Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Tuesday, July 1, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-85

                                

‘Muheshimiwa hakimu,...najua hii kesi ni ya mauaji, ambayo imekuwa na utata mwingi, na utata huo sio kuwa ni wa bahati mbaya, yote hiyo ni mipango, ilipangwa iwe hivyo, na imekuwa hivyo...’akatulia kidogo akisafisha koo.

‘Pia najua kila mtu anataka kujua ni kwanini, ni kwanini auwawe mtoza ushuru, japokuwa awali nimeshaelezea kwa muhutasari, basi  ..leo hii mimi nitawatajia kila kitu, tulieni, nipeni nafasi, na naomba pumzi isiniishie mapema, kabla sijamaliza kutaja ni nani alimuua mtoza ushuru, na ....hata huyu mlinzi wa mdada, ....’akawa anaongea kwa masikitiko..

‘Endelea mzee, akasema hakimu

‘Sawa muheshimiwa hakimu, nashukuru sana, nitajitahidi kadri ya uwezo na pumzi atakazonijali mungu kuliwakilisha hili kwenu,...’akasema na kutulia vizuri kwenye kile kiti chake...

‘Katika mikakati ya hilo kundi, kuna muda wakuu , waheshimiwa, wanajikuta wanapambana na matatizo ya mtu au kikundi ambazho kinawakwaza katika kufikia malengo yao....’akatulia kidogo

‘Basi wao wana kila mbinu, wamejipanga kwa lolote lile, wahusika wakuu wanapitisha azimio na kusema huyu sasa basi, huyu sasa ni kikwazo, tufanye nini, lakini pia kunakulindana, kuhakikisha mwenzetu hapatwi na madhara,kwahiyo kila mtu akiwa kwenye majukumu ya kikazi ni lazima kuwe na namna ya usalama wake, na hili ili liweze kufanikiwa, kuna idara maalumu ya kazi hii, wapo wataalamu waliobobea kuhakikisha kuwa usalama upo...

‘Wapo watu maalumu, muda wote wanatuangalia kila tunalolifanya...usione nimevaa hili kofia, na koti hili rafu, ukafikiri ni koti tu, ukafikiri ni nguo tu, usione watu wamevaa masuti ya namna fulani ukafikiri ni suti tu...hizo zote ni kinga za silaha za kujlinda,...’akasema na hakimu akawa anamuangalia kwa makini.

‘Muheshimiwa hakimu ukiwa umevaa hivi unakuwa na mlinzi nyuma yako, kuna watu wanakuona kila unapokwenda, wametuzunguka kila mahali, ...wakiona upo hatarini tu wanatokea watu wa kukusaidia, kuna watu wapo kila kona, sasa jiulize mwenyewe hao watu wamepatikana wapi, sio kundi la mchezo kama mnavyofikiria nyie..’akasema na watu wakageuka nyuma kuangalia

‘Msiangalie nyuma, maana hata mkiangalia nyuma hamtawaona, inawezekana hapo ulipokaa huyo aliyepo pembeni yake ni hao watu,...’aliposema hivyo watu wakawa wanaangaliana.

‘Huwezi kuwajua, anaweza akawa hata ni ndugu yako, mtoto wako mwenyewe, yupo kwenye kundi lakini ni siri kubwa ya kundi, hawezi kukuambia, ...lakini wapo hao watu wanatuangalia, wapo kwenye chumba maalumu cha siri, na mitambo yao, na chumba hicho sio cha kudumu, leo wapo hapa kesho wapo sehemu nyingine, kutegemeana na hali ya hewa...’akatulia akijinyosha kidogo.

‘Ila kwa vile nilishajua mbinu zao, nilishajua ni kitu gani nifanye, siku walipoanza kunihis vibaya, nikaharibu taratibu za mawasiliano zilizokuwepo kwenye hizi nguo, ...’akasema akionyeshea liel koti alilovaa,...

‘Kwahiyo toka siku nilipoharibu hiyo mitambo iliyounganishwa kwenye hizi nguo,wakawa hawanioni wakawa hawanipati, maana kwenye nguo hizi kuna nyuzi zimeungwanishwa na nyuzi hizo ni waya ndogo sana zinaweza kunasa matukio, sauti , na kuwezesha silaha isiweze kupenya..

