Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, July 16, 2014

DUNIA YANGU-5  Ni ndani ya ofisi moja,

  Msichana mrembo alionekana akijipodoa, akiwa kakaa kwenye kiti ambacho kilionekana kidogo kutokana na makalio yake, msichana huyu akiwa anaimba wimbo, kwa kutoa sauti bila maneno, aliendelea kujipodoa, na mara mlango ukafungulia..

Yule msichana aliacha ile kazi haraka na kusimama, na huku mkono mmoja ukifanya kazi ya kuficha vile podozi kwenye makabrasha yalikuwepo, na kuvisukuma ndani ya kabati,halafu akalifichua tabasamu la pekee ambalo alishajiandaa nalo, na alijua akilitoa tu bosi wake huyo hata kama alikuwa na hasira atalainika tu.

Kutokana na ujuzi wake, uzuri wake, na ujanja wa kujua kuishi na watu hawa, msichana huyu hakupata taabu kuajiriwa kwenye kampuni hii ya Computer network limited, kampuni kubwa iliyofunguliwa na mtaalamu kutoka Marekani ikiwa inaanza kuvuta wateja kidogo kidogo, ilikuwa haijawaweza kushika hatamu kama alivyotajia muwekezaji huyu.

 Binti huyu aliinuka pale alipokuwa amekaa, na kwa haraka akavuta sketi yake chini ilikuwa imembana na kuchora umbile lake bara bara, ilibidi aivute chini kwani ilishapanda sana na kuacha sehemu kubwa ya mapaja yake wazi, alifanya hivyo akihakikisha bosi wake anaona,na alipomaliza kuivuta chini akatoka kwenye kile kiti chake na kutembea kumpokea bosi wake mkoba uliokuwa amebeba, ilikuwa ni mkoba wa komputa ndogo.

‘Karibu bosi....’akasema na bosi alimkabidhi yule binti ule mkoba, na yule binti akatangulia mbele kueleka ndani ya ofisi ya huyo bosi wake bwana Ngekewa. Na huo mwendo aliokuwa akitembea ulikuwa wa aina yake, wa makusudi kwa ajili ya bosi wake, na mwenyewe alijua huku nyuma bosi wake atakuwa anamuangilia jinsi makalio yake yalivyokuwa yakitikisika.

‘Ukitaka kuishi na hawa watu ni lazima uwafanyie hivyo, lakini akilini kwako unajua ni nini unachokifanya,...’alikuwa akisema hivyo huyo binti siku moja alipoulizwa na rafiki yake aliyekuja kumtembelea hapo ofisini kwake.

‘Mhh, lakini wewe umezidi, huyo si mume wa mtu unayemfanyia hivyo’akaambiwa

‘Bosi akiwa ofisini si mume wa mtu,....mimi ndiye mtu wake wa karibu, natakiwa kumliwaza, natakiwa aifanye kazi yake akiwa na raha..mkewe na huko huko kwake...’akasema

‘Lakini mbona sisi tunafanya kazi na bosi kama wako, lakini hatufanyi hivyo...’akasema huyo rafiki yake

‘Kazi zetu hini zinahitaji ujanja, akili na maarifa, kama unahitaji kupata mkopo, au kuna kitu unakifukuzia, hufanyi tu bila malengo, hata hivyo, mimi kama katibu muhutasi wake, nahitajika kuwajibika kwa bosi wangu, natakiwa kumliwaza bosi wangu ajisikie furaha...lakini zaidi huyu ndiye anayekuweka mjini, halafu nikifanya hivi, hata wateja wenyewe, wanavutika kuja hapa kwetu mara kwa mara, kwani bila wao hakuna pesa itakayoingia , na zaidi mwisho wa siku siwezi kutoka mkono mtupu, wewe nini bwana, shauri lako..’akasema.

‘Huoni huko ni kujizalilisha..?’ akaulizwa na mwenzake

‘Ninachokifanya hapa ofisini kinaishia hapa hapa, nikitoka hapa, sio yule binti uliyemuona, najigeuza kama kinyonga, huko mitaani, wananifahamu tofauti, katika maisha haya ya kibongo, ni lazima uwe na akili ya ziada...’akasema

‘Mimi kazi hiyo siwezi...’akasema mwenzake

‘Sawa, lakini usinionee gere nikishuka kwenye gari la  bei mbaya, na kuingia kwenye nyumba ya kisasa, ujue yote hayo yametokana na hayo matendo unayosema huyawezi...’akasema

Bwana Ngekewa alimuangalia yule msichana anavyotembea kimikogo, akiwa amemtangulia mbele yake na tamaa za kimwili zikawa zinamtuma vibaya, lakini kila mara kuna hali ya kushituka, hasa alipokuwa akimkumbuka mkewe. Hakutaka kabisa kuisaliti ndoa yake, lakini alishangaa jinsi gani huyu binti alivyoweza kuiteka nafsi yake, na kila akimuona, alijihisi akivunja amri ya ndoa ya kutokutamani wanawake wengine zaidi ya mkeo wako.

