‘Nawataka wataalamu wa kila fani, wa mashine hadi wa siasa ...Niwe na nguvu, niogopewe.....’
‘Hahaha hao wataalam wa kila aina ya fani, ndio wataniwezesha, nifanye kile
nilichokitaka. Nahitaji mikono mingi ya wataalamu...yah, hili ndio wazo
langu...’
`Nikifanikiwa hilo, basi nitakuwa na dunia ninayoitaka
mimi, dunia ambayo naimiliki mimi kina mna yangu,...hahaha...'
'Ukiwa na akili na
pesa, bhwana, dunia unaweza kuiweka mikononi mwako,...lakini kwanza ni lazima
nipate mikono ya wataalamu mbali mbali, ambao watakuwa wakifuata amri yangu,
hawa watasaidia kuijenga dunia niitakayo mimi...’
`Dunia yangu...'
Tuendelee na kisa chetu
***********
Simu iliendelea kulia na kushiria kuwa mupigaji ana jambo muhimu
sana, Inspekta Moto akiwa bado usingizini, aliinua mkono hadi alipoiweka simu
yake ya mkononi, na wakati anataka kuishika ikawa imeshakatwa.
Akashukuru na kulivuta shuka vizuri, baada ya kuangalia saa
ukutani na kumuonyesha kuwa bado ni bado ni alfajiri, na alikuwa na saa nzima la
kulala kabla hajaamuka kuanza shughuli zake za siku hiyo, lakini kabla
hajatuliza kichwa simu sasa ya mezani ikaanza kuita, na mlio wa simu ya mezani
ni mkubwa kiasi kwamba hata iweje utaamuka tu kuipokea.
‘Hivi hawa watu hawataki na mimi leo nipumzike kidogo, huyu ni
nani asubuhi ya leo na leo ni siku ya mapumziko...’akawa analalamika
Akasimama kwa uvuvi akiomba na hiyo simu ikatike, lakini
haikuonyesha dalili, kwani ilikatika na kuanza tena kulia, akawa sasa
ameshafika kwenye meza ndogo haikuwa mbali na kitandani, akasogea karibu yake
akizidi kupoteza muda ili simu hiyo ikatike, lakini haikuwa hivyo, akaishika na kuiinua
akaweka sikioni, na akilini alishahisi kuna jambo, mara nyingi simu za namna
hii huwa zina jambo zito. Akaiweka sikioni na kusikiliza , na mpigaji akawa
kama anahema kabla hajasema neno
Inspecta alisubiri mpigaji aanza kujitambulisha, lakini alipoona
yupo kimiya akasema yeye;
‘Inspecta Moto,oooh, hapa nikusaidie nini’ Alipiga miayo miwili
mfululizo, na wa pili ulikatishwa na sauti ya Inspekta mwenzake.
‘Mimi ni Inspekta Majuto anaongea, nipo Maeneo ya Mbezi Beach,
nyumbani kwa Muheshimiwa Shingo, kama unakumbuka vyema muheshimiwa huyo pia
ndiye mmiliki wa makampuni ya `Private Telecommunication’. Kwa uhakika sasa
hivi ni marehemu, ingawaje madakitari hawajafika na kupima, na kutoa taarifa
yao…’
‘Ok, kwahiyo unahisi ni.....’kama hajamaliza, akasikia kama mlio wa
kuguna kutoka huko kwa mwenzake, lakini ulikuwa sio sauti ya mpigaji wa simu,
na kukawa kimiya, na Inspecta ,Moto akasema;
‘ Ok basi nakuja sasa hivi, endelea kuchukua taarifa muhimu..’
Inspekta Moto alikata simu na kukimbilia bafuni, akiwa anaoga kichwani alikuwa
na mawazo mengi kumuhusu huyo marehemu, kwani jana tu walitoka kuongea naye, na
walikuwa na miadi ya kukutana leo, na alikumbuka marehemu alisema kuna jambo
nzito ambalo alihitaji msaada na alisema maneno `ushauri wa kiusalama’.
