Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, June 10, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-74


‘Mhasibu iliyotokea hapa ni kama vile unaangalia sinema , ni tukio ambalo ninaweza kusema lilipangwa iwe hivyo na limekuwa hivyo, nashindwa hata kuamini..’akasema mpelelezi akiwa kashika shavu, ilionekana imemgusa sana, na hata pale alipo alionekana kutokulia kiakili, alikuwa akimuangalia kila daitari aliyepita.

‘Hebu niambie imekuwaje, maana nimezuiwa kabisa kuingia kuonana na mzee...?’ nikamuuliza

‘Huwezi kuingia kumuona tena kwa sasa, na nakushauri ni bora kwa hivi sasa ukawa mbali na hiyo familia...’akasema mpelelezi

‘Kwanini wanifanyie hivyo?’ nikauliza nikiangalia kule alipolazwa huyo mzee.

‘Kwa kauli ya shangazi wewe na mdada hamtakiwi kabisa kufika maeneo ya hiyo familia, japokuwa mdada aliweza kuruhusiwa kuongea na mzee, lakini aliongea naye kwa masharti na masaa maalumu, akisimamiwa na shangazi.

‘Hutaamini baada ya maongezi hayo mdada aliondoka, akisindikizwa na maneno makali kutoka shangazi kuwa hataki amuone tena kwenye hio familia...

‘Lakini kwanini haya yote, mbona mimi simuelewi huyu mtu, mimi au mdada kafanya kitu gani kibaya kwenye hiyo familia....?’ nikauliza

‘Mhasibu usilazimishe mambo, haya mambo yaache yatulie na yataenda hivyo hivyo, na huenda huko baadaye mkaja kuelewana na hiyo familia lakini kwa sasa nakushauri uwe mbali kabisa na hiyo familia...’akasema

‘Hebu nikuulize wewe umeweza kuongea na mzee, na hata huyo shangazi kuna tatizo gani, sisi tunahusika na nini na hiyo familia, mimi ni mkwe wao, kwanini waninyanyapae, au mzee kakuambia nini?’ nikamuuliza

‘Mimi sijui undani zaidi wa matatizo yako na hiyo familia, nahisi inatokana na wewe kumtelekeza binti yao,..si ndio hivyo?’ akaniuliza mpelelezi.

‘Lakini mimi sijafanya hivyo, sijamtelekeza...’nikajitetea

‘Mimi sijui, ...nina mambo makubwa zaidi ya hayo ya kifamilia,...’akasema

‘Wewe na hiyo familia mpoje?’ niamuuliza

‘Mimi sina matatizo na hiyo familia, mzee na familia hiyo tunaelewana, hata huyo shangazi mara nyingi nakutana naye tunataniana...unajua yule mama anavyopenda kuongea utani mwingi, mipasho basi ndivyo alivyo na nimemzoea hivyo hivyo....’akasema

‘Mimi sijawahi kuiona furaha ya huyu shangazi japokuwa nasikia sifa zake kuwa ni mcheshi, na mtu wa watu...lakini mimi na yeye hatuivani mara zote nilizokutana naye ni hasira, na kunikaripia tu....sijui kama nitakuja kuelewana na huyo mama...na alishaniambia nihame huu mji maana atakachonifanyia sitakisahau...’nikasema

‘Hayo yataisha tu, ukweli upo wazi kwa sasa, tusubiri mahakama itakavyoamua, lakini ..’akatulia maana nilimuona docta akija kwa kasi, akatupita, na alionekana kama ana anafuatilia au kuna jambo limetokea, nikamuangalia mpelelezi, na mpelelezi akasimama na kuelekea kule alipoelekea docta.

