Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, July 22, 2014

DUNIA YANGU-7


'Doctor kuna mgonjwa mmoja anataka kukuona’ sauti ya nesi ikasema.

 Doctor Chize, aliinua uso uliojaa kilevi, macho yalikuwa mazito kufumbua, hakutamani kufanya kazi yoyote siku hiyo, japokuwa alihitajia pesa, lakini leo alitaka kunywa tu hadi hamu yake iishe, ilikuwa siku ya furaha kwake, alikuwa keshaweka mambo yake sawa, na anataka arudi huko majuu kufanya kazi, na kuishi  huko huko.

‘Mwambie tumeshafunga, ...au hata mwambie nina mgonjwa mwingine, mwambie chochote unachoweza, unaona leo sipo sawa, kwani msaidizi wangu hayupo mpeleke huko kwake, leo sitaki kukutana na mgonjwa yoyote, leo ni siku yangu ya furaha...’akasema na kucheua huku akijibaragua kujiweka sana.

Yule nesi wake akawa anamuangalia kwa macho ya huruma, keshamfahamu bosi wake tabia yake, lakini mara nyingi hata alewe vipi, huwa hakatai kuhudumia mgonjwa, alishangaa leo imekuwaje, hata hivyo alikumbuka jinsi huyo mgonjwa alivyomsisitizia kuwa ni muhimu sana aonane na docta mumiliki wa hiyo dispensary, kwahiyo akawa hana la kufanya zaidi ya kumsihi bosi wake, kuwa huyo aliyekuja ana umuhimu sana.

‘Docta huyu mwanadada aanonekana ni tajiri, na anasema.....’ akaanza kumsihi bosi wake na docta akasema;

‘Nimeshakuambia umwambie kuwa leo sina muda wa kuonana na mgonjwa yoyote hata awe nani, kama ni tajiri, mpeleke kwa msaidizi wangu, huyo ndiye atakuwa bosi wenu, ....mimi nakwenda zangu Ulaya,...kwahiyo huyo atakuwa kila kitu, unanisikia vyema,...’akasema docta kwa sauti ya kufoka, na nesi alitaka kumjibu lakini akaghairi akataka kama kuondoka, lakini akawa kasimama akimuangalia huyo docta.

‘Kwani huyo mgonjwa ni nani mbona unamshupalia sana kuonana na mimi...una miadi gani na yeye ni mchumba wako, ni nani kwako?’ akauliza alipokumbuka jambo, kuwa kweli alihitajia pesa kidogo kumalizia mambo yake kabla hajaondoka, basi huenda hizo pesa atakazo lipwa haitakuwa na haja ya kuingie kwenye mahesabu ya ofisi.

Akakumbuka pia kuwa kuna pesa inahitajika kwa malipo kadha wa kadha pale alipopanga, pia kuna malipo ya kodi za serikali, na pango la hiyo ofisi vyote hivyo vinatakiwa vilipwe kabla yeye hajaondoka, akawa anapiga mahesabu yake kichwani, kujua anahitaji kuwa na shilingi ngapi,halafu akasema;

‘Aaah hizo pesa zitapatikana tu, hata hivyo kama kuna madeni yatashindikana kulipwa, kazi hiyo itafanywa na msaidizi wake, kwahiyo hahitajiki kuumiza kichwa zaidi tu....

‘Hahaha mimi sasa ni mtu wa majuu, hahahaha...’akawaza anacheka akikumbukia enzi zake za msoto, na kumfanya nesi wake amuangalia kwa mashaka, na docta alipoona huyo nesi bado kasimama hapo akasema;

