Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Friday, June 13, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-76



‘Kuna tatizo limetokea....’

‘Tatizo gani...?’ 

‘Mlinzi kakutwa kwenye chumba chake akiwa hajiwezi, na akakimbizwa hospitalini, lakini hakufika hospitalini, akafia njiani, na docta alipomchunguza alisema huyo mlinzi kafa kwa sumu, alikuwa kanywa sumu....’

‘Na huyo wakili wake yupo wapi? 

‘Alikuwepo hapa, hajaondoka, nimetoka kuongea naye muda mfupi uliopita,

‘Nataka kuonana na huyo wakili ni muhimu sana.....


‘Nipo hapa mkuu...’

Tuendelee na kisa chetu

************* 

Mpelelezi alimgeukia yule wakili, na mimi kwa taratibu nikageuka kuwaangalia,  kuona ni nini kitatokea na katika hisia zangu nikajua sasa ni ugomvi, mafahali wawili wamekutana, na ukiangalia maumbo yao yanafanana, wote wamejazia kifua...niliona pingu ikiwa mfukoni mwa mpelelezi, niliona ajabu ya yeye kutembea na kitu kama hicho.

Mpelelezi ni mwepesi kweli, alivyogeuka utajua huyo mtu ni wa mazoezi, na mwenzake alikuwa keshajiandaa, akawa kasimama  kimtego, tayari kwa lolote, na wakati huo mkuu wa lile gereza alikuwa naye keshajiandaa kuamulia, kwani nilimuona akiwaangalai kwa tahadhari

Mimi nikawa nasubiria, nikipiga chabo la kujiiba, moyoni nikisema cha kwanza atakachofanya mpelelezi ni kutupa ngumi, na itatua kwenye shavu la huyo wakili, na wakili ataenda chini, akisimama , atakuwa na hasira nay eye atamrukia ile ya dume la ngombe lililokasirika, na hapo mpelelezi kwa vile ni mwepesi atampisha, na wakili ataenda moja kwa moja kugonga ukuta,....nashukuru mdada hayupo na kilini mwangu nikawa namuona akiangalia tukio hili huku akitabasamu

Akili bwana, ilikuwa ikiwazia kitu ambacho hakijatendekea, na huenda kisitendeke, pale nilimuona mpelelezi akimsogelea wakili kwa tambo, na alipomkaribia huyo wakili alisimama, na wakawa wanaangalia usoni kwa muda hivi, halafu  mpelelezi akasema;

‘Nataka uniambie ukweli wote,...najua unafahamu mengi,  sizani kama hujui kilichosababisha kifo cha huyo mlinzi, sizani kama hujui ni jambo gani huyo mlinzi alitaka kuniambia na mkaamua kumuwahi kabla hajakutana na mimi, sasa ili kupoteza muda nataka uniambie yote, sasa hivi….’akasema mpelelezi

‘Mlinzi alitaka kukuambia jambo mbona mimi sifahamu hilo?’ akauliza yule wakili akionyesha uso wa kushangaa. Na mara simu ya mpelelezi iliita, mpelelezi akaichukua na kuangalia mpigaji, akasema

‘Samahani kidogo, usiondoke, nataka kuongea na wewe.....’akasema na kuanza kusikiliza ile simu, alisikiliza kwa makini kwa muda mrefu, hadi yule wakili akawa anaangalia saa yake, na karibu kutaka kuondoka, ndipo mpelelezi akakata simu na kuanza kuongea na huyo wakili

‘Haya tuongee, nataka uniambie ukweli....’akasema

‘Ukweli upi, kama ni kuhusu kifo cha mteja wangu mimi sijui zaidi, ndio nafuatilia kujua ukweli, ....’akasema

‘Sio kweli, ...haya niambie ulipofika uliongea na mkuu wa kituoa hiki, na uligundua nini au utakwenda kuwaambia nini wanafamilia wa huyu marehemu?’akauliza

‘Kama alivyoniambia mkuu, kuwa marehemu kafa kwa sumu, na inaonekana amejiua, na uchunguzi bado unaendelea,...hakuna zaidi...’akasema

‘Wewe unafahamu kuwa mteja wako alitaka kuongea na mimi hii leo?’ akaulizwa

‘Ndio nakusikia wewe, ukisema hivyo...’akasema kwa kauli ya kutokujiamini

‘Ndio maana siamini hiyo kauli ya kuwa aliamua kujiua,…ni nyie mliamua kumuua kabla hajaniambia hicho alichotaka kuniambia, na mkafanya hivyo ili ionekana kajiua, yule sio mtu wa kujiua, namfahamu sana…’akasema mpelelezi

‘Mimi sijui ...nimepata taarifa hizo ndio nikaja hapa, na hata mimi siamini hilo la yeye kujiua, lakini ni mpaka uchunguzi ufanyike, ndio tutagundua ukweli, hata hivyo mimi ninakushangaa kwa wewe kunihusisha mimi na hayo, mimi ningeliwezaje kumuua mteja wangu, ambaye ni tajiri wangu , nafanya kazi kwake ili baadaye nipate pesa, halafu nimuue, hebu tumia akili yako vyema, halikuingii akilini….’akasema huyo wakili kwa kujiamini.