Haikupita muda, docta na mpelelezi wakarudi wakiwa katika mwendo kasi kidogo, na mpelelezi, akawa anaongea na simu;

‘Hakikisheni mnakagua kila chumba, ..ni nesi, alikuwa kavaa kinesi ....huyo nesi ana umbile la nane, mweupe hivi, na alikuwa kavaa raba nyeupe, ndio, ....’akasema

‘Kuna nini kwani...?’ nikawasogelea na kuwauliza

‘Invyoonekana mzee kanyweshwa sumu, na hivi sasa madocta wanajaribu kuokoa maisha ya mzee, haijajulikana ni aina gani ya sumu...’akasema mpelelezi

‘Kanyweshwa sumu..na nani?’ nikauliza kwa mshangao

‘Ilivyokuwa ni hivi, wakati nimeongea naye kwa muda mfupi, akinisimulia mambo mengi ambayo mimi nilikuwa siyajui, ilifika muda akawa na kiu, lakini kuna dawa alipewa aliambiwa asinywe maji kwanza asubiri kidogo , na tulipoongea kwa muda, yule nesi aliyekuwepo hapo akamwambia asubiri kama dakika tano hivi, ataweza kumpa maji,...basi tukawa tunaongea na kila mara mzee alikuwa akiangalia saa yake, na kuniambia;

‘Nina kiu dakika tano hazijaisha tu....’ basi mimi nikamuambia yule nesi aliyekuwepo hapo, kuwa mgonjwa anahitajia maji,....

‘Sawa ngoja nimchukulie gilasi...’akasema yule nesi, na mimi nikaangalia pale kwenye meza kuna maji ya kunywa, nikataka kumpa mgonjwa, anywe na vikombe vilivyokuwepo,lakini moyo wangu ukasita, na shangazi alikwenda kusafisha vyombo.
Mzee akasema;

‘Hawa watu bwana, kila kitu mpaka wanipe wao, maji si hayo hapo, wanataka kunipa maji gani...’akasema mzee, na mimi nikamwambia ni vyema tukafuata maelekezo na masharti yao, wasije kusema kwanini tulifanya hivi au vile

‘Basi yule nesi akarudi akiwa na gilasi mkononi, nakumbuka kabisa alikuwa na gloves amevaa, tokea awali, akaichuua ile gilasi na kumimina maji yale yale yaliyokuwepo pale mezani, akayainua juu, ..mimi pale akili yangu ikawa inajiuliza mengi, sijui kwanini niliingiwa na shaka

‘Nipe maji bwana, mimi nina kiu, wewe unayafanya hayo maji kama dawa...’akasema mgonjwa na muda huo shangazi naye alikuwa ameshafika akiwa kebeba vile vyombo alivyokwenda kusafisha, na shangazi akachukua ile chupa ya maji, na kuyamimina kwenye gilasi aliyokuwa kaishika yule nesi...yote hayo nimeyaona kwa macho yangu

‘Basi yule nesi ndiye aliyempa mgonjwa maji, huku wakitaniana na huyo nesi kuwa mzee akipona yeye anataka awe mke wake wa pili,...na mzee akayanywa yale maji yote na kataka mengine, wakamuongezea, na safari hii akawa anamnywesha shangazi...yule nesi akawa anaangalia na baadaye huyu nesi akaondoka kwenda kwenye chumba chao, kipo karibu na akiwa pale kwenye chumba chao unamuona.

‘Oh, sasa najisikia safi....sasa nataka kuongea na huyu mpelelezi,...’mzee akamwambia shangazi na shangazi akasema;

‘Lakini mimi naona umeongea kwa muda mrefu, umeongea na yule muhuni, kwa muda mrefu, kaondoka, na bado umeongea na huyu mpelelezi, kwa hivi sasa ni bora upumzike...’akasema dada yake

‘Muda huo haupo, muda wa kupumzika utafika mtu utapumzika moja kwa moja, lakini sio sasa,...wewe niachie nafasi hayo ninayotaka kuongea naye ni muhimu na ni mambo nyeti, tupe nafasi kidogo...’akasema na dada yake akaanza kuweka vitu vyae kwenye kiapu alichokuja nacho huku mzee akinisimulia mambo:

‘Nimeshakusimuliza chanzo cha madudu yaliyopo kwenye sehemu nyeti za nchi yetu, kuna watu wamejiona wao wamefika na hii nchi ni yao...’akasema

