Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Wednesday, June 25, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-82


Kabla hakimu hajatoa kauli yake mara kukasikia vurumai upande ule wa mlangoni....

Hakimu aliposikia hizo vurugu, kwanza akawatizama walinzi, ambao na wao sasa walikuwa wakiangalia nini kinachoendelea huko maeneo ya mlangoni...na bila kitoa kauli na hakimu naye akageuza kichwa kutizama upande huo wa mlangoni..

Na kwa muda huo karibu watu wote waliokuwepo pale mbele na wao walielekeza macho yao huko kunapotokea sauti za kusukumana, na mnong’ono na manung’uniko ya watu,...hakimu akajaribu kuangalia vyema ili kujua ni nini kinachotokea,

Kwangu mimi niliyekuwa nimekaa kwenye mabenchi ya hapo mahakamani, sikuweza kuona vyema , na ilibidi nifanye kazi ya ziada kujigeuza, hata pale nilipojigeuza haikusaidia kitu, sikuweza kuona ni kitu gani kinachoendelea,kwani kwa nyuma yangu kulikuwa na watu, ambao kwa hamasa zao, walifikia kusimama ili kutizima vyema upande huo

Watu walijaa, na wengi wa upande huo wa nyuma walikuwa wamesimama, na kuziba mlango kabisa, kwahiyo kama ni mtu anaingia inabidi kusukamana na watu waliojazana hapo mlangoni ili aweze kupita, na uzuzri wake ni kuwa mashahidi wanaoingia walikuwa wakitumia mlango wa mbele, ambao haruhusiwi mtu mwingine kupitia mlango huo zaidi ya wahusika....

Nikawa na mimi najitahidi kufanya uchunguzi wa macho wa kutaka kujua kuna nini kinachoendelea, na uzalendo ukanishinda na mimi nikasimama, .....

      Tuendelee na kisa chetu

          ***********
Na mimi kwa hamasa sasa nikasimama, na kwa muda ule, haikuwa na haja ya mimi kusimama tena, kwani, ilikuja kugundulikana kuwa kumbe kuna mtu alikuwa akitaka kupita, na sio kupita tu, bali alitaka kwende mbele kabisa...na wakati najiuliza huyo mtu ana umhimu gani, mara kukapitishwa kigari, vile vya wagonjwa vya kukokotwa, na ndani yake kakaa mtu.

Nilijitahidi kumtizama kuwa ni mtu gani, lakini haikuwa kazi rahisi, kwani wenzangu walishasimama na kuanza kumtizama huyo mtu, na hapo nikawa nimebanwa, na sikuweza hata kupata nafasi ya kumuangalia vyema huyo mtu akawa keshapitishwa kuelekea mbele, nikasema kimoyo moyo, huko mbele sasa nitamuona vyema.

Ilivyojionyesha ni kuwa huyo mtu alikuwa na matatizo, au mgonjwa, hakuweza kutembea mwenyewe , alikuwa kakaa kwenye kiti cha hicho kigari cha kukokotwa na mkono na nyuma yake yupo askari, akimuendesha kuelekea mbele.

‘Askari ndiye anaye muendesha,...!’ nikajiuliza kwa mshangao, na kujitahidi sasa kumchunguza yule mtu,lakini haikuwa kazi rahisi.

Hakuna aliyeweza kumuona sura ya yule mtu, na hili liliwafanya watu wazidi kuhangaika kutafuta upenyo wa kuiona sura yake, lakini haikuwezekana kabisa na kwa hali hiyo vurugu zikazidi, watu wakawa wanasukumama, na walinzi wakawa na kazi ya ziada kuwarudisha watu nyuma.

Na hakimu kuona hivyo, akasema kwa sauti ya ukali ;

 ‘Ni nani huyo anayevuruga utaratibu wa kimahakama kwani kuna umuhimu gani wa huyo mtu kupita huku mbele, na kwanini, walinzi mnamruhusu huyo...’hakimu hakuweza kumalizia maneno yake kwani huyo mtu alikuwa ameshafikishwa pale mbele, na alikuwa katika upeo wa macho yake, kwanza alipigwa na butwaa, kama vile kaona kitu cha ajabu halafu akasema;

‘Utulivu, nataka utulivu, vinginevyo wote tutawatoa nje,...’akasema hakimu, na muda huo yule alishafikishwa pale mbele, wanaposimama mawakili, na alikuwa kati ya upande wa watetezi na washitakiwa, na mimi hapo sasa nikapata nafasi ya kumuangalia huyo mtu vyema, japokuwa haikuwa rahisi kumuona sura yake, kwani alikuwa amenipa mgongo.

