Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, August 4, 2014

DUNIA YANGU-11


  Inspekta Moto, aligeuka kumwangalia mwenzake inspekta Majuto, hali aliyomuona nayo, ilimpamashaka, mwenzake alionekana mwingi wa mawazo, na mara nyingi alikuwa akisimama kama ana wasiwasi na jambo,halafu hurudi kukaa tena, na kabla hajamuuliza kitu, mara simu yake ya mkononi ikiita, akaangalia mpigaji, na kwa haraka anachepuka nje , na haikupita muda akarudi, na safari hii alionekana kabisa kuchukia, hakuwa na raha usoni.

Inspecta Moto, akashindwa kuvumilia, ikabidi amuulize mwenzake kulikoni,kwani ni karibu siku ya tatu mwenzake huyo haonekani kutulia na huenda kuna jambo ambalo wangeliweza kusaidiana,likaisha;.


‘Haya ni maswala yangu binafsi, usijali, nitayatatua pindi….kuna mambo hayajakaa sawa…’ hili lilikuwa jibu lake na alipenda kulirudia kila akiulizwa swali linalofanana na hilo.

Inspekta moto alihisi kuna tatizo zaidi ya mwenzake anavyoelezea, lakini aliona si vyema kuingilia maswala ambayo huenda yataleta kutokuelewana ndani ya kazi, kwahiyo alijifanya hafuatilii tena maswala ya mwenzake. Mara simu ya mezani ikaita, na aliyehitajiwa kwenye simu ni Inspekta Majuto, ya kwamba kuna mgeni wake nje anamuhitaji..

‘Huyo mgeni yukoje?’ aliuliza Inspecta Majuto.

‘Ni binti, ambaye anasema anamiliki kampuni ya warembo , anasema unamiadi na yeye…’ sauti ilisema

‘Miadi na mimi, ngoja nakuja mwambie anisubiri chumba cha wageni’ alisema inspekta huku akionyesha kuchanganyikiwa zaidi. Mawazo ya wiki nzima yalizidi kumchanganya kichwa. Alihisi huyu binti atakuwa amekuja na tatizo jingine kubwa, na hakutaka matatizo mengine kichwani mwake.

Inspecta Moto akawa anafuatilia yale mazungumzo na mwishowe akilini mwake akavutika amuone huyo binti ni nani, akajifanya anafuatilia mafaili yaliyopo ndani ya chumba cha wageni, naamu, huyo binti alikuwa binti kweli, na amjuavyo Insekta Majuto sio mtu wa mabinti, yeye ni mpenzi wa pombe, na sigara., lakini tabia ya mabinti hakuwa nayo! Je huyo binti kaja na maswalagani.

Na kipindi anaingia chumba cha wageni, aliona yule binti akimkabidhi Inspecta kadi, ilikuwa kadi iliyonakishiwa vyema, na yule binti alionekana kumwangalia inspecta yule kwa macho ya udadisi zaidi, sio ya mahaba, kuashiria kuwa swala hilo halihusiani kabisa na mapenzi.

Inspecta alisita kuipokea pale alipoona mwenzake akiingia,akajibaragua, na yule binti akatabsamu, na kumshikisha yule askari ile kadi, na hapo hapo akasimama kuondoka,na inspecta yule akaichukua ile kadi na kwa haraka akaificha kwenye mafaili yaliyokuwepo pale mezani,na kitendo kile kilimfanya yule binti kutabasamu.

Na yule binti akiwa alisimama kwa madaha na kuelekea mlangoni. Aligeuza shingo kimadaha na kusema;

‘Usikose, ukikosa utamkosea bosi wako, na unajua nini matokeo yake..’ alisema kwa kujiamini.

‘Bosi wake?, ni nani huyo bosi wake,…?’ Inspecta Moto alijiuiliza bila kupata majibu, ina maana mwenzetu ana mabosi wengine ambao hawajulikani. Alijifanya kuchukua mafaili na kujifanya faili analotafuta halionekani.

