Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, August 7, 2014

DUNIA YANGU-13


Alimkagua marehemu, na hakuonyesha dalili zozote za majeraha, kama alivyosema dakitari,na hii ilionyesha kifo chake kinaweza kuwa na matatizo ya ndani ya mwili na huenda ikawa shinikizo la damu

‘Hajaumia, au kuumizwa mahali popote, na kwa hali hii siwezi kujua tatizo ni nini mpaka tumfikishe hospitalini kwa uchunguzi zaidi...

‘Yah...ni kweli, lakini kila kitu kinaweza kuwa sababu...ni muhimu kujua ikiwezekana kila kitu, je kwanini alialikwa, kuna nini huko, na kwanini na kwanini itatupa jibu, nahisi hiki sio kifo cha kawaida....

Nitaifanya hiyo kazi, usijali...

Tuendelee na kisa chetu...

                             **************
 Inspekta Moto, alipata maelezo kutoka kwa mwenzake ambaye alikuwa na zoezi la kuwahoji wanafamilia, lakini yeye hakutosheka kabisa na maelezo aliyoyapata, akataaka kuwahoji tena, baadhi yao, hakusema moja kwa moja kuwa hajaridhiswa, ila kwa wakati wake mwenyewe aliona ni vyema kuthibistisha baadhi ya maelezo.

Kwahiyo baadaye alirudi tena kwa wanafamilia, na kwa maelezo ya wanafamilia Mheshimiwa alianza kutokujisikia vizuri wiki iliyopita, na kwa historia ya afya ya marehemu hakuwa na dalili kama hizo za ugonjwa wa moyo au shinikizo la damu, na cha ajabu alipoenda kuangalia afya yake waliambiwa ana tatizo la shinikizo la damu.

Inspecta akaona aongee na mjane kwa undani zaidi, na aliweza kukaa faragha wakiwa wao wawili tu, hakupenda mtu mwingine ahusike, mjane kwa muda huo, alikuwa bado analia, akiwa kwenye majozni makubwa, lakini alikuwa tayari kuongea na askari huyo.

Mjane huyo alisema bila kuficha kuonyesha hisia zake kuwa, ameona ajabu sana, kusikia eti mume wake kafariki kwa shinikizo la damu, haamini, kwani mumewe wake ni mtu wa mazoezi na tangu waishi naye hakuwahi kusikia matatizo kama hayo, kwahiyo yeye alimshauri waende kwenye hospital nzuri zaidi.

`Alienda hospitali gani?’ Inspekta aliuliza.

‘Tulimpeleka kwenye hii hospital inayosifika sana siku hizi ya Docta Chize, yeye ana wataalamu wengi wanaotoa huduma toka Muhimbili’ alisema yule mjane.

Ni kweli vipimo vilionyesha wazi kuwa Mheshimiwa alikufa kutokana na shinikizo la damu, na inaonyesha kuwa alipatwa na mshituko mkubwa uliomfanya apoteze fahamu. Inaonyesha kuwa hakuweza kupata huduma yoyote kwa muda tangu alipopata mshituko na mshituko huo na kusababisha damu kuganda ndani ya ubongo.

 Wanafamilia walisema hawakulitambua hili mapema, kwani mara nyingi marehemu anapokuwa kwenye chumba chake maalumu hahitaji usumbufu, mpaka atapohitaji mtu.

‘Ni nani aliyegundua kuwa Mheshimiwa yupo katika hali mbaya, au kuwa amefariki’ inspekta aliuliza

‘Ilipigwa simu na mmoja wa wasaidizi wake kuwa amejaribu kuwasiliana naye lakini simu yake ilita kwa muda bila kupokelewa. Mimi nami nikajaribu kumpigia na kweli iliita bila kupokelewa,moyoni nikahisi kuna tatizo. Nikaingiwa na wasiwasi mkubwa hata watoto wakaliona hilo, na wote tuliogopa kwenda huko ndani, maana alishatupiga marufuku,...’akasema

‘Ina maana anapokuwa huko huwa hakuna anayeweza kuingia, kama akihitajia kitu, mfano maji, ....?’ akaulizwa

‘Humo ndani kuna kila kitu, mwanzoni nilikuwa naingia bila kujali, akawa anakasirika, na akatupiga marufuku, akisema akiwa humo, hataki usumbufu, kwani ana mambo yake mengi ya kufikiri, na kufanya, na akiwa humo anawasiliana na watu wake muhimu kwa simu, na akasema, kama akihitajia kitu atatuambia, ....’akasema

‘Ulipopiga simu ukaona kimiya, ulifanya nini,..?’ akaulizwa.