Baadaye waliingia kwenye ofisi ya huyo bosi, na bosi alikuwa bado anamuangalia yule binti, na yule binti, akawa anahangaika kuweka meza ya huyo bosi vyema, na akasimama pembeni, kimadaha, kama yale madaha ya warembo wa mitindo kumpisha bosi wake apite, na alitaka apite karibu yake, ili asikie ile harufu ya manukato aliyokuwa kayapaka kwa ajili hiyo.

Yule bosi akapita, na kujifanya sasa hajali tena, yupo kikazi zaidi, akamshukuru yule binti na kukikalia kiti chake cha enzi akasema;

`Ahsante mrembo, nitakuhitaji baadaye, ngoja niweke mambo yangu sawa.’ Akasema sasa kwa kujitutumua kama bosi.

Yule binti, alipohakikisha bosi wake amekaa, akatoa lile tabasamu tena, na kusema;

‘Sawa bosi nipo kwa ajili yako.....’akataka kutoka, lakini bosi alikumbuka, jambo akasema;

‘Oh, samahani naomba unipatie hilo faili la wateja, ....’akasema na yule binti kwa haraka lakini kwa mikogo, akafungua kabati kubwa la viyoo, na kutoa faili hilo aliloagizwa na bosi wake, na kuja nalo mezani, na bosi wake, akalipokea, akawa anasome majina, akasema;

‘Huyu mteja wetu mkubwa alishafika , alisema jana atafika...?’ akauliza na yule binti akajifanya kama hajui ni mteja gani akasogea kule alipokuwepo bosi wake, akainama, kuangalia lile jina, na alihakikisha sehemu ya matiti yake inagusa mabega ya bosi wake, na sehemu kubwa ya juu inakuwa wazi.

‘Huyu mteja, alikuja na aliondoka akasema leo atafika tena, nimeweka kwenye mpangilio wako wa kazi za leo, atafika saa nne, labda kama kuna mpangilio mwingine zaidi...’akasema huyo binti

Bosi yule alipoona ile hali, sasa akashindwa kujizuia, akanyosha mkono wake na kushika bega la yule, na yule binti akajilegeza kidogo, na yule bosi alipotaka kuendelea kusmhika zaidi,  mara akahisi sura ya mkewe ikimuangalia akilini, hapo hapo akaurudisha ule mkono wake kwa haraka, ilikuwa kama vile mtu aliyeshika kaa la moto anavyoshituka.

Binti yule akatabasamu na moyoni akasema;

‘Bado hujakaa sawa, usijifanye hutaki, huku unataka, dawa yako inachemka...’akasema kimoyo moyo, huku akiondoka pale pembeni ya bosi wake akielekea mlangoni kwa mwendo ule ule wa  kinamna na alijua kuwa bosi wake huyo atakuwa akimuangalia na alipofika  mlangoni akagaeuka na kwa macho ya kimahaba na tabasamu nzito, alimwangalia bosi wake huku anafunga mlango.

Bosi akajikuta akisema;

`Wewe Tausi wewe,....unahatari, hebu punguza hizo mbwe mbwe zako, usije ukanitia majaribuni....’akasema

‘Kwanini bosi, mbona hii kawaida tu, au hupendi ninavyofanya...?’ akauliza Tausi

‘Baadaye tutaongea..’ alisema huyo bosi, huku akijifanya kufanya kazi kwenye computa yake, lakini akilini mwake alikuwa akipambana na mawazo mengi, na mojawapo ni jinsi gani angalipata nafasi ya kuwa karibu na huyo binti japo kwa masaa kadhaa, wakistarehe, alitamani sana iwe hivyo, japokuwa akili nyingine ikawa ikimsuta kuwa hilo ni kosa kubwa katika ndoa yake, na hapo akakumbuka jinsi alivyomuoa mkewe;

Bosi huyu aliporejea toka masomoni, cha kwanza alichofanya ni kwenda kuoa, huko kwao kijijini, na mkewe alikuwa mcha mungu wa kweli, na kwa tabia hiyo ya mkewe, aliogopa sana kumsaliti, japokuwa moyoni, na akilini mwake, alitamani mkewe naye awe na madoido kama hayo, lakini kwa jinsi amjuavyo mkewe hawezi hata siku moja akamfanyia hivyo, mkewe ana aibu sana

‘Hata hivyo mke wangu nampenda, japokuwa hanionyeshi mbwembwe kama za huyu binti, ...hivi itakuwaje, nikipata nafasi ya kuwa na huyu binti, mmh, sijui,...hayo yapitlie mbali, maana mke wangu akifahamu anaweza kujiua, hapana, haya yapitilie mbali...’akawa anasema kimoyo moyo.