‘Inspecta Majuto faili maalumu la wale watuhumiwa namba moja la ile kesi ya mauaji,umeliona wapi?’ Aliuliza akiwa na uhakika kuwa ndio lile lililokuwepo pale mezani. Inspecta majuto akajibaragua na kuliinua lile faili na wakati huohuo ile kadi iliyopo kwenye bahasha ikadondoka chini. Na yeye akajifanya kama haioni

‘Naona kama kuna kitu kimedondoka,…..’akasema inspecta akitaka kuinama kukiokota lakini inspecta akawahi kuinama na kuichukua ile kadi, lakini inspecta moto alishaona kile alichotaka kukiona.

Kwa jicho la haraka, inspecta akaona nembo na jina kubwa likionyesha mualiko kwenye hoteli moja kubwa sana, `Paradise…’.

‘Oh, kumbe….’akasema kimoyo moyo, akikumbuka hiyo hoteli, inayomilikiwa na tajiro mmoja ambaye hajulikani anaishi wapi.

Hakutaka kupoteza muda akalichukua lile file kutoka kwa mwenzake na kugeuka kuondoka, alitaka amuwahi huyo binti hapo nje, lakini alipotoka hakumuona tena, na akaona haina haja alichotaka kukijua kwa sasa kimetosha.

‘Ni lazima nifuatilie huko kuna nini , na kwanini mwenzangu anaonekana kutokuwa na amani ….’akasema kimoyo moyo

**********


Wakati haya yakiendelea kichwani mwa Inspecta majuto kulikuwa na mambo mengi na kila hatua alijiona akiiingia kwenye mitihani mikubwa, na kutokana na misongo ya mawazo isyokwisha, akahisi maumivu makali upande wa mkono wa kushoto,maumivu hayo hayakuwepo kabla.

Kichwani alihisi kuna tatizo, mwanzoni alijua labda ni zile pombe alizokunywa jana, lakini alihisi zaidi ni mawazo ya kazi ambayo alielekezwa kuifanya na jamaa wamuitaye bosi.  Huyu bosi ni nani…akawa anajiuliza

   Hakupenda hii hali ya kuwa na mabosi wa uraiani yeye ana mabosi wake wa kazini, lakini kuwa na mabosi wa uraiani,hakutegemea, na hakupenda iwe hivyo, hata hivyo kwa jinsi ilivyo ilimlazimu kufanya hivyo ili kufanikisha maisha yake na mkewe, ili kuficha aibu kubwa ambayo haijawahi kutokea katika maisha yake.

Alipokumbuka kuhusu mkewe, kwa haraka akajizoa zoa, akikumbuka ahadi aliyompa mkewe kuwa leo hatachelewa, wanatakiwa kwenda kutafuta nguo mpya, toleo jipya….

‘Huyu mwanamke atanitoa nyongo….’akasema

Mke wake ni mpenda anasa, na kama akihitaji kitu ni lazima akipate, asipokipata ndani hakukaliki. Hali hii ilimfanya Inspecta kubuni ajira za pembeni, na aliyemsaidia kufanikiwa hili ni tajiri mmoja mwenye makampuni mengi ambaye hajawahi kumuona kwa sura na mara moja aliyoonana naye alikuwa kavaa mawani meusi, na ilionekana hakutaka kabisa kuonekana sura yake.

Na walipoonana naye akamuahidi kazi maalumu, iliyokuja baada ya yeye kupitia mafunzo maalumu, mafunzo yaliyokuja kumbadili, hata hivyo akilini, na kazi yake alijiona anafanya makosa, hakuwa na raha, hata hivyo, hakuwa na la kufanya.

Alikumbuka jinsi alivyokutana na huyo aitwaye bosi...

                *******

ilikuwa ni kwenye sherehe ya wakubwa, matajiri wa nchi hii, na mualiko ulikuja kupitia kwa mkewe. Na hiyo kadi ya mualiko haikuja kwake moja kwa moja, hiyo kadi ya mualiko alipewa mkewe, hata alipoambiwa na mkewe kuhusu huo mualiko, hakupendezewa, kwani licha ya kazi aliyokuwa nayo mbele yake, hata yeye mwenyewe hakupenda kujumuika kwenye hizo sherehe kutokana na kazi yake ilivyo, lakini mkewe akalazimisha kuwa wamealikwa mke na mume,na yeye kaalikwa ni lazima aende na mume wake.