‘Ilishawahi kutokea hivyo kabla..nakumbuka alikuja mgeni muhimu, nikampigia simu hakupokea kabisa, na nilipokuja kumuuliza akasema huyo mgeni alishamuona kupitia dirishani, na hakutaka kuongea naye ndio maana hakutaka kupokea, simu,...unaona hapo, kwahiyo kwa namna nyingine, tuliona ni jambo la kawaida, ila  moyoni nikawa nahisi kuna tatizo.

‘Kwahiyo ukafanyeje?’ akaulizwa

 ‘Kwasababu alikuwa na hali ya kuumwa kabla, nikaona nimpigie simu dakitari wake, aongee naye, najua akiona simu ya mtu kama huyo atapokea tu...’akasema

‘Ukampigia dakitari wake, akasemaje?’ akaulizwa

‘Ndio nikampigia simu dakitari wake, ni dakitari wake wa karibu, nikamwambia ajaribu kumpigia simu mume wangu maana anaumwa, na bado anafanya kazi za kumuumiza kichwa, sikumwambia wasiwasi wangu huo kuwa nahisi kuna tatizo kwa mume wangu, lakini mwilini nilikuwa na wasiwasi kweli, sijui kwanini..., na yeye akafanya hivyo....’akasema na kutulia

‘Halafu ikawaje....?’ akaulizwa

‘Kweli alimpigia, na baadaye akatupigia simu, akasema amepiga simu lakini haipokelewi, hapo nikahisi kuna jambo, nikaamua nikaingie mwenyewe, nina ufungua wa akiba, nikaanza kufungua mlango na wakati umefunguka, nataka kuingia ndio nikasikia docta akisalimiana na wanafamilia, mlango ulishafunguka nusu, nikachungulia kwa jicho la haraka. Nilimuona kakaa kwenye kiti kaegemea upande kama vilevile mlivyomkuta...hapo miguu yaote ikaisha nguvu, ile hali sio ya kawaida...’akasema.

‘Ina maana huwa anajifungia na ufunguo akiwa humo kwenye ofisi yake?’ akaulizwa

‘Mlango ulivyo, ulivyotengenezwa, huwa unajifunga wenyewe, lakini ukiwa ndani unaweza kufungua bila ufunguo, ila ukiwa nje ni mpaka utumie ufunguo....’akasema.

‘Ikawaje...?’ akaulizwa

‘Bahati nzuri dakitari wake akaja kwa haraka, maana haishi mbali sana na sisi alipofika akaja na kuniambia nimuacha aingie, na mimi nikasogea pembeni, mwili ulikuwa sio wangu, nilikuwa kama nimepigwa ganzi ya mwili mzima, yeye akaingia na kumuangalia, na mara akatoka na kunikuta nimesimama pale mlangoni, akaniambie niondoke pale, nije kukaa na watoto.

‘Kuna tatizo gani docta?’ nikamuuliza

‘Ni tatizo la kawaida, ngoje poliisi waje waweke mambo sawa, ....’akasema

‘Mume wangu hajambo, je kazidiwa...kwanini polisi?’ nikauliza maswali mengi

‘Hali yake sio ya kawaida, lakini ni vyema nihakikishe usalama wa humo ndani kwanza, msiwe na wasiwasi, nitamchunguza mgonjwa, ...tutajua ni tatizo gani....’akasema na niliona akikwepa kuniangalia machoni, nikahis kuna tatizo, mimi nikakurupuka kutaka kwenda kujionea mwenyewe, lakini docta akanizuia akisema