Huyo mtu alikuwa amevaa koti refu, koti hilo lilikuwa limeshuka hadi miguuni, na kwa vile alikuwa amekaa kwenye hicho kigari cha kusukumwa, usingeliweza hata kujua urefu wake, na kofia pana lilikuwa kichwani mwake, nikashangaa kwanini anaingia mahakamani na kofia kama lile, na isitoshe, ilionekana kama kavaa mawani, sikuwaweza kuona hayo mawani ni ya ukubwa gani, lakini niliona vile vishikio vya miwani vikijitokeza kwa nyuma.

Nikasikia mtu akisema nyuma yangu;

‘Huyu ni nani, mbona anaingia mahakama kama vile ni yake, halafu angalia alivyovalia, kofia pana kama la macowboy,..inaonekana ama anaficha sura yake,....?’ akauliza

‘Labda ni mgonjwa hatakiwi kupata mwanga wowote ule, maana alivyovaa hilo kofia, na miwani makubwa ni lazima kuna sababu kubwa, na huoni anaendeshwa na polisi, sio mtu wa kawaida huyo, atakuwa muheshimiwa fulani...’akasema mwingine

‘Hapo kuna jambo ngoja tusubiri tuone...’akasema mwingine na sauti ya hakimu ikasikika ikisema kwa hasira

‘Hebu niambieni maana yake ni nini?’ akauliza hakimu kwa hasira akimuangalia yule askari aliyekuwa nyuma ya huyo mtu,  na kabla yule askari hajasema neno au walinzi wa pale ndani hawajamvaa huyo mtu,wakili muendesha mashitaka, akamsogelea yule mtu na kuwa kama anamkagua, na yule mtu akainua kichwa taratibu, kumtizama huyo wakili na taratibu akawa anajiinua kwenye kile kiti, kutaka kusimama

‘Mzee, kama huwezi kusimama usihangaike....’sauti ya yule askari aliyekuwa nyuma yake ikasema, lakini yule mtu hakujali hayo akasimama , japokuwa ilionekana ni kwa shida, lakini alijitahidi hadi akawa kasimama, na taratibu akainua mkono wake, hadi kichwani na kulitoa lile kofia lake, na taratibu akatoa mawani yake..

Yule wakili aliyekuwa karibu yake akaonyesha mshangao, na kuhema kama mtu aliyekuwa akipandisha mlima, na hakimu naye ambaye sasa aliweza kumuona huyo mtu vyema, akasema;

‘Mzee....’akasema hakimu kwa mshangao, na nilimuona wakili muendesha mashitaka akizidi kumkodolea macho huyu mtu waliyekuwa wakimuita kwa jina la mzee, ni kweli alionekana ni mzee, japokuwa kichwani hakuwa na nywele zenye kuonyesha mvi, nikatmtupia jichoa mpelelezi aliyekuwa bado pale mbele akisubiri kuendelea na maelezo yake, nilishangaa kumuona akitabasamu na kuonyesha alama ya ushindi.

Watu wakawa wananongonezana na mnong’ono wa watu wengi hugeuka kuwa kishindo, basi hakimu akiwa kazindukana kwenye mshangao akasema;

‘Hebu tulieni....’akasema akigonga kirungu chake mezani, na watu wlipotulia, akawageukia watu waliope mbele yake na kuuliza

‘Nyie watu hebu niambieni hii maana yake ni nini, mnavuruga utaratibu wa mahakama, walinzi kwanini hili linafanyika na nyie hamuchukui hatu sitahiki, hebu niembieni mara moja maana ya haya yote ni nini...’akasema hakimu

Yule mtu ambaye walimtambulisha kama mzee, akakohoa kusafisha koo, na mimi nilitaka hata kusimama ili niweze kumuona huyo mzee ni mzee gani, akilini sikuwa na mawazo ya mtu yoyote yule,

‘Samahani sana muheshimiwa hakimu, kwa kukuingilia kwenye himaya yako, najua nimevunja sheria na utaratibu wa kimahakama, lakini sikuwa na njia nyingine, maana ukiwa katika hali kama hii, unawindwa kama swala anayetafutwa kwa kitoweo, unakuwa huna njia nyingina bali ni kukimbia hata kama huko unakokimbilia kuna hatari zaidi...’sauti ya huyo mzee, ikasikika, ikisema ni sauti iliyoonyesha kuchoka, lakini bado ilijitahidi kutoka kwa ukakamavu fulani

Nilijaribu kujiuliza sauti kama hiyo niliwahi kuiskia wapi, lakini akili yangu haikuweza kutambua , nilikuwa nimefungwa kabisa, nikawa naombea huyo mtu ageuke, angalau tumuone sura yake.

