Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, June 5, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-71‘Mdada hebu tuambie baada ya tukio la kuuwawa kwa mtoza ushuru uligundua nini ndani ya nyumba yako,kulikuwa na mabadiliko yoyote?’ akaulizwa

‘Moja ya dirisha langu lilionekana halipo sawa, kuna mtu alilinasua na kufyatua vidude vya kuliwezesha kubana na kufunga vyema…’akasema

‘Kwa namna nyingine lilivunjwa …?’akasema wakili

‘Ndio….muheshimiwa’akasema mdada

‘Je dirisha hilo lilikuwa na matatizo kama hayo kabla’ akaulizwa

‘Ndio kabla ya hapo niligundua kuwa halifungii vyema,tofauti na ilivyokuwa awali, nikalirekebisha mwenyewe, kwa kuvinyosha vidude vilivyokuwa vimejipinda, …’akasema mdada

‘Kwahiyo dirisha hili sio mara ya kwanza kuvunjwa, kulazimishwa kufunguliwa?’ akauliza

‘Ndio..’akasema mdada

‘Uliwahi kumuuliza mlinzi wako kuhusu hilo tukio,maana kama ni mtu alifanya hivyo, ni lazima aliingia kupitia getini, …?’ akaulizwa

‘Niliwahi kumuuliza na yeye akasema hawezi kujua, na hakuna mtu aliyewahi kuingia, akasema huenda ni tatizo lilijitokeza wakati wa kufunga kwa nguvu, lakini mimi niliingiwa na wasiwasi kwani hayo madirisha wakati wa kufunga hayatumii nguvu, ila likishajifunga, ukiwa nje huwezi kufungua mpaka utumie pisipisi kukwanyua na hapo unaharibu uimara wake …’akasema mdada

‘Na ulivyoona ndivyo ilivyofanyika kuwa mtu alitumia pisipisi kulazimisha kulifungua kutoka nje?’ akaulizwa

‘Ndio, hata ukiangalia utaona michirizi ya kitu kama pisipisi imeacha alama, ipo dhahiri kabisa...’akasema

‘Hiyo michirizi uliigundua lini?’akaulizwa

‘Kwa mara ya kwanza sikutulia maanani sana, ila hii safari ya pili ilinifanya nichunguze kwa makini ndio nikaona hiyo michirizi...’akasema

‘Je ulipooa hivyo kwa hii mara ya pili na kugundua pia dirisha halifungi, ulifanya nini?’ akaulizwa

‘Nilipoona dirisha halifungi, nikaanza kuingiwa na wasiwasi, nikaanza uchunguza mle ndani, kama kuna kitu kimeibiwa, ni wazi ikitokea kitu kama hicho hisia za kwanza ni kuwa umeibiwa. Nilifanya utafiti kujua kama kuna kitu kimeibiwa, na nikagundua kuwa moja ya kabati langu ninapoweka vitu vyangu muhimu lilikuwa limevunjwa, mara nyingi silifungui hilo kabati…’akasema mdada

‘Ulifanya nini baada ya hapo?’akaulizwa

‘Nilifanya uchunguzi wa kitaalamu zaidi,mimi nina vifaa vya kuchunguza alama za vidole,kwahiyo nilijaribu kuangalia kama kuna alama zozote za vidole zilibakia hapo dirishani…’akasema

‘Uligundua alama gani au za nani?’akauliza na wakili mtetezi akaweka pingamizi lakini hakimu akasema swali hilo lijibiwe

‘Niligundua alama za vidole ni za mlinzi wangu…’akasema mdada

‘Mlinzi wako ndio huyo mshitakiwa namba moja kwenye kesi hii?’ akaulizwa

‘Ndio muheshimiwa…’akasema mdada na mimi nilijaribu kumuangalia huyo mlinzi,na nilimuona kama akitikisha kichwa kusikitika.

‘Je wewe unamuamini sana mlinzi wako?’ akaulizwa

‘Kwakweli namuamini sana mlinzi wangu, na hata baada ya kugundua hivyo, bado moyoni nilihisi huenda ni katika kuhakikisha kuwa dirisha limefungwa vyema, ndio maana alama hizo zilibakia, yeye kama mlinzi anaweza kufanya hivyo kuhakiki kama madirisha yote yamefungwa vyema...’akasema mdada

Msimamizi wa mashitaka hayo akasogea hadi pale pilipowea vielelezo, na kutoa kielelezo kimoja wapo, na kumuuliza mdada kama anakitambua na mdada akasema ni alama za vidole alizozichukua yeye tarehe imejionyesha na saa, kwani wakati unafanya hivyo vipimo, kila kitu kinajiandika, muda, na tareha ya tukio la kufanya uchunguzi huo.

