lakini
nilikuwa spo upande ule, hakuniona ila niliweza kusikia wanachoongea;
‘Ulikuwa
umbali gani mpaka usikie walichoongea...?’ akaulizwa
‘Sio
mbali, kama angeligeuka upenda nilikuwepo angeliniona, lakini ilijua kaguswa na
kile kilichonigusa kwa binti huyo, ndio maana hakuhangaika sana kunitafuta...’akasema
‘Niamuona
jamaa yangu huyo akimgeukia yule msichana na kusema;
‘Hii
meza imeshachukuliwa na watu, ……’akamwambia na yule binti akajifanya kama
anasimama na kusema;
‘Usijali,
nilikuwa napoteza muda tu, kuna jamaa kaniahidi kuwa atafika, lakini hadi sasa
sijamuona, kwani nyie mna tarajia kuitumia kuanzia saa ngapi?’ akauliza huyo
binti akirembua yale macho yake, wewe...ndugu yangu kuna watu wameumbika,
...ungemuona mwenyewe ungenisaidikisha ....’akasema.
‘Muda
huu...wewe huoni nimeshafika mwenyewe,
kuna watu wangu watafika…muda huu huu, naomba utafute sehemu nyingine,maana
tuna mazungumzo nyeti....’akasema na mara muda huo wakaja jamaa wawili mwanamke
na mwanaume wakiwa wameshikana tete-atete,
siunafahamu huo mtindo, wa kushikana kwa wapendanao, basi wakafika hadi kwenye ile
meza, na yule binti akasimama kuwapisha na kuuliza;
‘Ndio
hawa?’ akauliza na wale wapendwa wawili walionekana kama kutokujali, kama vile
haliwahusu hilo la kuwepo huyo binti asiyealikwa, wao walikuwa wakionyeshana
yale yanayosimuliwa kwa wapendanao wa ukweli. Ungewaona ungeliwapa ushindi wa
bure, afande kuna watu wanajua kuigiza...huwezi amini..
‘Ndio
wenyewe, samahani lakini…ni bora ukatafuta sehemu nyingine sijui huyu jamaa
yangu kwanini hakukuambia...’akasema huyo jamaa yangu, na yule binti akageuka
huku na kule na kuuliza;
‘Kwani
na wewe mwenzako yupo wapi?’ akauliza yule binti,na yule ndugu yangu akamtupia
tena jicho yule binti, na safari hii niliona ile tamaa yake machine, akajitahidi
kutokuonyesha kumjali yule binti, lakini kwa jinsi nimjuavyo huyo jamaa yangu,
kama asingelikuwa na jambo muhimu angelishaanza mambo yake kwa huyo binti,
nikasikia akisema;
‘Aaa,
mimi sihitaji mwenzangu, kwani mmhi, nina maongezi na hawa watarajiwa tu, ni
jamaa zangu, nilisoma nao, kuna jambo muhimu wanataka kulifanya, sasa ni vyema
ukaondoka, tutaongea, wapi unakwenda kukaa, nitaka tuonane kama hutojali, maana
kukutana hivi hivi tu,...…’akasema na akawa anasita kuendelea kuongea na yule
binti akasema;
‘Basi
unaonaje wakati namsubiri mwenzangu niwe mwenzako hapa kwa muda kama hutojali,
maana kwa hivi sasa nipo peke yangu nah ii hoteli ilivyo, ukikaa peke yako
unajisikia mpweke…siounaona palivyo, au...’akasema yule binti
‘Kama
huna tatizo hakuna shida, ilimradi ujue kuwa mimi ni mume wa mtu, na ya kuwa
hawa wenzangu wana jambo lao, mmh,…’akasema huyo jamaa na kuwageukia wale jamaa
na msichana wake kuona kama watapinga, lakini wao wakatikisa kichwa kukubali,
huku wakiendelea kupeana yale mambo ya wapendanao...’akasema huku akionyesha
vitendo;
‘Nashukuru
sana msiwe na wasiwasi kwani hata mimi ni mchumba wa mtu, tatizo ni kuwa mchumba wangu ana mambo mengi sana, na
huenda keshajisahau,…akiendelea hivii mimi nitamuacha kwenye mataa…’akasema na
vinywaji vikaagizwa na mazungumo ya watu hao yakaendelea.