‘Usiingie kabisa huko, utaharibu kila kitu, ngoja kwanza watu wa usalama wafike.....’akasema na kunivuta pembeni, akaanza kunielezea;

‘Wewe ni mke wake, na ni muhimu ukajua ni kitu gani kinachoendelea, hali ya mume wako sio nzuri, na huyu ni mtu wa serikali, haitakiwi mambo yake yajulikane kwa haraka, hata kama kazidiwa, inatakiwa iwe siri, ...sijawa na uhakika kapatwa na nini, sijamchunguza vyema, lakini lolote laweza kutokea, wewe kama mtu mzima unatakiwa ujifunge mkanda ili usiwaumize watoto...’akaniambia.

‘Niambie ukweli mume wangu yupo hai au ameshakufa?’ nikamuuliza sasa nikiwa najaribu kujiamini, lakini kiukweli ndani kwa ndani nilikuwa sio mimi.

‘Hilo kwasasa sijawa na uhakika nalo, maana shinikizo linaweza kumpata mtu akawa kama amekufa, lakini baadaye akazindukana, ila kwa hali niliyomkuta nayo, sio nzuri, jiandae kwa lolote lile, kama atapona yote ni mapenzi ya mungu, ila jitahidi sana kwa ajili ya watoto...’akasema

Kauli yake hiyo ikavunja nguvu nikajua tena hakuna uhai hapo docta asema hivyo, kwanini asimchunguze kwanza...’akasema na hapo akashindwa kujizuia.

‘Poleni sana, naomba ujikaze kidogo maana msiba ndio umeshatokea, na hatuna jinsi nyingine yote ni mapenzi ya mungu, lakini ni muhimu tukawa na uhakika na kifo chake je unahisi kafa kifo cha kawaida au kuna sababu nyingine?’ akaulizwa

‘Ukiniuliza mimi, kiukweli moyoni,mimi siamini kuwa mume wangu kafa kifo cha kawaida, mbona tangu anioe sijawahi kusikia ana shinikizo la damu, kwanini haya yatokee hivi karibuni tu...nahisi kuna tatizo, nahisi kuna watu wamemfanya hivyo....’akasema.

‘Kwanini unahisi hivyo?’ akaulizwa

‘Mume wangu karibuni, kama mwezi, kuna simu nyingi alikuwa akipokea, na mara nyingine anaitwa kwenye vikao visivyo rasmi, na kila akirudi alionekana kuwa na mawazo, nikajaribu kumuuliza, lakini kama walivyo wanaume wengi, hakutaka kuniambia, alisema ni mambo ya kawaida tu...’akasema

‘Kwani mume wako ana maadui unaowafahamu au uliwahi kusikia kwake, kuwa kuna watu wanamfuata fuata, au ana wasiwasi na jambo fulani?’ akaulizwa, na hapo mjane huyu akamtupia jicho la haraka Inspecta, na kusema;

‘Kwa kazi yake ilivyo, hawezi kukosa maadui, lakini ni mambo ya kisiasa na nilijua hayo yanaishia jukwaani tu, lakini binadamu bwana hawana uvumilivu, lolote laweza kutokea, na kauli za watu nyingine zinatisha....’akasema na kukatisha na hapo Inspekta akahisi kuna jambo anafichwa, hakutaka kushinikiza zaidi hapo, akauliza swali jingine;

‘Je mume wako ana watoto wakubwa wangapi, kuacha hawa ulio nao hapa?’ akaulizwa

‘Yupo mmoja mkubwa, lakini hayupo hapa nchini, tangu niolewe,nakumbuka alifika mara moja tu, na haonekani kuivana sana na baba yake...’akasema

‘Kwanini?’ akauliza

‘Sijui,.... mimi nahisi hakupenda mimi niolewe na baba yake...’akasema

‘Kwani wakati unaolewa yeye alikuwepo?’ akaulizwa

‘Alikuwepo, na hilo lilisababisha akosane kabisa na baba yake, akaondoka kwenda kusoma nje, na hawakuwa wakiwasialiana mara kwa na baba yake,lakini baba yake alisema hayo ni kawaida ipo siku atarudi na wataelewana tu ...’akasema

