Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, July 8, 2014

DUNIA YANGU-2





 Baada ya miaka kadhaa, maisha yakawa yamebadilika kabisa, utawala wa sheria , mila na utaratibu uliokubalika na jamii ukaanza kusahaulika, na maisha ya mjanja kupata yakashika hatamu, utawala usio na mipaka ukiongozwa na kijana Diamu ukaanza kuenea kwa kasi ....

Tuendelee na kisa chetu....

Ndani ya ofisi ile ile ambayo miaka kadhaa nyuma ilikuwa ikimilikiwa na mtawala anayeongozwa na sheria na katiba, sasa yupo kijana, mtanashati, akiwa na suti maridadi, akiwa kashikilia kitabu kidogo tu...

Alikiangalia kile kitabu, na akilini mwake, akamkumbuka baba yake mlezi, maana kumbe alikuwa na baba mzazi ambaye mama yake likuja kumuambia baadaye kuwa sio baba yake wa kumzaa, japokuwa hakutaka kusema  zaidi, yeye hakujali hayo, lakini baba yake mlezi ndiye aliyemuwezesha yote hayo hadi akafikia hapo, alipomuwaza baba yake mlezi hali fulani ya huzuni ikatanda kwenye moyo wake, akimkumbuka jinsi alivyomhangaikia, ....

‘Huyo keshaondoka na zama zake...’akajipa moyo na ile hali ya huzuni ikafutika, sasa akawa anakifungua kile kitabu chake, na kuanza kuangalia maajabu yaliyomo, hapo akatabsamu...na ila huzuni ya muda ikaondoka kabisa na kilichotawala nafsi yake kwa sasa ikawa ni tamaa, uchu, na hamasa ya kufanya jambo...

'Mara wazo lake likatanda akilini akawa analichanganua,wazo la siku nyingi, sasa kaliona linawezekana, na kwa muda huo huo, akawa akimuwaza mama yake ambaye kila mara akikitana naye haachi kumuasa, maneno ya mama yake yalimchochea kuwa sasa anatakiwa kufanya jambo, akakumbuka mama yake alivyosema;

‘Mwanangu sasa wewe ndio kila kitu, utajiri, utawala vyote vipo mikononi mwako, lakini haitoshi, sasa na wewe unatakiwa uwe mbunifu, utengeneze tofauti, watu waje kukuumbuka, sio tu kwa kuendeleze kile alichokuachia baba yako,lakini kiwe na manufaa kwako, na kwa watu wako,...lakini cha msingi, hakikisha unawajali sana wale waliowahi kudhulumiwa na huyo baba yako...’akasema mama  yake.

‘Nakuelewa sana mama, usiwe na wasiwasi wewe niachie hii kazi, na endelea na taratibu zako zingine, mimi najua ni nini cha kufanya, wewe utaona tu mama ni swala la muda...’akasema bosi huyo huku akigusa gusa mawani yake ya  bei mbaya machoni mwake, huku mama akimuangalia mtoto wake huyo kwa hamasa.

Nakukumbusha tu, usije ukazungukwa na hao watawala wenzako ukawajali wao tu, hakikisha fungu kubwa linakwenda kwenye milki ya damu yako, miliki ya kizazi upande wa mama yako, unielewe vyema hapo, nataka wazazi wangu huko walipo wasterehe...’akasema mama

Diamu aliyakumbuka maneno ya mama yake, huku akiendelea kukifungua kile kitabu na kwa upande mwingine akiwa anatafakari wazo lake, wazo ambalo limekuwa likimsumbua sana kichwani mwake, akakiweka kile kitabu mezani, na kukiangalia kwa makini, lakini kila akikiangalia alishangaa kuona sura ya baba yake ikimtawala akilini.

‘Kwanini huyu baba haniachi, ameshakuwa marehemu na zama yake imekwisha...’akasema huku bado akimkumbuka baba huyo ambaye siku kama hiyo wakiwa kwenye hiyo ofisi, baba yake huyo alimkabidhiwa hicho kijitabu.