Mimi
kwa muda huo nilikuwa nimeshafika sehemu yangu ya kukarisbisha wageni,sikuwa na
kazi ya kuwahudumia wao, kazi hiyo ilikuwa kwa wahudumu wengine, ila nilivutika
kutaka kujua ni kitu gani kinaendelea hasa kwa yule msichana, kwahiyo nikawa
nimetega sikio sikutaka hata neno moja linipite.
‘Wakati
wale wapendwa wakifanya vitu vyao, vya kutambulishana na kuvalishana pete, hivi
na vile na mpiga picha akichukua kumbukumbu hizo, mimi nikawa naangalai ile
picha kwa makini, ilinasa kwenue ubingo wangu kila hatua ya lile tukio
nalikumbuka, na walipoamaliza ikawa ni mazungumzo tu ya kawaida.
Ikawa
ni zamu ya kutambulishana, kwani tangu awali hilo zoezi lilikuwa halijafanyika,
wapendwa wale walihamanika na zoezi la kuvishana pete, na mbwembwe za kuonyesha
kuwa kweli wanapendana, sasa niliposikia wakisema ni vyema kujuana, na mimi
nikawa na hamu ya kumjua yule msichana anaitwa nani na anafanya kazi
wapi...lakini halikuwahi kutokea....
‘Labda
nianza kujitambulisha mimi mwenyewe, hasa kwako shemeji, nimefurahi sana
umemkubalia rafiki yangu kuwa wako mtarajiwa, alishanielezea zaidi kuhusu wewe,
na leo akaniomba niwe kama shahidi yake wenye hili tukio,....nimefurahi sana,
na natarajia nyie mtakuwa mke na mume mwema, siku hiyo ikifika, na sioni
kwanini msilifanye hilo haraka iwezekaanvyo....mnaonaje?’akasema huyo jamaa
yangu.
‘Usijali
shemeji, kila kitu na wakati wake, hili la leo ni muhimu na nimefurahai kuwa kweli
mwenzangu ananipenda kama ninavyompenda mimi, ...na kwa vile limefanyika,
tutaona huko mbele itakuwaje...’akasema huyo msichana, na yule msichana
mwingine akasema;
‘Lakini
shemeji mimi nahisi niliwahi kukuona mahali....’akasema yule msichana
akimuuliza jamaa yangu na jamaa yangu akatoa lile tabasamu lake...anajua hayo
mambo mimi ni cha mtoto.
‘Hata
mimi nilishawahi kukuona mahali fulani?’ akasema yule msichana aliyevishwa pete.
‘Ni
kweli, wengi wananifahamu ila mimi siwafahamu, …kutokana na kazi yangu
ilivyo…’akasema jamaa yangu kwa kujitutumua, jamaa yangu huyo anapenda sifa, na
ukimsifia umemloga, ila kiukweli anachojisifia anacho, anakipaji huwezi
amini...’akasema
‘Kwahiyo
wewe upo kwenye kampuni gani?’ akauliza yule msichana aliyevikwa pete hapo
‘Nipo
kwenye kampuni ya mitandao ya simu za mikononi…’akasema jamaa yangu ni kweli
yupo huko na alikuwa jembe lao la ukweli, wanajutia kulikosa, had leo ukienda
hapo na kutaja jina lake, wanasikitika sana...’akasema
‘Oh
nimeshakukumbuka, nilifika siku moja nikiwa na simu yangu ikiwa na matatizo,
wenzako walihangaika sana, lakini ulipofika wewe tu, uliirekebisha kwa dakika
moja…’akasema
‘Oh,
huo ndio utaalamu wangu,…ni ujuzi ambao naufahamu sana, namshukuru sana mungu,
na kampuni yangu inanitegemea sana,…na wengi wananitafuata, lakini siwezi
kuondoka hapo , hata siku moja, nina malengo yangu ya kujiendeleza tu hapo hapo
nikitoka nina changu, sio kuajiriwa tena, ....’akasema kwa kutamba.
