Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Thursday, May 29, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-66



Cha msingi asichokitaka yeye ni kuingilia mambo yake, kuwaharibu mabinti wadogo, na wanaume wanaowatesa wake zao, ...hayo kayafungia kazi na amefanikiwa sana hapa mjini, kila mwanamke akionewa anakimbilia kwa huyo mama, kama kuna binti kabakwa huyo mama anatafutwa....

‘Ole wao umbake binti wa shule, huyo mama atalifungia njuga hadi mbakaji apatikane na akipatikana cha moto atakiona...na ni lazima atafungwa, na akitoka huu mji ataukimbia......

Uwe makini naye, yule binti mjanja sana,...akikuweka kwenye kona zake, atakuumiza huku anacheka....hebu jiulize mtoto mzuri kama yule kwanini haolewi, kila aliyejaribu kumuoa sasa ni marehemu, angalia huyo mtoza ushuru, yupo wapi...chunga sana kujuana na huyo binti...

Hayo maneno yakawa yananireeja kichwani mwangu hadi nafika maeneo ya nyumba ya Mdada bila hata kujitambua, nikaoitiliza gari langu hadi mbele kidogo nikafanya kama kawaida yangu, kumkabidhi mtu hilo gari alinilidnie na mimi nikatembea kwa miguu hadi nyumbani kwa mdada, nikagonga hodi kwenye geti na akaja mlinzi, huyu alikuwa mlinzi mwingine aliyeajiriwa na mdada.

‘Habari yako ndugu...’akanisalimia

‘Nzuri nataka kuonana na mdada...’nikasema

‘Una miadi na yeye?’ akaniuliza

‘Ndio wewe mwambie mgeni wake mhasibu amefika...’nikasema

Akaniangalia kwa makini halafu akasema;
Mbona kama nakufahamu vile..’akasema

‘Kamwambie mdada kuna mgeni wake, ananisubiria ....’nikasema kwa sauti ya hasira kidogo, nilikuwa nimekasirika, na nilitaka niwe na hali hiyo hata nikikutana na mdada

‘Sawa bosi, lakini usiingie na hasira kwa bosi wangu, hataki hali kama hiyo, ukiwa na hasira zako ni bora utulie kwanza ndio uonane naye, vinginevyo hamtaelewana, atakufukuza....’akasema

‘Namuelewa,....’nikasema na yeye akagauka kuondoka , lakini kila mara akawa anageuka kuniangalia, nahisi alikuwa akiniwazia jambo fulani, baadaye akarudi na kusema;

‘Unaweza kwenda, gari lao lipo wapi?’ akaniuliza

‘Sikuja na gari...’nikasema

‘Umepita nalo hapo....nilikuona....’akasema na mimi nikamwangalia kwa mashaka nikasema;

‘Fanya kazi yako na usichunguze chungeza masiha ya watu wengine unanielewa...’nikasema

‘Nimekuelewa bosi.....’akasema na mimi nikatembea hadi kwenye mlango wa nyumba ya mdada, nikahisi nywele zikinisisimuka, nilihisi kitu kikinipa wasiwasi, mpaka nikageuka kuangalia nyuma, nilimuona yule mlinzi akiongea na simu huku ananiangalia mimi...

‘Huyu mtu ana jambo na mimi...’nikasema kimoyo moyo, nikagonga mlango na sauti ya mdada ikasema;

‘Ingia , mlango upo wazi.....’nikafungua mlango na kuingia ndani.
Mdada alikuwa amekaa kwenye sofa huku miguu kailaza kwenye sofa na laptop mapajani, alikuwa akifanya jambo kwenye hiyo laptop yake, na hakuniangalia moja kwa moja nilipoingia, ....baadaye akasogeza miguu, na kuniashiria niende kukaa pale kwenye sofa alilokalia yeye,nikasita;

‘Karibu njoo kaa hapa, ili nisikie unachoongea, nina mambo mengo ya kufanya, ukiwa mbali sitakusikia...njoo hapa...’akasema na kuashiria nikae pale alipoweka miguu yake, nikasogea na kukaa, akainua miguu kidogo, na mimi nikakaa, akaniashiria nisogee, ili miguu yake ikae mapajani mwangu, sikupenda hiyo hali maana nilikuwa na hasira zangu lakini kwa mdada, nilijikuta nafanya kila atakacho.

