Diamu akiwa pake yake kwenye ofisi yake, na
kitabu chake bado kikiwa mezani, alianza kuweka wazo lake kwenye maandishi, hakutaka mtu awe karibu naye kwa muda huo, japokuwa mara kwa mara akiishiwa na kinywaji alikuwa akimuita mrembo wake, hii kwake ni kazi na dawa.
Leo ndio siku muhimu aliyoipanga kuhitimisha wazo lake kimaandishi kabla hajaliweka mezani kwa watu wake, ilikuwa simu muhimu ya kuanza kufungua kitabu chake muhimu, na yeye aliiona hii siku kama yaliyomo kwenye kitabu chake cha wazo la ndoto yake...ni siku pia ya maamuzi ya kile alichokipanga miaka mingi nyuma, alitaka
aanze mara moja, bila kumuogopa mtu, hakutaka kabisa ushauri mwingine, kwanza
kama kawaida yake akaitisha kinywaji chake akipendacho, na mrembo wake akafika;
Mlango ulifungulia na mrembo huyo akasimama
mlangoni kwa pozi analolijua yeye, mrembo huyo alifanya hivyo makusudi, alitaka
bosi wake amuangalie kwa makini, alishamfahamu bosi wake anachotaka ni nini,
hasa akiingia mlangoni...wanaume wana siri yao... , na kweli bosi akaacha
alichokuwa akiandika, akawa anamtizama huyo mrembo, halafu akatabasamu na
kusema;
‘Unanifanya nihisi nipo sehemu nyingine, maana
macho yanaburudika, hilo vazi la leo, mmh, hongera...nataka na masikio nayo yaburudike,
hebu niimbie kidogo...’akasema
Hapo akawa kachokoza, kwani kwa kuimba binti
huyu sio haba, kajaliwa sauti, yule binti alianza kuimba kwa sauti nyororo, na
bosi akawa kama anafumba macho, akisikiliza sauti hiyo, hadi yule binti
akamaliza
‘Mhh, mambo si hayo, masikio nayo yameburudika
....’akasema bosi
‘Ushindwe tu mwenyewe bosi...’akasema huyo
mrembo
‘Hahaha, tutakaa baadaye , ila kama
nilivyokuambia,nataka uende shule maalumu, kuna mtaalam mmoja, ninamkubali,
nataka ukafundwe naye, na huku unasoma masomo ya kiofisi, uive vyema,
isionekana kuwa wewe hujui kitu,, ...’akasema
‘Bosi naye bwana, mimi ni kitu gani
nisichokijua, ukatibu muhutasi nimeusomea naufahamu vyema, mambo mengine mimi
nayafahamu sana, labda mimi nikawe mwalimu wao...’akasema
‘Nataka uwe nitakavyo mimi,...kufundwa huko sio
unavyokujua wewe, utaona mwenyewe, kuna mtaalamu mmoja, kanisomesha, na
nimeshamuweka kwenye watu wangu, anajua ni nini cha kukufundisha, mwenyewe
utaona....kuna mambo ya ukatibu muhutasi ambayo huyafahamu,, kuna mambo ya kila
namna utajifunza, pia hata kutumia silaha...’akasema
‘Kutumia silaha!..... hapana mimi naogopa sana
silaha, sipendi kabisa bunduki...’akasema
‘Utafundishwa, na hutaiogopa tena, utafundishwa
kupigana karate, na mafunzo ya kila namna nataka ukiwa nami nijue nina mtu ,
sio mti.....Nataka ukiwa karibu yangu uwe kweli mtu wangu, ujue kunilinda kwa
hali na mali...’akasema
‘Sawa bosi, mimi nipo kwa ajili yako
tu....’akasema huyo mrembo
‘Upo kwa ajili yangu kwa vile unatafuta pesa,
hahaha, usinifanye mimi mjinga, nakufahamu sana, mbele ya pesa unaweza kufanya
lolote...’akasema
‘Sio hivyo bosi, unajua tulikotoka, wewe na
mimi hatutupani,hata kama ungekuwa huna pesa, ningelifanya hivi hivi
...’akasema huku akishika kichwa kuonyesha aibu kwani huo ndio ukweli wenyewe,
kinachoangaliwa hapo ni pesa tu.