‘Wanakulipa
vizuri lakini?’ akaula yule mwanaume aliyemvika pete mwenzake
‘Mhh,kwa
hivi sasa kwangu inatosha kabisa, sijawa
na familia....’akasita kusema ana mke na mtoto, nilijua hilo hawezi
kuliongelea, akakatisha hapo na kusema;
‘Mimi
kawaida yangu sitaki makuu, nikitaka zaidi kampuni yangu hiyo wanaweza kunilipa
lakini sitaki papara, unajua tena ukiwa mtaalamu, huhitaji kujishushia hadhi
kwa kuombaomba nyongeza, yenyewe itajipa. Na mimi sina tamaa…’akasema
‘Kwahiyo
unafanya hapo ukiwa umerizika kabisa, kwanini usitafute sehemu nyingine,
ukapata pesa nyingi, ukasomeshwa,…kuna watu wanakutafuta kwa udi na uvumba?’
akaulizwa
‘Hapana
sina tamaa sihitaji kabisa kuondoka hapo kwa sasa...kwanza nikasome nini
nischokijua...ni kweli , kuna mfadhili mmoja alinitaka, nikamtolea nje, ....namfahamu
sana yule jamaa, ana mambo ambayo sipendezwi nayo, na mimi sitaki maisha ya
namna hiyo.....’akasema
‘Kweli,
ina maana umepata bahati hiyo ukaitolea nje...?’ akaulizwa
‘Kwani
kama ni kusoma kampuni yangu haiwezi kufanya hivyo, ...hapana, sina haja na
kwenda popote, Hata hivyo kampuni yangu naipenda nimetoka nayo mbali, na nimeshawaahidi
kuwa sitatoka kwa sasa hivi, kwanini nifanye hivyo. Mimi kwa matarajio yangu
baadaye nikitaka nitaanzisha kampuni yangu mwenyewe, na nitaachana na kuajiriwa kabisa.....’kasema
‘Kwani
lengo la huyo mtu tajiri aliyekutaka ni nini na kwanini alitaka kukuchukua, mimi
naona ni mwema kwako, kwani angelikusomesha zaidi?’ akaulizwa yule msichana
ninayemtamani, na yule jamaa yangu akasema;
‘Mhh,
huyo jamaa ana malengo mengi,kubwa ni kutaka kuteka soko la mitandao ya simu,na
ana mipango mingi tu, mingine ya kibinafasi ambayo hata huwezi kuyaelewa, anayaelewa ni yeye mwenyewe
na ndoto zake, mara kwa mara ananichukua namuelekeza mambo fulani fulani
anayoyataka, zaidi , na ni mwepesi kukariri, akiona unafanya jambo, analishika
kwa haraka, kiukweli ana kipaji, lakini sio mtu wa aina yangu…’akasema
‘Kama
ingelikuwa mimi,ningemkubalia tu,ninaimani atakulipa pesa nyingi sana…mtu kama
huyo anachojali ni utendaji, pesa kwake sio tatizo, nimeshasikia sifa zake..’akasema
yule mwanaume aliyemvika pete mwenzake.
‘Hutaamini
hadi muda huo hakuna aliyewahi kutaja jina lake, japokuwa walikuwa kwenye
sehemu ya kutambulishana, kwahiyo pale niliyekuwa namfahamu ni huyo jamaa yangu
tu, wengine ni sura tu...’akasema
‘Waliendelea kunywa na mara yule jamaa yangu
akatoka kidogo, na mimi nikamfuatilia huko alipokwenda kujisaidia nikasalimiana
naye nikamuomba samahani kwa kuingiliwa kwenye meza yao na yule binti, lakini
jamaa yangu huyo alisema;
‘Oh,
ungelijua, ..yaani ndege yule kajileta mwenyewe ...lakini kwa pale inabidi
nijiheshimu kidogo, nitahakikisha namchombeza huyo binti mpaka nimjue,kwani
umafahamu ...?’akaniuliza na mimi moyoni nilitaka kumwambia hata mimi
nimempenda huyo binti, lakini jamaa yangu huyo kwa haraka akaondoka, na kurudi
kwa wenzake.
Baadaye
nikarudi sehemu yangu ya kupokea wageni na nikawa bado nawaangalia, kuona
kinachoendelea, muda mwingi jamaa yangu akawa anaongea na huyo binti, na
niliona ile meza imgeuka kuwa ya kila mtu na wake, haikichukua muda,jamaa yangu
nikaona kama amelewa kupita kiasi, sio kawaida yake kulewa hivyo, mimi namfahamu
sana, wale wenzake walipoona jamaa kazidiwa wakambeba na kuondoka naye……
‘Huyo
si jamaa yako wewe hukusaidia na kuhakikisha anafika nyumbani kwake salama...?’
akauliza Inspecta.
