Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, July 31, 2014

DUNIA YANGU-9



Docta alikuna kuna kichwa huku akimuangalia nesi wake kama ataweza kumpa wazo la kumsaidia, lakini kwa muda huo nesi naye alikuwa na mawazo  yake kichwani, akiwa kashikwa na wasiwasi kuhusu mabadiliko aliyoyaona kwa bosi wake, akawa tu anamuangalia bosi wake kwa mshangao,

‘Huyu bosi ana nini leo au ni hizi pombe alizokunywa leo,....’akawa anajiuliza kichwani kwani hii sio kawaida yake anapotajiwa mteja mwenye sifa kama hizo alizomtajia ambazo kweli sifa hizo anazo huyo mteja aliyekuja,...

Docta alipoona nesi wake kaduwaa akimuangalia akajua hapo sasa hana jinsi , akageuka nyuma kuangalia kama kuna sehemu ya kuweza kujificha au kutokea, akaona hakuna hutaamini, kwa muda huo alishaisahau ofisi yake mwenyewe kuwa ina mlango mmoja tu wa kuingilia na kutokea, ...

‘Hii sasa ninalo, sina jinsi, huyu nesi hawezi kufanya lolote, keshaharibu toka awali, anganipigia simu kwanza,...ooh, siwezi kumlaumu sana...’akawa anajisemesha kichwani huku akiendelea kujikuna kichwani.

‘Huyu mdada kama ndio yeye sizani kama ataweza kunisamehe, hata kama ni tajiri, lakini kwa hayo niliyomtendea, mmh, sijui, na hawa akina dada, huwa hawasahau mabaya waliyotendewa kwa urahisi...hili sasa ninalo, lakini.....’akajaribu kufikiria njia ya kufanya

Wakati anawaza afanye nini, ...akilini akaanza kukumbuka tukio lilisababisha haya yote, tukio ambalo lilimtia doa, na alijua hataweza kulisafisha hilo doa, mpaka mtendewa mwenyewe akiri kumsamehe,...na huenda angelifanya hivyo kama wangelikutana, je leo kaja na kwa nia mbaya au ndio kaja kumfunga,....hapo akataka kumuuliza huyo nesi kama hakuja na polisi,

‘Ni kimuuliza huyu nesi nitazua maswali mengi....’akajisema na mara kichwani kumbukumbu ya yalitokea kati yake na mwanadada huyo zikaanza kumjia kichwani, akaanza kukumbuka tukio lenyewe, na kumbukumbu hizo zilimjia kwa haraka sana....

******
 Siku hiyo akiwa ofisini kwake ofisi isiyo rasmi, akiwa na chupa ya kinywaji chake akipendacho, alijilaza kwenye kiti huku akiwa jinsi ya kupata pesa, kwani mshahara wake alishaukopa wote, na ofisi yake ya vichochoroni hailipi, polisi wanamuandama.

Akainua chupa yake juu kuangalia nini kimebakia, akakuta ni kama robo tu, akajifuta mdomo, akainama na kutulia, alihisi kama sauti inakuja mlangoni, na kwa haraka akavuta droo ya meza na kuiweka chupa yake, baada ya kuhakikisha kuwa ameifunga vyema mara , akasikia mlango ukigongwa.

‘Naomba huyo awe mteja...’akaomba kwa imani yake, na kuanza kujirekebisha vyema, huku akisema

‘Mhh, kama ni mteja mmh...’akawa anahakikisha meza yake ipo makini kwa ajili ya kupokea mgeni, akashika kipimio chake cha kidakitari akakivaa shingoni,...pamoja na ulevi wake, lakini akilini alikuwa makini.

Pale alitamani aitoe chupa yake apige mafundo mengine mawili, lakini akaona atafumwa, na hakupenda mteja wake amuone akinuka pombe, akavuat droo nyingine akatoa chupa ya manukato ya kuondoa harufu akapuliza na kujipulizia mdomoni..

Come in....’akasema,

Mara mlango ukafunguliwa, akaingia mdada mmoja mrembo, akili yake ilisimama kwa muda, hakuamini, lakini kitu kilichomshangaza na kumfanya ile hali yake ya kushangaa iwe ya namna nyingine ni ile hali ya yule mdada, pamoja na urembo wake, lakini alikuwa analia

Hii ilionyesha wazi kuwa huyo mdada ana tatizo kubwa, docta akavuta pumzi na kuzikaribisha hisia za maliwazo , alijua ni nini afanye kwa muda kama huo, hiyo ilikuwa akzi rahisi kwake, lakini kuna kitu kingine kilishateka nafsi yake,....tamaa.