‘Ni kweli, wewe na mimi hatutatupani, kama ni
kufa tutakufa sote, nataka uwe karibu yangu kiukweli,...’akasema Diamu
‘Usikonde bosi, mwenyewe utafurahi....’akasema
na kuweka beseni lenye gilasi na kinywaji ,mezani, na akamimina kinywaji na
kumnywesha bosi wake, baosi wake akanywa fundo moja, halafu akasema;
‘Inatosha, wewe acha kila kitu hapa mezani,
nenda kaendelee na shughuli zako, nitakuita baadaye kwa mazungumzo
yetu....’akasema na huyo binti, akatoka kwa madaha akimuacha bosi wake akiendelea
kumuangalia
‘Hii ndio nataka...’akasema huyo bosi huku
akifunua kurasa kwenye kitabu chake
‘Hii ndio nataka, kazi na dawa, siumizi
kichwa,....ni lazima huyu binti nimjenge vyema, atauwa hazina ya mambo yangu,
kwanza akasome, akimaliza masomo, atakuwa zaidi ya hivyo,....atakuwa akitembea
na dogo dogo wengi pembeni yake, kila mmoja akiwa na kazi yake maalumu,
nitakuwa mfalme, anayelindwa na mabinti wazuri....hahahaha...’akasema na kukuna
kichwa akiwazia ndoto yake hiyo.
‘Sasa ngoja niliweke wazo langu sawa
sawa...’akasema
‘Wazo
langu ni pana sana, lina mambo mengi, lakini nia kubwa ni kuhakikisha naweza
kuitawala dunia kinamna yangu, dunia nitakavyo mimi, sitaki kufungwa na mtu,
mara hiki sio sahihi, hiki sitaki hapana, nataka niwe na nafasi ya maamuzi
yangu ..niwe na namna ambayo nitaweza kufanya lolote , mahali popote bila kuwa
na wasiwasi, au kikwazo,...’akaandika hivyo
‘Hii inawezekana, ukiwa na pesa na akili kama
zangu, nahisi wengi wataniona mimi ni mwehu, au labda nimeleweshwa na pesa za
urithi, pesa zipo lakini zikae tu, hapana lazima zifanya jambo, na jambo
nitakalo mimi nataka liwe la kipekee, nataka uzalishaji wa pesa za mkupuo,
nikitaka pesa zinamwagika tu...hahaha, waache wasema ni ndoto za Alinacha
‘Hamna ndoto hapa, siku nikikamilisha hili
zoezi, kila mtu atanivulia kofia...’akasema kimoyo moyo
‘Mimi wazo langu ni kuwa nataka niwe na mamlaka
ya kila jambo, nataka niwe na dunia yangu, nitakavyo mimi....’hapoa akatulia
kidogo akiangalia ile picha ya dunia iliyozungukwa na mikono, akaigusa, na mara
ile mikono ikatawanyika, na kila mkono ukawa unafanya shughuli
fulani,.....halafu kukaanza kumwagika pesa nyingi tu na baadaye ikatokea picha
yake akiwa kazikalia hizo pesa...
Aliangalia ile picha kwa muda, ikijirudia rudia
badaye akasema;
‘Yah, wazo langu ni hilo kwa kifupi, niwe na
dunia yangu nikavyo mimi....’akakuna kichwa na kuangalia ile picha ya dunia
iliyozungukwa na mikono mingi ikijikusanye tena
‘Katika
dunia hiyo nawataka wataalamu wa aina zote, yaani kila nyanja, nimpate bingwa
wake, niwapate wataalamu waliozidi utaalamu unaojulikana hapa duniani, ni pesa
tu, na nitawawezesha zaidi...lakini kazi ipo hapa, nikikamisha hili,
nikawakusanya hawa mabingwa, nimemaliza kila kitu, hapa natakiwa nitumie pesa
kweli kweli, ...’akasema
‘Kwanza , namtaka dakitari bingwa wa kila kitu
kinachomuhusu binadamu...docta bingwa, huyu ataweza kunisaidia kumiliki mambo
yote ya hospitalini, huku kuna umuhimu wake,..maana mtu akipelekwa huko,
anaumwa, na ni mtu wangu, nitajua jinsi gani ya kumfanyia lolote, huyu anaweza
kumtengeneza mtu akawa sivyo ndivyo, hahaha, hili tutakuja kuliona huko mbele.....