‘Kama hutaki kwenda huko kwenye huu mualiko, ambao ni muhimu kwangu, kwa biashara zangu, basi nitafutie mume wa kwenda naye, nataka umtafute mwenyewe ili usije kusema nimevuka mipaka ya ndoa…’akasema

‘Mke wangu unafahamu fika kuhusu kazi yangu…sehemu kama hizo mimi sitakiwi kufika, labda iwe ni shughuli ya kikazi…isitoshe nina kazi za watu zipo mbele yangu...’akasema

‘Ifanye hiyo ni shughuli ya kikazi…..tafadhali mume wangu , tafadhali usiniharibie siku….’akasema

‘Unaweza kwenda peke yako mke wangu nimekuruhusu kwa leo...,sio lazima uongazane na mwanaume, mimi nina kazi muhimu ya kazini, nahitajika kesho kuonana na mkuu, kutoa taarifa ya kesi niliyokuwa naichunguza…’akasema

‘Unasema nini, hebu angalia hiyo kadi imeandikwa nini, MR, and MRS,sasa nitafutie huyo MR, nakuambia ukweli, usipotaka kuondoka na mimi huyo Mr, atatafutwa, ..usije kunilaumu, unakumbuka baba yangu alivyokuambia, mtoto wangu hana matatizo, matatizo labda uanzishe wewe, na haya unayotaka niyaanzishe ni wewe..’akasema

Inspekta akakumbuka kuhusu baba mkwe wake huyo, akakumbuka jinsi alivyomuoa huyo mwanamke kwenye ushindani mkubwa, na yeye alishinda kwa kutetewa na baba mkwe wake huyo, na siku alipofungishwa ndoa, aliambiwa;

‘Umempata binti yangu, binti yangu alikuwa na nafasi ya kuolewa na matajiri, lakini nimewakataa kwa ajili yako, kutokana na nafasi yako, kutokana na kukuamini, sasa usije ukaniharibia binti yangu,binti yangu nampenda sana….’akasema baba mkwe

‘Nashukuru sana mkuu wangu, mimi nakuahidi nitamlinda kama ninavyolinda mboni yangu ya jicho...’akasema kwa kujiamini

‘Huyu binti kalelewa vyema…hana dosari, ukija kumharibu, akija kuharibikia kwako, nitahakikisha hicho cheo chako,hiyo kazi yako unaisahau, na nitahakikisha unakwenda kusota jela…’akasema mzee huyo ambaye alikuwa muheshimiwa mkubwa, na kweli akitaka kumharibia angeliweza kutokana na wadhifa wake, na kutokana na kumuoa huyo binti vyeo vikapanda haraka haraka hadi kufikia hiyo ngazi aliyo nayo kwa sasa.

Kutokana na msisitizo wa mke wake, hakuwa na lakufanya, ikabidi akubali,akakubali kuongozana na mkewe kwenye mualiko huo, na alipofika kwenye huo ukumbi uliosheheni wageni mashuhuri, matajiri wa makampuni, wafanya biashara,...akaona ili kuondoa wasiwasi ni bora kuzibugia pombe kwa wingi, na kweli alikunywa kupita kiasi, alitaka alewe ili waondoke mapema, hakutaka kuonekana na mtu.

Kutokana na kunywa kwa pupa akazidiwa, kuna muda alitaka kwenda kujisaidia,ili apunguze akainuka kwenye kiti na kumuambia mkewe;

‘Nataka kupata hewa, napitia shotozi,nikitoka hapo nitatoka nje kidogo, kupata upepo….’akasema

‘Ukichelewa mimi utanikuta nyumbani, na ukichelewa kurudi nitampigia simu baba yangu aje kukufuata mwenyewe,…’akasema mkewe akiendelea kunywa kinywaji akipendacho huku akichezesha mkono wake uliojaa vito vya thamani.