Na Inspecta akamuuliza
‘Una mashaka gani muheshimiwa?’ alikumbuka kumuuliza hivyo
‘Ni maswala nyeti kidogo nahitajia tuongee faragha mimi na wewe tu,
kwenye simu haitapendeza...’akasema huyo muheshimiwa, na sauti yake kwenye simu haikuonyesha wasiwasi, aliongea kwa kujiamini tu, kwahiyo hata Inspecta alijua ni mambo ya kawaida tu, ila alipomuuliza
swali jingine;
‘Kwahiyo tukutane wapi?’ akamuuliza, na muheshimiwa hakujibu moja kwa moja kwanza alitulia kwa muda kidogo kama anawaza jambo, na baadaye akasema
‘Nitakuambia nikiwa tayari, maana yote ni tahadhari,
...nitakupigia au kukupa ujumbe, kama hatutakutana hapa na pale, lakini sitaki tuongee juu kwa juu ...’akasema na kukata simu.
Kauli hii ya mwisho ilamfanya Inspecta kuwazia jambo, kuwa huenda
muheshimiwa huyu ana tatizo, lakini hata hivyo hakuweza kumuuliza zaidi kwani
simu ilishakatika, akaacha kama yalivyo, akijua wakikutana wataongea kwa mapana, na mara nyingi wanakutana, ila hawajawahi kuongea maswala mazito ya kutia wasiwasi.
Baadaye usiku akapokea ujumbe kutoka kwa muheshimiwa huyo kuwa
wakutane nyumbani kwake, huko Mbezi alipo na makazi yake mapya. Inspecta
alishawahi kufika nyumbani kwake kabla, ni makazi mapya, maeneo ya Mbezi, kwahiyo anapafahamu vyema. Yeye na
muheshimiwa huyu wanafahamiana sana, na mara kwa mara wanakutana. Makazi ya
muheshimiwa huyu mwanzoni yalikuwa Msasani.
Inspecta japokuwa alikuwa na kazi nyingine siku hiyo, lakini
alilichukulia swala la muheshimiwa huyo kwa uzito mkubwa, kwahiyo kwenye ratiba
zake za siku aliweka miadi hiyo, sasa leo anasikia ameshafariki, je kuna
mahusiano na kukutana kwake na hicho kifo au imetokea tu kwa bahati mbaya...
Akawa anajiuliza huku akiingia kwenye gari kuelekea huko nyumbani
kwa marehemu. Na kwa vile siku hiyo ni siku ya mapumziko, na kwa vile ni
asubuhi, wananchi wengi bado wapo majumbani, na hakuna magari mengi barabarani,
kwa hiyo Inspekta Moto aliendesha gari lake kwa kasi kidogo akielekea eneo la
tukio .
Njiani alijaribu kumuwaza muheshimiwa huyu ambaye pamoja na
kujiunga na mambo ya siasa, lakini alikuwa ana vitega uchumi vyake vingi,
vikiwemo makapuni ya mawasiliano na baadhi ya viwanda. Alikuwa mtu anayependa
sana kusaidia wanyonge na mara nyingi utasikia amejitolea kiasi kadha, au
kujenga mahospitali na mambo mengine.
Katika ulingo wa siasa anajulikana kama mtu mwenye msimamo akiamua
kitu huwa hatetereki. Na kuingia kwenye ulingo wa siasa kulitokana na wananchi
wenyewe kumtaka awe mmoja wa wabunge wao kwa jinsi moyo alivyokuwa na upendo wa
watu na kusaidia watu kwa hali na mali, kwa hali hiyo matajiri wenzake walikuwa
hampendi, ndivyo dunia ilivyo, watu wanaopenda jamii, kusaidia watu kwa moyo wa
upendo, anakuwa hapendwi na wale wasio na tabia hiyo
‘ Je kifo chake ni katika ulingo wa kisiasa au biashara au ni kifo
cha kawaida tu..’akawa anendelea kujiuliza, na alipoona anawaza jambo ambalo
hana uhakika nalo sana, akasema;
‘ Well, Nitajulia hukohuko......’akasema kwa sauti na kufungulia
redio ya kwenye gari kusikia kama kuna tangazo lolote kuhusiana na kifo chake,
lakini kwa ajabu kabisa hakusikia lolote, hata kwenye vyombo vyake vya habari,
hawakusema kitu
‘Kwanini mbona ...labda kifo chake hakijajulikana...’akasema
‘Lakini kwanini wamuue mtu kama huyu, mtu ambaye hana kinyongo na
watu,..na watu wazuri kama hawa ni wachache sana, wengi na utajiri wao
hawapendi kabisa kusaidia watu, mungu amulaze mahali pema peponi’...akasema
wakati anaingia maeneo ya makazi ya muheshimiwa huyo.