‘Mhh, kazi na dawa, ukiwa na warembo kama hawa inasaidia maana hata kama umechoka, unajikuta unasahau uchomvu, wanasaidia kusahau matatizo mengine, japokuwa kiukweli, mmhh, sijui, itakuwaje, ...ooh, hata hivyo,...hapana shetani ashindwe...’akajikuta akijisemea mwenyewe baadaye akazama kwenye mambo yake ya kikazi na kuisahau ile hali.

**********

Ngekewa akiwa ofisini kwake, alijikuta sasa akiwaza mambo ya kikazi zaidi, na akilini mwake alikuwa akijisifia kwa jinsi alivyoweza kufikia hatua hiyo kibiashara japokuwa hajafanikiwa kiasi akitakacho, japokuwa ndoto yake ilikuwa imeshatimia, ndoto ya kuweza kuijua vyema komputa na mitandao yake, ndoto ya kumiliki kampuni yake, na kuweza kufanya vile apendavyo...na elimu hiyo alikuwa kaipata Marekani, hii ilimpa sifa sana

Tangu akiwa shuleni, ndoto yake kubwa ni kuwa mtaalamu wa komputa na hasa upande wa mitandao, japokuwa katika kusoma kwake, aliweza kujifunza kila kitu, ufundi, mitandao, na kila kinachostahili kwenye komputa.

‘Cha muhimu sasa ni wateja....’akasema kimoyomoyo

‘Ni lazima nifanye zaidi ya hayo, ni lazima nitoke kule nilipotoka niwe matawi ya juu, kwanini nisifanikiwe, kwani hao waliofanikiwa walifanya nini cha ziada, elimu ninayo, na sasa kampuni imeshajitangaza, na ni lazima niweze kutimiza ndoto yangu ya kuweza kuwasaidia wazazi wangu,...’akasema

Elimu yake hiyo ya huko Marekani, ilikuwa ndio chaguo lake, na hakubahatisha kwani alihitimu mafunzo yake ya komputa, kwa daraja la hali ya juu, fani ambayo ilimkaa kichwani na alikuwa akiipenda sana tangu alipokuwa shuleni, japokuwa alipomaliza kidato cha sita, hakuweza kuendelea zaidi, kutokana na nakama za maisha, akakimbilia kutafuta ajira, lakini ikawa ni mitihani, na aliyekuja kumuokoa,akawa huyo mfadhili wake.

‘Mfadhili, ....’akakuna kichwa alipoanza kumuwaza huyo mfadhili wake, lakini alihisi moyo wake ukmuenda mbio,mashaka,na wasiwasi ukawa unamjia, na hali hii ilimkumbusha siku za nyuma alipokuwa kidato cha kwanza,....

‘Huyu mtu kanifadhili na....lakini kwanini anakuwa mwiba kwangu, kwanini....’akawa anajiuliza

Ni kweli huyu mfadhili alimsaidia kwa kiasi kikubwa sana, na lengo lake ilikuwa ajitahidi ajae kuzilipa hizo fadhila na kuachana naye, hakutaka kuwa naye karibu, moyoni hakupenda kabisa, japokuwa ndio lengo la huyo mfadhili wake...ndio maana aliporudi tu, alichofanya ni kinyume na makubaliano yake na huyo mfadhili wake..

Alichofanya yeye ni kuanzisha kampuni yake, alitaka afanye hivyo haraka haraka, kabla hata ya huyo mfadhili wake, hajagundua kuwa amesharudi,na akipata pesa za kutosha, amrejeshee huyo jamaa gharama zake, kiasi ambacho ataona kinatosha, lakini cha ajabu kila siku akijaribu kupiga mahesabu akajikuta ana mambo mengine makubwa ya kulipa ili aweze kuendelea kibiashara, na akawa hawezi kufikia lengo lake, akawa anajipa moyo, kuwa ipo siku atapata kiasi cha kutosha, na hapo ataweza kulipa deni la fadhila, na kuachana na huyo mtu...,

Alikumbuka siku ile wakati anaondoka, aliyemfikisha uwanja wa ndege kwa gari lake mwenyewe ni huyo huyo mfadhili wake, na alikumbuka kauli yake aliyoitoa siku wanashikana mkono wa kwaheri;

‘Nakushukuru sana mfadhili wangu, sijui nitakulipa nini, ulichonifanyia ni kikubwa sana, kwani hii ndio ilikuwa ndoto yangu, ...’akasema

‘Usijali, mimi nipo na wewe, na cha muhimu ni wewe kuzingatia kile kilichokupeleka huko, ukirudi tutaonana, naweza kukuchukua ufanye kazi kwenye kampuni yangu...ndio lengo langu kubwa lakini hayo tutaona ukirudi...’akasema huyo mfadhili wake.