‘Unaweza kufanya hivyo, kama umepata fedha zaidi, na ndivyo nyie watu mlivyo,  lakini nikuambie ukweli, fedha kama hizo hazina faida, utatumia zitaisha, lakini dhambi ya hicho kifo haitaisha abadani, damu yake itakuandama hadi unaingia kaburini, na ukifika kwa mungu utachomwa moto….’akasema mpelelezi

‘Kwanza naomba tuelewane, chunga sana kauli yako, hizo shutuma mimi sizikubali, na kwa kauli yako hiyo ninaweza kukuchukulia hatua za kisheria, wewe ni mtaalamu na unafahamu hayo, huwezi kumshuku mtu tu ....’akasema

‘Fanya utakalo, nenda kachukue hizo hatua, tutakutana mahakamani na utaona jinsi gani nitakavyokufanya, nitaweka machafu yenu yote hadharani, unafikiri mimi siwajui, nazungumza haya nikiwa na ushahidi...’akasema mpelelezi na kumfanya yule wakili amuangalia wa macho makali.

‘Una ushahidi gani wewe..msipende kuchukulia mambo juu kwa juu, mimi sijui lolote, na kifo cha mteja wangu ni changamoto kwangu,  ikizingatia kuwa mimi ndiye niliyekuwa mtetezi wangu...’akasema kwa uchungu. Mimi nafahamu hasira inayokuandama, lakini hata mimi nina hali kama hiyo hiyomoyoni, naumia, na kuwalaani wote waliofanya hivyo,…na sitatulia mpaka hao watu wafikishwe mbele ya sheria, wewe utaona tu…’akasemana mpelelezi akamshika huyo wakili begani na kusema;

‘Sikiliza wewe, watu kama nyie nawafahamu sana, kwa jinsi gani mnavyoweza kuigiza,nawafahamu sana hata kwenye msiba mtafika mkilia, mkiigiza kuwa mna majozi, lakino moyoni mna malengo yenu, kwenye nyie mali ni muhiimu kuliko uhai wa mtu, mpo tayari kuua, kama mtu huyu anaziba nafasi zenu za kunufaika,lakini mimi nawaahidi kuwa siku zenu zimeshafika ukingoni…’akasema mpelelezi

‘Naona hapa hatutaelewana, kwani wewe hapa nakuona una hasira na unachofanya ni kumshuku kila mtu na hiyo ni hatari, maana unakiuka maadili yako ya kazi,mimi nimekusamehe, kwani najua hapa unalolifanya sio kusudio lako, hata hivyo, sioni kwanini wewe ujione unamhusu sana huyu marehemu wakati wewe ulikuwa msitari wa mbele kumuona kuwa ana hatia,...’akasema

‘Kushikwa kwake ni utaratibu wa kisheria, na sio kuwa hakuwa na haki, ...nyie mnanyima hata haki ya kuishi, huo ni utetezi gani,...mtaniambia ukweli, naahidi kuwa sasa sirudi nyuma, ni lazima nipambane na nyie hadi nione kundi lenu lote limesambaratika.....’akasema mpelelezi kwa hasira

‘Hata mimi nakuunga mkono kama nia yako ni njema ya kuliondoa hilo kundi, kama lipo, lakini fuata utaratibu unaokubalika, usichukulie jaziba, jaziba hazitakusaidia 
kabisa...’akasema.

‘Natumai familia hiyo ya marehemu itagundua ukweli kuwa wewe ni ndumila kuwili,  kuwa wewe unahusika moja kwa moja kwenye kifo hicho….na mimi nitaongea nao kuwa wasikuamini tena…’ akasema mpelelezi na na yule wakili akatikisa kichwa  kama kusitikia, na kuanza kuondoka

‘Unaenda wapi, hutajamalizana, nimekuambia uniambie ukweli kuhusu marehemu, je alitaka kuniambia nini?’ akauliza mpelelezi

‘Mimi siwezi kujua, kwasababuhakuwahi kuniambia kuwa anataka kuongea na wewe, na tulishakubaliana naye kuwa hataongea na mtu mwingine mpaka mimi niwepo, naona ajabu kuniambia kuwa mlipanga mje mkutane naye, hapo na mimi nakutilia mashaka,..’akasema

‘Mlipoongea naye kwa mara ya mwisho alikuambia nini?’ akaulizwa

‘Alisema amechoka kukaa jela,na anahitajia kutoka nje, kwani yeye hana hatia, na alisema nifanye haraka kumtafutia dhamana yake,na pia akasema anahitajia kusimamishwa mahakamani ili aeleze ukweli kuwa hahusiki na kifo cha mtoza ushuru..’akasema

‘Na kwanini wewe ukawa kikwaza cha maombi yake hayo,mtu alitaka kusema ukweli mahakamani , lakini wewe kwa ujanja wako ukawa unamzuia…?’akauliza

‘Mimi ni mwanasheria nafahamu athari za  maombi yake hayo, yeye alitaka kusimama mahakamani na kuongea mambo ambayo yangelimtia matatani na kuonekana kuwa kweli alihusika, ndio maana nikawa na mzuia kwa nia njema maana nilijua athari zake…’akasema

‘Hivi kumzuia kusema ukweli ndio kumsaidia, nini maana ya mahakama, ..mahakama ipo hapo kwa kusikiliza ukweli, na yenyewe itajua ukweli upo wapi,..huoni kuwa kwa kufanya hivyo umasababisha ukweli aliokuwa nao huyo marehemu usitambulikane tena,na mumemzuia na mlipoona bado anataka kuongea ukweli, mkaona mumunyamazishe kabisa...’akasema mpelelezi

‘Aliyotaka kuyaongea kama yangesikika mahakamani yangeli mtia mteja wangu matatani mimi nafahamu sana sheria kuliko wewe, kwahiyo nafahamu nini cha kufanya, nilifanya vile kwa masilahi ya mteja wangu, kwa nia njema kabisa ya kumsaidia mteja wangu, sasa wewe elewa unavyojua wewe, haijalishi, …’akasema.

‘Ukweli upi, ambaoalitaka kuusema,ambao unahisi ungelimuingiza matatani...kama sio ujanja ujanja wako?’ akauliza mpelelezi.

‘Kwa mfano huyo mlinzi alitaka kukiri kuwa ni kweli yeye hakuingia kwa kupitia mlangoni,kama ilivyoelezewa awali, japokuwa baadaye ilikuja kubainika hivyo,kuwa yeye alipitia dirishani….’akasema wakili

‘Na huoni jinsi gani ulivyomzuia kusema ukweli huo hadi nilipoleta ushahidi wa kubainisha kuwa kweli hakupitia mlangoni alipitia dirishani, hivi ndivyo sheria zako zinavyokuelekeza kuwa mtu afiche ukweli, wakati huo ukweli ndio unaohitajika?’akauliza.

‘Ukweli unahitajika kwa wakati maalumu, kwa masilahi ya mteja wangu, na ukiona ukweli huo upo, na unamuathiri mteja wangu, ni lazima nimshauri kwa manufaa yake...’akasema

‘Huo sio uadilifu na huo sio uwakili wenye manufaa kwa taifa, nyie ndio watu mnaofanya kazi kwa ajili ya matumbo yenu, na sio kwa ajili ya kutafuta haki na ukweli...’akasema mpelelezi

‘Wewe sema unavyotaka, lakini hujui misingi ya kazi zetu, na mimi ninajua ni nini cha kufanya kwa waati gani kwa masilahi ya mteja wangu, jiulize ni nini maana ya wakili mtetezi, nitakuwa mtu wa ajabu kama nitafanya kazi ya muendesha mashitaka kwa mteja wangu badala ay kumtetea, wewe vipi bwana....’akasema

‘Haya niambie jambo gani ambalo lilikufanya usimsimamishe marehemu na ambalo angelisema lingemtia matatani..?’ akauliza mpelelezi

‘Sio lazima nikuambie yote, hayo ni mambo yangu na mteja wangu, hata hivyo nitakuambia hili la bastola, najua unataka kulifahamu kuwa yeye aliwahi kuchukua bastola ya mdada,japokuwa bastola hiyo haijahusishwa na kifo cha mtoza ushuru…hayo na mengine kama angeliyaongea mahamakani unafikiri hakimu angelihukumu vipi, ni moja kwa moja ingeonekana mlinzi ana hatia, ndio maana nikamzuia kwa manufaa ya mteja wangu,..…’akasema.

