Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeFriday, May 30, 2014

BAADA YA DHIKI NI FARAJA-67
 Kwanza mdada aliniangalia kwa makini, kama ana wasiwasi na mimi, halafu akageuka na kuanza kutembea ule mwendo wa kiaskari ujulikanao kama mwendo-pole, alitembea hivyo hadi kwenye kabati kubwa lililokuwa hapo varandani

Akatoa ufunguo na kufungua hilo kabati, akawa anavuta kitu, na mara akatoa mfuko mkubwa wa nailoni

Aligeuka na huku ameushikilia ule mfuko wenye kitu ndani yake akanisogelea na kuja hadi pale nilipokaa, akauinua huo ule mfuko, na nilipoangalia vyema ndani ya huo mfuko nikaona mkoba,(briefcase), lakini ni hizi briefcase za kawaida tu, na akili yangu kwa haraka ikakumbuka kuuona huko mkoba mahali, ....

‘Ule mkoba (briefcase), niliiona wapi vile...ooh, ndio...’nikawa nasema kimoyo moyo, na mdada alipoinua juu ule mfuko wa nailoni, ili nione kilichope ndani yake, alisema;

‘Huu mfuko nimeuchukua chumbani kwako,…..kabla polisi hawajafika, mimi nilikuwepo chumbani kwako....’akasema

‘Ulifika saa ngapi?’ nikamuuliza

‘Nilifika muda ule ule uliofika wewe...’akasema

‘Hao polisi, walikuwa wakivitafuta hivi vitu vilivyopo humu ndani…’akasema mdada nilibakia nimeduwaa huku nikimkodelea macho mdada, kwa kutoamini maneno yake kuwa alifika muda nilipofika mimi, na kwanini sikumuona, baadaye nikasema;

‘Haiwezekani….’nikasema sasa nikiuangalia ule mfuko wa plastiki na ndani yake ule moba ulionekana dhahiri, na sikuwa na shaka, utakuwa ni ule mkoba aliokuwa nao mmoja wa wale jamaa wawili waliofika hotelini kutaka kuweka kitu ofisini kwangu...

Tuendelee na kisa chetu

**********
`Unasema haiwezekani,hahaha masikini mhasibu, mimi sio mwenzako....’akasema mdada akiinua ule mfuko , halafu akauweka ule mfuko sakafuni mbele yangu akasema;

‘Kama haiwezekani, hivi vitu nimevipata wapi, na wewe jiulize kwanini polisi hawakuvipata vitu walivyokuwa wakivitafuta wakati wewe mwenyewe uliona wale jamaa wakiviweka au wakitaka kuviweka kwenye chumba chako....’ akasema sasa alikuaj kukaa karibu yangu, na mimi nilibakia kimiya nikiendelea kuangalia ule mfuko uliokuwa umewekwa huo mkoba.

‘Wewe niulize ilikuwaje....’akasema mdada na mimi nikahema, na nikasogea nyuma na kukaa vyema kwenye sofa nikiwa kama naogopa kabisa kukaribia huo mfuko na mdada akaendelea kusema;

 ‘Mimi nilifika kwako hotelini pale wakati unaoga, nilikuwa nyuma yako, sikuwa na shaka ya kujificha sana, nikijua utaniona ukigeuka, lakini haikuwa hivyo......ulipoingia ndani, ukafunga mlango. Hukufunga kwa ndani, niliponyonga kitasa mlango ukafunguka, nikaingia ndani, na ili kujua wapi upo,  nikaipiga simu yako, nikaisikia ikiita chumbani kwako,nikaingia na kumbe ulikuwa bafuni....’akasema.

‘Unakumbuka wakati unaoga,simu yako iliita ,….mimi ndiye niliyepiga,  kujua utachukua hatua gani, na hakutoka haraka bafuni, ....mimi nikachukua nafasi hiyo kujificha sehemu ambayo hata ukirudi usingeliniona kirahisi, nilitaka kuona unataka kufanya nini.

‘Cha ajabu, kukuthibitishia kuwa wewe haupo makini, hata ulipotoka bafuni hukutaka hata kukagua kagua chumba chako, ulichokimbilia kuangalia ni simu yako,...’akasema

‘Na nilikuona ukiwa na mwazo sana, labda ulikuwa ukiwaza jinsi gani ya kuongea na baba mkwe wako, ...ningeweza kukuambia usihangaike kwenda huko, lakini akili yangu ilinituma nisikushitue....’akasema

‘Wakati nataka kujitokea ili unione, wewe ukawa unavaa  kwa haraka, nikaona nikupe muda, nikijua utageuka kuangalia upande ule nilipokuwa nimejificha, simu yangu nilikuwa nimezuia sauti kusikika, ila nilihisi kuna ujumbe umeingia, nikawa nausoma na wewe ukawa umeshatoka nje ya chumba chako...’akasema