‘Maisha yangu ya utendaji wa kazi nikiwa serikalini yalikuwa ni ya kujituma, nikiishi kwa mshahara wangu tu, hebu fikiria mishahara yetu ilivyo, lakini sikupenda kabisa kuwa mbadhirifu, na sikuwa na marupurupu mengi, hata pale nilipokuwa bosi wa kitengo, sikupenda kupata zaidi wakti wengine hawana kitu...’akasema na kipindi hicho shangazi alikuwa hajatoka, bado alikuwa akikusanya vyombo, ili aondoke navyo.

‘Nikuambie ukweli, katika maisha haya yetu ya uhalisia, watendaji kazi wazuri, wenye kujitolea ndio wanaishia katika umasikini baada ya kustaafu kwao, na wale wanaofanya kazi kiujanja ujana ndio wanakuja kuwa na maisha mazuri kutokana na ufisadi walioufanya wakiwa makazini, angalia kiukweli jinisi ilivyo kwa watu unaowafahamu.

Watu wale waliojitolea, wakifikia uzeeni, wakati mwingine wanakuja kujijutia, hasa wakiangalia yale waliyoyafanya kwa kujitolea kwa hali na mali, ..na jinsi wanavyosahaulika,...ni lazima kama binadamu utakuwa uanawaza sana.....na muda huo hawana la kufanya tena, ,matokea yake wanakufa haraka kwa kihoro,...au wanapatwa na magonjwa ya kuwatesa hadi wanakwenda kaburini...’akasema

‘Kwa mfano mimi mpaka nafikia kustaafu, nilikuwa sina hata nyumba ya maana, maana ungelijenga na nini, kipindi hicho, watendaji tulikuwa tukiangaliwa sana, na pia mshahara wangu ulikuwa wa kawaida tu, na mimi sikuwa nafahamu kuiba,..wenzangu wakawa wajanja,kisiri wakawa wanafanya vitu vyao wakajijenga mimi nawaona, na ndio unawaona wana makampuni, vitega uchumi, na hayo hawakuyafanya kihali,lakini ungelisema nini.....’akatulia

‘Nilipofikia muda wangu wa kustaaafu nikaenda kuishi kwenye kibanda changu kijijini, huko nilikuwa na shamba langu, maana kipindi hicho mashamba yapo mengi tu, unapewa na wananchi bure, kwahiyo huko shambani nilijenga kibanda changu, nikaweka mifugo, basi nilipostaafu nilirudi huko kujitegemea,..

‘Kiukweli  sikuwa na ujanja, nisingeliweza maisha ya mjini japokuwa nilikuwa nimeshayazoea, na muda huo nikawa nadanganywa na bima ya uzeeni kuwa itanisaidia, haiwezi , haikuweza, kwani thamani ya pesa inapungua kila siku, ni pesa wanayotoa ni ndogo tu...maisha yakaanza kuniendea vibaya, usiombe....’akasema

‘Maisha yalikuwa magumu, na nikawa nikifikiria nilivyojitolea kwa hali na mali kuitumikia nchi yangu, na sasa ndio nimefikia fainali, sina mbele wala nyuma, nikaanza kupatwa na maradhi ya ajabu...mawazo ni kitu kibaya sana, nikatibiwa tibiwa wewe, sasa na miti shamba, hela ya hospitali ninayo....

Sijui ni nani aliniona akaipeleka hiyo taarifa kwa wakubwa, ikawagusa, ndio hivyo tena wavumai papa baharini lakini samaki wengine wapo, na kila penye ubaya kuna na uziri wake, wakatokea watu wenye moyo wa huruma, wakaenda kuongea na wakubwa,  baadaye nikaitwa....’akasema

‘Nilishangaa siku hiyo aliponijia kijana na gari, akanipa barua kuwa nahitajika wizarani, serikalini, nahitajika kwenda kutoa ushauri na kusaidia kazi maalumu, katika vitengo nyeti vya serikali, ...sikuamini, nilishajua muda wangu wa kulipa fadhila za kujituma umefikia, nisubiri kufa na thawabu zangu nitazikuta peponi,...