‘Nitashukuru sana bosi, maana nitakuwa nimeweza kushinda maisha,..nitakuwa nasoma nikijua pia kuna ajira nyuma yangu, sitakuangusha bosi wangu...’akasema na yeye akaelekea kuingia kwenye ndege. Kinyume na kauli hiyo, siku alipomaliza masomo yake, alijikuta akipinga kurudi na kufanya kazi kwa huyo mfadhili wake, alijiona kama ataendelea kuwa mtumwa wa ajira wakati mwenyewe anaweza kujiajiri.

Akiwa sasa anafungua mtandao, mtandao ambao ndio anaoweza kupata wateja wake, kwani kazi yake inahitaji makampuni makubwa, huko ndipo anapoweza kuweka mitandao na shughuli zote alizozisomea,...kwanza akafungua mtandao wa makampuni makubwa hapa nchini

 Alishangaa, kwani kwenye kiwango cha matajiri wakubwa, wenye makampuni makubwa, aliyekuwa akiongoza ni yule mfadhili wake, hapo akahisi moyo ukimuenda mbio tena

‘Sasa nitafanyaje, maana ili niweze kwenda mbali zaidi ni lazima nipate kazi za kufanya kwenye hizi kampuni tanzy, tatu, na zote zinamilikiwa an huyu mfadhili wangu, ambaye naogopa kukutana naye....’akawa anajiuliza

‘Lakini kwanini naogopa kwenda kuonana naye,...?’ akajiuliza na hapo akaanza kukumbuka maisha ya shuleni, wakati wanasoma shule moja na huyo mfadhili wake, ambaye yeye kutokana na utajiri wa baba yake, aliweza kuanza maisha ya amani kabla yake, na hakutarajia kuwa huyo aliyekuwa adui yake shuleni angeliweza kuja kuwa mfadhili wake kwenye maisha yake.

Alikumbuka kwanini wakiwa shuleni, alikuwa na uadui mkubwa na huyo mfadhili wake, kwani huyo mfadhili wake, alimtangulia kwa mwaka mmoja, yeye akiwa anaingia kidato cha kwanza alimkuta huyo mfadhili wake akiwa kidato cha pili

Uadui huu ulianza kutokana na ile hali ya wanafunzi wa kidato cha pili kuwanyanyasa wale wa kidato cha kwanza, hasa katika shule za kulala bweni. Yeye mara nyingi alikuwa akinyanyaswa na huyu mfadhili wake, kiasi kwamba walijenga uadui mkubwa sana. Hata kipindi huyo mfadhili wake, anamaliza kidato cha nne, hakuwa akitaka kabisa kuongea naye.

Sasa anajikuta tena, huyo huyo anakuwa maafdhili wake, ina maana yeye ataendelea kuwa chini wa huyo jamaa, hiyo hali kimoyoni hakuipenda, lakini hakuwa na la kufanya, akasema; baniani mbaya, lakini kiatu chake ni dawa, ni lazima nimtumikie kafiri, ili tu nipate mradi wangu...

Akiwa bado anaendelea kutafuta majiri wengine, akajikuta akitaka kumfahamu zaidi huyo mfadhili wake, akarudi kuanza kusoma habari za huyo tajiri, aligundua kuwa pamoja na utajiri wa huyo jamaaa, kama ataweza kupata kazi za kuweka mitanao kwenye hiyo kampuni anaweza akalipiza kisasi chake.

‘Hivi kwanini nimuogope, kwanini na mimi nisifanya jambo ambalo huyu tajiri atakuja kunikubali, nikamuweka mikononi....?’ akajiuliza

‘Lakini nitakuwa nimevunja miiko ya kazi yangu...’akasema

‘Aaah, ni nani atajua, itakuwa kati yangu mimi na yeye, akubali, au nimlipue, sizani kama atakubali nimharibie...’akasema akijenga jambo kwenye akili yake

‘Kwanza ni lazima nijue kazi zake, na makampuni yake yote ynavyofanya kazi, nikashajua, nikaweza kupenyeza mitandao yangu kwenye miradi yake, nikajua kila kitu anachokifanya, nitakuwa nimemuweka mikononi mwangu...’akasema na siku hiyo akaichukua kama siku ya kumsoma mfadhili wake, ambaye moyoni pia alimuona kaam aui yake.

Alisoma miradi na makampuni anayoyamiliki huyu tajiri, akatikisa kichwa. Alijua wazi kuwa utajiri huo na miradi hiyo mingi ilikuwa ni ya kidhuluma. Moja ya ndoto za Ngekewa ni kuhakikisha analipiza kisasi cha kuzalilishwa na huyu jamaa, alichomfanyia akiwa kidato cha kwanza hakikuweza kumtoka akilini , na alikuja kuapa kuwa ni lazima katika maisha yake, nay eye atakuja kumfanyia jambo baya.