‘Wewe ni mtu wa ajabu sana, kiukweli mimi ukiingia ndani na kujificha, kuna hali inanionya, nahisi kitu mwilini, nywele sinasisimuka lakini wewe, mmmh, inatisha.Lakini mhasibu mimi ninakupa ushauri wa bure, siku zote ukifika sehemu hata kama ni nyumbani kwako, hebu jaribu kuwa makini sana….utakuja kuwawa kirahisi tu…’akasema

‘Mpaka sasa siamini….ina maana muda wote ulikuwa mle ndani?’nikauliza kwa mshangao.

‘Ulipotoka hapo chumbani kwako ulionekana kuwa na mashaka,nikajua utaweza kunigundua, lakini hukuwa makini kuangalia tena ndani hukutaka kuitumia vyema hisia yako ya sita, hisia inayokuashiria jambo, ni hisia ambayo ukiitumia vyema unaweza kuhisi kama kuna hatari  karibu. Ulipotoka tu nikajiweka sawa na mimi kukufuata ili nikuambie kuwa hutaweza kuongea tena na baba mkwe wako umeshachelewa, lakini nikarudi nyuma haraka baada ya kupokea ujumbe kutoka kwa wangu…’akatulia kidogo

‘Nikiwa hapo nikapata taarifa kwa ujumbe wa maneno kuwa kuna hao jamaa wawili wamekuja huku juu, na wamebeba mkoba, tofauti na ile mikoba yao, ya kikubwa,na watu wangu wakautilia mashaka, wakawa wanawasilia na askari waliopo kwenye kundi langu....’akasema

‘Ina maana una kundi lako lenye maaskari?’ nikamuuliza na yeye akanitupia jicho, na hakujali swali langu akaendelea kusema;

‘Mtu wetu upande wa polisi akasema kuna taarifa kuwa kuna vitu muhimu vilivyokuwa vikitafutwa na polisi kama ushahidi vimebainika kuwa vipo ofisini kwako, kwahiyo kuna watu wanaandaliwa kuja huko....’akatulia

‘Hapo machale yakanicheza, nikaona kwa ahli ilivyo ni bora nisikutane nawe wanza, nikawaambia watu walifuatilie hilo jambo, na wanipe taarifa haraka iwezekanavyo...mimi nina vijana wanaojua kazi, ukiwaambai jambo, wanajua umuhimu wake, wakanipa taarifa kuwa hao jamaa wawili walionekana kuja huku juu, walikuwa na huo ushaidi, inaonekana wanataka kuuweka huko ofisini....

Vijana wangu wakawasiliana na mtu wetu aliyekuwa upande wa utawala wanakofanya kazi hao watu, tukapata taarifa kuwa kuna mpango wa kuhakikisha kuwa wewe unakamatwa, na hicho cheo kinahtajika kwa mtu mwingine, kwahiyo wewe unaandaliwa uonekane kuwa ndiwe uliyemuua, mtoza ushuru, na ushahidi kamili umeshatayarishwa....’akasema

‘Niliposikia hivyo nikajiandaa kufanya lolote, maana ukikamatwa wewe, na kwa jinsi ninavyokufahamu unaweza kuropoka ovyo,..na pili nilitaka kujua huo ushaidi ni kitu gani, nikataka  kukukimbilia kukuonya, lakini nilikuwa nimehachelewa,nikavuta subira, baadaye nikatoka kuangalia ni nini kinachoendelea na wakati natoka nikakuona ukikimbilia kwenda chini...nikawasiliana na watu wangu wakufuatilie..’akatulia

Mimi nikahisi kuna jambo unalikimbia, nikasubiri, ...nikaona sehemu nzuri ya kusubiria ni chumbani kwako, huku nikiwasiliana na vijana wangu, nikiwa nawaza nifanye nini, mara nikasikia mtu akifungua mlango wa chumbani kwako,kwa haraka nikajificha  pembeni mwa kabati la nguo. Nilijua ni wewe umerudi,...kumbe ni wao.

Nilifanya vyema kujificha humo chumbani kwako, kwani walipoingia humo, hao jamaa, wakiwa na huo mkoba, waliangaza huku na kule, sikujua kwa muda huo wanatafuta nini, na mmoja akasema;

‘Tuuweke chini ya kitanda, ionekane alikuwa anauficha....’akasema mmojawapo Na wakakubaliana hivyo,wakaelekea chumbani kwako, na kuuweka huko huo mkoba chini ya kitanda, na kwa haraka wakatoka mbio. Na niliwasikia wakisema polisi wanakuja, na lengo lao litakamilika walipotoka mimi kwa haraka,nikawasiliana na watu wangu wakanipa habari ya kinachoendelea.