‘Mimi ni mzee wenu, nimeitumikia hii nchi hii zaidi ya wote mliopo humu ndani, hata hao wazee wa baraza mliokuwepo humu ndani, hakuna anayenifikia mimi, na sizani kama nitakosea pia kwa kusema, hata katika kazi mimi nimefanya kazi zaidi ya wote nyie, kujitolea kujituma,..na hata kujitolea mhanga kwa ajili ya taifa hili..’akasema

‘Muheshimiwa hakimu,nakuomba sna univumilie, kwani haya nitakayoyaongea yatakurahisishia kazi yao na huenda leo ikawa mwisho wa yote....kama mtakubaliana na mimi, na hata msipokubaliana na mimi lakini ukweli utakuwa umedhihiri....’akasema na hakimu bado alikuwa kwenye mshangao, akawa katulia kimiya

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, leo nikiwa kitandani, nikiwa kuzimu, ...maana hali niliyokuwa nayo nilikuwa mfu, na nahisi hata madakitari walikuwa wakisubiria kuondoa zile mashile za 
kusaidia pumulia, maana sikuwa na dalili za uhai, nahis ilikuwa hivyo....’akasema

Nikiwa mfu, maana siwezi kuelezea kwa namna nyingine hali niliyokuwa nayo, au nisema nikiwa nasubiria umauti, huko kwenye kusubiria, ambapo ilikuwa kama mtu aliyekuwa kwenye njozi, ....nilijiwa na mtu mwenye sura nisiyoweza kuielezea hapa...’akatulia na mahakama nzima ilikuwa imetulia kimia.

‘Mtu huyo aliniambia, je nipo tayari kuiacha dunia, nikamwambia yote ni mapenzi ya mungu, kama muda umefika mimi nitasema nini,...

Akaniuliza, je nikipewa muda angalau mchache nitafanya nini?’ akaniuliza na mimi kwaa kili ya haraka, kama vile nilishapanga kusema hivyo nikamjibu

‘Mimi nikipewa muda angalau mchache, nitakwenda kutubu dhambi zangu zote mbele ya mahakama, ili nife nikiwa sina kosa, ili nife nikijua kuwa haki imetendeka,na ili nife kukiwa hakuna kinyongo kwenye nyoyo za watu, ili nife kukiwa hakuna udaku, maana dunia sasa inatawaliwa na udaku, propoganda...’ 

'Wakati nayasema haya nilikuwa kama mtu aliyefumba macho, nilipoyafumbua, nilijikuta nimezindukana, nipo hai, nipo kwenye dunia ya kweli, yule mtu hayupo, na akili haipo tena huko kwenye dunia ya kuzimu, na cha ajabu, nilihisi nguvu za ajabu, nikaweza kujiinua kitandani na hata kusimama, na sio kusimama tu, balai hata kutembea kama mtu aliyekuwa mzima...

‘Nilisimama na kuanza kutembea , na kwa muda huo humo ndani kulikuwa hakuna mtu, sikuamini, nilikaa pale kwa muda, nikaona nachelewa nikatoka nje, na mtu niliyekutana naye wa kwanza alikuwa mlinzi.

Ndugu muheshimiwa hakimu, sio kwamba nayazungumza haya kuwapotezea muda, ila nataka muwe na uwoni wa yaliyonikuta. Yule mlinzi aliniangalia huku kapanua macho ya uwoga, akiwa haamini , na mara akasogea nyuma kutaka kukimbia.

Na haikupita dakika moja wakaja walinzi wengine, na wao waliponiona , walifanya hivyo hivyo, kapanua macho ya kushangaa, na kushikwa na bumbuwazi, hawakuamini, ilivyoonyesha ni kama vile wamemuona mnzuka, mimi nikatabasamu tu na sikusema neno, ila moyoni niliwaza sana...

‘Niliwaza jinsi sisi wanadamu tulivyo,ina mana kweli, kumbe binadamu mnzuri ni yule aliyekufa, ina maana hawa watu ambao nahisi muda mchache uliopita walikuwa wakilia, wakiomboleza, wakionyesha kusikitika, wakionyesha mapenzi yao kwangu, walifanya hivyo kwa vile waliona kuwa nimeshakufa,...lakini sasa nipo hai mbele yao, sasa wananikimbia, wananiogopa, ajabu kabisa...