Alipopewa, alijua ni kitabu tu na kwa muda hakupenda kusoma sana, na alisita kukipokea, baba yake akamwambia;

‘Pokea utawala wa baba yako, huuu ndio ufungua wa utawala wangu, ...’aliposikia hivyo akajikuta akinyosha mikono kwa hamasa, akikumbuka maneno ya mama yake;

‘Mwanangu ujaribu kuwa karibu sana na baba yako, kwani yeye ndiye mwenye ufungua wa kila kitu kuhusu utajiri wake, ipo siku atakua huo ufungua, basi na wewe utakuwa kama yeye...’

Alikipokea kile kitabu, na kwa nje kilionekana kama kitabu tu cha akwaida, kumbe ndani kuna mambo, ndani kulikuwa na computa ndogo ambayo ungeliweza kuandika, kuchukua picha, na yale yote yanayowezwa kufanywa na computa.

Hapo akaguna akiusiafia utaalamu uliotumika hapo, na moyoni akasema;

‘Mmh katika dunia hii kuna watu vichwa...ukiangalia kwa nje ni kitabu tu, kumbe ndani kuna mambo...hahaha, sasa nina ufungua wa utajiri, utajiri ulihangaikiwa na vizazi baada ya vizazi, sasa upo kwa wenyewe, kichaa kapewa rungu, hahahaha,  yote haya sasa yapo kwenye miliki yangu, diamu, mtoto wa shetani, hahaha.....’akasema kwa sauti kubwa huku akijizungusha kwenye kile kiti.

Akaafunua ukurasa wa kwanza, ilikuwa ni kama jalada gumu, au mfuniko wa hicho kitabu na sasa akawa anaangalia uso wa hicho kitabu, uso ambao unaonekana kama kurasa za kitabu, humo sehemu ya kwanza kuna utangulizi wa yote yaliyomo, na unachotakiwa kufanya ni kubuza kwa kidole, kama vile unafungua ukurasa, na kunatokea sehemu nyingine, bila ukurasa kufunuka kama inavyokuwa kitabu au ukachagua kwa namba.

Alipofunua ukurasa wa kwanza, akaona yaliyomo yanahusiana na mambo binafsi, au mambo ya kikazi, akaacha mambo ya kikazi, akafungua yale ya kibinafsi, na hapo akatakiwa kuweka neno la siri, akakumbuka neno aliloambiwa na baba yake, yeye alikuja kulibadili na kuweke neno jingine lililomjia  akilini, akaandia neno jipya, `dunia yangu...’ ule ukarasa ukafunguka, akaanza kusoma maelezo yaliyokuwepo, uso wake ukameta meta kwatabasamu

Akaanza kucheka, na kucheka, halafu akatulia ghafla kama vile kaambiwa tulia, na hapo fikira pana, zikaanza kumjia, akasema;

‘Mhh, hiki kijitabu ni zaidi ya urithi wote alioniachia baba, kutokana na hiki kitabu, nitabuni mambo yangu mwenyewe, mambo ambayo hayajawahi kufikiriwa kabla na hiki kizazi kilichopita, nataka kumuonyesha mama na wale wote wanaonizunguka kuwa mimi ni kichwa, zaidi ya vichwa vingi vya hii dunia...’akasema na kushika kichwa akitafakari kwa makini

‘Mimi nikitumia kichwa changu, nikichanganya na vichwa vingine vyenye kuona mbali kama mimi, nitaweza kufanya jambo kubwa sana, jambo kubwa zaidi ya ya majambo yote yaliyowahi kufanyika,...’akawa anaongea laafudhi ya kizungu, huku akifungua ukurasa baada ya ukurasa, na baadaye akafikia sehemu aliyoiandika yeye hivi karibuni, humo aliandika anuani mbalimbali na namba za simu

‘Kwanza  ni lazima niwasiliane na watu wangu, wa kwanza ni huyu rafiki yangu mkubwa  anayesoma Marekani, nafahamu na kila mtu anafahamu hivyo, kuwa huko ndiko kitovu cha ufundi na mambo mengi ninayoyataka mimi, huko kuna vichwa vimejificha, nataka kuvitumia, visipoteze muda wao bure....’akasema na akawa kama anawaza jambo , halafu baadaye akasema;

‘Huyu rafiki yangu tumetoka naye mbali, licha ya kuwa yeye alikwenda kusoma huko nje, lakini .....mmh, bado tupo pamoja, ni lazima nimuelezee wazo langu, sitaki apoteze muda wake huko , aje huku kwetu tufanye mambo, kwanza ni lazima nimuweka sawa...hahaha....’akacheka na kuanza kuipiga ile namba ya huyo rafiki yake, ikaita na badaye ikapokelewa, wakaanza kuongea, na baada ya maongezi mengine ya kawaida, akasema kwa sauti ya kikazi zaidi;

‘Rafiki yangu, mimi nina wazo kubwa sana, wazo kama lile nililowahi kukuambia wakati tupo shuleni,....’akasema

‘Yah, niambie, ..bado unaota kuwa mtawala, kuwa na nchi ya kufikirika...’akasema huyo rafiki yake..

