Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 3, 2014

DUNIA YANGU-UTANGULIZI


‘Kile kisu kilipopokelewa na yule mtoto, mwili wote ulianza kusisimukwa,..’ alianza kunisimulia mpelelezi kuhusu chimbuko la dunia yangu.

‘Na hadi kufikia kumpa huyo mtoto hicho kisu ilikuwa ni baada ya juhudi kubwa sana ya kwani ilikuwa kama kuna mtu anamzuia yule baba asiweze kufanya hivyo, na ilikuwa ni lazima huyo baba afanikishe hilo, kwani kuna mambo ya utangulizi alishayafanya, na hapo ilikuwa ni hitimisho.

‘Baba huyo alitakiwa kukabidhi majukumu na utaratibu mzima kwa huyo mtoto, kutokana na ile hali ya ugumu wa kulifanya hilo, yule mzee alihisihuenda mtoto wake huyo alikuwa akikiogopa kukishika kile kisu.

‘Japokuwa mtoto huyo alijengwa, alifundishwa na kulelewa kijasiri, ikitambulikana kuwa ndiye atakayeshika hatamu za familia hiyo, kwahiyo hakuwa muoga, na asingeliweza kuogopa kitu kama hicho, sasa kwanini hali ile itokee, mzee akawa anajiuliza, kwanini kitu kidogo, kisu tu kimuogopeshe yule mtoto(kijana)

Hata hivyo yule mzee ambaye kwa muda huo alikuwa kalala kitandani, sio kulala kwa moja kwa moja, hapana, alikuwa kalala huku kaegemea mtu, kwahiyo alilala nusu na nusu huku mto aliolalia ukiwa umeweka sehemu ya mgongo na kumfanya awe kakaa nusu na nusu kalala...

Baba yule pale hakuweza kusema kitu, alichofanya ni kujitahidi kumuashiria yule mtoto asogee ili aweze kumkabidhi hicho kisu mkononi, hapo hakukutakiwa kutamkwa neno zaidi ya yale maneno ya kukabidhi majukumu, kauli hapo sio muhimu, cha muhimu ni vitendo, ndio maana ya kutokuongea hapo.

Baba yule alikuwa ameanza kuumwa, na ilifikia hatua hakuweza kutoka nje, akawa mtu wa kitandani, na ndipo siku moja akaota kuwa muda umefika kukikabidhi hicho kisu kwa mrithi wake, na mara ya kwanza alipuuzia, lakini alipoona hali inazidi kuwamba mbaya, ndipo akamuambia mkewe, kuwa wakati umefika way eye kutoa majukumu yake kwa mrithi wake.
‘Kwahiyo unataka kumpa nani hayo majukumu?’ akauliza mkewe

‘Hilo swali la kuniuliza mke wangu, mwenyewe uliona juhudi zangu kwa mtoto wetu huyu tunayeishi naye, wengine wamekuwa mbali na mimi, huyu ndiye ninayeona anafaa kushika hatamu za kifamilia...’mzee akasema na yule mama akatabasamu na kusema

‘Mambo si hayo, nahisi muda sas amefika, haki ichukue mkondo wake, na mimi roho yangu itulizwe,..nilikuwa naliombea sana hilo lija kutokea, lakini nilikuwa naona linachelewa...’akasema mkewe na mume mtu akamuangalia mkewe akijiuliza ana maana gani, lakini hakuweza kupata muda wa kumdadisi maana dakitari alishafika, na kuendelea na matibabu ya kumpima na kumfanyia mazoezi ya viuongo, baada ya hapo, mze yule akamuita mtoto wake.

Mtoto wake alipofika, alionyesha adabu zote, halafu, akawa kama ana jambo anataka kumuambia baba yake, lakini baba yake akamuashiria kuwa huo sio muda wa kuongea.
Mzee akajitutumua na kuweka mto vyema, na akawa sasa kalala mtindo wa kukaa, ili aweze kumuona mtoto wake vyema, wakaangalia kwa muda, halafu baba akachukua ala ya kisu iliyokuwa pembeni mwake, ala hiyo huwa haachani nayo,..

Mzee akaifungua ile ala, na kukichomoa kile kisi kwenye ala yake, akakishikilia mkononi, kilikuwa kisu cha kawaida, ukikiona juu juu, lakini kiimani zao ni zaidi ya kisu, kilikuwa kinameta meta kwa weupe na makali yake yalikuwa sawia,...mzee akakitembeza mkononi, halafu akakishikia mfano wa mtu anayetaka kumchoma mtu mwingine, akakiashiria mara tatu, kama vile anachoma kitu..