‘Najua huyu jamaa ni tajiri, lakini utajiri wake, nahisi umegubikwa na dhuluma, na mimi dhamira yangu ya sio kulipiza kisasi, bali nataka kuhakikisha kazi kama hizi za dhuluma zinakwisha, ...kila nitakapoweka mitandao yangu, nitakuwa pia nachunguza uhalali wa biashara za hawa watu, na nikigundua kuna dhuluma, nitapambana nazo kinamna, nipi au nikutose...’akasema na kucheka

‘Kwanza kabisa ni lazima niwe na uhakika na ninachokifanya, cha muhimu ni kuwa na kumbukumbu za uhakika , nyaraka, na mawasiliano ya hawa matajiri, ..hii ni kazi ndogo tu,....’akasema akifungua mtandao wake wa uaskari kanzu wa kwenye mitandao.

Pamoja na kufanikiwa kwa ndoto za Ngekewa za kusoma, lakini moyoni aliumia sana pale alipopata shida wakati alikuwa na nafasi ya kusoma, lakini kwa vile hakuwa na uwezo wa kipesa akakamishwa kuendelea na masoma, na badala yake nafasi yake ikaja kuchukuliwa na mtoto wa tajiri, hili ilimuuma.

Hiyo haikutosha, kwani hata pale alipoamua kutafuta kazi, haikuwa jambo rahisi, na alipopata kazi akawa analipwa pesa ndogo sana, akawa analalamika, na ilivyo kwa hao matajiri wa kampuni binafsi, ukilalamika sana, wanakutafutia njia ya kukuondoa, mara ikatokea ridandansi, akaondolewa na kwenda kusota mitaani.

‘Hivi mimi nina mkosi gani, wazazi wangu ni masikini, wananihitajia sana, wale ambao wazazi wao wanajiweza, ndio wanaopata kazi, na ikifikia hatua ya kupunguzwa kazi, wanaobakia ni wale watoto wenye majina makubwa...’akawa analalamika.

Japokuwa alikuwa akipata kazi ndogo ndogo za watu binafasi, za kutengeneza komputa akiwa mitaani lakini pesa aliyokuwa akipata ilikuwa ni ndogo sana, akawa anajiuliza kwanini ya aliondolewa kazini wakati aliowaacha pale ujuzi wao ni mdogo ukilinganisha nay eye, hapo ndio ndoto yake ya kusoma zaidi ikawa anamjia akilini

‘Najua kama ningelisoma zaidi, nikaweza kujiajiri, haya yote yasingelikuwepo, alipenda ajisomeshe zaidi sio  kwa kuajiriwa, aliona kuajiriwa ni utumwa,maana matajiri wanakutumia wa masilahi yao tu, kwake yeye ni kusoma na kuja kujiajiri, lakini je angeliwezaje kusoma wakati hana pesa. Alijilaumu sana kwa kuzaliwa ndani ya familia ya kimasikini. Hata hivyo, akilini alijipa moyo kuwa ipo siku atafanikiwa na kuja kuisaidia familia yake.

Wakati akiwa kazini, aligundua kumbe utajiri mwingi wa watu hawa, ni wa dhuluma, hapo ndipo akaweka dhamira moyoni kuwa akiweza kujiwezesha akasomea vyema utaalamu huo wa komputa atahakikisha anawachunguza hao matajiri kama kweli utajiri wao ni halali na kwa jinsi anavyojua wengi wameupata utajiri wao isivyo halali.

‘Nikijua siri za makampuni mengi, nitaweza kujijengea mtandao wa namna nyingine, ambao utaniwezesha na mimi kuogopwa,...ni lazima nipambane na hawa watu walijijenga kwa dhuluma, ni lazima utajiri wao tugawane ili niweze kuwasaidia wanaostahiki.....’akawa anajisemea moyoni.

Kiukweli, hata alipokuwa akisoma huko nje, japokuwa alifadhiliwa na mmoja wa watu anaowachukia, moyoni, alijawa na usongo wa kuja kupambana na hao matajiri aliowaona kwake ni watu wa dhuluma.

Na ndio maana aliporudi tu kutoka nje, kwanza alichofikiria ni kuanzisha kampuni yake na kila alipopata wateja cha kwanza alichokifanya ni kuhakikisha kuwa anazipata kumbukumbu zote muhimu za matajiri wa hapa nchini, na kwake ilikuwa ni kazi ndogo, kwani kwenye mtandao wake alikuwa ameweka kifaa cha ukachero wa mitandao,.

Akiwa bado yupo ofisini kwake, akiendelea kuzipitia kumbukumbu za mfadili wake, huku akiwaza, jinsi gani atakavyoweza kuingiza mitandao yake ndani ya hiyo kampuni, lakini sio kuwa muajiriwa wa kampuni hiyo, hakupenda kuendelea kuwa mtumwa wa huyo jamaa...