Nikakaa kama alivyonielekeza lakini kwa mbali kidogo na miguu yake, na yeye akasema;

‘Sogea kidogo huku nataka miguu yake ikae vyema....eheee, okey, mbona unakuwa akma unaniogopa kulikoni leo...’akasema na kuniangalia usoni.

‘Nimekuja kwa dharura, na ni muhimu sana tukaongea , kwani nahisi hali sio shwari, muda wowote polisi wanaweza kunikamata...au kutukamata...’nikasema na yeye akaendelea kuandika kitu kwenye laptop yake alipoona nimetulia akanitupia jicho na kusema;

‘Ehee, endelea nakusikiliza....’akasema
Nikaanza kumuelezea jinsi ilivyokuwa toka mwanzao kule hotelini, hadi kwa shangazi, lakini sikumuelezea aliyoniambia yule fundi wangu wa gari...

‘Okey,...sasa...mmh, hebu kidogo....’akasema na kuendelea kuandika jambo, halafu akawa anataka kuifunga laptop yake lakini akasita, akainua uso kuniangalia kama kwa kujifichaficha kuniangalia moja kwa moja, akasema;

‘Umemaliza maelezo yako...?’ akauliza

‘Mdada hili ni tatizo kubwa mbona unalichukulia kwa wepesi...’nikasema

.........

‘Kwahiyo wewe una wasiwasi gani?’ akaniuliza mdada, sasa akiwa ananiangalia moja kwa moja usoni.

‘Ina maana wewe huoni kuwa polisi walichokuwa wakikitafuta wameshakipata…’nikasema

‘Polisi walikuwa wakitafuta nini?’ akaniuliza mdada, kama vile hayo yote niliyomuelezea awali hakuyasikia, na mimi kwa vile nilishamjulia nikaona niende naye hivyo hivyo,nikasema;

‘Walikuwa wakimtafuta huyo mtu aliyekuwa na ndevu ambaye aliongea na mlinzi,na  kama ujuavyo  wao wanaamini kuwa huyo mtu ndiye wanayehisi kuwa ndiye muuaji..’nikasema

‘Kama ni hivyo kwanini walimkamata mlinzi wangu, na wakasema wana ushahidi wa kutosha kuwa huyo mlinzi ndiye aliyefanya hayo yote, si kila siku unasikia yanayoendelea huko mahakamani...?’ akaniuliza

‘Wanasema mlinzi hakuwa peke yake kulikamilisha hilo, .....’nikasema

‘Na hao polisi wanasema wamepata ushahidi, na wameshamfahamu huyo mto aliyekuwa na ndevu wanasema huyo mtu ni nani?’ akaniuliza na mimi kwanza nikamuangalia mdada, kwa hali ya kutahayari kwani niliona kama hayupo na mimi, nikijitahidi kuwaza nini lengo lake la swali hilo mimi nikasema;

‘Wewe unafahamu fika kuwa huyu ni nani, unafahamu fika kuwa huyo mtu ni mimi, …’nikasema na yeye kwanza akashikilia ile laptop akitaka kuifunga, halafu akaangalia kitu alichokuwa akikiandika, na baadaye akainua kichwa kuangalia pembeni, hauniangalia moja kwa moja sasa akatabasamu huku akiwa anajikuna kichwani, alikuwa kaweka nywele zake ovyo ovyo, nahisi alikuwa na mpango wa kwenda saloon,akasema;

‘Unaonaeeh, kumbe polisi wanamtafuta huyo mtu ambaye alikuwa na ndevu si ndio, na hii ni kutokana na maelezo ya mlinzi, kuwa huyo mtu ndiye aliyeongea na mlinzi, au sio...na yeye, ndiye wanayemshuku kuwa huenda kahusika na hayo mauaji...’akatulia kidogo na kupitisha mkono wake kichwani, na akasema

‘Kwa maana nyingine, polisi sasa wanaamini maelezo ya mlinzi kwa vile wamepata  ushahidi wa hizo ndevu au sio, na kwahiyo wanaanza kuamini kuwa alichosema huyo mlinzi kumbe ni sahihi, ...kwa hali hiyo sasa polisi sasa wanaanza kuyafanyia kazi maelezo ya mlinzi, ni muhimu kuyaangalia maelezo yake kwa kina, je sisi yanatugusa vipi, unaona point yangu hapo...’akatulia kidogo.