‘Je wewe na mke mwenzako mnaivana, mnaelewana?’ akaulizwa

‘Kwakweli hatuna tatizo na hilo, ....sisi tunalewana kama mtu na mdogo wake, kiukweli ni mwanamke wa pekee kabisa, yeye alirizia kabisa mimi kuolewa, na hata kwenye harusi alishiriki,..na yeye akanipokea, kama mdogo wake, kiujumla mimi na yeye hakuna tatizo, tatizo ni kwa huyo mtoto wake...’akasema

‘Kwahiyo mke mwenza ana mtoto mmoja tu?’ akauliza

‘Ndio...’akasema

‘Unahisi uliolewa kwasababu hiyo?’ akaulizwa

‘Kuwa kwa vile mke wake hazai au?’ akauliza na yeye

‘Unahisi hivyo?’akaulizwa

‘Ni moja ya sababu, maana mume wangu aliponioa alitukalisha kikao na mke mwenzangu, akasema yeye ana mali nyingi sana, na furaha yake ni mali hizo ziwe mikononi mwa watoto wake,....muda huo nina ujazito, ..kwahiyo japokuwa halikuwahi kusemwa, nahisi ndio sababu kubwa ya mimi kukubaliwa kuolewa kwenye familia..’akasema

‘Wewe una watoto wangapi?’ akaulizwa

‘Mimi nina watoto wanne, kwa mume wangu huyu watatu, wa kwanza sikuzaa naye, nilizaa kabla hajanioa, na anafahamu...’akasema

‘Lakini uliwahi kuishi na huyu mtoto mlipo-oana?’ akaulizwa

‘Hapana, yeye ni mkubwa tu, ana biashara zake, anajitegemea, hata wakati naolewa, alishaanza shughuli zake, japo kwa shida, nilimzaa nikiwa shuleni, nilipata mimba ya bahati mbaya, kwahiyo ni mkubwa tu...’akasema

‘Unahisi kifo cha mume wako ni mambo ya ndani ya familia yenu, labda kuna kitu kimemkwaza, labda kuhusu mtoto wake huyo mkubwa au?’ akaulizwa

‘Hilo sikubaliani nalo kabisa, ni kweli kuna muda anamtaja mtoto wake huyo mkubwa na anampenda kweli, ila hawaivani katika baadhi ya maamuzi, unajua tena mtoto akishakua mkubwa, akajiona na yeye anaweza kuishi...hata hivyo kiukweli baba mtu anampenda sana mtoto wake huyo, na angelifurahi mtoto wake arudi amkabidhi usukani wa mali yake, lakini hilo sio tatizo kubwa kwake...hilo sikubaliani nalo, kama ni shinikizo litakuwa linatoka nje ya familia...’akasema huyo mama

‘Je kuhusu mke mwenza wako, hawezi kuwa ni sababu...labda hakuna mikwaruzoni ya hapa na pale?’ akaulizwa

‘Nikuambie ukweli, mume wangu anampenda sana mke wake huyo mkubwa, licha ya kunioa mimi, yeye alishasema kama mimi nataka kukosana na yeye basi nimuuzi mke wake mkubwa, anasema mke wake mkubwa ndio chanzo cha mali yote aliyo nayo, kiujumla penzi lao sio la kawaida, na nimeshakuambia, mke mkubwa ndiye aliyemshauri mume wangu anioe mimi,......’akasema

‘Mtoto wako mkubwa anapatikana wapi?’ akaulizwa na hapo akakunja uso na ilionyesha hakupendezewa na hilo swali.

‘Huyo niliyezaa kabla sijaolewa na huyu mume wangu?’ akauliza na yeye swali.