‘Nawakilisha alama za vidolezilichokuliwa na mdada zikionekana wazi kwenye dirisha la mdada, na alama ya dole gumba lilipatikana kwenye mshikio wa kabati la mdada lililovunjwa,…..’akasema wakili na wakili mtetezi akatoa pingamizi na kusema;

‘Hvyo vielelezo vilichukuliwa na mtu ambaye hatuwezi kumkubalia, maana yeye sio ofisa usalama au mtaalamu wa kazi hiyo aliyetambulikana, na alifanya hivyo kwa utashi wake, na sio kwa utashi wa polisi waliopewa jukumu hilo….’akasema na muendesha mashitaka akasema;

‘Hajalishi ushahidi umechukuliwa na nani,kama ushahidi huo unakubalika kitaalamu, kutegemeana na muda, mahali na ukiangalia chombo cha kunasia hizo alama za vidole ni cha kitaalamu zaidi kinaonyesha hadi muda wa alama hizo za vidole kuwepo hapo,…na upo sahihi, mimi sioni kwanini uweke pingamizi hapo, mimi nawakilisha kama vidhibiti vya kimahakama…’akasema muendesha mashitaka na hapo kukatokea mlolongo wa ubishi hadi hakimu akaingilia kati na kusema

‘Ushahidi huo utapokelewa na kama utakuwa na ushawishi zaidi ,hatutasita kuutumia, na kama hauna vigezo au ushawishi mwingine utatupiwa mbali, hiyo sio kazi yenu mawakili, tuendelee…’akasema hakimu.

‘Mdada,hebu tuambie wewe unamiliki bastola?’ akaulizwa na mdada akainua uso bila kusita akasema.

‘Ndio muheshimiwa….lakini katika vitu nilivyoona kupotea siku hiyo ni pamoja na bastola yangu..’akasema na mimi nikashangaa kauli yam dada.

‘Ulipogundua hivyo ulichukua hatua gani?’ akaulizwa

‘Kwanza nilifanya uchunguzi wangu kama nilivyofanya kwenye kabati langu,na katika kuangalia alama za vidole niligundua alama ya dole gumba la mlinzi wangu, ….’akasema mdada na hapo  hata mimi nilianza kumshuku mlinzi wa mdada kuwa anahusika sana na hayo mauaji.

‘Ndugu muheshimiwa hakimu,nawakilisha ushahidi wa bastola ya mdada iliyokuja kugundulikana baadaye,ambayo ilichukuliwa kwenye kabati la mdada…’akasema muendesha mashitaka

‘Je kuna kitu gani zaidi uligundua kupotea?’akaulizwa

‘Kulikuwa na nyaraka za siri ambazo nilipewa na marehemu nimuhifadhie…’akasema mdada

‘Kwanini marehemu alikupa wewe nyaraka kama hizo uhifadhi wewe, kwani wewe ni mfanyakazi wa idara hiyo?’ akauliza

‘Yeye mwenyewe aliniambia kuwa hizo ni nyaraka muhimu sana, na anaogopa kuwa zinaweza kupotea, na ni ushaidi wake wa mambo yake, mimi sikutaka kumkatilia, nikazichukua, na alisema pia hakuna sehemu anayoiamini kwasasa akiipata atakuja kuzichukua ,kwahiyo mimi sikuona sababu ya kumkatalia, ilimradi ni kwa muda….’akasema mdada na wakili huyo akawa amemuangalia hakimu, ambaye alikuwa akindika jambo, na alipogeuka kumuangalia shahidi wake, akasema;

‘Endelea…kutoa maelezo...’

‘Na nilikuja kugundua kuwa hizo nyaraka ni moya ya vitu vilivyokosekana  kwenye kabati langu….’akasema mdada.

‘Ina maana viliibiwa na huyo aliyeiba ndio huyo huyo aliyevunja dirisha, na kuvunja kabati, na uiba hivyo vitu ikiwemo bastola,...na huenda bastola hiyo ilitumika kwenye uhalifu ikiwemo mauji’akasema wakili

Wakili wa utetezi akasimama na kutoa pingamizi akasema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu,kesi hii ilipoanza tulisikia kuwa bastola iliyotumika kumuua mtoza ushuri ni bastola yake mwenyewe aliyoingia nayo,hii bastola nyingine haina umuhimu kwenye hii kesi...na ni wapi imeonyesha kuwa ilitumika kwenye  uhalfu,...’akasema wakili huyo na hakimu akakubali pingamizi hilo.