‘Naona huyo mtu ni muhimu sana, hata mimi bosi wako hutaki kunisikiliza au sio?’ akauliza
‘Sio hivyo bosi natumai mwenyewe ungemuona huyo mgonjwa, usingelikataa kumuhudumia,...’akasema
‘Kwani yupoje,....unajua wewe nesi, unanifahamu sana, sijawahi kumkatalia mgonjwa yoyote, lakini leo ni siku muhimu sana kwangu, mimi nimetoka mbali sana, ...nimasota sana, sitaki mchezo kwenye kazi, ukiona nakataa jambo ujue kuna sababu kubwa sana,.....’akasema
‘Nakufahamu sana, bosi wangu, lakini pia nafahamu jinsi gani unavyowajali wagonjwa wako, najua nikimkatalia huyo mtu akaja kukutana na wewe tena baadaye utakuja kunilaumu, ndio maana nakusihi kuwa ni muhimu umuone yeye mwenyewe...’akasema

‘Hahaha, wewe nesi, unanikumbusha mbali sana, hapa nilipo nilikuwa nawaza maisha yangu ya msoto, unajua kusota, basi mimi nilisota, hadi kugeuka omba omba,..tumetoka mbali kwa kweli...’akasema huku anatabasamu na kichwani kumbukumbu hizo za msoto, zikamjia kama njozi fulani;

***********

Alianza kukumbuka pale, alipofukuzwa kazi hospitali ya kubwa hapa nchini kwa kujihusisha na wizi wa madawa na utoaji wa mimba isivyoruhusiwa. Siku alipoitwa ofisini na kupewa barua ya kusimamishwa kazi eti kwa ajili ya uchunguzi ya madai kuwa yeye anajihusisha na wizi wa madawa, na pia kuna kesi ya kujibu polisi, alijua ndio basi tena taaluma yake ya udakitari ndio mwisho wake, hakupewa hata nafasi ya kujitetea, hata hivyo angejitetea vipi wakati ni kweli hayo yote aliyafanya.

Chamuhimu alichokiona ni jinsi ya kuwakwepa polisi, na ili kufanikiwa hilo akawa kajichimbia uswahili ndani ndani, na huko akawa anatibu watu kisirisiri, hata hivyo dawa alizokuwa nazo zikamuishia na matuzimi yake, kodi ya nyumba vikawa vikubwa kuliko pato analilipata, akajikuta hana kitu kabisa.

Siku moja aliamuka na kujikuta hana hata senti moja, siku hiyo hataisahau katika maisha yake.

‘Hawa watu wamenitime kweli, maana wamenifukuza kipindi ambacho sikuwa na pesa kabisa...’akasema akijalaumu

‘Lakini haya yote ni sababu ya yule mrembo...ole wake siku nikija kukutana naye, nitahakikisha nakwenda polisi kwasababu nyingine...’akasema

Jamaa huyu kilichomuhaibu zaidi yeye ni mtu wa matumizi, japokuwa alikuwa akipata pesa nyingi, kutokana na biashara yake hiyo haramu ya kuiba madawa, na kwenda kuyauza kwenye maduka ya mitaani.

Alichokuwa akifanya ni kuwa, yeye kwa vile alikuwa ni mmoja wa viongozi hapo hospitalini, alikuwa na mamlaka ya kuagiza kiasi kikubwa cha dawa, na kudai kuwa zinapelekwa mahali kwingine, yeye mwenyeweanaingia bohari ya madawa, anaongea na mtunza store, anapewa kiasi anachohitajia, anajua jinsi gani ya kuandika.

Yeye hakuishia hapo, kwa vile alikuwa ni docta wa akina mama na upasuaji, basi alianza tabia ya kuongea na wagonjwa waliokuwa na matatizo ya kutaka kutoa mimba, akawa anawahudumia nje ya hiyo hospitali, na akajulikana kwa kazi hiyo.

Alitarajia akiwa mitaani atafungua dispensary yake aendeleze hiyo kazi, lakini aliogopa polisi, kwani alikuwa akitafutwa kwa kosa hilo hilo, na akashindwa aifanyie wapi hiyo kazi, na kila siku akawa anasikia kuwa anatafutwa na polisi, na hapo akashindwa kabisa kutoka.

