Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeWednesday, May 14, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-57


Upande ule waliokuwepo mwanadada kulionekana hakuna maelewano, lakini muda wa mahakama ulipofika wakatulia, na mimi ile taswira ya yaliyotokea nyuma ikagota, nikatuliza kichwa changu kusikia kinachoendelea leo mahakamani, lakini moyo wangu haukuwa na amani kabisa.

Kesi ilianza na kilichotawala siku hiyo ni mabishano ya mawakili hao wawili mtetezi na muongoza mashitaka, mabishani hayo kwa sasa yalilenga ni nani asimamishwe kutoa ushahidi, na watetezi waling’ang’ania kuwa mimi na mdada tusimamishwe kwanza, kabla hawajamruhusu mtuhumiwa kutoa maelezo yake, na hapo mwendesha mashitaka, akasema;

‘Mdada na mhasibu ni mashahidi wangu na mimi ndiye ninayejua ni muda gani nitawasimamisha, hamuwezi kunishurutisha kwa hilo,…’akasema mwendesha mashitaka na wakili mtetezi akasema;

‘Sasa kwanini wewe unang’ang’ania kuwa nimsimamishe mteja wangu, wakati unafahamu kuwa hata mimi nina mpangilio wangu , kwanini ulianza kuniingilia mpangilio wa kazi zangu. Ndugu muheshimiwa hakimu, mimi naona kuwa mdada na mhasibu ni mashahidi muhimu sana, kwani wao ndio waliokuwepo humo ndani wakati mauaji yanatendeka…’akasema  wakili mtetezi

‘Hata ama walikuwepo, lakini tendo hilo hawakuliona ...’akasema wakili muendesha mashitaka

‘Hayo unawasema wewe, ni muhimu wakasimama na kujieleza wenyewe ili haki itendeke, sisi tunahisi kuna jambo mnaficha,...’akasema wakili mtetezi

‘Lakini hebu rejea maelezo yako ya kesi iliyopita wewe mwenyewe ulisema leo ndio aambayo mshitakiwa ataweza kutoa maelezo yake, lakini hadi sasa unawasimamisha mashahidi wengine huoni kuwa unamyima haki mteja wako, wakati alishajiandaa kutoa maelezo yake..’akasema muendesha mashitaka

‘Unajuaje kuwa alikuwa kajiandaa kuongea leo hata kama ni hivyo, lakini mimi naweza kubadili ratiba, kwa mpangilio wangu, na hilo halikuhusu wewe, yeye ni mteja wangu na hao niliowasimamisha ni mashahidi wangu nikitaka kujenga hoja kuwa mteja wangu hakuhusika na hayo mauaji, …’akasema wakili mtetezi

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, sisi tulikuwa tumeshajiandaa kumsikiliza mshitakiwa, kama ilivyokubalika katika siku ya kesi iliyopita, lakini cha ajabu tunashangaa leo wanasimamishwa mashahidi wengine,nahisi  wenzetu wanamnyima haki mshitakiwa, na wanatufanya na sisi tuanze kujipanag vingine,…’akasema wakili muendesha mashitaka

‘Kwahiyo wewe upo upande gani?’ akauliza wakili mtetezi na wakili muendesha mashitaka akatabasamu na kusema;

‘Mimi ni muendesha mashitaka na lengo letu ni kuona haki inatendeka , sio kwamba kwa vile ni muendesha mahitaka basi nitashikiza mshitakiwa kuchukuliwa adhabu tu, hapana ni lazima hatua zote zifuatiliwe ikiwemo mshitakiwa kupewa nafasi ya kujitetea, kama alivyoomba yeye mwenyewe...’akasema wakili huyo

‘Lakini hakimu hajasema kuwa mshitakiwa ajitetee, na hili litafika atasimama na kufanya hivyo, lakini kwa mpangilio wangu mimi kama mtetezi wake…’akasema wakili mtetezi,na hapo hakimu ikabidi aingilie kati na kuuliza;

‘Je upande wa utetezi, mnatarajia  kumsimamisha mshitakiwa lini, maana kwenye kumbukumbu zetu kweli ulitakiwa kumsimamisha mshitakiwa leo kutoa maelezo yake, lakini muda unakwenda, hujamsimisha na sasa unataka shahidi mwingine asimame kutoa maelezi,…?’ akaulizwa wakili mtetezi

‘Bado naendelea na mashahidi wangu wa utetezi, na muda ukiruhusu nitamsimamisha mshitakiwa muheshimiwa hakimu, nalifahamu hilo na hapa ninajenga hoja, ili akisimama kila kitu kiwe wazi…’akasema wakili mtetezi na wakili muendesha mashitaka akaingilia kwa hoja.