‘Na kutokana na maelezo yako wewe, huyo mtu aliyekuwa na ndevu ni wewe, na kwahiyo polisi wanakutafuta wewe, au sio? Sasa nikuulize swali  mimi nahusika vipi hapo, na kwanini kama ni hivyo maana wewe unajifanya mwaminifu kwanini hujajipeleka polisi, ukawaambia jamani ulimi uliteleza, niliyosema awali sio sahihi mimi ni yule mtu mwenye ndevu.....’akasema mdada na kuniangalia mimi moja kwa moja usoni

‘Mdada una maana gani kusema hivyo, `wewe unahusika vipi hapo, mbona sikuelewi, unataka kusema nini hapo, kuwa wewe huhusiki na hayo yote, wakati unafahamu fika kuwa wewe ndiye uliyenishauri kufanya hayo yote, wewe ndiye uliyenivalisha hizo ndevu bandia kwa mikono yako mwenyewe, halafu unanisema kwanini nisiende polisi,….’nikasema

‘Nikuulize, je polisi wataamini hayo maneno yako,je kuna kitu gani cha kuthibitisha hiyo kauli yako, kuwa mimi ndiye niliyakuvalisha hizo ndevu bandia,...je kwenye hizo ndevu bandia kuna alama zozote za kwangu, kwa mfano labda kuna alama zangu za vidole,...mmmh, hebu fikiria hilo, ....’akasema mdada huku kainama chini kama anatunga sheria.

Mimi nilijaribu kukumbuka ile siku, ni kweli sikue ile mdada alikuwa na tahadhari zote yeye hakubanduka na kinga za mkononi, na nikajua kayasema hayo kwa akiaminisha hivyo kuwa yeye alikuwa amevaa kinga za mikononi, na alama zilizoonekana kwenye hizo ndevu bandia ni za kwangu,  maana nakumbuka wakati nakimbia, nikiwa nazivua hizo ndevu sikuwa na kinga yoyote mononi....

‘Mdada unataka kusema nini hapo....’nikamuuliza nikianza kuingiwa na mashaka.

‘Nikuulize wewe kwanza, je polisi wanamtafuta huyu mtu aliyemvalisha huyo mtu aliyekuwa na ndevu au wanamtafuta huyo mtu mwenye ndevu?’ akaniuliza mdada akiniangalia kwa macho ya udadisi.

‘Wanamtafuta huyo mtu mwenye ndevu , lakini nijuavyo mimi hawataishia hapo ni lazima watataka kujua ni kwanini alifanya hivyo, na hapo ndipo na wewe utaingia nikikutaja kuwa wewe ndiye aliyevalisha hizo ndevu, unaona hapo, mimi kila nitakachofanya ni lazima niangalia na athari zake kwako...’nikasema

‘Mhasibu kuwa makini hapo...’akasema huku akiwa kama anawaza jambo

‘Mdada kama lengo lako ni kuniruka, huwezi kabisa kufanikiwa,na polisi wanahisi kuwa huyo mtu mwenye ndevu alikuwa akishirikiana na wewe, na huyo mtu ndiye aliyemuua mtoza ushuru…’nikasema

‘Wanahisi au wanaamini hivyo, kwa ushahidi gani, …na hiyo hoja ya kushirikiana na mimi imetoka wapi, walitamka polisi au umeitunga wewe mwenyewe kichwani mwako, hiyo hoja naiona ni ngeni kwangu, usitunge hoja zako mwenyewe, sema polisi wanachokisema wao, hebu niambie hiyo hoja umeitoa wapi ?’ akauliza

‘Wanahisi hivyo,..ndio maana wanakusanya ushahidi, kama hizo ndevu, na hata kama hawatatoa kauli ya moja kwa moja kuhusiana na huyo mtu kushirikiana na wewe, lakini ipo wazi, ….’nikasema

‘Ipo wazi kwa vipi, acha kuzua mambo, usitunge kauli, tuangalia kauli zao na ushaidi uliopo, ukijitungia mambo yako mwenyewe unajidanganya, nikuulize swali, kwanini unakuwa na wasiwasi sana kuhusu hizo ndevu kuonekana,…?’ akaniuliza na mimi nikakaa kimiya nikianza kuhisi uwoga wa kusalitiwa, moyoni nilianza kumuhisi mdada kuwa hana nia njema na mimi, na sikujua nimwambie nini kwa muda huo.