Alikaa siku mbili hajui hata afanye nini, na mwishowe uzalendo ukamshinda, akawa anapiga mguu kwenda kwa marafiki zake kwa siri, kuomba msaada, kwani hali ilishaanza kumuendea vibaya, hakuwa mtu wa kubakia nyumbani kabla alizoea kubadili bar leo hii keshi ile, na matumizi yake yalikuwa sio haba.

Siku zikaenda na maisha yakazidi kuwa magumu, akaamua arudi kule hospitalini ajaribu kuonana na marafiki zake, au kama anaweza kuongea na yule mtunza store, ili awe kuchukua dawa, akiuza pesa watakuja kugawana naye, akajipange vyema jisni gani ya kumshawishi. Siku hiyo alitaka afanye juu chini ili biashara yake ya dawa, iweze kuanza tena;

‘Ni lazima niongee na mtunza store, mimi nafahamu siri zote za pale hospitalini, na akijafanya kunikatalia nitamwambia nitamchomea na yeye, maana tulikuwa tunashirikiana naye, nilimtetea kuwa yeye hahusiki kwa lolote, sasa ni zamu yake kunilinda...’akasema huku akitembea kuelekea huko hospitalini.

Akiwa njiani kuelekea huko, mara akamuona jamaa akitokea dukani, jamaa huyo alikuwa kabeba mfuko, kuonyesha ametoka kununua kitu, na alikuwa akieleka kwenye gari lake, alihisi kama anamfahamu, akaona ajaribu bahati yake, alitaka apate angalau pesa kidogo ya nauli maana kutembea nako shughuli, akamsogelea, na yule jamaa kwa muda huo alikuwa akifungua mlango wa gari lake.

‘Ndugu kama nakufahamu vile.....’akasema huku akinyosha mkono kusalimiana na hauyo jamaa, na yule jamaa akasimama akimuangalia usoni kwa mashaka, kwani dunia ya sasa imeharibika, unaweza kusalimiana na mtu kumbe ni mwisi wa mazingaumbwe, na yule mtu akaonekana kumtambua, na haraka yule mtu akasema;

‘Wewe si docta Chize, mmh, school mate huyo, upo docta....’akasema huyo jamaa, akizidi kuonyesha mshangao usoni, ni kweli huyo alikuwa mmoja ya watu aliosoma nao, na anakumbuka walikuwa wakitaniana sana wakati wapo shuleni, wao wa masomo ya sayansi walikuwa wakiwatania wa masomo mengine yasiyokuwa ya sayansi, kuwa masomo yao laini-laini.

Jamaa huyo waliachana kipindi yeye anakwenda kuchukua udakitari, na hawakuweza kuwasiliana tena, na kwa mara ya mwisho walionana wakati jamaa huyo alipofika hospitali ya Muhimbili akitaka kujaziwa fomu yake ya taarifa fulani za kiafya, kwa ajili ya kufanikisha mambo yake, na walipokutana walitambulishana na hawakuna na muda wa kuongea kila mtu alikuwa na haraka zake.

Leo wanakutaka tena, lakini kwa hali ambayo ilimtia mashaka huyo mwenzake, hakutegemea kabisa kumkuta huyo dakitari katika hali hiyo, kachoka ile mbaya, mijasho inamtoka kwa kutembea juani,....

‘Nakukumbuka kumbuka, hebu nikumbushe kidogo, tulikuwa wote wapi vile....’akasema Chize, ni kweli kutokana na nakama za maisha na kazi yake ya kukutana na watu wengi, akili yake ilishaanza kumsahau huyo jamaaa, na jamaa akasema;

‘Wewe si ndio dakitari Chize, tuliwahi kusoma wote A-Level,japokuwa wewe ulikuwa mchepua wa sayanasi, lakini vipi kulikoni, mbona upo mitaani huku unaonyesha kuchoka sana, vipi umegomewa na wagonjwa nini...maana pale hospitalini kwenu hapaishi migomo?’ akatania huyo jamaa

‘Kabla hatujaendelea na hayo maongezi, naomba unipoze koo, hapa nilipo nina kiu, nina njaa, huwezi amini....’akasema docta.