‘Japokuwa huyu jamaa ndiye aliyenitoa juani na hatimaye akaniwezesha kwenda kusoma Marekani, lakini bado nina kinyongo naye moyoni, na sizani hata hivyo kanifanyia hivyo kwa nia njema, hawa matajiri wanakuwa na ajenda ya siri..’akasema

‘Na mimi sitampa nafasi hiyo, sitakubali kuajiriwa kwenye kampuni yake na kuwa mtumwa wake tena, japokuwa nafahamu nina deni kubwa la kulipa la pesa na utu alionifanyia...’akasema

Akiwa bado anamuwaza mfadhili huyo, ambaye alikutana naye, siku akiwa ameshakata tamaa ya kimaisha, siku hiyo hakuwa na pesa kabisa, na hakujua aende wapi tena, hata akawa anatamani hata kuiba, maana mwenye nyumba alipoapanga, alikuwa amekuaj juu, anataka pesa yake ya pango, vinginevyo ahame, na hakujua ahamie wapi, ...

Siku hiyo akiwa anatembea mitaani, akiongea mwenyewe kama mtu aliyepungukiwa na akili, akasikia gari likimpigia honi nyuma yake, hakutaka kugeuka, alitamani hilo gari limgonge, ajifie, akapumzike, lakini bado akazidi kusikia gari hilo likiendelea kumpigia honi nyuma yake, hakutaka kabisa kugeuka, na moyoni akasema;

‘Huyu mtu ana nini, mbona nipo pembeni ya barabara, bado ananipigia honi, angelijua nilivyojawa na hasira, asingelinisumbua na honi zake...’akawa anajisemea

Mara lile gari likampita na kuja kusimama mbele yake, akajua jamaa kakasirika, anataka kumbwatukia, na moyoni, akasema, huyu mtu akinianza kunisemesha, nitamtapikia maneno machafu, na akizidi nitampa kichapo nikalale jela, kwanza mwenye nyumba anataka kunifukuza, nitalala wapi.

Gari la kifahari likasimama mbele yake, na jamaa aliyekuwa ndani ya hiyo gari, akashusha kiyoo, na akajikuta akiangaliana uso kwa uso, na bwana Diamu.

‘Di-amu...’akajikuta akisema

‘Vipi formu one wangu.....’akasema huyo jamaa kwa utani, na utani huo hakuupenda kabisa kuusikia, lakini kwa muda huo, alihitaji angalau hata pesa ya maji ya kunywa na akajua huyo jamaa anaweza kumfadhili, japokuwa hakutaka kabisa iwe hivyo,hasa kutoka kwa mtu kama huyo.

‘Ndugu yangu za siku nyingi,...’akajikaza kumchangamkia

‘Ni zuri, mwenyewe si unaona, ...’akasema na hata kabla Ngekewa hajasema kitu, huyo jamaa akasema kwa mshangao

‘Mbona upo hivi, ingia ndani ya gari, nikutoe kidogo, kwani unaelekea wapi?’ akaulizwa

‘Hata najua ninapokwenda, yaani hapa nilipo ni miguu tu inanisukuma, popote nipo tayari kwenda...’akajikuta akisema, na jamaa akacheka, na kusema;

‘Nyie watu vipi, mnafanya nini hapa mjini, kwanini msiende kijijini kulima, unakumbuka nilipokupokea pale shuleni, nikakkuambia utakuwa mtumwa wangu, ....hahaha...’akasema na kucheka kwa dharau, na kicheko na kauli hiyo ilimuuma sana Ngekewa, lakini hakuwa na la kufanya.

‘Haya panda ndani ya gari, ukapate chochote, usijali, tutaona jinsi gani nitaweza kukusaidia, yote maisha ndugu yangu...’akasema na akaingia ndani ya gari, huku akichelewa, kuharibu hali ya hewa ya hilo gari ni mijasho jasho yake.

Waliondoka hapo hadi kwenye hoteli moja ya hali ya juu, na wakaagizia chakula, wakawa wanakula, huku wakiongea hili na lile, na baadaye jamaa akauliza;

‘Hebu niambie, mambo yako ya kikazi yanakwendaje?’ akaulizwa

‘Hivyo hivyo tu, leo upo hapa kesho upo pale, sijawa na kazi ya uhakika....’akasema

‘Ooh, nakumbuka kwa mara ya mwisho nilipokutana nawe ulisema umepata kazi kwenye kampuni moja hivi, vipi tena?’ akauliza