‘Kati ya wale askari, alikuwepo kijana mmoja, huyu ambaye nipo naye hapa, kweli nimuamini,...huyu kijana ni jasiri, yeye hakuonyesha dalili ya kuogopa, wakati wenzake wanaonyesha wasiwasi, yeye alibakia vile vile, na ndiye aliyeweza kunisogelea na kuniuliza;

‘Mzee vipi mbona umetoka mwenyewe, nikusaidie nini, unahitaji nini..?’ akaniuliza na wenzangu wakawa kama wanamshangaa, na mimi nikamwambia;

‘’Nataka kufika mahakamani haraka, na huenda sina muda wa kupoteza, sijui nimepewa muda gani wa kusubiria, ...naomba unipeleke huko haraka iwezekanavyo, ukinichelewesha wewe ndiye utakayebeba lawama zote...’nikambia huyu kijana, na nashukuru mungu alinielewa

‘Huyu kicheo ni mtu mdogo hana mamlaka, asingeliweza kuniruhusu kuondoka, hapo bila kibali cha wakubwa zake, na niliona huo mlolongo utakuwa mrefu, na wakubwa zake wanaweza wasimruhusu, wakijua mimi ni mgonjwa na huenda nimechanganyikiwa...

‘Cha ajabu kabisa huyu kijana hakusubiri amri za wakubwa zake, alikubali moja kwa moja, akaingiwa na nguvu na kujiamini, akasema;

‘Mzee mimi nipo tayari kukusaidia kwa vyovyote utakavyo,...’akaniambia, basi mimi nikamwambia,

‘Huko ndano kuna koti langu refu, niliwaagiza waniletee, nahis lipo kwenye mfuko, niletee, pamoja na kofia na mawani yangu...’nikamwambia

Hilo koti nililihitajia sana, kuna muda nikiwa hapo hospitalini nikipambana na umauti, kuna muda nipata fahamu, na kitu nilichokumbuka kuwaambia ilikuwa hilo, kuwa, mtu akija aje na koti langu, kofia yake na mawani, hata sijui kwanini niliwaagiza hivyo vitu mwanzoni, kumbe ni zile hisia kuwa kitu kama hicho nitakihitajia...mungu alishapanga kwua itakuwa hivyo.

‘Nimekuja na vazi hili, ili uwe ni ushaidi niliotaka kuja nao hapa mahakamani, ili kuondoa duku duku lenu, maana hata nilipofika hapa nilisikia mkiulizana, kuhusu huyo mtu aliyefika kwa mdada, na kumtuma mlinzi kwenda ndani kwa mdada, ...kama mnavyoniona, ndivyo ilivyokuwa siku ile, nilikuwa nimevaa hivi hivi....’akasema na sasa akageuka kujionyesha kwa watu,...

‘Oh, ni mzee, ni baba mkwe...’nikajikuta nikisema nilipoweza kumuona sura yake.
Pale nilipokaa, nikajikuta moyo wangu ukienda mbio, nikakumbuka maelezo ya mpelelezi, alipokuwa akimuelezea huyo mtu aliyefika pale kwa mdada akiwa kavalia hivyo, na hata mpelelezi hakuweza kumgundua siku hiyo, kumbe ni huyu mzee.

‘Sasa kama ni huyu mzee, basi ina maana anahusika na hilo kundi, kama ni huyu mzee, basi ina maana walikula njama za pamoja za kumuua mtoza ushuru, oh, mzee sasa yupo matatani, kwanini alifanya hivyo...’nikawa najiuliza

‘Natumai sasa mumeniona kuonyesha kuwa mimi siku ile ndiye niliyefika kwa mdada, nikamuagiza mlinzi kwenda ndani kwa mdada, kunichukulia vitu muhimu sana, vitu ambavyo nilivihangaika miaka mingi na ndio ushahidi wangu mkubwa niliouhitajia kwa akzi niliyoagizwa kuifanya. Lakini ushahidi huo ukaibiwa na kupotea,...ila baadaye ikagundulikana kuwa ushahidi huo alikuwa nao mtoza ushuru.....’akasema

Niliwahi kuongea na mtoza ushuru, nilipomuuliza hakukubali kabisa, na hata nilipofanya uchunguzi wa kina sikuweza kugundua wapi huo ushahidi ulipokuwa, kwahiyo ikawa kazi zote nilizofanya zikawa zimepotea...hata hivyo sikukata tamaa,,...baadaye nikaja kugundua kuwa hizo nyaraka muhimu zenye ushahidi mkubwa zimechukuliwa na mdada