Akijitahidi kusimama akayumba karibu adondoke, lakini akajishikiza kwenye meza, akaona akisimama kwa muda huo ataumbuka, akarudi akakaa, na kumkazia yule mdada macho, sura ya yule mdada ilionekana kama lulu machoni mwake, akasema;

‘Kwaza tulia sitaki mtu kulia kwenye ofisi yangu, maana hapa ni sehemu ya neema, sehemu ya kuondoa matatizo sio ya kulia, hebu niambie una tatizo gani...?’ akauliza, na mdada akawa anafuta machozi

‘Kaa kwenye kiti, ....’akasema docta, na yule mdada akawa sasa katulia, na akasogea kwenye kiti

Yule mdada kwanza alimuangalia yule docta, alishasikia sifa zake, hakuona ajabu, alijua kabisa kalewa, lakini alishaambiwa kuwa huyo docta ili afanye kazi yake vyema ni mpaka alewe, hiyo ndio tabia yake, kwa mashaka akasogea kwenye kiti ni kukaa

‘Niambie mrembo una tatizo gani?’ akauliza

‘Nina mimba, na siitaki hii mimba, lakini.....’akasita na machoni kukaanza kujawa machozi

‘Lakini nini... wewe sema usiogope, umekuja kwa mtaalamu mwenyewe...’akasema docta huku akimkagua yule mdada kwa macho, hakuamini dada mrembo kama huyo anaweza kukutwa na hayo aliyoyasikia, akataka kujua zaidi, japokuwa kwake muhimu ilikuwa pesa, au vinginevyo....

‘Sina pesa kabisa,...nilikuwa nazo lakini nimeibiwa, ...na wazazi wangu walishanifukuza nyumbani, na aliyenipa mimba kanikana kabisa...sijui hata nifanye nini, ndio maana nimeona  niitoe hii mimba....’akasema huyo mdada

‘Oh, my God, ndio kinakufanya ulie, ...hapana, labda kama kuna jambo jingine,..lakini usijali, mimi nitakusaidia,unasikia mrembo, mimi nipo kwa ajili ya warembo kama nyie..hapa umefika,  ...’akasema docta akisimama, sasa alikuwa kajiamini.

‘Kweli docta, nitashukuru sana, nakuhakikishia nitakuja kukulipa pesa zako, ngoja mambo yangu yakae sawa, kwani kuna kazi nimepata, lakini....’akasita tena kuongea akawa kama anataka kulia.

‘Usijali, ....umesema umepata kazi, ....okey, sasa kwanini unaweka uwalakini...?’ akauliza

‘Ni kuhusu masharti ya hiyo kazi, wao hawataki mwanamke mja mzito, au aliyezaa...kwahiyo sitaki nijulikane kabisa kuwa nilikuwa na mimba....’akasema huyo binti.

‘Hahaha, hapa umefia, haina shaka kabisa nikuambie kitu, mimi najua jinsi gani nitakufanyia, haiwezi kabisa kujulikana, na nitakuandikia cheti cha kuthibitisha kwua wewe hujawahi kuzaaa, unasikia, ...’akasema docta

‘Lakini mimi sina pesa zakukulipa...’akasema huyo mdada

‘Nimeshakuambia pesa kwangu sio tatizo, kwanza kwanini utoe pesa, ...wewe mwenyewe ni pesa tosha kabisa, hahaha, wewe, ni mamilioni....’akasema na yule mdada akabakia mdomo wazi, hakujua huyu docta ana maana gani, akauliza
‘Una maana gani kusema hivyo?’ akauliza
‘Mhh, jamani ina maana huelewi, wewe sio mtoto mdogo, maana mpaka ukafikia kupata mimba, ina maana unajua kila kitu, sio lazima unilipe pesa,unaweza kunilipa kwa njia nyingine,...nikuambie ukweli wewe dada ni mrembo sana...’akasema na yule dada akashituka sasa akawa anataka kusimama ili aondoke.

‘Mmh, docta, hapana mimi sio kama unavyonifikiria, hata hiyo mimba niliipata kwa bahati mbaya, sana, siku hiyo alitumia nguvu...docta mimi naahidi nitakuja kukulipa pesa yako....’akasema

‘Mimi nimeshasema sitaki pesa yako, nitakusaidia, ila na wewe unisaidie, ni kitu kidogo tu kwangu..unajua nikishapiga gilasi nikaona mrembo kama wewe siwezi kabisa kuvumilia,...ni kidogo tu, tunamaliza tunaanza  shughuli nyingine....’akasema docta sasa akimsogelea yule mdada, na yule dada  akawa keshasimama na sasa akawa anarudi nyuma.