‘Haya yana hadithi ndefu, na sipendi kabisa kuihadithia, .....’akasema

‘Na vipi ile ndoto yako ya kuwa mtaalamu wa komputa imeishia wapi?’ akamuuliza

‘Hata sina mawazo nayo tena, maana kazi zenyewe  shida, nitapata wapi pesa za kujisomeshea, ningeliweza kupata kazi yenye uhakika, nikaweka akiba ningeliweza kujisomesha, lakini kazi hakuna kazi zina wenyewe, sio sisi akina Kayumba....’akasema na mwenzake akacheka sana

‘Najua utanicheka sana, na kuniona mimi ni mzembe, lakini hujui kilichotokea na kwanini nasota mitaani...’akasema na huyo jamaa akaangalia saa yake, na ilionekana kama anawahi jambo, akasema;

‘Ok, kwahiyo tatizo kubwa ni pesa, na ufadhili, unajua mimi nilikuwa nawatafuta marafiki zangu wa zamani ninaowaamini niweze kufanya nao mikataba ya kuwawezesha ili baadaye na wao waniwezeshe kinamna ninayotaka mimi,..sijui unanielewa...’akasema

‘Kwa vipi, labda nifafanulie...?’ akauliza

‘Nipo tayari kutoa pesa za ada, hata kwenda kusoma nje ya nchi, lakini kwa masharti kuwa ukimaliza masomo uje kufanya kazi kwenye kampuni yangu, upo tayari kwa hilo?’ akaulizwa na Ngekewa hakuamini, akabaki kumkodolea macho huyo jamaa, akawa anahisi anamtania

‘Kweli unaweza kufanya hivyo...?’ akauliza

‘Kwanini nishindwe, pesa ninayo, na moyo wa kusaidia upo, mimi sitaki kuona marafiki ninaowafahamu wapo mitaani wanasota, ...nipo tayari kukusaidia ni wewe tu...’akasema

‘Nitashukuru sana nikipata bahati hiyo...’akasema

‘Basi jiandae, mimi nataka ukasome, na sio hapa nchini, nataka ukasome nje, nataka uwe mtaalamu kweli, uweze kutimiza ile ndoto yako, unasemaje,?’ akasema

‘Oh, siamini....’akasema

‘Huniamini au huamini kuwa hiyo inawezekana?’ akaulizwa

‘Nakuamini sana kuwa unaweza kumuwezesha mtu, lakini sio kwa ...hadi kusome nje, kweli unaweza kufanya hivyo, ili ndoto yangu itimie, ?.’akauliza kwa mshangao.

‘Amini hivyo...’akasema na huyo jamaa akasimama na kutoa pesa mfukoni akamkabidhi na kusema;

‘Chukua pesa hizi kidogo, zikusaidie katika maandalizi yako, mimi nitafanya mawasiliano na chuo kimoja, nakiamini sana hicho chuo kuna jamaa yangu niliwasiliana naye jana akaniambia hapo wanatoa mafunzo ya hali ya juu, huko utapata mafunzo unayoyahitajia, na ambayo hata mimi nayahitajia kwenye kampuni yangu,...’akasema

‘Nashukuru sana,...’akasema bado akiwa haamini kwani alikuwa katika hali mbaya, alikuwa hana hata senti moja mfukoni, lakini mfadhili huyu alimpa pesa ambayo hakutegemea kuipata.

‘Basi tutawasiliana, nikiweka mambo yangu tayari...’akasema huyo jamaa baada ya kutoa kadi yake ya simu na kumkabidhi Ngekewa, kuwa mambo yakiwa tayari ataitwa tayari kwa safari, kwenda kusoma Marekani, hakuamini, hadi siku alipokabidhiwa tiketi na masurufu mengine. Yeye kwa muda huo hakujua kuwa ameingia kwenye chambo cha bwana Diamu, kwa muda huo alimuona kama mfadhili muhimu wa maisha yake.

Akiwa bado anamuwaza tajiri huyo, akataka kupiga simu kwa wateja wake, lakini kabla hajaigusa simu yake ya mezani, simu ile ikaanza kuita, alijikuta akishituka, kama vile aliogopa mtu kumpigia asiyetaka kuongea naye...

Alishangaa kwa jinsi gani ule mlio wa simu ulivyomshitua, na akilini akawa anajiuliza ni kwanini alishituka kiasi kile, wakati siku zote anapigiwa simu, lakini haijawahi kutokea kushituka kiasi hicho. Lakini moyoni akasema labda ni kwa vile alikuwa akimwaza mtu mmoja asiyependa kumuwaza. Aliinua ile simu na sauti nyororo ya katibu wake muhutasi alipenya ndani ya ubongo wake.

`Bosi, kuna simu yako toka kwa, bwana mmoja...’huyo binti akasema kwa madaha
‘Mtu gani, akauliza kwa sauti ya hasira kidogo, hakutaka kuongea na mtu mwingine zaidi ya wateja wake.