‘Dakitari huyu nataka awe anacheza namba nyingi...inawezekana
asiwe peke yake, atakuwa na wasaidizi wake, lakini wenye mtizamo wetu,...
kukitokea hata mauaji, huyu ataweza kuandika tutakavyo sisi, ukweli unabakia
kwetu, uwongo unakwenda huko kwa wanaochunguza, hata hivyo, huko nako kwa
wachunguzi, kutakuwa na watu wetu...hapo imeleweka,
‘Sasa huyu dakitari natakiwa nimpate haraka
iwezekanavyo, maana tukianza mambo ni lazima kutakuwa na purukushani za hapa na
pale, ...nataka kwanza watu waniogope, na wataniogopa vipi,kama sikufanya jambo,...huyu
ni muhimu sana na anahitajika kwa haraka...’akakuna kichwa na kuwawazia marafiki
zake madakitari.
‘Nikimuacha dakitari, pia namtaka mtaalamu wa
komputa ambaye kichwa chake ni zaidi ya computa zote duniani. ...hahaha huyu
atakuwa akichunguza kila kinachotokea duniani, na kila linalofanyika linakuwa
mikononi mwake....huyu ni mtu muhimu sana...nitashirikiana naye, maana ni mtu
wa usalama, atakuwa anamlinda kila mtu wetu...’akakuna kichwa akiwaza kazi
nyingina za huyu mtu, lakini akasema
‘Huyu kwa vile nitakuwa naye sambamba, sihitaji
sana kuandika kazi zake..ni msiri wangu muhimu...’akasema na kutulia kidogo.
‘Mhh, namtaka mkemia, mtengenezaji madawa
ambaye anaweza kutengeneza madawa ya kila namna, kitengo chake kitakuwa
sambamba na watu wa silaha za kemikali,..hapa nataka, silaha na kila kitu
ambacho ni muhimu kuangamiza kila atakayeleta fyofyoko, bila hata mtu
kufahamu...hahaha, lakini mimi sio muuaji, kitakachofanya hivyo ni hizo kemikali,
sio mimi....mmh, nitakuwa mbali kabisa, .....’akatabasamu.
‘Haya , pia namuhitajia mtaalamu wa mashine, mtaalamu
wa magari, mtaalamu wa kila aina ya ufundi, nyumba, vitasa, na kila aina...na
kwanini natafuta utaalamu wa magari , ni kwasababu kuna mihangaiko ya hapa na
pale, gari likifanya jambo, linahitajika kubadilishwa haraka iwezekanavyo,
kinamna yoyote ile,leo walione hivi kesho vile polisi wakilitafuta waishie
patupu...hahaha, mimi kichwa bhwana....’akasema huku akionyesha kwenye komputa
yake jinsi gari linavyobadika, kutoka muundo huu na kwenda kwenye muundo
mwingine.
‘Pia namtaka mtaalamu, ….mtaalamu wa ...’ akawa
anawataja watalaamu wa kila fani zilizopo duniani, na alihitaji wale waliobobea
kwenye hiyo fani, nia ni kuwa juu ya kila fani ili aweze kumiliki kila utendaji
kwenye hiyo fani, alipomaliza kuainisha watalaamu anaowahitajia, akacheka
kicheko cha dharau,
‘Hahaha hawa ndio wataniwezesha, nifanye kile
nilichokitaka. Nahitaji mikono mingi ya wataalamu...yah, hili ndio wazo
langu...’akasema huku akinywa mafundi mawili ya kinywaji chake
Nikifanikiwa hilo, basi nitakuwa na dunia ninayoitaka
mimi, dunia ambayo naimiliki mimi kina mna yangu,...hahaha, ukiwa na akili na
pesa, bhwana, dunia unaweza kuiweka mikononi mwako,...lakini kwanza ni lazima nipate
mikono ya wataalamu mbali mbali, ambao watakuwa wakifuata amri yangu, hawa watasaidia
kuijenga dunia niitakayo mimi...’akatulia na kutabasamu.