‘Siamini, kwanini lakini, ...?’ akaulizwa huyo jamaa kwa mshangao

‘Kwanza fanya kama nilivyokuambia, naona wewe ni matawi ya juu, mmh, nona una gari, umenawiri, mmh, nyie watu wa masomo laini laini, mnakula sana nchi...’akasema

‘Acha utani wako, hakuna masomo laini-laini, hayo ni mambo ya shule, ukiwa mitaani ni akili kichwani mwako...’akasema

‘Ni kweli, kama hivyo, naona umejilengesha mwenyewe, nimeshakukumbuka vyema sasa, ulikuwa mtani wangu sana wewe...nakuona sasa upo softi- softi, sisi tunaumiza kichwa nyie mnakula pesa ya nchi kilaini...sasa nimekupata, ni lazima unisaidie, nisije kufa kwa njaa, je nikifa mimi docta mtatibiwa na nani...’akasema huku akijua hapo keshapata chochote.

‘Sawa docta japokuwa nina haraka,lakini...mmmhh,  pia nilikuwa nakuhitaji sana, sasa mhh naona ni fursa pekee ya kukutana na wewe, nilikuwa natafuta mtu kama wewe....’akasema.

‘Sawa, kama kuna demu wako anataka kucholopoa.... wewe niwezeshe tu, kazi rahisi tu, ni pesa yako tu..na mhali pa kujihifadhi maana hawa watu wa magwanda njaa imewazidi, hawanipi nafuu....hawajui siku hizi kila mtu anafadii mezani kwake....’akasema na jamaa yake akacheka, akijua huenda docta anamtania, na akasema;

‘Docta bwana, huogopi kuharibu fani yako, ...haya twende pale hotelini, mimi nitakununulia chakula nikuache ule maana nina mtu ananisubiria, wewe ....’akasema na huyo jamaa akamkatiza na kusema;

‘Hapana,..huo ujanja wa mjini si utaki, nataka nakula na wewe upo karibu, nimekuambia hawa watu wa magwanda na njaa zao wananimulika kila mhali lakini ukiwepo karibu hawatanishuku....hata hivyo nina shida nyingine muhimu sana nataka unitatulie, maana maisha sio mchezo, huwezi amini, chumba nimeshafukuzwa, unaweza kuamini hilo docta mzima kama mimi nazalilishwa, ....’akasema na jamaa yule moyoni akasema;

‘Sasa nimeshampata huyu mtu kirahisi kabisa...kama hali yake imefikia hivyo, basi naona ni bora nianzane naye na huyo mwingine nitakutana naye baadaye...hapa nimeshapata mtu mwingine ....’ Akawa anasema kimoyo moyo huyo jamaa na sasa akituma ujumbe wa maneno kwa mtu ambaye alitarajia kukutana naye, kuwa kapatwa na dharura kwahiyo wakutane kesho

Kweli wakaondoka hapo na hadi kwenye hoteli iliyokuwepo karibu, wakapata chakula, na jamaa anavyopenda kunywa, akaagiziwa kinywaji akanywa

‘Unajua rafiki yangu sijawahi kula hivi kwa miezi kadhaa sasa...’akasema kilevi levi

‘Unafunga au?’ akaulizwa

‘Hahaha, wewe vipi bwana, mimi nifunge!,... hahaha, na wala sijui kufunga ni nini, kwanini nigomee kula bwana, kama nina pesa, natumia, ....,,mimi namshukuru mungu kuwa sio bahili wa matumizi, nikiwa nazo nakula na kusaza, na kinywaji ndio maji yangu...’akasema

