Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, June 17, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-78


Kama ilivyotarajiwa mahakamani kulijaa watu wengi, lakini sio kama ilivyokuwa kwenye siku ya kesi liyopita, siku hiyo kwa walio wengi ilionekana siku hiyo kama hitimisho, japokuwa mshitakiwa mkuu wa mauaji alikuwa hayupo.

 Watu wengine waliofika siku ile, siku ya kesi iliyopita waliogopa kufika leo,wakikumbuka tukio lililotokea siku ile, na wengine wapya wakajitokeza ili na wao wamuone huyo mdada, aliyeweza kuwafukuza watu wote mahaamani, ...

‘Huyo mdada yupo wapi ,mbona mimi sijamuona, mimi nimekuja kwa ajili yake tu,.....’akasema mtu mmoja

‘Wewe usiseme hayo, tuombe mungu isitokee tena kama siku ile, maana siku hiyo sitaisahau unaniona na unene wangu huo, lakini siku ile nilikimbia ,  karibu nivunjike mbavu maana nilikwenda nikagonga kwenye mti, kwa vile nilikuwa nakimbua huku nageuka nyuma kuangalia nyuma kuhakikisha kuwa kweli huyo mdada hajanifuata mimi.

‘Hahahaha, ama kweli nyie watu waoga, ina maana mnaogopa mashetani, mimi siogopi kamwe, ningelikuwepo ningemsomea akatulia, unayakaripia hayo madude hali inatulia, tatizo nyie mnakimbilia kuogopa..’akasema na mara kukatokea kitu kimedondoka, yule yule aliyekuwa akimcheka mwenzake kuwa ni muoga, ndiye aliyekuwa wa kwanza kutaka kukimbia

‘Oh, ni mjuzi kadondoka toka juu ya paa, unakimbia nini sasa, wewe si umesema huogopi kitu...’akasema mwenzake

‘Yaani mawazo yangu yalishakwenda huko mbali nikajua huyo mdada kafika kaanza purukushani lake, nikawa napiga mahesabu ya kuwahi mlangoni....lakini siogopi...’akasema

Ndio hali ilivokuwa kwa siku hiyo mwenye mwana abebe mbereko na asiye na mwana aeleke jiwe, muda wa mahakama ukafika, wahusika kila mtu kwa nafasi yake, na sehemu ya washitakiwa kuliokena watu wameongezeka, sio mtu mmoja tu, ni zaidi ya sita,na wengi wao ni watu mashuhuri tu, waheshimiwa..

Hakimu alifika, na kesi hiyo ikatajwa kwa mujibu wa utaratibu, na mwendesha mashitaka akaanza kutoa maelezo;

‘Japokuwa mtuhumiwa wetu namba moja hayupo, ameuwawa, lakini katika kesi hiyo, kama tulivyowahi kusema awali, kuna watu wengine walioshirikiana naye, japokuwa sio moja kwa moja...’akasema

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, kesi hii inagubikwa na kundi haramu , lililojijengea utawala haramu na kujipanga kinamna,...kama tutakavyokuja kuelezea hapa..’akaendelea kutoa maelezo marefu na mwisho hakimu akauliza

‘Tuna kesi ya mauaji, je kutokana na maelezo yako, inaonyesha hiyo ni kesi nyingine, na washitakiwa wengine..’akasema hakimu

‘Hapana muheshimiwa hakimu, kesi ni hiyo hiyo, ila wahusika wameongezeka, na chanzo cha mauji hayo kinatokana na hawa wahusika, kwa pamoja, waliandaa mbinu ya kuhalalisha taratibu zao, wakapandikiza watu kila idara, ili tu waweze kufanikisha malengo yao wakiwa na lengo la kutengeneza dunia yao haramu kwa mikono yao..