‘Hahaha, kweli nikifanikiwa hili, nitakuwa
nimewezesha ndoto yangu, ndoto ya kuwa na dunia yangu...pesa itaongea, na mapesa
yatakuja kwa wingi, ni siri ndogo tu, wenyewe wataona.
‘Nikisema dunia yangu, watu wataniona
nimekufuru, hapana, mimi sio hivyo, hili neno wasilitafsiri vibaya, mimi
similiki dunia, sina uwezo huo katu, mwenye uwezo huo ni mungu, ila mimi
ninachotaka ni kuwa na namna niitakavyo mimi, utaalamu, uwezo wa kufanya mambo
nipendavyo mimi, yaani niwe na namna dunia inayokwenda kwa matamanio
yangu.....labda nitaeleweka kidogo...’akakuna kichwa.
‘Haya ndio mawazo yangu,....’akasema Diamu
akifunga kile kitabu chake, na kujizungusha kwenye kiti chake.
Haya ndiyo mawazo ya kijana Diamu, na wakati
anawaza haya, alikuwa ameshapitishwa kuwa raisi na mumiliki wa makampuni yote
aliyoacha baba yake, japokuwa kulikuwa na upinzani wa hapa na pale, lakini
baadaye ikapigwa kura na yeye akashinda.
Alishaongea na wazee, na wahusika wakuu, na
baadhi ya wawekezaji akawaahidi kuwa hatawaangusha, ila baadhi ya wazee
walisusia hicho kikao, wakijua kuwa hakina ajenda nzuri kwao, hata hivyo zaidi
ya nusu ya wajumbe walifika, na kikao kikaendelea
Baada ya ushindi wake, ikaja zamu ya kuchagua
wasaidizi wake, aliwachagua marafiki zake, na kuhakikisha kuwa safu ya wazee
wote waliohanganika na baba yake hawapo kwenye wasaidizi wake, aliwachagua
wawikilishi wa wazee, ambao alijua wapo upande wake, na cha kusangaza zaidi,
msaidizi wake wa karibu akawa mrembo wake.
‘Huyu mtu ataweza kweli hii kazi, anaonekana ni
muhuni tu, mlevi, na malaya...’akasema mzee mmoja
‘Ngoja tuone, maana baba yake alisema
alishamuandaa kushika hatamu, na kuna waraka uliandikwa na baba yake kuwa mtoto
wake huyu ndiye mrithi wake, hapo huwezi kuweka pngamizi lolote, ikizingatiwa
kuwa wao ndio wenye hisa kubwa,...ni ujana, utaisha tu, akipata mshauri mnzuri,
nahisi mambo yatakwenda vyema...’akasema.
‘Nasikia sisi wazee katusahau, kashindwa kujua
sisi ndio tuliohangaika na baba yake kubeba matofali, hadi hapa, wanaona
matunda yake,...leo hii anaingia madarakani anakosa shukurani, naona tamaa zimemzidi,
yeye anajifanya kijana , hajui wazee tupo, tutapambana naye tu, mimi nakwambia
sitatulia mpaka nione mwisho wake ....’akasema mzee mwingine.
‘Hayo sio ya kuongea hapa, tutakutana na wazee
wenzetu tuone tutafanya nini,..’akasema mwenzake
‘Wala mimi sisubiri hicho kikao chenu, nakwenda
kufanya yangu, siwezi kukubali jasho nililopoteza hapo sio dogo, ujana wangu
wote uliishia hapo,leo hii ndio imekuwa hivyo.....’akasema huyo mzee
‘Yote yana mwisho, walianza wengine leo wapo
wapi....nasikia ana ndoto yake ya kuleta mabadiliko,...sijui ni ndoto
gani...’akasema mwingine
‘Ndoto, mwisho wake ni kuzindukana, atalala
ataona, akizindukana, dunia ipo pale pale...’akasema mzee mwingine
‘Labda ana dunia yake, huwezi kujua...’akasema
mzee mwingine
‘Anajidangaya.....