‘Mimi
sikuwa na wasiwasi nao, nilijua kuwa hao ni wenzake marafiki zake, kwahiyo
sikufuatilia sana, nilikuja kumpigia simu baadaye lakini hakuweza kupatikana
kabisa...’akasema
‘Ikawaje...?’
akaulizwa
‘Ni
ikawa ndio mwisho wa kuonekana kwa huyo jamaa yetu,hadi leo tunamtafuta lakini
hatujui kapotelea wapi,….tulitoa taarifa polisi, na wao wakasema watachunguza
lakini hakuna jibu la muafaka, mpaka tumekata tamaa kabisa...’ Akamalizia
kuhadithia huyo muhudumu wa hoteli, na Inspecta akamuuliza
‘Je
wale jamaa wengine uliwahi kuwaona wakija tena kwenye hii hoteli, hukuwahi
kuwaona kabla au baada ya tukio hilo?’ akaulizwa
‘Sijawahi
kuwaona, inaonekana kama ni jambo lilipangwa,na hao jamaa walitumwa kwa kazi
hiyo, wakijifanya ni wachumba, kumbe walikuwa na lengo moja kumteka huyo jamaa
yetu, na wameyeyuka, sijawahi kuwaona tena....’akasema.
‘Kwani
hao jamaa hawakuwa wanafahamiana na huyo jamaa yako...mbona yaonekana kama
walikuwa wakifahamiana kutokana na maelezo yako?’ akaulizwa
‘Yule
mwanaume na jamaa yangu walisoma pamoja sekondari, wakaachana kwenye vyuo,
lakini wakaja kukutana kwenye kazi zao za hapa na pale, na huyo jamaa ndio
akaja kumuomba huyo jamaa yangu awe shahidi kwenye hilo tendo la kuvishana
pete....
'Kiukweli..., ndivyo nijuavyo , zaidi sifahamu jinsi walivyokuja kujuana kiasi hicho,….lakini
nahisi waliona njia ya kumpata huyo mwenzao ni kutumia huo ujanja, kama kweli
ni ujanja au ni bahati tu imetokea hivyo..sijui kabisa, kazi hiyo tulijua
polisi watatusaidia lakini hakuna kitu kilichofanyika, sijui kama wewe unaweza
kulifuatilia hilo jambo, ila kama familia tumeshakata tamaa....’akasema
Na
mara akaingia dada mmoja akiwa na mwanaume, yule dada alikuwa kavaa mawani, na
alipoingia akayavua maar moja na kuyavaa kwa haraka, na huyu muhudumu aliyekuwa
akiongea na Inspecta akasema;
‘Ndio
yeye......’akasema kwa shauku huku akimkodolea yule mdada, ambaye kwa muda huo
alikuwa akiongea na mwenzake, anayeonekana huenda ni rafiki yake wa karibu.
‘Ndio
yeye nani...?’ akauliza Inspecta ambaye kwa muda huo alikuwa kavalia kiraia
kama askari kanzu, ni kwa wale wanaomfahamu tu wangeliweza kumtambua.
‘Yule
msichana niliyekuambia nimevutika naye,...ooh ndio yeye my God,..., lakini sasa
ana mtu,ooh, sijui, nifanye nini, na sijui kama anaweza kusaidi akujua alipo
ndugu yangu au siku ile ilitokeaje, ...’akasema
huku akizidi kumtolea macho yule binti, na kwa vile walikuwa hatua chache,
hawakujua kuwa kuna watu wanawaangalia kwa hamasa hiyo.
Inspecta
alimuangalia yule msichana akiongea na jamaa yake, wakafika kwenye meza na
kuagiza walichoagiza, wakawa wanakula na kunywa na walipomaliza, haikuchukua
muda wakainuka kuondoka, na Inspecta akajiandaa, akageuka kumuambia huyo
muhudumu;
‘Basi
tutaonana, nitakuja tumalizie kisa chetu....’akasema lakini yule muhudumu
hakuwa makini na inspecta macho na
mawazo yake yalikuwa kwa huyo binti, na hata Inspecta alivyoondoka huyo
muhudumu hakuwa amefahamu mawazo na akili yake ilikuwa kwa huyo binti.
Inspecta
akawaangalia wale jamaa wakiingia kwenye gari, na yeye akachukua pikipiki yake
na kuwafuatilia kwa nyuma, aliwafuatilia kwa muda, na alihakikisha hawawezi
kumtambua, na hiyo ni moja ya kazi yake, anajua jinsi gani afanye hasa
anapomfuatilia mtu kwa lengo maalumu.
Lile
gari likafika kwenye kampuni moja, ni ile kampuni kubwa ya Warembo,
inayomilikiwa na mdada mmoja, na lile gari lilisimama, na yule binti
akateremka, aliteremka peke yake na lile gari likaondoka, na yule binti
akaingia kwenye jengo la hiyo kampuni.
