Hii ni blog maalum kwa kumbukumbu za kimaisha, matukio yenye mafunzo ndani yake, ndio maana nikaiita 'diary', na kwa kuifanya iweze kuvutia zaidi tunaandika matukio hayo kwa mfumo wa visa, hadithi au tamithilya..pia tunakaribisha mijadala na yale yote unayopenda yawemo humu. Wewe ukiwa mdau muhimu, unaweza kuchangia na wenzako kwa kutoa hoja (comments). Pia unaweza kutoa maneno ya hekima, utaalamu, au dukuduku lako (kilio chako)kwa jamii ili kuweza kukidhi mahitajio yetu. SOMA , CHANGIA, NA TOA kisa chako, au lolote lenye mafunzo ili tuliweke hewani.

TUPO PAMOJA DAIMA


Tushirikiane, Tusaidiane, Tupendane, Tuvumiliane, Tusaidiane, Tusameheane.

Kwa visa motomoto tunapatikana pia kwenye mitandao ya kijamii ya: Facebook, na Twitter, bofya hapa upate visa zaidi;

https://www.facebook.com/emu.three, na kwa ajili ya kuitangaza hii blog, ingia hapa:

https://www.facebook.com/diaryyangu/

`u-like' na pia unaweza kutwitter hapa;

https://twitter.com/emuthreeThursday, May 8, 2014

BAADA YA DHIKI FARAJA-53‘Nakuhitaji haraka tuonane hotelini kwako, ni muhimu na haraka, nakupa nusu saa tu...’sauti ya mdada ikasema ikionyesha hasira au uharaka wa hilo jambo

‘Kuna nini tena mdada, nipo na bosi, nina maongezi muhumi na yeye...’nikasema

‘Bosi gani huyo, ..kwani wewe una mabosi wangapi wewe?’ akauliza kwa hasira

‘Nipo ofisini kwetu bosi aliniita mara moja...’nikasema na bosi akanionyeshea ishara kuwa tumeshamaliza, naweza kuondoka tu, akamalizia ahawa yake aliyokuwa akinywa na kusimama kwenye ile meza ya kuongelea wageni kwenda kwenye meza yake kubwa ya kiofisi, na mimi nikamwambia mdada .

‘Hata hivyo tumeshamaliza, nakuja...’nikasema kabla hajaanza kuongea, kwani kama ningempa nafasi najua maneno yangekuwa makali zaidi.

‘Fanya hivyo, tena haraka siunafahamu haraka, basi iwe hivyo...’akasema na kukata simu, na bosi akatabasamu na kusema;

‘Ni mdada huyo eeh...?’ akauliza

‘Ndio yeye bosi, anasema ananihataji haraka tukaonane naye hotelini...’nikasema

‘Ok, mimi na wewe tumeshamalizana, sizani kama kuna zaidi....’akasema

‘Lakini sizani kama mdada ana jipya namfahamu mambo yake...’nikasema

‘Mdada,jamani kabadilika...., yaani nilipoongea naye safari ya mwisho sikuamini kuwa ndiye yule mdada niliyekuwa namfahamu mimi,..kabadilika kabisa, kawa mtu wa amri,majivuno ...yaani, siamini, lakini ...simlaumu sana ni kawaida yetu wanadamu...’akasema

‘Lakini mimi siwezi kufanya hivyo....’nikasema

‘Usiseme hivyo, unafikiri ,wakati unatenda hayo huwezi kujijua, inakuja tu...tumepitia huko, kwahiyo siwezi kumlaumu sana,kwani ndivyo binadamu tulivyo,ni wepesi sana kusahau tulipotoka, na hilo ni tatizo, unatakiwa ikilifahamu ujirudi kwa haraka sana, kabla hali nyingine haijafika, maana sio kwamba utakuwa juu wakati wote, hapana katika maisha kuna kupanda na kushuka, ....’akasema.