‘Sikiliza mrembo, kwani kipi cha ajabu kwako wewe, wewe umesema huna pesa, lakini mwili wako unazidi pesa zozote utakazonilipa, kabla ya yote tumalize hili sio kitu kigeni kwako au sio....’akasema docta.

`Wewe docta vipi, nimekuambia pesa sina mimi ni pesa kwa vipi una maana gani wewe mbona sikuelewi....hebu niache, usinisogelee nitapiga kelele....’ ubishi mkali ulizuka, na kwa muda huo mzuka wa uzinzi ulishampanda docta huyo, hakuwa anajali kitu, pombe ilishamvuta hisia zake, na ibilisi akawa anashabikia....

‘Kumbe ndio tabia zako..mimi sitaki tena,....’yule mdada akawa kajitoa kwa docta na kumsukuma , na docta akapepesuka, lakini akajitulia na kujiweka sawa, akasema;

‘Unajua wewe dada, mimi nimeshakupenda, usijali, mimi nipo tayari kwa lolote lile uwe mpenzi wangu unaonaje, hata hiyo mimba mimi nitailea mwenyewe, lakini kwanza unipe uhakika wa hapa hapa...’akasema

‘Sitaki mwanaume mimi, yaliyonikuta yanatosha ninachotaka ni kuajiriwa niishi maisha yangu kivyangu....’akasema huyo binti na docta akaona atashindwa kumshawishi huyu binti, na hata akitumia nguvu, anaweza akazidiwa, lakini yeye ni docta ana mbinu nyingi tu.

Docta akajaribu kumuhadaa hivi na vile na alipoona binti haeleweki, akaanza kutumia nguvu tena, na alipoona hata nguvu hazifanyi kazi, akatumia dawa anazojua yeye mwenyewe na yule binti wa watu akapotewa na fahamu, na hapo docta akatimiza adhima yake, ....

‘Alipomaliza zoezi la kwanza, kwa haraka, akafanya kazi ambayo binti huyo aliijia, kabla binti hajazinduka jamaa akawa ameshaitoa ile mimba..ilikuwa rahisi kwake, lakini kwa pupa, na kwa haraka alijikuta kafanya kosa ambalo hakuwahi kulifanya kabla....
Binti akazindukana na kujikuta yupo kitandani, akasimama na kwa haraka akahisi maumivu tumboni, akalishika tumbo lake, akahisi maumivu yakiendelea, na mara docta akaja akiwa kashika dawa, akasema;

‘Maumivu ni kawaida, yatakwisha tu, tumia dawa hizi....’akasema

‘Umenifanya nini docta...?’ akauliza

‘Kwani wewe ulikuja kufanya nini hapa?’ akauliza

‘Mimi sikubali kwanza umenibaka, halafu ....mmmh,...’akawa amahisi maumivu makali tumboni, akawa anajinyonga nyonga, na hapo docta akajua ni lile kosa alilolifanya, akaanza kujijutia, kwanini hakutuliza kichwa chake..kwanini imetokea hivyo, na hajawahi kufanya makosa kama hayo kabla..

Yule mdada akapoteza fahamu, na alipozindukana, alijikuta yupo hospitali nyingine, akihudumiwa na docta mwanamke, na yule docta alipoona huyo mdada kazindukana akaanza kumhoji

‘Hebu niambie ilikuwaje?’ akaulizwa

‘Mhh, nimefikaje hapa?’ akaulizwa

‘Umeokotwa barabarani karibu na mtaro, na ukafikishwa hapa, na tulipokuchunguza tukagundua kuwa umetolewa mimba..lakini.....’akasita

‘Lakini vipi?’ akaulizwa

‘Aliyefanya hivyo alikosea, kakuharibu sana, inabidi tukusafishe, na sijui...tutaona baadaye, naona aliyefanya hivyo, hakuanya kwa uangalifu, ...ni nani huyo?’ akaulizwa

‘Kwani kanifanyeje, mbina hata sijui alichofanya...?’ akauliza akianza kulia

‘Kwanini kwanza ulifanya hivyo, hivi nyie mabinti mna akili gani, kwanini ukakimbilia kutoa mimba, huoni balaa ulilokumbana nalo, umeshaharibu kizazi..’akasema

‘Oh, mungu wangu,....’akasema na mwili mzima ukaishiwa na nguvu, ..