Alifika eneo la makazi ya Mheshimiwa huyu, eneo lake ni kubwa na
ukiingia kwenye geti utakutana na walinzi wa Group Four, na hapo utakaguliwa
gari lako , na kuna mwendo kutoka hapo getini hadi nyumba ya familia ilipo,
napo kuna geti dogo, kwahiyo kwa maana ya ulizi jamaa huyu alijitahidi na huenda
ni kwasababu ya shughuli zake ndio maana alijihami hivyo.
Alipofika kwenye nyumba ya familia aliwakuta askari wakifanya kazi
yao ya usalama kuhakikisha kuwa hakuna kitu kinachoharibika, na kuhakikisha
kuwa ushahidi wote upo, na wakati huo huo madakitari wa uchunguzi wakawa nao
wanaingia. Lakini hawakuanza kazi yao mara moja, hadi Inspekta kwanza aone
tukio lilivyo.
Inspecta alipoingia akakagua kwa haraka haraka kwa macho kwa
kuangalia eneo zima la chumba, kilikuwa ni chumba kidogo cha maongezi, na kwa pembeni
yake walikuwepo wanafamilia wakilia, na Inspecta Majuto alikuwa akiteta na
mmjoa wa wanafamilia, Inspecta mwenzake alikuwa bado akiwahoji baadhi ya
wanafamili, lakini alipomuona mwenzake akasimama kuwahoji wanafamilia na
kumsogelea mwenzake, akasema;
‘Karibu Inspekta Moto, twende huko ulipo mwili wa marehemu, na
hakuna mtu ambaye amegusa kitu tangu nifike…ni makitaba yake’ Aliongea na
inspecta Moto, akawatupia macho ya haraka wanafamilia, na baadaye kamfuata
Inspecta mwenzake, kwenye chumba kinachoitwa makitaba, ni chumba ambacho ni
kikubwa na kina kila kitu kama ofisi.
Wakaingia kwenye hicho chumba kinachoitwa makitaba, na hali ya
hewa ya hapo ndani ya chumba ilikuwa ni ya ubaridi sana, inaonekana kipozea
hali ya hewa kilikuwa kinafanya kazi toka muda mrefu. Na inspecta alikagua kwa haraharaka
kwa macho na hali aliyoiona haikuonyesha uvamizi, mapigano , kulikuwa kuna
ushwari, kwani kila kitu kilionekana kipo katika mahala pake, kwani sio mara ya
kwanza kwa inspecta huyu kufika kwenye hiyo maktaba.
Aliangalia pembeni kwenye makabati makubwa, yaliyojaa vitabu, na
makabrasha mbali mbali, kuonyesha kuwa mtu huyu alikuwa msomi, na kila kitu
kilipangwa vyema kabisa, na picha za viongozi wa siasa zilikuwepo pia ukutani,
kuashiria kuwa huyo jamaa pia ni mkereketwa wa siasa ya nchi yake.
Akatupa macho kwenye meza iliyopo karibu na dirisha, ni meza ya
kiofisi, na juu yake kuna simu ya mezani ya kisasa, kuna kitabu kilichofungulia
nusu kuashiria kuwa kilikuwa kinasomwa, kulikuwa na mafaili mawili yapo mezani,
na maandishi makubwa yalionekana, `AJENDA ZA VIKAO...’ kulikuwa na makabrasha
mengine, kuashiria kuwa huyo mtu alikuwa anafanya kazi fulani, pia kulikuwa na
komputa ndogo `laptop’ ,iliyokuwa imefunguliwa
Akazidi kusogeza macho yake na sasa akafikia kwenye kiti, aina ya
sofa, hapo kulionekana mtu kakaa , mkao usio wa kawaida, mdomo umefungua nusu,
kuashiria kuwa huyo mtu ama amelala, au ndio hivyo tena, mmh, kwa dalili ile,
iliashiria kabisa hakuna uhai, alikuwa huyo marehemu.