‘Ndio...huyo huyo, naweza kumpata wapi?’ akaulizwa

‘Wanini , maana yeye ni mtu baki, lakini kama unataka kuonana naye, yeye ana kampuni yake ya magari na maufundi mengine, yeye ni fundi mkubwa sana, ana vipaji vingi tu vya ufundi, kila kitu yeye anaweza kutengeneza, hata hivyo kiukweli mimi sijawahi kuwa karibu naye, alilelewa na bibi yake, na tangu niolewe na mume wangu huyu, hafiki sana, alifika mwanzoni mwanzoni wakati hajajiweka sawa....’akasema

‘Je yeye alipendezewa na kuolewa kwako?’ akaulizwa

‘Hakuwahi kusema lolote, maana ananijua, nikiamua jambo langu hatuingiliani, yeye ana maisha yake na mimi nina maisha yangu...kiujumla hatujaishi pamoja sana na huyo mtoto kama nilivyokueleza, alelewa na wazee wangu wakamsomesha akakua....mmh, yaani ni mtoto aliyekosa malezi ya mama yake kabisa....’akasema akionyesha kutokupendezewa na hayo maongezi kuhusu mtoto wake.

‘Kwahiyo kwa ujumla hamuivani, maana ulimtekeleza, na kwahiyo hata hamuwasiliani...?’ akaulizwa

‘Kiujumla kama mama na mtoto wake tunawasiliana, lakini sio kihivyo...ni mtu ana maisha yake, kwahiyo hatufuatani sana..na mimi sikumtelekeza, nilimzaa nikiwa mdogo, na sikuwa nafahamu malezi, nikachukuliwa kuwa mfanyakazi wa ndani, na maisha yangu yakaanzia hapo, nikainukia, na ...ni habari ndefu, nikaja kukutana na huyu mume akanipenda, tukaoana, ukitaka nikuhadithie maisha yangu utachoka...ni ya kupanda kushuka, mabaya, mazuri, kihivyo tu.....’akasema.

‘Huyo mtoto wako hajawahi kuja kukushauri jambo lolote, mkaongea kama mama na mtoto wake, ....?’ akaulizwa

‘Hap....ana, aaah, unajua tena, sio kila neno la mtoto lina maana kwako, ni kweli wakati mwingine mwanzoni wakati ana hali mbaya, alikuwa akinishawishi nihakikishe mali yote ya mume wangu, ipo kwa jina langu, na mazungumo kama hayo ya kitoto, lakini baadaye nahisi alipevuka, hayo maneno sikuyasikia tena, na kwa vile sasa ana uwezo wake ana kampuni yake ni kubwa tu, hana haja ya kuwa na wasiwasi na mimi tena...’akasema

‘Hiyo kampuni yake ni mali yake peke yake au ana ubia na mtu mwingine...?’ akaulizwa

‘Mhh, sizani,sijui saana mambo yake, na sipendi sana kuyafuatilia, ila nakumbuka mwaka jana alipelekwa ulaya kusoma...mmh, sio ulaya ni Marekani, yah, ndio nakumbuka huko alikwenda kuchukua ujuzi zaidi wa ufundi wake, ....’akasema

‘Unasema alipelekwa, kwani kwa muda huo hakuwa na uwezo wa kujisomesha mwenyewe,...au wewe na mume wako hamkuhusika kumsomesha, maana mlikuwa na uwezo wa kufanya hivyo?’ akaulizwa

‘Kuna muda alikwama sana kibiashara, biashara yake ikalega lega sana, akawa na maisha magumu sana, nakumbuka alikuwa akija na ninamsaidia pesa za matumizi, na mume wangu alijitolea kumsaidia, lakini hakupenda kusaidiwa na mume wangu, maana ana tatizo ambalo mume wangu halipendi, mtoto wangu yule anapenda sana ulevi na uhuni, anapenda sana kunywa, kuvuta na wanawake, ndio maana hakai na mke...’akasema kwa huzuni

‘Ok....kwahiyo, ...akasaidiwa akaenda kusoma, ni nani alimfadhili, ni nyie au,....maana kama ulivyosema hakuwa na pesa, na nyie au mume wako hakumuamini sana, au sio,...?, Lakini ukasikia kaenda kusoma, alikuambia ni nani alimafdhili au ni nyie wenyewe?’ akaulizwa