Kumbe  kwa papara za yule docta, aliitoa mimba na kumaribu binti wa watu kizazi, kiasi kwamba kupata mtoto mwingine ingekuwa ni miujiza. Alitibiwa hapo hospitalini na akashauriwa, kwenda polisi kumshitaki huyo dactari..

Na kweli huyo binti akiwa na ushahidi wa udakitari, akaenda kushitai polisi na polisi walishasikia taarifa za huyo jamaa toka kwa watu wengi, na walisubiria ushahidi kama huo;

‘Kwahiyo kakubaka, na kukutoa mimba bila rizaa yako...ushahidi upo wazi, ngoja tukalisokomeze ndani, safari hili harina ujanja...’akasema askari wa hicho kituo.

Polisi wakafika eneo alilokuwa akifanyia hizo shughuli huyo dakitari, kama walivyoelekezwa na huyo mdada, maana huyo jamaa naye alikuwa mjanja, kila siku alikuwa akibadilisha kituo cha shughuli zake, lakini hata hivyo, polisi walipofika kwenye eneo wakakuta kweupe, alishakimbia, japokuwa kulikuwa na mabaki mabaki ya ushahidi kuwa kulikuwa na dispensari isiyo rasm kutoka kwa mwenye nyumba, na mwenye nyumba akakamatwa kuisaidia polisi, lakini baadaye akaja kuachiwa na jamaa hakuonekana hata kazini kwake akawa haonekani.

Jamaa hakuwa na ofisi moja, hata hivyo aliona hali sio shwari kwake, akahama jiji kwa muda na kwenda kujificha mikoani... aliishia mikoani kwa muda, akitoa uzuru kazini kwake kuwa anauguliwa na baba yake, na baadaye akaomba uhamisho wa muda kufanyia kazi hiyo ya udakitari huko mikoani, akakubaliwa...kwani alikuwa na watu wakimsaidia huko kazini kwake, ...., alikaa huko mikoani karibu mwaka mzima bila kujulikana.

Docta huyu aliporejea, ndio akaanza harakati nyingine za kupata kipato cha ziada, ndio akajiingiza kwenye biashara ya madawa, na alijua jinsi gani ya kupooza mambo, bongo hii ukiwa na pesa hakishindani kitu...akajitahidi hadi akawa mmoja wa wakuu kwenye kitengo cha madawa, kwahiyo ikawa rahisi kwake kufanya kile alichokianza.

Mitaani yule mdada akawa anahangaika, akifika polisi anaambiwa bado wanamtafuta;

‘Mimi nimeambiwa karudi na kesharudi kazini kwake...’akasema

‘Sisi kila tukifika hatumuoni, usiwe na wasiwasi dada tutamkata tu...’akaambiwa

Yule mdada akaona kuna kitu kimechezwa hapo, akaamua kwenda ngazi za juu, na taarifa zake zikafika ofisini alipokuwa akifanyia kazi rasmi, kuwa huyo jamaa ana kesi ya kujibu kwa kuendesha shughuli za utoaji mimba na hata kubaka, na pale kazini waliposikia hivyo sasa wakaona hawawezi kumbeba tena huyo jamaa.

Walichofanya wao, ni kumsimamisha kwa muda wakisema wanafanya uchunguzi kujirizisha, kwani hata wao walishashuku hilo tatizo lakini walikuwa hawana uhakika ni nani anafanya hiyo hujuma, na waliona ili uchunguzi uweze kufanikiwa vyema, inabidi huyo docta apewe barua ya kusimamishwa kazi kwa muda...

Docta akasimamishwa kazi, kwa uchunguzi....

NB: Jembe na mtandao vinanipa shida, inabidi nimalizie hapa kwa leo....tupo pamoja

WAZO LA LEO: Udhalimu ukizidi, mioyo ya watu huota sugu, na hata ubaya ukitendeka watu wanaona ni awaida tu, hasa wakitendewa wale wanaoona sio wenzao. Tukumbuke kuwa dhuluma anayotendewa mwenzako kama wewe unaona na unafahamu kuwa ni dhuluma, halafu ukakaa kimiya bila kukemea, au kufanya jitahada zozote basi na wewe ni dhalimu, laana ya udhalimu huo itakuandama...na ipo siku utaulizwa.

Tuteeni haki, pale tunapoona wenzetu wasio na hatia wanadhulumiwa, tuache ushabiki usio na tija, ili dunia iwe ya amani na upendo. haki ikipotea, na dhuluma ikatawala, ujue ni swala la muda tu,  leo ni kwao na kesho ni kwako





Ni mimi: emu-three

No comments :