Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, July 25, 2014

DUNIA YANGU-8


 Docta alimshuku vibaya yule jamaa yake japokuwa kweli walisoma wote, mwanzoni alihisi huenda mwenzake ni mmoja wa watu waliotumwa kumchunguza, hasa kutokana na kauli zake, ikabisi amwambie;

‘Kwahiyo unataka kusema nini, una ushahidi gani kuwa nimekuambia hayo yote...achana na mimi bwana...’akasema akijaribu kujitoa mkononi mwa huyo jamaa.

‘Kwani vipi mate, una mashaka gani na mimi, mimi nina jambo muhimu nataka tuelewane, nataka nikutoe, kutoka hapo ulipo na kuwa dactari bingwa, wa ukweli, na uachane na udokozi...’akaambiwa, na docta sasa akatulia, akisikiliza kwa makini,  na moyoni akasema;

‘Nahisi kama jamaa anajileta mwenyewe kama sio kunitega...’, na alipoona jamaa katulia akasema;

‘Kwahiyo ni nini lengo lako,maana mimi ni mwanaume, usije ukategemea kulipwa fadhila kutoka kwangu,...hahaha, tutagombana..usione nimelewa, ukafikiri kuwa sina nguvu..niambie unataka tuongee nini....na kama umetumwa ujue kwangu hupati kitu hao polisi wenyewe tunagida nao kijiweni, utaniambia nini...’akasema sasa akiweka utani wa kujiamini, huku akishika tumbo kuonyesha kashiba vyema.

‘Mimi nataka tuingie kwenye dili za kipesa, ....’akasema huyo jamaa, na docta kusikia hivyo, `dili za kipesa’, akagutuka, na kusafisha kichwa kwa kukitikisa, akamkodolea jicho huyo jamaa yake, moyoni akisema; `anajileta mwenyewe’

‘Sijakusikia vyema, umesema dili za pesa au za posa, hebu rudia tena nikusikie vyema, maana hapo umenipandisha uchu wangu, ukitaja dili za pesa mimi napandisha mashetani, hooooho...au sikusikia vyema, sema tena....’akajitikisa na mwenzake akatabasamu na kusema.

‘Lakini sio rahisi kama unavyofikiria...inahitaji maandalizi na gharama....’akasema na jamaa akatabasamu na kusema;

‘Oh, unasema nini tena, hayo nafahamu bwana, hakuna dili ya pesa rahisi, nafahamu sana, mimi kiukweli natafuta pesa kama mtu mwenye kiu anavyotafuta maji, ...niambie dili yoyote, kama ipo kwenye fani yangu, nipo na wewe, sijali inafananaje, ilimradi ilete pesa,...haya niambie haraka kabla sijaghairi ’akasema akijipweteka kwenye kiti

‘Sikiliza kwa makini...’akasema yule jamaa na kuanza kumuelezea jinsi anavyotaka yeye, na alipomaliza yule docta akakuna kichwa huku akitafakari kwa makini,.....akasema;

‘Kweli wewe kichwa,....’akageuka kuangalia huku na kule, na akilini alikuwa kazindukana, kwani aliona kapewa jambo ambalo hakulitegemea na hapo alipo hakuwa na jinsi ila kukubali;

‘Mhh, lakini mambo ya kusoma tena...’akasema

‘Unaogopa kwenda kusoma?’ akaulizwa

‘Hapana, kichwa hiki ni cha aina yake, chuoni wenyewe walikuwa wakinionea gere, mtu husomi ile ya kusoma, nasoma kidogo tu, lakini mambo yanajipanga yenyewe, na nikipata gilasi moja tu, mtihani hauoni ndani.....’akasema na kucheka.

‘Sasa sikiliza , mimi nimekuelewa, ...lakini kama unavyoona sina mbele wala nyuma, hapo inahitajika pesa ya maandalizi, sijui hili , nguo, ada unaonaeeh, je hapo utanisaidiaje...?’ akauliza.

‘Mimi, sitaki usomee hapa nchini, nataka ukasome nje, ....’akaambiwa
‘Unasema nini?’ akauliza kwa kung’aka

‘Marekani.....’akasema huyo jamaa.