'Ndio maana hawakujua wapi nilipokuwepo tokea waanze kunitafuta ili waniue, waulizeni  hao jamaa mliowakamata ,wanafahamu zaidi.....lakini kama nilivyosema wana mbinu nyingi na wana watu wengi, hata huko mahospitalini wana watu wao....’akasema na wale washitakiwa wakainamisha vichwa vyao, na hakimu akatupa jicho kuwaangalia, na machoni alionyesha hasira...

‘Najua nikitoka hapa watahakikisha sifiki huko ninapotakiwa kwenda, lakini hata hivyo, wameshachelewa...kwani yote nataka niyaweke hadharani hii leo...’akasema na kuwaangalia wale washitakiwa ambao muda mwingi walikuwa wameinamisha vichwa vyao chini.

‘Nimetimiza wajibu, na sitajutia kile nilichokifanya kwani yote nimeyafanya kwa ajili ya taifa langu, toka awali, na sasa pia, nimeamua kujitolea muhanga kwa ajili ya taifa langu, nikifa nakufa nikiwa nalitetea taifa langu....’akasema kwa sauti ya ukakamavu.

‘Ndio maana sasa nataka kuyaweka haya hadharani kabla siku yangu haijafika, maana kanuni ya kundi ukisaliti kundi adhabu yake ni kifo,..nilitakiwa kufa kwa sumu, lakini mungu amenisaidia nipata muda angalau kidogo, maana sumu hiyo haikwepeshi, najua inanitafuna ndani kwa ndani, na sijui ilikuwaje hata sumu hiyo ikashindwa kunimaliza mara moja, kwani sumu hiyo haikwepeshi, haichukui muda....’akasema

‘Huenda ni kwa sababu ya maombi yangu kwa mungu, kuwa angalau nipate muda kidogo wa kuja kuyasema haya, maana nimeyaona kwa macho yangu,na pia nikayafanyia kazi, japokuwa waliweza kuiba nyaraka zote muhimu...’akatulia kidogo

‘Lakini mimi ni mpigananji, mzoefu, sishindwi kirahisi, bado nina ushahidi ambao unaweza kuwafikisha wote wanaohusika mbele ya sheria kazi itabakia kwenu nyie mliopewa dhamana ya kuhakikisha kuwa sheria inatimiza wajibu wake, sijui, na inawezekana hata huku kwenye mahakama wapo watu wao.....’akasema mzee na hakimu akatabasamu.
Mzee akaonyesha hali ya kuchoka, na sauti ikawa inakwaruza, na hakimu akaliona hilo akasema;

‘Mzee naona umechoka,...tunaweza kuahirisha hili zoezi,ukaja kutoa ushahidi wako muhimu ukiwa na afya nzuri...’akasema hakimu na mzee akajitutumua na kisema;

‘Sijachoka, bado nahisi nina puumzi ya kutosha kumalizia sehemu hii muhimu, hili ninalotaka kulifanya hapa haliwezi kuahirisha…sina muda mwingine wa kuja kuyaongea haya, labda kama hamtaki kuyasikia yote, sizani kama nikitoka hapa nitaweza kurudi tena, sizani , na huenda hata nisiweze...’akasema mzee kwa shida na kuanza kukohoa mfululiozo, hakimu akaongea na mtu wake, nahisi alikuwa akimwambia dakitari aitwe.

Mzee hakujali, akajitutumua baada ya kutulia kidogo, akajinyosha kidogo, na kuvuta kitu kama kamba, kutoka kwenye koti lake, na mwisho wa ile kamba kukawa na kidude kidogo (flash disk)

‘Ushahidi wote upo hapa...’mzee akasema na kukiinua kile kidude juu,, kitufe kile kina uwezo mkubwa wa kuhifadhia kumbukumbu, ni kidogo sana, lakini kina uwezo wa kuweka kumbukumbu nyingi sana zikiwemo kumbukumbu za matukio ya picha na sinema..
Alikitoa na akageuka kumuangalia muendesha mashitaka na kusema;

‘Muheshimiwa hakimu namkabidhi huyu, mbele yako, naye atakukabidhi kwa himaya yako, sijui wenyewe mtakavyofanya, mimi nimetimiza wajibu wangu....’akasema