Nikawaambia wanilinde,kwani nilihitajia muda ili niweze kuuchukua huo mzigo, nikaangaza huku na kule na bahati nzuri, nikaona huo mfuko wa plastiki,na sikupoteza muda nikainua godoro na kuuona huo mkoba nikauweka ndani ya huu mfuko, nikiwa na tahadhari zote nisiuguse kitu bila kinga ya mkononi, nikauweka huo mkoba kwenye mfuko na nailoni, nikatoka nao.

Sikutaka kutoka na kuteremka chini na huo mzigo  kwa muda huo, kwani nilijua ningelionekana, japokuwa vijana wangu walikuwa chini wakifuatilia, na ningeweza kuwaelekeza nikajua wapi pa kutokea, lakini nilichofanya kwa muda huo ni kutoka kwenye chumba chako na kuingia chumba cha jirani....’akasema

‘Chumba cha jirani cha nani?’ nikauliza na moyoni nilihisi kitu kama wivu, sijui ni kwanini na mdada akatabasamu na kuangalia pembeni halafu akasema;

‘Kuna chumba nilikichukua karibuni kwa kazi zangu…’akasema na mimi nikamuangalia mdada bila kummaliza na yeye akaendelea na maelezo yake kwa kusema;

‘Nilipofika kwenye hicho chumba nikasubiri, vijana wangu wakiwa wananipa kila kinachoendelea, na polisi walipopanda juu, wakielekea ofisini kwako, nilikuwa nafahamu. Ila sikujua kwa jinsi gani walifahamu kuwa huo mzigo unaweza kuwa kwako, hii inaonyesha kuwa kuna mpango uliopangwa na hao jamaa wawili na hao polisi,....’ akasema

‘Baadaye wakaja chumbani kwako, nafikiri walikuwa wameshaelekezwa wapi wakakague, hapo nilisubiri hadii polisi walipomaliza msako wao,na walipokosa hicho walichokuwa wakikitafuta walitoka nje, na wakawa wanapigiana simu na wenzao, kwa muda huo nilikuwa nimesimama mlangoni nikiwa wachungulia kwenye upenyo wa mlango.

‘Nilisikia wakisema; twendeni, hakuna kitu hapa..muda wa zoezi hili umekwisha...naona zoezi hilo lilikuwa na muda maalumu, wakaondoka na kurudi huko walipotoka,na mimi nikarudi kwenye hicho chumba changu na kitu nilichofanya ni kukagua ni kitu gani kipo humo ndan, nikimaliza niurudishe huo mzigo hapo nilipouchukua..’akasema

‘Niliufungua huo mkoba na nilifanya zoezi hilo kwa haraka na kitu kilichonishutka sana, ni kuona humo ndani kuna bastola, na zile nyaraka zilizoluwa zikitafutwa na nyaraka nyingine nilizokuwa nazo mimi ambazo ndizo marehemu alikuwa akizitafuta...’akatulia akionyesha hisia ya mshangao usoni.

‘Kulikuwa na bastola, oh, hiyo bastola ilikuwa  ya nani?’ nikauliza na yeye akaangalia ule mkoba pale chini, akausogelea na akiwa amevalia kinga mkononi mwake, akautoa ule mkoba, na kuufungua na dani yake kulionekana bastola, mimi nilihisi mwili ukiisha nguvu.

‘Mungu wangu, ina maana walitaka kunibambikia kesi ya mauaji, mimi sijawahi kumilii bastola, hiyo bastola ni ya nani, na kwanini watake kuniwekea mimi....?’ nikawa nauliza maswali mengi, na mdada akawa anaufunga ule mkoba na kuurudisha kwenye ule mfuko wa nailoni akaubeba na kuuweka kabatini kwake na kulifunga lile kabati, akasema;

Hiyo bastola ni ya kwangu....’akasema na kuniangalia machoni, na mimi nikabakia mdomo wazi.

NB: Mambo hayo...nawamegea tu kidogo, kutokana na muda, na diary yangu inataka kutoa tukio la wiki lilitokea karibuni huko maeneo fulani.

WAZO LA LEO: Ubinadamu sasa umekwisha, wiki hii kulitokea kisanga huko eneo la Kipunguni Moshi Bar. Ni tukio la namna yake, la kuokota mamilioni kadhaa ya pesa,zilizodondoshwa na gari moja likiwa kwenye shughuli za kibiashara. Nahisi walidondisha kwa bahati mbaya, na sijui watakuja kusema nini kwa muajiri wao.