‘Tunaomba sababu muhimu za kuendelea kumchelewesha huyo mshitakiwa... kwani kama ni kujenga hoja, sio katika hatua hii, hatua hii ilikuwa ya kuiweka wazi hoja na kutoa hitimisho’akasema

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, sisi tulitaka watu wawili wasimame kutoa ushahidi wao kwanza kwa upande wao, lakini upande wa wenzetu wakadai hao ni mashahidi wao, hatuna mamlaka ya kuwasimamisha mpaka waidhinishwe kama mashahidi wetu…'akasema na kuendelea kusema;

'Sasa ninachoshangaa ni kuona wao wakitaka mtu wetu ndiye asimame, na ikionyesha kuwa ni hitimisho,hili halitawezekana mpaka hao mashahidi wawili wasimamishwe, ili na wao waeleze jindi ilivyotokea siku hiyo, tuna uhakika kuna ammbo mengi hayajawekwa wazi, na wakisimama hao watu hayo mambo yatabainika.’akasema wakili mtetezi.

‘Sisi tuna mapangilio wetu, na tunafahamu kwanini hawa watu hawajasimamishwa, ..wao, hawakuona tukio la mauaji, na kuna watu wameshatoa maelezo ambayo hata wao wakisimamishwa watayatoa hay ohayo,....ni marudio tu..’akasema wakili

‘Lakini sisi hatujarizika na hayo maelezo waliyotoa wengine, kwanini yatolewe na wengine wakati wao wapo,....na kwanini muombe mshitaiwa asimame, je mshitaiwa ni shahidi wenu?’ akauliza wakili mtetezi.

‘Sisi hatujasema asimame kama shahidi wetu,...yeye mwenyewe aliomba kusimama kutoa maelezo yake, baada ya kuona nyie mnatoa mashahidi wasiotosheleza kile alichokiona yeye….’akasema wakili huyo na hapo hakimu akawaita mawakili hao wawili mbele na kuanza  kuteta nao, walichukua muda kidogo na baadaye hakimu akasema;

‘Kwa vile muda uliobakia ni mchache, na tumeona kuwa mshitakiwa akianza kutoa maelezo yake itachukua muda, kwahiyo upande wa waendesha mashitaka ni zamu yenu kutoa mashahidi, na muda uliopo utatosha kutoa shahidi mmoja, ambaye hatachukua muda sana…’akasema wakili na muendesha mashitaka akiwa kama hajajiandaa kwa hilo akasema;

‘Japokuwa sisi kwa upande wetu tulishajiandaa kumsikiliza mshitakiwa , lakini wenzetu kwa namna yao wameendelea kumyima haki yake, hata hivyo sisi tupo makini wakati wote na tumesha jitosheleza kwa hilo, na katika moja ya hoja za watetezi ni kuwa wanawahitajia mdada na mhasibu kuja kutoa ushahidi wao, sisi hatuna pingamizi kwa vile tunajiamini,na tunajua ni nini tunachokifanya …’akasema muendesha mashitaka na wakili mtetezi akatoa pingamzi na kusema;

‘Ndugu muheshimiwa hakimu, wakili muedesha mashitaka anapoteza muda, badala ya kumsimisha shahidi wake, yeye anatoa maelezo, hiyo ni mbinu ya kupoteza muda, na hakimu akasema;

‘Hiyo sio kazi yako wakili mtetezi, ,....’akasema hakimu na kuangalia saa, halafu akasema;

‘Wakili muendesha mashitaka, msimamishe shahidi yako…’akasema hakimu na muedesha mashitaka akasema;

‘Nitamsimamisha mhasibu,aje kutoa ushahidi  wake…’akasema.