‘Naishia hapa kwa sehemu hii, wakili mtetezi unaweza kuendelea...’akasema wakili muendesha mashitaka

*********

Wakili mtetezi hakuacha mbwembwe zake, akamsogelea mdada na kuonyesha alama za imani yake na kusema;

‘Kama kuna shetani na dalili zake zishindwe, niweze kuitafuta haki, shetani ushindwe kabisa.....’watu wakacheka, na yeye akiogopa hakimu atamkemea akasema

‘Katika imani za dini kabla hujaanza jambo ni vyema kujikinga na mabaya ikiwemo imani za mashetani, sio kwamba nafanya haya kwa kuwafurahisha watu....’akasema

‘Uliza maswali wakili, usipoteze muda....’akasema hakimu

‘Mdada, wewe unasema ulitumia utaalamu kuchunguza alama za vidole, huo utaalamu umeupatia wapi?’ akauliza, na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi kuwa swali hilo halina msingi kwani hayo ni mambo binafsi hayafungamani na hiyo kesi...

‘Nimeuliza hivi kwasababu vielelezo alivyovichukua vimewakilishwa kama ushahidi, tutaamini vipi kuwa huyu mtu hakugushi hivyo vielelezo, au kwenda kwa mtaalamu akavitengeneza...’akasema na hakimu aktulia kidogo, akasema hilo swali lijibiwe

‘Nimewahi kuhudhuria mafunzo ya vitu kama hivyo katika vyuo vinavyotambulikana, na kama unahitaji ushahidi ninaweza kuleta vyeti vyangu ,....’akasema

‘Kwahiyo kumbe wewe ni mtaalamu wa kuchunguza alama za vidole, kwanini ulichukua mafunzo hayo..?’ akauliza na wakili msimamizi akaweka pingamizi, lakini hakimu akasema lijibiwe, na mimi hapo nikaona kuna kitu hakimu anakitafuta.

‘Ni katika kuendeleza kipaji changu, mimi huwa napenda sana kuchunguza mambo kitaalamu zaidi..’akasema

‘Ulisema unapotokewa na ile hali, mmh, ya kibinadamu na ukatawalia na shetani, shetani ushindwe kabisa...’akasema kunyosha mkono kwa mdada, na watu wakacheka

‘Hebu niambie sio kwasababu uliogopa kuwa ulijuwa kuwa wewe ndiye uliyefanya hayo mauaji wakati umepoteza akili za kibanadamu ndio ukaanza kufanya huo uchunguzi ili uweze kumsingizia mtu mwingine...na ukijua kuwa mlinzi anaweza akaacha alama za vidole kutokana na kazi yake, ukaona huyo ndiye anayefaa kusingiziwa....’akasema na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi na hakimu akakubali hilo pingamizi.

‘Naomba nimjibu huyu muheshimiwa hilo swali kuwa mimi nina matatizo na hayo matatizo yanatambulikana kitaalamu, na nina dakitari bingwa anaweza kulithibitisha hilo, siwezi kusingizia kitu kama hicho, na ni kitu kinachonisumbua sana, usifikiri mimi naifurahia hiyo hali...’akasema mdada kwa sauti ya kuonyesha uchungu, lakini hakutaka kuonyesha unyonge.

‘Sijasema umesingizia huo ugonjwa, nimesema ugonjwa huo upo, na kweli unao na unakubalika sawa kutokana na dakitari wako bingwa,...na kama ulivyosema ugonjwa huo ukikutokea unakutoa kabisa katika hali ya kawaida ya kibinadamu si ndivyo ulivyosema...’akawa kama nauliza na mdada akawa anamuangalia tu.

‘Ndivyo ulivyosema wewe mwenyewe kuwa hali hiyo ikikuingia unaweza kufanya jambo usilikumbuke, na unaweza hata kuua, kama ulivyomua mtoza ushuru, usikumbuke kabisa si ndio hivyo....?’akasema wakili huyo na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi kuwa wakili huyo anazidi kuliongelea jambo ambalo limeshawekewa pingamizi, na kufanya hivyo anataka kuvuruga utaratibu...’