‘Siwezi kuchelewa mke wangu siunafahamu mambo yetu ya kiaskari ni chapu chapu.., wewe nisubiri…’akasema na kutembea kwenda kujisaidia na kwa vile alikuwa kabanwa sana, alipofika eneo la chooni, hakuangalia juu, akajikuta kaingia …

Alipoingia, akawa keshafungua fifungua vya suruali yake, na  kabla hajaanza kukojoa kwa pembeni akamuona mwanamama, bonge la mwanamama, wale akina mama waliofungasha,kama wamepandikiza, lakini ndivyo alivyo.

Cha ajbu kabisa mwanamama huyo alikuwa na chupi tu, chupi zenyewe, zile za vipande, na alikuwa kakaa kwenye kiti na kufanya sehemu kubwa ya makalio yake kukuzidi kile kiti, huyo mwanamama hakuhangaika kujifunika, alipoona huyo jamaa kaingia, aliendelea na mambo yake,alikuwa akijipodoa,…

‘Oh nimekosea nini,lakini juu niliona kumeandikwa choo….’akasema,kwani mwanamamahuyo alikuwa akipodoa,na mbele yake kulikuwa na kiyoo kikubwa, ambacho aliweza kumuona mtu akiingia mlangoni.

Huenda huo ulikuwa ni mpango, au jamaa alikosea, akaingia chumba kisichostahili, labda chumba hicho kilikuwa maalumu kwa akina mama kujipambia,…akawa anawaza yule askari, wakati huo alishaanza kuachia mkojo ukutani, hakuwa na la kufanya.

‘Wewe…nani kakuambia huku ni chooni….’akasema yule Shangingi

‘Oh,lakini nimeona mlangoni kumeandikwa Toilet…..’akasema Inspecta

‘Umesoma maneno yote yaliyoandikwa juu ya mlango, au ulipitiwa kidogo, uliponioa nimeingia humu, wanaume wengi wanajigonga kwangu, huu mwili umekuwa ni tatizo, lakini sio mbaya...juu ya mlango kumeandikiwa kuwa , hii ni toilet ya akina mama ya kujirembea, sasa wewe umeingia na mkwaju wako na kuanza kutuharibia chumba,….’akasema huyo mwanamama.

‘Sahamani sana…’akasema mkuu akimalizia kumwanga mkojo wake

‘Hahaha, samahani eeh, ili nikusamehe,inabidi ufanye nitakavyo mimi, unaniona nilivyo, wanaume wanautafuta huu mwili kama wanavyotafuta almasi, sasa wewe umepata bahati ya kuuona mwili huu nikiwa hivi, fully naked, inabidi uwajibike…’akasema

‘Unataka nifanye nini…..acha upuuzi wako huo, unanifahamu mimi ni nani?’ akauliza na wakati huo yule mwanamama akawa kasimama kwenye kile kiti alichokuwa amekaaa, akamsogelea mkuu huyu kwa madaha,akijirembua, na mkuu huyu, akataka kugeuka kukimbia lakini alichelewa, akawa keshaingia mikononi mwa mwanadada huyu.

‘Hahaha ni mara ya kwanza kukutana na mwanaume anayekimbia mwanamke na mwanamke mwenyewe kama mimi, hahaha, hivi wewe kweli wewe ni mwanaume ajabu kabisa....hahahaha….usiniangushe,….’akasema huyo mwanamama akiwa keshaanza kazi yake, na mkuu huyu akawa anajiuliza hili limetokea kwa bahati mbaya au ilipangwa

‘Oh, samahani wewe mwanamke, …mimi sio kama unavyonifikiria,…..’akasema Inspecta, akigeuka kutoka kuondoka na kusogelea mlangoni, alisahau kuwa alishafungua suruwali yake, na yule mwanamke alishavita mkanda, kwahiyo ikawa inamvuka..., akashika kitasa kufungua huo mlango kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukishikilia ile suruwali yake..., lakini mlango ukawa haufunguki, kumbe ulikuwa umefungwa kwa nje.

