Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeMonday, May 26, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-64


Lakini kuna kitu muhimu,....mhasibu nakupa muda mwingine, nataka uniambie ukweli, maana mimi bado nina mashaka nanyi,...’

‘Una mashaka gani na sisi...?’ nikauliza

‘Ni kuhusu wewe kujivika ndevu, mimi nina uhakika na hilo kuwa wewe ulijivika ndevu...’akasema na mimi nikaanza kuhisi uwoga fulani, moyoni nikijilaumu kwanini sikuweza kumuambia ukweli toka mwanzo, lakini hapo hapo nikakumbuka onyo la mdada.

‘ Mimi ninachotaka kujua kutoka kwako,... kutoka kwenu  ni kwanini mlifanya hivyo, kama sio mlikuwa na mpango fulani dhidi ya mtoza ushuru, mlipanga pamoja kuwa uvae hizo ndevu, ili huyo mtoza ushuru sikutambue wewe ili kufanikisha lengo fulani, ambalo lilifikia hadi kuuwawa kwa mtoza ushuru....’akasema huku akitaka kuondoka,

‘Lakini mimi sijafanya hivyo, na ukisema una uhakika una maana gani, mimi sijavaa ndevu za bandia una ushahidi gani wa kusema hivyo ina maana huniamini tena ndugu yangu?’ nikamuuliza.

Kwanza akaniangalia kwa uso wa kunionea huruma, halafu akatikisa kichwa kuashiria kusikinisikitikia, akasema;

‘Nimejaribu sana kukuamini, lakini naona nina beba mzigo ambao haubebeki, na nionavyo hata kama nitajitahidi vipi, sitaweza kuujua ukweli wote kutoka kwako, sasa mimi sina budi kutimiza wajibu wangu, nilijua wewe utanisaidia,ili na mimi nikusaidie, ...lakini nionavyo mmi huenda sivyo ninavyokufikiria wewe....’akasema

‘Kwanini mpelelezi?’ nikamuuliza

‘Kwasababu wewe sio mkweli, ...niambie ni kwanini unafanya hivyo, ni kwasababu ya mdada,...?’ akaniuliza.

‘Lakini mimi nimekuambia ukweli wote, wewe unataka ukweli gani zaidi ya huo....na hilo la kuvaa ndevu, nahisi ni ...mlinzi katunga tu, halipo, hakuna mtu kama huyo...’nikasema

Mpelelezi akaniangalia kwa makini, halafu akafungua mkoba wake,na mara akatoa mfuko wa plastiki na ndani ya huo mfuko wa plastiki kulikuwa na ndevu za bandia...akanionyesha na kusema;

‘Unataka ushahidi sio, ushahidi huu hapa....haya niambie, lakini kwa vile muda umekwisha, na muda wangu wa kukuamini wewe pia umekwisha, inabidi mimi nifanye kazi yangu, ni ukweli usiopingika wewe na mdada mnahusika kwa namna moja au nyingine na kifo cha mtoza ushuru, ....’akasema na kabla sijasema kitu,akaondoka kwa haraka....
Tuendelee na kisa chetu

Unataka ushahidi sio, ushahidi huu hapa …’

Haya yalikuwa maneno ya mpelelezi  ambayo yalinifanya nikose raha, na hasa pale nilipoangalia sura yake iliyobainisha kuwa mimi siomkweli kwake,kwahiyo hawezi kuniamini tena na hapo nikahisi mwili wangu ukinisisimuka kwa woga,nikawa naendesha gari huku nikiwa sijaamini,nikihisi kuwa kwa muda wowote sasa ninaweza kukamatwa kwani polisi wanaamini kuwa huyo mtu mwenye ndevu ndiye muuaji au ndiye mshirika wa mauaji

‘Lakini...kama huo ushahidi alikuwa nao mpelelezi muda wote huo,  kwa nini hakuweza kuufikisha kwa polisi?’ nikajiuliza huku nikiendesha gari,na nilijitahidi kuendesha kwa mwendo wa kawaida kwani kwa hali ile ya mawazo ningeendesha kwa mwendo kasi ningeliweza kusababisha ajali, akili haikuwepo hapo kabisa.