Wakili mtetezi akasema huku akimuangalia hakimu;

‘Mimi nilikuwa namjibu shahidi wake, kumfafanulia kile alichokisema, sikuwa nauliza swali, sijavuruga utaratibu hapo...’akasema na alipomuona hakimu yupo imiya akamgeukia mdada, huku akisema;

‘Unasema kati ya vitu vilivyoibiwa ni pamoja na nyaraka za siri, ambazo ulipewa na marehemu, sijui ni siri kinamna gani, ....lakini kuna tetesi kuwa wewe na marehemu mlikuwa marafiki kabla, bila kujali huyo ni mume wa mtu,...’akasema na wakili muendesha mashitaka akatoa pingamizi, lakini wakili huyu akaendelea kuongea

‘Urafiki wenu baadaye ukaanza kulega lega, kama kama kawaida yak oleo huyu kesh yule hayo yapo wazi huna haja ya kuyakubali, nazungumza kwani mimi ni mwanajami na namfahamu mdada....’akasema na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamzi kuwa wakili huyo anaingilia mambo binafsi, ambayo hayana msingi kwenye hiyo kesi, na hakimu akamuonya huyu wakili, na wakili huyo akasema

‘Samhani muheshimiwa hakimu, lakini mimi nilikua najaribu kuelezea hali halisi iliyosababisha hayo yote, hayo yaliyotokea hapo yana historia pana...’akasema na bila kujali, akaendelea kuongea

‘Kutokana na kukorofishana kwenu, kukosana kwenu, wewe hukutaka kumrejeshea marehemu nyaraka zake ndio maana akaja juu, siku hiyo mauti yalipomkuta, alishasema basi liwalo na liwe, ndio maana alikuja na bastola...’akasema wakili huyo na wakili muendesha mashitaka akasema

‘Muheshimiwa hakimu, wakili mtetezi anatoa maelezo, badala ya kuuliza maswali, je huo ndio utaratibu na wakili akamuonya tena huyo wakili na wakili bila kujali onyo hilo akasema

‘Mdada, sema ukweli, hayo niliyozungumza nakusingizia ...?’akasema kama anauliza na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamizi kuwa wakili anatoa maelezo yasiyo na msingi wa hoja na ushahidi, na anamshinikiza shahidi kujibu maelezo aliyoyatoa mwenyewe huyo wakili na hakimi akakubali hilo pingamizi, na kusema;

‘Wakili mtetezi, nakuonya tena, fuata utaratibu wa kiuwakili,....’akasema hakimu na wakili huyo akasema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, haya ninayoeleza naweza kuja kuyatolea ushahid kama yakihitajika, lakini kwa hivi sasa ninachotaka mahakama yako tukufu ifahamu ni kuhusu  tabia ya huyu mdada, yeye anachofanya hapa ni kujaribu kuficha ukweli, kwa vile marehemu sasa hivi hayupo hapa, ndio maana anasema kuwa  alichokuwa amekifuata marehemu ni nyaraka za gari lake, kitu ambacho sio kweli, ...’akasema na wakili muendesha mashitaka akasema;

‘Thibitisha kauli yako kwa ushahidi na vielelezo, sio kwa hisia zako...’  wakili muendesha mashitaka akasema

‘Ninaweza kuthibitisha hilo kwa majibu kutoka kwa huyu shahidi yako mwenyewe, mpe nafasi ajibu...’akasema na hakimu akaingilia kati na kumwambia wakili mtetezi aulize maswali na sio kutoa maelezo yake binafasi.

‘Unadai kuwa nyaraka za siri ulizokuwa nazo zilikuwa kati ya vitu vilivyoonekana kutoweka kwenye kabati lako , na wakati huo umedai kuwa marehemu alikuwa kuchukua nyaraka za gari lako, kwanini aje nyumbani kwako, wakati kazi kama hiyo ni ya kiofisi...?’ akauliza na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamzi, na hakimu akalikubali hilo pingamizi.

‘Ndugu muhehimiwa hakimu, nahitaji mdada ayajibu maswali yangu ili kuthibitisha kuwa marehemu hakuwa amefuata nyaraka za gari, marehemu alikwua amefuata hizo nyaraka za siri, na hizo nyaraka za siri, mdada alishaziondoa hapo, na alichofanya yeye ni kuvunja hilo kabati, ili ije ionekane kuwa mtu mwingine aliingia akafanya hivyo...’akasema wakili na wakili muendesha mashitaka akaweka pingamzi kuwa wakili huyo anatoa maelezo yake anavyohisi yeye, hayana msingi na hitimisho la hoja.

‘Mdada kwanini unamiliki silaha?’ akauliza swali

‘Kwasababu raia yoyote anaweza kufanya hivyo,..na nina kibali cha kufanya hivyo...’akasema

‘Kwahiyo wewe ni mtaalamu wa kutumia silaha...?’ akaulizwa

‘Ndio nafahamu kutumia silaha, nisingeliichukua kama pambo..’akasema mdada

‘Na  hata ukipotewa na fahamu zako unaweza kuitumia hiyo silaha..’akasema na mdada akacheka na kusema

‘Nikipotewa na fahamu sijui kinachoendelea, ...na nimeshakuambia ili ujue vyema kuhusu tatizo langu dakitari wangu yupo anaweza kuja kutoa maelezo, ya kuwa mimi nikiwa katika hiyo hali sihitaji silaha,...’akasema

‘Utajuaje kuwa huhitaji silaha, wakati hujitambui...huoni kuwa unaidanganya mahakama, wewe ulipopotewa na fahamu ya kibinadamu uliweza kufanya lolote ikiwemo kuua,...’akasema wakili huyu akiongea kwa haraka haraka, bila kujali pingamizi la hakimu.

‘Nna hutaki kukubali tu kuwa wewe ndiye uliyemuua mtoza ushuru, kwasababu ulikuwa na hasira naye,na yeye alikuwa mwanaume, na yeye mlishakorofishana kwenye mambo yenu, na kwa vile alikuja kufuatilia hizo nyaraka ambazo wewe ulizichukua kwa lengo la kuzitumia kum-black maili, ili akutolee gari lako bure...na hiyo ndio tabia yako, ya kuwarubuni watu, kwa kutoa mapicha mabaya, na baadaye kuwadai pesa ili upate unachokihitajia,..naweza kutoa ushahidi wa hili, ninao ushahidi...nasema ninao ushahidi...’akawa anasema kwa jaziba

‘Sio kweli....’akasema mdada kwa sauti na ilikuwa sauti nzito kidogo, mimi pale nilipokuwa nimekaa nikaanza kusimama, na wakati huo wakili muendesha mashitaka aliuwa akiweka pingamizi lakini wakili huyu akaendelea kuongea, na akimu akawa anamuangalia kwa mshangao....

‘Hata huyo mhasibu umemtumia kwa njia hiyo hiyo, ulimchukua picha mbaya ili aweze kuingia kwenye anga zako, kubali hayo ili haki itendeke usitake, kumsingizia mlinzi wako kwa kosa ambalo hakulifanya, kubali kuwa wewe ndiye uliyeua...kubali ili damu uliyoimwanga isifukiwe hivi hivi, kubali haki itendeke, kubali kubali...’akaendelea kuongea kama wahubiri wanavyofanya bila kujali pingamizi huku akimnyoshea mdada mkono juu chini...

‘Stop...’akasema mdada kwa sauti nzito, sauti iliyofanya chumba kizima cha mahakama kuwa kimiya, na wakili mtetezi naye akatulia ghafla kumuangalia mdada, na walipokutanisha macho yao, wakili huyo akaanza kurudi kinyume nyume, na nilipomuangalia mdada nikamuona akianza kutikiswa, na mara akaanza kutoa mngurumo kama wa simba....

NB: Jamni tuendelee kidogo hapo?,.....mmm samahani kidole kinauma...

WAZO LA LEO: Kila mtu ana mapungufu yake na wengine wanajijua kuwa wana mapungufu hayo , na mbora wa hayo ni yule anayekubali na kutubu, lakini kuna wengine wanajijua, lakini hawataki kukubali kuwa wana mapungufu hayo. Hawa ni wale wenye tabia za uwongo, wanafiki, mafisadi.

 Kuna watu wana tabia za uwongo na uzushi kwao  ni starehe, na hawajali athari za uzushi huo kwa wengine. Uwongo, uzushi, propaganda potofu,utesi  ni tabia za hawa watu. Na watu hao, ni wanafiki kwani hawaaminiki, wanapenda kusema uwongo, kuwazulia wenzao mambo wasiyoyafanya, ili tu kukidhi matakwa yao,na watu hao hawatekelezi amana walizokabidhiwa hasa wakipewa madaraka.


Jamani mkiwa na tabia hii mukajijua ni bora kutubu, kwani ni dhambi , na unapowafanyia wengine wanaumia, kama ungeliumia wewe ukifanyiwa hivyo hivyo, huo ni ufisadi, huo ni unafiki, tuuache. 

Ni mimi: emu-three

No comments :