‘Baadaye yule mzee, akashika kwenye makali, na kule kwenye mpini akaelekeza kwa mtoto wake, akitaka, mtoto huyo akishike..pale ndipo mambo yalipoanza..

‘Baba mtu mkono ukawa unatetemeka, kukawa na ni kitu kinamrudisha mkono wake nyuma,...lakini baba mtu akihisi labda ni kutokana na kuumwa, yeye akaendelea na taratibu za kutamka yake maneno ya kujitoa kwenye majukumu na kumkabidhi mtoto wake majukumu hayo, ni maneni ambayo mzee hakuweza kuyasahau hadi muda huo toka alipokabidhiwa kisu hicho akiwa mdogo hadi umri huo wa uzee...

Ilitokea nguvu ya ajabu ikawa inautetemesha mkono wa yule baba, na mkono ukawa kama unavutwa nyuma, kwa muda ule hakutakiwa kusema neno jingine, ni yale yale maneno ya kukabidhi kisu kwa mtoto, lakini mtoto alikuwa mbali kidogo na uwezo wa mkono wake ulikuwa umeshindwa, mkono ulikuwa mnzito kusogea na ulikuwa kama unavutwa kurudi nyuma, na mzee akawa anajitahidi kumuashiria mtoto asogee karibu akipokee kile kisu, lakini mtoto alikuwa akimuangalia baba yake kwa uso wa mshangao.

Mtoto yule alikuwa kama yupo mbali kabisa, mawazo yake hayakuwepo hapo, kitu ambacho kilimfanya baba atake kutamka neno la ukali, au kumuashiria asogee karibu,lakini hakutakiwa kusema neno, angeliharibu taratibu za hilo zoezi, na yule mtoto hakuweza kuiona ile hali kwa mtoto wake, mtoto alikuwa amekaa pale pale, uso wake ukiwa umejaa kitu kama mshangao, kama vile anaona kitu kingine cha ajabu kutoka kwa baba yake!

‘Hata hivyo yule baab hakukata tamaa, akajitahidi,akijua huenda ni moja ya changamoto, za hayo makabidhiano, na huenda alitakiwa kufanya juhudi kuonyesha dhamira ya kweli, ya kuyatoa hayo mamlaka kwa mtoto huyo.

Juhudi zake baadaye zikazaa matunda, yule mtoto naye aliona kile kisu kikiwa mkononi mwa baba yake kwa muda mrefu, na baba anahangaika, akataka kuinua mkono wake, ili akipokee, na hapo napo ikawa ni maajabu mengine, maana ule mkono wa yule mtoto ukawa kama unatetemeka, na mtoto alionekana kupambana na kitu kilichokuwa kikimvuta mkono wa yule mtoto ili asifikie kile kisu, lakini mtoto naye akawa anajitutumua, akikumbuka mazoezi ya baba yake  ya kutokukubali kushindwa, akajitahidi kunyosha mkono kukipokea kile kisu....

Yule mtoto hatimaye mkono wake ukaweza kushika eneo la mpini wa kile kisu, ghafla sura ya yule mtoto ilibadilika..hili mzee aliliona akilini, sio kwamba kweli sura ya yule mtoto ilibadilika, hapana, ni kama hali ya kumbukumbu ya taswira ikaonyesha hivyo, ni kama akili kufunguka na kukumbuka sura ambayo licha alizoea kuiona lakini sura ile ikawa inamkumbusha jambo, mzee akahisi labda ni kuchanganyikiwa kwa akili

Na muda ule ule wakati kisi kimeshashikwa na mtoto,kwenye mpini na baba kashika kwenye makali, mzee aliona kisu kile kama kinabadilika rangi, kutoka kwenye weupe wake, na kuanza kutapakaa rangi nyekundu, rangi ya damu, kilianza kidogo kidogo kutoka kule aliposhikilia mtoto na kuja hadi kwenye ncha ambayo baba alikuwa bado kaishikilia, na hapo akakumbuka kauli ya babu yake...

Kisu hiki ni kisafi, na usafi wake ni ishara ya utakatifu, na kinatakiwa muda wote kiwe hivyo, na hali ikiwa shwari, haki ikitendeka, na kukawa hakuna uvunjifu mkubwa wa amani, kisu hiki kitabakia hivi hivi, kitaashiria, upendo na amani kuendelea kuwepo, na ilivyo kinatakiwa kiwe hivyo wakati wote, kisibadilike rangi yake, hakikisha unakitunza, na kutunza mila na desturi zetu....’ilikuwa sauti ya babu

‘Kisu hiki kinaweza kubadilika rangi, kiabdilike rangi chenyewe...?’ nikauliza kwa udadisi.