‘Sio ya kufikirika tena..baba alipofariki wengi walijua familia yetu itayumba, lakini sivyo hivyo, nipo na nitaendelea kuwepo, nimekuja na zama mpya,...’akaanza kumuelezea mawazo yake, na alipomaliza mwenzake akamuambia;

‘Mhh, wewe kweli kichwa, nilijua tu ipo siku tutafanya jambo, maana naona kama upo na mimi kichwani, mimi mwenyewe nilikuwa na wazo kama hilo, na nimeshaongea na marafiki zangu wengine, tumekubaliana hilo, lakini tulishindwa sehemu, maana mambo bila pesa, huwezi kufanikiwa, tunaweza kuwa na mawazo mazuri, lakini kianzio, kimekuwa ni shida, sasa wewe una pesa,...unaona mambo yanavyojileta, sisi tuna akili, tukikaa pamoja tutaweza tukafanya jambo...’akaambiwa na huyo rafiki yake.

Waliongea kwa muda na kukubaliana kuwa sasa muda umefika wa kuanza kazi, na hapo akakifunika kile kitabu na kulaza kichwa chake kwenye hicho kiti, akabonyeza kitufe cha simu ya mezani, alitaka kujifaririji, na sauti ikatoka kwenye simu ya mezani, ni sauti ya kike ikauliza;

‘Bosi nikusaidie nini...’sauti tamu anaoyoipenda ikasikika ikiuliza

‘Kiburudisho...’ akatamka hivyo tu

**********

Wakati anasubiri kiburudisho chake, huku akiwa kaegemea kwenye hicho kiti chake cha enzi, akashikwa na kitu kama usingizi, na mara akili yake ikatekwa na taswira ya tukio lilitokea muda sasa, likionyesha siku ile baba yake alipofariki, hakupenda hayo mawazo yarudi akilini mwake tena, lakini yalikuja bila kutegemea ilikuwa kama njozi vile....

Akawa kama mtu aliyekumbushwa jambo la kutisha, na mwili ukaanza kumchemka kwa wasiwasi, mwili ukamlengea, akawa hawezi kujiinua, akabakia vile vile akiweweseka na akiwa katika ile hali, moyoni akasema kama kujitetea;

 ‘Mhh, haiwezekani ina maana mimi ndiye niliyemuua baba yangu mwenyewe, lakini sikumbuki kufanya hivyo, nakumbuka mimi nilikuwa kama nimelala na nilipofumbua macho nikajikuta nimeshika kisu, na hicho kisu kimejaa midamu...’akasema

‘Wewe ndiye umemuua...’sauti nyingine ikasema

‘Hapana...’akajitetea, na mara hali ile ikabadilika, lakini akiwa bado kwenye hiyo njozi, sasa alijiona yupo kitandani anawaza;

Alikuwa akiwaza tukio hilo, na huku moyoni na akilini akijutia, na kujisikia vibaya, akawa akijiona kama kweli yeye ndiye aliyemuua baba yake, japokuwa mama amekuwa akimwambia sio yeye, sasa kama sio yeye ni nani alifanya hivyo, mama yake anamwambia na shetani wa kuzimu

‘Kama ni mimi nilifanya hivyo, sizani kama nitaweza kusamehewa...’akasema kimoyo moyo

‘Hata hivyo kama ni mimi nilifanya hivyo, huenda nilifanya  kwasababu ya mama, huenda kuna kitu alinifanyia hivyo ili tendo hilo lifanyike, hapana, kwanini mama hakuwahi kuniambia kuwa ana mpango kama huo na hata lilivyotokea  pale mama hakuwepo, ...