‘Ndio maana unakuwa hivyo, maana hujui kupangilia matumizi yako, hata uwe na pesa vipi kama huna mpangilio mnzuri wa kipato chako ni lazima utaishiwa, unakumbuka ule usemi pesa bila daftari hupotea bila habari...’akasema huyo jamaa

‘Achana na uswahili bwana, maisha yenyewe yapo wapi,..tumia ukiwa, na wasaa, tumia ukiwa nazo, maana utakufa wenzako watakuja kutumia bila kusaza, sasa utapata faida gani, mimi ni docta nimeona watu wakifa, wengine hata hawastahili kufa, wanaacha utajiri wao nyuma...’akasema

‘Kufa kupo, lakini sio sharti la kutumia ovyo, haya niambie ulikuwa na shida gani zaidi maana nina maongezi mengine...’akasema

‘Ndugu yangu, niseme huu mguu ni wako japokuwa sikutarajia kukutana na wewe hapo barabarani...hapa nilipo sina pesa, unajua kuishiwa, basi mimi ni mfano wa hao watu walioshiwa, na sio mfano, ila ni kweli nimeishiwa, yaani hapa nimebakia mimi na mwili wangu tu,....’akasema akijiangalia.

‘Kwa vipi bwana docta, mbona nasikia unahudumia hata watu mitaani wewe wanakufahamu sana kuwa ni docta bingwa, hapokuwa haujafikia kuitwa hivyo...au sio wewe wanayekutaja docta Chizi, kwasababu ya kulewa, ukilewa ndio unatibu vyema...’akasema

‘Unajua watu wakitaka kukutukana hawakuchagulii tusi, waache waniite hivyo wapendavyo, lakini mimi bado Docta Chize.., ilimradi naingiza mapesa..ila sasa wameniharibia, sasa wamenipata maana nipo kwenye mawe huwezi amini...’akasema

‘Kwanini?’ akaulizwa.

‘Hawa wapuuzi walinisimamisha huko kazini nilipokuwa nimeajiriwa, eti wanifanyie uchunguzi, na miezi mingi imeshapita, hawajaniita tena, sio ndio kufukuzwa kazi huko...’akasema

‘Kwanini usiende kujitetea, wewe ni docta mzuri watakusamehe...’akasema

‘Hivi kweli kuna Uzuri unaweza kukaa kwenye ubaya, hilo halipo, hata uwe mnzuri,lakini kama una doa la ubaya, wewe sio mnzuri tena....ni ujanja tu, huwezi kusema kitu kizuri kimefanya mabaya, hilo halipo ni propaganda na kutokuelimika, mimi najijua mwenyewe...’akasema

‘Kwanini?’ akaulizwa

‘Kwanini, kwanini....we hujui, nikuambie, mimi nimesota sijwahi kusota kihivi, maana hawa watu walinishitukizia, kabla sijajipiga mzinga wa maana, kuna mzigo uliingia karibu nilishaupangia mahesabu yake, wakaniwahi kabla sijafanya hivyo, unajua huku uraiani mzinga wa kikweli ni jinsi gani ya kupata dili, ya kuingiza pesa, ....’akasema

‘Docta acha utani, wewe sio mtu wa kufanya hayo, ina maana ulikuwa unafanya dili za kuingiza pesa kinyume na sheria, unakwiba..?’akaulizwa.

‘Hahaha, ndio maana nikakuambia kuwa huwezi kusema mimi ni mnzuri, uzuri wangu una doa la ubaya, labda utafute jina jingine huo uzuri unaoutaja wewe, hata hivyo yote ni maisha, unafikiri ningelifanya nini mimi kwa hali kama hiyo...’akasema

‘Kwani ilikuwaje?’ akalizwa

‘Unajua ukiwa kwenye nafasi yako ya kazi kuna mambo mengine inabidi yafanyike tu vinginevyo hutaweza kujijenga, hutaweza kustarehe, na starehe ni gharama, sijui ni nani aliwatonywa hawa watu, nilitaka nifanye vitu vyangu halafu nipotee kwa muda,...wakaniwahi nikiwa sijajipanga vyema,...ila safarini nyingine, kama watanirudisha, ni lazima nijipange, nitafanya kitu wenyewe hawataamini, na hapo nitapotea kabisa...’akasema