Akamkagua kwa macho kwa haraka haraka, na kwa mtizamo wa kawaida,
inaonyesha marehemu hakufa kifo cha kuhangaika, maana alikuwa katulia kwenye
kiti, na kichwa tu ndio kilionekana kuwa upande.
Inspecta akausogelea ule mwili, na kwasababu alishaambiwa, alijua sasa
anakabiliana na maiti, alikuwa ameshavaa kinga za mikononi, lakini bado
alijaribu kuwa makini asiguze kitu, akaangalia mandhari ya pale alipokaa huyo
marehemu.
Marehemu, mkono wake mmoja ulikuwa karibu kabisa na simu ya
mkononi, simu hiyo ilikuwa mezani ikiguswa kidogo na vidole, ilionyesha kuwa marehemu
alikutwa na umauti, wakati akiongea na simu, au akitaka kuongea na simu. Na
inspecta alipohakikisha kuwa kaona kila kitu muhimu, na kwa vile hakutaka
kugusa kitu kabla taratibu nyingine hazijafanyika akasema;
‘Mumeshachukua picha na kila kitu humu ndani...?’ akauliza na kabla
haajjibiwa, akasema
‘Kama bado picha zichukuliwe, na docta aingie .....’akasema na mwenzake
akatoka kuwaita wapiga picha na wataalamu wa alama za vidole, wafanye kazi yao.
Na wakati mwenzake anatoka, Inspecta akamsogelea marehemu na kwa haraka
akipitisha mkono kwenye mifuko ya koti la marehemu na akatoa karatasi na nyaraka mbali mbali zilizokuwa kwenye mifuko, akaziweka hizo nyaraka kwenye mfuko wake na nailoni, alihakikisha hakuna kitu kimbebakia
kwenye mifuko hiyo ya marehemu, na mara watu wakaingia kufanya zoezi lililohitajika
na kwa utaratibu unaotakiwa.
Walipomaliza kazi yao Inspecta akasogea pale mezani na kuchukua
simu ya mkononi, na kuikagua vyema,
ilionyesha imezimika, sijui kwa kuisha chaji, au ilijizima yenyewe. Akaandia
kwanza kwenye kijitabu chake, na kuchukua picha ya video, akaiwasha...wakati
inawaka akawa anaendelea kukagua pale mezani huku simu yake ikichukua kila
tendo analolifanya.
Simu ikawa imeshawaka, na ilionyesha kujaa chaji, sasa kwanini
ilizimwa, ni kitu kingine kilimtia mashaka huyu Inspecta, akaanza kukagua miito
ya karibuni, cha ajabu kulikuwa hakuna
kumbukumbu ya miito ya karibuni, hii ilimpa wasiwasi sana Inspekta, kwasababu
kwa taaswira ilionyesha alikuwa akiongea na simu, je iweje kumbukumbu zifutwe,
alizifuta mwenyewe au kuna mtu alifika hapo baada ya tukio, au ndio alikuwa
akitaka kuongea na mtu...haiwezekani awe alifuta kumbukumbu kabla....
Alimkagua marehemu, na hakuonyesha dalili zozote za majeraha, kama
alivyosema dakitari,na hii ilionyesha kifo chake kinaweza kuwa na matatizo ya
ndani ya mwili na huenda ikawa shinikizo la damu. Lakini hayo yatasubiri
maelezo ya dakitari wake, ambaye alishamaliza kuchukua kumbukumbu za haraka, na
alihitajia marehemu kufikishwa hospitalini kwa uchungiz zaidi.
