Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, May 27, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-65

  

 Halafu kwa haraka nikarudi hotelini lakini wakati nakaribia pale hotelini kwa mbali nikasikia king’ora cha polisi kikija kuelekea hapo hotelini, nikajua ni polisi hao wanakuja kunikamata, hapo hapo kwa haraka nikarudi kinyume nyume hadi nje ya hiyo hoteli, nikasubiri, nilihakikisha sehemu niliyokuwepo hakuna mtu anayeniona.....

Gari la polisi lilipofika pale waliingia moja kwa moja hadi ndani na kshi kasha zao, huku wakiwa wamevalia nguo zao rasimi na pingu zimening’inia kiunoni, wakaingia hadi ndani ya hoteli, sikujua huko ndani kinaendelea nini...nikasubiri, na jambo la kusuibri linachukua muda, lakini baada ya nusu saa hivi nikawaona wale polisi wakitoka.

Na walipotoka kwenye eneo la wazi la ile hoteli, wakawa wanaangalia huku na kule, kulizunguka hilo jengo, walipita kwenye eneo la kuegesha magari, nahisi walikuwa wakitafuta gari langu,

Baadaye nilimuona polisi mmojawapo akiwasiliana na simu na wenzako nahisi ni huko ofisini kwao, haikupita muda, wote wakaingia kwenye gari lao, nahisi waliambiwa waondoke tu, wakatoka nje kabisa na kuingia barabara kuu, wakatoweka.

Niliangaza sehemu zote kuhakikisha kuwa hakuna aliyebakia kwenye eneo la hiyo hoteli, ndipo namimi nikajitoa pale mafichoni, sijui kama kuna watu waliniona , sikutaka kukaa pale zaidi nikaondoka kwenyeeneo la hiyo hoteli,

Nilitembea kwa tahadhari hadi kule nilipoweka gari langu, nikamuuliza yule jamaa kama kuna mtu yoyote alikuja kuniulizia, akasema hakuna mtu aliyefika kuniulizia, akasema;

‘Ile nimesikia polisi wamevamia hiyo hoteli kubwa hapo mbele, sijui wanatafuta nini hapo hotelini, umetokea huko?’ akaniuliza

‘Nimewaona, lakini sijui wanatafuta nini, walifika wakaingia ndani na baadaye wakatoka, nahisi ni katika misako yao ya kutafuta wahalifu...ndio kazi yao’nikasema

‘Mhh, na hiyo hoteli siku hizi inakumbwa na majanga, sijui imekuwa ni chaka la wahalfu, siku za nyuma ilikuwa hoteli tulivu, lakini waliiongeza na kuifanya iwe na huduma nyingi, naona mambo yamebadilika...’akasema

‘Sizani kama ni chaka la wahalifu, mimi nahisi ni moja ya majukumu ya polisi kufika sehemu mbali mbali kukagua usalama ....’nikasema huku nikiingia ndani ya gari langu na kabla sijaondoka yule jamaa akasema;

‘Sasa bosi wangu vipi,  huniachii hata pesa kidogo ya soda....’akasema na hapo nikakumbuka, nikatoa chochote mfukoni na kumkabidhi, alinishukuru sana akidai kuwa siku ile hali yake sio nzuri sana, kwani tokea asubuhi alikuwa hajapata hata tone la maji, moyoni nikasema;

Hayo ndio maisha ya walio wengi hapa kwetu, mtu unaamuka asubuhi hujui hata utakula nini, wakati huo huo kuna wengine wanajiuliza wakale kwenye hoteli gani ya kifahari, lakini yote ni maisha.

Nilipotoka pale niliendesha gari kwa tahadhari mpaka nilipokaribia eneo karibu na nyumba ambayo nimeambiwa baba mkwe huyo anaishi hapo kwa ajili ya matibabu , ni nyumba aliyojenga baba mkwe huyo kwa ajili ya dada yake, ni nyumba kubwa ya kifahari.

Mimi sikutaka watu wajue kuwa nimefika hapo nikapita hadi mbele, ambapo huko kuna gereji, na huyo jamaa mwenye hiyo gereji ninafahamiana sana na yeye, huwa wakati pikipiki langu likisumbua nampelekea yeye, namuamini sana kwa kazi za ufundi wa magari na pikipiki

Nilipofika tu, jamaa akajua nina tatizo la gari, akanipokea kwa shangwe, na huku akishanglia kwa kuita, bosi,bosi.... bosi,...sikupenda sana kuitwa jina hilo, lakini wakati mwingine sina jinsi kila mtu anatumia jina alipendalo kwa malengo yake.