‘Mdada nilishazoeana naye,...nikaona kumba itakuwa rahisi, nikajaribu kumuuliza mdada, lakini ...’akatulia kidogo, akionyesha kuhitajia maji...akaletewa maji, na kabla hajanywa, yule askari nyuma yake, akayakagua na kuchukua chombo kingine akanywa kidogo, baadaye alipomaliza kunywa, akaendelea kusema;

‘Mdada hakukubali kabisa,...lakini nilijua kama hizo nyaraka anazo yeye ni lazima nitazipata ni swala la muda tu...sasa siku ile niliposikia kuwa kapagawa, ..kashikwa na hayo wanayoita mashetani , nikaona ni wakati muafaka wa kulifuatilia hilo , na kuhakikisha nimeupata huo ushahidi...nilijua ni kazi ngumu, hasa kwa mtu kama huyo ambaye nasikia akipandisha anakuwa kama faru aliyejeruhiwa,lakini mimi nilishajipanga....

‘Mlinzi wa mdada alikuwa mmoja wa watu wangu,...’akasema na kukatokea mnong’ono kwa watu...

‘Mimi na mlinzi tulijuana siku nyingi, na nilipopaat hiyo kazi, nilijaribu sana kuwakumbuka watu niliowahi kuwajua ambao ni wachapakazi wazuri, huyo mlinzi ni mmoja wa wachapakazi wazuri, na ana kipaji...

Niliposikia kuwa mdada anatafuta mlinzi wa kuaminika, mimi ndiye niliyempendekeza huyo mlinzi na mdada akamkubali, lakini mdada hakulijua hilo,kuwa huyo ni mtu wangu, kwahiyo mimi na mlinzi tukawa tunawasiliana na kunipa habari ni kitu gani kinachoendelea kwenye maisha ya mdada...

Mlinzi ni mtaalamu wa ufundi, anajua mambo mengi, na aliweza kuingia mara kwa mara kwa mdada kutafuta hizo nyaraka, na ikaja kugundulikana kuwa nyaraka hizo zipo kwenye safe yake maalumu, kuifunua kwake, ni shughuli...tukatafura safe kama hiyo, na huyo mlinzi akaifanyia kazi, na kujua jinsi gani ya kuivunja, kwahiyo hata nilipomtuma kuingia pale, alijua jinsi gani ya kufanya....’

Alipofika hapo akatulia kidogo, na kumuangalia hakimu akasema;

Nitawaelezea kiuwazi zaidi jinsi gani niliyafanya haya yote, na kwanini nilifanya hivyo, ila sasa nataka nikae kwenye kiti changu, je naweza kuendelea muheshimiwa hakimu, ...?’ akauliza na hakimu akawa katulia,

Hakimu alitizama saa yake, halafu akamgeukia muendesha mashitaka, halafu akamuangalia mpelelezi ambaye alikuwa bado kasimama kwenye kizimba cha kutolea ushahidi, baadaye akasema;

‘Huu sio utaratibu, lakini kwa vile umeanza kutoa maelezo, na kwa ahli uliyotuambia, tunafiki hatua ambayo siipendi...’akasema hakimu kwa sauti nzito, na yule mzee akasema;.

‘Kama nilivyosema muheshimiwa hakimu, nayafanya haya kutokana na hali, sina uhakika,...sijui nimepewa muda gani wa kulitekeleza hili, ni bora msikie ukweli wote, ili baadaye muwe na maamuzi ya haki katika kesi yenu...ni kwa manufaa ya kesi hii...’akasema

Hakimu alitulia kidogo, baadaye aliwaita mawakili wote wafike pale mbele ili watete jambo, huku mahakama yote ikiwa kimiyaa...

Je itakuwaje.....


WAZO LA LEO: Kuna watu kwa namna moja au nyingine wamepatwa na matatizo, au wamekosea jambo, na watu hao kwa vile wamekosea, au kupatwa na hasara , wanataka na wengine wakutwe na mikasa kama hiyo hiyo...huu sio uungwana.

 Mwenye imani sahihi ya dini, ni yule aliyekuwa tayari,kutoa kile alichokipenda kwa mwenzake, ni yule aliyekuwa tayari kuona mwenzake anapata jema, anapata masilahi, kabla yeye hajapata, kuhurumiana na kupendana ...
Ni mimi: emu-three

No comments :