‘Na kwanini inakuwa kama njozi, na kwa nini nisiweze kukumbuka kulifanya hilo jambo...hapana sijafanya mimi, japokuwa kuna muda nilikuwa namchukia sana baba yangu kutokana na suluba alizokuwa akinipa, kila kosa ni fimbo, adhabu na mihangaiko isyokuwa na mpangilio

Kuna muda hata yeye mwenyewe alitamani kumuwekea baba yake sumu, ili aachane na 
hayo mateso aliyokuwa akiyapata, eti ni jinsi ya kumkomoza,...hiyo haikuwa sahihi, kunikomoza ili iweje wakati utajiri upo, akawa kila akimuona baba yake anakosa raha kabisa, alikuwa akitamani baba yake asirudi huko anapokwenda kwenye shughuli zake.

 ‘Hata hivyo sikutaka mimi nimuue baba yangu...’akasema kwa huzuni na mara mwili ukapata nguvu tena, akajiona kama mtu aliyeshituka kutoka usingizini...macho yake yalipokaa sawa, akaangalia mlangoni, macho yake yakakutana na uso wa binti aliyekuwa kasimama huku kashika sinia, na kwenye sinia lile kuna gilasi na chupa iliyo na kinywaji...

‘Mhh, mrembo, umeingia saa ngapi?’ akauliza

‘Nimeingia kama dakika tano hivi, niliogopa kukushitua maana ulikuwa umelala, huku unaweweseka, unaongea maneno ya ajabu ajabu....’akasema

‘Maneno gani?’ akauliza

‘Oooh, naona ulikuwa kwenye dunia yako tena, maana ulikuwa kama mtu aliyelala, anaota, mara unasema sio mimi niliyemuaa baba yangu, oooh hivi ooh....’akasema huyo binti.

Aliposikia hayo Diamu akashika kichwa kwa muda na kumuangalia huyo binti, na kusema

‘Unajua nina kawaida ya kuota hivyo, hata mama yangu anasema tangu baba yangu afariki ndoto kama hiyo huwa inanitokea...sijui kwanini, ...’akasema

‘Ni kawaida, mtu akifiwa na mtu wake wa karibu hujiwa na manjozi ya ajabu ajabu, cha muhimu ni kujitahidi kuyasahau, baba yako alishakufa, na siku nyingi zimekwisha, iliyobakia ni wewe kupanga maisha yako ya mbele, sahau ya kale, haya chukua kiburudisho chako, au nikunyweshe....’akasema huyo mrembo..

‘Hahaha, ndio maana nakupenda wewe, nikiwa nawe kwenye hii ofisi nasahau dunia ya kufikirika, japokuwa sasa nataka iwe dunia ya kweli, sogea hapa mpenzi uninyweshe hicho kiburudisho....’akasema, na wakati huyo binti anasogea kuingia upande ule aliokaa bosi wake, mara jicho la huyo bosi likatua kwenye kisu kilichopo kwenye chombo, kisu kile bado kilikuwa na alama nyekundu, kama mabaki ya damu.

Alipokiona tu, akajikuta akishituka, na hata hamu ya kufanyiwa hayo aliyotakiwa kufanyiwa na huyo binti, yakaisha,..akasema kwa sauti ya kukwaruza;

‘Mhh, tafadhali mpendwa wewe weka hiki kinywaji hapa mezani na ondoka, akili yangu haipo sawa..’akasema na yule binti akiwa tayari keshajiandaa kufanya mambo yake, akasimama ghafla, na kumuangalia huyo jamaa kwa mshangao, akajiuliza huyu jamaa ana nini leo mbona sio kawaida yake, na kwanini anakiangalia kile kisu ndani ya kabati la kiyoo.

Yule binti kwa vile alishamfahamu huyo bosi wake, akisema jambo anataka litekelezwe mara moja,  akageuka na kuanza kuondoka kwa haraka, na jamaa akabakiwa akiwa anawaza , anawaza huku akikiangalia kile kisu, na kumbukumbu za habari za hizo kisu zikawa zinamjia akilini kama alivyohadithiwa na mama yake...

`Kisu ni hicho ni cha urithi,  ni cha kifamilia kinachorithiwa na mtoto maalumu wa kifamilia,  kisu hicho pamoja na kupewa, kama urithi wa kifamilia, lakini kina nguvu ya ajabu, kinaongeza nguvu mwilini, ukiwa nacho hakuna mtu anayeweza kukuzuru na unakuwa mwanaume kweli kweli....