Na muendesha mashitaka akakipokea kile kidude, na kukiangalia kwa makini , halafu akamsogelea muheshimiwa hakimu, na hakimu naye akakiangalia kwa makini na kusema

‘Wataalamu wetu watakifanyia kazi..lakini kwa hali uliyo nayo mzee, naona ni bora upumzike kwanza,...’akasema hakimu

‘Natamani iwe hivyo muheshimiwa hakimu lakini ni bora nikamalizia sehemu iliyobakia, kwani sijui ....’akatulia kidogo, halafu akasema;

‘Nataka kuwaambia hili mnielewe, kuwa nikitoka hapa sitaweza kurudi, ila nawaambieni, hicho kidude kina kila kitu, kama mnataka haki itendeke vyema, basi fanyieni kazi hayo yaliyomo humo...najua inaweza kutokea pingamizi kwa wajanja, wakatoa hoja hizi na zile, lakini yote yanahitajika yawafikie wanancho wajue ukweli...’akassema

‘Humo mna kila ushahidi wa kundi, lini kundi lilipoanzishwa na wanachama wake wake wa awali, kuna mambo mengi wameyafanya, mauaji ya namna kwa namna...kuna siri za miradi mbali mbali,wanazoziendesha wao, kuna kumbukumbu za akunti za beni nje ya nchi, na pia mwishoni utaona inaonyesha jinsi siku mtoza ushuru alivyouwawa...’mzee sasa akaonekana kukosa nguvu

Yule askari akamsogelea na kumshikilia vyema, akamkagua mzee, na mzee alionekama kuzidiwa, lakini hakutaka kutulia kuongea, akawa hawezi hata kukaa vyema, ilibidi askari yule amshikilie vyema kwenye kiti, hata hivyo sauti yake , iliyokuwa ikiendelea kupungua nguvu ilisikika ikisema;

‘Nasikia mlinzi wa mdada kauwawa, wamefanya hivyo kwa vile walijua  anafahamu mengi, ni mtu aliyekuwa akinisaidia kazi zangu za hapa na pale, walijua huyo mlinzi anafahamu kuwa kulikuwa na hizo nyaraka kwa mdada, na kwa vile wanauhakia kuwa hizo nyaraka watazipata kwa mdada, waliona waondoe uzia kwa kumuua huyo mlinzi, nina uhakika aliyefanya hivyo ni wakili wake.

Mdada alipewa kazi maalumu na mtu wa kundi, mdada hakulijua hilo, yeye alijuwa kuwa huyo mtu ni mmoja wa watu waaminifu wa taifa, na siku nilipokutana na mdada kumuelezea hilo, hakuniamini, ila aliposikia kuwa siku ile mimi ndiye niliyemuokoa asiuwawe, alibakia mdomo wazi....

‘Sasa sijui huyu mdada yupo wapi, kama kawapelekea hawa watiu hizo nyaraka basi zimeshaharibiwa, ...mdada anamuamini sana bosi wake, akijua ni mtu mwema, kumbe ni wale wale, na huyo mtu akawa akimtumia mdada kwa masilahi ya kundi, ....mdada hakulifahamu hilo, kama wamemkamata, sijui kama atakua hai...’akasema

‘Ndugu zanguni, mliokamatwa, nawaombeni sana, jitakaseni, tubuni zambi zenu, hayo mnayoyatafuta hayatawasaidia lolote, angalieni waliokwisha tangulia, wapo wapi, kulikuwepo matajiri wenye kila aina ya sifa za utajiri, wapo wapi,...’akasema akiwaangalia wale washitakiwa.

‘Kulikuwa na, maraisi, wanaoweze kutibiwa kwa kila aina ya dawa, lakini wapo wapi, na wapo watu wa kila namna wenye uwezo wao, lakini utajiri wao, uwezo wao, sifa zao, hazikuwasaidia kitu, wamekufa, na wataendelea kufa, hebu jiulize, kuna mmoja aliondoka na utajiri wake,….je utajiri wao uliwasaidia nini…hakuna kitu,...’akasema

‘Nawaombeni sana, na kuwakumbusha kuwa utajiri, au mali utakayoenda nayo kaburini ni matendo yako mema kwa watu,  wahurumieni wanyonge, wahurumieni masikini, ambao wanataabika kutokana na dhuluma zenu, huruma hiyo ndiyo itakayowasaidia, ndiyo utakayokuja kwenda nayo siku yako ikifika…..’  hapo akatulia kidogo na akawa kama anavuta pumzi kujipa nguvu.