‘Sasa kwanini walikufukuza, maana mimi hapo sijakuelewa, hujaelezea kilichosababisha kwa wewe kufukuzwa?’ akaulizwa

‘Sijafukuzwa bwana, wamenisimisha eti kwa kisa la udokozi...wao wanaita hivyo, eti nimekwiba madawa,....unajua kuna watu wanapesa zao, wanahitaji dawa, na dawa zipo ningelifanyeje, nikaona dawa ni kutoa dawa, nipate pesa....’akasema na huyu jamaa akavutiwa na sana na kauli hiyo.

‘Yah, hebu niambie ulifanyaje maana hapo ni muhimu sana, kutumia akili kwa ajili ya kupata pesa hilo ni jambo kwangu muhimu sana, hebu nifafanulie hapo kidogo...’akasema

‘Hao watu wanasema hawana pesa, sio kweli kuwa hawana pesa, ni kwamba hawajui kuzitafuta hizo pesa...hebu niambie dawa zipo nyingi tu...halafu hospitali kama hiyo ikose pesa, na wakati wateja wake ni wagonjwa,na wagonjwa ni wengi sana, nikaona hawa watu wanahitajia fundisho dogo tu, nikawaonyesha japo kwa siri, jinsi gani ya kutafuta pesa....’akasema

‘Ukafanyeje...?’ akaulizwa

‘Mbona unaniuliza kama polisi, usije ukawa shushu...’akasema

‘Hahaha, mimi na mambo hayo ni kama maji na mafuta, usiwe na wasiwasi kabisa,mimi ni rafiki yako nimesoma na wewe siwezi kukutosa, wewe niambie maana nahisi unaweza ukanifaa sana...’akasema

‘Ni hivi, eti wao wanaweka madawa mpaka yanaota ukungu, wagonjwa wakifika, wanaambiwa hakuna dawa, hizo dwa wanamuwekea nani, nikaona hawa watu hawanajijui,halafu wakanichagua mmoja wa viongozi wa bohari ya madawa, nikacheka kimoyomoyo, nikisema kichaa kapewa rungu,...nikasema basi kama hakuna dawa mimi nitakuwa nazo, ...nikawa nazibeba kilaini,  na wagonjwa wakawa wanazipatia kwingine, mitaani.....’akasema.

‘Na hilo la kucholopoa vipi,...?’ akauliza huyu jamaa akiona anapoteza muda, na kile alichokitaka keshakifahamu.

‘Hahaha ina maana huyajui hayo,...ipo siku utanitafuta, ...Mimi ni docta bwana, siunajua nimesomea nini, mambo ya kina mama kwangu ni rahisi sana, kuna akina mama hawataki kuzaa, na ...’akasita na kuanza kuongea kwa sauti ndogo

‘Unasikia ngoja nisije kukamatwa hapa, tuongee pole pole, unaye msichana ana tatizo hilo....?’akasema akimsogelea huyo jamaa huku akiangalia huku na kule, na jamaa akawa anashangaa kwanini docta anaogopa kuongea kwa sauti.