‘Kiujumla hakupenda kuniambia mambo yake hayo, alisema tu anatarajia kwenda kusoma, hakuniambi kwa vipi, na nilijaribu kumdadisi, lakini alisema mimi nijue hivyo tu inatosha....lakini nahisi, na ndivyo ilivyo, maana dunia hii haina siri, kuna tajiri mmoja, anayemiliki hoteli kubwa, inaitwaje vile, ni hoteli kubwa sana....’akawa kama anafikiri na baadaye akasema

‘Para...paradiso.., kitu kama hicho...naikumbuka sana maana wakati inaanza kujengwa nilikuwa napika mama Ntilie, tumetoka mbali wewe, usione sasa hivi nipo hapa.....’akasema

‘Ni hiyo ya Paradise Hoteli....’akasema Inspekta, na huyo mama akatabasamu na kusema

‘Hiyo hiyo....huyo mwenye hoteli hiyo ni mtu ni tajiri,...kaupata utajiri kutoka kwa baba yake,...ana bahati sana, maana anajua kuuendeleza, sio kama watoto wengine wanapata utajiri na kuanza kuufisidi, huyu ana akili, na mara nyingi anapenda kuwasaidia watu wengi, na nahisi alipomuona mtoto wangu huyo ana kipaji kikubwa hivyo, akaona amuendeleze zaidi, ili washirikiane, ni mjanja sana huyo jamaa, hasaidii hivi hivi, anasaidia kwa malengo...ndio huyo mfadhili wake,..

‘Ulishawahi kumuona huyo jamaa mwenyewe moja kwa moja?’ akaulizwa

‘Mhh, Inspecta bwana, ...hayo sasa ni mambo ya ndani...mimi ni mtoto wa mjini bwana.....’akatulia na kutabasamu

‘Nauliza maana mimi sijawahi kuonana naye uso kwa uso...?’ akasema

‘Aliwahi kuwa mpenzi wangu....kabla sijaolewa na marehemu...’akasema na Inspecta akashituka akamkagua yule mama, na kumlinganisha na huyo jamaa, kiumri hawaendani, na kabla hajauliza swali, mara simu ya Inspecta ikalia, ikabidi akatize mazungumzo kwani aliyempigia ni Inspecta mwenzake.

NB Mambo yanapandana na kuchanganya, ndio diary yangy hiyo, lakini kisa chetu kipo kwenye dunia ile ile aliyokuwa akiiota mwenzetu bwana Diamu, tutakuja kuona baadaye, tuzidi kuwa pamoja.

 WAZO LA LEO: Ubinafsi, kutokujali haki na tamaa ya ulimbikizaji wa mali ndio tatizo linaloiharibu dunia. Utajiri wa kulimbikiza mali sio mbaya, kama ungelikuwa ni wa halali, ila ubaya wake ni kuwa utajiri huo unatokana na dhuluma, ufisadi, na utawala mbaya, watu wanadhulumuwa, hasa wanyonge wasiojua haki zao.

Maliasili yao inachukuliwa na wajanja, ardhi, vitega uchumi vinamilikiwa na wajanja ambao wanatajirika kwa migongo ya hao wanyonge, kwa  hali hii umasikini unazidi, majanga yanazidi, magonjwa yanazidi, na amani haipatikani kwani kunakuwepo na msuguano wa waliona nacho na wasio kuwa nacho, wanyonge wachache wanaojua nini kinachoendelea wanajaribu kudai haki yao.



Ni mimi: emu-three

2 comments :

Anonymous said...

Highly energetic article, I liked that bit. Will there be a part 2?



Feel free to visit my web blog - Wikipedia Info about the Chinese

Yasinta Ngonyani said...

Ndugu yangu kazi uifanyayo ni kubwa mno hakika wastahili pongezi...naona mengi yamenipita nilikuwa safarini mwezio kwa hiuo sasa nitakuwa na kazi kusoma ila ni raha tu:-)