‘Nani kaufunga huu mlango tena, nataka kutoka haraka, waambie wafungue huu mlango kwa haraka, kabla sijauvunja, mnanielewa mimi ni nani…’akasema Inspekta

‘Nakufahamu sana, wewe ni Inspekta wa polisi, na mara nyingi askari mnapenda sana wanawake, au sio..., na ndio maana nipo hapa kwa ajili yako, kukuondolea kile unachokikosa kwa mke wako…..’akasema na Inspecta akaona sasa hilo ni tatizo, akageuka akijiandaa kutumia umaarufu wake ili atoke humo ndani kwa haraka, alimkumbuka mkewe, hakutaka kabisa kumsaliti.

Wakati anataka kugeuka, alihisi kama mkono umetoka kwa nyuma, ukashika pua yake, na alichoweza kuhisi kwa muda ule ni kujiona kama anaelea hewani, na hakujitambua tena, hadi alipoamuka asubuhi…,

‘Samahani bosi nimeambiwa nikuletee nguo zako hizi hapa uwahi kazini…?’ ilikuwa sauti ya mwanadada, mwanzoni mkuu huyu alijua ni mfanyakazi wake wa ndani, lakini macho yalipozoea mwanga, akamuona sio huyo mfanyakazi wake, alikuwa muhudumu wa hoteli,kutokana na mavazi yake.

‘Nimefikaje humu ndani, na ni nani kakupa nguo zangu hizi za kazini?’ akauliza akiziangalia kwa makini , ni kweli zilikuwa ni nguo zake hakuwa na shaka nazo.

‘Nimepewa na bosi wangu?’ akasema

‘Bosi wako…bosi wako ni nani?’ akauliza

‘Vaa nguo zako utaonana naye pindi…..’akasema na Inspecta akajiinua kitandani na kujiona kweli yupo uchi kama alivyozaliwa, na hapo akakumbuka tukio la jana, akageuka kumuangalia yule binti, akauliza;

‘Yule, yule...yupo wapi huyo malaya,...yupo..yupo wapi?’ akauliza

‘Mimi sijui maana nimeingia asubuhi ya leo, sikuwepo jana, lakini …nimesikia uliingia chumba hiki na shangingi….yule mwanamama mwenye mwili mkubwa na umbo la nane…’akasema

‘Shangingi! Shangingi ni nani, na yupo wapi maana nikimpata ni lazima akalale jela, hawezikunifanyia hivi?’ akauliza huku akionyesha hasira

‘Mhh, mbona wanaume wengi wanamfahamu sana kwa umbile lake, na wengi wanamtaka sioni ajabu kwako ….’akasema na huyo mkuu akamkatisha kwa hasira na kusema.

‘Mimi ni mume wa mtu siwezi kumtaka mwanamke yoyote zaidi ya mke wangu, yupo wapi, maana anastahili kuadhibiwa, hawezi kunizalilisha kiasi hiki....’akasema kwa hasira

‘Mhh, naona ajabu kweli, hata hivyo aliondoka asubuhi hii hii, saa hizi yupo kwenye ndege, kasafiri kwenda Ulaya kwenye mafunzo na maonyesho ya mavazi,akirudi hapa atarudi na mwanadada mmoja, ambaye yupo huko huko….’akasema huyo muhudumu

‘Oh, mmh, kuna nini kimetokea,..’akajiuliza kichwani,na kabla hajapata jibu akasikia saa yake ikitoa mlio wa ishara kuwa anahitajika kuwa kazini, akamuangalia yule mwanadada, na yule mwanadada akaweka nguo pembeni ya kitanda na kuanza kuondoka.

 Inspecta, akasimama na akajiona hajisikii vyema, akatoka na kuingia bafuni, akitaka kujimwagia maji huku akijiuliza maswali mengi kichwani,na kujaribu kukumbuka yaliyotokea jana, lakini akili ilikuwa haifanyi kazi kabisa, akawa hakumbuki, anachokumbuka ni kuingia choo cha kina mama kwa bahati mbaya, na baada ya hapo hakumbuki kitu…..