Inspecta
akahisi huenda huyo binti kaja kujilimbwende, na atatoka, lakini ilichukua
masaa mawili hakuona dalili ya huyo dada akitoka , walitoka wanawake kadhaa,
lakini huyo mdada anayemtaka yeye hakutokea, baadaye akaona aende kuteta na
yule mlinzi wa pale.
‘Mlinzi
habari yako....’akasema na kuvua mawani na yule mlinzi akamuona na kumtambua;
‘Oh,
ni wewe afande, sikukutambua kabisa, vipi afande kuna mtu wako umemleta hapa
nini, maana hapa ni kiboko ya warembo, akina mama wakiingia hapa wakitoka
huwezi kuwatambua tena, wanapambwa na kupambika na hata kujibadili sura....’akasema
‘Mhh,
ndio kuna mdada mmoja nilikuwa namtafuta kuna dada mmoja alifika na gari
jekundu, gari halikuingia, yeye alingia peke yake na nina imani hajatoka, nataka
kuongea naye....’akasema
‘Gari
jekundu?!,..mmmh, unamuongelea binti mrembo ‘Jemba,..’. hahaha, na wewe afande
bwana umeingia anga za huyo binti, utaumia afande...hiyo sio anga yako afande
hayo maji marefu...’akasema na kucheka.
‘Hahaha,
mimi tena, hakuna mwanamke anayeniweza kuniumiza, unasikia, kwanini wanamuita
jembe huyo binti?’ akaulizwa
‘Mmh,
afande mambo ya hapa yaache kama yalivyo, maana ukiyachunguza sana unaweza
kuumia, huyu binti ni mmoja wa watendaji wakuu wa hii kampuni, kukiwa na jambo
la muhimu, wanamtumia huyu binti, na hafanyi makosa hata siku moja, .....’akasema
na kuonyesha wasiwasi akiangalia huku na kule kama kuogopa mtu asimsikie.
‘Jambo
kama lipi...?’ akauliza Inspecta akiwa ameshavaa mawani yake na alihakikisha
hapo aliposimama haonekani, na yule mlinzi akaonyesha wasiwasi sana, na alitaka
hata kumwambia huyo afande aondoka, lakini alichelea kusema hivyo, akasema;
‘Afande
unajua mimi ni mfanyakazi wa hapa na sitakiwi kutoa siri za kampuni yangu,
nimekuambia wewe kwa vile ni afande wangu na umenidhamini sehemu nyingi...lakini
kwa hali hii utanifukizisha kazi wenyewe wakijua...’akasema
‘Ndio
maana nakuuliza wewe kwa vile nakuamini, na mimi siwezi kukuangusha , siri yako
ni yangu, na nitahakikisha na kulinda kwa lolote lile, lakini pia ukumbuke kama
kuna tatizo ukaniificha, na mimi nikaja kuligundua utapoteza kazi na
nitakufunga....hilo nakuhakikishia maana siwezi kukuuliza jambo lkama halina
umuhimu...’akasema
‘Afande
kwani huyo binti ana tatizo gani maana mambo yao mengi ni ya starehe,
kufurahishana na kuwakomoa wabaya wao, na hawajafanya jambo baya la kuvunja
sheria, wanajua ni nini wanachokifanya, hata siku moja sijasikia wameingiliwa
na polisi kwa kuvunja sheria, kwani kuna tatizo afande?’ akauliza akionyesha
wasiwasi wa wazi.