‘Mhasibu unatakiwa ujue jinsi gani ya kujitetea pale unapokumbwa na matatizo kama hayo, na ujue jinsi gani ya kujielezea wewe mwenyewe...’akasema akinionyeshea kidole.

‘Kamwe, usitegemee kuwa mimi nitakubeba wakati wote,...leo nipo kesho sipo...mimi ni mjanja nafahamu jinsi gani ya kupambana na majanga kama haya...’akasema kwa kujiamini na mimi nikamwangalia kwa macho yakutokuamini, na mdada aliponiona nipo hivyo, akasema;

‘Mimi, nimekuuliza maswali hayo yote kutaka kukuweka katika hali ya kujiamini zaidi, …nikuambie jambo la ujasiri, kamwe usiwaogope polisi, polisi ni watu kama sisi, wao kama wao ni fani yao hiyo, na watafanya kila namna kutimiza wajibu wao, na wakati mwingine ili wafanikiwe ni lazima wakutishe wewe raia, kuona uthibiti wako,  cha muhimu ni kuwa tayari kukabiliana nao,….’akasema

‘Lakini mdada, kwanini unafanya hivyo, mimi kuja kwangu hapa ni ili tuweze kujipanga, ili tuwe kitu kimoja nitakachoongea mimi na wewe iwe hivyo hivyo , na kama unavyoona hilo swala la ndevu linatuweka pabaya, je tutasema nini sasa, ...tuendeele kuongopa, ndio maana nikaja kwako tuongee..’nikasema

‘Ni sawa hujafanya vibaya, ndio maana nikawa nakuhoji kujua jinsi gani utakavyojieleza mbele ya polisi, nikuambie kitu, unapokabiliana na hao watu jieleze kivyako, usiongee ukiwa na lengo la kumkinga mtu, hapo ni wewe na pilato...’akasema akitabasamu.

‘Ukiongea kumkinga mtu huku ukijua ni makosa, ujue unafanya kosa juu ya kosa, na ujue jinsi gani ya kuyafuta hayo makosa mawili, uliyojitakia...ongea ukiwa na lengo moja, kama ni kujihami ujue jinsi gani ya kuja kupambana...unanisikia

‘Na kama ni kujitetea, basi na ujue jinsi gani ya kujiweka sawa kwa hatua inayofuata, kama ni kukimbia au kujitoa muhanga, yote yanatakiwa yajipanga kichwani mwako,hata siku moja usitegee ukimtegemea mtu fulani, atakuja kukusaidia, kama hayupo, ama keshauwawa kwenye uwanja wa mapambano,...ni vyema ujipange....’akasema mdada na kunifanya nimuangalia mara mbili tatu na yeye akaendelea kusema;

‘Usipende kusema yeye aliniambia nifanye hivyo,sijui yeye ndiye, yeye , yeye inaonyesha hujiamini, kwanza hao watu, watakuona wewe una kili za kitoto,utaonekana  mjinga, hujiamini,…unanisikia…’akasema

‘Lakini kwa kuhusu swala la ndevu huo ndio ukweli wenyewe…’nikasema

‘Ukweli gani hapo…?’ akaniuliza akiniangalia kwa mashaka na kwa udadisi

‘Kuwa wewe ndiye uliniambia nifanye hivyo na wewe ndiye uliyenivalisha hizo ndevu, ..’nikasema

‘Nilikushika kwa nguvu nikakuvalisha kweli si kweli?’ akauliza

‘Hukunishika kwa nguvu…’nikasema lakini kwa hali kama ile haina tofauti na kunishika kwa nguvu maana sikuwa nafahamu lengo lako..’nikasema na yeye akacheka na kusema;

‘Masikini mhasibu, ...wewe sio mtoto mdogo bwana, upo zaidi ya miaka mingapi sijui,muhitimu wa chuo.., wewe hukuwa mfungwa kwangu,...nilikufunga...’akawa kama ananiuliza.

‘Wewe ni mwanaume bwana, si ndivyo mnavyojinadi nyie wanaume,na kusema mimi mwanaume, mimi najiamini, mimi kiongozi wa familia, ndio hivyo eeh,..., hivi kweli utawaambia polisi kuwa mimi nilikuvalisha ndevu, kwa nguvu, au kwa hiari, na wao wakubaliane na hiyo kauli yako….hebu fikiria hilo kwa makini…’akasem

‘Lakini mdada ni kweli kuwa ulinivalisha hizo ndevu na mbele ya sheria hapo natakiwa kusema nini, natakiwa niseme ukweli au nidanganye, je ni kweli hukunivalisha hizo ndevu,...na kiukweli , mimi sikujua ni nini kusudio lako,…ningelijua kusudio lako nisingelikubali kufanya hivyo’nikasema

‘Sikiliza wewe mwanaume hebu jiamini, kwanza jua lipi la kusema kwa nani, hapo polisi sio mbele ya sheria, wao wanakusanya ushahidi tu, na utakavyojikanyaga kwako, ndivyo watakavyolichulia hilo tukio hata kama sio sahihi, ukweli halisi utajulikana sasa mbele ya sheria, kwenye kiapo, na kwa wakati muafaka….’akasema na mimi nikawa najilaumu kwanini sikusema ukweli pale niliposimamishwa kutoa ushahidi, mdada akasema;

‘Sawa haya tuseme mimi nilikuvalisha hizo ndevu baada ya hapo ukafanya nini?’ akaniuliza

‘Nikaenda kuonana na huyo mgeni ambaye alikuwa na huo  mzigo wako…’nikasema

‘Halafu…?’ akauliza sasa akiendelea kuandika mambo yake kwenye laptop, ilionekana kama nampotezea muda wake, nikaanza kuhisi vibaya, nilitaka kukasirika, lakini kila akinitupia jicho tukiangaliana tu, inakuwa kama ufuto umepita kwenye nafsi yangu na kuifuta ile hasira na kuingia kitu kingine.

‘Mdada mimi naona tunapoteza muda hapa, mimi nakuona kama wewe una lengo jingine kabisa, na lengo hilo ni kuniruka ili mimi nionekane ndiye niliyefanya hayo kwa matakwa yangu binafsi, sasa niambie ukweli,…’nikasema na kabla sijamaliza akafunga laptop yake na kushusha miguu yake chini, ni kama vile kawaza jambo la kutisha, akasimama na kusema;

‘Wewe ndio unanipotezea muda wangu najaribu kukusaidia, nikijipanga wa kugawa muda wangu, huku nafanya mambo yangu, huku nakusaidia...lakini mmh,...’akasema kuonyesha kukerwa.

‘Ujue muda ni mali,kesho mimi natakiwa kusimama kizimbani kutoa ushahidi ni lazima nijiandae,wewe umekuja na porojo zako zisizo na kichwa, wala miguu, najaribu kukusaidia kwa kupanga muda wangu, lakini wewe hunielewi, unataka mimi nifanye nini…..’akasema kwa hasira

‘Unasema kesho unasimama kutoa ushahidi una uhakika na hilo, …?!’ nikauliza sasa nikiwa na mshangao sikuwa nimelithibitisha hilo kuwa kweli mdada ataweza kusimama kizimbani na kutoa ushahidi, kwani mdada alishasema siku akisimamishwa mahakama hali ya hewa inaweza ikabadilika kabisa...

‘Nimeshapata barua rasimi kuwa kesho ni zamu yangu ya kutoa ushahidi, na dakitari wangu kathibitisha kuwa ninaweza kufanya hivyo, sina jinsi nyingine ya kukataa kwahiyo hapa nilipo nina mambo mengi ya kuweka sawa, na wewe unakuja na shida zako unahitajia msaada wangu, sawa siwezi kukukatalia ni lazima nikusaidie....’akasema na mimi nikatulia.