‘Basi nikafika kwa huyo mkurugenzi, nilimkuta ni kijana mdogo tu,....tofauti na enzi zetu, nafasi kama hizo walikuwa wakishika watu wazima, elimu sasa inalipa eeh, haya ndio enzi zake hizi....’akasema

‘Basi yule kijana akaniambia;

‘Mzee nimekuwa nikifuatilia utendaji wako katika makabrasha yetu, nimevutiwa sana na wewe, na nimeomba kwa wakubwa zangu kuwa tunahitaji wazee wa siku nyingi ili tupate uzoefu wao, maana kuna mambo ambayo mimi nayaona sio sawa,...na tumetumia juhudi zetu za kisomi  lakini imekuwa ni kazi kubwa sana , imekuwa kama ile hadithi ya kumtuma mjumbe, na huyu mjumba akifika anapotea huko huko....’akaniambia

‘Unasema kuna mambo hayapo sawa ni mambo gani hayo?’ nikamuuliza

‘Kuna ubadhirifu wa hali ya juu unaoendelea kwenye viteng vyetu nyeti hasa vile vinashughulika na masilahi, lakini unafanyika kitaalamu sana, tumefanya uchunguzi lakini hatujaweza kubaini kiicho chake na nani yupo nyuma ya hayo yote..’akaniambia

‘Mhh, lakini hiyo si kazi ya polisi, mimi nitawezeje kusaidia, kwanza na huu uzee mimi nitafanya nini, na hata hivyo mimi mwenyewe sipendi hayo mambo nimeshajichokea, nahitaji kujipumzisha nisubiri umauti wangu, sitaki tena misuko suko....’nikamwambia

‘Mzee kuna kitu nimejifunza, ...na mimi kama mimi nataka kulipa fadhila za watu kama nyie ambao mumelitumikia hili taifa kwa moyo mmoja, na mumefikia hatua hiyo lakini hakuna anayewajali tena, wanachosubiri wakubwa zetu ni nyie mfe, waje kuwazika kwa mbwembwe za kitaifa,....mimi hali hiyo siipendi, kwanini wasiwajali muda huu mkiwa hai wakawasaidia....’akasema

‘Kwahiyo unataka mimi nifanya nini?’ nikamuuliza

‘Ni hivi mzee kazi ninayotaka wewe ufanye, ni nyeti kidogo, mimi naiita ‘uma huku unapuliza..’ yaani wewe utaingia ndani ya jamii inayotenda yasiyofaa, utaishi nao, ...utafanya kila wanachofanya wao, maisha mazuri, starehe, utajikita pia kwenye huo ubadhirifu, na hapo ina maana utapata kila kitu na utafanya kama wao, ili tu uwajue ni nani na wanafanya nini, unauma huku unapuuliza, hadi tuone ni nani yupo nyuma ya haya yote....’akasema

‘Ohi, kwanza nilikataa kabia, lakini baadaye nikafikiri kwa makini, hivi mimi maisha mazuri nitayapata wapi, nimesoma hadi chuo kikuu, nikawa bosi, lakini maisha yangu yalikuwa kama yakujitolea kwa jamii, sikuwahi kuishi kistarehe, hata siku moja, sikuwa na muda wa starehe kwangu mimi kazi ilikuwa mbele..., nilitaka kila jambo nilifanye mimi kuhakikisha linafanikiwa,...usinione hivi, mimi nilikuwa nakuwa wa kwanza kuingia ofisini na wa mwisho kutoka...’akasema

‘Ni nini nimekipata baada ya hayo yote, hakuna,umri wa kustaafu ulipofika kila mmoja alishukuru niondoke, maana mimi nilikuwa mnoko, naziba riziki za watu ... hata watani wangu wakawa wananitania, kuwa nilikuwa najipendekeza sasa faninali uzeeni, wanasubiri kuja kula maharage..ni kweli nimebakiza nini ...’akasema kwa uchungu.