Mimi ndiye niliyemuua mtoza ushuru, kwa vile mtoza ushuru alitaka kumuua mdada…’alipoyasema haya maneno kwa sauti ya utulivu, kama vile alitaka kila mtu ayaskie, watu waliguna, na hata hakimu akaonyesha kushituka.

‘Ilikuwa hivi,...nilipofika pale kwa mdada, nikiwa na koti langu la ulinzi, na nilipanga nifike, nikisema nina jambo nafuatilia, japokuwa haikuwa safari rasimi,...

Nilipofika pale kwa mdada, nikiwa kiaskari zaidi, nilikutana na mlinzi naye mara moja akanitambua, nikampa maagizo, na yeye anajua ni kitu gani akifanye, maana nilishaonega anye kabla,...

‘Mlinzi akaenda kutekeleza kile nilichomuagiza, lakini muda ukawa umepita, kila kazi ina muda wake maalumu ukipita inabidi ufanay jambo jingine kwa haraka, mimi niaona nihakikishe, basi nikasogea kwenye jengo, kwanza nilichungulia dirishani kwa chombo maalumu,...mara nikamuona mtu akitoka mbio,

‘Yule mtu wakati anatoka, alikuwa akiondoa midevu kidevuni kwake, mwanzoni sikumtambua, lakinia lipoondoa zile ndevu ndio nikamtambua,...hata hivyo sikuwa na muda wa kumfuatilia..

‘Kipindi hicho nilikuwa nimezima mawasiliono yaliyopo kwenye koti na watu wetu wa usalama, kwahiyo nilikuwa nafanya yangu binafsi, nina kitu kama tocho unaweza kuangalia kupitia kwa dirisha la kiyoo lililowekewa, kizuizi cha kuona ndani, nikaweza kuona kinachoendelea kule ndani.

‘Muda ule nilipochungulia, ndio muda mdada kaanza kuishiwa nguvu, ile hali inayomtokea iliashaanza kupotea, na ikifikia hapo anakuwa hana nguvu anadondoka,...ukumbuke ili mlinzi aweze kufanya hiyo kazi, nilimpa maagizo kuwapoteza fahamu hao waliopo ndani...

‘Alishaniambia kuna silaha maalumu ataitumia, kuwapoteza fahamu hao watu, na kama malivyosikia alitumia nyundo, yeye ni mjuzi wa yote hayo, sikuwa na wasiwasi na hilo anajua amgonge wapi mtu ili apoteze fahamu...

‘Nilipoona mdada anapepesuka na yupo tayari kudondoka, nikageuka kumuangalia mtoza ushuru, mtoza ushuru, alikuwa anasimama, akiyumba yumba na nilimuona akiifuata silaha, iliyokuwa sakafuni...hapo nikaingiwa na mashaka, nakaona ni lazima nifanye jambo…

Nilielekea pale mlangoni, sikuwa na mashaka, kwani nilikwua nimevaa kinga, risasi haiwezi kupenya,...nilichotaka ni kumuwahi huyo jamaa kabla hajafanya analotaka kulifanya...

‘Siku moja kabla nilishamtuma mlinzi kuhakikisha kwa mdad hakuna silaha, ..kwahiyo nilikuwa na bastola ya mdada....’akasema na hakimu akawa kama anashangaa

‘Haya mambo yana mipangilio , japokuwa hili halikuwa mikononi mwa kundi, lakini mimi na mlinzi na baadhi ya watu wangu niliowaamini tulishalipangilia vyema..