‘Hapana kwasasa sina...’akasema

‘Unajua hii fani yetu wakati mwingine mshahara hautoshi,mimi kama docta nahitajia kula vizuri, kulala vizuri, kunywa, kustarehe, ili kichwa kitulie, sasa vyote hivyo ni gharama, na muda mwingi unakuwa kazini,unapambana na matatizo ya watu, kichwa hakiwezi kuwa sawa, kama hutapata mahitajio hayo muhimu...’akasema

‘Nakuelewa sana...’akasema huyo jamaa
‘Watu hawajui, kazi inayotumia kichwa inaumiza sana,..kuliko ya mitulinga, ubongo unachoka haraka sana, na ili uufanye usiwe tatizo, basi utimiziwe mahitajio muhimu, kama hayo niliyokutajia....’akasema

‘Sasa hawa jamaa wanaoitwa watawala, siwapendi hawa jamaa, meneja utawala, meneja masihali, hamna kitu hapo, kazi yao kuongea tu, wengine mnaumiza kichwa,...nikaona oke, kama ndio hivyo, na mimi nimjanja zaidi yao nikawa napata vikazi kazi vya ziada, baada ya watu kunitonya, wakaniambia wewe una utajiri, lakini hujijui tu...’akasema

‘Ehe...kweli wewe una kipaji kizuri, watu wanakusifia...’akasema huyo jamaa

‘Ndio hapo nikaamuka, nikajua kumbe na uzuri wangu ninaweza pia kufanya ubaya na ukakubalika, na nikajifunza jambo, usione watu wanapiga propaganda za jambo nzuri kwa watu wabaya, ili tu lile jambo lionekane baya,...kweli mimi ni docta mnzuri siwezi kukataa, lakini nina tamaa ya maisha mazuri, ndio maana nikasoma sana, hilo siwezi kukuficha, kila mtu anahitajia hivyo, sasa kwanini mimi nijidanganye, kamwe sikuweza kujidanganya...’akasema

‘Una maana gani?’ akaulizwa

‘Kuna hawa kina mama, eeh, nisisema akila mama, niseme hawa watu kama nyie wenye pesa za bure, mumewapa watoto wa watu mimba,...maana wanaume jamani mna dhambi sana nyie, mmmh, siwezei kujikataa, kuwa na mimi nimo, ila ninachotaka kusema ni kuwa, watu kama nyie mnakuja kwangu kuomba niwasawazishie, siwezi kukataa, ilimradi tu uwe na cash, ....sasa nikuambie kitu, kama unaye binti, msichana mwanamama, kapata mimba isiyotegemewa, niletee, tutaelewana tu,....’akasema kwa sauti ndogo ndogo.

‘Kweli eeh, docta bwana, ina maana umefikia hapo, sasa...mmh, kwanini usifungue hospitali yako...?’ akaulizwa

‘Sikiliza bwana, hayo ya hospitali yangu kwa sasa sio dili,nielewe hapo, kuna tatizo, lakini kama nilivyokuambia wewe kama unaye usijali,mlete,....mimi naitoa kirahisi tu, awe mwanafunzi au msichana wako atadunda, kama vile hajawahi kupata mimba....’akatabasamu huku akitikisha kichwa kwa kujiamini.

‘Mhh, hiyo sasa kali...lakini nakuamini sana docta...’akasema.

‘Unajua mimi mwanzoni nilikuwa nawasaidia watu, unajua hilo ni tatizo, likikupata utajua ugumu wake ulivyo, mimi nikawa natumia ujuzi wangu kuwasaidia watu kama hao,... kuna watu wakanichomea mbovu....’akasema

‘Oh, wakakukushitaki au...?’ akaulizwa
‘Mhh, kitu kama hicho,usisikie kuna watu wana roho mbaya....lakini bado naifanya kwa siri, wewe kama unaye mwanamke anataka kutoa au kusafishwa, wewe nitakulipisha kidogo tu sio sana kama wengine..wewe ni rafiki yangu bwana, unaona jinsi ulivyonifadhili leo....’akasema akiongea kwa sauti ndogo.