‘Ni bwana mmoja, anajina la ajabu kidogo...’akasema

‘Ni nani, mbona unaongea kwa kukatisha, ...?’ akauliza

‘Ni jina lake linanipa mashaka, eti anaitwa Di-a-mu...au Daamu, anasema wewe unamfahamu sana?’ Sauti aliyoiona ni nyororo iligeuka kuwa nyongo, na kutamani kumwambia aikate ile simu na amwambie huyo mtu kuwa hayupo, lakini alishindwa kutamka na mara yule binti akamuunganisha na bwana Diamu, alipoona bosi wake yupo kimya kwa muda.

`Ngekewa vipi wewe unarejea nchini bila hata ya kuniarifu, lakini hutaamini tangu unapanda ndege Marekani kurejea huku, nilikuwa nipo na wewe..na kila unalolifanya hapo nalifahamu sana, nilikuwa nasubiri nione ahadi yako ilivyo...’akasema

‘Umejuaje...?’ akauliza

‘Hilo sio muhimu kwa sasa, nataka tuonane kwenye hoteli yangu ya Paradiso kesho saa mbili za usiku, usikose tafadhali…’ Na mara simu ikakatwa kabla hajatoa udhuru kuwa hatafika.

Bwana Ngekewa alibaki ameishikilia ile simu mkononi huku ameshikwa na kigugumizi, na alimyemzindua ni katibu wake muhutasi aliyeingia na kwa nyuma yake alionekana kuongozana na mgeni. Hali ile ilimtonesha kidonda kwani alishahamaki, hakupenda tabia ya kuletewa mgeni moja kwa moja kabla hajaulizwa kama yupo tayari na huyo mgeni au la.

 Alijikuta akiibamiza ile simu kwenye sehemu yake na kumkodolea yule binti kwa macho ya hasira. Alitaka kumfokea kwanini aliunganisha ile simu kabla hajampa ruhusa na tena anataka kumleta mgeni hata kabla hajamuuliza kuwa aingie au la,

Pale alipokaa kwenye kiti chake alitaka kumfokea huyo katibu muhutasi wake ili hasira zake ziishie kwake, lakini mara yule mgeni aliyekuwa nyuma ya huyo katibu muhutasi wake akajitokeza kwa kumsogeza huyu binti pembeni

Moyo wa Ngekewa ulilipuka kwa mshindo wa aina yake, na kujikuta akitoa macho na mshangao, na mdomo ukimkauka, na kisa ni kutokana na urembo wa huyo mgeni hajawahi kuuona maishani mwake na mkononi ana mauwa na kwenye maua yale kuna kadi kubwa ya nakshi. Yeye akaishia kusema

`Oh, oh, ka-ka-ka-ribu mgeni...’akasema na kujibaragua kusimama na kuanza kutoka pale alipokuwa amekaa ili aje kumkaribisha mgeni wake, na wakati huo katibu wake muhutasi yupo nyuma ya huyo mgeni, akisubiria ataambiwa nini.

`Ahsante Bwana Ngekewa , mimi sio mkaaji, mimi ni msaidizi wa bwana Diamu...’akasema huyo mgeni, na aliposikia hilo jina Diamu, akawa kama kapigwa sindano ya ganzi, akasimama ghafla

‘Haiwezekani,....’akasema.

‘Mimi nimekuja mahsusi kukukabidhi hii kadi ya mualiko ili uhudhurie mkutano maalumu kwenye hoteli yake ya Paradiso, bila kukosa...’akasema

‘Kakutuma hivyo Diamu...?’ akauliza

‘Ndio kwani vipi, ..., au unasemaje bwana Ngekewa?’ Yule binti mgeni akatoa tabasamu dogo, ambalo lilimfanya Ngekewa azindukane kwenye mshituko, na kujikuta akisema kile ambacho hakukusudia kukisema

`Ahsante mrembo, ha-ha-mna ta-bu, laakini…hebu kaaa kidogo, utie baraka’ Kabla hajamaliza yule binti akawa ameshamsogelea na kuhakikisha ile kadi imefika mkononi mwa mlengwa na kugeuka kuondoka

 Bwana Ngekewa akajikuta akiwa ameangaliana na katibu wake muhutasi ambaye kwa muda ule alimuona si chochote kwenye warembo...alikuwa akitaka kuiangalia ile kadi,...

‘Shiiiiiiti....’akasema Ngekewa kwa hasira

NB Mambo yanaanza hivyo, je mpo tayari

WAZO LA LEO: Wakati mwingine tuwe makini na zawadi tunazopewa, hasa tukiwa kwenye majukumu yetu ya kikazi, zawadi nyingine ni mitego, zawadi nyingine hugeuka kuwa rushwa. Cha muhimu hata kama tutazipokea hizo zawadi, lakini utendaji wetu wa kazi, uwe pale pale, tujiamini tukijua kuwa kazi tulizonazo ni dhamana tu. 


Ni mimi: emu-three

No comments :