‘Sasa niambie unataka nini kwangu, unataka mimi nikusaidie vipi?’ akaniuliza akiwa kashika kidevu kuonyesha kutafakari, huku akiwa haniangalii mimi moja kwa moja na mimi hapo nikashindwa kabisa kumuelewa mdada

‘Hivi mdada hapa  ni swala la kunisaidia mimi au ni swala la sisi tutasaidiana vipi,….hivi unahisi polisi wakinikamata mimi sasa hivi unafikiri mimi nitasema tena uwongo, nakuambia ukweli safari hii sitakubali kusema uwongo tena,nitawaambia kila kitu, toka mwanzo nilivyokutana na wewe hadi hatua ilipofikia ili niwe huru ...…’nikasema na mdada akanigeukia na kuniangalia akasema;

‘Mhasibu kwanini hukuwaambia hayo toka awali ukawa huru kama ndivyo unavyojidanganya hivyo,...hujui sasa hivi upo nje kwa dhamana kwa sababu ya hayo uliyoyaelezea, kama ingelikuwa hivyo unavyofikiria wewe, ....’akasema huku akitabasamu, halafu akasema kwa sauti ya utani.

‘Ungelishaolewa huko jela, na kwa jinsi ulivyo wewe handsome boy....mmmh, sijui, masikini mhasibu, jeribu kuamuka, jaribu ujiamini...hata hivyo, mimi sikuwahi kukuzuia kusema ulivyotaka wewe, nikuulize , niliwahi kukuambia usiwaambie polisi hayo yote? Hayo ulisema kwa hiyari yako bwana,....’akasema

‘Sawa mimi nimejipanga kuja kusema uweli wote, ili nisiwe msaliti wa haki na ukweli..’nikasema

‘Mhasibu, nimekufahamu udhaifu wako, kweli wewe hujiamini, ...nikuambie ukweli usione mimi nakuuliza maswali hayo yote ukafikiri miimi nimekusaliti…hapana nia yangu ni kukuweka wewe sawa...uweze kujiamini,..lakini naona kama namsaidia mtoto mdogo anayeanza kusimama....’akasema na kutembea tembea mbele na kurudi tena hatua mbili nyuma.

‘Hivi hadi sasa wewe mtu hjanielewa, hivi wewe unanionaje mimi, unahisi  kuwa hayo yote niliyokuuliza nilikuwa na lengo la kukuruka, ndivyo akili yako inavyokutuma au sio...hahaha, masikini mhasibu...’akasema huku akitikisa kichwa.

‘Ndio hivyo..’nikasema

‘Mhasibu hebu kuwa na ujasiri wa nafsi,...unajua nafsi ni kitu kidogo tu, lakini kinaweza kukutawala na kukuyumbusha, lakini sivyo inavyotakiwa, ...sisi kama wanadamu tunatakiwa tuweze kuitawala nafsi, usipoweza kufanya hivyo, utakuwa muoga, utakuwa hujiamini na mwisho wake utakufa kwa shinikizo la damu...’akasema mdada.

‘Mdada sizani kama nitakuja kukuelewa, sikuelewi kabisa,...mara nyingi wewe hueleweki, leo upo hivi kesho upo vile, na nakuona kama unanitumia tu kwa malengo yako binafsi....’nikajitetea

‘Jamani mhasibu yaani ndio imekuwa hivyo...’akasema huku kashika shavu, akiniangalia kama ananisikitikia, na mimi nikawa simuangalii nimeangalia mbele huku napitisha mkono wangu kichwani, sikusema kitu, yeye akasema kwa utulivu;

‘Kwanza elewa kuwa polisi bado hawajamfahamu huyo muuaji ni nani hilo nina uhakika nalo, hata huyo mlinzi waliyemkamata hawana uhakika kuwa kweli ndiye aliyafanya hivyo, hata hivyo ni lazima mtu awajibike, ni lazima waonekane wanafanya kazi,....’akasema na kuanza kutembea tena hatua kadhaa mbele, halafu anageuka na kutembea hatu nyingine , akawa anarudia hivyo hivyo na mimi nikainua kichwa na kumuangalia, nikasema

