Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeTuesday, May 13, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-56


Mdada  alifungua mlango , akionyesha kabisa yupo tayari kwa shari, mimi nikawa nasubiria nione ni kitu gani cha kufanya, sikuwa na amani pale nilipokuwa nimekaa, hata hivyo wa muda ule sikuweza kuingilia, nikasubiria kwanza. Mlango ukafunguka nusu, nikashangaa kumuona mdada kasimama huku kaduwaa, na huku kashikilia mlango, mara nikasikia akisema;

‘Oh ni wewe....’akasema huu akifungua mlango zaidi na kuchungulia kwa nje, halafu akasema;

‘Lakini sio wewe uliyegonga mlango mwanzoni, yupo wapi aliyegonga mlango mwanzoni?’ akauliza, na sauti niliyokuja kuitambua kuwa ni mfanyakazi wa humo hotelini ikasema;

‘Mimi nimeambiwa nije kufungua chumba hiki, na kuangalia kama ninaweza kufanya usafi, kwani kuna wakubwa wanakuja kufanyia mkutano wao humu, sina habari ya mtu huyo unayemuulizia,….’akasema huyo mfanyakazi wa hiyo hoteli na mdada akasema;

‘Haiwezekani,..hata hivyo, kwani nyie mnakuja kufanya usafi hata kama mwenyewe hayupo, hii ni ofisi ya watu au sio, kuna mtu anatumia chumba hiki kama ofisi,ulimfahamisha hilo?’ akauliza mdada

‘Mimi sijui hayo, maswali kama hayo kamuulize bosi wangu, ninachofanya mimi ni kufuata amri, hata hivyo nimesikia kuwa huyo mtu anayetumia hii ofisi hayupo, hapatikani,… hata kwenye simu akipigiwa hapatikani,  kazima simu yake...nasikia alikuwa huko mahakamani, wametumwa watu huko hawakumkuta, ndio hivyo ikawa haina jinsi maana wakubwa wanahitaji hii ofisi…’akasema.

Ni kweli mdada,alininiambia awali kuwa nizime simu yangu kwahiyo huenda kweli walimtafuta kwenye simu wakanikosa;

‘Lakini hao ni wakubwa gani, au ni wale walinionifanyia usahili, ...’nikawa najiuliza mdada, na wakati huo mdada alikuwa kanigeukia, na kusema;

‘Una mgeni wako, anataka kufanya usafi humu ndani...’akasema na bila kusubiri kauli yangu akamgeukia huyo mfanyakazi na kusema;

‘Haya unaweza kufanya usafi , lakini sioni kama kunahitajika huo usafi, kupo poa, au vipi, hebu ingia mwenyewe maana nisikuingilie kazi yako...’akasema na akamshika yule mfanyakazi mkono, na kusema;

‘Utasema kila kitu kipo sawa, nitahakikisha hilo au unasemaje....’akamuongelesha kwa sauti ndogo na yule mfanyakazi akasema;

‘Na wewe dada bwana, huachi vituko vyako, haikuwa na haja kufanya hivyo, sawa mimi sina shida, nimemaliza...’akasema na kuondoka

‘Mhasibu, huyu mtu aliyegonga, kayeyuka, nahisi yupo mahali, anakusubiria, sasa mimi sitacheza mbali, mpaka nionane naye leo hiii, nina hamu ya kuonana naye, sitamuacha hivi hivi , nataka anikome,...’akasema

‘Una uhakika kuwa ndio yeye aliyegonga...?’ nikamuuliza

‘Nina uhakika, nina macho ya nyuma na mbele, mimi sio kama unavyonifikiria, unasikia hata kama nisipoonana naye leo, ukionana naye, mwambie anikome, ....’akasema mdada

‘Sawa mjumbe hauwawi, ...lakini jamaa huyo hana matatizo kabisa, ni wewe tu unayemfikiria vibaya...’nikasema