‘Au ni kwa vile hana uhakika kamili kuwa mimi ndiye niliyekuwa nimevaa hizo ndevu,...lakini atakuwa kachunguza alama za vidole,...sasa ni kwanini bado anataka ukweli, wakati ukweli anao yeye, ...oh, ataka kujua sababu ya sisi ufanya hivyo, mimi nahisi anvuta muda ili apate ushahidi mwingine wa kutosha kunikabidhi mimi kwa polisi kuwa mimi na mdada ndio tuliokuwa na njama za kumuua mtoza ushuru….kweli mtu huyu mjanja...sasa tumekwisha, hatuna ujanja...ni lazima tuseme ukweli....’nikaendelea kujiuliza

‘Lakini haya yote kayasababisha mdada,…..huyu mwanamke hana mema kwangu, nisipoangalia atanipeleka kubaya, lakini kwanini moyowangu hautaki kuachana na huyu mtu…sijui kanipa nini huyu mwanamke,sijui …mmh,lakini siwezi kujidanganya mbele yake, ….’nikasema nikimuwaza mdada

‘Hata hivyo ni lazima niongee naye ili afahamu kuwa mpelelezi anafahamu kila kitu, …ni lazima nimkanye asishindane na mpelelezi kama kweli hataki kuingia matatani, na hiyo tabia yake ya kunitumia mimi kama chambo ni lazima aiche,...kama kweli ananipenda kidhati, basi na yeye anisikilize mimi…..vinginevyo, oh,sijui nifanye nini, ina maana nitafungwa tena kwa ajili yake, haiwezekani…

‘Safari hii ni lazima nimueleze,ni lazima niongee naye, ni lazima tukubaliane…’nikasema na kuchukua simu yangu kumpigia mdada, na simu ikawa inaita bil kupokelewa, nikahisi labda mdada kafanya hivyo kwa vile bado anaongea na baba mkwe.

‘Ni lazima nionane naye kwa haraka zaidi, maana sijui mpelelezi ana mipango gani dhidi yangu kwa sura aliyonionyesha pale inaonyesha wazi haniamini tena na ile hali ya kuondoka kwake kwa haraka akisema keshagundua jambo ni lazima kuna kitu kingine kakigundua cha kuwezesha kuunganisha ushahidi wake ‘ Na kwanini wanamtafuta sana  huyo mtu mwenye ndevu ambaye ni mimi…’nikajiuliza

‘Haya yote bila kuonana na mdada, sitaweza kupata uhakika wa kutosha, ….ni lazima nionane na mdada nione yeye kajipanga vipi, na safari hii siwezi kukubali kufungwa…wakati hayo yote kayapabga yeye….’nikasema.

Kwa vile muda wangu wa kuonana na mzee ullikuwa haujafika, kwani kila mmoja alipangiwa muda wake wa kuonana na huyo mgonjwa, nikaona ni vyema kwanza nipitie hotelini kwangu kubadili nguo, na kujimwagia maji kidogo, na pia kwa vile nilihisi ninaweza kukamatwa tena nikaona ni vyema nijipange vyema.

Nikafika hotelini kwangu na kuingia kwenye chumba changu moja kwa moja, niliona ni bora nijimwagie maji kidogo, na wakati naoga nikasikia simu yangu inalia,nilikuwa nimeiacha kitanani, haikuchukua muda mrefu ikanyamaza, nikahisi huyo mpigaji anaweza kuwa ni mdada,ndiye mwenye kawaida ya kunipigia simu hivyo. Yeye anapiga simu kwa muda mfupi tu usipopokea anakata simu.

Nikaharakisha kuoga na kukukimbilia chumbani kwangu na nikachukua simu yangu,kuangalia huyo aliyenipigia simu ni nani, namba niliyoiona hapo ilikuwa ni ngeni kwenye simu yangu, nikaipiga hiyo namba, lakini simu ilisema mtu unayempigia hapatikani kwa sasa, basi nikajiandaa na kuvalia vizuri kwa safari ya kwenda kwa baba mkwe.