Nilipofika pale mlangoni, nikiwa na silaha yangu tayari, mtoza ushuru naye alishasimama , sasa alikuwa kashika bastola akimlenga mdada..na ile hali niliyoiona kwa mtoza ushuru ilikuwa ni ya tayari kuua...akawa sasa anamuonyeshea mdada ile bastola kumlenga, akisema;

‘Bye bye mdada, sasa mwisho wako umefika….’ Akawa sasa anafyatua kiwambo, mimi ni askari nafahamu mtu anapofyatua kiwambo kidole kinakuwaje,...kwahiyo sikuwa na shaka nilijua kabisa huyu mtu anataka kuua,...’akatulia

‘Mimi  sikutaka mdada auwawe,..maana sikuwa na uhakika kama kweli mlinzi kazipata hizo nyaraka, hata hivyo, kwanini mdada auwawe, na auwawe akiwa hawezi kujitetea,. Akili akiniambia ni lazima nimuokoe huyu mtu , lakini pia sikutaka mtoza ushuru auwawe, maana huko mbele yeye ndiye anayeweza kujibu mashitaka yote, anafahamu kila kitu, anafahamu mengi kuliko mimi...’akatulia

‘Kwa muda huo ilitakiwa maamuzi ya haraka,…nikaona  nizuie hayo mauaji, nikamuwahi huyu mtoza ushuru...lengo ilikuwa kumpiga sehemu ya mikononi, ili kumvunja nguvu, lakini  haikuwezekana, nilijitahidi iwe hivyo,lakini haikuwezekana....kiukweli sikuwa na dhamira mbaya, na kumuua yeye iliniuma sana, nikamuwahi kabla hajamfyatulia mdada risasi…ilikuwa ni kitendo cha haraka sana….

Nilimuwahi kabla hajamuua mdada, hapo ilikuwa swala la muda, ama mdada auwawe, au .....kwani nilipompiga risasi, risasi yake ilitokaikawa imemkosa mdada hatua chache na kupiga ukutani,...nilipoona hivyo sikuwa na jingine, nikaondoka haraka na wakati huo mlinzi alishatoka, akanipa bahasha, kumbe mle ndani kulikuwa hakuna kitu ...

‘Vilivyokuwepo mle ndani na mapicha ya ovyo ovyo mengine ni mapicha yam dada aliyowahi kupiga na mkwe....ni mapicha mabaya yasiyofaa...hata sitaki hata kuyakumbuka...sitaki hata kuyaelezea niliyachoma moto.....

‘Kitu ambacho nilichokiona ni cha ajabu, na sijui kwanini askari hawakuelezea, ni ile risasi iliyopiga hewani ukutani,...risasi hiyo ilitoka kipindi namuwahi mtoza ushuru,... ukiangalia kwa makini kwa mdada utaona tundu la risasi eneo la ukutani, hiyo ni risasi iliyotakiwa kumuua mdada...pili risasi iliyomuua mtoza ushuru haikutoka kwenye bastola yake, japokuwa waliona mabaki ya risasi ya bastola ya mdada, lakini hili halikuongolewa...

‘Utaona jinsi mambo yalivyofichwa,...yaligeuzwa geuzwa, hata ripoti ya awali ya wachunguzi haikufika kwa muendesha mashitaka, iliyofika ni ripoti nyingine iliyopangwa kinamna...lakini yote yaliyotokea siku hiyo yapo kwenye hicho kidude, inaokenaka moja kwa moja jinsi ilivyotokea...

‘Kiukweli mimi sikuwa na lengo la kufanya hivyo, pia haikuwa lengo la kundi hilo haramu, kumuua mtoza ushuru,. Kifo cha mtoza ushuru ilikuwa ni pigo kwa kundi,  maana mtoza ushuru ni miongoni mwa viongozi wa kundi, waliokuwa wameandaliwa kushika hatamu, japokuwa kulikuwa na sintofahamu miongoni mwao,...

‘Naweza kusema mtoza ushuru alikufa kwa bahati mbaya, akiwa katika harakati za kuzipata hizo nyaraka za siri zilizoibiwa kwake, nyaraka ambazo mtoza ushuru aliniibia mimi, akiwa na lengo la kuokoa kundi......

‘Mimi nimetimiza wajibu wangu...sasa naichia kazi mahakama hii, uamuzi ni wenu, mimi ndiye muuaji wa mtoza ushuru kwa bahati mbaya katika harakati za kumuokoa mdada, mtaona wenyewe tukio lilivyotokea,....lakini...ooh,...oh, mmh, ......’akasita, na mzee alionekana akitoa jicho kama mtu aliyeona kitu cha kutisha.