Alipotamka hilo, nikabakia mdomo wazi, sikutarajia, na nilijua kama ni kutoa ushahidi, mdada angeitwa kwanza. Kwa muda ule, nilikuwa kamamtu aliyebebeshwa mzigo mzito bila kujiandaa japokuwa tulishaarifiwa kuwa mimi na mdada wakati wote tunaweza kusimamishwa kutoa ushahidi na ndio maana siku hiyo tulikuwa nje, upande wa mashahidi.

‘Mhasibu unahitakiwa kuingia ndani ukatoe ushahidi….’nikasikia sauti ikiita na mimi wakati huo nilikuwa mbali nikiwazia tukio lililopita, nilikuwa nakumbuka kauli ya wale waheshimiwa wakati nilipoitwa kwenye ofisi ambayo sasa inaitwa ofisi yangu, na wale wakubwa na katika moja ya maelezo yao ni kuwa niwe makini wakati wa kutoa usahhidi wangu, nisije kuongea mambo ambayo hayanihusu

‘Mambo kama yapi ?’ nikauliza nikianza kuingiwa na wasiwasi kwani ilionyesha dhahiri kuwa kesi ijayo nitasimamishwa kutoa ushahidi.

‘Unaweza kuulizwa kuhusu marehemu  na kazi yake,ujue wewe hukuwahi  kufanya kazi na marehemu na kwahiyo hakuwahi kujua kiundani ni kitu gani alikuwa akikifanya,  kwahiyo huwezi kujua lolote linalomuhusu yeye, kwahiyo ukiulizwa mambo yake ni bora useme hujui lolote, usije ukaropoka tu...kwa labda kuna mambo umeyaona humu ndani au umesikia lolote kuhusu yeye na ofisi yake, ukifanya hivyo ni kosa maana utakuwa unatoa siri za ofisi ambazo hazihusiani na hiyo kesi….’akasema mmoja wapo.

‘Sizani kama wanaweza kuniuliza mambo kama hayo, na hata wakiniuliza hayo mimi nitakuwa makini jinsi gani ya kujibu…’nikasema kwa kujiamini

‘Ufahamu mawakili ni wajanja sana, wakiwa wanatafuta jambo wanaweza kutumia njia yoyote ya kukupoteza akili yako, na unaweza ukayumbushwa na kujikuta umeropoka bila hata kutarajia, sisi tuna uzoefu na hayo, ….’akasema huyo muheshimiwa.

‘Nitakuwa makini kwa hilo...’nikasema

‘Na jingine ni kuwa huu mkataba tunaokupa sasa hivi ndio utakaotambulikana rasimi...’akasema

‘Sizani  kama ulishawahi kupewa mkataba wowote kabla, ambao una orodha za vitu vyote vilivyokuwemo humu ndani na ambavyo unatakiwa kuvifanyia kazi..’akauliza mwingine akiniangalia kwa makini.

‘Mkataba,..na orodha, hapana...nakumbuka niliambiwa nisubiri hadi hapo kesi itakapokwisha,..naona ajabu leo….’nikasema na kabla sijaendelea zaidi huyo muheshimiwa akanikatisha na kusema;

‘Usione ajabu, hii nafasi inahitajika mtu awepo, angalau afanye kazi ..., hatuwezi kuacha shughuli ziende kienyeji japokuwa kuna watendaji wengine wanaendelea kufanya zile kazi za marehemu, lakini hata hivyo, hapa kulikuwa na ofisi maalumu, na kuna mambo ambayo yanahitaji mtu kuyasimamia, haya yaliyopo humu ni mambo nyeti, hatuwezi kumpa mtu yoyote tu,, na kwa vile wewe umeaminiwa,ni vyema ukayafanyia kazi...’akasema

‘Lakini ....’nikaamza kujitetea

‘Hakuna cha lakini, hakuna kitu kigeni, hakuna kitu kigumu, kinachohitajika kwa sasa ni kuhakikisha kuwa kumbukumbu muhimu zipo mikononi mwa mtu mwaminifu, mengine yapo kwenye mitandao, na hayawezi kupotea, lakini kuna kazi zipo humu, zilikuwa hazijafanyiwa kazi, na nyaraka za siri ambazo hazitakiwi kusambaa ovyo...’akasema

‘Lakini  orodha ya vitu hivi naona kama haijakamilisha baadhi ya vitu, nakumbuka wakati walipokuwa wakinisaili wale waheshimiwa kuna vitu walinionyesha, hapa sivioni….’nikasema

‘Vitu kama vipi,...wewe huwezi kujua vitu gani unastahili kukabidhiwa na vitu gani unastahili, sisi ndio tunaofahamu  hilo, kwahiyo wewe unachotakiwa kwasasa ni kupokea huu mkataba kama ulivyo, na vitu vilivyomo,huna haja ya kudadisii kitu ambacho hakipohumu, umenielewa…’akasema na mwenzake akaitikia kwa kichwa

‘Na hata kwenye kesi ikatokea kuulizwa makabidhiano ya ofisi , wewe utasema ulikabidhiwa kama inavyoonyesha hapa, kabla ya hapo, kama uliona kitu fulani , na sasa hakipo, huna haja ya kuumiza kichwa chako, hivyo visahau katika kichwa chako, …’akasema

‘Na je wewe uliwahi kupitia kabla na kuangalia vitu vyote alivyoviacha marehemu humu ndani?’ akauliza

‘Hapana sikuwahi kufanya hivyo, maana nilikuwa sijakabidhiwa ofisi …’nikasema

‘Unaonaeeh... , hilo ndilo jibu sahihi, na popote utakapoulizwa unatakiwa kusema hivyo,na kwa vile umetuelewa, sisi hapa hatuna zaidi, kwa leo tunaishia hapa, lakini tutaendelea kuja mara kwa mara kukuelekeza baadhi ya kazi kabla hujaanza kazi rasimu...’akasema muheshimiwa.

‘Kiujumla bado hujaajiriwa, kama unavyosoma huu mkataba ni ajira ya muda, ya majaribio,...unachofanya kwasasa ni kushikilia ofisi hadi hapo kesi itakapokwisha, ….natumai umetuelewa’akasema na wakasimama na kunyosha mikono tukashikana na wakaondoka zao.

Walipoondoka waheshimiwa hawa , nikawa nausoma ule mkataba, na mara mlango ukagingwa,akaingia mdada, nilishasahau kabisa habari zao, na nilipomuona nikawa na hamu ya kujua ni kitu gani kimetokea kati yake na mpelelezi, yeye akionyesha hasira usoni, akasema;

‘Mumemalizana na watu wako, ...?’ akauliza

‘Ndio, je na wewe umemalizana vipi na ...’nikasita kuendelea na yeye akasema;

‘Nasikia kesho mimi au wewe tutasimamishwa kutoa ushahidi, kwahiyo tunahitajika kujiandaa…’akasema na alionyesha hakutaka kuongea yaliyotokea kati yake na mpelelezi

‘Ni nani kakuambia?’ nikamuuliza nikimuangalia usoni na yeye akaangalia ule mkataba, akauchukua, na kabala haujaugusa akawa kama aumbuka jambo, akachukua kidude chake wenye moba akatoa kitambaa cheupe, akapitisha juu juu kwenye ule mkataba halafu akakiweka kile kitambaa kwenye kitufe fulani, akasubiri.

‘Yah, ndio wao...hamna shaka...’akasema

‘Ndio wao wamefanya nini?’ nikamuuliza

‘Mumeongea nini na hao watu?’ akaniuliza badala ya kujibu swali langu

‘Kuhusu makabidhiano ya ofisi na vilivyomo, na ya kuwa huu mkataba ndio unaoonyesha kila kitu ninachotakiwa kuwa nacho, hakuna zaidi ya hayo yaliyoandikwa hapo...’nikasema

‘Nilijua tu....’akasema

‘Kwahiyo wewe umegundua nini?’ nikamuuliza nilipoona akiweka kile kidude kwenye mkoba wake, nay eye bila kujali swali langu akasema;

‘Muendesha mashitaka kasema wewe au mimi au wote wawili kesho kuna uwezekano mkubwa wa kusimama kutoa ushahidi,….’akasema na kunifanya niishiwe nguvu, kwani nilijua kikombe hicho kimeshapita kumbe mambo bado na hadi muda huo sikuwa nimefikia uamuzi kuwa nisimamie upande gani...’nikasema

‘Sasa naona muda umefika kusema ukweli wote maana siwezi kuapa kwa kitabu kitakatifu halafu niseme uwongo, mimi siwezi hilo kabisa...’nikasema

‘Sawa, kwani nani akuambia useme uwongo, ...sema ukweli, lakini uwe ukweli kwa masilahi yako, ukisema ukweli wa kukuangamiza sijui kama hata mungu atakusamehe...’akasema

‘Mimi sikuelewi, ina maana ninachotakiwa kusema ni ukweli wa kunipendelea, je kama unanipendelea mimi na kukuweka wewe hatiani, nitafanyaje?’ nikamuuliza

‘Kama ni ukweli, ....nijuavyo mimi, hakuna cha kuniweka mimi hatiani, labda uwe hujatumia akili yako,...nimekuambai ukweli uwe ukweli kweli...siwezi kukufundisha kila kitu cha muhimu,kwanza jua ni nini unachokifanya, na adui yako ni nani, maana hapo ujue unapambana na adui...’akasema

‘Adui yetu ni nani?’nikauliza

‘Hilo swali la kuniuliza, wewe mwenyewe unawaona, watu ama hawa, ambao wanachukua vidhibiti na kuvifisha, watu kama hao, ambao lengo lao ni kujijali wenyewe, ...hao ndio uwaangalai kwa jicho jingine, na hao ndio wauwaji...’akasema

‘Lakini...’nikaanza kujitetea

‘Hakuna cha lakini hapa...ukifika sema kila kitu, wao wamekuja kuiba nyaraka, wamezipeleka wapi...halafu wanakuabidhi mkataba kama huu, mimi ninao mkataba wa awali ambao ulitakiwa upewe, na humo kuna kila kitu, ikibidi mimi nitautoa kama ushahidi, wasitubabaishe,..unasikia sema kila kitu...’akasema

‘Mhh, mdada huoni hapo tutajichanganya, mimi naona muda wa kufanya hivyo haujafika,....’nikasema

‘Wewe unasubiria muda gani tena...mtu wa ajabu sana wewe, siri ya ushindi ni kuwa kama unapambana na adui, na mara ukimpatia adui yako nafasi, ...mshindile makonde ya nguvu ili aishiwe nguvu, ukimuachia hiyo nafasi, atakuja ufahamu udhaifu wako, ...na unakuwa umeshampa nafasi ya kuweza kukuzidi nguvu,....’akasema,  na mimi nikawa imiya nikikumbuka maneno ya mpelelezi

‘Kama utasimamishwa kabla ya mshitakiwa hajatoa maelezo, uwe makini na ile utakachokielezea, cha muhimu ni ukweli, huku ukivuta muda, kwani wakati muafaka wa kusema kila kitu haujafika, ..

‘Wakati gani muafaka wa kusema kila kitu...?’ nikamuuliza

‘Wakati mshitakiwa akishamaliza kutoa maelezo yake, hapo utajua ukweli wake, je yupo na kundi au na jamii,...’akasema

‘Mimi kwakeli hapo sijui, maana tangu mwanzo unasema niseme ukweli na nafasi ya kusema ukweli imeshafika, nab ado unaniambia nisubiri, ...mbona mnanichanganya...’nikasema

‘Unajichanganya wewe mwenyewe, kwasababu kama ungeniambia ukweli wote toka awali mimi ningejua nifanye nini, na huenda kesi hii ingelishamalizia, lakini wewe na mdada mna ajenda ya siri,..sijui mna ajenda gani...’akasema

‘Hata mimi sijui...’nikasema na mara sauti ikasema;

‘Mhasibu pita mbele na inua mkono wako utoe kiapo cha kusema ukweli...’sauti ikanishitua

NB: Haya ukweli utaanza kuelezewa


WAZO LA LEO: Ikitokea upo kati kati ya sintofahamu, kila mtu anataka usimamie upande wake, na wewe unashindwa kujua usimamie wapi, cha msingi ni kuangalia ukweli na haki ipo wapi. Usiogope kulaumiwa, kwani lawama hizo ni za muda, ogopa kujuta kwa kusema yasiyo kweli na haki, kwani majuto huja baada ya athari, na huwezi kujua athari hiyo itadumu kwa muda gani na ni yupi ataumia.

Ni mimi: emu-three

No comments :