‘Katika wahusika hao, kila mmoja alitakiwa kukubali amri moja, na kama yupo mwanachama atakayesaliti,baada ya kujiunga, alipatikana na adhabu ya kifo, kama tutakavyokuja kuelezea kwa ushahidi, na leo tuna shahidi wetu ambaye aliweza kulibaini hili, baada ya kufanya uchunguzi wa kina, tutaonyesha hayo hatua kwa hatua,...’akasema

Mawakili wa utetezi walikuwa wengi, na kila mmoja alikuwa na hamu ya kutoa pingamizi lakini kwa vile hakimu alikuwa akihojiana na muendesha mashitaka, wao ikawabidi wakae kimiya.

‘Mshitakiwa mkuu ameuwawa, na hiyo ni kesi nyingine, je kuuwawa kwake kunahusiana na hili kundi?’ akauliza hakimu.

‘Ndio muheshimiwa hakimu, kama nilivyosema, katika kundi hili waliweka sheria, kuwa ukijiunga, hutakiwi kutoka, au hata kama hujajiunga lakini wao kwa namna moja au nyingine, wamakupa kazi yao, na ukaonekana kujua,...au kukiuka yale waliyokuagiza, wanakuua,..japokuwa mlinzi aliyuwawa, hakuwa ndani ya kundi moja kwa moja, lakini yeye alitumiwa na kundi bila hata yeye kujijiua...’akasema

‘Haya tusipoteze muda, tuanze ....unasema utamsimamisha shahidi wako, aitwe ili tuanze, na upande wa utetezi mpo tayari...?’ akauliza

‘Tupo tayari muheshimiwa hakimu, ila tuna pingamizi kuwa mshitakiwa mkuu hayupo, na ameuwawa, ina maana kesi yake haipo , hatuwezi kumshitaki marehemu, sisi tulitaraji isomwe kesi nyingine, kuhusu wateja wetu hawa, ambao wamesingiziwa mambo ambayo hawayajui kabisa,...’akasema na hakimu akageuka kumuangalia muendesha mashitaka, ambaye alisimama akasema;

‘Katika kesi hiyo, tuliainisha awali kuwa kuna wahusika wengine, ambao walikuwa hawajakamatwa kutokana na sababu mbalimbali, na sasa ndio hawa wamekamatwa, kwahiyo kesi ni ile ile, nab ado wapo wengine, kama orodha itakavyokuja kukabidhiwa mahakama hii tukufu, wapo wameshakimbia, lakini mkono wa sheria ni mrafu....’akasema muendesha mashitaka, kukatokea ubishani wa kitaalamu hadi hakimu akaingilia kati

‘Mimi naona kesi ni hiyo hiyo tuendelee, kama itaonekana ni kesi mpya, hatutasita kuliangalia hilo, lakini kama ni kundi ambalo limejumuika kwa pamoja na wao wakawa wahusika waliosababisha kifo cha marehemu, kesi ni hiyo hiyo..tuendelee na kesi yetu, shahidi aitwe...’akasema hakimu, na shahidi akaitwa

Wakati shahidi huyo anatoka kutoka chumba cha mashahidi, mimi nilikuwa nimekaa mle ndani ya mahakama, sikuwa nimeambiwa nikae chumba cha mashahidi nikajua kuwa mimi sitaitwa kama shahidi, kama nilivyokuwa nimejua hivyo...

Nilihangaika kuangalia huku na kule kuwa labda ninaweza kumuona mdada, lakini hakukuwa na dalili yake, ilionyesha wazi kuwa binti huyu kashikiliwa kama alivyosema mpelelezi, au huenda sasa ni maiti...nikakumbuka mazungumzo yangu na huyo mpelelezi.

***********

Kikao changu na mpelelezi kilinifunua akili, na hata baada ya hicho kikao, nilianza kuogopa kila mtu, nilikujua sasa nipo hatarani zaidi ya nilivyokuwa nawazia,....sasa nilianza kuogopa kuwa wakati wote naweza kuuwawa...

Kikao changu na mpelelezi kilionekana ni kikao cha kunilazimisha niongee kila kitu ninachokifahamu kuhusu mdada, sikuweza kukwepa, na ilinibdii niongee hata yale aliyonikataza mdada, sikuwa na jinsi....