********
Siku zilivyokwenda ndivyo watu walivyoanza
kumtambua huyu kijana, kwa mbwemwe zake, akipita mahali, akiwa na walinzi kila
upande, na gari lake liliongozwa kwa king’ora, na hata polisi wakamfahamu.
Watu wakaanza kumuongelea kila kona ya jiji
hili, kuwa ni mmoja wa matajiri kijana, na tajiri mdogo hapa duniani, ...ikawa kila
akipita watu wanamuita,, Diamu....Damu....
‘Hahaha kila kona ya huu mji wananitaja
mimi,....na hata magazeti, ...’hapo akakumbuka jambo, akafungua kitabu chake na
kuandika
‘Pia katika watu ninaoawahitaji, ni pamoja na
mtaalamu anayejua propaganda, uzushi,fitina, huyu atakuwa karibu na magazeti
yote, pia tunahitajika kuwa na magezti yetu mengi, hasa ya udaku, hapa kuna
biashara nzuri tu, hawa waheshimiwa na matajiri wanzizi, nahitaji pesa yao kwa
wingi tu,...na ili nifanikiwe hili ni lazima na sisi tuwe na chombo cha
mawasiliano..yes hili ni muhimu.’akatulia akiwaza
‘Lakini mimi sitaki nionekane popote, sura
yangu nataka iwe siri, na nikionekana mahali isiwezekana kupigwa pichwa, hii
miwani itafanya kazi yake.....’akaivua ile miwani, ile miwani alipewa kama
zawadi, ukipigwa pichwa ukiwa umevaa hiyo miwani picha hatoki, na ikitoka
haionyeshi sura, ni lazima kutakuwa na mawingu ya kuziba muonekano wa uso...
Akawa sasa anakiwazia kitengo cha fitina,...ni
jambo ambalo aliliona linaweza kumletea pesa, kama ataliweka sawa.
‘Katika kitengo hiki cha fitina, propaganda na
uzushi,, nataka mtu aliyesomea uandishi, anayejua kuandika kitu kikakubalika,
lakini pia awe intelegensia,...kuna hawa watu vyuoni walikuwa wakiitwa father
punch,...nitamtfauta jamaa yangu, nitampeleka shule ya kiaina yangu,,...
‘Mmmh,halafu nimekumbuka kitu, kuna biashara
nzuri ya silaha, hili nitaongea na jamaa yangu huko majuu zinapotengenezewa
silaha za moto, aliniambia kipindi cha
nyuma biashara hii ilidorora sana kwani siasa imekuwa haina chokochoko sana
ndio maana vita vimetulia kidogo, ila wanasema wamejipanga upya, wameona sehemu
inayoweza kuingilika na kuweka fitina ni kwenye makundi ya kidini, huko wamejaribu
na inaonekana kufanya kazi, sasa na mimi kama naweza kuifanya hii biashara ni
muhimu niwe na kitengo mahususi cha fitina
‘Yes,
halafu sasa kuna hii, propaganda ya magaidi..., yes, hapa naona kuna pesa, hawa
watu wanaoitwa magaidi, wanatafutwa kila kona, lengo ni biashara ya silaha
ipambe moto, hizi silaha zimetengenezwa za nini, ni kuulia watu, sasa
zitauzwaje,...wakagaundua hii propaganda ya magaidi,...imeweza kulipa kwa kiasi
kikubwa, kila kukitokea tatizo linaelekezwa huko, kwa magaidi....watu wajanja,
‘Nimegundua jambo, watu wengi hawapendi kufanya
utafiti, wanakurupuka tu, wakisikia jambo, wanalichukulia kama
lilivyo,....hahaha, magaidi, magaidi kumbe kuna watu wana malengo yao .....mmh,
ni lazima na mimi nijikite huku nione kama na mimi nitapata kitu, niunde tume mahususi
ya fitina, nipandikize watu wangu kwenye hawa watu wenye kuchukiwa...