‘Hapana mimi sipo huko kabisa...hebu sasa nikuulize kwanini uogope kufungua hospitali yako mwenyewe, ukajisajili rasimi, kwani hiyo ni fani yako na watu wenyewe wanahitajia kufanyiwa hivyo...?’ akaulizwa

 ‘Kuna watu wabaya wewe wana roho zao mbaya,...usiwaone wanapita mitaani wamependeza, wameniharibia, lakini, hata hivyo nimeshamfahamu mbaya wangu ni nani, huyo jamaa nina usongo naye, ipo siku atakuja kwenye anga zangu, nitamfundisha kulewa, hahahaha...’akasema na kucheka na huyo mwenzake akaangalia saa yake, na docta alipoona hivyo akasema;

‘Nashukuru sana school mate wangu, sasa cha muhimu ni wewe kunitafutia usafiri, nikalale nyumbani maana nimechoka...nimetembea leo, nisingelikuona leo sijui ingelikuwaje..., unajua kuchoka, hapa miguu inauma, kiatu chote kimakatika, yaani ni aibu kwa docta kama mimi kuvaa hivi, lakini ipo siku...’akasema kilevi huku akijikagua miguuni.

‘Usijali ndugu yangu ipo kweli, haina haja ya mimi kukutafutia usafiri,  mimi mwenyewe nitakupeleka nyumbani kwako, nataka nihakikishe umefika nyumbani, maana ulivyolewa, unaweza ukapatwa na ajali,...lakini sasa umesema umefukuzwa na baba mwenye nyumba au sio, sasa unaishi wapi....?’akaulizwa

‘Hayo ya kuishi wapi niachie mwenyewe, ...unasema nimelewa, hahaha, mimi nilewe,...hizo chupa nne tu nielewe, unanitania,...wewe kama unataka kujilengesha tena, nichukue kwenye gari lako, nitakuambia wapi pa kunishusha, ukinichunguza sana, hutaniweza...unasikia, wewe nitakuambia wapi unipeleke, tukimaliza hapa, au unataka kuniagizia kinywaji kingine, maana mimi baado kabisa...?’ akauliza huku akijilambalamba

‘Umeshalewa bwana docta, ila kuna kitu muhimu nataka kuongea na wewe,ndio maana sitaki uelewe, nataka unisikilize kwa makini na unielewe, lakini kama upo tayari kuongea, na sio swala la mambo yako, ni dili nyeti kidogo,...’akaambiwa

‘Wewe sema usiogope....’akasema docta

‘Nataka tuongee ukiwa makini, lakini hapa nakuona umeshalewa, na umesema umechoka na hili ninalotaka kukuambia ni muhimu...kutokana na wewe na udocta wako, je upo tayari?’akaulizwa, na docta akamuangalia huyu mtu kwa macho ya udadisi, akilini akajiulize asije akawa anaongea na shushu,akataka kusimama kuondoka, lakini akasita, akasema;

‘Wewee, ... mimi ni mtoto wa mjini bwana, huwezi kunipata kirahisi, ngoja niondoke zangu, kama umetumwa kunichunguza, hapa hupati kitu....’akasema akisimama kuondoka huku akipepesuka, na yule jamaa akamshika, na kusema;

‘Sikiliza Docta, mimi nimeshakujua vilivyo, kwahiyo ni vyema ukanisikiliza, tukaelewana, vinginevyo ....’akaambiwa na docta akabakia ameduwaa.

NB: Jamaa anataka waongee nini?

WAZO LA LEO: Uwongo na uzushi ni tabia chafu sana, siku hizi tabia hii imekuwa ni fani ya watu, watu hawaogopi kuzisha uwongo, au kuutengeneza uwongo, ilimradi tu watu fulani waonekane wabaya, na wao waonekane ni wazuri, hata kama ni kuua, hata kama mzushiwa atafungwa, au kufukuzwa kazi, hawajali familia za wenzao, ilimradi wanakipata wanachokitaka.

 Jamani, uzushi, uwongo ni jamii ya fitina, na fitina  ni mbaya sana, mfitinishaji ni mbaya kuliko hata mchawi. Tuache hii tabia kwani mfitinishaji kalaaniwa, hadi hapo atakapojirekebisha na kutubu dhambi zake.


Ni mimi: emu-three

No comments :