Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, August 1, 2014

DUNIA YANGU-10Docta akasimamishwa kazi ili uchunguzi ufanyike, na kipindi alichosimamishwa kazi alikuwa hana pesa za kujikimu, japokuwa alikuwa kitegemea ujuzi wake wa udakitari, na dawa kidogo alizokuwa nazo lakini hazikuweza kumfikisha popote, kwani matumizi yake yalikuwa mabaya, akaanza kusota, maisha yakawa magumu....

Tahamaki siku moja akakutana na rafiki yake waliyewahi kusoma naye, akamchukua na kumpa chakula cha mchana na hapo wakaanza mazungumzo;

Na jamaa akamwambia kuwa wanataka waingie kwenye dili ya kipesa, na dili yanyewe inahitajia maandalizi makubwa, gharama na uvumilivu kidogo,

‘Mimi nataka tuingie kwenye dili za kipesa, ....’akasema huyo jamaa, na docta kusikia hivyo, `dili za kipesa’, akagutuka, na kusafisha kichwa kwa kukitikisa, akamkodolea jicho huyo jamaa yake, moyoni akisema; `anajileta mwenyewe’

‘Sijakusikia vyema, umesema dili za pesa au za posa, hebu rudia tena nikusikie vyema, maana hapo umenipandisha uchu wangu, ukitaja dili za pesa mimi napandisha mashetani, hooooho...au sikusikia vyema, sema tena....’akajitikisa na mwenzake akatabasamu na kusema.

‘Lakini sio rahisi kama unavyofikiria...inahitaji maandalizi na gharama....’

Ni kweli gharama zikatumika jamaa akaenda kusoma Marekani, na huko akaonyesha kipaji chake,na hata wenyewe wakamkubali, na Ulaya na Marekani kama una kipaji mara nyingi wanataka ubakie huko huko, lakini jamaa akatoa udhuru kuwa alihitajia kurudi kwanza nchini, ili kuweka mambo yake sawa, na kweli akaruhisiwa akarudi nchini.

Tuendelee na kisa chetuSiku docta aliporejea hapa nchini kutoka masomoni Marekani, cha kwanza kukifanya ni kuwachunguza maadui zake, kuona kama kuna usalama, na alikuja kugundua kuwa mmoja wa maadui zake, yule mdada, siku hizi ni matawi ya juu, sasa hivi anamiliki kampuni kubwa ya urembo.

‘Nahisi atakuwa ameshasamahe, hata hivyo ni lazima niwe makini...’akajipa matumaini huku akiendelea na mikakati yake ya kuanzisha hiyo hospitalini akaipa jina ambalo, alijua haligundulikana kuwa ni yeye, moyoni alikuwa na wasiwasi, na hakuna kitu alichokigopa kama kwenda jela,...

‘Hata jina nitatumia jina jingine, japokuwa kwenye vyeti,  sitaweza kubadilisha kitu...’akasema na kweli wafanyakazi wake wakawa wanamuita kwa jina hilo alilolibuni yeye mpaka likazoeleka hivyo.

Baada ya muda akawa ameshafanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwani hospitali aliyoinzisha ilikuwa ikimiminika kwa wingi kila aliyetibiwa hapo alikuwa wakala wakufikisha ujumbe kwa wengine;

‘Kuna hopitali moja imeanzishwa ni kiboko, kuna docta aliyetoka Marekani, anajua kazi yake, matatizo ya akina mama, matatizo ya akili, ...yaani utamwambia tatizo gani ashindwe kulitatua, kweli ana kipaji...’mmoja wa waliotibiwa hapo akawa anawaambia wenzake.

‘Ni Mmarekani kweli?’ akauliza mwingine
‘Sizani, nahisi ni Mtanzania aliyebobea huko, alisoma huko, na karudi kuwekeza nyumbani kwake,hata Kiswahili chake ni cha shida....’akasema mwingine.
‘Nitampeleka mke wangu maana anasumbuliwa na matatizo ya uzazi, ni miaka mitano sasa akishika mimba inatoka...’akasema
‘Hapo umefika, wahi mapema, maana watu wanavyojaa, ni balaa...’akasema mwenzake

Sasa ikawa kila aliyetibiwa hapo akawa anapeleka taarifa kwa wengine, na taarifa zikaenea kwa haraka, na jamaa akajua sasa anatakiwa awe makini zaidi, akaachia ndevu, na kuwa habanduki na mawani usoni kuficha sura yake, hata hivyo, hilo halikusaidia, kwani pamoja na kupata elimu na utaalamu wake, udhaifu wake wa kunywa pombe, haukumtoka, pombe ikawa ni tatizo kwake, na akilewa hujisahau akavua mawani, akaonekana na watu

Juhudi zake zikamsaidia, ikabidi sasa atafute wasaidizi, akawachukua watu anaowafahamu, ambao alijua hawatamsaliti, akawapa shule ya kile alichoona wanaweza kumsaidia, na akawa anawalipa vizuri, na mmoja wa marafiki zake wa zamani, akamteua kuwa mwekezaji mwenzake, lengo ni kuwa akiondoka, huyo ataendeleza kazi aliyoianza, na huyu rafii yake alikuwa mmoja wa madakitari bingwa, kwahiyo kazi iliendelea kama kawaida.
Siku moja wakakaa na rafiki yake huyo na akaona amwambie ukweli, kuwa yeye hatakaa sana hapa nchini, ana kazi anakwenda kufanya huko Marekani, na kwahiyo yeye atamwachia kila kitu

 ‘Mimi nitarudi tena majuu, kwahiyo wewe utashika usukani wa hii hospitali, nakuaminia rafiki yangu hii iwe ni kitega uchumi chetu...unaona mambo yanavyokwenda, hapa hatuna shida tena, sasa tusiangushane....’akamwambia.

‘Usiwe na wasiwasi na mimi, tumetoka mbali, mimi nitahakikisha kila kitu kinakwenda bara bara...hapa ni mwanzo tu, wewe mwenyewe utaona, wewe nenda kahangaike huko, na unipigie debe na mimi nikasome zaidi....’akaambiwa

‘Usijali na mimi ndio lengo langu, nataka tuwe na matawi mengi nchi nzima, na humu kuwe pia kama chuo, mimi nitafanya yote, udakitari na kufundisha kile ninachokijua, kwa madakitari wetu....’akasema

‘Hilo ni muhimu sana,....’akasema mwenzake

Ni kweli huyo msaidizi wake, alikuwa naye mmoja wa madakitari wazuri, na hata kaam hayupo, yeye aliweza kufanya mambo mengi, japokuwa hakuwa na utaalamu kama aliokuwa nao yeye.

Siku aliyoongea na huyu msaidizi wake, ndio siku ambayo alipokea simu kutoka Marekani kuwa anahitajika, nafasi yake bado ipo, na akawajibu yupo tayari kwenda huko, na wao wakamwambia kama ni tatizo la usafiri, wao watagharamia kila kitu, na kweli wakatuma stakabadhi ya usafiri,...

 ‘Ok, sasa najipanga kuondoka, wiki ijayo, napanda ndege kurudi kwa wazungu...’akasema kwa kujiamini, lakini....

*******

Dakitari alisogea dirishani, na kuchungulia kwa nje ili kuhakikisha kuwa huyo anayemuhisi ndiye huyo kweli,je  ndio huyo dada, mmoja wa maadui zake, aliokuwa akiwakimbia.

Taratibu akafunua pazia la dirishani na kuchungulia nje, huku nesi akimuangalia kwa mshangao. Jamaa jicho lilipotua kwenye gari, akaachia lile pazia kwa haraka, akasema kimoyo moyo;

‘Oh ni gari lake,..lakini mbona sijamuona...’akasema na kuinua pazia tena kuchungulia ni kweli lilikuwa gari la yule adui yake, lakini yeye mwenyewe hakumuona sehemu ile ya kusubiria wagonjwa, akageuka kumuuliza nesi wake ili aweze kumuuliza huyo mwanadada mbona hayupo hapo nje...

Alipogeuka kuangalia, alikutwa na mshutuko mkubwa, karibu akadondoke, maana pale alipokuwa kasimama nesi wake, sasa alikuwa kasimama huyo mwanadada mrembo, akiwa kashikilia miwani kwenye mkono mmoja na kuigonga gonga kwenye kiganja cha mkono mwingine, huku akibenua mdomo kwa dharau

Wakaangaliana...na taswira ya tukio lililopita, vile alivyomtendea huyo mwanadada,  lilitanda kichwani mwa docta, na kumfanya ahisi kujisaidia, hata hivyo akajipa moyo, na kujitutumia, akataka kusema neno lakini yule mwanadada akamuwahi kwa kusema;,

`Doctor, docta, unarudi bila hodi, ..hahaha, ok, lakini mbona umenisubirisha sana nje, tofauti na nilivyosikia sifa zako,...ok, lakini kwanza hapa nina RB yako...’akasema yule mdada akiwa anatoa karatasi kwenye mkoba wake, na kushikilia karatasi, ilikuwa ni karatasi kutoka kituo cha polisi cha kutaka huyo jamaa akamatwe kwa kushukuwa kubaka, na kutoa mimba kinyume na sheria za nchi, na pia kwa kumharibu kizazi huyo binti.

Nesi alikuwa bado kasimama nyuma ya mlango, alikuwa hajaondoka,akasikia hayo maneno, akashindwa kuvumilia,na akajikuta akiuliza;

‘RB!!?...RB, yanini tena mungu wangu...’akasema

‘Mungu wako wa nini, hebu ondoka hapo bosi wako anafahamu RB, ya nini,...naomba uondoke hapo mlangoni, haya hayakuhusu...’akasema huyo mdada kwa sauti kali, na yule nesi akaondoka, akiwa na wasiwasi na bosi wake kuwa leo kaja kukamatwa kwa kosa ambali hakuweza kulifahamu, yeye anachojua kuwa bosi wake ni mtaalamu toka Marekani, japokuwa ni Mtanzania.

Yule mdada akahakikisha kuwa yule nesi ameondoka kabisa pale mlangoni, akafunga ule mlango, na kumgeukia docta, akasema;

‘Docta unafahamu fika kuwa unatafutwa na polisi, unakumbuka kosa ulilolifanya, sitaki kukumbusha,maana kila nikiliwazia, natamani niwe na bastola nikipasue kichwa chako,.. lakini kwa hivi sasa hayo tuyaache...’akasema na sasa akawa anarudisha ile karatasi kwenye mkoba wake, na docta akapumua kidogo.

‘Haya tuyaache, ila  mimi nimekuja na jingine muhimu kwako, hii RB na mambo ya polisi yanaweza kuja baadaye, kwa leo, chenye umuhimu ni hii kadi...’sasa akatoa kadi kwenye mkoba wake.

‘Hii kadi ni ya mualiko maalumu.....’akasema na docta akiwa anapumua kidogo, akahisi kuna kuna mtego mwingine, na aliposikia kadi ya mualiko, akahisi ni mtego wa huyo mwanadada, nay eye hakutaka kujionyesha zaidi kwa jamii, akauliza;
‘Kadi ya nini...?’ akasema kwa sauto ya mkwaruzo na yule mwanadada akamuangalia kwa macho ya udadisi na kubenua mdomo kwa dharau, akasema;

‘Hii kadi imetoka kwa bwana mmoja unayemfahamu sana...’akasema, huku akiwa kaishikilia ile kadi mkononi, akiipepea huku na huku,

‘Bwana gani...?’ akauliza docta huku akionyesha wasiwasi, hakutaka kabisa kujihusisha na jambo lolote zaidi ya maandalizi yake ya kwenda Marekani, na alishaanza kujenga hoja za kumshawishi huyo mwanadada, ikibidi waingie ubia naye, hayo yaliyotokea nyuma yaishe, kwanza moyoni alishampenda.

‘Bwana Di-amu....’akalitaja hilo, na docta hakuweza kuficha ule mshituko alioupata ilikuwa kama mtu kaguswa na waya wa umeme

‘Eti nini, Di-amu..., hapana...’akasema kwa wasiwasi na mshangao, kwa sauti ya kukoroma maana mdomoni mate yalishamkauka na hapo alitamani kupata kinywaji ili akili iweze kufanya kazi vyema.

Jina hilo lilimfanya akose raha, alijua huyo anaweza kuwa kikwazo kikubwa sana kwenye safari yake ya kurudi Marekani, sasa akajua keshapatikana na safari yake ya Marekani inaweza kuingia dosari,  akataka kusema neno, lakini mwanadada akazidi kuongea

‘Natumai unamfahamu vyema huyo mtu, na wajibu wako kwake, cha muhimu, kabla hujafanya lolote, kabla hujapanda ndege kurudi huko Marekani, kitu ambacho sizani kama kitakuwepo tena, unahitajika kufika huko ulikoelekezwa, ukisoma hii kadi itakuelekeza yote...’akasema huyu mwandada akisogea pale aliposimama huyo docta.

‘Kama sitaki ...na siwezi, nina mambo yangu mengi....’akasema

‘Hahaha, docta, docta,....umesahau eeh, kuwa unatafautwa na polisi,..umesahau eeh, yale uliyonifanyia, ...docta fikiria kwa makini, unaifahamu jela wewe...’akasema mdada

Docta akawa sasa anahema kwa haraka, alitamani apate kinywaji, bila kinywaji haweze kuongea kwa jaziba,...docta alijikuta akiwa imekuwaje huyu mwanadada awe na mafungamano na mfadhili ambaye sasa alishapanga kumsaliti ....

‘Oh, kumbe huyu mwanadada ni kitu kimoja na Diamu, mbona nimeshapatikana..’akasema kimoyo moyo, na mwanadada bado akiwa kashikilia ile kadi, na alionekana hataki kuondoka mpaka ahakikishe huyo docta amekubaliana na huo mualiko, akasema;

‘Unasikia vyema, ukikosa kufika kama ulivyoelekezwa, huyo bwana Diamu, kasema yeye mwenyewe atahakikisha anakufikisha polisi, nimeshampa nakala ya hii RB,...’akasema huyo mwanadada, na jamaa akawa kimiya.

 ‘Natumai unakumbuka kosa lako, kosa lako lipo kituo cha polisi, wao muda wowote wanaweza kukukamata, hata huko uwanja wa ndege wameshaweka watu wao, anayekudhamini kwa sasa ni huyu Diamu, nikuambie ukweli, kama  asingelikuwa ni huyo jamaa, ungelishakamatwa muda mrefu tu, siku unakanyaga uwanja wa ndege kutoka huko Marekani mimi mwenyewe nilikuwa hapo uwanja wa ndege, nilikuwa nimetoka safari zangu, nikakuona...’akasema

‘Nilipokuona nilitamani kutapika, nikikumbuka yale uliyonifanyia, nikataka kupiga simu polisi, lakini nikaingiwa na uungwana, nikaona nikupe nafasi, uje , uonane na jamaa zako...nikawaarifu polisi, na sasa niliongea na mkuu wa kituo, akalifufua jarida lako, nay eye mwenyewe akasema atalifuatulia, huyo mkuu wa kituo, ni mmoja wa jamaa zangu...’akasema

‘Wakatumwa wapelelezi kuhakikisha kuwa hupotei, na mimi mwenyewe, nikawa nakufuatilia hatua kwa hatua, hadi unafungua hospitali yako mimi nafahamu, na mimi mwenyewe kwa kuhakiki, niliwahi kuja kutibiwa hapa, japokuwa niliyeonana na huyo msaidizi wako....’akasema

‘Nafahamu yote, na jinsi unavyowasiliana na watu wako huko Marekani, jana walikupigia simu kuwa unahitajika kwenda, nafahamu yote, kuwa sasa unajiandaa kurudi Marekani huko wamekuahidi kazi nzuri, lakini ukumbuke, mwenye kovu hata siku moja usizani kapoa...kovu uliloniachia ni kubwa sana,.....’akasema huyo mwanadada, japokuwa alishasahau na ujasiri ulishajijenga lakini alipofika hapo machozi yalimlenga lenga.

Yule docta akabakia ameduwaa, hakujua afanye nini, alijua kabisa alishafanya kosa, na hapo alitaka kumwambia huyo mwanadada kuwa atatumua ujuzi wake wote kuhakikisha anamwezesha huyo mwanadada kurekebishwa kizazi chake tena, lakini kwa jinsi anavyofahamu itakuwa vigumu, lakini ...

‘Sasa basi,uamuzi upo kwako, uwe na Diamu, ili aendelee kukudhamini, au uachane naye, ujitutumue kupanda ndege, na nitahakikisha, kuwa siku hiyo unakamatwa na unakwenda jela...

‘Nina kisasi na wewe, nitahakikisha unakwenda jela, unasikia, hapa nilipo natamani nikufanye kitu mbaya, mimi sio yule mdada aliyefika kwako akilia tena...hili chozi linalonilenga lenga, ni kwasababu nakuona bado upo hai,...’akasema akionyesha uso wa hasira, chuki...
‘Nikuambie ukweli, mimi ni mtu mwingine, nafahamiana na wakubwa, hapo polisi kuna watu wangu, na wameshalifufua jalada lako la mashitaka, wameshakusanya ushahidi wote unaohitajika,...mshukuru sana huyo bwana Diamu....’akasema huyo mdada sasa akamsogelea karibu na wakawa wanaangalia uso kwa uso.

‘Haya niambie docta unasemaje, ...utakwenda kuonana na Diamu, au nifanye kazi yangu?’ akauliza huku huyo mdada akinyosha mkono kumkabidhi huyo docta hiyo kadi....

Docta taratibu akainua mkono, huku mkono ukimtetemeka,....NB: Hebu niambie umeionaje sehemu hii...tuwe pamoja yote haya yanapatika ndani ya diary yangu , na huyo ni mtu mwingine, akitafutwa kuingia kwenye mtandao wa Diamu, je alikubali, je safari ilikuwepo..., tuzidi kuwemo

WAZO LA LEO:Maisha ya ujanja ujanja yana mwisho wake, usione umefanikiwa na mali ya dhuluma ukafikiri umeshinda, hapana dhuluma uliyomtendea mja wa mwenyezimungu haiishi kirahisi, dhuluma hiyo itakuandama, ni swala la muda tu, hujui lini hali itabadilika...

Angalia mifano hai, wangapi wangapi wanataabika kitandani, wakijuta kwa yale waliyowatendea wenzao, dhuluma wizi, ufisadi, ilikuwa kazi yao, wakatajirika, sasa wapo kitandani, hawajiwezi, utajiri wao hauwezi kuwasaidia tena, mali ya dhuluma haina msaada tena, waliodhulumiwa wanazidisha kilio, na kilio cha mwenye kudhulumiwa hakina kinga,...


Oh, ewe mja wa mwenyezimungu, jamaa, tajiri, bosi, muheshimiwa,tubu makosa yake, muombe msamaha uliyemkosea, rejesha mali ya dhuluma kwa wenyewe kabla mlango wa toba haujafungwa....

Ni mimi: emu-three

No comments :