Akamaliza kuoga, na kurudi chumbani, na kuzichukua zile nguo, zilikuwa nguo zake, anazifahamu sana, kwani jana asubuhi zilivyoshwa vyema na mfanyakazi wake wa nyumbani, na aakazichukua mwenyewe na kuziweka kwenye kabati lake, na ndizo alitarajia kuzivaa leo akiingia kazini, sasa zimefikaje hapo...akazidi kuchanganyikiwa.

Akaziinua zile nguo akijiandaa kuzivaa, na mara kukadondoka kitu, akakifuatilia kwa macho,akaona ni bahasha inayoonyesha kuwa kuna kitu kizito ndani yake,akainama na kukiokota, na kabla hajaifungua ile bahasha simu yake ikaita, alipoangalia akakuta ni mkewe,hakuipokea kwa haraka akavaa zile nguo, huku simu ikiendelea kuita.

‘Oh sasa nitamuambia nini huyu mwanamke….’akasema na ile bahasha aliyokuwa nayo mkononi, ikamdondoka,na kutoka kwenye ile bahasha kukatoka picha kadhaa na kusambaa sakafuni…

‘Picha,...’akasema kwa mshangao, hakumbuki kuweka picha kwenye hizo nguo zake, akaina kuziangalia zile picha.

Picha iliyokuwa juu ni picha ambayo ilimfanya mapigo ya moyo yasimame kwa muda, akahisi kichwa kikiuma, akahisi pumzi ikimuishia, akafumba macho na kukaa kitandani, alipofumbua, akahisi hayupo peke yake, na aliona mtu kasimama mlengoni.

‘Wewe ni nani?’ akauliza kwa sauti nzito ya kiaskari

‘Haina haja kuniuliza mimi ni nani, …lakini kama unataka kunifahamu basi fuata nitakayokuambia..’akasema huyo jamaa.

‘We-we-we ndio umefanya haya yote…?’ akauliza akitaka kuangalia chini, lakini aliona aibu, na alitamani aifiche ile picha isionekane

‘Mhh sina uhakika unaongelea nini, naona hapo chini kuna bahasha, na pembeni kuna picha, ndio hilo unaloongelea au... ooh, mungu hebu angalia hiyo picha,..ooh, hivi kweli mtu na wadhifa wako unaweza kufanya huo uchafu, ma-ma-ma, mmh ni aibu mkuu mzima kama wewe unatembea na ..ni nani huyo?’ akauliza akichungulia chini.

Mkuu akitumia mguu wake azisogeza zile picha kwa mguu kama kuzificha, lakini ndio akawa kasababisha picha nyingine zitoke kwenye hiyo bahasha, na yule jamaa akawa anacheka, huku akiwa kashikilia kanda ya Cd’s mkononi, akasema;

‘Usijali mkuu, hiyo ni kazi ndogo kuisawazisha, mtu kama wewe huhitajiki kuaibika, mimi nitakulinda kwa nguvu zangu zote nawafahamu hawa watu waliokufanyia hivyo, hata mimi wamenitumia hii Cd’s niinunue kwa milioni kadhaa, nimeiona kidogo, nikaona kweli thamani yake inalipa, lakini, sio vyema kumuabisha mkuu kama wewe.....’akatulia na huyo mkuu akasema;

‘Sikuelewi unasema nini, kwanza nimeshachelewa kazini, sasa hivi wewe na wenzako mpo chini ya ulinzi ni lazima niwafishe nyote kituoni….’akasema kwa hasira

‘Usijali mkuu tumeshaongea na mkuu wako wa kazi, na anajua kuwa umepitiwa kidogo na pombe ulizokunywa jana, ila hajui ulichokifanya, na nahisi akikijua sizani kama utadumu kwenye kazi yako, hebu angalia hizo picha vyema, halafu ndio ufikirie kufanya hiyo kazi yako ya kutuweka chini ya ulinzi, nahisi wewe ndio unatakiwa kuwa chini ya ulinzi, na mimi nitakuwekea dhamana, unasemaje….’akasema huyo jamaa akitabasamu kwa dharau.