‘Acha utani....’akasema, akaambiwa mpango mzima unamuhitajia yeye kwanza kwenda kusoma Marekani, kuhusu ada, usafiri na gharama zote za maandalizi hiyo itashughulikuwa, yeye atapewa pesa kidogo kwa maandalizi yake binafsi. Jamaa hakuamini, akafurahi na kuomba aongezwe kinywaji kwa kujipongeza.

‘Sasa hivi siwezi kukunulia tena kinywaji, ninachotaka ni kuhakikisha umefika huko unapokaa....’akaambiwa, na jamaa akakubali huku akisema;

‘Kama kuna siku nimepewa jambo la maana katika maisha yangu, basi siku ya leo itakuwa kumbukumbu, kumbe ndio maana akili yangu ilikuwa ikiwaza ulaya ulaya, nikifika huko nitazibwia hizo za huko, hadi damu yangu inuke ulaya-ulaya hahaha, hata kama ni marekani hao ni wale wale tu...’akasimama na kucheza cheza, baadaye akagundua watu wanamuangalia, akakaa na kujinama kama mtu anajificha.

‘Mmm, naona wasije wakaniona kabla sijapanda ndege,..., hahaha, lini niondoke, maana sitaki kukaa tena hapa nchini, hapa nchini kuna nuksi, nilishashaingia choo cha kike nikatolewa baro,....na sitaki tena kukosea, ni bora niondoke mapema....’akasema

Yule jamaa akafungua pochi yake akawa anahesabu pesa, na docta akamuangalia akijilamba lamba, huku akihesabu zile pesa zikihesabiwa na huyo jamaa, alipoona jamaa katulia, akataka kusema, ongeza kidogo, lakini yule jamaa akasimama na kumkabidhi hizo pesa;.

‘Hizo pesa usilewee, zitumie kujiweka sawa, jiandae vyema, mimi nitakutafutia chuo kizuri tu, nina jamaa yangu yuko huko Marekani, nikitoka hapa nakwenda kuwasikilana naye, nataka uje kuwa dakitari bingwa wa ukweli, uwe tishio unasikia, tishio, natambua wewe hapa kichwani sio haba,lakini kinachokuharibu ni pombe,.....’akaambiwa

‘Weee, mwenyewe utaona, kipaji bado kipo hapa kichwani, tatizo, naishi nchi isiyojua umuhimu wangu, ndio maana nalewa weee, ili kuondoa mawazo, nikimpata dada mmoja, akanipa kampani, basi siku imekwenda, sina shida, sitaki kuoa, sitaki matatizo na mtu, kulewa, kustarehe, ndio fani yangu,...’akasema huku akijidekeza.

‘Basi tutaliona hilo,...jiandae, nataka uende huko, na ukimaliza ukirudi sasa ndio tutakaa tupange dili kali ya pesa, mwenyewe utafurahi, hakikisha unafanya vizuri, sitaki ufike huko uwe mlevi, nataka usome, na hakikisha unarudi hapa nchini, usije kupotelea huko, ni lazima urudi hapa nchini vinginevyo, utatafutwa na kuswekwa jela, mimi huko nina watu wangu...’akasema

‘Oho, usinitishe, kwanza kwanini nibakie huko, ...nitarudi tu bwana, .....’akasema

‘Ndio nakuambia hivyo maana mimi nimewekeza gharama zanguna nataka watu kama nyie tufanye jambo kubwa sana, natumai hutaniangusha....’akaambiwa

‘Ndio maana nakupenda, ....wewe ni kichwa, una pesa na unajua jinsi gani ya kuzitumia, na kuziwekeza, hapa kwangu utakuwa umeziwekeza kweli kweli, mwenyewe utafurahi , nikirudi huko majuu, nitakutafuta, nitakuwa mwingine, nitalewa kizungu, siunajua tena, wenzetu wanakunywa kistaarabu, sio kama sisi ukizipata za dezo unasakamia, ...nakuahidi nitakuwa docta bingwa wa, nini umesema ...ok, nitajua huko huko nikifika.....’akasema

Na kweli jamaa akapata nafasi ya kwenda kusoma nje, siku anaondoka akamshukuru sana jamaa yake huyo aliyemfadhili na kumuahidi kuwa hatamuangusha. Na akafika huko Marekani, na akaanza masomo yake mara moja, na akiwa huko kipaji chake kilidhihiri hadi jamaa wa huko nje wakataka abakie huko huko, lakini aliomba arejee kwanza nchini ili aione familia yake na kukamilisha baadhi ya mipango yake, akawaahidi kuwa baada ya miezi kadhaa atarejea kufanya kazi huko majuu.