‘Sasa sikiliza kwa kauli ya huyu mhudumu, ni kuwa unatafutwa na wakubwa zako, kinachotakiwa sasa washa simu yako, wakikuuliza sema iliisha chaji au vyovyote vile,na usije kusema ulikuwa na mimi…’akasema mdada huku akitembea kuelekea kwenye lile kabati lililokuwa na nyaraka,akalichunguza halafu akageuka kuniangalia  na kuuliza;

‘Una uhakika kuziona hizo nyaraka karibuni na lini kwa mara ya mwisho ulifungua hili kabati...?’ akauliza

‘Jana, hata asubuhi wakati nimefika hapa ofisini abla sijaelekea huko mahakamani, nilifungua kabati na kila kitu kilikuwepo, basi kama ni mtu kaja kuchuua kafanya hivyo, kipindi tukiwa mahakamani,....’nikasema

‘Atakuwa nani,...na kwanini afanye hivyo?’ akauliza mdada huku akiwa akiniangalia kwa macho ya kujiuliza

‘Siwezi kujua kabisa, kwani walishaniambia kuwa hakutakiwi kitu chochote kiyolewe humu ndani, na vyote vipo kwenye mikono yangu, ndio maana wakanipa ufunguo za hizo kabati, kama kuna mtu atahitaji kitu inabidi awasiliane na mimi, na kwa hili lilitokea, inabidi nitoe taarifa...’nikasema

‘Usifanye hivyo, kaa kimiya kama hujui kitu...’akasema mdada na kunifanya nimuangalia kwa mshangao.
‘Kwanini sasa, kama nisipofanya hivyo huoni mimi naweza kushukiwa vibaya, watu wameniona mimi na wewe tukiingia humu,....’nikasema

‘Ndio maana nasema usiseme kitu, kwani utaonekana kama unajihami, cha msingi kama utaulizwa chochote kuhusiana na hizo nyaraka, wewe sema kwa mara ya mwisho uliziona,...hujafaungua tena hili kabati, inatosha, mengine waachie wao wenyewe, usiumize kichwa kuwafikiria wao, kitu gani watasema, ...’akasema mdada

‘Tatizo lako mdada, kila mara unataka kunitia matatani, hujui hiyo ni dhamana ya watu nilikabidhiwa mimi, ..’nikasema

‘Hebu kidogo nifikirie....’akasema na kushika kichwa, halafu akageuka na kusema;

‘Hao jamaa wanaokuja kufanya kikao, nawashuku,kuna kitu wanataka kuhakikisha, na huenda hawataulizia hilo, na nia yao ni kubadili kumbukumbu, wanaweza kuja na makabrasha mengine yakiwa na orodha ya vitu vingine, lakini , …’akasita kidogo

‘Lakini nini?’ nikauliza

‘Hizo nyaraka za awali hazitatambulika tena, ndio zimeshapotea hivyo, sijui kwanini sikulifanyia hili kazi mapema,...hata hivyo, bado nina ushahidi mwingine mkubwa tu...’akasema

‘Ushahidi gani?’ nikauliza

‘Unakumbuka,.... marehemu alipokuwa kwangu, alikuwa akitaka nini wangu,..moja ya vitu alivyouwa akivitafuta kutoka kwangu ni pamoja na nyaraka muhimu nilizokuwa nazo mimi,,....wakati tupo mle ndani, kuna watu walivunja kabati langu la kumbukumbu zangu, wakijaribu kuzitafuta hizo nyaraka, lakini hawakuzipata, bado nina nondo za kutosha...’akasema

‘Sikuelewi..wewe hizo nyaraka ulizipata vipi.? ’nikamuuliza

‘Sio tatizo, usiumie kichwa kwa kuliwazia hilo, ...’akasema mdada,na kabla hajamaliza simu yangu ikaanza kuita,nikaangalia jina la mpigaji,  na mdada akaniuliza ni nani, na kwa muda huo alikuwa na simu yake mononi akiangalai kitu, na mimi niasema;

‘Hii namba ni ngeni kwangu, sijui ni nani….’nikasema na mdada akaniashiria nisubiri kidogo, wakati huo simu inaendelea kuita, mdada akawa anaangalia kitu kwenye simu yake, akawa anafanya jambo na kwa haraka akasema;

‘Pokea hiyo simu…’na huu akiendelea kuangalia simu yake

‘Upo wapi,mbona hupokei simu, ulikuwa umelala nini, sisi tunakutafuta sehemu zote hupatikani na simu ulikuwa umezima, sasa sikiliza, tunahitajia kufanya kikao hapo kwenye ofisi yako, lakini hatujui upo wapi,…’sauti ikasema

‘Mbona nipo hotelini kwangu…’nikasema

‘Sawa..hamna shida, ila ni kukuarifu tu kuwa, kuna mfanyakazi wa hapa hotelini tulimtuma kuja kufanya usafi, usije kushangaa, maana hukuwa hewani, pili sisi tupo njiani tutafika tuonane hapo ofisini kwako..’sauti ikasema

‘Sawa nitafika hamna shida..’nikasema

‘Nusu saa inatosha, au sio,  tukukute ofisini  kwao, hatutachukua muda wako mrefu, …’sauti ikasema na mzungumzaji akakata simu, na mdada akasema;

‘Hawa watu wamo humu humu ndani kwenye hoteli, wapo chini,wamesema nini...?’akauliza mdada

‘Mbona wamesema wapo njiani, ?’ nikamuuliza na yeye akatabasamu na kusema

‘Wapo humu ndani, hii ni kuonyesha kuwa kuna jambo, sio watu wa kawaida, ni wakubwa lakini wanajua ni nini wanachokifanya kuwa makini...’akasema huku akiangalia saa yake, na kusema;

‘Umepewa nusu saa, au sio...’akawa kama ananiuliza huku akikikagua hicho chumba kwa macho, na baadaye ukaingia ujumbe kwenye simu yake, akausoma na kusema;

‘Hao ni wakubwa wa idara ya ushuru, ni kweli,wana kikao leo hapa ofisini kwako, sio kikao rasimu, kwahiyo kuna ajenda ya siri, unatakiwa kujiandaa kujibu maswali yao,na sijui utasema nini wakiuliza kuhusu hizo nyaraka, na sizani kama watauliza hilo, na huenda wakaja ya nyaraka nyingine, kuwa makini na hilo…’akasema na akachukua ufungua wa lile kabati.

Wakati huo ufunguo, ulikuwa mezani, akauchukua ule ufunguo lakini mononi alikuwa leso, inaonekana hakutaka kuligusa lile kabati kwa mikono yake mitupu, akalifungua lile kabati, akachukua simu yake na kupiga picha mle ndani, na akawa anachukua picha za video kwa sekunde chache, alipomaliza akatoa kitambaa kikasha, na kutoa kitambaa cheupe, akawa anapitisha kwenye mshikio wa hilo kabati, alikuwa akifanya hivyo kwa tahadhari, hakutaka kugusa kitu, nahisi alikuwa akichukua alama za vidole.

‘Najaribu kufanya hivi, japokuwa haisaidii sana, ...’akasema na kukiweka kile kitambaa kwenye kikasha fulani, ...okey, nimemaliza, akafunga, halafu akaichukua ile fungua akiwa na leso, akaifuta vyema, na kunikabidhi mimi...

‘Lakini huo sio ufunguo wangu...’nikasema.

‘Okey, sawa, nimesahau...’akasema na uzichukua funguo zake, akaziweka kwenye mkoba wake, halafu akasema;

‘Nahisi hawa watu ndio wamezichukua hizo nyaraka, ngoja vijana wangu wafanye hiyo kazi...’akasema na kuandika ujumbe kwenye simu yake

‘Kama walizichukua wao,ina maana wana ufunguo wa hapo,kwanini sasa wakawa wanakutafuta wewe ili waweze kuingia humu,huoni kama kuna kitu ..anyway,let the time  tell, …watakuwa wameomba wa wahusika wa hapa hotelini, bila shaka’akasema mdada akiangalia saa yake na kusema