‘Tuliliona lile gari, likgeuza baada ya kumaliza kazi waliyokuwa wakifanya, na wakati linageza tukaona mfuko ukidondoka toka kwenye hilo gari, na kwa muda huo hakuna aliyehisi kuwa ule mfuko una pesa, na mara likapita gari jingine na kuukanyaga ule mfuko, ukapasuka....

Pale karibu yake klikuwa na mtoto anacheza, akauona ule mfuko, na sisi tuliokuwa mbali tukaona jinsi gani yule mtoto alivyoshangaa, kashika mdomo na mkono kama aliyeona kitu cha kutisha au cha ajabu, na alipouliza kaona nini akisema;

‘Pesa....’ na hapo wote tuliokuwepo pale macho yetu yakafunguka kuangalia ule mfuko uliokuwa barabarani ukiwa sasa umepasuka, na rangi nyeundu za pesa zikanasa macho yetu,..jamani pesa ni shetani...

Kila mwenye shughuli yake akaacha, na mioyo yetu ikaanza kupiga, na kila mmoja akifirikia jinsi ya kuruka pale tulipokuwa hadi pale penye hizo pesa. Hakuna aliyefikiria jinsi gani ya kumpata mwenye lile gari, ili azipate dhamana zake.

Kwa vile pale ni barabarani, wanapita watu wengi, na muda ule kulikuwa na vijana wanapita wakikimbilia maeneo ya Moshi Bar, kwenye mishemishe zao, na wao wakaziona zile pesa, na sisi tuliokuwa mbali,tulishaanza kujongea pale, na kulaani kwanini hatukufanya haraka, na mmoja wetu nafikiri ni yule mzazi wa yule mtoto akawa anamuita yule mtoto aziokote zile pesa haraka, akachelewa, mmoja wa wale vijana wapiga debe, akaziwahi...

Purukushani zikaanza hapo, kwanza kwa wao wenyewe kwa wenyewe, hakuna ati yao aliyeweza hata kuuliza hizi pesa ni za nani, wao walichofikiria ni kuzichukua hizp pesa na kukimbi nazo.

‘Ni zangu, nimeziona mimi...’ waaanza kugombana wao wenyewe kwa wenyewe, na yule aliyeziwahi mkononi, akatoa kiasi cha pesa na kuwapa wenzake, wenzake wakasema;

‘Hapana sisi tunataka hizo pesa tugawane sawa kwa sawa, huwezi kutupa kiasi hicho kidogo,..hali ile litufanya na sisi tuliokuwa mbali tukimbilie pale, na yule kijana, ni hawa wapiga debe, alipoona hivyo akaanza kutimua mbio na zile pesa..

Watu tukaanza kumkimbiza, utafikiri mnakimbiza mwizi, watu wakazidi kuongezeka, kila aliyepata taarifa hiyo akawa anafukuzia huko, na kila aliyemkaribia huyo mpiga debe, alipewa kiasi, akikipokea anaona hakitoshi, anaendelea kumfukuza huyo jamaaa..jamaa alikimbia utafikiri mwizi...akawa anakatisha kwenye majengo ya watu akiruka ukuta, na kila aliyemkaribia alipewa kidogo.....

Sijui aliishia wapi , na sijui kama yeye atasalamika, maana wale wenzake walishageuka wanyama wanataka hata kumdhuru ili tu azitoe hizo pesa zote...

Jamani ubinadamu umekwisha...badala ya watu kusema tumeona hizo pesa ni za nani, au ni nani kazidondosha tuzihifadhi na tuweze kumuwakilishia mwenyewe, kila mmoja anawazia kuwa ni zake, anataka kuzipata , tunagombea jasho la wengine...’akamalizia kusema

‘Hivi kweli ukipoteza kitu kama pesa, unatarajia kuzipata, siku hizi simu ukidondosha mwenzako akiwa nyuma yako akaiona, akiipata mkononi imeshakuwa yake....hilo la ubinadamu wa namna hiyo sasa sahau...’akasema mwenzake.

Jamani hali ngumu za kimaisha, umasikini uliokithiri, kupungua maadili ya dini kunamgeuza mwanadamu kuwa mwingine kabisa,ni heri ukutane na mnyama sasa hivi kuliko kukutana na mwanadamu aliyekengeukiwa. Hivi sasa utu, huruma upendo hakuna tena, watu wanatumia nyumba za ibada, wanajivika vazi la ucha mungu, lakini moyoni mwake anawaza mali,jinsi ya kupata pesa,jinsi ya kuhadaa watu ili achume zaidi na zaidi ....utu sasa umeyeyuka, ..kinachotawala kwenye nyoyo za binadamu hisia za changu, hata kama sio chako....


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Anonymous said...

Kweli kaka Mira dunia imelewalewa mpk walimwengu tumelewalewa