‘Mimi nahisi ni kwasababu ya haya matukio, yanamfanya mdada ashindwe kutuliza kichwa chake, na wakati mwingine anaona watu wengine kama hawapo makini,...yeye keshaona ni vyema kifanyike hiki, hataki wewe au mtu mwingine asema vinginevyo,...ndivyo alivyo ,na mara nyingi alivyo, yeye anataka kila jambo alifanye yeye kwa jinsi aonavyo yeye. Kwahiyo atachkua hiki na kile na kukifanya kwa haraka haraka...’nikasema

‘Pamoja na hayo sikatai, lakini jifunze jambo moja katika maisha yako, kwa vyovyote itakavyokuwa usisahau ustaarabu wako, heshima adabu na utii viwe pale pale. Ukipata ukajaliwa, usisahahu hayo, hivyo ni vitu vya msingi sana katika maisha, na huo ndio ubinadamu...’akasema

‘Lakini tunatofautiana....’nikasema

‘Kutofautina kupo, na ndio maana tunaliongea hili, ukimuona mwenzako yupo hivi jaribu kumushauri kihekima,...nikuambie ukweli, nidhamu ni tabia njema sana, ifanye kwa yoyote yule, awe mkubwa au mdogo, usimdharau mtu hata siku moja,,ukifanya hivyo, thamani yako itashuka saana, ubinadamu wako na utu wako utakuwa hauna maana kabisa, nini mali bwana, nini utajiri, hivyo ni vitu vya kupita tu, lakini utu mwa mwanadamu upo pale pale...’akasema bosi, nikabakia kumuangalia, nikitamani aendelee kuongea, halafu nikasema;

‘Bosi wewe ulifaa kuwa mwalimu,...yaani nikikaa na wewe najifunza mambo mengi sana...’nikasema, akatabsamu na kuangalia saa yake, akasema;

‘Naona muda umekwenda, mimi naona uondoke, sio kwamba nakufukuza, lakini nafahamu una mambo mengi hasa kuhusu kesi yenu, ...na kama mdada keshakupigia kuwa anakuhitajia ni muhimu ukaenda uona anakuhitajia nini, na huenda sasa hivi ameshafkika hotelini kwako, mmh nenda usije ukakosana na mpenzi wako, hujui anakuitia nini..’akasema

‘Bado yupo nyumbani kwake, amesema anajiandaa na kanipa nusu saa, ...nimalizane na wewe kwanza, kwahiyo bado dakika nyingi tu, nikitoka hapa mpaka hotelini sio mbali...naomba unimalizie lile simulizi letu, kuhusu maisha yako...’nikasema na bosi akaniangalia huku akitabasamu akasema;

‘Simulizi la maisha yangu, ...oh, mimi nakumbuka tulishamalizana au...?, Nakumbuka tulifikia sehemu nimeshaanza maisha mazuri, dhiki ilikuwa imeshakwisha, na faraja ikaingia kwa mapana yake, nikawa na kila kitu, nyumba, kampuni, gari...si ndio hivyo?’ akauliza.

‘Lakini ulisema baada ya kupata hivyo vyote, ulianza kupambana na mitihani mingine, mitihani ya mali, maana wewe sasa unacho, lakini mume wako alikuwa hana, wewe ukawa ndiye unayebeba majukumu ya kifamilia, ukasema utaendelea na sehemu hiyo kuonyesha changamoto ulizipombana nazo...’nikasema.

‘Hiyo ni sehemu nyingine ndefu tu, nikianza kukuhadithia hapa tutaanza kitabu kingine kipya, maana maisha yangu yalikuja kubadilika kabisa, nikawa mtu mwingine, mtu mwenye kila kitu, nikaanza kutembea sehemu mbali mbali hadi nchi za nje....’akasema.