‘Basi nilipofikiria sana, nikaona ni bora nikubali kuifanya hiyo kazi, nikajipanga vyema, nikaja kujadiliana na yule mkurugenzi , nikapewa ofisi ya kinamna...sikutakiwa niwe na ofisi ya kutilia shaka , kwahiyo ofisi zangu mara nyingi zilikuwa mahotelini..nikawa natoa ushauri kwa vijana, jinsi gani ya kuingia huko kusipoingiwa....

‘Nikaanza maisha adimu, maisha ambayo sijawahi kuishi,starehe, na kula nchi,...watu wengine wakaanza kunong’ona, mmh, mzee yule bhana, uzee kaucha njia panda, alishindwa kutumia ujanani, kujirusha sasa ndio anakumbuka,,..ndio ilibidi nifanye hivyo, ili niweze kufanikisha kazi yangu, na vijana wangu walijua jinsi gani ya kuigiza, huwezi amini walifanya kazi niliyoibuni mimi...’akasema

‘Nikuambie ukweli pamoja na kuwa nilikuwa na usongo wa kulipiza kuwa na mimi nipate nafasi ya kutumia, lakini moyoni mwangu nilikuwa na hasira na hawa mafisadi, kwahiyo nikawa najitahidi niweze kujua siri zao kiundani zaidi...’akasema

‘Nikajitahidi kujionyesha nilivyoweza hadi nikakubalika, kuwa huyu sasa ni mwenzetu, ...’akatulia

‘Kuitwa mwenzetu sio mchezo, ...kuna mambo kwenye hii sifa ya uwenzetu, ...na nilikuja kugundua jambo kumbe haya maneno, hizi sifa usione inatamkwa ukafikiria ni maneno tu, mara waheshimiwa, mara wenzetu , mara .....yote haya yana maana fulani kwa wahusika, kwa wengine ni majina tu...’akatulia

‘Ili nifanikiwe hilo nilihitajika kuwa na watu wangu ninaowaamini, sikuwa na shaka na hilo, kwani katika utendaji wangu wa kazi huko nyuma kuna watu niliwaona wanafaa sana kulitumikia hili taifa, vijana niliowahi kuwafundisha mwenyewe, basi nikawapata hao, nikawapika ipasavyo, nikawaonyesha njia...na kweli walifuata ninavyotaka...’akasema

Na wao wakawatafuta watendaji wao...unaona hapo, ni aina fulani ya mnyorororo wenye ndoana mwishoni, lakini nia na lengo ni kumnasa samaki kubwa lao.....

‘Kuna siku moja nilikuambia kuwa kuna kundi lilitokea kipindi cha nyuma, lenye mlengo mbaya wa taifa, hilo kundi lilianzishwa na jamaa mmoja aliyetaka kuunda dunia yake, akasema anataka kuwa na ‘dunia yake..’ kama ni mfuatiliaji mnzuri wa mambo haya yetu utakumbuka kitu kama hicho...’akasema

‘Sasa yaliyotokea, na yataendelea kutokea ni matawi ya hiyo dunia aliyoianzisha na huyo jamaa, huyo jamaa hayupo hapa nchini kabisa, ila ni tajiri wa hali ya juu huko nje anapoishi baada ya kufanikiwa kuiba na kuwekeza...sasa hivi yeye ni mfadhili wa watu wa kundi lake...lakini sio rahisi kuligundua hilo...ilibidi nipenye kwenye vizingiti vikali sana, mpaka nikafikia cheo cha uwenzetu..’akasema

‘Mimi niliweza kuifikia hiyo ngazi kwa muda niliopewa hiyo kazi, na nilifanikiwa baada ya kuniona nimerudi kuhangaika, nikiwa nimechoka, sina mbele wala nyuma, wakajua huyu hana la kufanya, dawa ni kumrubuni tu, na kwa vile anajua mengi kwenye system, basi ataufaa, kwahiyo kidogo kidogo wakawa wananiingiza kwenye anga zao...