‘Unasema jana mliongea na mteja wako, ukaondoka, na  kuelekea kwa mdada, maliongea nini na mdada?’ akauliza

‘Mdada ni bosi wa mteja wangu, kuna malipo yanahitajika , aliyokuwa akidai mteja wangu na alihitajia hizo pesa kwa ajili ya familia yake, ndio maana nilikwenda kuonana na mdada...’akasema

‘Na ulipotoka hapo ulikwenda wapi?’ akauliza mpelelezi

‘Nilirudi ofisini kwangu, ..’akasema

‘Muda wa saa mbili za usiku ulionekana maeneo ya hapa gerezani, niambie huku ulifuata nini ?’ akauliza

‘Mimi nina uhuru wa kwenda popote, na ndio nilikuja maeneo haya lakini sio kuja huku gerezani, nina fundi wangu wa gari yupo maeneo ya huku, nilikuwa kuonana naye, kwa ajili ya gari langu..’akasema

‘Ulipomaliza kuongea na huyo fundi, ulimpigia simu mteja wako, mliongea nini...?’ akaulizwa na hapo akawa kama kashituka halafu akasema

‘Nilikuwa namjulia hali....ni wajibu wangu kuongea naye kujua anaendeleaje...’akasema

‘Ulimuambia kuwa awe makini na mimi, ...wewe ulijuaje kuwa mimi nataka kuongea na yeye...?’ akaulizwa

‘Yoye hayo umeyapatia wapi, ...usizue mambo, mimi ni kweli niliongea naye, na ni wajibu wangu kumkanya kwa lolote lile...’akasema

‘Ujue siku hizi dunia ni kijiji, usione kuwa wewe ni mjanja,...nakuambia ukweli, sitatulia mpaka wote niwaweke ndani,...wewe ulimtisha mteja wako kuwa akiongea na mimi na kufanya nitakavyo mimi, itakuwa mwisho wake..na huoni kuwa kauli yako ndio imatimiliza...’akasema mpelelezi

‘Niliongea naye kwa kumkanya, nawafahamu sana nyie watu, mtamdanganya halafu mwisho wa siku mnamuhukumu...ndio maana nilimkanya...’akasema

‘Ulipotoka hapa gerezani ulikwenda wapi?’ akaulizwa

‘Nilirudi ofisini kwangu..’akasema

‘Ulimpigia nani simu kwa muda huo?’ akaulizwa

‘Niliwapigia watu wengi sana, siwezi kukuambia wote maana ni maswala ya kikazi, na wateja wangu mbali mbali, na wewe huna haki ya kuwajua..’akasema

‘Wewe mwanzoni ulijifanya kuwa hujui kama mteja wako alitaka kuonana na mimi, na sasa hivi nimekubana hadi umekiri kuwa ulionngea naye ukamkanya kuwa asiongee na mimi, ...huoni hapo unaficha jambo, hebu niambie na uliporudi ofisini kwako, uliongea na askari mmoja wa hapa gerezani kuwa ahakikishe mimi sipati nafasi ya kuongea na mimi kweli au si kweli.....’akasema mpelelezi

‘Sasa nakuona unazua mambo, mimi siwezi kuendelea kuongea na wewe hapa, kama unaona mimi ninahatia nishitaki, na tutapambana mahakamani....’akasema

‘Jibu maswali yangu kama wewe ni wakili unayejiamni, ...kama huna hatia mbona unaogopa, ..’akasema mpelelezi

‘Nimeshakujibu yale ninayostahili kukujibu zaidi ya hayo nione ofisini kwangu, au kama unaona nina kosa nishitake, mimi nitakuja kujieleza kituo chochote cha polisi,...’akasema na kuanza kuondoka, na mpelelezi akamuendea na kumshika begani

‘Usiondoke mimi sijamalizana na wewe...’akasema mpelelezi na yule wakili akageuka na kusogeza mkono wa mpelelezi pembeni na kusema;

‘Naona sasa unataka kunipanda kichwani, nimeshakuambia kuwa kama unataka kuongea na mimi kisheria, na ili nijibu maswali yako kisheria, njoo ofisini kwangu au nifungulieni mashitaka, na mimi nitafika kituoni, na kujajibu maswali yenu kisheria, lakini hapa tunaongea kama wapiti njia tu...’akasema

‘Sasa mimi ninakushika kwa kosa la kuhusika na mauaji ya mlinzi...’akasema na mara nikamuona mpelelezi akitoa pingu aliyokuwa kaiweka nyuma,...

‘Eti nini.....’akasema wakili sasa akibadilika na kuwa mkali na muda huo mkuu wa hapo gerezani akawa anawasogelea akijua sasa hali sio shwari tena...

NB: Ni kweli kuwa huyu wakili anahusika na kifo cha huyo mlinzi, tutaona sehemu ijayo


WAZO LA LEO: Katika maisha yako ya kikazi, (waajiriwa) kamwe usifanye kazi kwa ajili ya bosi, fanya kazi kwa mujibu wa kazi yako inavyotakiwa iwe- kitaaluma. Kuna baadhi ya wafanyakazi maofisini wana tabia hiyo, ya kuvizia bosi akiwepo ndio wanawajibika, au kuwahi kazini kama bosi yupo kama huyupo wanachelewa au kama hayupo wanaongea tu,....huu ni utumwa, huu sio uwajibikaji na huo sio utawala bora, jaribu kuwa muadilifu wakati wowote....

Ni mimi: emu-three

No comments :