‘Je mume wako yeye alikuwa akifanya kazi gani?’ nikamuuliza

‘Mhh, mume wangu,..!’ akatulia kama anasita kuliongelea hilo, lakini baadaye akasema;

‘Unajua wanaume walivyo, wengi hawapendi kufanya kazi na wake zao, au kuwa chini ya wake zao, ni kweli waume ndio waliotuoa, na kiutamaduni, kidini na kihalisia, waume ni viongozi wetu, mimi hilo slikatai kabisa...’akasema

‘Lakini wakati mwingine inatokea, na inabidi tukubali ukweli, kuwa kuna wanawake wengine mungu anawajalia, wanakuwa zaidi ya wanaume, hapo haina haja ya kupatwa na kizungumkuti,...na sio nasema hivyo kuwa mwanamke ukiwa hivyo ndio uwe juu ya mume wako, hapana, maswala ya ndoa ni kitu kingine na maswala ya kazi, utendaji, na kipato ni kitu kingine...mimi siwezi kulipinga hilo kuwa wakati wote mume wangu ndiye kiongozi wa ndoa...’akasema

‘Lakini kwa sio elewa, wakaona wake zao wapo juu kikipato, kikazi, basi wanaanza kuona vibaya, hata wivu unakuwa mkubwa kupindukia, na hata ndoa nyingine hufikia kuvunjika, maana mume hataki hilo, anaweza hata kukuachisha kazi, ....sio vizuri kabisa,...ama kwa upande wa mume wangu hakuwa mbali na wanaume wengine, hakutaka kabisa kujiunga na mimi, kwahiyo yeye aliendelea na kazi zake za kubangaiza hapa na pale, lakini majukumu mazima ya familia yalikuwa mikononi mwangu, kwani yeye kipato chake kilikuwa kidogo sana....’akasema

‘Je na familia ya mume haikuendelea na chokochoko zao?’ nikamuuliza

‘Binadamu tumeumbwa na wivu, na wivu mwingine ni mbaya, wivu mwingine ni kama uchawi, hauna tija wala maendeleo, ni wivu hasi huo hautakiwi, na ukiwa nao basi wewe huna tofauti na mchawi, maana mchawi kazi yake ni kupinga maendeleo yaw engine. ...’akasema na mimi nikawa kimiya tu.

‘Wivu mzuri ni ule wa kuleta maendeleo kuwa mwenzangu kapata na mimi nataka nipate kama yeye au zaidi yake, kwahiyo unajibidisha katika shiughuli zako,na ukiwa muadilifu unaweza hata kwenda kumuuliza, ukapata ushauri wa jinsi gani alivyofanikiwa, huo ndio wivu chanya, wivu wa kimaendeleo, lakini wengi wa sisi binadamu, hatuna hilo...’akasema

‘Ehe ilikuwaje kwa hiyo familia?’ nikauliza, lakini niliona kama anasita kuongelea hilo sijui ni kwanini, na yeye kwanza akageuka huku na kule, halafu akasema;

‘Hulka na tabia za wanadamu hazibadiliki sana, mtu atakuchekea tu kwa vile anahitajia kitu kwako, lakini moyoni kwake anakung’ong’a, ..na ole wako itokee hukuweza kumpa kile alichokuomba, anaweza akakusema vibaya hapo hapo au akaenda kukusema vipembeni...’akasema na mimi nikawa imiya tu.

‘Ni heri wa yule anayekusema hapo hapo maana utaweza kumuelimisha hata kama hataelewa,...maana wengine wameshajiaminisha hivyo,na wanajua muda wote unacho, na ukisema huna unakataa...sio kweli, hata kama una utajiri, sio kwamba kila muda utakuwa na pesa,...hata kama zipo, lakini wakati mwingine zile pesa zimeshaingia kwenye bajati yake, sasa watu wengine hawaelewi...sasa huyu anayekusema hapo hapo kidogo ana uafadhali fulani sio yule anayeondoka hapo akitabasamu kinafiki na kwenda kukusema pembeni....’akatulia na kuangalia saa

‘Mimi pamoja na kufanikiwa huko, lakini sikuwa na lengo la kulipiza kisasi kwa hayo waliyonitendea, mimi niliendelea kuwaona kama ndugu zangu, nilifahamu kuwa wao bado ni familia yangu vyovyote iwavyo...’akasema na ukunja uso kuonyesha uchungu, au huzuni fulani.

‘Pamoja na kujitahidi kwangu kote huko, kwani nilijua hali zao zilivyo,nikajitahidi kuwasaidia kila walipohitajia kitu, au hata kama hawajaniomba, mimi mwenyewe nilifahamu kuwa hiki kinahitajika kwa wakati fulani, kwahiyo kwa nafsi yangu niliweza kwenda kuwapa, na kila niwezavyo, sikusita kutoa kila nilichoona kinahitajika....’akasema

‘Ukiwapa wanapoea, na kukushukuru au ....?’ nikauliza

‘Ndio maana nilitangulia kukuambia kuwa wanadamu hawana wema,.na hulka na tabia za binadamu sio rahisi kubadilika , ni wachache sana wanajiona wana tabia mbaya, wakajuta na kubadilika, kitu kama wivu mbaya, ukimtanda mwanadamu, anakuwa hajijui tena..na hilo ndilo lililowapata ndugu wa mume, wakajaribu kila hila kumpotosha mume wangu kwa maneno ya uchonganishi, ....’akasema

‘Walikuwa wakimwambia nini mume wao?’ nikauliza

‘Walifikia kusema kuwa kwa vile sasa mimi nina kila kitu, simtambui tena mume wangu, simthamini tena mume wangu, kwa vile eti mimi sasa ninacho, eti mimi sasa namdharau mume wangu...’akasema

‘Walifikia hata kusema mimi nikitoka kikazi, ninakuwa na nyumba ndogo huku na kule...ilimradi watufitinishe, lakini mimi nilijitahii kumuweka mume wangu sawa na kujaribu kumkumbusha huko tulipotoka,...lakini....’akatulia kidogo maana simu yangu ilikuwa inaita,nikaangalia aliyepiga simu ni nani, alikuwa mdada. Nikapokea hiyo simu kwa haraka;

‘Mimi nimeshafika hotelini kwako nakusubiri....’akasema na kukata simu, niliona ajabu kwa jinsi mdada alivyofanya haraka hivyo, hii ni kuashiria kuwa hilo jambo analonihitajia ni kubwa sana.

‘Mdada huyo, kama nilivyokuambia, kama ana jambo la haraka, hataki kusikia kitu kingine, ...sasa bosi nakuomba tena, usinipoe hiyo barua ya kuvunja mkataba wangu wa ajira kwa sasa, naomba unipe muda, nione kitu gani kinachoendelea, ..nakuomba tafadhali, nisije nikaumbuka....’nikasema

‘Mimi sina shida, ila kiukweli hilo limeshapitishwa kwenye kikao cha wakurugenzi,na kama kuna mabadiliko mengine...mimi kama mimi siwezi kuamua mwenyewe, itabidi nikae tena na wenzangu, ndivyo taratibu za kikazi zilivyo hasa pale mnapowekeza zaidi ya mtu mmoja, wakurugenzi tupo watatu, sasa siwezi kujiamulia mimi mwenyewe,....’akasema

‘Oh, kweli hivi bosi huyo mkurugenzi mwingine mbona sijawahi kumuona, akiwajibika, nawaona nyie wawili tu, wewe na baba yake mdada?’ nikauliza

‘Huyo mkurugenzi mwingine ni muheshimiwa fulani, kawekeza hapo, siunajua tena, ili uweze kupata zabuni za hapa na pale ni lazima uwe na mshika shati, tunaye mkurugenzi mwingine japokuwa yeye sio mshiriki mkubwa katika utendaji, anafika kama kukiwa na kikao kikubwa kama hicho tulichokifanya,yeye ni mdhamini muhimu sana,....’akasema