Ndio lakini ni pale ukikosea masharti, na kawaida dalili hizo huanzia mwanzoni pale mrithi anayechukua hayo mamlaka anapokuwa anamkabidhi mtu mwingine asiyefaa, au huyo aliyekichukua akawa anafanya mabaya,...ndio maana mtawala wa kipindi hicho anatakiwa kuwa makini, awe na uadilifu, amlee huyo anayehisi ni mrithi wake katika maadili mema, kwani kiongozi mwema huanzia utotoni ...’akasema babu

Yule mzee alianza kuwaza pale pale, kwa kujiuliza nimekosea nini, maana kiukweli mtoto huyo nilimlea vyema kabisa na kuonyesha dalili zote za mtoto mwema, hakuwahi kufanya mabaya ya kuiaibisha familia, na kama alikosea ni makosa madogo madogo ya kiutoto na sasa kafikia ujana, na kuwa kijana jasiri....sasa hili linalotokea hapa lina maana gani

Wakati anajiuliza hayo kichwa chake kikawa kama kimefunguka, na hisia fulani zikamjia akilini mwakeu, yule mtoto ambaye sasa alikuwa kashikilia kile kisu, akiwa anahangaika nacho kukishika vyema na wakati huo mkono wa yule mtoto ukawa unaonyesha maajabu mengine,ule mkono ukatuna kama le mikono ya wainua vyuma, kuashiria kuwa kashika kitu kizito sana, asichoweza kukihimili, lakini akawa akijitahidi kukishikilia

Na muda ule mzee aliona kisu chote kikiwa chekundu, ...damu, ishara ya damu, ishara mbaya...

Yule mtoto kwa juhudi kubwa akawa kakishikilia vyema sasa kile kisu mikononi mwake, na kwa zile juhudi.Baba mkono wake ukabakia mtupu, lakini baba alikuwa akimuangalia yule mtoto kwa uso wa mshangao, kwanza kijana yule hakuwa na mwili bado wa kuwa na misuli yenye nguvu kiasi hicho, maana mkono ulituna na misuli ukaonekana imejipanga mkononi,...mzee akajipa moyo kuwa huenda ndivyo ilitakiwa iwe, japokuwa kwake haikuwahi kutokea hivyo.

Mzee yule aliendelea kumuangalia yule mtoto wake usoni, na wakati huo akili ilikuwa kama imemfunguka kumuelezea jambo...na sasa sura aliyoiona sio sura ile aliyoizoe,japokuwa ni sura ile ile, alihisi kama kaona sura ambayo hakuwa ameifikiria kabla,na sura hiyo ikamkumbusha jambo...

‘Sura ya mtoto huyu mbona sasa naiona inafanana kama mtu niliyewahi kumjua, ni sura ya...’hapo akahisi kitu kikichoma kwenye moyo wake, na kuhisi mwili ukiwa kama umekufa ganzi upande wote wa kushoto, lakini akili ilikuwa vile vile ikiwaza, na kujikumbusha

Ilikuwa ni sura ya mtu mzima, sura ya mtu aliyewahi kumfahamu, japokuwa sasa ni marehemu..., sura ya aliyekuwa mpinzani wake, mpinzani wake toka utotoni hadi pale alipomshinda na kuweza kumpata mama wa mtoto huyu...

‘Mhh mbona hili sikuwahi kuliona kabla, mbona sura hii naiona sasa kama ngeni kwangu, mbona mtoto huyu nimekuwa naye wakati wote lakini sikuwa kufikiria hivyo...’yule baba mtu akawa akiwaza, na hapo akasikia sauti ikisema akilini mwake, ni sauti ya aliyekuwa babu yake, pale alipogundua sura ya mtoto wake, na kumfananisha na huyo marehemu, sauti ile ya babu ilisema;

‘Kisu hiki ni cha urithi wa kimila, na anayestahili kukipokea ni mmoja wa damu ya familia, na ilivyo ni kuwa baba anatakiwa kumkabidhi mtoto wake anayestahiki,mtoto huyo awe ni damu yake,na awe amemzaa huyo mtoto ndani ya ndoa halali kwani kisu hiki kinajulikana kama kisu kitakatifu cha kimila...’sauti ya babu yake ikasikika ikisema akilini mwa huyo baba mtu.

Oh, sasa itakuwaje, maana ishara niliyoiona hapa ni kuwa huyu mtoto sio damu yangu,..lakini haiwezekani, maana nimeishi na mtoto huyu tangia akiwa mchanga, sikuwahi kuhisi sura hii kabla, sikuwahi kumafananisha na huyo aliyekuwa adui yangu, sikuwahi kusikia mtu akisema mtoto huyu anafanana na huyo marehemu, sasa leo imekuwaje, na hapo sauti ya babu ikaendelea kusema;

Kama ukimkabidhi mtu ambaye sio damu ya familia hii, mtu ambaye hastahiki, ujue ni lazima kuna baya litatokea, na baya hilo litaanzia kwako, na hali hiyo isipozuiwa na mtu wa familia haraka iwezekanavyo, basi kutazuka balaa, na balaa hilo litakwenda mbali zaidi...uwe makini kwani tumekuwa makini kizazi hadi kizazi,...’akakumbuka alivyoambiwa

 Baba mtu alipoiona ile ishara, ishara ya sura ya mtoto wake, akifanana kabisa na mpinzani wake, kitu ambacho katika maisha yake, katika malezi yake, hakuwa amekigundua hicho, mwili wote ukawa hauna nguvu, aheri mkewe angelikuwepo hapo akamuuliza, lakini mkewe hakutakiwa awepo hapo akifanya hilo jambo, ni jambo kati ya baba au babu na anayestahiki kukabidhiwa jukumu hilo...

Baba mtu akamtupia mtoto wake jicho jingine, sasa likuwa jicho la uwoga, wasiwasi, mashaka,  na kweli sasa aliweza kuiona sura ya yule mtoto, ni kweli sura ile ilikuwa ikifanana na aliyekuwa mpinzani wake, hakuna shaka hapo huyo mtoto, ambaye sasa kafikia ujana sio damu yake,..

‘Sasa nifanye nini...?’ akajiuliza, huku akihisi shinikizo la damu likiongezeka, kichwa kikawa kinamuuma sana, na mara akahisi kitu kikimtafuta upande wa kushoto,na alipojaribu kuinua mkono wake upande wa kushito, akashindwa, ilikuwa kama sehemu hiyo haipo, haiinuki, hii iliashiria kuwa upande huo umeshapooza, hawezi kuuinua tena...hapo moyo ukazidi kumuenda mbio, na alitaka kutamka jambo, kumuambia yule mtoto amuite dakitari, lakini sauti haikuweza kutoka.

Kisu sasa kilikuwa mkononi mwa yule mtoto, akiwa kakidhibiti vyema, ile hali ya kutetemeka kwa yule mtoto ilikuwa imekwisha, lakini sura ilikuwa ni ile ile, ni sura yake ya kawaida, lakini sura ile ilikuwa ikifanana na huyo marehemu, baba mtu hakuwahi kuligundua hilo akilini mwake kabla

‘Ina maana kweli huyu mtoto sio damu yangu.....’akajiuliza akilini

‘Sasa nitafanya nini..?’ akazidi kujiuliza, lakini sasa kisu kilishafika mikononi mwa mtoto ambaye kumbe sio damu yake, na taratibu za awali zilishapita, na ina maana sasa hapo mzee hana mamlaka, hana nguvu za asili alizokuwa akitamba nazo, sasa atafanya nini.

‘Ni lazima nimnyang’anye huyu mtoto hiki kisu haraka, halafu nikaulize taratibu gani nifanye, ili kulisafisha hili kosa,lakini nitafanyaje na mimi siwezi kuinuka, na mimi siwezi hata kuongea...’akawa anajiuliza akilini

‘Lakini kwanini, kwanini mke wangu akanifanyia hivyo, na kwanini akili yangu muda wote huo haikuwa imeligundua hili...’akawa akijilaumu...

Hapo akamtizama yule mtoto tena, mtoto ambaye sasa alikuwa kakishikilia kile kisu, na sasa akianza kutabsamu, lakini tabasamu lile halikuwa la furaha, lilionyesha chuki fulani,...na hapo mzee huyu akakumbuka chuki aliyokuwa nayo huyo mpinzani wake, hasa siku ile alipomtamkia kuwa sasa keshamuoa mama wa mtoto huyo, ambaye kabla ya hapo, alikuwa mchumba wa huyo adui yake.

Wakati anawaza hayo, mara kitu cha ajabu kikatokea, yule mtoto akiwa kakishikilia kile kisu mara sauti nzito, ikaanza kutoka mdomoni mwa yule mtoto, sauti nzito kweli, na sauti ile ilimtetemesha yule mtoto, na kumfanya yule kijana, atoe macho, kama anatishika, na ni dhahiri ilikuwa kama kitu kimemuingia yule kijana, kwani alikuwa akitetemeshwa huku jasho likianza kumtoka, yule kijana sasa akawa akinguruma,na ghafla akasimama kutoka pale pembeni ya kitanda alipokuwa amekaa.

Baba mtu akamuangalia yule kijana, kwake yeye ni mtoto tu, alimuangalia kwa hali ya kuogopa sasa, ..akiwa amelala pale kitandani, akiwa bado  anaugulia , akajua sasa siku zake za kuishi zinahesabika,,na alitakiwa kulifanya hilo, kumkabidhi huyo mtoto wake kisu cha urithi, sasa kumbe kavuruga, sasa kumbe huyo mtoto sio damu yake, na kwa kufanya hivyo kakiuka mila, na balaa linaweza kuanzia kwake...lakini kwa upande mwingine mapenzi ya baba kwa mtoto huyo yalikuwa hayajaondoka, kwani alimlea na kumpenda, ....kosa ni kutoka kwa mke wake.

‘Oh, mungu, nimefanya kosa gani...?’ akawa anajilaumu

Mke mwema,...mwanangu hakikisha kabla hujaoa uwe umefanya uchunguzi wa kina, hakikisha kuwa kweli unayetaka kumuoa ni mke mwema, maswala ya ndoa sio ya kukimbilia tu, ni maswala yanayohitaji umakini, ...mchunguze mwenza wako, uliza wakubwa zako, watakuambia, watakuelekeza mke mwema ni yupi,..’hii ilikuwa kauli ya baba yake siku alipotaka kuoa, baba yake kipndi hicho alikuwa anaumwa, na kifo chake kikatokea hata kabla baba huyu hajamuoa mama wa mtoto huyu aliyekabidhiwa kisu leo.

Baba huyo mchumba wangu nimempenda sana, sitaweza kuachana naye, nina uhakika kuwa yeye ni mke mwema kwangu, kwani mimi ndiye ninayemuoa, sihitaji kuuliza watu, ..baba usiwe na shaka, huyo atakuwa mkwe wako mwema...’akasema huyo baba mtu.

Baba yake huyu hakutaka kubishana na huyo mtoto wake, kwani yeye kwa muda huo alikuwa kwenye wakati mgumu, akigua, maradhi ambayo yalimtesa sana, hadi akafariki dunia bila kujua hatima ya mtoto wake huyo, na mtoto wake huyo akawa akimtegemea babu yake, babu ambaye baadaye alikuja kumkabidhi kisu , kwani hakukuwa na mrithi mwingine kwa wakati huo, wengine walikuwa mbali, wakihangaika na maisha yao.

Yule mtoto aliendelea kunguruma kama simba, na sasa alikuwa kasimama, na kusogea mbele, pembeni ya baba yake, wakawa wanatizamana baba na mtoto, baba akishindwa kufanya lolote, hawezi hata kutamka neno, machozi sasa yakawa yanamtoka akijuta kutokumsikiliza baba yake, alipenda kupitiliza, na hakuwa akiwasikiliza hata ndugu zake walipomshauri kipindi hicho, akaona na baadaye akaja kumzalia huyo mtoto anayepewa kisu leo..hakuwahi kuhisi kuwa mke wake anaweza kumsaliti,...alimpenda na kumuamini.

Yule mtoto sasa akiwa kakishikilia kile kisu vyema, akiwa ananguruma, akiwa katoa macho ya hasira, akitikisa kichwa kama kukataa, alikuwa akikataa nini, baba mtu akawa anamuangalia tu na kujiuliza, akiwa hana la kufanya

Baba mtu akaanza kuona wasiwasi, kinyume na alivyotegemea, alitegemea leo ingekuwa siku ya furaha kwa familia, siku ya kumhakikishia mwanae kuwa yote aliyokuwa akimfanyia mtoto huyo ya kumjenga kiujasiri,sasa matunda yake ndio hayo, ya kukabidhiwa jukumu la kifamilia.

Alikumbuka jinsi alivyokuwa akimfundisha mtoto huyo, ambaye mara nyingi alionekana kutokutimiza mambo mengi aliyokuwa akimuelekeza, tofauti na alivyokuwa yeye, babu yake aliwahi kumuambia kuwa yeye alikuwa mtiifu sana, na kila alichofundishwa alikifuata sawasawa tofauti na alipokuwa akimfundisha huyu mtoto wake, ilikuwa vigumu kumfanya ajue jambo, na kulifuata, ilichukua muda, japokuwa baadaye alikuwa kuweza na kuwa na muelekeo japo sio sana.

Mara nyingi mama wa mtoto alimtetea sana mtoto wake huyo, na baba ili kuonyesha ubaba wake, akawa anamchapa sana huyo mtoto ili aelekee anavyotaka yeye, lakini yota hayo yakiwa na lengo moja, vyote vilifanyika makusudi, ili mwisho wa siku mtoto huyo aweze kujengeka vyema ili aweze kulipokea jukumu kubwa la kuilea famlia, lakini kumbe alikuwa akimlea mtoto asiyekuwa damu yake bila kujua, ilikuwa siri ya mama wa huyo mtoto.

Baba akiwa na mapenzi, akamuomba mungu angalau aweze kumsaidia mtoto wake, maana aliona mabadiliko kwa mtoto wake yasiyo ya kawaida, na kweli dua zake zikapokelewa, mara sauti yake ikatoka;

`Vipi mwanangu unaumwa, nimuite dakitari’ Baba mtu ghfala akaweza kuongea, na kumuuliza mtoto yule kwani hakuwahi kuiona hali hii kabla kwa mwane, na japokuwa yeye ndiye aliyekuwa akiumwa zaidi , lakini sasa akawa anahisi mtoto wake ndiye anayeumwa zaidi, mapenzi ya mzazi kwa mtoto....

Baba mtu hali ile ilimtisha,akaona ni vyema amuite dakitari, akitumia mono wake wa kulia ambao ulikuwa sasa una nguvu tofauti na upande ule wa kushoto, akajitutumua na kuweza kujisogeza, huku mtoto akimuangalia, ...mtoto alikuwa akimuangalia huku macho yamemtoka, mdomo upo wazi, ukihema, kama anavyohema simba....

Baba mtu akajitahidi hadi mkono ukaweza kukifikia kitufe cha dharura cha kumuita dakitari...

Wakati baba mtu anataka kubonyeza kile kitufe cha kuomba msaada wa dakitari akizani mwanawe amepatwa na mshituko wa ghafla, mara akahisi kitu kikali kikichoma kifuani kwake, sasa sio kile cha awali, mchomo huo ulikuwa tofauti, kwani sasa alihisi maumivu makali yakipenya kifuani katikati ya moyo, na wakati macho yake hayaamini nini kinatokea, alisikia kisu kikivutwa toka mwilini na kikatua tena mwilini kikapenya moja kwa moja na safari hii hakikukosea kilimaliza maisha ya bwana tajiri, bwana Mapesa! ..gizaaaaaa....

NB: Karibuni kwenye kisa hiki kipya, chenye vionjo mbali mbali, mikasa , mapenzi, usaliti, mauaji..na huo hapo juu ni utangulizi tu...hebu tuone hii ndoto ya dunia yangu ilianzaanzaje...

WAZO LA LEO: Makosa makubwa huanzia kwenye chaguzi zetu za kumpata mke au mume mwema, tumekuwa tukipuuza sana haya maagizo na maelekezo ya wakubwa zetu, na hasa mafundisho tunayoyapata kutoka kwa viongozi wetu wa dini, na kuyazarau kabisa maandiko matakatifu, kuwa ili uwe na familia bora, unahitajika kumpata mwenza mwenye muelekeo, usikimbilie tu kwa ushahiwishi wa kimwili, ukaona sura, na mwili ni kivutio pekee,...amani , upendo, furaha huanzia hapa penye kumpata mke au mume mwema.


Ndugu wapendwa mnaotaka kuoa au kuolewa, kabla humjachukua maamuzi ya kuoa, au kuolewa, muombeni sana mwenyezimungu, pia ulizeni kwa wakubwa kumjua mwenza wako vyema, chunguza kwa makini kabla ya kutekwa na ushawishi wa kimwili, tukumbuke kuwa mke au mume mwema hutoka kwa mwenyezimungu, na hili ni kutokana na maombi yako kwa mwenyezimungu.

Soma sehemu ya kwanza

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hey! Do you knoա if thеƴ make any plugins to aѕsist with SEO?
I'm trying to get my blߋg to rаnk for some tɑrgeted keywords but I'm not seeing very good results.
If you know of any please shɑre. Cheers!

my ԝebpage temp2