‘Hajaumia, au kuumizwa mahali popote, na kwa hali hii siwezi kujua
tatizo ni nini mpaka tumfikishe hospitalini kwa uchunguzi zaidi...’akasema huyo
docta
Inspecta alipohakikisha kuwa amekagua mambo yote muhimu aliwaomba
wataalamu wa uchunguzi na dakitari wamalizie kazi zao zilizobaki na mwili wa
marehemu ufikishwe hospitalini kwa uchunguzi zaidi.
Wakati Inspecta anatoka akaona kitu kama kijijarida, au kadi,
ambacho ilikuwa imedondokea pembeni mwa meza ya kiyoo, kilikuwa kimejificha
sana, na aliichukua muda kukitoa sehemu hiyo.
‘Kuna nini Inspecta...?’ akauliza mwenzake
‘Kuna kitu kama kijarida, au kadi, mmmh, ok..inaonyesha ni kadi ya
mualiko....’akasema
‘Kadi ya mualiko, oh, ngoja nikusaidie kukitoa?’ akasema mwenzake
na kusogea ili kutoa msaada, lakini Inspecta alishaitoa hiyo kadi, na
kuipitisha jicho la haraka, halafu akaitumbukiza kwenye mfuko wa plastiki
aliokuwa nao mkononi.
‘Kadi ya mualiko,wa harusi au kikazi?’ akauliza mwenzake
‘Hapana haionyeshi hivyo, naona alialikwa kwenda kwenye kikao
maalumu, mmmh,inaonyesha alialikwa kwenda hoteli ya Paradise....’akasema
Inspecta Moto
‘Mhh, Paradise,........’akasema mwenzake akionyesha mshangao
kidogo
‘Hivi umafahamu mumiliki wa hiyo hoteli?’ akauliza huyu Inspecta
Moto
‘Mhh, hapana namsikia tu, na kwa hadhi ya muheshimiwa, kualikuwa
huko sio jambo la ajabu, au sio?’ akasema Inspecta mwenzake akionyesha
kutafakari jambo.
‘Yah...ni kweli, lakini kila kitu kinaweza kuwa sababu...ni muhimu
kujua ikiwezekana kila kitu, je kwanini alialikwa, kuna nini huko, na kwanini
na kwanini itatupa jibu, nahisi hiki sio kifo cha kawaida....’akasema Insepecta
‘Nitaifanya hiyo kazi, usijali....’akasema inspecta mwenzake na
kwa haraka akatoka kwenye kile chumba na kumuacha Inspecta akiendelea kukagua mle
ndani na safari hii kwa makini zaidi, na moyoni akahisi kuna jambo kubwa
kuhusiana na hicho kifo, hasa akikumbuka mawasiliano yake na marahemu, ....
NB: Sehemu hizi ni nyeti kidogo, kwahiyo inabidi niwe makini
kuziandika, lakini natumai tupo pamoja
WAZO LA LEO: Halahala na jirani,
jirani ni mtu muhimu sana kwako. Jirani, anaweza akawa jirani wa sehemu yoyote unapoishi, iwe kazini, majumbani au kinamna yoyote ile, ambayo
inakufanya wewe na yeye muwe majirani, kuna ujirani hata wa kiimani , kikabila
nk. Jirani ana haki zake muhimu, na usipokuwa makini na jirani yako, inaweza
ikawa sababu ya fitina, uadui na uvunjifu wa amani.
Cha muhimu ni kuwa makini
sana kwa kila tunachokifanya, tuangalie kisimkwaze jirani yako, tukumbuke kuwa
kosa dogo tu linaweza kuzua uhasama, chuki, na uvunjifu wa amani, ndio maana
tunaambiwa mpende jirani kama unavyojipenda wewe mwenyewe, hata ikibidi zaidi
ya hapo.
Ili kulifanikisha hili,
kama una uwezo, toa msaada wa hali na mali,kam ni bosi toa haki stahili,
hakikisha unashirikiana na jirani yako kwa shida na raha, kwa kufanya hivyo,
unajenga udugu, unajenga mahusiano mema, na jirani na jirani kunazaliwa mtaa,
au kijiji,au ofisi, kampuni nk, kama wote mtafanya hivyo nina imani, amani na
upendo vitakuwepo daima.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment