Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, June 30, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA -84


‘Ndugu muheshimiwa hakimu sitachukua muda wenu mrefu zaidi, nitakwenda harakaharaka ili niweze kufikisha kila nilichopanga kuwaambia, na inatakiwa niyafanye haya yote leo hii, maana ya kesho hatuyajui,maana ya baadaye mimi na nyie hatuyajui...’akasema mzee alipomuona hakimu akiangalia saa yake.

‘Nilianza kwa kuwauliza kuwa ni nani asiyependa maisha bora, jibu lipo wazi kila mmoja anapenda maisha bora, ...ndio maana viongozi wetu walipotuahidi hilo, tulifurahia na kuwaunga mkono, na ahadi hizo zipo kuwa kila mwananchi anatakiwa awe na maisha bora, ndio malengo ya kila mtu, na ndio malengo ya serikali, lakini je nadharia hiyo inatekelezeka...’akawa kama anauliza

‘Ni ndoto, mimi sijui maana sio mwanasiasa lakini kiukweli, naona ahadi hiyo ni nadharia tu, ....’akasema na kutulia

‘Nasema hivyo sio kwasababu sipendi kauli hiyo, sio kwasababu haiwezekani kabisa, ingeliwezekana, kama watu wenyewe wangelikuwa waadilifu, hasa wale waliopewa dhamana hiyo, dhamana ya kusimamia utekelezaji, tatizo kubwa ni ukosefu wa uadilifu, sio hapa tu, hilo ni tatizo la dunia nzima....

‘Niwape mfano rahisi je katika nyanja za kiserikali, ni watu gani wanaolipwa vizuri, tukianzia juu, utaona waheshimiwa wanalipwa vizuru tu, ukienda kwenye maidara yetu, huko kwa watoza ushuru, hawa watu wanalipwa vizuri tu, lengo la serikali ni kuwafanya hawa watu wawe nakipato kizuri, ili wakinai na tamaa, ili wasije kukengeuka, kwa kurubuniwa..’akatulia

‘Lakini wapiiii...wenyewe mnashuhudia, mkiangalia mfano wa mtoza ushuru na kundi lake,...nini walichokuwa wakifanya, walikuwa wakifanya madili yao ya pesa nyingi, pesa wanazotakiwa kulipwa hao watu sio pesa mchezo, ...angalia huo mafano kwa makini ndipo utaona kuwa kamwe binadamu hatosheki, hata umpe nini, milele hatarikika, leo umempa gari na nyumba, kesho atataka ndege..

‘Utampa nini binadamu atosheke, atajilinganisha na mataifa tajiri,kwanini sisi hatlupwi kama wao, kwanini, kwanini..bila kujali hali ya wanyonge,wavija jasho...watajilimbikizia kipato, na kipato....ilimradi awe juu ya wengine, huu ni ufisadi ulivuka mpaka, hii ni dhuluma, na wanaotenda hivyo, hata kama watafanya ibada, hata kama watajifanya wacah mungu, lakini kamwe hawatauona ufalme wa mbinguni....’akatulia

‘Katika utafiti wangu nililigundua hilo, kuwa kiongozi alitakiwa awekewe sheria kali sana, ili auogope hata huo uongozi,...ajue akikaa kwenye hicho kiti cha uongozi amekalia kaa la moto, angalau wangeliogopa...kama kila kiongozi akifanya kosa anawajibishwa mara moja, na pia mwananchi apewe mamlaka ya kumhoji huyu kiongozi kila mara...

‘Sasa je hawa raia wanaweza kuwahoji viongozi wao, thubutu, fanyeni haivyo kama hamtapigwa mabomu, fanyeni hivyo,kama hamtaozea jela...haya mnayaona sio kwamba nazua...sio kwamba ni uzee unanisumbua.....

‘Mimi kama mzee, nayasema haya kwa uchungu, maana niliingizwa huko kwa walaji, huko kwa wenzetu, kama una moyo wa huruma, utalia...watu hawa hawana imana kabisa na mungu, lakini wakiingia kwenye nyumba za ibada utafikiri wao ndio waumini wa hali ya juu,wanatoa mapesa tena kwa ria, kwa kujionyesha, na mara nyingi wanapendwa kutangazwa kwenye vyombo vya habari, ili waonekane wao ni watu wazuri..kumbe wanachotoa ni kile kile walichowaibieni nyie walala hoi...

‘Nilipopewa hiyo nafasi, na kuanza kunyonya asali kwa mrija, nilianza kujisahau...msishangae, ndio maana nikatangulia kuwauliza ni nani asiyependa maisha bora....ni nani asiyependa watoto wake wasome mashule ya bei mbaya, ..wakae kwenye nyumba nzuri,....angalieni hali ilivyo, mnaona ubaguzi huu ulivyokita mipaka, hata watoto wanafundishwa huu ubaguzi, kuwa wao ni bora kuliko akina Kayumba..

‘Mimi nami nikaanza kupata maisha mzuri, gari la bei mbaya , nyumba nzuri, na starehe zile nilizozikosa enzi hizo nikiwa kiongozi,  na mimi nikaanza kuonja matunda ya jasho la walala hoi, uzee ukanitoka, usisikie watu wakisema uzee mwisho wapi sijui, ndio misemo yao, uzee unakuja haraka kama huna pesa ukiwa na pesa uzee haupo bhana , na mimi nikawa kijana tena...’akatulia na watu wakacheka.

‘Kama nasema uwongo, tembeleeni sehemu za hawa watu, maana wana sehemu zao maalumu wanaingia kwa kulipia, mwanachama tu (members only), humo wazee, hauna mzee hapo wote vijana, watu wanakufuru na watoto wadogo,..makamo ya binti yake, anakuwa asali yake, honey, honey, binti yako honey, mkeo utamuita nani..ni, aibu , aibu, aibu...’akasema

‘Hakuna dhambi mbaya kama hiyo ya kudhulumu mali ya wanyonge, unafahamu ni wangapi wamekufa kwa dhuluma hiyo, ni wangapi wamekosa haki yao ya elimu, haki yao ya matibabu, kwa kunyang’anywa haki hiyo, watu wanakufa, wanapatwa na magonjwa mabaya, ...hilo hatulioni, ...wakiotokea wachache kutangazwa kuwa wanahitaji kutibiwa, oooh, wazee hawa, waheshimiwa, watajitokeza, kutoa misaada na kwa ria, kwa kujionyesha,na wanapendwa kuandikwa kwenye magazeti ukurasa wa kwanza, jamani hicho kinachotolewa ni jasho lenu...na hili nyoe mliopewa dhamana litakuja kuwahukumu....’akatulia

‘Nikaja siku moja nimeshapewa ofisi na kila kitu, yule kijana akanijia tena na kuniambia,;

Mzee umeonaeeh , haya ndio maisha, haya ndio maisha uliyokuwa ukiyakosa wakati ukiwa kiongozi,...kipindi hicho kilikuwa cha kuwabana viogozi,...sasa mambo yapo huria, ukiwa mjanja unakula mezani kwako,...’akaniambia na mimi sikuwa na kufanya hapo huyo kijana kwa vile ni bosi wangu ninamuita mzee..hahaha

‘Nikuambie ukweli ukiwa na maisha kama hayo hutapenda kuachia ngazi...hata hivyo wakiachia ngazi hawana wasiwasi maana wana vitega uchumi, angalia magorofa hayo, unafikiri yanatokana na nini, wakiwa kwenye madaraka, vitega uchumi hivyo vinapewa majina mengine, kuna mmliki bandia...wakiachia ngazi wanakuja wamilihi wenyewe wanaendelea kula nchi, wao wanasema pepo inaanzia hapa hapa duniani..’akaniambia huyo kijana

Sasa mzee hapo tulikuwa tunakuonjesha tu, sasa tunataka uanze kula bata...’akasema na mimi mate yakaanza kunitoka, nikauliza

‘Eeeh, mbona nimeshatosheka, hilo bata lipi tena...’nikasema na yeye akacheka kicheko cha pesa, unafahamu vicheko vya pesa, hawa watu utawajua hata wakicheka, vicheko vyao ni vizito, wanachekea kifuani, ha-ha-ha-ha...’akajaribu kucheke na watu nao wakacheka, hata hakimu naye akacheka.

‘Msicheke jamani, fungueni macho, fungueni masikio, na angalieni mbele, haya mnayataka nyie wenyewe, msije kuja kumlaumu mtu, msilaumu serikali yenu, maana serikali umeshaweka sera, utaratibu mnzuri tu, tatizo ni nyie, mliowachagua watu wabaya, na ukumbuke, serikali ni wewe na mimi, sio viongozi, na viongozi wanakuangalia wewe unavyotaka, yeye kazi yake ni kuhakikisha anashikilia usukani gari lisiyumbe, usipomuangalai vyema, anakengeuka,...’akasema mzee

Sasa mzee nimekuja kwako, najua kila mwezi unapeleka ile ripoti juu ya uchunguzi, kuhusu haya wanayolalamika watu,kuwa kuna ufisadi, kuna kundi haramu,.leleleeh, hiyo ndio kazi yako kuayaweka mambo sawa, sasa ili uweze kuipeleka vyema hiyo ripoti, ukiwa unajiamini, sisi tunataka kukupa cheo maalumu..’akasema na mimi nikawa najiuliza cheo gani tena, mzee kama mimi.

‘Oh, mimi tena, unafahamu nimesharizika, na umri huu sitaki kazi nyingi sana...’nikasema kwa kujivunga, huku akili yangu ikifikiria lile gorofa nililolianza kulijenga, ...jamani kuna pesa, nyie mnasema pesa hakuna,...pesa zipo, kama hazipo angalieni hawa wasanii, wanavyowekeza, wale wenye akili...siku mbili tatu humuwezi tena yeye anazungumzia mabilioni ya pesa, gari la kifahari, pesa inatoka wapi hiyo...’akatulia

‘Mimi nilipewa kazi ya kuchunguza sehemu zote zenye ulaji, nilitakuwa kuwachunguza wale wanaosimamia mapato, ushuru, na kila kitu,mali asili, huko kote nilitakiwa kuchunguza, sasa huko kote kulipandikizwa watu wao, ukifika huko unakutana na hao watu wao,wao wanajua, ukifika wanakuita pembeni, sio pembeni, kuna hoteli kubwa ya kifahari unatakiwa ukakae huko, huko, unakwenda fungate..na kila kituu kizuri sitaki kuvitaja mkaingiwa na tamaa, ukitoka hapo mwepesi, na zawadi juu....’akatulia na watu wakacheka, hata hakimu.

‘Zawadi ni zawadi kweli,....inauma sana, nikichungulia kwenye akili yangu nikavuta taswira za wagonjwa pale muhimbili, kule ocean road, wakiteseka kwa maumivu, nafikia hatua natoa machozi,..maana hizo zawadi, zingeliweza kuwasafirisha hawa watu wakaenda kupata matibabu mazuri tu...kusingelikuwa na shida, maisha bora kwa kila mtu yangelipatikana, kama ugawaji halali wa mapato ungelikuwepo, kama uadilifu wa viongozi ungelikuwepo, sera ni nzuri, ila watendaji hakuna....’akatulia

‘Nasema ukweli, sera ni nzuri sana, maelezo mazuri sana , mikakati mizuri sana, lakini watendaji wapo wapi, ndio hao hao mnawajua nyie, chunguzeni watu kabla hamjawachagua, hao watu mumesoma nao, manawafahamu udhaifu wao, na kiukweli udhaifu wa mtu huonekana zaidi pale akipata kipato, uongozi au wadhifa, hutaamini ni yule yule niyelikuwa nikihangaka naye, leo hii kawa hivi...

‘Ndio maana nasema  maisha bora kwa kila mtu ni nadharia isiyotekelezeka , ila ingeliwezekana, kama uadilifu ungelikuwepo....’akatulia kidogo

‘Sasa mzee, utakuwa kiongozi maalumu kwenye kundi letu,tuna chama chetu cha watu maalumu, unafahamu ili muweze kuishi kwa amani, muweze kufanya mambo yenu kisawasawa bila kubughudhiwa, tuliona tuanzishe kitu kama mshikamano, utaona hata huko mitaani wana vikundi vyao, inakubalika, basi na sisi hatukatazwi, ila sisi sio vile vikundi vya njaa kali, hapana vyetu ni vya shibe...vya kula bata, maisha nini...’akaniambia huyo kijana na kuniuliza lakini mimi sikuweza kumjibu,akaendelea kuniambia

‘Wewe una uzoefu, wewe upo katika mikakati ya kuhakikisha kuwa mali , miradi na sera zinakuwa katika msitari unastahiki, basi ukiwa kiongozi wetu, utajua jinsi gani ya kuelekeza, mambo yetu yawe wapi na mambo yao yawe wapi..tunakuwa tumemaliza, we waache wapige kelele weee, mwisho wa siku kelele zinakuja kwako,utajua jinsi gani ya kuziweka sawa,..huko huko kwenye kelele tunaweka watu wetu, wanakuwa ndio viongozi wao, wanajua jinsi gani ya kuwatuliza, hayo tumeshayaweka sawa, usiogope mzee, sisi vijana tutakulinda kwa nguvu zetu zote...’akaniambia

‘Sio siri, ukiwa kwenye kiyoyozi hutaweza tena kumjua mvuja jasho, ...huwezi tena kujua shida ilivyo,kwanza utamcheka yule anayelalamika, utamuona kama mtu asiye na muelekeo, utamzihaki kuwa hafanyi kazi , hasomi, kazi yake ni kulalamika tu..

‘Kikukweli niliona hayo malalamishi mengi kwenye meza yangu, na nilitakiwa kuyafanyia kazi, hawa wanalalamika kuhusu ubaguzi, hawa hawalipwi mishahara kwa wakati, hawa wanadai hiki au kile...yote hayo nilitakiwa kuyafuatilia, utayafuatilia saa ngapi na kila siku kuna semina ya kula bata...

Nikawa napeleka ripoti kwa mkubwa wangu nikionyesha malalamio ya watu na mkubwa wangu huyo ataipitia mwisho wa siku ataiweka pembeni na kuniambia,

'Hii ni kawaida, unafahamu mzee, imefika kwangu nitaifanyia kazi, wewe endelea na uchunguzi wako....

Unafahamu mzee hawa wote ni wavurugaji wa amani,...kwa vile huko tuna watu wetu, wao watajua jinsi gani ya kuwaziba midomo hao watu, unafahamu mzee kuna watu wana wivu, hawa dawa yao ni kuwapa kitu kidogo, wengine tunawavuta kwenye kundi, kidogo kidogo kundi linakuwa kubwa, wakileta ubishi, tuna magezeti yetu ya udaku, yanajua jinsi gani ya kuwaumbua, kote huko tumewekeza, wale wasiosikia tutawaweka ndani wataozea huko wakitoka hawamalizi mwaka, tunawapoteza......’nikaambiwa na huyo kijana.

‘Unajua kuna usemi usemao zimwi likujualo halikuli likakumaliza, mimi nimetoka kijijini, mimi nimekulia kwa wazazi masikini,...nimesomeshwa kwa shida, nimewaona wananchi wanavyoishi katika maisha ya dhiki,nimelitumikia taifa hili kipindi kigumu, tulifunga mikanda mpaka ikapitiliza, kipndi chetu kulikuwa hakuna mambo ya kifahari, leo hii ndio niwe msaliti wan chi yangu....hapana,japokuwa nilifikishwa kwenye ulaji, lakini moyoni nilikuwa naumia,...lakini kwa muda ule, ningelifanya nini, unayempelekea hiyo ripoti ni wale wale.....

‘Katika mikakati ya kundi, kuna watu wabishi, kuna watu huwezi kuwekwa sawa, lakini kwa namna fulani wanahitaji kutoa huduma kwenye kundi, ….wataalamu wa kundi walibuni njia ya kuwatumia mabinti wazuri,...hawa hawa mabinti zetu, jamani ni dhambi mnawarubuni watoto wa wenzenu, ili kuja kuwastarehesha, kuwafanyia machafu yenu,..inauma sana, mabinti hawa wanatumwa kwa lengo maalumu, kazi ni kuhakikisha kuwa hao watu wabishi wanaingia kwenye mitego yao,…..’akasema mzee

‘Mbinti hao na watu ,maalumu walitumiwa kutafuta kila mbinu kuhakikisha wananasa madhambi ya haoo wakaidi, waliweza kuwarubuni, wakawalewesha wakafanyiwa uchafu wa kila namna, uchafu ambao ukiwekwa hewani ni aibu kwao….na madhambi hayo yanatumwa kwa hao watu kuwa wasipofanya watakavyo kundi, wao watayaanika hayo madhambi hewani, ni lazima watakubali tu....kuna mikakati mingi tu, sitaweza kuitaja leo, kwani vile muda unakwenda mbio ...'akatulia kidogo

'Nafahamu ni nini nyote mnasubiria kusikia, na ndicho hasa kilichonileta hapa ....’akatulia

‘Muheshimiwa hakimu,...najua kesi hii ni ya mauaji, lakini pia ilikuwa ni muhimu kujua chanzo cha yaote haya, kwanini ikafikia mpaka watu wanauliwa ovyo, wanafungwa ovyo, ni kwanini, ..leo hii mimi nitawatajia kila kitu, tulieni, nipeni nafasi, na naomba pumzi isiniishie mapema, kabla sijamaliza kutaja ni nani alimuua mtoza ushuru, na ....hata huyu mlinzi wa mdada, ....’akawa anaongea kwa masikitiko...

‘Endelea mzee, akasema hakimu

NB: Nitaendelea sehemu hiyo muhimu sehemu ijayo, na huenda ikiwa ni sehemu ya mwisho , mungu akipenda. Kama  kuna maoni, kabla hatujafunga kisa hiki naomba nitumie, hapa au kwa e-mail...

WAZO LA LEO: Vyovyote tutakavyofanya, tukiwa na malengo ya kupata, lakini malengo hayo yakawa ya dhuluma, na dhuluma hiyo ikawa inamgusa mnyonge, masikini, watoto, mayatima, wasiojiweza tujue kuwa laana yake ni kubwa, na mipango hiyo hata kama itafanikiwa, mafanikio yake yatakuwa ni ya muda,..kamwe hutadumu nayo, na kama hakuna toba ya kweli, tujue mwisho wake utakuwa ni mbaya, kamwe dhuluma haina mwisho mwema.


BLOG YENU YA ‘’DIARY YANGU ‘’ INAWATAKIA FUNGA NJEMA YA MWEZI MTUKUFU WA RAMADHANI



Ni mimi: emu-three

No comments :