Kwahiyo jamaa yetu huyu ambaye sasa ni docta bingwa wa magonjwa zaidi ya moja, aliporudi nchini, akaona kuna umuhimu kwanza wa kuwekeza ndani ya nchi yake, kwahiyo akajiwa na wazo la kuanzisha hospitali yake mwenywe,na humo atawekeze taaluma yake, hakutaka kabisa waza la kuajiriwa hapa nchini,  na kwanini aajiriwe wakati kaahidiwa kufanya kazi huko nchi za nje,...

‘Hapo nchini kwangu nitafungua hospitali kama kitega uchumi changu ambacho kitaniingiza pesa, wakati mimi nipo huko nje ...’akasema kimoyo moyo.

‘Ni lazima nikafanye kazi nchi za nje, maana utaalamu nilio nao, hakuna hospitali itakayoweza kunilipa hapa nchini,....’akasema kwa kujinadi mwenyewe

‘Lakini....’akajikuta akishituka pale alipomkumbuka mfadhili wake, kiujumla hakuwa na mawazo naye baada ya kujiona yeye anahitajika sana, na wanaomuhitaji ni wazungu.

‘Huyu mtu ataniwekea kiwingu...’akasema alipomkumbuka mfadhili wake,

‘Hata hivyo kwani yeye nani bwana, kanisaidia sawa, ni ukimsaidia mtu sio lazima ufanye kama alivyotaka, cha muhimu kama anataka nitamrejeshea gharama zake...’akajipa matumaini

‘Kwanza ni lazima nianzishe hospitali yangu bila hata ya yeye kujua, nikimaliza nitaona kama kuna umuhimu wa kumuona au la...’akazidi kujiweka mbali na huyo mfadhili wake

Itabidi nihakikishe hospitali yangu imesimama, kwanza nilitangaze jina langu, ili hata nikiondoka hospitali yangu iendelee kupata wateja...’akasema na kuahirisha kuondoka kwa haraka kurudi huko alipoahidiwa kazi.

Hiyo ilikuwa moja ya ndoto zake na hakutaka ipotee hivihivi. Nia yake ni kuhakikisha anapata pesa za kutosha ili kwanza kama ni muhimu amlipe jamaa aliyemfadhili pesa zake, hakutaka kuwa naye kabisa, japokuwa alikuwa mafadhili wake. Hakutaka kabisa kuwa mtumwa wa mtu mwingine wakati yeye ni kichwa,...alijua akifanya kazi chini ya mtu mwingine hataifurahia kazi yake, na hilo hakutaka litokee.

Kwa kipaji chake na utaalamu aliyoipata, mwili wa binadamu aliujua vyema kama kiganja cha mkono wake, alijua wapi afanye nini, ili apate nini. Na fani nyingine kubwa aliyoisomea na kupata sifa kubwa ni maswala ya uzazi. Docta huyu alikuwa na kipaji, aliweza kusomea fani nyingi, na zote aliziweza, na hakutsheka na hilo, alikuja na kusomea mambo ya akili na mishipa ya ubongo na mwili, kiasi kwamba aliweza kufanya operesheni ya ubongo bila wasiwasi.

‘Huyu jamaa kichwa...hafai kurudi Afrika.’walisema walimu wake,

Japokuwa alikuwa na kipaji hicho, na taaluma hiyo ilibobea kichwani kwake, lakini tatizo lake kubwa lilikuwa ni ulevi na uzinzi. Na ili aifanye kazi yake vizuri lazima apate kinywaji kikali, na udhaifu wake mwingine mkubwa ni kutokupenda kufanya kazi akiwa amesimamiwa na mtu mwingine. Hakupendi kumwita mtu bosi, hakupenda kabisa kusimamiwa...

Kwahiyo akaona ili kuondokana na hilo tatizo ni vyema awe na hospitali yake binafsi, na kama yule mfadhili wake atakuja na wazo lake la kumtumia au kumuajiri, atamtolea nje, hatakubali kabisa, ....