‘Hapana
usiwe na wasiwasi kabisa, mimi nimependezewa na huyo binti, tu, ila usije
kumwambia, nitajua jinsi gani ya kumpata na kuongea naye, ila umenitajia jina
likanivutia ni kwanini wanamuita jembe, na mara nyingi wanamtumia kwa kazi
gani?’ akauliza huyo Inspecta la swali hilo lilimkera sasa huyo mlinzi, lakini
akawa hana jinsi akasema;
‘Afande
hapa kuna mengi, usione kuna mambo ya urembo, lakini kuna mambo mengine ya
chini kwa chini, mimi mwenyewe nilikuja kuligundua lakini sio kiubaya sana, ni
kwa wale wanaume wakware, wanaochepuka njia, hapa wana kitengo cha kuwaadhibu watu
kama hao, ukiwa na mtu kama huyo unawalipa wao wanajua jinsi gani ya kufanya,
kisheria,
hakuna baya kabisa
‘Hata
ukiwa na mtu unamtafuta, mara nyingi wanawalenga wanaume, labda wanamtaka kwa
jambo fulani, basi kuna wasichana wanapewa kazi hiyo na mmojawapo ni huyo
wanayemuita mrembo jembe....’akasema
‘Anaishi
wapi...?’ akaulizwa
‘Masaki,
alipangiwa nyumba huko siku nyingi, na sasa hivi nasikia anajenga nyumba yake
huko maeneo ya Mbezi, nasikia ana jengo
sio mchezo...’akasema huyo mlinzi
‘Na
yule aliyemleta ni mchumba wake?’ akaulizwa
‘Mhh,
hapana, yule ni mlinzi wake...ukiwaona wapo wawili ujue kuna kazi
wanaifuatilia...’akasema na mara kwenye jengo akatokea dada mmoja akiongea na
simu, na yule mlinzi akasema;
‘Jembe
hilo. ndio huyo keshajibadili mwendo wa kawaida,...huwezi kujua kuwa ni yeye tena,
ndiye yule binti aliyeingia muda uliopita ila mimi nawafahamu hata wajibadili
vipi...’akasema na Inspecta hakuamini kuwa ni yule dada aliyeingia muda ule.
Huyo
dada alikuwa tofauti kabisa kutoka chini hadi juu, hadi sura, sasa hivi
anaonekana maji ya kunde kidogo,kichwani nywele za Kiafrika, zaidi, sio kama
mzungu alipoingia awali,ila urembo wake ulikuwa pale pale, macho tofauti na
yale ya awali,...sasa nyusi sio nyingi kivile....yaani hakufanana kabisa na
yule msichana aliyemfutailia...
‘Una
uhakika ndio yeye..?’ akauliza afande
‘Hahaha,
ni jembe hilo linajigeuza kama kinyonga....ndio yeye’akasema huyo mlinzi
akielekea kufungua mlango,kwani kwa nje kulikuwa na gari linataka kuingia.
Mlngo
ulipofungulia likaingia gari la njano, na huyo binti, akalifuata pale
liliposimama,akaingia kwenye hilo gari, na hilo gari likaondoka taratibu.
Inspecta
akawapa dakika mbili , na baadaye akalifuata akiwa anaendesha hiyo pikipiki
yake, na aliwasiliana na jamaa, alipofika mbele kidogo, ikaja pikipiki, na
Inspecta wakabadilishana pikipiki na huyo jamaa, sasa akawa na pikipiki ndogo
ya kawaida, na moyoni akasema;
‘Ni
lazima niwe makini na hawa watu......’ huku akiendelea kulifuatilia hilo
gari...
JE
NI NINI KITAENDELEA...
WAZO LA LEO: Dunia sasa
inarejea enzi zile tulizozisoma kwenye maandiko matakatifu,kwani yaliyoandikwa
yatajitokeza, kwa njia moja au nyingine, matendo tuliyowahi kuyasoma kuwa ni
mabaya hadi kukatokea gharika, maangamizi, ndio hayo hayo yanayotokea hivi sasa,
tena kwa kiasi kikubwa kwa ubaya uliokirihisha.
Huu
nii wakati mzazi na familia yako mnatakiwa mkae na kuhakikisha malezi bora
yanakuwepo, msiige na kufuata yale ambayo hamna uhakika nayo, tuwe makini na
vishawishi na mawakala wabaya hasa vyombo vya mawasiliano tv nk, hivi ni vitega
uchumi vibaya kama tusipokuwa makini.
Pia
kuna ndugu na jamaa wanaotutembelea majumbani, tuwe makini nao hasa kwenye
malazi, tusipende kuwachanganya watoto wetu na watu baki, ambao pia wanaweza
kuwa ndugu, lakini hatujui nyoyo zao zina nini, wanaweza wakawa miongoni mwa
mawakala hatari. Dunia imeharibika, na wanaoiharibu ni walimwengu. Kosa dogo
kwa watoto wako ndio umemuharibia maisha yake ya baadaye.
Hebu
jiulizeni kuna haki gani ya kibinadamu ya kutetea mambo yanayokwenda na kinyume
na maumbile ya kibinadamu, kama huo sio ushetani, tuweni makini na hawa
wanajiona ni watawala wa dunia, hao tunaoona ni matajiri, tutaangamia, na tutaingamiza
dunia kwa maasi yetu wenyewe.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment