Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, na matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary'(shajara). Pia tunakaribisha mijadala yenye kuelimisha

Na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..

Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu.

MUHIMI, SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthree



Monday, May 19, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-60


‘Unajua siku ile nilikuwa nimejiandaa kupambana na huyo mpelelezi, na kama isingelikuwa yule muhudumu wa hiyo hoteli kuja, akifanya usafi wake,...' akakunja uso kama usikitika halafu akasema;

'Mhh, sijui ingelikuwaje, maana hasira zilikuwa zimeshaa kunipanda, nikahisi kichwa kinaanza kunizunguka, ...nikawa najaraibu kujizua, mwili ukaanza kutetemeka, yaani ilibakia kidogo, akili ianze kupotea, akaja huyo muhudumu na niliposikia sauti yake akibisha hodi nikazindukana ...’akasema akionyesha wasiwasi.

‘Ina maana ulishaanza kubadilika, na huyo muhudumu alisaidia kivipi kwani sauti yake ilikuwaje mpaka iweze kuzidi hiyo hali?’ nikamuuliza.

‘Hata mimi sielewi, ila mimi mwenyewe nilijitahidi sana kujizuia, na sauti hiyo ikawa msaada, ni mungu mwenyewe alitaka kuepusha shari. Na cha ajabu kwa muda huo huyo mpelelezi alikuwa nyuma yangu, kwani wakati naingia alikuwa nyuma ya mlango, nikamuhidi, na yeye alianza kujihami kwa kunisalimia,hapo ndipo mwili ulipoanza kusisimuka,...pale niliposikia sauti yake ya salamu....’akasema

‘Oh, sauti zina miujiza yake, moja inakupandisha hasira nyingine inashusha hasira...mh, pole sana...’nikasema

‘Sasa sijui huyu mpelelezi alihisi nini kwani nilipogeuka kumuangalia mpelelezi, nikakuta ameshaondoka, kakimbia, na muhudumu kabaki kaduwaa, akiniangalia mimi na kumuangalia huyo mpelelezi akitoweka, sikuweza hata kumuona alipoelekea, nahisi alishagundua kuwa hali yangu imebadilika...’akasema mdada.

‘Mungu wangu kumbe ingelikuwa ni balaa...’nikasema huku nikitabasamu na mdada aliniangalia huku yeye kakunja uso

‘Ingelikuwa ni balaa, na ujue kuwa balaa hilo ungelikuwa ni wewe umelisababishia, maana kama ungelianimbia mapema kuwa huyo jamaa yako yupo hapo ndani kwako ningelijua jinsi gani ya kupambana naye, ningejiandaa kivingine, wewe ukajifanya huku wauma huku wapulizia, ukabakia kimiya kujifanya upo na mimi kumbe pia upon a huyo mbwa wa wakubwa,...’akasema

‘Mdada unafikiri mimi pale ningelifanya nini, pale nilikuwa nimeshikwa na kigugumizi,wakubwa wananisubiri, muda umeenda, huyo mpelelezi anasikiliza nitakuambia nini, ilikuwa ngumu kwangu kufanya lolote...’nikasema

‘Mhasibu mimi nakuonya, Ole wako...nijue kuwa mna mipango ya kunisaliti, nikigundua kuwa wewe umeamua kunisaliti, nitakubadilikia na hiyo hali ya upendo , itageua kuwa chuki, na ujue kabisa mimi nikikuchukia, amani kwako itakuwa ni ndoto...’akasema

‘Utanifanya nini?’ nikamuuliza na yeye akawa kainama na kusema kwa sauti ya upoke

‘Mhh, mpaka sasa nashindwa kuelewa, kwanini wewe umekuwa tofauti...kiujumla nawachukia sana wanaume, hasa nikiwa na hasira..lakini kwako imekuwa ni tofauti, ni tofauti kabisa...sijui ni kwanini, ndio maana nataka tuishi pamoja, hilo kwangu naliona ni muhimu sana, sijui ...’akasema na kuinua kichwa kuniangalia.

‘Mhh, umeanza mdada, ..’nikasema na yeye akageuza kichwa kuangalia sehemu nyingine na kusema;

‘Nahisi safari nyingine mpelelezi atakuwa makini sana tukikutana naye , maana siku ile kidogo tu, ningeweza kubadili hali ya hewa na huyo mpelelezi, nahisi angeliishia chumba cha wagonjwa mahututi, sijui ingelikuwaje, ni hali ambayo hata mimi naanza uigopa, ni hali ambayo inabadili akili yangu na mwili kuwa sio mimi tena.....’akasema

‘Lakini mdada, ngoja nikuulize kidogo, ina maana hali hiyo ikitokea huwa hujitambui kabisa na huwezi kujua umetenda itu gani, na ukitenda huwezi kukumbuka kabisa kuwa ulifanya jambo gani?’ nikamuuliza na yeye akatulia kama anawaza jambo halafu akasema;

‘Siwezi kujua, au kukumbuka kabisa...’akasema

‘Kwahiyo kama ni hivyo basi inawezekana siku ile wewe ndiye uliyemuua mtoza ushuru, wewe ndiye uliyenipiga na nyundo..’nikasema na yeye akatulia kimiya kwa muda akitafakari , halafu akasema;

‘Unajua hata mimi mwanzoni niliwazia hivyo, kuwa pale hali ilipobadilika huenda mimi ndiye niliyefanya hivyo,...’akasema na kutulia kidogo

‘Lakini niliwazia mbali, kama kweli mimi ndiye niliyemuua mtoza ushuru, basi nitakuwa nimefanya hayo kabla...hali hiyo  ilinitesa sana, ...niaona nijifanyie upelelezi mwenyewe, nikaanza kufuatilia matukio ya hali hiyo huko nyuma kwa kuwauliza watu waliokuwa karibu nami, nikianzia kwa wazazi na ndugu wanaonifahamu, waliniambia kuwa mara nyingi naumiza watu tu kwa mikono yangu mwenyewe...na sijawahi kutumia silaha, na hali hiyo haihitaji silaha, maana mwenyewe nabadilika kuwa silaha....’akasema

‘Mimi nahisi, au nionavyo mimi ni kuwa ni kwa vile labda kwa kipindi hicho hali hiyo ilipokutokea eneo hilo kulikuwa hakuna silaha...wao walijaribu kuficha silaha,...hata hivyo vitu kama bastola panga na vitu kama hivyo, ni nadra kuwepo kila mahali au sio,..lakini kama vingelikuwepo  karibu ungeliweza kuvitumia..’nikasema

‘Yote hayo niliyaangalia na kuwauliza hao watu wangu wa karibu, na wao wanasema eti nina shetani la nguvu, na huyo shetani wangu hataki kutumia silaha, haihitaji silaha,...’akasema na kuinua kichwa juu kama anaangalia kitu.

‘Unajua mhasibu usione naongea hivi ukafikiri naipenda hiyo hali, ...hiyo hali inanitesa sana,  hata hivyo mimi  bado siyaamini hayo mambo ya mashetani, mimi namuamini dakitari wangu ambaye anasema hali hiyo inatokana na shinikizo la majanga yaliyonikuta, hata hivi karibuni niliongea naye, nikajaribu kumuomba anichunguze, kama kweli nilifanya hilo, kuwa huenda mimi ndiye niliyemuua mtoza ushuru...lakini alikataa...’akasema

‘Unahisi kwanini alikataa, huoni kwmba ni kwa vile, anaogopa ukweli...’akasema

‘Ukweli gani kuwa mimi kweli ndiye niliyafanya hivyo?’ akauliza

‘Inawezekana, wewe ni mgonjwa wake, pia wewe ni tajiri wake, anaogopa akikuambia ukweli huenda, itakuumiza sana kisaikolojia. Hata hivyo mimi najiuliza ina maana kuwa yeye anaweza kufanya hivyo, na kujua ukweli ulivyokuwa?’ nikamuuliza

‘Yeye aliniambia anaweza kufanya hivyo, kuna vifaa anavyoweza kuniwekea ambayo vinagusa hizo hisia, na kukulazimisha hiyo hali itokee, na yeye akawa ananihoji na mimi nikawa namuelezea kila kitu, lakini ni hatari,...’akasema

‘Ni hatari kwa vipi?’ niamuuliza

‘Ni hatari kwani anaweza akashindwa kunidhibiti, nikiamua kuchachamaa, alisema pia wasiwasi wake ni kuwa kwa kufanya hivyo, kulazimisha hizo hisia, inaweza ikitokea akakosea, na hapo akamuathiri mgonjwa kabisa, mgonjwa anaweza kuathirika au kupatwa na shinikio la damu, na huenda akapatwa na kiharusi, na hapo uwezekano wa kupona tena ukawa haupo kabisa...’akasema

‘Lakini kwa mtizamo wa dakitari nahisi anaogopa kukuambia tu ukweli, nahisi kagundua ukweli ulivyo, kuwa huenda wewe ulifanya hivyo, uliua, wewe hulioni hilo...?’nikasema na yeye akaniangalia na kukunja uso, na huku anatabasamu akasema;

‘Kwanini unalazimishia kuwa huenda mimi nilifanya hivyo, una wasiwasi na mimi, unaiogopa, kuwa ninaweza kufanya hivyo kwako,...hapana siwezi kufanya hivyo kwako, lakini kama ni kweli , basi ningeshafanya hivyo kabla...’akasema na kutulia

‘Mhh, labda huko nyuma hakukuwa na ulazima wa kufanya hivyo.....’nikasema

‘Mimi nina uhakika sio mimi niliyefanya hivyo, kwasababu nimeshafanya uchunguzi wangu wa kutosha, hebu niambie kwanini unanihisi hivyo?’ akaniuliza

‘Nakuhisi hivyo kwasababu kubwa, pale ndani tulikuwa watu watatu, mimi, wewe na marehemu, na huyo mtu mwingine mimi sikuwahi kumuona na hata wewe unalikubali hilo, sasa kati yangu mimi na wewe, ni nani alifanya hayo mauaji, mimi polisi wamenikamata wakafanya uchnguzi na kugundua kuwa sihusiki, na kweli mimi sihusiki huoni kuwa aliyebakia katika dhana ya kushuku ni wewe, ...’nikasema

‘Mimi nimefanya uchunguzi wangu wa kutosha, na hao polisi walifanya hivyo hivyo, hakuna walichokigundua dhidi yangu, sio kwamba wananiogopa mimi, lakini ukweli wa mazingira upo wazi,unajionyesha wenyewe...’akasema

‘Kwa vipi?’ nikauliza

‘Kuwa mimi sishusiki kwa lolote lile,...wao walilenga sana kwa huyo mtu mwingine,ambaye ni kweli kulikuwa na mtu kama huyo, hata mimi nimeligundua hilo,...kuna mtu aliingia akavunja kabati langu, ni nani huyo, na huyo mtu aliingia hiyo siku, nina uhakika na hilo, na atakuwa anafuatilia kitu muhimu kwao....na pia kuna kitu kingine kinachonipa wasiwasi  ’akasema

‘Kitu gani?’ nikamuuliza nikiwa na hamasa.

‘Kuna dirisha langu huwa halifungi vizuri, sina uhakika sana...’akasema na mimi namkumbuka mpelelezi alivyoniambia kuwa alimuona mlinzi akiingia kwa kupitia dirishani, lakini sikutaka kumuelezea hilo mdada, kwa tahadhari ya mpelelezi, nikatulia nikimsikiliza mdada.

‘Mimi nina uhakika madirisha yote nilifunga, ila hilo moja linanipa mashaka, unajua hali ile ya kuumwa na matukio yenyewe, siwezi kuwa na uhakika, inawezekana kweli siku ile nilisahau kulifunga vyema, lakini nina shaka, na ndivyo hivyo, ni lazima kuna mtu alilifungua,...’akasema

‘Una uhakika gani?’ nikamuuliza

‘Unafahamu, haya madirisha ya viyoo, unaweza ukatumia pisi pisi ukapachua kwa nje,na ukaweza kulisukuma hilo dirisha, na ukifanya hivyo, vile vidude vya kushikilia vinakuwa havina nguvu tena mpaka uvinyoshe,..nahisi hilo dirisha lilifunguliwa, ...sikuwa nimekigundua hicho kitu mapema,ningekuwa na wazo hilo mapema, huenda ningelikuwa na uhakika wa moja kwa moja.....’akasema

‘Kwahiyo unahisi huyo mtu alipitia dirishani?’ nikamuuliza

‘Uwezekano huo upo,..niliwahi kuchukua alama za vidole ili nibahatishe, lakini sikuona alama ngeni, nilizoziona ni zile zile za mlinzi wangu,..., lakini kuwepo kwa alama za vidole vya huyo mlinzi sio ajabu sana, kwani yeye huwa anapita pita mara kwa mara na kujaribu kusukuma  madirisha kuhakikisha kuwa yamefungwa vyema, na kama hayajafungwa vyema anayafunga kwa nje, au ananiarifu niyafunge ndio maana nakuwa na shaka na hilo,...’akatulia

‘Shaka ya...’nikataka kusema na yeye akaendelea kuongea;

‘Hayo madirisha ukiyafunga ukiwa nje, yanajifunga na kujibana kwa ndani, na huwezi kulifungua tena mpaka uwe ndani, hilo dirisha kwa sababu lilipachuliwa, halikuweza kujifunga vyema, huyo mtu alipotoka  alipolifunga kwa nje, lakini hilo dirisha likawa halijajibana vyema...’akasema.

‘Je uliwahi kumuuliza mlinzi wako?’ nikamuuliza

‘Sikuwahi , kwani kipindi hicho alikuwa katoweka, na alipokuja, akaja na taarifa hiyo ya dharura kutokwa kwa ndugu yake, ...na kwa muda huo sikuwa na shaka na yeye kabisa...nilikuwa nimeshamuamini vya kutosha, nilitaka kuongea naye huenda anaweza kukiri na kuniambia ukweli...’akasema

‘Unafikiri kweli huyo jamaa anaweza kukiri ukweli...asema kuwa kweli  aliingia kupitia dirishani! Huoni akisema hivyo, itakuwa ni hatari kwake, na itaonekana kweli yeye alihusika kwenye hayo mauaji, mimi nina uhakika hawezi kukuambia ukweli kama yeye ndiye aliyefanay hivyo...’nikasema

‘Mimi nahisi , yeye kwa kujihami anaweza kusema hivi kuwa wakati anakagua madirisha, alipita hapo akaliona hilo dirisha lipo wazi, na hapo  akawa anahangaika kulifunga...lakini kutokana na hayo matukio hakuwahi kuniambia hilo...kwa kujihami anaweza kusema hivyo...’akasema mdada.

‘Labda , ...ina maana muda wote huo hujawahi kuongea nay eye?’ niamuuliza

‘Polisi hawakuwahi kumpa nafasi hiyo, anaongea na wakili wake tu...’akasema

‘Hata hivyo sizani kama kweli yeye aliingia ndani maana angeliingia ndani hizo alama za vidole ningeziona huko ndani, ....hizo alama za vidole hazikuonekana  kwa ndani..hata lile kabati lililovunjwa halina alama za vidole vyake, kwahiyo huyo mtu aliyeingia ndani atakuwa alivaa kinga mkononi...’akasema

‘Kwanini sasa hukuwaambia polisi?’ nikamuuliza

‘Hiyo ni kazi yao kulitafuta hilo, mimi sikuwahi kuwaambia hilo polisi,na sitawaambia kwani hiyo ni kazi yao, waache wahangaike kivyao, kama wataweza kuliligundua hilo ni kazi yao wenyewe, na hata hivyo wameshachelewa kulifanyia kazi, hawawezi kugundua chochote kwa sasa,...’akasema

‘Sasa huoni kwamba kwa namna hiyo unaficha ukweli, ukweli ambao ungeliweza kuwasaidia polisi kuja kugundua ni nani hasa ni muuaji wa mtoza ushuru, au hutaki huyo mtu agaundulikane..?.’nikasema na kumuuliza.

‘Kuna ukweli mwingine wa sasa hauna maana, maana unaweza kuzua maswali mengi nisiyo yapenda, wanaweza kuanza kuuliza;, kwanini huyo mtu aliamua kupitia dirishani, je huyo mtu alikuwa akitafuta nini, na maswali kama hayo ambayo sipendi kuulizwa ulizwa kwa sasa, mpaka nimalize uchunguzi wangu binafsi...’akasema

‘Mdada, mara nyingi umekuwa ukisema unafanya uchunguzi wako binafsi...uchunguzi gani huo unaofanya na unaufanya ili iweje na kwa ajili ya nani...., hapo ndipo mimi nahisi kwa kuna mtu unamfanyia hiyo kazi, sizani kwamba unafanya hilo kwa kujifurahisha tu, au kwa ajili yako tu...’nikasema

‘Sikiliza wewe mwanaume..., tuyaache hayo, kwanza tumeongea mengi ambayo hayatakusaidia kitu,...’akasema akiangalia saa yake

‘Kwani una haraka gani ...?’ nikamuuliza na yeye akaendelea uangalia saa yake ama anapiga mahesabu ya muda.

‘Mhh, ...nina haraka, ratiba hapa imebana kweli, muda huu nahitajika kuonana na huyo mpelelezi, siku ile tulishindwa kuongea, na  kuelewana, na alinipigia simu baadaye, kuwa anataka tukutane tuongee, siwezi kumkatalia, hata hivyo, na mimi itanisaidia kujua ni kitu gani anakifahamu na kwanini ananifuatilia kihivyo....nikimalizana na yeye nataka kujaribu 
kuonana na baba mkwe wako..’akasema

‘Baba mkwe wangu wa nini, na huyo mpelelezi mnakutania wapi?’ nikamuuliza

‘Ndio baba mkwe wako, nataka kuongea naye mambo mengi tu,..nimalizane naye,...na huyo mtu wako nitakutana naye popote tu...’akasema

‘Popote utajuaje...?’ nikamuuliza

‘Yeye ndivyo alivyodai, popote kwenye usalama wake, kama alivyodai yeye, hakutaka kutaja wapi tukutane ni mjanja sana,nsubiri simu yake au ujumbe wa maneno kutoka kwake ...’akasema

‘Sawa lakini bado nina maswali mengi ya kukuuliza, ...’nikasema

‘Mswali mengi ya nini... au na wewe umegeuka kuwa mpelelezi,...achana na mambo hayo, nikuambie kitu, ,kazi hizo zina wenyewe, na sio kazi rahisi kama unavyofikiria wewe...ni hatari tupu...’akasema

Mara simu ya mdada ikalia, na mdada akaiangalia simu yake na kusema;

‘Mhhh mtu wako huyo, anasema anakuja hapa tulipo...inaonyesha yupo maeneo haya haya, japokuwa ujumbe wake unasema anakuja...tatizo lake anajifanya yeye ni mjanja kuliko mimi...nimegundua kitu, huyu mtu ni hatari sana...’akasema na kabla hajamaliza nikamuona akiinua uso kumuangalia kwa nyuma yangu, nahisi ni mtu na mara sauti kutoka nyuma yangu,ikisema;

‘Ni bora nimewakuta wote wawili, nitaongea na nyote wawili, kama hautajali mdada..’ilikuwa sauti ya mpelelezi, na mimi nikageuka kumwangalia mpelelezi na mdada akasema;

‘Unataka tuongelee hapa hapa, haiwezekani,.....

NB. Tukutane sehemu ijayo

WAZO LA LEO:Afya ya mtu ni kitu muhimu sana, kunapozuka magonjwa hasa ya mlipuko, ni vyema  wenye mamlaka wakachuku tahadhari haraka iwezekanavyo, ni ni muhimu sana kukimbilia kwenye  kinga zaidi, huu tiba zinaendelea. Inasikitisha sana kuwa  magonjwa yanatokea, yakijulikana sababu zake kubwa ni nini, na mengine yamekuwa yakirudiarudia, na vyanzo vya magonjwa hayo vinajulikana.Harakati zipo wapi za kupambana na hivyo vyanzo?

Kwanini tusifanye kitu kama harambe za pamoja , kila kata, kila nyumba kumi, watu wakapewa madawa ya kupulizia maeneo yao, na kuhakikisha kuwa hawa wadudu ambukizi wanatokemezwa kabisa, na kitu kama malaria, kipindu pindi na sasa homa hii ya dengue vinakuwa na historia, ...cha muhimu  sana kwa sasa ni kupambana na mazalio ya hawa wadudu, kuwa na mikakati ya usafi, imewezekana kwingine kwanini jiji la Dar, inashindikina.


Ajabu kabisa, tatizo linatokea na wengine wanalitumia hilo tatizo kibiashara zaidi, tutakula wapi!, Matibabu  sasa ni gharama kubwa, kama ilivyo elimu, hawa maadui wawili ujinga na maradhi wanazidi kuneemeka na kuneemesha wengine wakati asilimia kubwa wanaumia..., sasa hivi wenye uwezo, waheshimiwa  wanachoangalia ni masilahi yao tu, hilo lipo wazi...hivi jamani hata hili la homa ya dengue, inayosababishwa na mbu hatuwezi kupambana nayo mpaka tupate misaada toka nje, au ndio neema nyingine kwa biashara ya madawa, ama kweli kufa kufaana.

Ni mimi: emu-three

No comments :