‘Nenda hotelini kwako,kachukue hizo ufunguo,na uje hapa haraka, zimebakia dakika kumi na tano…’akasema

‘Na wewe,?’ nikauliza na yeye hakuniangalia akawa anaendelea kukagua hicho chumba kwa macho, na mimi nikamuuliza tena;

‘Na wewe unafanya nini humu ndani,..maana sizani kama itakuwa vyema uendelee kubakia wewe mwenyewe  humu ndani…?’ nikiamuuliza

‘Wewe nenda kajiandae kukutana nao,…hayo mengine niachie mimi mwenyewe, bado natafakari kuhusu huyu mtu wako, nina imani ndiye aliyefika mwanzoni akagonga mlango,pili kuna mambo nayaweka sawa,  ….’akasema akitoa vifaa kwenye mkoba wake, nikaona nisipoteze muda, nikasema;

‘Kama ndio yeye huyu unayesema ni jamaa yangu kuwa ndiye aliyeginga mlango, kwanini mhudumu hakumuona….?’nikauliza

‘Janja yake nitagundua tu….inaonekana sio mtu wa kawaida, lakini ajue mimi ni zaidi yake’akasema mdada na kuanza kuwasiliana na watu wake, na wakati huo mimi nikaondoka na kuelekea chumbani kwangu,nikafika na kufungua mlango,nikiwa na haraka maana muda ulikuwa unakwenda kwa kasi, nikaona niwashe taa...

‘Wewe huwa unawasha taa hata mchana….’Nikasikia sauti ikitoka nyuma yangu na kunifanya nishituke karibu ya kudondoka chini, ilikuwa ni sauti ya mpelelezi aliyekuwa kasimama pembeni ya mlango

‘Oh umeingiaje humu ndani namna gani?’ nikamuuliza nilipohakikisha kuwa nay eye na yeye akatabasamu na kusema;

‘Ukiwa kwenye kazi kama yangu hilo swali sio muhimu sana …naweza kuingia mahali popote, cha muhimu ni kuhakikisha kuwa usalama upo…’akasema

‘Sina muda wakubwa wanatakakuonana na mimi na sijui ni kitu gani wanatakakuongea na mimi…’nikasema

‘Je ulifanikiwa kumzuia mdada asizichukue hizo nyaraka?’ akaniuliza

‘Umejuaje kuwa anazihitajia hizo nyaraka,…?’ nikauliza

‘Jibu swali langu,ni muhimu sana’akasema

‘Hizo nyaraka hazipokwenye hilo kabati, na walasijui ni nani kazichukua…’nikasema

‘Haiwezekani,…sasa hilo ni tatizo,una uhakika hajazichukua huyo mdada…?’ akaniuliza

‘Yeye ndio alikuwa akizihitajia, na akanishauro nifungue kabati, na tulipofungua hatukukuta kitu, hata yeye alishikwa na mshangao, hajui ni nani kazichukua..’nikasema
Mpelelezi,akachukua simu yake na kuongea na mtu, nilimisikia akisema;

‘Ule ushahidi umetoweka…’akasema na kusikiliza kwa muda

‘Sawa,..kwahiyo tufanyaje, sijajua ni nani kazichukua …yah,nitamtafuta , na ni lazima atagundua kuwa  ni nakala,….’akasema na kusikiliza kwa muda, halafu akasema;

‘Ndio,anakwenda kuonana nao….hamna shida,..’akakata simu na kunigeukia, akasema;

‘Sasa sikiliza,hao unakwenda kuonana nao,ni wakuu wa hizo idara unazotarajia kufanya kazi,tunahisi wanakwenda kukukabidhi majukumu, lakini kablaya yote usikubali kupewa majukumu bila kuandikishana kwa kila kitu kilichomo humo,na usikubali kabisa kusaini mkataba mpaka uhakikishe vyote vilivyoorozeshwa kwenye huo mkataba vipo na umeviona…’akasema mpelelezi