‘Mzee sasa naona umekomaa, japokuwa umekwisha, sisi tunataka na wewe ule hii nchi...’siku moja akaniambia jamaa ambaye huwezi amini, ni mtu mwenye wadhifa na heshima zake, kumbe ni mmoja wa kinara ya hilo kundi..

‘Sasa tunataka uwe nasi,..utusaidie mambo fulani, na sisi tutahakikisha wewe na familia yako mafi njaa....’akasniambia na mimi sikujivunga, nikakubaliana na yeye, nikawa nauma na kupulizia...

‘Kwanza walianza kunijenga kiimani zao, maana na wao wana imani zao,...wakanipika kivyao, hadi wakaona nimeiva...hawakujua nina nini kichwani mwangu, huwezi amini, watu waliopo humo ni watu wa kawaida, tupo nao , ni watendaji wa kazi wazuri tu, wengine ni viongozi wa dini, yaani kila idara wapo...’akasema

‘Hiyo ndio mikakati aliyoifanya yule jamaa aliyeanzisha dunia yake...kuna makabrasha nimeyaandika kwa kirefu, nilitaka kutoa kitabu, lakini nilichelea ....na wakati nimefikia hatu ya mwisho, makabrasha yangu yakaibiwa,...ndio hayo unayosikia wakisema nyaraka nyeti, ...wajanja wakachukua kazi yangu .....na nilikuja kumgundua aliyefanya hivyo ni nani..huyo jamaa akaanza kunichongea kwenye kundi kuwa mimi ni msaliti...’akatulia

‘Sasa kazi ikaanzia hapo...nikawa nawindwa, ili upatikane ushahidi, ni ukipatikana mimi napotezwa...’akasema

‘Ohh, lakini mimi sikujali, nilijitahidi kujionyesha kuwa mimi bado ni mwenzao, na wahusika, hawakunitilia shaka moja kwa moja, wakawa wananiwinda usiku na mchana, lakini mimi nilishajiandaa,...sasa nafikia sehemu nyeti...’akasema na kumuangalia shangazi aliyekuwa sasa akisikiliza kwa hamu, mzee akamwambia shangazi

‘Nimekuambia utoke ndugu yangu, haya hayakuhusu....’akasema mzee

‘Kwani hayo ni siri, kaka naye bwana, mimi nayafahamu hayo yote, ...’akasema shangazi

‘Wewe si kila kitu unakijua, tatizo lako hujui hatari ya haya mambo, usipende kujiingiza kwenye maswala kama haya, watakupoteza hao watu, hao watu hawajali kumpoteza mtu....’akasema.

‘Mimi hawaniwezi...’akasema na kuanza kuondoka, na mzee akasema;

‘Mimi nataka kukusimulia yote, ambayo nayafahamu mimi, na hasa kuhusu yaliyotokea siku ile kwa mdada,..lakini muhimu jitahidi sana upate hizo nyaraka nyeti, kuna membo mengi nimeyafichua hapo...

‘Sasa kuhusu yaliyotokea kwa mdada, ni mlolongo mrefu, na imechukuliwa juu kwa juu tu,na kwa vile hilo kundi halijulikani, na mambo yao ndivyo yalivyo, kutokea kitu kiwe na utata fulani, na wao kwa vile wapo kila mahali, wanalivuruga lile jambo,...’akasema

‘Sasa yaliyotokea pale, yameshaharibiwa kabisa, na watu wengi hawafahamu hilo, ila yaliyotokea pale ni katika harakati za wenzetu kuhakikisha wanaondoa wasaliti kwenye kundi lao...japokuwa kifo cha yule jamaa ni bahati mbaya tu, hata hivyo ilibidi ifanyike vile, kuokoa watu wasio na hatia.....’akasema

‘Mhh, mbona...’akasema akikohoa, na kukunja uso...