‘Kisu hicho kiliasisiwa na kiongozi wa familia hiyo miaka mingi iliyopita, na kilitengenezwa na madini yanayopatikana baharini, wanadai madini hayo yalikusanywa na mashetani, wakaja kukiunda hicho hicho kisu, ni shetani aliyempenda binadamu, akampa na kumwambia hiyo ni zawadi yako, ukiwa nacho hiki kisu wanadamu wenzako hawataweza kukusumbua.

‘Lakini sharti kisu hiki kimilikiwe na watoto wa familia yako, sio vinginevyo...’aliambiwa huyo mtu wa kwanza kukabidhiwa hicho kisu, na kutokea hapo ikawa ni utaratibu, unaotoka kwa baba kwenda kwa mwana aliyempenda na kumteua ili awe mrithi wake...’ mama yake akamwambia.

Toka kisu hicho kilivyobuniwa, miaka zaidi ya mia mbili iliyopita hakijawahi kuonja damu, hadi kilivyofikia kwa mwana huyu ambaye upatikanaji wake na uhalali wake katika familia hii uliobakia siri ya mama mzazi.

Akiinua kinywaji chake akipendacho na kumeza mafundo kadhaa ili kuiondoa ile taswira kichwani mwake iliyomgubika ghafla, akasimama na kuiweka ile gilasi mezani na kwa mwendo wa kunyata, aliisogelea ile meza iliyopo mbele yake meza ambayo ina gilasi ya pembe nne, na ndani yake kuna kile kisu....akakiangalia kwa makini , halafu akageuka na kurudi pale kwenye kiti chake, akakaa na kutulia

Alitulia kwa muda, halafu akanyosha mkono wake, na kukishika kile kitabu, akakifungua, na akafunua ukurasa mpya ambao alishaanza kuandika mambo yake..

‘Hawa watu wanasema wana akili, lakini mimi nina akili zaidi yao, ngoja niwaonyeshe mimi nilivyo na akili zaidi yao,....’akasema,

Na hapo hapo akafungua ule ukurasa ambao alishaanza kuandika kwa kifupi jinsi dunia yake atakavyoitengeneza, alijua kabisa kuitengeneza dunia kama hiyo ilihitaji pesa nyingi zaidi, ilihitaji rasilimali watu na ilihitaji ujasiri, na pengine kumwaga damu. Akatikisa kichwa na kusema hivyo vyote sio tatizo, tatizo ni muda...akaandika mambo mengii tu yaliyomjia akilini, hadi ukurasa ule ukajaa.... 

Akafungua ukurasa wa pili na kuangalia kiasi cha pesa kilichopo benki, akaguna, kwani katika maisha yake yote hajawahi kufikiria kuwa baba yake aliweza kumiliki kiasi hicho cha pesa kwa ajili jamii yao, na nyingi tu kwa ajili ya familia yake ina maana hizo za familia yake ndio zipo mikononi mwake. Alipofungua ukurasa unaofuatia akabaki mdomo wazi, kumbe hata utawala wa siasa upo mikononi kwake...

‘Hahahaha Ina maana hata nguvu za kidola ...siasa, mmh, kumbe ndio maana mzee alikuwa kinyenyekewa, sasa nimezindukana, ....sasa nimepata wapi pa kuanzia, sasa ninaweza kukamlisha mipango yangu, sasa eeh, ninaweza kuendelea na ndoto yangu, ndoto ya kuunda kitu kikubwa duniani...hahahaha

NB: Huyu mtu anataka kuunda kitu gani


WAZO LA LEO: Urithi mnzuri kwa watoto ni elimu, elimu ni bora kuliko mali, kwani mali uliyoiahangaika miaka mingi, inaweza kufika kwa mtoto akashindwa jinsi ya kuiendeleza, ikaifisi na kuisha au mali hiyo hiyo ikampoteza mtoto wako mwenyewe,  akaifanyia mambo mabaya kuliko ulivyofikiria wewe. 

Ni mimi: emu-three


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Wewe mkali bro, najiuliza jinsi gani ulivyoweza kuweka hayo mawazo