‘Kwani hizo nyaraka zimekwenda wapi?’ akauliza

‘Ndilo swali hata mimi najiuliza,maana hizo nyaraka ni muhimu sana, na zilitarajiwa kutumiwa kama ushahidi, na huyo aliyezichukua atakuwa ni mhusika mkuu wa hili kundi ambaye anafahamu umuhimu wa hizo nyaraka na alifahamukuwa zipo humo…’akasema

‘Atakuwa ni nani?’ nikauliza

‘Wewe unakwenda kuongea na hao watu,wasikilize vyema uone kama watazungumzia hizo nyaraka,na kama kwenye hiyo mikataba ya makabidhiano ukiona hizo nyaraka zimeorodheshwa,hakikisha unauliza wapi zilipo,lakini nina uhakika wanaweza wasiziweke ndio maana zimetoweka….’akasema

‘Mimi naona muda umekwena ngoja niende kuonana nao…’nikasema na mpelelezi,akanionyeshea ishara kuwa niondoke, yeye akawa kasimama humo humo ndani, nikatoka, na nilipofungua mlango nikakutana na mdada akiwa kasimama mlangoni

‘Nimesikia kama unaongea na mtu,ni nani?’ akaniuliza

‘Nlikuwa naongea na simu, vipi wameshafika hao wakubwa?’ nikauliza

‘Hawajafika lakini wapo chini, nahisi wanapata kinywaji,wewe nenda kawasubiri,mimi nitakusubiri cumbani kwako….’akasema

‘Kwanini unisubiri chumbani kwangu wakati mwenyewe sipo…’nikasema nikiwa na wasiwasi kuwa mdada akiingia humo ndani atakutana na mpelelezi na lolote linaweza kutokea

‘Usiwe na wasiwasi na mimi siwezi kupekua pekua vitu vyako,na hata nikitaka nisingelikuambia,ningelikuja kwa wakati wangu na kufanya ninachokitaka,wewe harakisha kwenda mimi utanikuta humo ndani….’akasema na kushikilia kitasa cha mlango,mimi nikawa sina la kufanya, kwani muda ulishakwenda na simu yangu ikaita
Nilipokea haraka haraka bila kuangalia mpigaji, sauti ikasema;

‘Sisi tunakuja, natumai umeshafika ofisini kwako,….’sauti ikasema

‘Ndio ndio...’nikasema nikionyesha wasiwasi

Nilimuona mdada akiwa kasimama mlangoni, akisikiliza naongea nini na nilipomaliza kuongea, na ile simu, akanipungia mkono, n kusukuma mlango wa chumba changu kuingia, na mimi sikuwa na kufanya kwa muda huo, kwa haraka nikaanza kutembea kuelekea ofisini kuonana na hao wakuu

NB: Kwa leo tuishie hapa, mvua, mtandao, ilifanya jana tusiwe pamoja

WAZO LA LEO:Sio kila kitu kinafaa kuiga, hata kama anayekitenda hicho kitu ni mtu maarufu sana,yeye akifanya hivyo kwa hali yake inawezekana ikaonekana ni sahihi, kwa vile ni maarufu, ni tajiri nk, na huenda kwao ina maana fulani, je wewe unayeiga hayo anayoyafanya huyo mtu maarufu kama unavyomuona wewe, unafahamu maana ya hicho kitu anachokifanya, kuvaa au kutenda?

Tusiwe wepesi wa kuiga tu bila uchunguzi,kwani mengine tunayoiga ni kinyume cha maadili, na huenda yana athari kubwa kwetu kiafya, kitamaduni na hata kimaendeleo.

Kwa uoni wangu, kabla ya kuiga jambo hebu tuangalie umuhimu wa hilo jambo, kijamii , kiitikadi na kimaendeleo, tusiige tu kutaka sifa, kwani badala ya sifa tunaweza kuzalilika, japo wewe unatafuta umaarufu. 

Ni vyema, tukaiga mambo yenye tija, yenye kuleta maendeleo,na faida kwa vizazi vyetu . Tujue kuwa kuiga sana ni utumwa na kutokujiamini. 

Ni mimi: emu-three

No comments :