‘Kweli eeh, ...wewe umejuaje?’nikamuuliza

‘Ndivyo ilivyo, polisi ili wafanikiwe, ...sisemi kuwa hawawezi, wanaweza sana, lakini ili wafanikiwe katika kazi yao, wanategemea ushahidi na maelezo ya watu walishuhudia au kuwepo kwenye tukio.....mimi na wewe ndio wahusika wakuu, au sio...je umetoa msaada gani kwako ili waweze kufanya kazi yao..?’ akaniuliza

‘Nimewaambia yale niliyoweza kuwaambia....’nikasema

‘Kwahiyo basi kwa jinsi tukio lilivyokuwa, wao hawajapata ushahidi wa kutosha kuweza kumfunga mtu,wao hadi sasa wanategemea huo ushahidi kidogo walioupata, hata hivyo ni lazima mtu akamatwe hasa linapotokea jambo kama hilo...’akasema akiwa kasimama lakini sasa alikuwa akiangalia nje kupitia dirishani.

‘Nikuambie ukweli, huyo waliyemkamata mpaka sasa hawana uhakika wa mia kwa mia kuwa ndiye aliyehusika na hayo mauaji...ushahidi wa raia wema ndio utakaowasaidia wafanikiwe kwa hilo,..., sasa raia wema ndio wewe na mimi, ndio maana nakuuliza wewe kama raia mwema umewasaidia vipi hao polisi ili haki itendeke...? ’akaniuliza.

‘Hapo sikuelewi...’nikasema

‘Kwanza ujue kuwa muda umepita sana, tangu tukio lile litokee, kuna watu walifanya kazi yao vyema...polisi wakupima wakuangalia hiki na kile, wakawakisliha ripoti zao, lakini zilipofika kwa wakubwa, hao waheshimiwa, wakazifutika kibindoni kwa masilahi yao, na hapo ushahidi wa awali ukachakachuliwa...’akasema mdada

‘Kwanini?’ nikauliza

‘Kwanini, unaniuliza mimi kwanini...kawaulize wao...inawezekana hili lilifanyika kwa mipango maalumu, maana kama wewe ulikuwa ni mwenzetu, sasa umeamua kutusaliti, unafikiri wenzako watakufanya nini, na wakati wanafahamu fika wewe unafahamu kila kitu, dawa ni kukuziba mdomo...sina uhakika na hilo usije kuninakili vibaya.....’akasema

‘Huko kwa wakubwa kunawaka moto, kuna wakubwa wengine hawalikubali hilo sasa wenyewe kwa wenyewe wanazungukana,..ndivyo ilivyo kwenye mzunguko huu wa dunia, kama dunia inavyozunguka na mambo yake yanazunguka,...na yote yanawezekana, swali la kujiuliza ni kwa masilahi ya nani, mimi hapo sijui ….’akasema mdada

‘Mdada hayo yote mimi sielewi, wasiwasi wangu ni sisi tunaochukuliwa kama chambo, hujui linachoendelea , wewe unatumbukizwa tu, wewe huoni katika hali kama hiyo mimi nitafungwa kama mshukuwa, kama niliyeshirikiana na huyo mlinzi na hiyo ina maana kuwa mimi nitaenda kuteseka jela kabla huyo muuaji wa kweli hajapatikana, kama kweli akipatika, kama unavyodai, nikuambie ukweli mdada,jela sio mchezo, wewe unaisikia tu….’nikasema.

‘Masikini mhasibu kumbe wewe ni muogo kihivyo, na kama una hisia hizo za kwenda jela, usipoangalia vyema hao watu watakufunga kweli, mara nyingine simba akikosa nyama hula nyasi,sasa uwe makini na tabia hiyo, wakimkosa huyo muuaji wa kweli, kwa kutaka watoto wao waende choo, watawakamata wote wanaowashuku na kuwaweka ndani,....’akasema

‘Ndio wasiwasi wangu huo....’nikasema

‘Mhh, pole sana, maana baba mkwe sasa hayupo upande wako, ambaye ndiye aliyekuwa akikubeba, na nikuambie ukweli safari hii wakikumata ujue wanakupeleka jela, sio huko kwenye vituo vyao vidogo,..’akasema mdada.

‘Usiseme hivyo mdada, uliwahi kusikia habari za huko, jamaa mmoja alipelekwa huko mwezi mmoja aliporudi alikuwa kama kachanganyikiwa, anajikuna mwili mnzima, anakohoa kupita kiasi, masikini hakuchkua muda....’nikasema na kuinama kwa huzuni.