Wakati natoka chumbani kwangu, nilihisi mwili ukinisisimuka, hiyo hali iliniashiria kuwa kuna kitu hakipo sawa, sijui ni kwanini ....nikatulia kidogo kuhakikisha kama kila kitu kipo sawa, na mara akili ikanituma niende kwenye ofisi yangu, nikachapuka, kuelekea huko, na mara nikawaona wale jamaa wawili waheshimiwa, wakielekea kule ofisini kwangu,nikajificha ili wasinione.

Wale jamaaa walikuwa na mwendo wa haraka, na hawakuonyesha wasiwasi wa kuangalia huku na kule,walikuwa kimiya hawaongei, walikuwa briefcase mikononi mwao,na walipofika kwenye mlango wa ofisi wakaangalia huku na kule na walipohakiki, wanachokiangalia, wakapeana ishara , na wote wakavaa kinga za mkononi mwao, halafu wakafungua mlango na kuingia ndani.

Mimi nikajiuliza kuna nini kinaendelea kwa hawa watu wawili, na kwanini watumie kinga ya mikononi iliwasiache alama za vidole, nikashindwa kuvumilia nikatembea kuelekea pale mlangoni,nilipofika niliona mlango upo nusu wazi,nikasikia sauti zao kwa mbali

‘Fungua hilo kabati na uweke pale pale ilipokuwa awali….’nikasikia mmoja akisema, na baadaye mwingine akasema

‘Mbona hili kabati leo halifunguki..’sauti nyingine ikasema

‘Haiwezekani! labda hebu jaribu tena, au umebadili ufunguo...’sauti nyingine iasema na mwenzake akajibu

‘Hapana sijabadili, ufunguo ni ule ule,...nahisi huyu mtu kaamua kubadilisha vitasa vya kabati,huoni, hivi ni vipya kabisa,,….’akasema. Ni kweli, baada ya wao kunikabidhi dhamana za humo ndani, nilichofanya mimi ni kubadili vitasa vyote vya zile kabati,na hili nililifanya bila kumwambia mtu, hata mdada mwenyewe alikuwa halifahamu hilo.

‘Sasa tufanyeje…’mmoja akauliza

‘Tutafuta sehemu nyingine yoyote tuweke,..maana hapa tunahitajika tuondoke haraka iwezekanavyo, muda umekwisha ,polisi wanaweza kufika hapa muda wowote kuanzia sasa,hali sio shwari kabisa, unaona hali ilivyo, wakubwa wote wapo roho juu kuhusu hii kesi, …’akasema

‘Na huyu mhasibu mwenyewe atakuwa wapi, huenda yupo chumbani kwake,mimi naona twende tuonane naye,na tumuambie kuna vitu tunavitafuta ofisini kwake, halafu akitupa huo ufungua itakuwa rahisi kwetu kuviweka hivi vitu bila ya yeye kufahamu...’akasema

‘Tukienda kuonana naye, italeta shaka zaidi,hatutakiwi kueleweka kuwa tulifika hapa, hasa yeye asilijue kabisa hilo, na mbaya zaidi akigundua kuwa tumeingia ofisini kwake, usije kugusia kabisa kuwa tumegundua vitasa vya kabati vimebadilishwa, unakumbuka tulivyomwambia muhudumu , kuwa kuna mtu tunamtfauta huko juu, hatujasema tunakwenda kuingia kwenye hiyo ofisi...’akasema mwenzake

‘Kwahiyo sasa tufanye nini?’ akauliza mwenzake.

‘Ngoja nifikiri, cha muhimu tuhakikishe kama hayupo chumbani kwake, kama hayupo sisi tunaweza kuviweka huko huko chumbani kwake,, …..’akasema na nahisi alichukua simu na kuanza kunipigia mimi na mimi kwa haraka na kwa vile simu ilikuwa mononi mwangu, nikaizima wakati mlio wa kwanza ulishaanza kusikika, na kwa haraka nikaondoka maeneo hayo kushuka chini, sikutaka kuonana tena na hao watu.

Nilipofika chini cha kwanza kufanya ni kumpigia simu mpelelezi, lakini cha ajabu hakupokea, iliita mpaka ikakatika, nikaone niandike ujumbe wa maneno, nikaandika hivi;

Wale jamaa wawili wamefika ofisini kwangu wakiwa na vitu, nimewasikia wakisema ni vitu vinavyotafutwa na polisi, wamekuta nimeshabadili vitasa vya kabati, na wamepanga kwenda kuviweka vitu hivyo chumbani kwangu...’nikautuma huo ujumbe, lakini haukwenda ukawa hewani, kumbe simu iliisha salio.

Muda ukawa anakimbia kweli, nikakopa salio, na kuutuma tena huo ujumbe, mara simu ikazima, ....oh, haukuwa na chaji, ...oh leo mambo vipi, ndio kifo cha nyani nini..., sikutaka kupoteza tena muda, sikutaka kurudi kuchaji hiyo simu, muda ulikuwa hautoshi;

‘Nitachajia kwenye gari langu...’nikasema huku nikatoka nje, hadi sehemu nilipoweka gari langu.

Niliendesha gari na kutoka nje ya eneo la hiyo hoteli hadi sehemu nyingine mbali kidogo na hiyo hotelini. Nilipofika hapo nikaangalia kama simu imeongezea kidogo, lakini haikuingiza chaji. Nilitoka na kuongea na jamaa yangu mmoja ninayemfahamu kuwa anisaidie kunichajia simu yangu angalau ipate chaji kidogo, na aniangalizie gari langu kwani nimesahau kitu hotelini.

‘Sawa bosi najua ukirudi nitapata pesa ya soda...’akasema

‘Usijali ...’nikamwambia na kuondoka.

Nilirudi tena pale hotelini, lakini safari hii kwa tahadhari, nilijilaumu kwanini nilitoka haraka, kwanini nisingelihakikisha kuwa wale jamaa wameweka hivyo vitu chumbani kwangu, huenda wanaweza wakaweka sehemu nyingine na kama wameweka humo, nitafanya nini.....

Haikupita muda wale jamaa wawili wakatoka nje na kuelekea kwenye gari lao, waliendesha taratibu hadi bara bara kuu, mimi nikawa nawafuatilia kwa macho, niliwaona wakiangalia huku na kule wakiwa ndani ya gari lao, nafikiri walikuwa wakitafuta gari langu,na walipohakikisha kuwa sipo maeneo hayo wakaondoka.

Mimi kwa haraka nikarudi tena kule kwenye gari langu na kuwasha simu yangu na mara nikakutana na simu zilizopigwa na zote zilikuwa namba ngeni , na moja ilikuwa imejirudia, nahisi ni hao hao jamaa walinionipigia nikataka kuzipiga, lakini nikaona haina haja kwa muda ule, nikautuma ule ujumbe wa maneno kwa mpelelezi.

Halafu kwa haraka nikarudi hotelini lakini wakati nakaribia pale hotelini kwa mbali nikasikia king’ora cha polisi kikika kuelekea hapo hotelini, nikajua ni polisi hao wanakuja kunikamata tena, .....

NB: Ni nini kitatokea kwa mhasibu, tutaona sehemu ijayo

WAZO LA LEO: Wema mara nyingi haulipiki, ukitendewa wema, huwezi kusema nitaulipa huo wema ulionitendea. Ukitaka kuhakiki hilo, hebu, angalia muda wa wema uliotendewa, huwezi kuurudisha huo muda nyuma ukaulipa kwa muda ule, pia huwezi kujua, jinsi gani huyu mtenda wema alivyojitolea kwako, na hujui nafsini mwake alikuwa anajisikiaje, je wewe unaweza kubuni yote hayo, haiwezekani,


Kwahiyo wema haulipiki, cha muhimu ni kumshukuru mtenda wema, na kujitahidi na kuitakidi kimoyo kuwa utajitahidi na wewe kumtendea huyo mtu wema kama huo, na zaidi mshukuru yule aliyemuwezesha huyo aliyekutendea huo wema, kwani hata huyo aliyekutendea huo wema, sio kwa uwezo wake, hayo yote ni kwa uwezo wa ,muumba wa kila kitu.

Ni mimi: emu-three

No comments :