‘Oh, ….’akasema huyo mkuu sasa akiinama kuziokota zile picha, kila picha iliyofika mkononi mwake,ilikuwa mbaya, mbaya hajawahi kuuona, aliwahi kuziona picha kama hzio kwenye mapicha mabaya yanayoonyeshwa kwenye video chafu, na alikuwa akizilaani sana, sasa anachoona yeye ni tofauti, kwani muhusika mkuu kwenye hizo picha ni yeye na yule mwanamke...

‘Huyu mwanamke nikikutana naye tena, sijui nitamfanya nini....’akawa anaapiza kichwani, akawa anajiuliza jina lake ni nani, na huyo muhudumu kasema anaitwa shangingi, hakuwa kabisa kufkiria katika maisha yake kuwa angelikifanya kitendo kama hicho.

‘Mungu wangu..’akasema akibadilika sura, hasira, chuki,….lakini kikubwa kuzidi yote ni aibu, aibu kuwa hizo picha zikionekana kwa hao watu wa udaku, atakuwa kaumbuka, na uso wake atauweka wapi,  hiyo ni aibu ya mwaka, akamuangalia yule mtu aliyesimama mbele yake...huyu mtu, alikuwa kavaaa mawani makubwa,na ndevu zinazoonekana ni za bandia kwa uzoefu wake alijua kabisa huyo mtu hana ndevu za namna hiyo, japokuwa hamfahamu ni nani. Kwa hasira akasema

‘Nyie watu nawahakikishia nitawafunga,na nitahakikisha hamtoki,  mtaozea jela ….’akasema

‘Mhh,hilo sio muhimu sana kwetu, sizani kama una haja ya kupoteza pumzi zako kwa hilo, kopi kama hizo zipo mbioni kumfikia mke wako, na nyingine kwa nani yule ehe, nimewaambia wazipeleke kwa baba mkwe wako, au unasemaje na nyingine zipelekwe kwa mkuu wako wa kazi, hapo tutaona ni nani ataozea jela….’akasema na kucheka kwa kicheko cha dharau.

‘Hahaha, mkuu, inspecta mzima wa polisi unatembea na machangudoa, unamfahamu huyo mwanamke, wanamuita shangingi...kajazia, kaumbika umbo la nane, mkuu kama wewe ukashindwa kuvumilia...hahahaha...mke akiziona hizo picha sijui kama kutakalika...hahaha...’akacheka kwa dharau

‘Hivi mnataka nini kwangu?’ akauliza sasa akiwa kasawajika.

‘Hapo sasa umesema neno….utapata ujumbe pindi, leo au kesho, cha muhimu ni kuitikia huo ujumbe,na kufika huko utakapoelekezwa…mengine utayasikia huko huko….ukumbuke hizo ni picha, bado kuna CD’s zake zitakuwepo  madukani pindi ukijiafnya wewe ni mjanja....’akasema huyo mtu

‘Mkuu sisi, hatuna nia mbaya na wewe, ila tunachotaka ni wewe uishi maisha ya raha na mkeo, mkeo anapenda starehe, ni mtoto wa watu hajazoea shida, sasa kwanini upate vidonda vya kichwa wakati njia ya kupata pesa ipo, kama utakuwa mtu mwema ukawa mtu wetu, hizi picha na Cd’s tutazizuia, sizizagae mitaani….’akasema.

‘Mtu wenu…mimi niwe mtu wenu na mambo haya machafu mnayoyafanya, mna akili kweli...?’ akauliza.

‘Ni nani kafanya mambo machafu ni sisi au ni wewe, mkuu hebu angalia hizo picha vyema, ni aibu, mkuu kama wewe kufanya mambo machafu kama hayo,..lakini nikuambie ukweli, mwenyewe utafurahia, ….nakuambia usipate taabu, nchi na maisha yako utayaona mazuri tu, eti nikuulize kwanini uje kufa masikini, wakati kuna njia za kutajirika, hebu funguka kiakili, uone mbali, ....’akasema huyo jamaa, na mkuu huyu akawa kimiya

‘Mimi nakuhakikishia kwa mikakatii niliyo nayo, ukiwa na nami, hutakufa masikini, utakuwa tajiri, cha muhimu kwanza ufike kwenye mafunzo maalumu, kuna chuo chetu cha watu kama wewe, na ikiwezekana, utakwenda nje kidogo,…..’akasema

‘Nje kufanya nini?’ akauliza

‘Kazi yako hiyo inahitajia utaalamu fulani, mwenyewe utaona, sio lazima uende nje, ila ikibidi , nimefanya mpango, kuna mtaalamu fulani atakuja hapa nchini, huyo mtakutana naye na mafunzo atakayokupa, hutaamini, hutakuwa wewe tena, ...kuna utaalamu wa kisasa unatakiwa ujifunze...’akaambiwa
‘Utaalamu huo wa nini, ...?’ akauliza

‘Hayo maswali sio ya kuniuliza kwa sasa, kwanza fuata hayo ninayokuelezea, kuanzia sasa mimi ndiye bosi wako....’akaambiwa

‘Bosi wangu!?’ akauliza kwa mshangao  na mara simu ikalia, akaichukua simu yake kuangalia mpigaji wa hiyo simu ni nani, akakuta anayepiga ni baba mkwe wake….

‘Huyo ni baba mkwe wako sio…sasa uamuzi ni wako...hizo picha anazo mtu wa kupeleka vifurushi, anasubiri kibali changu, unasemaje mkuu?’ akauliza

Mkuu huyu akainama na kumbukumbu za hizo picha zilivyo, zikamfanya ashindwe hata kupokea simu ya baba mkwe wake, akamuangalia huyo mtu mbele yake, na moyoni akawa kajawa na wimbi la hasira, lakini angelifanya nini kwa muda huo, akasema;

‘Nitafika kama utakavyo, ila nakuonya, leo umeshinda wewe lakini.....’akasema na kukatishwa na simu alikuwa baba mkwe wake apiga tena, akajua huenda mke wake kapeleka mashitaka kwa baba yake kuwa haonekani.

‘Usijali, viitisho, hasira jaziba vyote vitayeyuka pale utakapoona mshahara wako wa kwanza, ulishawahi kupata dola elifu tatu hadi tano kwa mwezi,...na kila kitu kitu unapata,....?’ akauliza na Inspecta kwa haraka akawa anazibadili hizo pesa kwa pesa za kibongo

‘Eti nini?’ akauliza
‘Huo utakuwa mshahara wako wa kuanzia, nafikiri matatizo madogo madogo ya shemeji yatakwisha, hutapata shida ya kuumiza kichwa tena, unakosa nini hapo, ....fikiria kwa makini yote hayo....’akaambiwa

‘Pokea simu ya baba mkwe wako huyo, ujue anahitajia nini, maana hizo picha atazipata pindi utakapokwenda kinyume na makubaliano yetu, na ukijifanya mjanja simu kama hiyo akikupigia safari nyingine ujue ni nini atakuambia, nakutakia kazi njema…’akasema na kufumba na kufumbua jamaa akawa haonekani, ni kama vile kayeyuka…..

Inspecta akaiweka simu na kumsikiliza baba mkwe wake, huku akili yake ikiendelea kuwazia zile dola elifu tatu hadi tano.....

NB: Haya mmoja mmoja akawa anaingia kwenye dunia ya bwana Diamu, tuone ni nani atafuata au ni nini kitafuata.


WAZO LA LEO: Uwajibikaji wa kazi ni pamoja na kujiamini, na kujiamini hakuji bila ya kuwa na uhakika na hicho unachokifanya, na ili uwe na uhakika na unachokifanya unahitajika kusoma, kufanya utafiti. Tuwe na tabia ya kusoma na kufanya utafiti katika mambo yetu, badala ya kuongea tu, kuzua, na propaganda...

Ni mimi: emu-three

No comments :