‘Ndio hivyo ndio jela zetu hizo, lakini zimewekwa kwasababu gani,...?’ akaniuliza na mimi nilikuwa abdo nimezama kwenye mawazo ya kumkumbuka huyo jamaa aliyewahi kufungwa kwa kushukiwa tu na mdada aliponiona nipo kimiya akasema;

‘Haya hebu niambie kuhusu hao jamaa wawili ...’akasema akinisogelea na kunishika begani

‘Jamaa gani ...?’ nikauliza nikishituka pale aliponishika begani, na hali ile ilimfanya mdada aniangalie kwa mashaka, akasema;

‘Upo sawa wewe..?’ akauliza

‘Unauliza jamaa gani....?’ nikamuuliza tena, na yeye akatabasamu na kushika kidevu, halafu akasema;

‘Hao jamaa wawili uliosema walifika huko hotelini kwako, wakaweka au waliotaka kuweka vitu ofisini kwako,hebu niambie walisema wanataka kuweka vitu gani, hapo ofisi kwako au chumba kwako…?’ akaniuliza

‘Kiukweli sikusikia wakitaja ni kitu gani?’ nikasema.

‘Lakini walikuwa wameshika nini?’ nikauliza

‘Walikuwa na na hii mikoba ya safari, ....briefcase,...’nikasema

‘Ukiuona huo mkoba, au briefcase unaweza kuutambua..?’ akaniuliza

‘Kwanini nisiutambue, ulikuwa wa rangi, na sio hizi briefcase za bei mbaya,...ni kama mkoba wa safari....nitautambua sana....’nikasema.
Kwanza mdada aliniangalia kwa makini, kama ana wasiwasi na mimi, halafu akageuka na kuanza kutembea kwa mwendo wa kiaskari ule wa mwendo-pole, hadi kwenye kabati,akatoa ufunguo na kutoa mfuko mkubwa wa nailoni ndani yake kulikuwa na brifcase za kawaida tu, nikakumbuka ile briefcase, ....

‘Hivi vitu nimevichukua chumbani kwako,…..kabla polisi hawajafika kukagua chumbani kwako…’akasema mdada nilibakia nimeduwaa huku nikimkodelea macho mdada, baadaye nikasema;

‘Haiwezekani….’nikasema nikiuangalia ule mfuko wa plastiki na ndani yake kuna hiyo briefcase ambayo nili-iona akiwa nayo mmoja wa wale jamaa wawili...

NB: JE ITAKUAJE...TUZIDI KUWEPO


WAZO LA LEO: Kunapotokea tatizo, kupotea kwa kitu, kuharibika kwa kitu, kuibiwa kwa kitu, au jambo lenye kuleta hasara, hasa kwenye utendaji wetu wa kazi, kuna tabia ya watu kusingiziana ubaya, hata kama hawana uhakika na shutuma hizo, watakimbilia kusema ni huyu au yule ndiye anahusika.

WAZO LA LEO: Kunapotokea tatizo, kupotea kwa kitu, kuharibika kwa kitu, kuibiwa kwa kitu, au jambo lenye kuleta hasara, hasa kwenye utendaji wetu wa kazi, au katika maisha yetu ya kila siku, kuna tabia ya watu kusingiziana ubaya, kuonyesheana vidole,hata kama hawana uhakika na shutuma kama hizo, watakimbilia kusema ni huyu au yule ndiye anayehusika..

Muhimu kwanza tuwe na uhakika na shutuma tunazotoa dhidi ya wengine, tukwepe majungu, na kama ni kweli, basi hatua ya pili tujue namna gani ya kuzifikisha hizo shutuma kwa walengwa kwa busara, ili hata mshutumiwa aweze kuliona kosa lake na aweza kukiri hilo kosa ,na asipofanya hivyo, basi tutajua kuwa kweli kazamiria na jamii itamsuta. Ni vyema tukajua pia sisi kama wanadamusote ni wakosaji na aliyebora katika wakosaji ni yule anayekiri kosa, akatubu na kuahidi moyoni kuwa hatarudia tena.


Ni mimi: emu-three

No comments :