‘Karibu sana bosi, lisogeze hili gari lako ndani kabisa, kwa maaliwatani, ....wewe ni mtu mashuhuri ni lazima nikupe kipaumbele, ...’akasema na mimi nikaliingiza gari moja kwa moja hadi ndani nikateremka kwenye hilo gari na jamaa alishasogea tayari kusikia shida yangu.

‘Sijafia hapa kwa tatizo kubwa sana, ni ushauri tu,...muhimu hebu likague hili gari uniambie tu kama kila kitu kipo sahihi, maana natarajia kusafiri masafa...natumai unanielewa, nitaliacha hapa kwa muda, nakuaminia mtaalamu wangu...’nikamwambia na yeye kwanza akaliangalia kwa kulipitia kwa haraka halafu akasema;

‘Hili gari bado jipya kabisa...sizani kama lina matatizo ni bora umefika hapa kwangu , kwani ungeliwapelekea mafundi wa njaa kali, wangelichakachua na usingizia maosa ambayo hayapo, lakini sijaingia ndani zaidi, huko kama una muda tunaweza kuangalai wote...’akasema

‘Sina muda huo kuna sehemu na kwenda kwa miguu, nikirudi utaniambia...’nikasema

‘Ok, ni uamuzi wako,.....’akasema na mara moja akaanza kazi mimi nikaondoka hapo ndani na kuelekea kwa baba mkwe, ni hatua chache kutoka hapo kwenye hiyo gereji, nikatembea wa tahadhari hadi kwenye eneo la hiyo nyumba, ni nyumba anapoishi shangazi yake mchumba wangu, sijawahi kufika hapo kabla, ninapita tu, lakini sikujua kuwa ni sehemu anapoishi huyo shangazi.

nilihakikisha gari hilo lipo ndani kabisa sehemu isiyoonekana kirahisi

‘Mtaalamu wangu, gari langu hilo hapa sio bovu, nimelihifadhi kwa muda,...’nikasema

‘Hamna shaka tajiri wangu, ilimradi ukitoka unikumbuke, siunajua tena siku hizi kazi hakuna, tunaganga njaa tu...’akasema

‘Hamna shida, ....’nikasema na kuanza kutembea kuelekea kwa baba mkwe

**********

‘Baba mkwe wako haruhusiwi kuonana na mtu kwa sasa, kaongea vya kutosha…’aliniambia dakitari niliyekutana naye mlangoni akiwa anatoka na gari lake.

‘Oh, lakini alipanga kuongea na watu watatu, na mimi ni mojawapo…’nikasema huku nikiangalia saa na muda ulishapita sana.

‘Ndio hivyo, muda niliopanga wa yeye kuongea na watu umeshapita, na hata hivyo kutokana na hali yake kwa leo haitawezekana tena aongee na mtu mwingine nimeshampa dawa maalumu za kumsaidia kupumzika,…’akasema docta na mimi nikawa sina namna nyingine nikageuka kuondoka, na wakati nataka kuvuka bara bara mara nikamuona shangazi,akija kwa mwendo kasi, alikuwa katika mishe mishe zake.

‘Wewe mtu umefuata nini hapa nyumbani kwangu?’ akaniuliza aliponiona, nikaona sasa nimelikoroga, nikajinyenyekeza kwa kumsalimia;

‘Shikamoo shangazi...’nikasema

‘Kamshike huyo shangazi yako dada yake huyo hawara wako,nimekuuliza swali umefuata nini hapa kwangu, sitaki wanga hapa kwangu, mnataka kuniuliza ndugu yangu, nahangaika huku na kule ili apone, bado mnakuja kuwanga mchana, niambai umefuta nini hapa kwangu.....’akasema hayo maneno makali mpaka nikashangaa, sikutaka kusema lolote baya nikasema;

‘Niliitwa kuja kuongea na baba mkwe..’nikasema

‘Ni nani amekuita na ni nani baba yako mkwe?’ akaniuliza na mimi nikabakia kimya

‘Nikuambie tena na tena, sitaki kusikia hilo neno kutoka kwako, ukilitaja katika hii familia, kama ni baba mkwe wako nenda kwa baba wa huyo hawara wako, natumai na yeye ana baba sisi wewe kwetu ni kama mfu tu, unasikia, sisi tumeshakuzika zamani, hatukutambui tena, ulishawahi kuongea na binti hivi karibuni…?’akasema na kuniuliza

‘Hapana sijawahi kuongea naye, nikimpigia simu hapokei kabisa, sijui kuna nini kinachoendelea,...hata hivyo shangazi…’nikaanza kujitetea na akanisogelea na kuwa karibu na mimi akaniangalai usoni na kusema

‘Unaona nilivyofanya, hivi katika mile zetu kuna mkwe wako anaweza kufanya hivyo, akakusogeela hivyo, hii ni kuonyesha kuwa  mimi sio mkwe wako tena,kwahiyo, geuka na sahau kama uliwahi kuchumbia kwenye familia yetu...unasikia eeh, mpedwa...’akasema na kunisha na mkono wake shavuni

Kwakweli nilikereka kwani hata kama ni shangazi katika mila zetu mtu kama huyo anajitahidia sana kuwa mbali na mkwe wake, na tendo alilofanya hapo ni kuashiria kabisa kuwa mimi sio mkwe wake tena.

‘Shangazi hebu jaribu kunielewa, hivi mimi nina kosa gani, ...’nikasema

‘Huna kosa mpendwa,..nikushauri kitu, tafuta mwanamke wa kuoa, huyo hawara wao sijui anaitwa nani vile....eeh, mdada, hivi kuna jina kama hilo uliwahi kulisikia, sisi tunafahamu majina kama Tausi, Rose, na mengine lakini mtu anaitwa mdada, huoni kuwa ni majina ya kihuni....’akasema

‘Hapana hilo jina alilipendelea kutokana na maisha yake aliyoyapitia, hataki kulitumia jina lake hasa, maana linamkumbusha madhila hayo...’nikasema

‘Unaona eeh, jinsi gani unavyompenda, mpaka ukajua historia yake yote,kweli ukipenda sana chongo utaita kengeza, masikini kijana wewe, hapo umeingia choo cha kike, hapo eeh, 

umeingia mkenge, utakuja kuniambia....’akasema

‘Lakini shangazi ...’nikasema

‘Mpendwa,...niite mpendwa, kama umenipenda, lakini shangazi kwa maana kuwa ni shangazi wa binti, hilo lifute akilini mwako, umenisikia....’akasema na kunisogelea akitaka kunishika na mimi nikasogea nyuma, akacheka kicheko cha dharau, na kugeuka kutaka kuondoka.

‘Shangazi tafadhali nipo chini ya miguu yako...’nikasema nikijitahidi hata kupiga miguu, na aliposikia hiyo kauli akageuka na kuniangalia huku kashika kiuno, akasema

‘Nimessahau, niliongea na kaka, akanipa maelezo yako yote, na moja ya jambo tuliloliongelea ni kuhusu mkataba mliwahi kuandikisha kati yako na binti yangu, sasa kama mkataba unavyosema ukikiuka masharti ina maana nyumba na kila kitu chako ni mali ya mtoto, ambayo itakuwa chini ya binti yangu…unanielewa, kwa vile wewe ndiye umevunja mkataba, usahau kabisa kama ulikuwa na nyumba kule kijijini hilo ni la kukusaidia tu…’akasema

‘Una maana gani kusema hivyo shangazi kwani mimi nimevunja mkataba gani, mbona hamnipi nafasi ay kujitetea?’ nikauliza

‘Kwenye mkataba wenu mlisema kuwa,kwa yoyote ambaye atakiuka masharti ya uchumba wenu, akachepuka,...japokuwa mlikuwa hamjafunga ndoa, sawa, lakini kwa vile ulimzalisha mwenzako tena kwa kubaka, basi, kila kitu chako kitachukuliwa na mtoto,na mama yake akiwa msamamizi wake….mliandikisha hayo wenyewe, siku ulipokwenda huko kijijini na 
kujinadi kuwa una nyumba na nyumba hiyo ni mali yako na familia yako yaani mke na mtoto au sio, na kwa kujitamba ukasema upo tayari kuandikisha mkataba, ili kuhakikisha kuwa kweli upon a binti yetu...’akasema

‘Ni kweli niliyafanya hayo kwa nia njema kabisa, hadi sasa nina imani hiyo, binti yule ni mchumab wangu na tulikuwa tunasubiri tufunge ndoa....’nikasema

‘Mtafunga ndoa na hawara yako nimeshakuchunguza sana, ...nikuambie ukweli, mapenzi hayalazimishwi, nimekugundua kuwa unampenda sana huyo mdada, na binti yetu ulimtaka kwa tamaa zako za kimwili tu, ukambaka na kumpa mimba....’akasema.

‘Shangazi ile ilikuwa ni bahati mbaya, lakini tangu awali tulikuwa tunapendana na binti, ulishawahi kumuuliza hilo...’nikasema

‘Hayo yote nimeyafanya, nimafuatilia hatua kwa hatua kuhakikisha hilo, wewe humpendi binti yangu, usijidanganye, usije ukamuoa binti yanagu, ikawa ndoa ndoana...tumakubali hasara, lakini angalau umefidia kidogo na hiyo nyumba....’akasema

‘Shangazi hiyo sio haki kabisa,....ile ni nyumba niliyojenga kwa nia njema ili niweze kuja kuishi na familia yangu mimi na huyo binti na mtoto wetu, mkifanay hivyo itakuwa sio halali kabisa…’nikasema

‘Hilo liwe fundisho kwako na wenzako wenye tabia kama hiyo, manojifanya vijogoo, kwa tamaa zenu za kimwili,...kama mnajiona mna midadi kwanini hamuendi huko mitaani, wanawake wa namna hiyo wapo wengi....wanajiuza, wanajua jinsi zote ....’akasema akiwa hacheki kuonyesha kuwa hatanii.

‘Hao wanawake wamesomea hizo kazi, hawana haya kabisa, kwanini hukuwaendea, ukamaliza hizo tamaa zako, kwanini mnawaharibu mabinti wa wenzenu, wazazi wako wamehangaika, hawalali, nyie mnavizia kama fisi, wanahaarmu wakubwa nyie....’akafyonza na kutema chini.

‘Nikuambie ukweli, mimi nilichukia sana niliposia hivyo ulivyomfanyia binti yetu, mimi yule niliwahi kuishi naye nikamfunza na kumfunda tabia njema, kwa tendo hilo ulinizalilisha sana, nilionekana kama sijui kulea,...na hata hivyo binti hana kaosa wewe ulimbaka na ulikiri kufanya hivyo...’akasema

‘Shangazi ilikuwa ni bahati mbaya tu...’nikajitetea.

‘Unajua sijui kwanini naendelea kuongea na wewe hapa, nimekustahi sana, hebu uliza hapa mitaani, watu kama nyie nawafanya nini, nilimshangaa sana kaka yangu kwanini kaka hakukufunga wewe, anakudekeza, hadi anakutafutia kazi nzuri, na bado huna shukurani, unaona uliyoyafanya, mumeua, mishirikiana na mdada, bado mnabebwa tu, ngoja sasa jamaa wamecharuka huko juu, utakwenda kuozea jela kwasababu ya tamaa zako,..’akasema

‘Shangazi sisi hatujaua, huo ndio ukweli wa mungu, mungu ni shahidi wetu..na hayo ya binti naomba tukae tuyaongee nina imani kuwa tutafikia muafaka, nipeni nafasi ya kujieleza,...’nikasema

‘Nikuambie ukweli, ondoka mbele yangu nisije kukutukana, ...hunielewi eeh, hebu uliza hapa mitaani mimi naitwa nani, ...hilo sasa limefika kwangu, ujue hapo ni mwanzo tu, sijamalizana na wewe, utaukimbia huu mji...uliza wenzako, kesi ikiisha salama hakikisha unaondoka huu mji, nitakuharibu uonekane choo, kilichotapishwa, hilo nakuahidi, kama unabisha subiri...’akasema na kuanza kuondoka.

Niligeuka na kuona kundi la watu lilishaanza kuja kusikiliza, taratibu nikaondoka nikiwa na aibu tele usoni, nilijiona mtu wa balaa, maana kila ninapogeuka nakutana na matatizo, nikajiuliza nimekosa nini

‘Yote haya kayasababisha mdada, ni lazima niende kwake,..’nikasema na kuelekea pale nilipoweka gari langu nilipofika jamaa akaniuliza

‘Nimesikia kwa mama shughuli kuna mtu alikuwa akipashwa vipande vyake...’akasema

‘Mama shughuli ni nani, ..?’ nikauliza

‘Mama mipasho, mama yule ni hatari, akikuamulia utakimbia mji, ...anaongea,ana matusi, anaweza akakuzalilisha hivi hivi, na usimfanye lolote, yule mama ni balaa, halafu ana nguvu, aliwahi kupigana na midume miwili akaipiga kama watoto wadogo na kuwavua nguo hazarani...usicheze na yule mama, wanaume wanamuogopa....’akasema

‘Unasema kweli....?’ nikauliza nikionyesha wasiwasi

‘Hayo ni kwa nje, na kwa ndani, watu wanaamini kuwa huyo mama ana amini sana mambo ya kishirikiana, anaweza kukushusha mzigo....’akasema