‘Vipi mzee...’nikasema na nilimuona akijitahidi kutafuta hewa ya kuvuta, na mara nikamuona mzee macho yanamlegea mimi nikajua kachoka kwasababu aliongea na mimi kwa muda mrefu na kabla ya hapo alitangulia kuongea na mdada...’akasema mpelelezi

‘Kwani mdada yupo wapi?’ nikamuuliza

‘Mdada alifika mapema, na alipomaliza kuongea na mzee, alitoka,na kunikuta nipo nje , nikisubiria zamu yangu, alipotoka aliniona  akanipungia mkono...alionekana kuwa na haraa kidogo,  na mimi nikaona nimuwahi, ili nimkumbushe, kuwa nahitajia kuongea naye baadaye...kwahiyo nikamkimbilia kabla hajaingia kwenye gari lake;

‘Mdada nakukumbusha tukutane ,...na nitakuambia wapi...’nikamwambia na yeye akatabsamu na kusema;

‘Haina haja ya mimi na wewe kukutana na sioni kama kuna umuhimu wa mimi kuongea na wewe, natumai ukimalizana na mzee, utanielewa nina maana gani, ila cha msingi ninachotaka kukuambia ni kuwa uwe makini, ...hali ya hewa imechafuka,....wenyewe wameshagundua kuwa kuna watu wameingia kwenye anga zao...’akaniambia hivyo

‘Lakini mdada ni muhimu sana mimi na wewe tuongee...’nikamsisitiza na yeye akasema;

‘Haina haja, ...ila mimi nakutakia ushahidi mwema, mahakamani, nasikia wewe utaenda kufunga kazi,...mimi sizani kama nitakuwepo, na tukujaliwa huenda tunaweza kukutana kwenye anga hizi hizi, ....’akasema na kuingia kwenye gari lake na kuondoka

‘Ina maana gani kusema hivyo, na anakuaga anakwenda wapi?’ nikamuuliza

‘Sijui....mdada haeleweki, lakini nilikuja kuyagundua hayo nilipoongea na mzee, ...’akasema

‘Mzee alisema nini kuhusu yeye?’ nikamuuliza

‘Kuna mengi niliongea naye kabla, ila sehemu muhimu niliyoitaka kuijua, haikuweza kuongelewa, ...’akasema

‘Kwani ilikuwaje...?’ nikauliza

‘Wakati mzee anasubiri shangazi aondoke, ili anihadithie hiyo sehemu nyeti kama alivyoiita yeye, mara nikaona mabadiliko kwenye uso wake, alianza kuhema kusivyo kawaida, nikahisi kuna jambo, nikamuuliza

‘Mzee vipi, au unahitaji kupumzika kidogo, nakuona unahekam isivyo awaida, ...’nikasema na shangazi aliyekuwa anaondoka, akageuka kumuangalia kaka yake naye akaiona ile hali, na mzee akasema

‘Mhh, najiona kama nahama duniani,...mmh, naona sasa muda umefika, ...na mara akatulia kimiya...mimi nikaingiwa na mashaka, nikageuka kumuangalia yule nesi, aliyekuwa pale sehemu wanayokaa, lakini sikumuona tena, nikagonga kengele ya kuomba msaada, ...akaja docta, na alipofika akatufukuza tutoke....

NB: Je ni nini kilitokea


WAZO LA LEO: Siku hizi walio nacho wanataka kupata zaidi, hata ikibidi kuwanyang’anya wale waliokuwa nacho kidogo, huwezi kusikia hata siku moja tajiri akisema mimi sasa ni tajiri sitaki zaidi, utamsikia akisema maisha magumu,hali ngumu,...yeye kipato alicho nacho hakimtoshi,japo kuwa anacho, je yule ambaye hana kabisa ...ndio maana wanasema ukisema hakitoshi ujue unacho, hebu jiulize yule ambaye hana kabisa atasemaje...hilo katika dunia hii halipo tena.
Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Hi! I just want to offer you a big thumbs up for the
great info you've got here on this post. I am returning to your blog
for more soon.

Here is my website: Homepage besuchen ()