‘Nitawafunda watu, wajifanye watalaamu wa imani
za dini, wazame kwenye makundi ya kidini, huko watafiti kuna nini, wanahitaji
nini, na wakishajua udhaifu wao, tunapandikiza fitina,....likitokea tatizo, najua
makundi hayo yataelekezwa kidole,watakamatwa wakubwa zao, wakikamatwa, watu
wangu wanaendelea kutia fitina, kunatokea vurugu wakitaka viongozi wao waachiwe,
vurugu zitazaa chuki, chuki itazaa vita, hawa watawachukia hawa, baadaye watahitaji
silaha, ...hahaha lakini hili ni lazima niliangalie kwa makini...nitaua hata
ndugu zangu...
‘Lakini ngoja kwanza, nitaongea na jamaa yangu
atanielekeza jinsi ya kufanya, wao ni wazoefu wa biashara hii, ...lakini ni
lazima nijikite katika biashara hii ya silaha za moto, silaha za kemikali sio
tatizo, nitakuwa na wataalamu wataziunda....hili nitalifanyia kazi pia
‘Mhh, lakini hizi za moto, tutahitajika kununua
nje,....hata hivyo huwezi kununua kitu kikae tu, ni lazima upate wateja, au sio.....ni
lazima tujenge fitina kuwe na vita, na fitina ni kipaji, kwahiyo anahitajika
mtalaamu wa fitina, huyu atapatikana tu,...hahaha, watu hawajui kuwa kila
kipaji na mtaji, hahahaha....unacheza na kichwa wewe.’
‘Nikifanikiwa haya yote, najua wataanza
kunitaja, sio tu kwa utajiri, lakini pia watajua kuwa mimi ni mmiliki wa dunia ya
aina yangu, dunia nitakayoweza kuiendesha kwa kiona mbali, wenyewe wanaita `remote control,’
‘Yes, ndio maana nataka nisionekane, ndio maana
natakiwa sura yangu iwe ni adimu machoni mwa watu, nitakuwa sehemu nimejichimbia,
huko huko majuu, ukiwa na pesa huko unakaribishwa kwa mikono miwili,nitaona
jinsi gani ya kufanya.....’ akashika kichwa akiwaza, halafu akanyosha mikono
yake mbele na kusema;
‘Kwa hii- hii mikono yangu nitaweza kuyumbusha,
kunyoosha, kuelekeza, kuratibu,na kufanya lolote niwezalo,...kwa mikono yangu
hii hiii nitafanya dunia ya aina yangu,...ila ni muhimu nitumie pia mikono ya
watalamu wa dunia nzima, lakini wawe wakinifuata mimi...’akakohoa kidogo
‘Najua haya mambo ni hatari kidogo, nitatafutwa
sana, lakini mimi sitaonekani kirahisi, nitakuwa mbali na wao kukitokea tatizo,
lakini nitakuwa karibu na wao nikifanya vitu vyangu, nikivuna kile
nilichopanda, ni lazima niwe mtu wa aina
yake `invisible man’, hahaha.........’akacheka
sana, na baadaye akaiangalia ile picha ya dunia ikizungukwa na mikono, na
kusema.
‘Hii ndio dunia yangu....’
NB:
Hii ni nyongeza ya sehemu iliyopita, tutakuja kuona jinsi jamaa huyo alivyoweza
kukamilisha ndoto yake hiyo, ambayo ni sababu ya mambo mengi yanayotokea sasa
hivi kwenye hii dunia, fitina, ...
WAZO
LA LEO: Utajiri, na mali ni mtihani, watu wanaweza kutumia pesa zao na
mali zao kuwarubuni wengine, wakajenga fitina, wakapandikiza chuki, na kwa pupa
ya wanadamu wakachukulia kama inavyosemwa, kumbe ni malengo ya watu wenye nia
mbaya, wanaotumia mali na pesa zao vibaya au wanatumia mali kupata mali kwa
migongo ya watu wengine.
Muhimu tunaposikia jambo, au kukitokea tatizo, tusikurupuke na
kunyosheana kidole, tuweni makini, tuchunguze kwanza, tujiulizeni kwanini iwe
leo, mbona jana na juzi haikuwa hivyo. Fitina ni mbaya sana.
Ni mimi:
emu-three
No comments :
Post a Comment