‘Kunishusha mzigo una maana gani...?’ nikauliza

‘Unaweza kuota busha, na hata kupoteza kabisa sehemu zako za siri, ukawa sio mwanaume tena, wapo waliofanyiwa hivyo, ilibidi wahangaike sana na huyo mama ndiye aliyewasaidia kuwarejesha katika hali yake tena...mimi nilishudia kwa rafiki yangu mmoja, sasa hivi kahama kabisa huu mji....’akasema

‘Lakini hayo yana maana gani, anapata faida gani...?’ nikauliza

‘Cha msingi asichokitaka yeye ni kuingilia mambo yake, kuwaharibu mabinti wadogo, na wanaume wanaowatesa wake zao, ...hayo kayafungia kazi na amefanikiwa sana hapa mjini, kila mwanamke akionewa anakimbilia kwa huyo mama, kama kuna binti kabakwa huyo mama anatafutwa....ole wao umbake binti wa shule, huyo mama atalifungia njuga hadi mbakaji apatikane na akipatikana cha moto atakiona...na ni lazima atafungwa, na akitoka huu mji ataukimbia....’akasema

‘Oh, mbona balaa...’nikasema

‘Kwani humfahamu huyo mama,...?’ akaniuliza

‘Namfahamu lakini sio kwa mambo hayo...’nikasema

‘Sasa kama humfahamu kwa mambo hayo, jihadhari sana na mabinti wadogo, jiepushe sana kuwaonea wanawake...na akikunyoshea kidole, kimbia, hama kabisa huu mji,...vinginevyo ni mama mzuri tu, watu wanampenda sana kwenye shughuli, hasa akina mama maana anajua kutoa mipasho, ndio maana wanamuita mama shughuli., au mama mipasho.

‘Oh, sasa nimekupata, sijui hata nifanya nini.....nitakimbilia wapi mimi...’nikasema

‘Kwani umefanya nini?’ aakniuliza

‘Mdada....’nikasema

‘Oh, kafanya nini yule binti mzuri...?’akauliza

‘Nataka kwenda kwake, hajafanya kitu kibaya....’nikasema ili kupoteza lengo

‘Uwe makini naye, yule binti mjanja sana,...akikuweka kwenye kona zake, atakuumiza huku anacheka....hebu jiulize mtoto mzuri kama yule kwanini haolewi, kila aliyejaribu kumuoa sasa ni marehemu, angalia huyo mtoza ushuru, yupo wapi...chunga sana kujuana na huyo binti...’akasema na mimi nikasema

‘Mhh, haya sasa majanga, sijui nikimbie huu mji...lakini ni lazima nimuone huyu mdada kwanza,...’nikasema na kuingia ndani ya garii langu, huku akili yangu ikimuwa mdada, na nilipofika barabara kuu, nikakutana na gari la polisi , likanisimamisha...

NB:Haya  mambo ndio hayo yanaiva mhasibu bado anakumbana na mitihani je ataishinda

WAZO LA LEO:Ukikutana na mitihani mbali mbali ya kimaisha, majanga, shida, magonjwa, fitina, umasikini nk, usikate tamaa, jitahidi uwezavyo kwa kufuata njia iliyosahihi, kamwe usikimbilie kwenye ushirikina ukamkufuru mola wako. Kumbuka mitihani mingine ni kwa ajili ya kukupima imani yako, ni kwa ajili ya kukukomoza wewe ili uwe na uzoefu wa maisha,

Unapopatwa na mitihani ukakikimbilia kwenye shiriki, ukadanganywa, ujue hapo haupo na mola wako tena upon a shetani, adui mkubwa wa imani sahihi. Na ukifanya hivyo ukamtii shetani utakuwa umeshindwa katika mitihani ya maisha, na hata kama utajiona umefanikiwa kwa kufuata njia ya shetani, ujue mafanikio hayo ni kwa  muda tu,
Hebu jiulize wapo wapi waliofanikiwa kwa njia hizo za kishetani, mbona hawakuweza kupambana na umauti...ujue raha za dunia ni kwa muda tu.

Muhimu, pambana kwa namna iliyo sahihi, jijenge kwenye imani iliyo sahihi, yashinde majaribu kwa kujitahidi kufanya kazi kwa bidii kwa misingi ya haki na ukweli, huku ukimuomba mungu wako akusaidie, na hayo utayweza vyema kama utasoma,  ujue kuwa elimu ndio taa ya kukumulikia njia iliyo sahihi.

Ni mimi: emu-three

No comments :