*********

'Doctor huyu anayetaka kukuoana ni mwanadada mrembo na anaonekana ni tajiri, anasema anamiadi na wewe, naona ni vyema mkaonana naye, mimi naona ni mruhusu tu aingie au unasemaje docta?’ Nesi wake aliongezea na kumuondoa huyo bosi wake kwenye lindi la ndoto za yaliyopita.

Docta aliposikia ni mwanadada, tena mrembo na pia ni tajiri, akajiweka vizuri, ili aendelee kusikia wajihi wa huyo mwanadada kwa undani, hii ilikuwa moja ya starehe zake. Alikumbuka enzi za siku za nyuma jinsi alivyoweza kuwahadaa akina dada, wenye matatizo, alikuna kichwa huku akijuta. Akasema moyoni ile ilikuwa njaa, sasa hana shida tena akitaka mwanadada mrembo hahitaji hadaa, lakini huyo aliyetajwa hapo anaoneka ni tofauti, ameivuta hisia yake na kutamani sasa kumuona;

‘Kwanza kasema ana miadi naye ni-nani, kwani hakumbuki kufanya hivyo!...’hilo lilimpa kangaja la moyo, na kutamani kumuona, kama sio mbinu tu za kutaka atibiwe na yeye.

‘Mimi sijaweka miadi na mdada yoyote, kasema anatokea wapi,...?’ akauliza docta

`Docto huyo mwanadada anafahamika sana, sikuwa na hata na haja ya kumuuliza anatokea wapi, yeye ni yule mrembo anayemiliki kampuni ya warembo ya….’

‘Umesema mwanadada wa kampuni gani...?’ akauliza kwa mshangao, pale huyo nesi alipokatisha akijaribu kukumbuka jina la hiyo kampuni ya huyo mwanadada, na nesi akashituka pale bosi wake aliongea kwa hamaki, akatulia, na docta alipoona huyo nesi katulia akionyesha mshangao, akauliza sasa kwa utaratibu

‘Umesema kampuni gani ya huyo mdada....?’ akauliza akitoa uwoga ulioanza kumuingia akijipa moyo kuwa sio hiyo kampuni anayoifikiria yeye.

‘Kampuni yake, ooh, japokuwa ina jina gumu, lakini hata wewe unaifahamu, ila kasema ukimuona utamfahamu vyema, mlishaahidiana kukutana leo..’akasema

‘Mhh, kwakweli sikumbuki, ...sina miadi na mdada yoyote, unanipa hamasa ya kuonana naye tu, lakini kampuni yake inatwaje...maana asija akawa na huyo...umesema kampuni yake inaitwaje?’akauliza tena, pale akili yake ilipotulia vyema, na alipotajiwa hilo jina la hiyo kampuni, akawa kama kipigwa na kitu kichwani, mwili wote ukaisha nguvu.

Doctor aliinuka haraka kwenye kiti na kuangalia upande wa pili, kama kuna mlango wakupitia, alishasahau kuwa chumba chake hicho kina mlango mmoja tu. Alimwangalia yule nesi aliyekuwa bado kasimama mlangoni,...

‘Una uhakika,.....?’ akauliza kwa wasiwasi

‘Bosi kwani vipi, yeye kasema mlishaongea, na mimi nimemuamini maana mdada kama huyo , mrembo na tajiri hawezi kudanganya...au ...?’ akauliza huyo nesi alipoona jinsi gani huyo bosi wake anavyohangaika.

Docya alikunakuna kichwa chake na kuamuangalia nesi kama ataweza kumpa wazo la kumsaidia, lakini alijua hapo sasa hana jinsi , huyo nesi hawezi kufanya lolote, keshaharibu kila kitu....akilini akaana kukumbuka tukio lilitokea miaka kadhaa nyuma.

NB: Tutaishia hapa kwa leo, unajua tena, bado matatizo ya hapa na pale yananipa shida kichwani, lakini msijali, kisa kitaendelea kwa vyema tu, mungu atatusaidia kwa kudra zake.


WAZO LA LEO: Mtenda ubaya ni rahisi sana kusahau, lakini mtendewa, kusahahu kwake ni kutegemeana na aina ya huo ubaya aliotendewa kwani yeye ana kovu na mwenye kovu usizani kapoa.


Ni mimi: emu-three

No comments :