‘Leo nataka uniambie kila kitu, kuhusu mdada, jinsi mlivyojuana naye na yote aliyokutendea, na jinsi gani mlivyoweza kushirikiana ....’akasema

‘Lakini mkuu, nilishakuelezea kila kitu mengine ni maswala binafsi, hivi wewe unaweza kuelezea mambo yako na mkeo, au na ...?’ nikamuuliza

‘Usikwepe swali, hata hivyo huyo sio mke wako, mimi nafahamu mambo gani ni ya siri na mambo gani sio ya siri, sijasema uelezee mambo yenu ya mapenzi, natake unielezee mambo ambayo yanamgusa mdada katika shughuli zake, ...cha muhimu ni ukweli, huna jinsi nyingine, hapa unacheza na muda, na ni hatari usipoweka wazi...’akasema

‘Ok, mimi na mdada tulikutana kazini, na kutokana na ucheshi wake tukazoeana,kiukweli nilipomuona kwa mara ya kwanza tu moyo wangu ulishituka sana, sijui ....lakini ndio hivyo,mapenzi labda...’nikatulia na mpelelezi akawa kimiya

‘Mdada alianza kunizoesha mambo ambayo mimi sikuwa na tabia nayo kabla, ujana damu inachemka, nikavutika kirahisi tu...., kwake yeye alisema ananitoa ushamba, akanishawishi hadi nikaanza kulewa, nilifikia hatua nikawa mlevi kweli....lakini siwezi kumlaumu kwa hilo, kipindi hicho nilikuwa na matatizo mengine binafsi...’nikasema kama kumtetea mdada

‘Mdada akaanza kunifundisha jinsi ya kupata pesa, kwa njia nisizozipenda, kama nilivyokuambia kuwa kipindi hicho nilikua na matatizo binafsi na moja ya tatizo hilo ni kukwama kipesa, nilihitajika nijijenga haraka, ili niweze kumuona mchumba wangu ambaye kwa muda huo alikuwa na mtoto, mshahara wangu hakuweza hilo, japokuwa nilikuwa najua baadaye kwa muajiri wangu huyo ningeweza kupata maendeleo, lakini swala la muda, likanikwaza.

‘Kutokana na shinikizo la wazazi wa binti, nilitakiwa niwajibike, ...nionyeshe kuwa kweli, nitaweza kumlea huyo binti na mtoto wake kama nilivyoahidi, kwahiyo nilijituma, nikawa silali, na kila simu iliyotoka huko nyumbani, ilikuwa ikinitishia amani....wanakuwa kama wananishinikiza niwe tajiri wa haraka haraka, kitu ambacho sio rahisi...

‘Alivyotokea mdada na mapendekezo yake hayo, sikuweza kuyakubali moja kwa moja, maana mimi ni muoga sana kwa wizi, lakini kwa hali iliyokuwepo, niliona kama mtu aliyekuja kunikoa...’nikasema

‘Tamaa za pupa zikanijia japo kwa tahadhari, kwani kazi yangu ilikuwa inanihukumu, kwahiyo japokuwa moyo uliona huenda, nikafanikiwa , huenda na mimi naweza kukubali,hata hivyo mimi sikufanya, yaani sikukubali, mdada ndiye aliyefanya kila kitu..’nikasema kwa kujihamu na kujitetea.

‘Mdada ndiye aliyebuni stakabadhi za uwongo,hadi akafanikiwa kupata pesa nyingi tu, na kunigawia, na mimi sikuwa na jinsi nikazikubali, na kuanza kujijenga, angalau nikawa nimejionyesha kijijini kuwa naweza kummudu mtoto wa watu...

‘Jambo moja likazaa jingine, nikawa mfuasi wa mdada, japokuwa nilikuwa naumia sana moyoni, japokuwa nilikuwa sipendi, lakini kila alilolitaka mdada nikawa nalifanya, nikikataa yeye ananitishia kuwa atayaelezea machafu yangu kwa baba mkwe, kwa...’nikatulia

‘Machafu gani hayo...?’ akauliza mpelelezi na hapo akanifanya nianze kuhisi uwoga na wasiwasi, maana mambo kama haya sikutaka kabisa yaje kujulikana, lakini sikuwa na jinsi

‘Mdada aliwahi kuchukua picha za uchi, alinilewesha na kuweza kuchukua picha kama hizo kwa nia ya kunilazimisha ili nifanya kila anachokitaka yeye, kwahiyo ikawa ndio fimbo ya kunichapia kila nilipotaka kukataa...

‘Je hayo uliyafanya kwa sababu ya kutaka utajiri, au kwasababu ya mapenzi au kwasababu ya hivyo vitisho?’ akauliza

‘Mhh, siwezi kusema moja kwa moja kuwa ni kwasababu hii au ile, ila kila aliponilazimsiah mdada, sikuweza kupinga,...ilionekana kama kanijaza kitu kwenye ubongo wangu na kuwa goigoi..sikujielewa kabisa, labda ni kwa vile nilimpenda, labda..ni vitisho, hata sielewi...’nikasema

‘Je  kwenye mauaji ya mtoza ushuru, mdada ndiye aliyakufundisha kuvaa ndevu,akakuambia ufanye hivi na vile,...maana bado nahisi kuna mengi hujaniambia kuhusiana na kadhia hiyo..?’ akaniuliza

‘Ni kweli yeye ndiye aliyenilekeza kila kitu,...akanivalisha hizo ndevu, ..na hata siku ile niliyokuita kuwa nina ushahidi waliokuwa wakiutafuta polisi, yeye ndiye aliyenibadili na kunifanua nionekane kama mwanamke, na ndio nikaweza kuufikisha ule mzigo pale nilipokuelekeza...’nikasema na mpelelezi akawa kama anawaza jambo.

‘Kwa maelezo hayo, nahisi mdada, ...mmh, okey nimeelewa, na hadi sasa hujafahamu wapi mdada alipoelekea?’ akaniuliza baada ya kutoa maelezo mengi aliyoyahitajia

‘Kwakweli sifahamu nimeonana na mdogo wake, na hata mdogo wake hafahamu wapi alipoelekea mdada, naona kama kakimbia nchi...’nikasema

‘Hawezi kufanya hivyo...tutampata tu, ...’akasema mpelelezi huku akiwaza jambo, baaadaye akaniuliza

‘Wewe na mzee, mlikuja kuongea na kukubaliana baadaye?’ akaniuliza

‘Hapana, ...maongezi yetu na mzee baada ya kuanza kuumwa yamekuwa kwa kupitia watu waliosema wametumwa na yeye na kwa bahati mbaya kila nikifika kwake, nakutana na shangazi, shangazi ambaye hatuivani kabisa...’nikasema

‘Kwenye nyumba uliyokuwa umepanga, yule mwenye nyumba, unamfahamu vyema?’ akaniuliza

‘Namfahamu tu kama mwenye nyumba , kwani ana nini?’ nikamuuliza

‘Hili kundi lina mbinu sana, kila mahali wana watu wao, wewe ulianza kutayarishwa toka upo huko kijijini,...lakini kama chambo, sio kuingizwa ndani ya kundi moja kwa moja,na pale ulipofanya hayo machafu kwa huyo mzee, ikaonekana huo ndio wakati muafaka, unaweza sasa kuwekwa kwenye ndoana,

‘Wewe ulipokuja hapa mjini ukiwa umetuma maombi yako, wenzako walishajipanga, utafikia wapi, utaajiriwa wapi na utakutana na nani, lakini hujijua, kwasababu wewe ni chambo tu, na hukutakiwa ufahamu lolote,....’akasema

‘Haiwezekani...’nikasema

‘Hata nyumba hiyo, uliyopanga ilishapangiliwa , mle kulikuwa na vifaa maalumu, na mwenye nyumba, alikuwa mlinzi wa kukuchunguza...’akasema

‘Sio kweli...’nikasema

‘Huyo mzee hakutakiwa kulala,..yule ni askari aliyefukuzwa kwa makosa ya jinai, walimfunga baadaye akaachiwa kwa msamaha,baadaye watu hao wakamfuata na kumuweka kwenye kazi maalumu, hata hivyo, hata yeye hajui kuwa yupo kwenye kundi hilo haramu, anatumiwa tu...na yeye atakuwa mmoja wa mashahidi,...tumeficha mahali, maana akionekana atauwawa.....’akasema

‘Mhh, kumbe.....’nikasema

‘Hukuona huyo mzee, akikufuatilia, yeye alitakiwa kila ukitoka awe nyuma yako, alikuwa akijibadili kinamna, leo anavaa hivi kesho hivi, na usingeliweza kumtambua, na alipokuona na mdada, akashituka, akapeleka taarifa, akaambiwa mdada hata tatizo yeye aendelee na kazi yake..’akasema

‘Ohh...mbona sikuwahi kumuona yeye akiongea na mdada...’nikasema

‘Mzee alikuwa na kazi yake maalumu, na mdada alipewa kazi yake tofauti, lakini wao hawakujua wanafanya kazi kwenye kundi, mdada ni mjanja, alikuja kugundua kuwa huenda alivyotegemea sio, yeye alihisi labda anafanya kazi ya usalama wa taifa..kumbe yeye ni chamabo wa kundi, kama ulivyokuwa mlindi na wewe ulishaanza kuingizwa kinamna, kama chambo...’akasema mpelelezi

‘Mbona sielewi kwa vipi?’ nikauliza

‘Yote utayapata huko mahakamani,ila mengi hyawezi kuwekwa wazi kwa sasa, sipendi siasa, siasa imeingizwa hapo, na hutaamini, tangu mwanzo nimekuwa na kazi kubwa sana ya kuwashawishi hao watu,lakini wao walitaka hili tatizo lizimwe kia-ina...’akasema

‘Oh, kwanini....?’ nikauliza

‘Kwanini, wewe huoni, kila mahali watu wao wapo, ni nani asiyehusika, huwezi kujua, na masilahi ya watu yapo mbele...hakuna mwenye huruma tena na jamii, wachache wanaojitia kipaumbele, wanakuja kupewa kitu kidogo, wananyamaza, angalia mangapi yanafanyika sasa, ambayo yanaathiri jamii, hali ngumu za uchumi, vitu vinapandishwa bei ....’akatulia

‘Wapangaji bei ni nani...ni hao hao wenye masilahi yao, ...sio rahisi kupambana na hili kundi ndio maana siasa inaingizwa, na sijui...mimi nitatizmia wajibu wangu, halafu nitakaa pembeni, nione ni hatua gani itachukuliwa...’akasema

‘Wewe huogopi kufa...?’ nikamuuliza

‘Kufa kila mtu atakufa,..kifo hakiogopi kwa namna hiyo,...na mimi nimejifunza kazi za kifo, kazi zetu ni kifo muda wowote, kwahiyo hata uogope vipi, ipo siku utakufa kwa sababu unapambana na watu waliodhamiria kuua....’akasema

‘Oh, mimi sipendi kabisa kazi zenu...’nikasema

‘Na ndio maana wamekuchukua kama chambo tu...sasa kesho mimi.nikimaliza kutoa ushahidi wangu, wewe na mdada, na baba mwenye nyumba wako mnaweza kuitwa kutoa ushahid kuthibistiha haya niliyoyaelezea, nina ushahidi wa kila namna, lakini huenda, watakawataka kuthibitisha, japokuwa kiusalama inaweza isiwe hivyo....cha muhimu kwa sasa ni kuhakikisha kuwamdada yupo hai au wameshamuua...’akasema

‘Una maana gani, umajuaje hayo, umewasiliana na mdada?’ nikauliza maswali mengi kwa mkupuo

‘Mdada ametekwa nyara,hilo halijathibistishwa rasmi, lakini kama walivyo na watu wao kwenye watu wetu, hata sisi tuna watu wetu kwenye kundi lao, ila watu wetu hawajawa na uhakika wapi mdada alipofichwa, walimkamata wakati anapeleka ushahidi wake kwa mtu aliyemtuma, lakini akiwa njiani akashituka, sijui kwa vipi, alihisi huyo mtu anayempelekea sio mtu wa usalama kama alivyokuwa akijua awali,..’akasema

‘Mdada alipogundua hilo, akataka kuficha kila kitu, lakini huyo mtu wake, akamshitukia, kwani alipofika huko alimuambia huyo mtu kuwa ushahidi aliokuwa nao umeibiwa...’akasema

‘Mhh, mungu wangu, atakuwa salama kweli...?’ nikauliza nikianza kujiona msaliti...

‘Mwanzoni nilijua labda ni mbinu za mdada, maana kundi hili lina mbinu nyingi tu...lakini baadaye tulipofuatilia na watu wangu wa ndani ya hilo kundi, tulikuja kugundua ukweli..kiujumla  mdada yupo matatani, wamemshitukia kuwa ana sura mbili...

 ‘Unasema nini?’ nikasema kwa hamaki, maana niliona kama mpelelezi anataka mdada afe,

‘Kundi hilo kama walikuchukua kama mtu wao, wakaja kugundua kuwa umewasaliti wanakupoteza kabisa,....wanaweza kukupoteza kinamna, wana mbinu za kila namna...’akasema

 ‘Mbinu gani?’ nikauliza

‘Ni za kijasusi zaidi, ina maana mdada akitoka hapo salama, inabidi apate dakitari wa hali ya juu kumchunguza...ni tatizo kwakweli,...’akasema

‘Sasa...?’ nikauliza

‘Tangu mwanzo nimekuwa nikiwataka munieleze ukweli, lakini imekuwa ni kazi ngumu sana kupata ukweli, nilipogundua hilo..ikanibidi nitumie njia za zaida...unafahamu haya tunawakanya sana watu, kuwa wasiingiwe na tamaa ya kujiunga na makundi haya yenye mlengo wa kimataifa,...lakini wengi kwa tamaa zao wanahisi ni kitu rahisi tu, wataingia na kutajirika, sio rahisi hivyo, kwao ukiingia ni lazima uwe na faida kwao....’akasema

‘Lakini mdada ni mtu aliyealimika, sizani kama aliingia kichwa kichwa kwa kurubuniwa....na mimi nimekuwa nikimuamini sana anaweza kujilinda...’nikasema

‘Wewe unazungumzia elimu yetu ya hapa hapa, hao watu ,sio watu wa elimu ndogo, ni lazima kwanza uwe na akili ya ziada, hiyo ndio sifa ya kuingizwa kwenye kundi lao. Katika uchunguzi wangu, nilikuja kugundua kuwa wote waliopo kwenye hilo kundi wana kipaji, wana elimu, na akili zao ni zile akili za hali ya juu (IQ),...

'Sasa mtu kama mdada, ana kipaji hicho, lakini kwa vile hakuwa nao mapemda, na walitaka kumtumia kijuu-juu bila kujijua, huenda baadaye wangelimuingiza ndani zaidi, na walipogundua kuwa mdada kaweza kuchukua nyaraka zao muhimu, wakaanza kumuandama, na mdada akajaribu kuwazidi ujanja,kama asipo wapa hivyo vitu watamtesa sana, na ni lazima tavitoa tu mateso yao ni hali ya juu...’akasema

‘Sasa nyie watu wa usalama mumefanya nini cha kumsaidia mdada...?’ nikauliza

‘Sisi kama watu wa usalama, bado tunamtafuta hatujui wapi alikofichwa, ni kazi nzito kidogo ikizingatiwa kuwa hawa watu ni watu hatari na wanajua ni nini wanachokifanya, hawasiti kutoa roho ya mtu...’akatulia aliposikia ujumbe wa simu ukiingia kwenye simu yake, akausoma, halafu akanigeukia na kuniambia;

‘Tutakutana mahakamani, uwe makini...kuna walinzi watakuwa wanahakikisha usalama wako, ...sasa hivi sitaki kupoteza mashahidi wengine, wewe na mdada ni watu muhimu kwangu, mtakuwa mashahidi wangu wakubwa, ila usije kuongea na mtu yoyote kuhusiana na haya niliyokuambia, huwezi kujua ni nani unayemuambia....’akasema.

‘Lakini mdada ni mmoja wa washitakiwa, kutokana na maelezo yako, na kama ulivyosema, huenda yeye anahusika na hilo kundi au nimekosea...?’nikamuuliza

‘Kama alivyo mdada, ni kama ulivyo wewe, mdada na ujanja wake hakujua kuwa anatumiwa na hilo kundi, watu hao walikuja kumsoma mdada, wakagundua kuwa ana ujasiri, ana kipaji, lakini pia ana hasira za kisasi kwa madhila aliyokutana nayo,wakatumia udhaifu wake,wakatumia matatizo yake, kwa manufaa yao  ...’akatulia kidogo

‘Na kwa jinsi walivyojipanga, hata dakitari aliyekuwa akimtibia mdada ni mtu wao, huyo dakitari ni mmoja wa kundi hilo wa kimiya kimiya....unaona hapo, siwezi kukuelezea kila kitu mengi utayasikia mahakamani...’akasema akionyesha wasiwasi

‘Oh, hata dakitari wake...!’nikasema kwa mshangao na yeye akatabasamu na kusema;

‘Mpaka sasa dakitari wake hajafahamu kuwa keshagundulikana, labda aje kuambiwa na watu wao walipandikizwa ndani ya kundi letu, hata hivyo mimi sijamwambia mtu mwingine, zaidi ya vijana wangu ninaowaamini sana, ambao wananifanyia kazi zangu...

‘Mmm, mbona hatari, kwa hali kama hii utamuamini nani...’nikasema

‘Nimekuwa nikimfuatilia sana huyu dakitari, kwa jinsi alivyo karibu na mdada, na mdada akawa ufungua wangu wa kufinikisha kwa watu wengi bila ya yeye kufahamu kuwa namfuatilia, na baadaya akaja kugundua, ndio hapo tukaanza kukosana mimi nay eye..

‘Sasa huyo dakitari wake, ni mmoja wa kundi, mdada halijui hilo,...na hata hao tuliowakamata ni kama chambo tu, ni dagaa tu, wapo samaki na mapapa, kwa ujumla kuna kundi kubwa la watu, wataalamu, madakitari, wanasiasa, wakufunzi....waheshimiwa...’akatulia

‘Sasa mtawezeje kuwakamata watu wote hao na kwa ushahidi gani...?’ nikauliza

‘Muda utasema cha muhimu ni kuliweka wazi hili jambo mahakamani, nafahamu ni kazi kubwa sana,kwani hilo kundi ni mti mkubwa wenye matawi mengi sana, na baya zaidi shina la mti huo halipo hapa nchini, lakini...muda utasema....’akasema huku akiangalia saa yake.
Mpelelezi akawa ameshapita kwenye kizimba tayari kwa kuanza kutoa ushahidi wake,....

NB: Haya ushahidi huoooo

WAZO LA LEO:Matabaka katika jamii ndio chanzo cha matatizo, viongozi, watawala, mabosi, mara nyingi wanashindwa kuliona hili, wakitegemea, ile kauli ya mwenye kisu kikali ndiye mla nyama.


Angalia sasa hivi elimu inatolewa kimatabaka, na halikadhalika makazini, watu wanaajiriwa kimatabaka, na hata mishahara hutolewa kimatabaka, kwahiyo hata nyoyo za watu zinajikuta zina hisia za kimtabaka, hapo unategemea nini, na ni nini chanzo cha haya yote. Chanzo cha haya yote ni ukosefu wa hekima ya uongozi, wa kujenga jamii inayopewa haki yake bila ubaguzi.

Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hellօ, you uyilized to write brilliant articles, neѵertheless, tɦe last few posts Һave bеen sora
poor... I lose your tremendous composing. Ρast a feѡ plасes
aree only a little from track!

mү blog ... cat health bladder problems blood in urine