‘Kiukweli japokuwa haonekani mara kwa mara lakini ni mtu muhimu sana, na utendaji wake, japokuwa ni wa kimiya kimiya, lakini una tija sana kwa ampuni yetu hii...hizi kazi zetu pamoja na juhudi binafsi, lakini kwa namna nyingine, ufanisi wake, na uwezeji wake unategemea juhudi za ziada za watu kama hao...’akasema

‘Kama zipi?’ niauliza

‘Ili kampuni iaminike, hata kupaat zabuni, inahitajika kuwa na wadhamini wazuri, wenye jina, sio mchezo, serikali inakuwa makini sana katika kutoa zabuni zake,...kwahiyo huyo ni mtu anakuwa ni mdhamini muhimu sana wa kampuni....’akasema na mimi nilitaka kumuuliza swali jingine, lakini nikaona muda umekwisha, nikainuka kuondoka, na yeye akasimama na kunyosha mkono wa kwaheri.

‘Bosi sijui niseme nini, hapa nilipo naona kama machozi yakinilenga lenga, lakini kwa vile ni mwanaume ni lazima nijikaze kisabuni, ..bosi wangu wewe ni mtu wa pekee sana, sijui nikiondoka hapa kama nipata bosi mwingine kama wewe...’nikasema

‘Usijali, utapata na tena zaidi ya mimi, na huko utegemee kuwa bosi, nafasi hiyo ni sehemu nyeti na utakuwa na vitengo vyako, kimojawapo ndio hicho atakachokuwa anafanya kazi mdada, kwahiyo mdada takuwa chini yako...’akasema

‘Oh, nilikuwa sijui hilo....’nikasema

‘Anza kutafiti, ni muhimu sana unapotaka kufanya kazi mahali, ukapafanyia uchunguzi kwanza, ujue ni kitu gani wanafanya kiuzalishaji, masoko naladhalika, lakini pia ni muhimu ujue jinsi gani, utawala wao ulivyo, hili litakusaidia sana katika utendaji wako, ikizingatia kuwa popote utakapoajiriwa kuna kipindi cha majaribio ya kupimwa utendaji wako wa kazi...’akasema

‘Oh, hilo tena?’ nikauliza

‘Ni lazima popote utakapokwenda hiyo hali ipo....ukiwa umejiandaa , kwa kufahamu mazingira ya ile kazi, utendaji wao, na utawala wao, hutapata shida....’akasema huku akisogea na tuakumbatiana kwa kuagana, na akasema;

‘Tukijaliwa tutaona, tusisahauline, .....’akasema kitabasamu, namimi niksema;

‘Nitakuja, ni lazima nije ili nisikie zaidi kutoka kwako, ...kisa cha maisha yako ni muhimu sana kwangu nataka kujua zaidi,..na pia, kiukweli sitaki kuacha kufanya kazi na wewe....’mara simu ikaita, na safari hii ni mpelelezi alikuwa akinipigia,...nikajiuliza kuna nini tena

NB: Leo hicho kidogo kinatosha...tukutane sehemu ijayo

WAZO LA LEO:Ukipata , kwa kupanda cheo, au kubahatika kubadilika kutoka hali ya chini na kuwa hali nzuri zaidi, ukajaliwa kupata kila kitu, na kwa bahati mbaya wenzako wakawa bado hawajafanikiwa, ni vyema ukikutana nao ukawapa mkono, usiwasahau, usiwadharau, na ikibidi kama inawezekana kuwavuta juu fanya hivyo...ni bora sana, kwasababu kupanda kwako huenda kwa namna moja au nyingine pia kunatokana na wao, kimawazo na hata kiutendaji. Kamwe usisahau ulipotoka au kuwasahau mliohangaika nao.


Ni mimi: emu-three

1 comment :

Yasinta Ngonyani said...

Kisa kinazidi kisisimua ...Wazo la leo ni bonge la wazo na ni wengi sana wanasahau walikotoka. Ahsante kwa hili.Pamoja daima!