Mara mzee akatulia kimiya…ilisikika sauti ya kukoroma….hakimu akaamurisha mzee asaidiwe, na akasisitiza apelekwe hospitalini na dakitari wake aitwe, wakutane njiani, akiwa anawahishwa hospitalini, lakini hali ya mzee ikawa mbaya zaidi,….mzee hakufika hata hospitalini, siku yake ikafika, akaiga dunia,…

                                        Mwisho
NB: Yaliyofuata baadaye...

Siri kubwa ya kundi haramu ilijulikana kutokana na ushahidi aliutoa mzee, na wahusika wengi walikamatwa japokuwa wengi walikimbilia nje. Mdada hakuonekana kabisa,...
Baada ya kipindi kupita, mchumba wangu ambaye hakutaka kabisa kuongea na mimi, na familia yao ikawa haitaki kabisa mawasiliano na mimi, hasa waliposikia kuhusu hayo mapicha aliyokuwa kayapiga mdada, baadaye mchumba wangu akaolewa na askari, aliyekuwa mlinzi wa karibu wa mzee

Nilijitahidi sana kumtafuta mdada, lakini sikuweza kumpata, hata familia yao haikujua wapi mdada alipo, na wao walisema wameshazoe hiyo hali, hadi leo ninapowaletea hiki kisa, haijulikani wapi mdada alipokwenda kama yupo hai, au aliuwawa na kundi.....
Mimi badaye nikamuoa mdogo wake mdada...

NAWASHUKURUNI SANA KWA KUWA NAMI TOKA MWANZO WA HIKI KISA, MIMI NIMETIMIZA WAJIBU WANGU KUFIKISHA KILE NILICHOONA KINAFAA KUFIKA KWAKO, HUENDA HAKIKUWA SAHIHI KWAKO,SAMAHANI KWA HILO...NA NAKUSHUKURU SANA KWA KUNIVUMILIA,...

 NA KWA WALE WALIOONA NIMEFANYA VYEMA, NAWASHUKURU SANA KWA KUIFURAHIA KAZI HII, TUPO PAMOJA. LAKINI SITAKUWA MWEMA WA FADHILA KAMA SITAMSHUKURU MLETAJI WA KISA HIKI , SEHEMU ZA SIMULIZI ZA BOSI, MUNGU AMZIDISHIE KWA WEMA WAKE HUO, NA TUTAZIDI KUWA NAYE HUKO MBELENI, MUNGU AKIPENDA...MWISHO WA KISA HIKI NDIO MWANZO WA KISA KINGINE.


WAZO LA LEO:Kiongozi wangu bora ni yule anayeweka masilahi ya watu wake mbele, akijua kuwa kapewa dhamana ya watu, na dhamana ya watu ni deni kwake. Kiongozi huyu hataweza kulala, kula vyema, au kuishi kifahari huku watu wake wanateseka kwa njaa, na umasikini uliokithiri. Je kiongozi huyu nitampata wapi, je kweli yupo...?

Ni mimi: emu-three

4 comments :

Yasinta Ngonyani said...

Hatimaye wamekamatwa.. Unafikiri mdada atakuwa wapi?....mmhhh mimi naona yupo hai sehemu ...Ahsante sana kwa kisa na kama ww mwandishi ulivyomshukuru mleta kisa basi nami namshukuru kimekuwa ni kisa cha mafunzo mengi sana. Najua kuna kisa kingine kinakuja:-)

emu-three said...

Nakushukuru sana ndugu wangu Yasinta, tupo sote kama kawaida yetu, na swali wapi mdada alipo, hata mm sijui, huenda atakuwa nasi akiwajibika. Mhh kweli kisa kingine kinakuja, ngoja tukiweke sawa . Tupo pamoja

Anonymous said...

Asante sana kwa kisa kizuri,twasubiri kisa kipya,vipi boss wa mhasibu aliishia wapi?na mumewe je?au boss naye alikuwa member wa kundi?

emu-three said...

Kisa kipya hicho kinaanza muda si mrefu, kuhusu bosi wa muhasibu, yeye atakuja na simulizi lake kabambe, tuwe pamoja tu. Yeye hakuwepo kwenye lile kundi haramu.